Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Charles Muguta Kajege (6 total)

MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itazikarabati barabara za Jimbo la Mwibara ambazo zimeharibika sana ili kuruhusu mawasiliano kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mugeta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ina majimbo mawili ya Uchaguzi ambayo ni Bunda Vijijiini na Mwibara yenye mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 527.55. Serikali imekuwa ikitenga fedha za matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambapo katika mwaka wa fedha 2019/20 shilingi milioni 546.87 zilitumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara na shilingi bilioni 708.56 zimeidhinishwa katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo la Mwibara katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 28.2 na makalvati 11 kwa gharama ya shilingi milioni 237. 43. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/ 21 shilingi milioni 460.44 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu kilomita 54.5 na makalvati 29 ambapo utekelezaji unaendelea.

Mheshimwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za ujenzi na matengenezo ya barabara za Wilaya ya Bunda na nchini kote kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuipunguzia mzigo TARURA kwa kuzihamishia TANROADS barabara za Bulamba – Karukekere – Nakatubai – Igunchi – Mwitende na Busambara - Mugara zilizopo katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mugeta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya kupandisha hadhi barabara kutoka barabara za Wilaya na kwenda barabara za Mikoa yanatakiwa kuwasilishwa na kujadiliwa kwenye Vikao vya Bodi ya Barabara ya Mkoa. Endapo Bodi itaridhia mapendekezo hayo, yanatakiwa kuwasilishwa kwa Waziri mwenye Dhamana na barabara ambaye ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, hatua inayofuata ni maombi hayo kupitiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Kamati ya Kitaifa ya Kupandisha Hadhi Barabara ili kuona kama yanakidhi vigezo na Kamati kuridhia au kukataa kupandishwa hadhi barabara husika. Hivyo, nashauri utaratibu huo ufuatwe katika maombi ya kupandisha hadhi barabara za Bulamba – Karukekere - Nakatubai – Igunchi - Mwitende na Busambara - Mugara zilizo katika Jimbo la Mwibara.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA K.n.y. MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza dhamira yake ya kuwatua Wanawake ndoo kichwani kwa kuwasogezea huduma za maji safi na salama karibu na makazi yao katika Jimbo la Mwibara?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini sisi Wizara ya Maji. Nataka niahidi Waheshimiwa Wabunge na watanzania mimi Jumaa Aweso na timu nzima ya Wizara ya Maji, hatutokuwa kikwazo kwa watanzania kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya timu nzima ya Menejimenti ya Wizara ya Maji tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Spika Dkt. Tulia Ackson kwa kuaminiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi Wizara ya Maji tutatoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha tunafanikisha Bunge hili letu tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajenge, Mbunge wa Mwibara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Serikali ni kuhakikisha kuwa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ni ya uhakika na endelevu. Kwa sasa, upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Bunda ambapo Jimbo la Mwibara lipo wastani wa asilimia 69 kupitia visima virefu na vifupi 237 vya pampu za mkono, chemchemi moja na skimu za mtandao wa bomba tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaendelea na mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Mwibara kwa kutekeleza miradi mipya ya Buzimbwe, Bulendabufwe, Igundu, upanuzi wa mradi wa maji Iramba kwenda vijiji vya Mugara, Nyarugoma na Muhura. Kazi zinazofanyika kwa miradi mipya ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 135,000, ujenzi wa vituo 28 vya kuchotea maji, ujenzi wa ofisi moja ya jumuiya ya watumiaji maji na ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house).

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kazi zinazofanyika kwa mradi wa upanuzi ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 18.6, ununuzi na ufungaji wa pampu mpya (surface pump). Miradi hii kwa sasa imefikia wastani wa asilimia 15 za utekelezaji na inatarajia kukamilika mwezi Juni, 2022. Kukamilika kwa miradi hii kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wilaya ya Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kuwa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Bunda inapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 itakamilisha usanifu wa mradi wa maji wa Kisorya kupitia chanzo cha maji cha Ziwa Vicktoria. Mradi huo umepangwa kuhudumia vijiji 12 vya Sunsi, Masahunga, Kisorya, Nambubi, Mwitende, Nansimo, Nambaza, Busambara, Mwibara, Kibara A, Kibara B na Kasahanga. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kutekelezwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 baada ya usanifu kukamilika. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kukarabati Shule za Msingi za Nansimo, Kenkombyo, Kitengule na Namibu zilizopo katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege Mbunge wa Jimbo la Mwibara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Shule 2,147 shule za msingi kongwe nchini ambazo zilianzishwa kabla ya kupata Uhuru mwaka 1961. Hali ya miundombinu ya shule hizo ni mseto zikiwemo zenye hali nzuri na nyingine zenye miundombinu chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeanza kufanya tathimini ya hali ya miundombinu ya shule zote za msingi kupitia mradi wa BOOST ili kubaini mahitaji ya ujenzi wa miundombinu mipya ya shule na hali ya uchakavu wa miundombinu iliyopo. Tathimini hiyo imeanza mwezi Aprili, 2022 na itakamilika mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya tathimini hiyo yatatumika kuandaa mpango wa uendelezaji na ukarabati wa miundomibinu ya Shule za Msingi kwa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 zikiwemo Shule za Msingi Nansimo, Kenkombyo, Kitengule na Namibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ya shule kongwe za msingi kadri fedha zitakapopatikana.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga skimu za umwagiliaji Kata za Kisorya, Igundu, Kwiramba, Namuhura, Butimba na Kasuguti - Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Mwibara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na zoezi la kubaini maeneo yote yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini ili kuyapima na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata sgharama halisi za kutekeleza miradi hii kabla ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Tume imejipanga kuyafikia maeneo mbalimbali yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini ikiwemo maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji yaliyopo ndani ya Jimbo la Mwibara ili kuingiza kwenye mpango wa utekelezaji, nakushukuru.
MHE. CHARLES M. KAJEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha majengo ya shule na zahanati ambayo yalijengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Mwibara?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles Muguta Kajege, Mbunge wa Jimbo la Mwibara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 287.5 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 14 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi milioni 240 kwa ajili ya kukamilisha vyumba vya madarasa 14 katika Jimbo la Mwibara pamoja na ukamilishaji wa maabara tatu za kemia, baiolojia na fizikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imekwisha peleka kwenye Jimbo la Mwibara shilingi milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha maboma mawili ya zahanati za Sozia na Ragata. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/23 shilingi milioni 88 imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Nyamitwebiri.