Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Robert Chacha Maboto (16 total)

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ahadi ambazo Hayati Dkt. Magufuli aliahidi wakati wa kampeni ilikuwa ni pamoja na kujenga soko kuu la Mji wa Bunda pamoja na stendi mpya.

Je, kati ya stendi na soko kuu, ahadi hii yenyewe itatekelezwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKO ANA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hapa nimeelezea kwa chini kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa TACTIC, uendelezwaji wa miundombinu katika miji yetu. Na ule uendelezaji wa miundombinu kwenye TACTIC haihusu barabara peke yake, ni pamoja na masoko, stendi, madampo ya taka yaani tunatengeneza mji kuwa wa kisasa. Kwa hiyo, hata hiki anachokizungumza kuhusu soko kuu pamoja na stendi mpya katika Mji wa Bunda nafikiri itakuwa ndani ya package katika mradi huu wa TACTIC ambao mara utakapotekelezeka ni sehemu ya huo mradi, ahsante sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makao Makuu ya TANAPA Kanda ya Magharibi yako Bunda; na kwa kuwa Halmashauri ya Mji wa Bunda ilitoa eneo kwa ajili ya kujenga ofisi zao za Kanda ya Magharibi. Je, ni lini TANAPA wataanza kujenga ofisi hizo? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimshukuru Mheshimiwa Robert Maboto kwa swali lake hilo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, TANAPA ina kanda nyingi nchi nzima na kila kanda inahitaji fedha ili tuweze kujenga miundombinu husika. Katika bajeti ambayo tutaileta mwaka huu tumeomba fedha kutoka Hazina ambazo ni mahsusi kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo Ofisi ya Kanda ya TANAPA pale Bunda.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina Kata 14 na wakulima wake mazao yao yameathirika sana na wanyamapori, hasa tembo; Kata ya Nyatwali, Bunda Store, Mcharo na Sazila:-

Je, ni lini Waziri atatembelea Halmashauri hii ili aweze kujionea uharibifu huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wabunge wote ambao wanazungukwa maeneo ya uhifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria ambayo tulishapitisha kwamba wananchi wanapokutana na kadhia hii ya tembo na wanyama wengine tunatoa kifuta machozi. Nampongeza Mheshimiwa Robert Chacha kwamba ameendelea kulizungumzia suala hili la wananchi wake kuhakikisha wanapata kifuta machozi, lakini pia nimwahidi kwamba, nitafika kwenye eneo hilo ili tuweze kuzungumza na wananchi. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Halmashauri ya Mji wa Bunda ni makutano kati ya barabara itokayo Ukerewe – Mwanza – Simiyu kwenda Sirari – Tarime – Musoma kuja Mwanza na Serengeti kuja Mwanza:-

Je, ni lini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi itaweka taa za barabarani za kuongoza magari ili kupunguza ajali zinazotokea eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, kwa sasa barabara zote zinazojengwa na zinazopita kwenye miji, katika mikataba lazima watengeneze barabara katika miji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpango upo sasa wa TANROADS kuhakikisha kwamba sehemu zote za miji ambazo zilikuwa hazina barabara za kuongozea magari kama alivyosema, wafanye usanifu ili tupate gharama yake na tuweze kuweka taa za kuongozea magari, hasa maeneo ambayo yana magari mengi. Kwa hiyo, study hiyo inaendelea. Naamini Bunda itakuwa ni sehemu ya wanufaika. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimu wa zao la pamba umefunguliwa tarehe 10 Mei na mategemeo ya wakulima ni kwamba wanapokwenda kuuza zao lao waweze kulipwa fedha zao.

Je, Wizara ya Kilimo imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inawasimamia wenye viwanda wasiende kukopa zao la wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magoto, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumetoa waraka kupitia Bodi ya Pamba, nunuzi yoyote anapochukua pama katika chama cha msingi ni lazima mkulima awe amelipwa ndani ya muda usiozidi saa 48 na mnunuzi yeyote atakayekwenda kinyume na hili tutamfutia leseni na kumuondoa kwenye database ya ununuzi wa pamba, hakuna kukopa pamba ya mkulima, hili ni la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili tumetoa bei dira ambayo wakulima ni lazima walipwe kiwango kisicho pungua bei hiyo, lakini wakati huo huo ushindani unaendelea, bei dira tuliosema Wizara ya Kilimo haitakiwi kupungua shilingi 1,050 bei ya chini ingawa bei inayoendelea sasa hivi ushindani umefika mpaka shilingi 1,100/1,150 na kila mnunuzi aweke pango la bei yake kwenye AMCOS ili mkulima anapopima pamba yake ajuwe bei ya siku hiyo ni shilingi ngapi na viongozi wa AMCOS wahakikishe wanamlipa bei iliyoko sokoni siku hiyo.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini, Alhamisi ya wiki iliyopita tembo wamekula mazao yao, hasa Kata za Bunda Stoo, Balili na Kunzugu. Wapo baadhi ambao wamefanyiwa tathmini ya mazao yao, je, ni lini Serikali itawalipa fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Robert Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kulipa malipo haya ya kifuta jasho na kifuta machozi na kulikuwa kuna malipo ya kipindi cha nyuma ambayo walikuwa wanadai na niliahidi hata kwa Mbunge mwenzie Mheshimiwa Esther Bulaya, kwamba nitafunga safari niende kwenye maeneo husika tukaangalie ni madai gani ambayo wanadai kisha Serikali iweze kuyalipa. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa maji Bunda Mjini ulikuwa wa thamani ya shilingi 10,600,000,000 fedha zilizokwisha kutolewa mpaka sasa ni shilingi 2,600,000,000 bado shilingi bilioni nane. Je, ni lini Serikali itamalizia fedha hizi ili mradi ule uweze kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maboto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi ule umeweza kupelekewa fedha hizi shilingi bilioni 2.6 na bado hizo shilingi bilioni 8 na fedha hizi tayari zipo kwenye mpango wa Wizara kuona kwamba tunaendelea kupeleka fedha. Ili kuweza kukamilisha mradi ule na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ameendelea kuifanikisha Wizara ya Maji, kwa kuongeza fedha tofauti na namna ambavyo tulipitisha kwenye bajeti yetu. Hivyo, mradi kama huu na wenyewe pia tunaupa jicho la kipekee kabisa kuhakikisha kwamba unakwenda kukamilika. (Makofi)
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali ililipa eneo la Viwanda na Uwekezaji pale Bunda Mjini kwa muda mrefu na wananchi wakahama kwenye eneo lile, lakini leo wameanza kurejea kwenye eneo lile. Ni nini mpango wa Serikali katika kulitumia eneo lile?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Robert Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo lile ambalo lilo pale, lipo chini ya EPZA kwa maana ya maeneo ya uwekezaji huru kwa ajili ya mauzo nje. Serikali tunaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuyaendeleza maeneo yote ambayo yapo chini ya EPZA likiwemo eneo hili la Bunda Mjini.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutalitekeleza au tutaanza kulifanyia kazi hivi karibuni katika eneo hilo la Bunda Mjini. Nakushukuru.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wizara ya Kilimo itasambaza lini mbegu za alizeti katika Halmashauri ya Mji wa Bunda?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Robert, Mbunge wa Bunda na Wabunge wote, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka jana tulisambaza jumla ya tani 2,000 za zao la alizeti za standard seed ambazo zilikumbana na changamoto na mwaka huu tutasambaza certified seed tani 2,500. Nitumie nafasi hii, kusema kwamba, halmashauri ambazo ziko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, zilete maombi na tukubaliane, mbegu hizo tunazozigawa kwa ruzuku ni namna gani fedha ile itarudi kwa sababu tutazigawa kwa ruzuku ya asilimia 50.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine ambao watakuwa tayari, tumeshafanya hivyo Mkoa wa Singida na maeneo mengine ambao watakuwa tayari hasa Ukanda wa Kati na Ukanda wa Kanda ya Ziwa ambako uzalishaji wa alizeti unafanya vizuri zaidi.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kati ya hawa 21 hawa Nane ndiyo wako kwenye source ya eneo lenyewe la uchimbaji, ndiyo maana hawajakubaliana na masharti ya wale Wawekezaji. Wizara ningewaomba wao wafanye kila linalowezekana ili kuwaweka vizuri, kwa sababu wale mashamba Nane waliobaki ni kwa sababu hawaoni kama wanapata haki zao zinazowastahili.

Swali la pili, ningeomba Mheshimiwa Waziri mara baada ya Bunge hili kuisha tuende nae mpaka kwenye eneo la tukio ili akajiridhishe yeye mwenyewe. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza, kama nilivyokwishasema katika jibu langu la msingi, kwamba Mahakama imetoa fursa waendelee kujadiliana na endepo majadiliano hayo hayatazalisha ridhaa na wao waingie kwenye ubia kama wenzao, taratibu za kisheria, Sheria ya Madini Sura ya 123, Kifungu cha 97 kinachoeleza jinsi ambavyo suala la compensation, reallocation na resettlement, yaani fidia au kuhamishwa na kuwekewa sehemu mbadala au kujengewa makazi mengine utafuatwa kwa ushirikiano na Wizara ya Ardhi na Mthamini Mkuu wa Ardhi wa Serikali. Kwa hiyo, tumejipanga katika kuhakikisha kwamba maridhiano ama yafikiwe au sheria ifuatwe ili madini hayo yenye thamani katika maeneo hayo yaweze kuchimbwa na kunufaisha Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, ni mtu wa field sana niko tayari baada ya Bunge hili tutapanga ratiba pamoja nae, tuone siku muafaka ambayo naweza kufika ili tukashuhudie maeneo hayo na kumaliza mgogoro uliopo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kisangwa kilichopo Bunda ndicho chuo pekee kinachotoa fani mbalimbali za ufundi na tatizo kubwa pale ni mabweni.

Je, ni lini Serikali itatusaidia kupata mabweni hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maboto Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto kwenye Vyuo vyetu vya FDC lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 tumefanya ukarabati pamoja na upanuzi wa vyuo hivi vya FDC 54 kote nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie katika kipindi kijacho tunaendelea na upanuzi huo ambapo tunaamini kabisa, chuo hiki cha Bunda kitazingatiwa katika ukarabati na upanuzi pamoja na haya mabweni tutaweza kuyafikia. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, barabara ya Buramba – Bunda - Nyamuswa inayotekelezwa kwa kiwango cha lami wananchi wamebomolewa nyumba zao pale. Ni lini Serikali itawalipa fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maboto Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ilishafanyika, wananchi walishaainishwa na sasa hivi Serikali inafanya kupitia yale malipo ili waweze kulipa fidia hiyo.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Halmashauri ya Mji wa Bunda kuna wananchi wanaishi zaidi ya kilometa 40 kuja Kata ya Bunda Store ambapo ndipo kituo cha kuuzia mahindi kilipo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kituo kingine cha usambazaji mahindi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chacha Maboto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba kutokana na mahitaji hayo nitatoa maelekezo kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula kuhakikisha wanaongeza kituo kingine zaidi ili wananchi wasitembee umbali mrefu.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini mwaka 2021/2022 ambao mashamba yao yaliliwa mashamba yao hawajalipwa fidia yao. Je, Serikali itawalipa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maboto Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumejitahidi sana kupunguza madai ya kifuta machozi na kifuta jasho, kwa upande wa Mkoa wa Mara ninaahidi tu kupitia Bunge lako hili ndani ya kipindi hiki tunachoendelea na bajeti tutaenda kumalizia madai haya. Ahsante.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nina swali moja la nyongeza. Kutokana na tatizo hili kuwa kubwa katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na hasa kwa sababu kuna kata tatu, nne Kata ya Bunda Stoo, Kata ya Kunzugu, Kata ya Balili na Kata ya Mcharo ambazo zimepakana na Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti tatizo ni hili hili. Je, Serikali itakuwa tayari na yenyewe kuweka mipaka kwenye maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kuhakikisha kwamba mipaka yote katika maeneo ya nchi yetu inatambulika vizuri na hizi kata tatu alizozitaja ambazo zinapatikana na Hifadhi ya Serengeti. Kwanza, nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya hii na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kufika katika kata hizi na kuangalia mipaka hii kama iko sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama iko sahihi, basi wahakikishe pillar zinazoenda kuwekwa kwenye kata ile ambayo nimetoka kuitaja kwenye majibu yangu ya msingi, basi wahakikishe wanaweka pia pillars katika mipaka hii kati ya kata hizi tatu za Bunda Mjini na Serengeti.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Kata ya Guta, Mtaa wa Kinyambwiga kuna uchimbaji wa madini pale lakini kwa sasa kuna mgogoro kati ya wenye mashamba na wenye leseni. Je, ni nini kauli ya Serikali kwenye mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kwa ridhaa yako namuomba Mheshimiwa Mbunge alete swali hilo kama swali la msingi halafu tutalijibu hapa Bungeni. (Makofi)