Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi (5 total)

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwa kuwa, tatizo la maji katika Jimbo la Serengeti ni sawa kabisa na tatizo la maji kule Namtumbo. Naipongeza sana Wizara, rafiki yangu Mheshimiwa Jumaa amejitahidi sana kuhakikisha mradi wetu wa maji hasa ule wa chujio unakamilika hata hivyo mpaka sasa hivi mradi ule bado haujakamilika, lakini pia kupeleka maji katika vijiji vya Jirani. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi yote hii miwili?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa namna bora na nzuri ya kujibu maswali. Kweli nimeamini mtoto wa samaki hafundishwi kuogelea, hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa ambalo nataka niliseme ni kwamba Wizara ya Maji tumepokea miradi 177 ambayo ni kichefuchefu na ilikuwa ikichafua Wizara. Mkakati wa Wizara baada ya kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), tukasema miradi hii yote kichefuchefu ikiwemo mradi wa Mugumu ambao ulikuwa ukichafua, sasa hivi tunaukwamua. Katika wiki hii tunatoa fedha zaidi ya milioni 300 kuhakikisha tunakamilisha mradi ule na wananchi wa Mugumu waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Takwimu mbalimbali za wataalam zimeonesha kama Uwanja wa Ndege wa Serengeti ukiboreshwa utakuwa uwanja pekee katika Kanda ya Ziwa utakaoleta tija kubwa kiuchumi, kiuhifadhi na kijamii kwa wananchi wa Serengeti na Tanzania kwa ujumla. Kwa kuwa mpaka sasa tayari wadau mbalimbali na wananchi wamekwishachangia ujenzi wa uwanja huu. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa uwanja huu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Uwanja wa Serengeti ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi lakini pia katika eneo la Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla. Pia naomba nitambue kwamba ni kweli wananchi na Mheshimiwa Mbunge amejiunga, wametengeneza group la WhatsApp, wanachangisha fedha na Mheshimiwa Mbunge leo ameomba appointment watu wakija awapokee tuzungumze.

Mheshimiwa Spika, naomba nimwelekeze Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege atume watalaam wetu katika eneo hili ili juhudi nzuri za wananchi zisipotee, atuongezee utalaam wa Wizara yetu kazi hii ifanyike na uwanja ujengwe ili watalii wasizunguke Zaidi, washuke pale karibu na tutape huduma na fedha iongezeke.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kufuatia mvua nyingi ambazo zimenyesha katika Jimbo la Serengeti, barabara nyingi zilizo chini ya TARURA sasa zimeharibika sana ikiwemo barabara ya kwenda Iselesele, barabara ya kwenda Mosongo lakini pia barabara ya kuzunguka stendi ile. Pia barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kuzunguka soko la Mji wa Mugumu nayo haijajengwa muda mrefu:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hizi na zile za kufanyiwa marekebisho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, ameainisha barabara kadhaa ambazo zinahitajika zitengenezwe; na kwa kuwa nafahamu changamoto za barabara kama ambavyo Wabunge wamekuwa waki- debate humu ndani ya Bunge; niseme tu, jambo hilo tumelipokea na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika ule mchakato wetu wa pamoja, tunaandaa plan ambayo itahakikisha barabara zote nchini tunazipitia, tunafanya tathmini ya kutosha na kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha hizo barabara zinatengenezwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, awaambie tu wananchi wa Serengeti wakae mkao wa kula, hizi barabara tutazifanyia kazi na kazi yake mtaiona kabla ya miaka hii mitano kwisha.Ahsante. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ambayo yametolewa na Serikali. Pengine niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ningemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii akaambatana nami na kutembelea wananchi wa Jimbo la Serengeti kuona ni namna gani tatizo hili ni kubwa na mikakati iliyowekwa, je inaweza kweli kutekelezeka na kumaliza tatizo? Kwa sababu hivi ninavyozungumza kila mara tunapata ripoti za tembo, simba kuvamia wananchi. Pamoja na majibu haya yanayotolewa lakini bado hatuoni tatizo hili likiisha. Kwa hiyo niombe, kwa maana ya kwamba kwa majibu haya Waziri afike na yeye aona kama kweli haya yanaweza yakatosheleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ukitoka katika eneo la mpaka wa hifadhi katika vijiji vingi unaingia kijijini moja kwa moja, hili ni tatizo kubwa sana. Serikali iliwahi kutoa mpango kwamba kutaongezwa buffer zone ambayo ni nusu kilomita kuingia ndani ya hifadhi, lakini mpaka leo bado hawajatekeleza. Sasa je, ni lini Serikali itatekeleza uamuzi huu wa kuongeza buffer zone kuingia ndani ya hifadhi ambayo ni moja ya jambo linaloweza likasaidia sana kupunguza mwingiliano huu wa wanyama na makazi ya watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wake wako tayari kutembelea eneo hilo la Serengeti kama Mheshimiwa Mbunge alivyotaka. Na kwa sababu wako tayari kutembelea eneo hilo. Hata yale majibu yanayohusu buffer zone ambayo iliahidiwa napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yatatolewa majibu wakati wa ziara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni sote tumeona jitihada kubwa sana za Rais Samia za kuvutia watalii katika nchi yetu, lakini pia sasa hivi tayari Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi, pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii walianza jitihada za pamoja, wameanza vikao vya kuona namna ya kujenga uwanja ule. Hii ni kuzingatia pia kwamba kuna ushindani mkubwa kwa wenzetu, watu wa Masai Mara kule Kenya ambao wana-share ikolojia moja na Serengeti.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri nipate nafasi ya kukutana naye kwa mazungumzo maalumu kuona ni namna gani tutapata mwelekeo wa pamoja wa kuweza kujenga uwanja huu kwa viwango vikubwa kabisa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara hii ya Sanzate mpaka Natta, na ile ya Tarime – Mugumu – Natta, barabara hizi hazi-connect Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti pale Mugumu. Mwaka wa jana, 2020 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano alitupa ahadi ya ujenzi wa kilometa 30. Kwa hiyo, namwomba sana…

SPIKA: Unasema Tarime – Mugumu – Natta, haifiki Mugumu tena!

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, Tarime – Mugumu – Natta halafu kuna ile ya Makutano na Sanzate – Natta. Sasa zote hizi kwa jinsi ya ule mpango wa ujenzi, zitachukua muda mrefu kuja kuunganisha Makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, tukawa tumemwomba aliyekuwa Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba kipande cha Natta – Mugumu kiweze kupewa fedha kijengwe haraka ili barabara ile ya Makutano – Sanzate – Natta sasa itoke pale Natta mpaka Mugumu. Halafu na ile inayotoka kule Tarime – Nyamwaga – Mugumu iweze kuungana nayo mapema zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa ni lini Wizara inaweza kutekeleza mpango huu na ile ahadi ya Rais? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amsabi Jeremiah, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameomba tufanye mazungumzo namna bora ya kupata fedha ya kujenga uwanja wa ndege wa Serengeti.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nitumie nafasi hii kusema kwamba kwa sasa pia Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha za kutosha za kuanzia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma na mkandarasi ameshapatikana, yupo site anafanya kazi, lengo ni kuboresha huduma katika Hifadhi ya Serengeti.

Mheshimiwa Spika, tangu anazungumza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, walifanya kazi nzuri sana pamoja na Wizara ya Maliasili ya kufanya mjadala. Sisi tunaona kwamba uwanja ambao walipendekeza kujenga ni uwanja ambao unamilikiwa na TANAPA na Halmashauri, ambao ni uwanja mdogo. Sisi tunataka tujenge uwanja mkubwa wa Kimataifa ili tushindane na wenzetu wa Kenya ambao wanajenga kule Masai Mara uwanja mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumewaelekeza watu wa Maliasili Uongozi wa Mkoa wa Mara watuletee andiko maalumu, tukae pamoja na Wizara ya Ujenzi, tujenge Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ili tusigawane watalii wanaotaka kupata huduma katika mbuga yetu ya Serengeti. (Makofi)

SPIKA: Huo uwanja mnataka kujenga wapi?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, tunafikiria kujenga uwanja wa ndege Serengeti pale Mugumu, wanalo eneo pale la kutosha.

SPIKA: Haya endelea.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, sawa, ahsante.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba barabara ya Sanzatte inajengwa na ameleta ombi la kilometa 30, tumepokea ombi hilo na linafanyiwa kazi. Wakati huo huo, kilometa 25 zinajengwa kutoka eneo la Tarime kwenda Serengeti ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, mawazo yote ni mazuri, lakini kupanga ni kuchagua. Kadri tunavyopata fedha za kutosha, barabara hizo zitakamilika kwa wakati ili huduma iweze kupatikana katika eneo la Serengeti. Ahsante. (Kicheko)