Primary Questions from Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi (5 total)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka na wa kudumu wa kudhibiti wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Serengeti hasa Tembo na Simba ambao wamekuwa wakivamia vijiji na kuharibu mashamba pamoja na kuua watu?
NAIBU WAZIRI WA MADINI K. n. y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori umekuwepo kwa muda mrefu. Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni mwingiliano huo umeongezeka na kusababisha madhara kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuua mifugo na kuharibu mali nyingine za wananchi ikiwemo mazao. Changamoto hii ipo katika maeneo mengi nchini hususan yanayopakana na maeneo yaliyohifadhiwa kama ilivyo kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kuwepo kwa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali imeanza kutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu. Mpango huo unahusisha yafuatayo: -
i. Kutoa mafunzo yatakayowawezesha wanajamii kukabiliana na kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu;
ii. Kutoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya kujikinga na wanyamapori hao, na wananchi kuhamasishwa kufuga nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa; na
iii. Kutoa namba maalum za simu (toll free number) endapo matukio hayo yanajitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza Viwanja vya Ndege ndani ya Hifadhi ya Serengeti kwa kujenga Uwanja wa Ndege katika Mji wa Mugumu nje kidogo ya Hifadhi pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara ya lami ya Makutano Sanzate Natta na ile ya Tarime Mugumu Natta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri na Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kujenga Kiwanja cha Ndege cha Serengeti katika eneo la Mugumu, kitakachotoa huduma za usafiri ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Aidha, kiwanja hicho kitakapojengwa na kukamilika kitapunguza matumizi ya viwanja vya ndege ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwani ndege nyingi zitakuwa zikitumia kiwanja kitakachokuwa kimejengwa nje ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Makutano – Sanzate – Natta yenye urefu wa kilometa 90, ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea na umegawanyika katika awamu mbili. Sehemu ya kwanza ni Makutano – Sanzate yenye urefu wa kilometa 50; kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami zinaendelea na hadi Oktoba 2021 ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2022. Aidha, sehemu ya pili ni Sanzate – Natta yenye urefu wa kilometa 40; ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea. Hadi Oktoba, 2021 kazi za ujenzi zilikuwa zimefikia 7% na zinatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2022.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Barabara ya Tarime – Mugumu – Natta yenye urefu wa kilometa 122.97 itajengwa kwa awamu. Zabuni kwa ajili ya kupata Mkandarasi wa kujenga sehemu ya Tarime - Nyamwaga yenye urefu wa kilometa 25 zimefunguliwa mwishoni mwa Oktoba, 2021 na uchambuzi unaendelea ili kumpata Mkandarasi wa ujenzi. Serikali itaendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kusaidia Hospitali ya Wilaya ya Serengeti na Nyerere DHH kwa kuzijengea uwezo wa kutoa huduma bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 mpaka 2021/2022, imepeleka fedha Shilingi bilioni 2.36 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa ajili ya kuboresha huduma zinazotolewa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti. Fedha hizo zimetumika kujenga majengo saba (7) ya kutolea huduma ambapo majengo sita yamekamilika na yanatoa huduma na jengo moja la Wodi ya Mama na Mtoto lipo kwenye hatua ya ukamilishaji. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022, imepeleka katika hospitali hiyo watumishi 16 na vifaa na vifaatiba mbalimbali vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, Hospitali Teule ya Nyerere (Nyerere DDH) katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepokea vifaa tiba mbalimbali vya kutolea huduma za afya ikiwemo haematology machine, biochemistry machine na urine analyser. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Hospitali hii imetengewa bajeti ya kuajiri watumishi saba (7) wa kada mbalimbali za afya.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Wilayani Serengeti ili vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari wapate ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Serengeti ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya awali ikiwemo upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi pamoja na kuandaa michoro na makadirio ya gharama za ujenzi kwa kila chuo na ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara tu taratibu za manunuzi zitakapokamilika, nashukuru sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kudhibiti mafuriko katika Mto Mara kwa kuvuna maji kupitia Mabwawa na kujenga Skimu za Umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, tayari imezindua Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Environmental Master Plan for Strategic Intervention 2022-2032) ambao umeelekeza mikakati na shughuli endelevu zitakazoweza kufanyika katika maeneo hayo ni kama vile: kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji na kuhakikisha uwepo wa mtiririko wa uhakika katika mito ikiwemo Mto Mara, Mto Kagera, Mto Ruaha Mto Wami na Ruvuma; kuhamasisha matumizi sanifu kwa watumiaji wote wa Mto Mara, Kagera, Ruaha, Momba na Mto Ruvuma; na kuimarisha viwango vya maji katika vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mto Mara ni moja ya miongoni ya Mito mikubwa muhimu nchini Tanzania. Hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara nyingine za kisekta zitakaa na kuona namna bora ya kuvuna maji ili kudhibiti mafuriko, nakushukuru.