Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Francis Leonard Mtega (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. FRANCIS I. MTEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ya uhai wa wananchi, suala la maji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukomo wa bajeti nafahamu kwamba ipo miradi katika jimbo langu ambayo imeachwa kutokana na ukomo, ambayo ni miradi muhimu sana inayohudumia wananchi wengi, takribani wananchi 10,000,000. Mheshimiwa Waziri mfano wa miradi hiyo, mfano Mradi wa Mirade karibu milioni 500, Mradi wa Mbigigi milioni karibu 520, Mradi wa Ndala karibu milioni 350. Miradi hii yote imeachwa kutokana na ukomo wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba upo mpango wa Wizara hii kuongezwa fedha hasa kutokana na agizo la Mheshimiwa Rais kwamba Wizara hii anaingalia kwa makini sana na akamwambia Waziri akizingua na yeye atamzingua. Sasa pale pesa zitakapoongezwa, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri miradi hii irudi kwenye bajeti. Kwa sababu ni miradi muhimu, wengine naona wanaongelea miradi ya miji yao kupata maji, lakini sisi wa vijijini na Wilaya yangu ya Mkalama ni wilaya mpya, haina vitendea kazi na shida ya maji ni kubwa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atakapoongezwa pesa, miradi hii irudi ili wananchi hawa wa Mirade, Ndala na Mbigigi katika Wilaya ya Mkalama nao waweze ku-enjoy maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, pia Meneja wangu wa RUWASA pale Mkalama anafanya kazi nzuri sana Engineer Mark, ni msikivu, anafuatilia lakini tatizo kubwa hatuna vitendea kazi. Wilaya yetu iligawanywa kutoka Iramba na vitendea kazi vingi vilibaki kwenye Wilaya Mama. Hatuna gari, nimwombe Waziri katika bajeti zake atupatie Mkalama gari ili Engineer huyu na watu wake na Ofisi yake waweze kufanya kazi nzuri zaidi ya wanayoifanya sasa ya kuhudumia Wilaya yetu ya Mkalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuongelea jimbo langu sasa nishauri pia Wizara hii kitaifa. Kwa kushirikiana Wizara ya Maji na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wanaweza kutengeneza sera ambayo itawafanya Watanzania wawe na tabia ya kuvuna maji ya mvua. Unajua kila Mtanzania mwenye nyumba ya bati tayari ana chanzo cha maji, kinachobaki ni storage tu. Kwa hivyo kama tutatengeneza sera vizuri ya kuwashawishi Watanzania, wakaweka umuhimu kwenye ramani zao za nyumba wanapojenga kuwe kuna tank angalau la lita 50,000 za maji.

Mheshimiwa Spika, ukiwa na lita 50,000 za maji una mapipa zaidi kama 250 hivi. Kwa mwananchi wa Tanzania akiwa anatumia pipa moja lenye ndoo 12 anaweza akatumia miezi nane ya kiangazi. Kwa hivyo kama Watanzania wenye nyumba za bati wakatambua kwamba tayari wana chanzo cha maji na hivyo wakatengeneza storage tank, tutatumia, tutapata maji ya mvua ya kutosha na tatizo hili tutalipunguza kama siyo kulimaliza katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo ikiwepo sera maana yake kutakuwa na miongozo, kutakuwa kuna uhamasishaji na mambo mengine na hii tabia itaingia taratibu kwa Watanzania kujua kwamba tayari wana chanzo cha maji na hivyo kinachobaki ni kutengeneza storage tank angalau ya lita 50,000 na kuendelea. Mimi hapa nina ma-tank zaidi ya matatu yenye lita laki 200, na-enjoy, kwa hiyo naamini hiki kitu kikienda kwa Watanzania wengi shida hii itapungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, niiombe pia Wizara, badala ya kusubiri kila wakati maji yazame kwanza ardhini halafu ndiyo tuyafuate, unajua maji haya ya visima ni maji ambayo ni ya mvua, yakishazama yanaenda kwenye miamba yanatuama ndiyo tunafanya kazi ya kuyafuata chini. Hebu tujielekeze zaidi kwenye mabwawa kwa sababu mabwawa maji yanakuwa bado yapo juu na tukiyatega mabwawa ya maji yanakuwa na faida zaidi ya kunywa maji peke yake, kwa sababu bwawa la maji utapata maji ya kunywa, tutapanda samaki, tutavua samaki lakini na sehemu nyingine pia itamwagilia hata mazao. Kwa hiyo bwawa hili linakuwa lina kazi zaidi ya moja kuliko kusubiri yaende chini ndiyo tuyafuate kwa gharama kubwa kuyaleta juu.

Mheshimiwa Spika, ipo mipango mikubwa ya mabwawa, mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba, kuna mradi wa Farukwa pale umeoongelewa, ni mradi mkubwa ambao lengo lake lilikuwa ni kulisha Dodoma, sijaona kama umepewa kipaumbele kikubwa. Bwawa lile likijengwa linakuwa hadi na kisiwa ndani, sasa hatuoni kwamba mipango hii ya mabwawa ikifanywa vizuri italeta faida mara mbili, mara tatu zaidi ya kupata maji ya kunywa. Kwa hiyo niombe wizara ijielekeze zaidi kwenye mabwawa kwa sababu fedha nyingi na miradi hii itakuwa multipurpose itafanya kazi kubwa zaidi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia …

SPIKA: Ahsante sana muda wako umeisha.

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Aweso; na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Maryprisca Mapunda. Pia niwapongeze sana Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wote wa Wizara ya Maji kwani wamefanya kazi kubwa sana na tunajua nchi yetu hii ni kubwa sana lakini kwa jitihada zao kwa kweli wamejitahidi mpaka hapo walipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo naomba nijikite kuchangia mambo mawili tu. Moja ni kuwajibika na la pili ni kuwajibishana, kwani naamini hizi ndizo nguzo kuu kabisa kujenga nidhamu kwa wafanyakazi ili waweze kutimiza lengo la kuwapa maji wananchi wote kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba nitoe changamoto kadhaa zinazowapata wananchi wetu kule vijijini. Yawezekana kwa kuwa hii ni Wizara kubwa na inajumuisha Wizara nyingine, zile changamoto ambazo zitahusu moja kwa moja Wizara hii Mheshimiwa Waziri atazijibu anapojumuisha, lakini zile ambazo zitahusu labda Wizara zingine na wenyewe watapata nafasi kujibu watakapokuwa wanatoa hotuba zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa mambo ya washirika na mamlaka zilizo chini ya Wizara. Nimeona katika hotuba ukurasa wa 80, Waziri ameelezea namna anavyoshirikiana nao na ametoa miongozo. Hata hivyo, kanuni hizo zinafanya baadhi ya mamlaka hizo pengine kwa kutofahamu au kwa makusudi kabisa kufanya changamoto kubwa sana kwa watumiaji wa maji kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na maji safi na mazingira. Wananchi wanapata mfadhili awasaidie kujenga tenki kubwa la maji, naenda RUWASA, RUWASA wana masharti yao. Wanasema kwanza maji yale yapimwe na Mkemia Mkuu, lakini pia bonde waje waidhinishe, wapime kina cha maji. Sasa ukienda bonde wao watasema tunasubiri kwanza mvua zinyeshe tuone maji huwa yanajaa kiasi gani. Ukienda wakati wa mvua wanasema tusubiri kiangazi tuone maji huwa yanapungua kiasi gani. Hivyo wananchi wanakosa huduma ya maji. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, maji yale wananchi huwa wanayatumia muda wote. Sasa mfadhili anataka kuongeza wingi wa maji hivyo kumbe wangeweza kutoa kibali, tenki likajengwa huku wanasubiri vipimo hivyo viendelee kwa vile maji yale yanatumika moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika umwagiliaji. Wakulima wale huwa wanahangaika sana. Wanaenda Mamlaka ya Bonde, Bonde wanasema sisi tumesitisha vibali, hatutoi vibali kabisa, lakini unakuja kwa Sekta ya Umwagiliaji, wao wanasema sisi tunaruhusu mfereji upite hapa lakini kule kibali hawatoi. Sasa wananchi hawa wanaendelea kupata changamoto kubwa sana. Wananchi hawa muda wote wanapita mamlaka zingine za mifereji wanawatoza ada ya maji. Ukienda Mamlaka ya Bonde wanasema sisi hatujapata ada yoyote na hawa hawana control number, leo watapita na counter book jipya, kesho watapita na ki-note book, anakusanya fedha na hazieleweki zinaenda wapi. Huku analipa elfu 50,000 kwa heka moja, fedha haziingii Serikalini, lakini, mkulima huyu anauza gunia moja shilingi 45,000, kwa hiyo ni changamoto kubwa sana kwa watumiaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye kuwajibishana. Kuwajibishana kwa upande wa Wizara. Utendaji kazi kwa upande wa Wizara mambo ni mazuri sana, mambo yanaenda vizuri kama nilivyopongeza lakini kule kwa watendaji wa chini kwenye vijiji namwomba Mheshimiwa Waziri akae na wadau mbalimbali aongee nao. Hii itampa picha namna gani mambo yanaenda kule kwa sababu nimeona katika ukurasa wa 80 wa kitabu ametaja anavyoweza kushirikiana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba ushirikiano wa Waziri na Wizara ya TAMISEMI, ningeomba hizi Mamlaka zote ziwajibike kwa Waheshimiwa Madiwani. Waheshimiwa Madiwani kwenye Baraza lao ndiyo pekee wanaoweza kuhoji na wanaweza angalau wakafuatilia miradi ile kwa ukaribu Zaidi. Tumeona akienda Waziri mwenyewe na Mheshimiwa Naibu Waziri wanakuwa wakali lakini hawa Madiwani wanaweza kusimamia kwa ukaribu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya, lakini nimpongeze sana Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ningependa nichangie kuhusu migogoro ya ardhi na mipaka, hususan mipaka. Migogoro ya ardhi imekuwa mingi kwa nchi yetu kwa ujumla, lakini Mheshimiwa Lukuvi amekuwa hodari sana na mahiri kwa kuitatua, nampongeza sana. Hata Mbarali tulikuwa na mgogoro baina ya mwekezaji wa Kapunga na wananchi, lakini mwaka ule 2015 alikuja haraka sana na kuumaliza mgogoro ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mgogoro mkubwa sana wa mipaka kati ya TANAPA na vijiji 55 katika Jimbo la Mbarali. Huu mgogoro kwa kweli ni mkubwa sana na una athari nyingi. Namwomba Mheshimiwa Waziri aupe kipaumbele kuutatua mgogoro huu, vinginevyo Wana-Mbarali hawatakuwa na amani na utulivu kabisa. Mpaka huu wa GN Namba 28 bahati mbaya sana umepita vijijini, mawe mengine yako katikati ya vijiji. Sasa wananchi wale wanaishi kwa matamko; atakuja kiongozi huyu anasema msiwe na wasiwasi, endeleeni na shughuli zenu kama kawaida, Serikali inafanyia kazi. Anakuja kiongozi mwingine anasema mko ndani ya hifadhi hamruhusiwi kufanya kitu chochote. Sasa hii inawapa shida wananchi wale, hawajui wafanye nini, kwa sababu, shughuli nyingi wanazifanya ndani ya maeneo yao wanayoishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna mashamba mazuri kule Mnazi na mashamba yale yanatoa mpunga kwa wingi na tuna viwanda vikubwa pale Ubaruku vinachakata mpunga tena wa hali ya juu. Sasa kuwaambia wasifanye shughuli yoyote, maana yake ni kuwarudisha nyuma kiuchumi na kukosesha pato la Taifa. Kwenye Ilani imeainishwa kabisa kwamba tunaenda kuboresha kilimo na kuhakikisha wananchi hawa wanakuwa na kipato cha kutosha na vilevile Taifa linakuwa na akiba ya chakula. Sasa wanapozuiwa wasifanye shughuli zao za kila siku, kwa kweli hatuwatendei haki wananchi wale wa Mbarali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna shughuli mbalimbali, kwa mfano kule Luhanga kuna ujenzi wa Shule ya Msingi na ujenzi wa Zahanati. Sasa kiongozi huyu anakuja anasema endeleeni na ujenzi msiwe na wasiwasi, kesho kiongozi mwingine anakuja kuzuia kwamba msifanye jambo lolote la kuendeleza kwa sababu mpo ndani ya hifadhi, subirini Serikali itoe maamuzi yake kwamba wapi kutakuwa ni mpaka ndipo mtakapoendeleza ujenzi. Sasa hii inawavunja moyo wananchi wale, wamepoteza nguvu zao na sasa hawaendelei na ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, maamuzi ya Serikali yaharakishwe ili kubainisha mpaka sahihi ni upi? Yawezekana kuna vijiji vitaambiwa viondoke, yawezekana kuna vitongoji vitarekebishwa, sasa hii ingefanyika haraka ili wananchi wawe huru kufanya kazi zao za kila siku wajipatie kipato na vilevile waweze kuliongezea pato Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije upande wa GPS. Zamani mipaka ilikuwa inawekwa mawe tu, kiasi kwamba wazee wanakuwepo ni mashuhuda kwamba mpaka ulikuwa hapa na viongozi wa eneo lile wanashuhudia, lakini sasa ni GPS. GPS hii ni wataalamu peke yao wanaoweza kutafsiri. Sasa naomba Waziri atakapojumuisha, atuambie ni nani ata-cross check kuona kwamba hawa wataalam wetu wanaotafsiri coordinates zile kuweka mawe, je, hawawezi wakawa wanaingia ndani zaidi au pengine kutoka nje zaidi? Kwa sababu, wananchi pale hawana utaalamu wowote, wao wakishaona jiwe limewekwa ni kulalamika tu kwamba, sisi mpaka tunajua ulikuwa kule, sisi mpaka haukuwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo tuna migogoro mingi sana kuhusu GPS katika tafsiri yake na mawe yanavyowekwa, wananchi hawawi na uhakika, wanakuwa na wasiwasi mkubwa sana. Kwa kweli, Mbarali tuna uhaba mkubwa sana wa ardhi, Mbarali tuna mifugo mingi, Mbarali tuna mashamba ya mpunga, Mbarali tuna hifadhi ya TANAPA; ile hifadhi ni kubwa mno kiasi kwamba eneo linalotumika kwa wanyama liko upande wake, lakini eneo la wananchi ambapo linaonekana ni oevu, kwa kweli ni kubwa mno na kwa sasa hivi ule u-oevu haupo. Nimezunguka sehemu nyingi ni vumbi tupu na mashamba, lakini Ihefu kwa kweli bado ni sehemu oevu na inahifadhiwa na wananchi hawaruhusiwi kwenda kule. Sehemu nyingine zote ni kavu, zina mashamba, hakuna uoevu, hakuna maji; maji yanapita tu mtoni, yanatoka Makete, pale ni mapito ya maji, wala hakuna madhara yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kweli aende mwenyewe kule ashuhudie, aone haya mawe yaliyopandwa vijijini yanavyoathiri wananchi na kwamba, sehemu zile kwa kweli hazihusiani kabisa na uoevu unaoongelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika bajeti hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu anayetujalia uhai na anayezidi kulinda Taifa letu na ustawi wa wananchi wake. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya, nimshukuru sana Makamu wa Rais, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri wanazofanya. Hii imetuletea bajeti nzuri, bajeti ambayo imegusa kila eneo, kila kundi kwa kweli ni bajeti ambayo inaenda kuinua hali za Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wangu ujikite katika kilimo; kwa vile asilimia 65 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, lakini pia vijana wetu ambao hawana ajira wanaweza wakajiunga na kilimo. Vile vile Bunge lako Tukufu hili Bunge la Kumi na Mbili limebainisha kwamba linaenda kujikita zaidi katika kufanya mageuzi makubwa katika sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika bajeti ukurasa wa tano, ukurasa wa 16 na wa 17 namna ambavyo Serikali inaenda kuboresha kilimo, namna Serikali inavyoenda kuleta tija na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, nilitarajia kuona kwamba Serikali inaweka fedha nyingi kama mtaji kuinua hii sekta; kwanza kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, lakini pili, kwa kutafuta masoko na kuboresha ya ndani na nje na kikanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kabla ya kuanza mtaji huu naona kuna tozo mbalimbali zimewekwa pale. Kwa mfano katika ukurasa wa 33 kuna tozo ya zuio, sasa pale imefafanuliwa vizuri kwamba tozo hii inaenda kutozwa kwa NFRA kama Wakala wa Ununuzi, lakini bahati mbaya kinachotokea kule ni tofauti kabisa, ni wakulima ndio wanaotozwa tozo hii. Wakulima wale hawajafafanuliwa vizuri, tozo hii inatozwa wakati gani kwa sababu kuna ushuru wa halmashauri na wakulima wanatozwa njiani wanavyotoka shambani wakati wanarudisha mazao nyumbani, wanatozwa barabarani, lakini pia wakulima wanatozwa wanapopeleka gulioni wanatozwa mara ya pili na tatu wengine wanatozwa pale wanapouza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri aje na ufafanuzi, kwamba muda sahihi wa kumtoza mkulima hasa mdogo ni wakati gani? Anaposafirisha au anapouza? Ni wakati gani atozwe na kwa kiasi gani? Tumeona nyuma huko, ilikuwa kawaida ni kwamba anayebeba chini ya tani moja hatozwi chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ukurasa wa 33 imebainishwa kabisa, hii haitahusu wakulima wadogo wadogo magulioni, itahusu tu wakala wa ununuzi, lakini kinachotokea kule ni tofauti kabisa; wale wazabuni wanaotakiwa watoze njiani, hata wakiona gunia chini ya tani moja, wanatoza. Wanatoa visingizio mbalimbali; watasema umeweka mfuko haufai siyo wenyewe, watasema sijui sasa hivi tunatoza tu kwa vile umechelewa kurudi toka shambani, ili mradi wao wapate kodi kubwa. Wanapiga hesabu ya kutosha kupeleka Halmashauri na nyingine ibaki kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tungependa ufafanuzi, tujue hali halisi, inatakiwa itozwe kwa nani? Kama ni mkulima, basi ni wakati gani? Je, ni pale anapofanya biashara au wakati gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, changamoto nyingine kwa wakulima hawa ni mbolea. Mbolea ina ruzuku lakini kwa kweli ruzuku ile inafika mahali haiwezekani, bado ni bei kubwa sana. Nitoe mfano, mwaka jana 2020, Jimbo la Mbalali mbolea aina ya CAN imeadimika kabisa. Huwa bei ya kawaida uwa ni shilingi 45,000/=, imepanda mpaka shilingi 55,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine kwa wakulima ni skimu zile. Kwa kweli skimu zilizo nyingi zina hali mbaya sana. Kwa hiyo, wakulima wanakosa pato kwa sababu skimu zile hazijakarabatiwa kwa muda mrefu. Kule Mbarali kuna skimu moja inaitwa Mwendamtitu, imekuwa ikijaa mchanga mara kwa mara. Halmashauri kupitia mapato ya ndani imejaribu kuzibua, imeshindikana na wale wameomba mkopo kutoka TAB Bank mpaka sasa hivi hawajapata mkopo wowote na baadhi yao hawajavuna kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni mtaji. Wakulima wadogo wale hawana mtaji wa kutosha. Mtaji kwa maana ya kwamba wanaenda benki wanaahidiwa kukopeshwa, lakini ukifika msimu kwamba wanaenda shambani, benki hawatoi mikopo kwa wakati na pengine hawatoi kabisa. Wamekuwa wakinilalamikia. Mwenyewe nimeenda benki kuulizia, mbona hamuwapi wakulima hawa mikopo na msimu unapita? Wananijibu kwamba mtandao haupatikani, waombaji ni wengi, tunaendelea kuchambua, tutawapa tutakapoona majina yao, lakini muda unazidi kwenda, wengi wamekosa mikopo, wachache wamebahatika kukopa na wengine wameenda kukopa kwa watu binafsi, kitu ambacho ni gharama kubwa, kwani riba ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wamehangaika, wamepata mikopo, wamepata shida zote hizo, lakini masoko hakuna. Wamevuna mipunga, imejaa ndani na soko hakuna. Kwa mwaka uliopita Mbarali tumevuna tani 275,000 uzalishaji, lakini mahitaji yetu ni tani 125,000 tu. Kwa hiyo, tuna ziada ya tani 150,000; na hizo tani zimekutana na mavuno ya mwaka huu. Kwa hiyo, wamekopa, hawajauza, wamelipa ushuru, tozo mbalimbali, mpunga umekwama ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka nije kwenye suala la masoko ya ndani. Naiomba Serikali iwape NFRA fedha nyingi wanunue mazao yote ya wakulima. Njia nyingine katika kuimarisha masoko ya ndani ni kuanzisha mradi wa Liganga uanze kufanya kazi, watauza mazao yao kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa sana la Tume ya Umwagiliaji, inafanya kazi kule bila mawasiliano na Halmashauri. Wanaenda site, wanaongea na wakulima moja kwa moja; sehemu nyingine wanafukuzwa na sehemu nyingine kuna miradi ya ajabu kabisa ambayo Halmashauri haijui na mingine iko chini ya kiwango. Kwa mfano, tuna bwawa moja Rwanyo pale Igurusi la miaka mingi halifai na ni hatari kwa wananchi pale. Tuliomba Chuo Kikuu Mzumbe waje kutathmini namna ya kurekebisha, wakasema gharama ya marekebisho itazidi gharama hata ya ujenzi. Sasa fedha ya Serikali ndiyo imeisha hiyo, ni hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba, ili tuwe na usimamizi mzuri kwa Wilaya ya Mbarali, kwa kweli jimbo lile ni kubwa mno, tunaomba ligawike yawe majimbo mawili au Halmashauri mbili, kwa sababu inapitia mikoa mitatu; imeanzia Mbeya, Njombe, hadi Iringa; na ukiwa katikati pale kwenda upande wa mashariki ni kilomita 97, kwenda magharibi ni 134, jumla ni urefu wa kilomita 231. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtaalam kwenda kufanya supervision, akienda anarudi usiku kabisa na inabidi anywe Panadol ndiyo alale usingizi na akirudia analazwa. Sasa kwa kweli tuna hali ngumu sana. Kuna miradi mikubwa na mizuri ya ujenzi wa madarasa; mnaenda kule mnaambiwa cement tulimwazima Mwenyekiti wa Kijiji, tuliona itaganda. Mbao, kiongozi fulani tuliona azitumie, fedha hatuna. Kwa kuwa ni mbali mno, tunaomba sana igawanywe iwe Halmashauri mbili na ikiwezekana na Mji wa Lujewa iwe mamlaka kamili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. FRANCIS L. MTEGA Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)