Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Daniel Baran Sillo (19 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa ujumla kwa kazi nzuri sana katika sekta mbalimbali hapa nchini, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri sana wanayoifanya katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Hii ni pamoja na hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri aliyowasilisha leo asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Wizara kwa kazi nzuri ya kuunganisha mikoa ya nchini kwetu kwa mtandao wa lami ikiwepo na Mkoa wangu wa Manyara ambao leo hii unaunganisha Mikoa ya Arusha, Singida na Dodoma. Zamani kutoka Babati tu kuja Dodoma ilikuwa ni saa nne mpaka siku tatu, lakini leo hii ndani ya saa mbili hadi tatu unafika Makao Makuu ya nchi hapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Wizara kwa kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini kwa ununuzi wa ndege nane na hivi karibuni tunatarajia ndege nyingine tatu, moja ikiwa ni ndege ya mizigo. Hii ni hatua nzuri sana, tunaipongeza sana Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Wizara kwa kuimarisha usafiri wa majini ikiwa ni ujenzi wa meli za mizigo na abiria katika maziwa makuu hapa nchini. Ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Wizara lazima tuipongeze sana. Hii inaenda sambamba na uboreshaji wa huduma za bandari katika Bandari ya Dar-es-Salaam, Tanga pamoja na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye Mkoa wa Manyara. Mkoa wa Manyara una barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kilometa 1,656. Kati ya hizo barabara kuu ina kilometa 207, lakini zilizobaki kilometa 1,449 ni barabara za mkoa ila kilometa ambazo zina lami ni kilometa 41 tu kwa mkoa mzima. Nadhani Kiteto kilometa sijui mbili, kule kwangu kilometa tisa, kwa hiyo, tuna kazi kubwa sana Wizara ya Ujenzi kuhakikisha kwamba, inajenga barabara za lami katika Mkoa wetu wa Manyara ambao una miradi mingi ya maendeleo, ni mkoa wenye utalii, wakulima na wafugaji wa kutosha. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iangalie sana Mkoa huu wa Manyara kwa jicho la pili kwa upande wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jimbo la Babati Vijijini kuna barabara ambazo ziko kwenye Ilani ya Uchaguzi ambazo ni mkataba kati ya Serikali na wananchi wake. Barabara ya kwanza ni kutoka Dareda mpaka Dongobesh, kilometa 60. Bahati nzuri barabara hii upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika, alikiri Mheshimiwa Naibu Waziri wakati akijibu swali langu la msingi, kwa hiyo, sina mashaka na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa utendaji mzuri wa Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi, naamini barabara hii kwenye bajeti ya 2021/2022, itatengewa fedha na itaanza kujengwa, sina mashaka na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inaunganisha wilaya mbili; Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Babati, lakini inapita kwenye kata ambazo zina uchumi mkubwa sana. Kuna wakulima kule wakubwa wa vitunguu maji, vitunguu saumu, mbaazi, ulezi na kadhalika. Kwa hiyo, naamini Mheshimiwa Waziri atakuwa ameipata hii vizuri, ili kuhakikisha kwamba, wananchi hao wanapata barabara hii kwa ajili ya manufaa makubwa, licha ya usafiri, lakini pia kwa ajili ya uchumi wa maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ya pili ni kutoka Mbuyu wa Mjerumani kwenda Wilaya ya Mbulu. Niipongeze sana Wizara imejenga daraja kubwa sana la bilioni 13, Daraja la Magara. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika pale amejionea, lakini kinachosikitisha upande huu wa Mbuyu wa Mjerumani mpaka Darajani barabara ni mbovu mno na kutoka darajani kwenda upande wa Mbulu barabara ni mbovu mno, daraja limebaki kuwa la utalii wa ndani na umaarufu wa kupiga picha. Naomba sana Wizara itilie mkazo barabara hii ya Mbuyu wa Mjerumani mpaka Mbulu, ni ukanda mkubwa wa kilimo cha mpunga, waliofika pale Magugu wanajua mpunga ule unazalisha wali mtamu kweli kweli. Naomba sana Wizara iliangalie hili, tuna wakulima wa mahindi, mbaazi na kadhalika, ni barabara ambayo ina manufaa makubwa sana kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kutoka darajani kwenda upande wa Mbulu barabara ni mbovu mno daraja limebaki kuwa la utalii wa ndani na maharusi kupiga picha. Naomba sana Wizara itilie mkazo barabara hii ya Mbuyu wa Mjerumani mpaka Mbulu ni ukanda mkubwa wa kilimo cha Mpunga waliofika pale Magugu wanajua Mpunga wali mtamu kweli kweli, naomba sana Wizara iliangalie hili, tuna wakulima wa mahindi mbaazi nakadhalika ni barabara ambayo inamanufaa makubwa sana kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni barabara ya Babati inapita Galapo Orkesument mpaka Kibaya kule Kiketo ina kilometa 225 ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025 niiombe sana Serikali iangalie barabara hizi kwa jicho la pili. Kuna muonekano mkubwa sana wa utalii lakini pia wakulima na wafugaji na itasaidia pia usafiri na usafirishaji wa wananchi wetu hawa kwa hiyo niiombe sana Wizara iangalie barabara hizi ambazo pia ni mkataba tumejiwekea sisi na wananchi wetu kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Manyara, Mkoa wetu wa Manyara kama mnavyoujua wengi ni Mkoa wa Utalii Mkoa mkubwa sana wa Kilimo, Ufugaji na kadhalika. Naomba sana Wizara ianze mchakato wa Ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Mkoa wa Manyara ni Mkoa Mkubwa unafursa nyingi za kiuchumi. Kwa hiyo, ninaomba Wizara kwakweli ilichukulie suala hili kwa uzito maana tunauhitaji sana wa kuwa ujwanja huu wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo mimi nikushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanyia taifa letu, na sisi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, kwamba kuna kazi kubwa imefanyika katika majimbo yetu kwenye miradi mbalimbali ya maji, afya nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais lakini ikitokea pia nimpongeze Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia miradi mbalimbali ya Serikali pamoja na hotuba yake nzuri aliyotoa tarehe 6 mwezi huu katika Bunge lako Tukufu. Bajeti ambayo imeonyesha muelekeo wa Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia kwangu nitajielekeza katika maeneo makuu matatu. Eneo la kwanza ni Eneo la kilimo, eneo la pili ni migogoro ya ardhi, tatu ni ujenzi au uwekezaji katika balozi zetu za nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Sekta ya Kilimo. Ni kweli kwamba tunafahamu sekta hii ya kilimo imeajiri Watanzania nguvu kazi zaidi ya asilimia 65, na asilimia 90 ya walioajariwa katika sekta hii ni wakulima wadogo na wa kati ambao bado hawana uwezo wa kupata mikopo katika Benki mbalimbali ikiwemo Benki yetu ya Kilimo. Kwa hiyo, wanategemea sana ruzuku ya Serikali ili waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba wakulima wetu wengi wanafanya kilimo cha kujikimu; kilimo cha chakula tu, lakini siyo kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana inatakiwa ifanyike ndani ya Serikali kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanawezeshwa ili wafanye kilimo chenye tija, kwa maana ya kilimo cha chakula pamoja na kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu, takwimu zinasema Sekta ya Kilimo inachangia karibia asilimia 27 pato la Taifa, pia inachangia zaidi ya asilimia 60 ya malighafi viwandani, lakini mauzo ya nje ya nchi ni takribani Dola za Kimarekani bilioni 1.2 kwa mwaka. Sekta hii ndiyo inayolisha asilimia 100 ya chakula hapa nchini, kwa hiyo, ni sekta muhimu katika maendeleo ya Taifa letu na mustakabali mkubwa wa wananchi wetu. Hata hivyo, sekta hii inakua kwa wastani wa asilimia nne hadi tano kwa mwaka. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana ya kufanyika ndani ya Wizara ya Kilimo ili tuweze kuwakwamua wananchi wetu katika sekta hii muhimu. (Makofi)

Mheshimu Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, kuna umuhimu mkubwa sana kuwekeza katika sekta hii muhimu ya kilimo. Tuna mpango wetu wa Taifa wa Uchumi Shirikishi. Bila kuwekeza kwenye kilimo itakuwa ni ndoto kufikia uchumi shirikishi. Najua Waziri wetu wa Kilimo ana mipango mizuri sana kwenye sekta hii, namwomba sana aangalie sekta hii kwa jicho la pili ili kuhakikisha kwamba tunafikia uchumi shirikishi kwa kuiwezesha sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira haya basi, kazi kubwa ya Serikali ni kuandaa mazingira, maana tunaamini Serikali pekee haiwezi kufanya kazi hii ya kilimo lazima tushirikishe na sekta binafsi. Tuna mfano mzuri wa nchi yetu ya jirani hapo Zambia, Zambia leo kuna sekta binafsi imewekeza sana kwenye kilimo na kilimo kimefanikiwa sana. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Serikali kuandaa mazingira mazuri ya kuwezesha sekta binafsi kushiriki katika suala zima la kilimo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia sekta mbalimbali, sekta kama ya nishati pamoja na miundombinu, zinachangia sana katika pato la Taifa, ni kwa sababu Serikali imewekeza. Kwa hiyo, hata sekta ya kilimo hii ikiwezeshwa, basi inaweza ikachangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Serikali ielekeze kwenye kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji. Manufaa ya uzalishaji ni kama ifuatavyo: moja, unaongeza ajira kwa Watanzania, unaongeza malighafi za viwandani, unakuza biashara ya nje na ya ndani; na kupanua wigo wa kodi. Tumekuwa tukilalamika kwamba walipa kodi tunawarudia wale wale; tukiweza kwenye sekta za uzalishaji ni wazi kwamba tutapanua wigo wa walipa kodi na baadaye Serikali ipate mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu sasa kwenye sekta hii ya kilimo, kwanza kama nchi lazima tujielekeze kwenye uzalishaji na siyo kwenye matumizi. Mambo ya kufanya ni kama ifuatavyo: Moja, ni kujenga au kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ili kuwe na kilimo cha msimu wote wa mwaka; la pili, lazima tuainishe maeneo maalum ya kilimo na aina ya mazao katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka kulikuwa na crop map hapa nchini, ni vizuri sana tukaifuata ili tuweze kuzalisha, tuwe na maeneo mahsusi kwa ajili ya mashamba, pia tuwe na aina ya mazao husika. Eneo lingine, lazima tuboreshe utafiti ili tuweze kuzalisha mbegu bora hapa nchini. Leo hii tunalia kilo moja ya mbegu ni Shilingi 12,000/=; gunia la mahindi ni Shilingi 20,000/=. Haileti tija kabisa! Kwa hiyo, kuna haja kubwa sana ya kuendeleza utafiti na hatimaye kuzalisha mbegu bora hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kutafuta masoko ya uhakika kwa mazao ya wananchi wetu. Nitatoa mfano, Mkoa wa Manyara au Babati Vijijini kuna mashamba makubwa ya mbaazi, lakini wakulima wanalima na baada ya kuvuna, hawana pa kuuza. Kwa hiyo, naomba sana Serikali itafute masoko ya uhakika ya mazao yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuwa na mfuko maalum wa kuwalinda wakulima wetu hasa wakati bei za pembejeo zinapopanda na wakati bei za mazao yao zinavyoshuka. Mfuko utawasaidia sana wananchi wetu kujikumu na kuendelea na kilimo cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kujenga maghala ya kutosha ili kuokoa upotevu wa mazao. Taarifa inasema kuwa tunapoteza karibia asilimia 30, postharvest loss. Nina imani kubwa sana kwamba tukijenga maghala ya kutosha, basi hili litapungua sana. Kwenye eneo hili, naipongeza sana Serikali, imejenga maghala kule Babati, Sumbwawanga na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni migogoro ya ardhi kati ya wawekezaji na wananchi wetu. Naipongeza Serikali, iliundwa timu ya Mawaziri nane, walizunguka nchi nzima kutatua migogoro hii, lakini bado kuna migogoro katika maeneo yetu kati ya wawekezaji na wananchi wetu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, bado kuna changamoto hii ya migogoro kati ya wawekezaji na wananchi wetu na katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua sana Sera ya Uwekezaji ni nzuri, inaleta ajira kwa Watanzania, lakini pia inaleta mapato kwa maana kulipa kodi ya Serikali. Nitatoa mfano, kule kwangu Babati kuna migogoro kati ya Kata ya Kiru kule Magara, lakini pia kiwanda cha Minjingu na wananchi wa vijiji vya City na Minjingu. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijielekeze katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kati ya Hifadhi na Vijiji vyetu. Natambua kazi kubwa ya Serikali iliyofanya kutatua migogoro kati ya Hifadhi za Taifa na vijiji, lakini bado changamoto ipo. Naiomba sana Serikali, Mawaziri washirikiane na Wabunge ambapo sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi, ndio tunajua migogoro iko wapi? Tukishirikiana kwa pamoja, naamini tukienda pamoja, basi migogoro hii itapungua au itakwisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ni ujenzi au uwekezaji katika Balozi zetu nje ya nchi. Natambua Balozi zetu zina viwanja vingi nje ya nchi; na ninaipongeza Serikali imeanza kujenga katika Balozi zetu kule Oman, lakini bado kuna viwanja havijaendelezwa. Nitatoa mfano kwa nchi ya Zambia. Zambia kwenye Balozi yetu kuna viwanja karibia nane na vipo kwenye very prime area. Kwa hiyo, nadhani tukijenga humo tutapata fedha za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna njia tatu; kuna mortgage financing, kuna mifuko yetu ya kijamii na PPP. Serikali ikijielekeza huko tutapata fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya, sekunde tatu malizia.

MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa nafasi hii, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, nami niweze kutoa mchango wangu katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Pamoja na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka huo 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Taifa letu pamoja na maono makubwa ikiwemo pia Mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka wa Fedha unaokuja wa 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Profesa Kitila, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa taarifa nzuri ambazo wamewasilisha ndani ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, nimpongeze Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mheshimiwa Kigua pamoja na Wajumbe wa Kamati, kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati wa uchambuzi wa Taarifa hizi ambazo leo zinawasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo machache. Jambo la kwanza ni ukusanyaji wa mapato. Tathmini ya ukuaji wa mapato ya ndani kwa maana ya vyanzo vyetu vya ndani kwa miaka mitano 2017/2018 hadi 2022/2023 inaonesha kwamba, mapato ya kodi yamekua kwa asilimia 10.5. mapato yasiyo ya kodi yalikua kwa asilimia 2.5. mapayo ya halmashauri yalikua kwa asilimia 14.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini makisio ya ukuaji wa jumla ya mapato yetu ya ndani kwa vyanzo vyote kwenye mpango unaopendekezwa wa 2024/2025 unatarajiwa kuwa ni asilimia 10.5. Hili linawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 Kifungu cha 18_B(3) Chama kinaielekeza Serikali. Naomba ninukuu; 18_B(1). “Kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiwemo kuibua vyanzo vipya vya mapato, kuongeza idadi ya walipa kodi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara na kukusanya maduhuli yote kwa kuitumia mifumo ya kielektroniki.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufiklia malengo haya ya ukuaji wa mapato ya ndani kwa wastani wa asilimia 10.5 kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, lakini ili mapato ya kodi yaweze kuchangia ile asilimia 12.4 kwenye mapato ya taifa kama ilivyowasilishwa kwenye mapendekezo. Vile vile, ili Pato la Taifa liweze kukua kwa asilimia 5.8 kama ambavyo imependekezwa kwenye Mpango. Pia, bajeti inayotarajiwa ya trilioni 47.4 kati ya hizo trilioni 34.4 Ikiwa ni mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 70. Yako mambo ya msingi ambayo kama Taifa lazima tuyafanye: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha mifumo yote ya ukusanyaji mapato hapa nchini. Tuna mifumo mingi. Kwa mfano, Mfumo wa Kodi za Ndani ambao ni Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS). Mfumo wa TRANCIS wa ushuru wa forodha. Tuna Mfumo wa Tausi ambao uko kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya halmashauri zetu. Vile vile, tuna Mfumo wa Bandari ambao unaitwa Terminal operating system, tuna GEPG nakadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo hii yote inafanya kazi kubwa ya kukusanya mapato ya Taifa letu. Jambo kubwa la kufanya hapa ni kuhakikisha mifumo hii yote inakuwa imara ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea kama Taifa katika kulifikia Pato la Taifa pamoja na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa, uimara wa mifumo hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba mifumo yote hii inasomana, kwa maana ya kwamba mifumo ya Serikali za Mitaa isomane na mfumo wa TRA, Bandari na mifumo yote. Kwa hiyo, tukiwekeza kwenye mifumo hii yote ikasomana nina imani kubwa kabisa haya yote tunayoyatarajia kama Taifa tutayafikia katika mwaka wa fedha 2024/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia ni upande wa sekta ya utalii. Sekta ya utalii inachangia takribani asilimia 14 kwenye Pato la Taifa. Vile vile, inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa huu wa miaka mitano ambao tunao, wa mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026, ukisoma ule ukurasa wa 102, mpango katika sekta ya utalii umeelekeza kwamba, kuendeleza mazao mapya ya utalii kwa ajili ya ukuaji wa uchumi. Pili, kuendeleza Kanda ya utalii kusini mwa Tanzania. Lengo ni kukuza sekta hii muhimu sana katika ukuaji wa uchumi kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2025 kifungu kile cha 67 kwenye ukurasa wa 11, kimeweka malengo kwamba, kufikia wastani wa watalii milioni tano ifikapo 2025 lakini pia mapato kutokana na sekta hii ya utalii kufikia dola bilioni sita ifikapo 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya si rahisi kuyafikia bila kuwa na mipango thabiti kwenye mipango yetu ya Taifa. Mambo ya kufanya: -

(i) Kuhakikisha kwamba tunatangaza vivutio vyote ndani na nje ya nchi yetu ili kuvutia watalii wa kutosha katika Taifa letu na kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

(ii) Kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji hasa kwenye sekta ndogo ya malazi. Tunapozungumza kwenye sekta ya malazi katika Taifa letu kwenye sekta hii ya utalii tuna vitanda chini ya 150,000. Hivi ni vichache sana ukilinganisha na hali ya utalii pamoja na fursa zilizopo katika Taifa letu. Lakini nchi Jirani ya Kenya kuna vitanda zaidi ya milioni moja. Kwa hiyo, utaona jinsi ambavyo tuko nyuma katika kuwekeza kwenye sekta hii ya utalii, hasa hoteli zenye hadhi mbalimbali za kuhakikisha kwamba watalii wanafika kwenye nchi yetu na kuchangia Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ikiwekewa mikakati mizuri katika Mpango tunaopendekeza, kwanza itachochea ukuaji wa sekta yenyewe, pili, itapunguza nakisi ya urali wa malipo ya huduma, tatu, itaongeza mchango katika Pato la Taifa, kukuza uchumi na utalii katika Bajeti yetu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Serikali katika mpango huu tunaupendekeza, tuhakikishe tunaweka mikakati mizuri sana katika sekta hii ya utalii ambayo ukiwekeza unapata fedha za kigeni mara moja, na haichukui muda mrefu. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Mipango mtu makini sana (Profesa) na Waziri wetu wa Fedha, mhakikishe kwamba kwenye Mpango huu unaokuja tuweke mikakati mizuri sana katika sekta hii muhimu sana ya utalii hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni tathmini ya Mpango wa Tatu wa Maendelo ya Taifa huu wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026. Ili ujue unakokwenda ni lazima ujue ulipotoka, ulipo, ili ujipange vizuri kwa safari ya mbele. Mpango huu unaopendekezwa ni Mpango wa nne ambapo tayari tumekwishatengeneza mipango mitatu. Kwa kuwa tumekwishatekeleza mpango huu zaidi ya nusu, kwa maana tayari tumekwishatekeleza mipango miatatu, iko haja ya kufanya tathmini ya vipaumbele vyote tulivyovipanga kwa miaka mitatu katika kila sekta tumekeleza kwa kiasi gani ili tujipange kwa mipango inayokuja. Kwamba ni wapi tumefeli, wapi tumefanikiwa ili tujipange vizuri katika mipango iliyobaki, kwa maana ya mpango wa nne na mpango wa mwisho, ule wa tano, wa 2025/2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungefanya midterm revue ya Mpango huu itasaidia sana kuona ni nini tumefanya, nini tumekwama wapi na kwa sababu gani? Mpango huu ni wa Mwisho kwa maana ya Dira ya 2025. Kwa hiyo, tukifanya tathmini ya uhakika kwa Mpango huu unaokwisha tutakuwa tumejenga msingi imara wa kuweka dira mpya ya 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaamini kabisa kwamba tukijipanga vizuri, nchi yetu ina fursa nyingi sana na Watanzania wako tayari kufanya kazi. Kazi kubwa ni kupanga na kusimamia fedha zote za uchumi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa fursa; naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Kilimo, Wizara ambayo inachangia asilimia 27 ya pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni lakini inaajiri Watanzania wasiopungua asilimia 65.

Mheshimiwa Spika, Sera ya Serikali sasa ni Serikali ya viwanda na ni ukweli kwamba raw materials au malighafi zaidi ya asilimia 60 zinatoka kwenye kilimo. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iwekeze kwenye kilimo, ikishawekeza kwenye kilimo maana yake tunapata viwanda vya kutosha, tukishapata viwanda tunaajiri Watanzania wengi, lakini pia Serikali inapata kodi. Ni ukweli usiopingika kwamba kilimo ni biashara ya chakula na ajira. Kwa hiyo niiombe sana Wizara iwekeze kwenye kilimo ili tupate na wigo wa kodi pia katika Taifa letu, (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kwa kifupi pia kuhusu wakulima wadogo hasa wa vijijini. Wakulima wa vijijini toka anaandaa shamba hadi anavuna hajawahi kutembelewa na Afisa Ugani hata mmoja. Hii ni changamoto kubwa sana kwa wakulima wa vijijini, watabaki kulima kilimo cha kujikimu, hawatapata kilimo cha tija. Kwa hiyo niiombe sana Wizara iangalie sana wakulima wa vijijini, wanateseka kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, kuna mashamba yasiyoendelezwa; nchi yetu ina sera ya kubinafsisha mashamba kwa wawekezaji. Ni kweli kabisa tunawahitaji wawekezaji maana wakiwekeza watalipa kodi na wataajiri Watanzania, lakini kuna mashamba mengi katika maeneo mbalimbali nchini ambayo mtu amebinafsishiwa lakini anatumia labda robo tatu au robo tu ya eneo lote. Eneo lililobaki linabaki wazi wakati kuna wakulima wanaozunguka eneo hilo wanateseka hawana eneo la kulima. Naomba sana Wizara hii isaidiane na Wizara ya Ardhi, mashamba haya ambayo hayajaendelezwa Serikali iwagawie wananchi waweze kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mifano kule kwangu Babati Vijijini; kuna Bonde la Kiru, Kata za Kisangaji na Magara, kwenye msimu huu wa kilimo juzi watu walikatana mapanga kwenye Kijiji cha Magara, shamba lilikuwa na mwekezaji, mwekezaji haonekani, watu wamevamia. Kwa hiyo niiombe sana Serikali itatue migogoro hiyo ili wananchi wapate maeneo ya kulima.

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie masoko ya mazao. Wanachi wetu wanateseka sana na masoko ya mazao yao. Mfano mdogo tu wa kilimo kama cha mahindi, mbegu ya mahindi kilo mbili inauzwa Sh.13,000, lakini leo gunia linauzwa Sh.18,000 mpaka Sh.20,000 gunia la kilo 100. Niiombe sana Wizara ya Kilimo iwasaidie Watanzania hawa wanyonge hasa wa vijijini, wanateseka mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri yangu ya Babati Vijijini kuna wakulima wazuri sana wa mbaazi. Mwaka jana msimu uliopita mbaazi zilibaki shambani, hakuna pa kuuza kilo Sh.200, sijui Sh.300, mkulima ameteseka mwaka mzima, kwanza hajashauriwa na wataalam wa kilimo na pia masoko asipatiwe. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ijielekeze kutafuta masoko ya mazao ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, kule kwangu kuna Vijiji vya Nar, Madunga, kuna wakulima wazuri sana wa vitunguu, lakini hawapati ushauri. Wanabaki kuhangaika na virobo heka vyao. Hii haiwasaidii, naomba sana Wizara iwasaidie wananchi hawa wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kupanga ni kuchagua, niiombe Wizara hii ya Kilimo ijielekeze kuchagua kuwekeza kwenye kilimo, nchi hii itatoka hapa itasonga mbele, wananchi watasogea mbele katika mapato yao na umaskini utapungua kwa wananchi wetu hasa wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika Wizara hii ya Maji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuongoza Taifa letu kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri wa Maji pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya katika sekta hii ya maji. Pia naipongeza Wizara kwa miradi mikubwa ya maji katika Jimbo la Babati Vijijini hasa miradi ya Darakuta - Magugu hadi Mwada; Mradi wa Mayoka - Minjingu, Vilima Vitatu, Madunga na maeneo mengine. Fedha za UVIKO zimesaidia mradi wa maji wa Bashnet na Secheda.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara itekeleze ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya mradi wa maji wa Darakuta-Magugu-Mwada hadi Minjingu.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Dareda; mradi mkubwa wa Ziwa Manyara ambao utahudumia kata zote za Tarafa ya Bashnet.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Kata za Gidas, Duru, Riroda na Endadosh na Ayasanda.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza tena Wizara hii kwa kazi nzuri na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangai walau kwa uchache katika Wizara hii ya Fedha na Mipango. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Naibu Waziri Eng. Hamadi Masauni, Katibu Mkuu pamoja na Manaibu Makatibu Wakuu wote na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao mkubwa sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti, sambamba na hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri asubuhi hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza Makamu Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bajeti kwa kuwasilisha taarifa yetu vizuri, pamoja na wanakamati wetu wote kwa ujumla kwa kweli kwa ushirikiano wao mzuri na umakini wao mkubwa katika uchambuzi wa bajeti mbalimbali ikiwemo bajeti hii ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika utendaji wa TRA. Kwanza kabisa nachukua nafasi hii kwa kweli kwa moyo wa dhati kuwapongeza TRA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya Serikali yetu, tunawapongeza sana. Nasi wote ni mashahidi, mwaka 2015/ 2016 tulikuwa na wastani wa shilingi bilioni 850, mwaka 2019/ 2020 tuna wastani wa shilingi trilioni 1.5 na lengo hasa ni kufika shilingi trilioni mbili, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili TRA iendelee kuboresha makusanyo ya mapato ya Taifa letu, naomba nishauri mambo machache. Jambo la kwanza ni kupanua wigo wa kodi kwa maana ya kuongeza walipa kodi wapya. Tukibaki na walipa kodi wachache hawa kwa miaka mingi, tunawaumiza. Tuongeze wigo wa kodi kwa kuwasajili walipa kodi wapya. Hii inaenda sambamba na kuajiri watumishi wa TRA. Kama kuna upungufu, basi Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuomba sana, tuongeze watumishi wa TRA, wafanye physical surveys, waimarishe block management ili kuwatambua walipa kodi ambao hawako kwenye mfumo.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ni kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji, ukadiriaji pamoja na kutoa taarifa sahihi za walipa kodi wetu. Bahati nzuri Ilani ya CCM ukurasa wa 13 umesisitiza sana hili kwamba tuongeze mifumo pamoja na kuongeza walipa kodi pamoja na wigo mpana wa walipa kodi wetu. Hatua hii itarahisha ulipaji wa kodi na kuongeza ulipaji wa kodi wa hiari (voluntary task compliance) na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ameshamteua balozi humu ndani, nadhani kazi inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kupata taarifa sahihi za walipa kodi wazawa (resident tax payers) ambao wanafanya biashara nje ya nchi kwa kutumia wale wenzetu ambao tunawa-share mambo ya kodi. Nchi kama Italy, India, South Afrika na kadhalika, kwa sababu Sheria ya Kodi ya Mapato inasema, ni lazima mlipa kodi ajaze returns zake kuonyesha mapato yake ya dunia nzima yaani well wide income, yote iwe tax kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato. Kwa hiyo, ni vizuri kupata taarifa hii ya mapato sahihi ili tupate kodi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine kwa kweli ni kuwapatia watumishi wa TRA mafunzo ya ukusanyi wa kodi hasa kwenye biashara za kidijitali. Leo dunia yetu inakusanya kwenye digital economy, kwa hiyo, ni muhimu sana watumishi wa TRA wakapata mafunzo ya kutosha katika mambo ya online businesses; ni maeneo ambayo dunia tulipofika leo. Tusipowekeza kwenye technolojia hii ya habari, kwa kweli tutapoteza mapato mengi ya Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni maslahi ya watumishi wa TRA naomba sana Waziri wa Fedha waangalie watumishi wa TRA hasa katika upandishaji wa madaraja. Mtu anakaa kwenye daraja moja miaka mitano mpaka saba, anakosa morali ya kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri alichukue hili kwa uzito wa hali ya juu, maana hii ndiyo pale hata anashawishiwa na rushwa, maana mtu anakaa daraja moja miaka mitano, saba, mpaka kumi hapandi. Naomba sana liangaliwe kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuwapanga wafanyakazi kutokana na maeneo ya kodi. Kwa mfano, mikoa mikubwa ya kodi kama Ilala, Temeke, Kinondoni tupange wafanyakazi kutokana na weledi. Pia nia na malengo kwa mfano kwa Mkoa wa Ilala unakusanya karibia asilimia 80 ya kodi za ndani. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuwapanga wafanyakazi vizuri hasa kwenye ukaguzi wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni ucheleweshaji wa misamaha ya kodi kwenye miradi ya Serikali. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) section 6 (2) inampa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi kwa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali. Hata ukisoma hata pale 2(c) na kadhalika Waziri wa Fedha ana mamlaka ya kuteua Technical Committee, wataalam kutoka Wizara ya Fedha, TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha yenyewe. Hawa ndio wanaomshauri Mheshimiwa Waziri ili aweze kutoa msamaha huo. Taarifa tulizonazo ni kwamba mizigo inayobaki bandari mingi sasa ni ya miradi ya Serikali kwa sababu ya kutokupata GN. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi hii ni ya kwetu, ni ya Serikali; mradi ni wa Serikali, Waziri ni wa Serikali, timu ya wataalam ni wa Serikali, timu ya watalaam ni wa Serikali, gazeti ni la Serikali, tunakwama wapi? Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa kweli alichukulie kwa uzito mkubwa. Miradi inapokwama, tunachelewesha maendeleo ya nchi yetu wenyewe. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, mtani wangu, tafadhali kwenye hili tuache utani, tufanye kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SILLO D. BARAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo kwenye mapendekezo ya Mpango huu wa Taifa wa mwaka 2022/2023. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu, Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanyia Taifa letu ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa Uviko ambao tumepata mkopo wa masharti nafuu wa shilingi trilioni 1.3 ambao umesaidia sana katika maendeleo yetu mbalimbali katika nchi yetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti pamoja na timu nzima ya Kamati ya Bajeti kwa kazi nzuri na ushauri ambao imetoa katika Mapendekezo ya Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nakupongeze wewe Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Spika kwa kutuongoza vizuri sana katika Bunge letu Tukufu. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati ya Bajeti pamoja na kuleta mapendekezo ya mwongozo huu wa Mpango wa Taifa wa mwaka 2022/2023. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo machache, moja ni upande wa kilimo. Amesema Mheshimiwa Ali King kwamba ukitemewa mate na wengi, utalowa. Kilimo chetu kinachangia asilimia 26.9 katika pato la Taifa. Pia kilimo kinaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 66. Vile vile malighafi za viwandani zaidi ya asilimia 60 zinatoka kwenye sekta ya kilimo. Kama tunasema kilimo kinachangia asilimia 26.9 ya pato la Taifa, maana yake Watanzania zaidi ya asilimia 66 wanachangia asilimia 26 tu kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo, maana yake, kwa kuwa kilimo kinaajiri Watanzania wengi zaidi, tulitarajia basi na mchango wa kwenye pato la Taifa ungekuwa mkubwa, siyo asilimia hii ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja kubwa sana ya Serikali kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ili kuhakikisha kwamba inachangia vizuri kwenye pato la Taifa ambako pia itakuza uchumi, itakuza ajira na itaongeza wigo wa walipa kodi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mapendekezo haya, namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika Mapendekezo haya ya Mpango huu tunaouandaa, Serikali iwekeze vyema kabisa kwenye sekta ya kilimo. Ninaamini kabisa tutakwenda kuondoa Watanzania kwenye umasikini na pia na kufikia dira ya nchi yetu ya mwaka 2025. Kwa hiyo, naomba sana kwenye Mpango wazingatie sana sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni sekta ya afya. Naipongeza sana Serikali imewekeza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, tumejenga vituo vya kutosha, kuna hospitali za Halmashauri pamoja na zahanati katika maeneo yetu, lakini kuna upungufu wa rasilimali watu watumishi wa afya zaidi ya asilimia 53. Tumejenga majengo najua Serikali italeta dawa lakini hatuna wataalam wa kutosha, upungufu wa asilimia zaidi 53 ni kubwa sana. Kwa hiyo niombe kwenye mpango huu tunaouandaa sasa Serikali iwekeze vizuri kwenye kuajiri wataalam wa afya katika maeneo haya ambayo tumejenga vituo vya afya pamoja na zahanati na hospitali za Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo ukienda unakuta zahanati ina nesi mmoja tu akiugua na huduma haitoki, kwa hiyo niiombe sana Serikali kwenye mapendekezo ya mpango huu sasa, iweke mkakati kabisa wa kuchambua na kuajiri hawa watoa huduma za afya katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ni sekta ndogo ya fedha. Unakumbuka mwaka 2018 Bunge lako Tukufu lilipitisha sheria pamoja na kanuni zake mwaka 2018 kuhusu sekta ndogo ya fedha, Kifungu cha 14 cha sheria hiyo kiliipa mamlaka Benki Kuu kukaimisha usimamzi wa mikopo kwenye maeneo yetu kwa Serikali za Mitaa na Kifungu cha 54 cha Sheria hiyo kinamlinda mkopaji, waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakuwa mashahidi watu huko vijijini wanakopeshana, wafanyabiashara walio rasmi na wasio rasmi wanawakopesha walimu na wananchi wetu na kuwatoza riba kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki Kuu haijafanya vizuri kwenye eneo hili, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha isimamieni Benki Kuu sheria hii isimamiwe, sheria zinazotungwa na Bunge lako Tukufu zisimamiwe kama tunaona sheria haina manufaa kwa wakati huu tuifute, wananchi wanateseka hasa walimu na wakulima wetu kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuserma hayo nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha wazingatie maoni na ushauri wa Kamati, jana nilisema humu ndani kuna madini ya kutosha wasome wazingatie naamini kwamba watakuja na mpango mzuri sana na bajeti inayokuja ya mwaka 2022/2023 itakuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushkuru kwa nafasi hii naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DANIEL B. SILLO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii niweze kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niweze kuwapongeza sana Wabunge wote waliochangia na kwa bahati nzuri wote wameunga mkono hoja. Kwa hiyo, hatuna hoja ya kujibu, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yameongelewa mengi wamechangia Wabunge wapatao kumi kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambao ni Mheshimiwa Subira Mgalu, Mheshimiwa Josephat Kandege, Mheshimiwa Issa Mtemvu, Mheshimiwa Shally Raymond, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mheshimiwa Ali King, Mheshimiwa Luhaga Mpina, Mheshimiwa Esther Matiko na Mheshimiwa Reuben Kwagilwa pamoja na Mheshimiwa Tarimba Abbas. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi yamezungumzwa naomba nisiyarudie yote lakini nitoe msisitizo kwa mambo machache. La kwanza, ni mahitaji ya fedha za dharura kwa ajili ya barabara za vijijini imefanyika tathimini inatakiwa Shilingi bilioni 111.3, ili kurejesha hali ya mawasiliano katika barabara zetu vijijini. Kwa hiyo, tunaomba tena Serikali ijielekeze kuhakikisha kwamba hili linafanyika ili watanzania, waweze kuendelea na huduma mbalimbali za wawasiliano kwa maana ya usafiri na usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni kufanya marejeo kwenye viwango vya Mfuko wa Jimbo. Mfuko huu wa Jimbo fedha hizi za miaka 20 iliyopita leo hii mfuko wa cement ni shilingi 18,000 mpaka shilingi 25,000 lakini wakati ule ulikuwa shilingi 10,000 mpaka shilingi 15,000. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ifanye marejeo ili kuongeza fedha za Mfuko wa Jimbo liendane na hali halisi ya uchumi wa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa ni kununua cargo scanners kwenye mipaka yetu. Tuna mipaka kama tisa mikubwa tumeenda Namanga pale hakuna cargo scanner, msururu wa mabasi, wa malori ni mkubwa sana na gharama ya usafirishaji inakuwa ni kubwa sana. Kwa hiyo, tuiombe sana Serikali iweze kununua cargo scanners, kwa ajili ya kusaidia mizigo kutoka lakini pia itaongeza mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ajira kwa TRA upungufu wa staff wa TRA umefanya walipakodi wengi kutokufikiwa hasa kwenye maeneo ya Tax Audit pamoja na Block Management. Tax Audit ni truly for voluntary tax compliance kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana wa TRA kuajiri wafanyakazi wa kutosha ili sasa waweze kufanya Tax Audit pamoja na Block Management ili ku-enhance voluntary tax compliance.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni bima ya afya kwa wote. Watanzania wanaotumia bima leo ni chini ya asilimia 20 kwa hiyo, kuna haja kubwa sana Serikali ikajielekeza ikaleta Sera na Sheria, ili sasa Watanzania waweze kuingia kwenye bima ya afya kwa wote ili kuwasaidia Watanzania kupata huduma za afya katika maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa habari ya daraja la Tanzanite nadhani Wabunge wamechangia sana kwa nguvu kubwa kabisa. Nadhani ni vyema basi Serikali ikajielekeza ikaangalia umuhimu na uwezekano wa daraja hili kuwa toll bridge ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya kuendesha mkopo huu wa Shilingi bilioni 243.8 waliotoa kwenye Serikali ya Korea Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamesemwa lakini hasa hili la TARURA ameongea Mheshimiwa Reuben kwa msisitizo mkubwa sana. Kwa kweli tulitenga bajeti hii ya tozo shilingi bilioni 322, lakini tunapotoa leo dharura shilingi bilioni 111 tumeharibu utaratibu wa bajeti. Naomba Serikali iliangalie hili kwa umakini mkubwa sana ili bajeti yetu iende vizuri, watanzania wapate huduma ambazo wanatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze sana Waheshimiwa Manaibu Waziri wote wawili waliochangia, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ameongelea habari ya Blue Print. Tunaomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri hili mlizingatie sana ili kurahisisha ufanyaji biashara hapa nchini, kupunguza mlolongo mkubwa sana wa taasisi zetu za Serikali. Katika ufanyaji wa biashara na ili biashara ziwe rahisi watanzania wafanye shughuli za kiuchumi waweze kulipa kodi na kuwanufaisha watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Waziri wetu wa Fedha ameongea habari ya riba kwa wakopaji. Hili kwa kweli waliangalie kwa mfano mikopo kama ya watu binafsi risk ni ndogo sana kwa hiyo, waangalie kwa ukaribu ili watanzania waweze kukopa kutoka benki yao ya biashara. Waweze kuwekeza na shughuli za kiuchumi ziendele walipe kodi kwa manufaa makubwa na mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni Ofisi ya mpokeaji wa malalamiko ya kodi Tax Imbursement ni miaka mitatu sasa tumetunga sheria lakini bado haijaanza ofisi hii, malalamiko ya walipa kodi ni mengi sana mtaani. Naomba sana Serikali ijielekeze kuhakikisha kwamba Ofisi hii inaanza ili kupunguza malalamiko ya walipa kodi wetu ili walipe kodi kwa hiari na nchi yetu iweze kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nawapongeza sana wote lakini niombe sana wenzetu upande wa Serikali wachukue haya yote maoni ya Wajumbe wa Kamati ya Bajeti; na sisi kama kamati tutaendelea kusimamia na kuishauri Serikali kila hatua ili tuweze kuwa na bajeti bora kwa manufaa mapana ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na baada ya maelezo haya naomba kutoa hoja ahsante sana. (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMBU: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana kwa kupata nafasi niweze kuchangia katika hoja ambazo ziko mbele yetu. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi kwamba kuna miradi mingi inaendelea katika majimbo yetu pamoja na huduma za jamii. Nikupongeze pia wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kuongeza Bunge letu vizuri na tunakupongeza kwa umahiri mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nipongeze wenyeviti na makamu wenyeviti na wajumbe wa kamati hizi tatu, kwa maana ya PIC, PAC pamoja na LAAC kwa kuchambua taarifa hizi, ripoti ya CAG pamoja na uwekezaji wa mitaji ya umma katika taasisi ya mashirika mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza kwanza kwenye kamati ya PIC, uwekezaji wa mitaji ya umma. Faida ambayo inatarajiwa kupata na Serikali katika utendaji huu ni gawio, mchango wa asilimia 15, marejesho kutoka TTMS, yaani mtambo unaosimamia masuala nchini riba na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha uliyoishia Juni 30, 2021, kwa upande wa gawio, malengo ambayo TR aliweka kwa kukusanya ilikuwa ni Shilingi bilioni 408.4, lakini makusanyo halisi ni Shilingi bilioni 308 sawa na ufanisi wa asilimia 76.3. Tukienda kwa upande wa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, Msajili wa Hazina aliweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 395.4, lakini makusanyo halisi ni Shilingi bilioni 202.2, sawa na ufanisi wa asilimia 51 ya lengo. Kwa upande wa marejesho kutoka TTMS, malengo kwa mwaka wa fedha huu uliyoishia Juni 2021 ilikuwa ni Shilingi bilioni 15, lakini makusanyo halisi ni Shilingi bilioni 10.3 sawa na ufanisi wa asilimia 68.3.

Mheshimiwa Spika, picha inayoonekana hapa ni kwamba kwa ujumla mwenendo wa mapato yasiyokuwa ya kodi, yanayotokana na uwekezaji huu uliofanywa na Serikali, yamepungua sana kwa mwaka huu wa fedha uliyoishia Juni 2021. Vilevile tukumbuke kwamba fedha hizi ni sehemu ya bajeti zetu, maana mapato yote haya yanaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali (consolidated fund). Kwa hiyo, tunapokuwa hatufanikishi bajeti zetu ni kwa sababu ya usimamizi usioridhishisha kwa baadhi ya taasisi au mashirika ambako Serikali imewekeza. Matokeo haya yanaonyesha dhahiri kwamba baadhi ya taasisi ambazo Serikali zetu imewekeza kodi za wananchi hayasimamiwi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati ya PAC kusomwa ukurasa wa 22 inazungumzia taasisi kutokuwa na Bodi za Wakurugenzi. Bodi ya Wakurugenzi ni chombo kikuu cha uamuzi katika taasisi na mashirika ya Umma. Kwa hiyo, unapokosa chombo cha maamuzi pale ambapo Serikali imewekeza, unatarajia nini? Lazima utarajie matokeo haya ambayo hakuna mahusiano yaliyofika hata asilimia 80. Kwa hiyo, kutokufikia malengo haya ni kwa sababu kuna maamuzi ambayo yalitakiwa yafanyike, hayakufanyika. Hata wanaofanya biashara binafsi, kama ndani ya mwaka mzima hakuna kikao kinachokaa kufanya maamuzi, unatarajia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, suala la Bodi ni la msingi sana. Lazima kuwe na checks and balance. Kwa hiyo, naomba sana wale wanaohusika na uteuzi wa Bodi, wateuliwe Wajumbe wa Bodi wenye weledi katika taasisi hizi na mashirika ambapo Serikali imewekeza. Taasisi hizi zikifanya vizuri, haitaishia kupata gawio asilimia 15 ya mapato ghafi na marejesho haya, lakini yatapata faida ambayo pia italipa kodi ya mapato. Kwa hiyo, mashirika haya yakiboreshwa katika misingi hii yataongeza Mapato ya Taifa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na Bajeti Kuu ya Serikali. Kwa hiyo, naomba sana kwa kweli jambo hili tulichukilie kwa uzito mkubwa sana kwa upande wa Serikali maana ni kwa faida ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC). Nampongeza sana Mwenyekiti na timu yake nzima kwa kazi kubwa waliyofanya, wamepitia Taarifa ya CAG, imeonyesha madudu ambayo tumeyaona. Taarifa ya CAG inasema, Serikali imepata hasara ya Shilingi bilioni 68.73 ambayo ilisababishwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kuchelewa kuwalipa Wandarasi. Taarifa inasema, kusimama kwa ujenzi wa vihenge unaotekelezwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi (NFRA) wakati Mkandarasi ameishalipwa Dola za Marekani 33.4 sawa na karibu Shilingi bilioni 76.8; taarifa inaendelea kusema, malipo ya Dola za Marekani milioni 153.43 yalifanywa na TANESCO kwa SYMBION ambayo takriban ni Shilingi bilioni 350; taarifa hii inasema, fedha hizi ni nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, leo Waheshimiwa Wabunge tunalia hapa miradi ya barabara kwenye majimbo yetu, nishati ya umeme haipo, lakini kuna wenzetu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia fedha za Umma, wanazichezea. Naomba sana wenzetu wenye dhamana hizi wawe na uchungu na Watanzania. Wawe wanatembea vijijini kuona hali halisi ya maisha ya Watanzania. Tukumbuke hizi ni kodi za Watanzania. Tunakaa Bunge hapa miezi mitatu tunapanga bajeti, halafu watu wachache wanakaa wanachezea fedha za Umma. Jambo hili linaumiza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna miradi mingi ya kimkakati inataka fedha, tuna upungufu wa kibajeti, tunataka fedha, tuna upungufu wa watumishi wa Afya, Elimu katika maeneo yetu, tunataka fedha; tuna deni la Serikali, tunataka fedha tulipe; Watanzania wana shida ya maji katika maeneo mbalimbali; tuna shida ya nishati ya umeme vijijini, lakini wapo wenzetu wameamua kucheza na fedha za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge toka Bunge hili limeanza, inatia uchungu sana pale ambapo fedha za Umma zinachezewa. Kwa hiyo, naomba Bunge lako Tukufu liazimie kuwachukulia hatua wote waliohusika na ubadhirifu huu wa fedha za Umma. Sisi ni wawakilishi wa wananchi, tunaelewa uhalisia ulioko kwa wananchi kule. Kuna msemo wa Mheshimiwa Waziri wa Maji, kwamba mihemo ya mgonjwa anajua anayelala naye. Sisi ndio tunalala na wananchi wetu. Kwa hiyo, naomba Wenyeviti wa Kamati, pamoja na maazimio ambayo wameweka, basi tuongeze yetu kwamba lazima waliochezea fedha za Umma wachukuliwe hatua za kisheria na kikanuni za kiutumishi ili liwe fundisho kwa wengine kwa miaka mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kila mwaka katika taarifa za CAG makosa yanajirudia kwa taasisi hizo hizo, na watu wapo tu. Jambo hili halikubaliki, sisi kama Wabunge lazima tusimame na kuwatetea Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache, nashukuru kwa kunipa fursa na ninaunga mkono hoja zote tatu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. DANIEL B. SILLO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kwa kushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuhitimisha hoja ambayo iko mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechangia Waheshimiwa Wabunge 15 na Waheshimiwa Mawaziri watu; Mheshimiwa Waziri wa kilimo, Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi Mheshimiwa Bashungwa pamoja Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Mawaziri kwa sababu wote wameunga mkono hoja. Nawapongeza na ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni mengi yamechukuliwa na Serikali katika kuyafanyia kazi lakini ningependa kuongeza mambo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, limezungumzwa sana kuhusu Deni la Serikali. Naomba niwahakikishie na niwatoe wasi wasi Waheshimiwa Wabunge kwamba, Deni la Serikali kwa Biashara zote za kimataifa liko himilivu kwa viwango vyote vya kimataifa. kwa hiyo, tusiwe na wasi wasi Deni liko salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati ya Bajeti tumejiridhisha, tumepitia hii mikopo yote inayokuja na tumehakikisha kwamba hakuna kifungu chochote cha Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana ya Serikali Sura ya 130 ambacho kimevunjwa. Kwa hiyo, mikopo imekopwa katika uhalali wake na iko ndani ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha Tano cha Sheria ya Matumizi, kinampa Mamlaka Waziri wa Fedha kukopa kiwango chochote cha Fedha ambacho kimeidhinishwa na Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo mikopo yote imekopwa kutokana na sheria ambayo imetu-guide, Sheria ya Matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye deni hilo hilo mwezi Juni, 2022 deni lilikuwa trilioni 71.56 lakini kufika Disemba, 2022 deni lilikuwa ni shilingi trilioni 74.64, ongezeko la shilingi trilioni 3.08 ambayo ni growth rate ya asilimia 4.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo Mjumbe alichangia limekuwa kwa asilimia 12,13 lakini uhalali ni kwamba imekua kwa asilimia 4.3, kwa hiyo deni liko salama na liko himilivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu mfumuko wa bei. Kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo iko na asilimia tano mpaka sasa. Ukiangalia nchi kama Rwanda asilimia 23.7, Kenya asilimia 9.7 na Uganda asilimia 9. 7. Kwa hiyo sisi tuko salama kwa maana ya mfumuko wa bei pamoja na changamoto ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna uhusiano wa moja kwa moja wa kwamba mfumuko wa bei unatokana na usimamizi mbovu wa sera za fedha pamoja na Bajeti. Kwa hiyo, naomba niwatoe wasi wasi Waheshimiwa Wabunge, kwamba nchi iko salama katika suala hili la mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kuzungumzia ni eneo la mifumo ya TEHAMA ya kukusanyia mapato. Mifumo ya TRA tuna mifumo ya TANCIS Pamoja na Mfumo wa IDRAS. Mifumo hii haisomani na Mfumo wa TPA wala Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo niombe sana Serikali katika eneo hili, Mheshimiwa Waziri wa Fedha unanisikia, naombeni sana mkaboreshe mifumo ya ukusanyaji wa Mapato. Mifumo inapokuwa haisomi na ni ya taasisi moja ni changamoto. TRA wenyewe kuna Mfumo wa Forodha wa TANSIC lakini kuna kodi za ndani wa IDRAS hii yote yenyewe haisomani. Kuna changamoto na Mapato yanapotea. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili mlichukue mboreshe sana maeneo haya mifumo iweze kusomana ili tuweze kukusanya mapato yetu ya Serikali kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo pamoja na huduma za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuiwezesha kampuni ya Mbolea. Kampuni ya mbolea imeomba ipatiwe mtaji wa bilioni 60 ili iweze kusambaza mbolea kwa wakulima wetu. Tuiombe sana Wizara ya Kilimo kampuni hii ya mbolea muiwezeshe ili iweze kuagiza mbolea moja kwa moja kutoka kwa ma-supplier. Hivi sasa wananunua kwa mawakala kwa hiyo hawawezi kushindana na wauzaji wengine wa mbolea hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi kwenye huu Mkopo wa ECF ambao ni trilioni 2.4. Mkopo huu wa trilioni 2.4 si wa mwaka mmoja, huu ni mkopo wa miezi 40 kuanzia Julai, 2022 hadi Julai, 2025. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na ambao tumepitisha ndani ya Bunge lako Tukufu, kwenye bajeti tumetenga shilingi bilioni 760; na mwezi Agosti, 2022 tumepokea awamu ya kwanza ya bilioni 349.8 na awamu ya pili mwaka wa fedha 2023 tutapokea mwezi machi, 2023. Kwa hiyo mkopo huu si kwamba wote umepokelewa kwa mara moja. Maana kuna Mjumbe ameongea kuwa kuna hela zinaingia nje ya bajeti, hapana. Ndani ya bajeti mwaka wa fedha 2022/2023 ni bilioni 720 na awamu ya kwanza kama nilivyosema ni bilioni 349. Niiombe tu Serikali, kule ambako mkopo umeelekezwa muweze kuusimamia vizuri hasa zile za uzalishaji. Umeenda kilimo, nishati na mifugo na uvuvi, hizi zote ni sekta za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mkopo huu ni katika kuboresha urali wa malipo na urali wa biashara kati ya nchi yetu na nchi nyingine hapa duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja pia nizungumze, kuhusu reallocation ndani ya mafungu na pia nje ya mafungu. Kifungu cha 41(8) cha Sheria ya Bajeti Sura ya 439 na Kanuni zake zinamtaka Waziri wa Fedha kuwasilisha taarifa ya uhamisho wa ndani (within the votes) au nje au between votes mara baada ya nusu mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge lako Tukufu, kwamba uhamisho kwa mwaka wa fedha 2021/2022 uliwasilishwa kwenye Ofisi ya Bunge tarehe 1o Novemba, 2022. Hata hivyo, kwa nusu mwaka hii ya mwaka wa fedha ambao tunaendelea nao, wa 2022/2023, ripoti hii itawasilisha kwenye Ofisi ya Bunge Mwezi Machi 2023. Taarifa hii inapatikana kwenye ukurasa wa 72 wa taarifa ya Kamati ya Bajeti kipengele cha 7.7 na kiambatisho (B) ambacho pia kimeambatishwa kwenye taarifa yetu ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa pia kulizungumzia ni eneo la Sheria yetu ya Manunuzi. Sheria yetu ya manunuzi ina changamoto, wote tunakubali; kwamba Sheria yetu ya Manunuzi inachukua muda mrefu sana. Kamati ya Bajeti ilipata fursa ya kuishauri Serikali na Serikali ilikubali, kwamba sheria hii itafanyiwa marekebisho. Sasa tuiombe Serikali iwaishe muswada wa sheria katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 ili Sheria ya Manunuzi tuibadilishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna miradi mingi sana, Mheshimiwa Bashe amezungumza hapa, kwa mfano kwenye Tume ya Umwagiliaji tumetengea shilingi bilioni 215 lakini utoaji wa fedha mpaka sasa ni asilimia kidogo sana. Hata hivyo ukiongea na Serikali wanasema tayari fedha ziko kwenye commitment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment hii inacheleweshwa na Sheria hii ya Manunuzi. Kwa hiyo naomba muswada huu uletwe haraka iwezekananvyo ili Sheria hii ya Manunuzi tuibadilishe. Tusiicheleweshe wenyewe, nchi hii ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la mwisho, si kwa umuhimu, ni miradi ya muda mrefu; amezungumza Mheshimiwa Waziri Kiongozi Mstaafu, Mheshimiwa Shamsi Vuai Naohodha, kuhusu Miradi ya Mchuchuma na Liganga pamoja na gesi asilia. Miradi hii ikikamilika itaokoa sana fedha za kigeni tunazoagiza chuma kutoka nje pamoja na maeneo mengine. Kwa hiyo niombe sana Serikali iharakishe majadiliano ya miradi hii ili iweze kukamilika kwa wakati ili kuokoa fedha za kigeni ambazo zinatumika kuagiza chuma na bidhaa nyingine nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaomba sasa Maoni, Ushauri na Mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yawe Maazimio ya Bunge zima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara yetu hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupanua diplomasia ya Kimataifa ya kiuchumi ambako sasa itafungua fursa kubwa nyingi sana za uwekezaji hapa nchini. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri wetu wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, dada yangu Mheshimiwa Ashatu pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi zile wanazozifanya pamoja na hotuba nzuri aliyowasilisha katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo machache la kwanza ni mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchi (easy of doing business). Kwenye ukurasa wa 26 mpaka 27 wa hotuba hii, ameelezea ufanyaji wa biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya Benki ya Dunia ya Mwaka 2018 inasema Tanzania ilikuwa nchi ya 141 kati ya nchi 190; lakini nchi ya jirani ya Kenya ilikuwa 56 kati ya nchi hizo190; Uganda ilikuwa 116; Rwanda ilikuwa ya 38. Mwaka 2019 Tanzania ni nchi ya 141 kati 190 na Kenya ya 56, Uganda 116 na Rwanda 38. Nchi yetu katika region hii ndiyo iko chini kabisa urahisi waufanyaji biashara hapa nchini. Kwa hiyo niombe sana Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara iitoe nchi yetu katika...

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Abbas Tarimba.

T A A R I F A

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, anayozungumza Mheshimiwa Sillo ni mambo mazito sana, ni mambo muhimu sana na ukiangalia maandiko mengi ya Serikali yanahubiri private sector kwa maana ya taasisi binafsi au sekta binafsi kwamba ndiyo engineer ya growth, kila mahali Serikali inazungumzia hivyo. Vile vile ukiangalia Tanzania Private Sector Engagement Fact Sheet inatuambia kwamba private sector yenyewe mchango wake ni asilimia 90 ya ajira hapa Tanzania, lakini vile vile ni asilimia 60 ya uwekezaji na zaidi ya asilimia 80 ya kodi za Serikali. Hivyo analolizungumza ni suala zito ambalo naliunga mkono, naomba nimpe taarifa katika mchango wake. Ahsate sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Daniel Sillo, taarifa hiyo.

MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ya Mheshimiwa Tarimba, mjumbe makini kabisa wa Kamati ya Bajeti naipokea kwa mikono yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mwarobaini wa tatizo hili nini? Mwarobaini wa suala hili ni ukamilishaji wa Blueprint for Regulatory Authority – Mpango Maalum wa Kuboresha Ufanyaji wa Biashara hapa Nchini. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili jambo la Blueprint limeanza muda mrefu, naomba likamilike. Zipo taasisi za Serikali zinafanya ama shughuli zinazofanana, lakini mwekezaji au mfanyabiasha anaingia kwenye taasisi nyingi za Serikali. Naamini kabisa kama huu mpango utakamilika basi itarahisisha sana ufanyaji biashara hapa nchini. Tunalia kila siku kwamba tupanue wigo wa walipakodi, tunapokuwa tunawafukuza hawa wafanyabiashara hatuwezi kukuza wigo wa walipakodi hapa nchini na kwa maana hiyo Serikali inapoteza mapato mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarijia kupata ajira kwa Watanzania Ilani ya Uchaguzi ya 2025 inasema tuajiri Watanzania milioni nane. Bila kuwezesha Sekta Binafsi hatuwezi kufikia lengo hilo, kwa hiyo niiombe sana Wizara iboreshe mazingira ya wafanyabiashara hapa nchini ili nchi yetu itoke kwenye rating hii ya nchi iende kwenye hatua ya juu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la kuelekeza; nielekeze kwenye mifumo, ukienda kwenye taasisi zetu unakuta kuna OSHA, kuna TBS, kuna TMDA waweke mifumo inayosomana ili mwekezaji au mfanyabiashara akienda ofisi moja akilipa basi iende moja kwa moja kwenye zile sector zingine kuliko kumsumbua mfanyabiashara aingie jengo hili, aingine jengo lile, tunajikwamisha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la uwekezaji. Hapa naipongeza Serikali imechukua hatua mbalimbali katika mazingira ya uwekezaji hapa nchini. Tunapenda Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC) pamoja na EPZ kiwe ni one stop shop kwamba akiingia mfanyabiashara pale, mambo yake yote yanakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye EPZA tuna TRA pale, tunataka mifumo isomane mtu wa TRA pale awe na maamuzi, akishaona mfuko umehakikiwa pale ukienda bandarini unasafiri kwenda nje ya nchi bila shaka biashara inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kwenye eneo la TIC pia tuweke wataalam wa Serikali wenye maamuzi. Inapoteza muda mwingi sana unaweka watu ambao hawana maamuzi, document zinafika pale zinabebwa kwenda makao tena tunapoteza muda mwingi sana wa wafanyabiashara. Kwa hiyo niombe sana wawepo watu watoa maamuzi wa Serikali katika maeneo haya ambayo tunayasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, tumeletewa wawekezaji wengi, kwa hiyo, niombe sana Wizara ijielekeze katika kuhakikisha kwamba tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika juhudi hizi za kuweka wawekezaji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengine ya wawekezaji, yapo mashamba makubwa ya wawekezaji hapa nchini, lakini yana migogoro na wananchi, mashamba hayaendelezwi, watu wamewekeza, wanachukua robo ya shamba, lingine sijui wanakopea, kwa hiyo, wananchi wetu hawapati maeneo ya kufanya shughuli zao za uchumi kama kilimo, ufugaji na kadhalika. Niombe sana Wizara ijielekeze kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukiwa na migogoro mwekezaji hatawekeza. Kwa hiyo hata Serikali inakosa mapato iliyotarajia, lakini wananchi wetu wanakosa kufanya shughuli zao za uchumi, lakini Serikali pia inakosa mapato ambayo ingeyapata. Kwa hiyo niombe sana Waziri wetu msikivu kabisa, dada yangu Mheshimiwa Ashatu ajielekeze kabisa ili wananchi wetu waendelee na shughuli zao za kiuchumi kwa manufaa makubwa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, kule Halmashauri ya Babati kuna mashamba makubwa kwenye Kata za Kiru, Magugu, Magara na Kisangaju lakini migogoro mitupu. Napongeza Serikali kuna ziara za Waziri wamefanya kazi kubwa, lakini bado migogoro ipo. Naiomba Serikali iweze kujipanga vizuri kumaliza migogoro hii ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu, ambayo ni hotuba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafsi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi yetu. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wote pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara hii kubwa inayohudumuia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu upo katika maeneo makubwa mawili; eeneo la kwanza ni eneo la sekta ya afya. Niipongeze Serikali kwa ujenzi wa hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati katika maeneo yetu, kazi kubwa sana imefanyika.

Mheshimiwa Spika, ili kuipa thamani kazi hii kubwa ya ujenzi wa hospitali za halmashauri vituo vya afya na zahanati tuiombe sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI sasa tuweze kupata dawa za kutosha, vifaa tiba lakini pia na watoa huduma katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, tumejenga majengo mazuri sana. Tumejenga zahanati, tumejenga vituo vya afya, tumejenga hospitali ya halmashauri; sasa tunaomba tupate wahudumu ili tuwe na thamani ya majengo haya tumeyajenga.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine muhimu sana katika vituo vya afya zahanati na hospitali zetu ni upatikanaji, utunzaji na utoaji wa dawa. Kumekuwa na upotevu mkubwa wa dawa katika hospitali zetu. Dawa zinapikelewa, zinatunzwa lakini zinavyotoka kuna dawa zinatoka lakini hazijulikani zinaenda kwa nani.

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri wa TAMISEMI ni shahidi, tulifanya ziara takakuta dawa zimepokelewa na zimetunzwa, lakini dawa zimetolewa hakuna mfumo rasmi wa kutoa dawa katika maeneo yetu. Kwa hiyo niombe sana TAMISEMI waliangalie jambo hili kwa umuhimu mkubwa sana kwa sababu ni kero kwa wananchi wanapo kosa dawa kwenye hospitali ya Serikali, anapokosa dawa kwenye kituo cha afya lakini anapata dawa kwenye duka la watu binafsi. Hatukatazi watu binafsi wafanye biashara lakini naomba uwekwe utaratibu wa wazi wa upokeaji, utunzaji na utoaji wa dawa kwenda kwenye huduma za wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa pia nichangie ni kufanyika ukaguzi wa wataalamu wetu wa kutoa huduma za afya; kwamba kuna Madaktari wangapi, kuna Manesi wangapi kwenye hospitali za halmashauri, vituo vya afya pamoja na zahanati. Ninatoa mfano; kuna zahanati nyingine vijijini kunakuwa na nesi mmoja tu. Inatokea changamoto yoyote zahanati inafungwa. Inapotokea mama mjamzito anachangamoto ya kujifungua unakuta zahanati imefungwa; ni shida kubwa sana kwa wananchi wetu. Kwa hiyo niombe sana ifanyike human resource audit, kwa maana ya Manesi na madaktari ili tuwagawe kwa usahihi katika maeneo yetu waweze kutoa huduma kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, ninasema hayo kwa sababu nina mfano kuna Zahanati ya Meri, Zahanati ya Gosbert kule Babati vijijini yuko nesi mmoja; akifiwa, akiugua zahanati inafungwa. Kwa hiyo niombe sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI ifanye tathmini hiyo ili wananchi wote wapate huduma.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la elimu. Tunashukuru sana Serikali imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa madarasa, madarasa 12,000 ya sekondari na madarasa 3000 ya shule za msingi. Tunaomba sasa, baada ya kazi hii nzuri ya ujenzi wa madarasa wapatikane walimu wa kutosha katika maeneo yetu, sambamba na afya, kama nilivyosema. Upande wa elimu pia ifanyike tathmini ya idadi ya walimu nchi nzima tuwagawe kutokana na taaluma pamoja na jinsi pia.

Mheshimiwa Spika, ziko shule za wasichana katika wilaya yetu hazina walimu wa kike. Watoto wetu wadogo wa kike wanakua lakini hawana walimu wa kike; hii ni changamoto kwenye shule zetu. Kwa hiyo niombe sana waangalie taaluma. Ziko shule ambazo kuna walimu wa sayansi wengi lakini walimu wa sanaa hawapo. Zipo shule, kama nilivyosema za wasichana hazina walimu wa kike. Kwa hiyo niombe sana wafanye human resource audit ya Walimu wawagawe vizuri kwenye shule zetu ili wanafunzi wetu wapate huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia tulianzisha ujenzi wa Maabara; na sasa kuna maboma mengi sana ya Maabara ya sayansi Biology, Chemistry na Physics. Kwa sababu sasa majengo yameshakamilika niombe sana Wizara ya TAMISEMI ijielekeze katika kumalizia maabara hizi ili wanafunzi wetu wapate kujifunza masomo haya ya sayansi kwa ajili ya manufaa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine la mwisho niombe sana. Zimetangazwa ajira za walimu, tunajua. Kuna walimu wa kujitolea kwa muda mrefu sana kwenye maeneo yetu; wamefundisha watoto wetu na watoto wamefaulu. Sasa, linapokuja suala la ajira wanakosaje sifa ya kuwa ualimu? Kwa hiyo niombe sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI ifanye tathmini ya walimu waliojitolea kwa muda mrefu. Wamefanya kazi kubwa kwenye nchi yetu, wamefundisha watoto wetu na Watoto wamefaulu. Kwa hiyo wapate sifa ya kuajiriwa katika shule zetu ili waendelee kutoa huduma hii kubwa ambayo walishaanza kuitoa kwa kujitolea.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya mimi nashukuru sana naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara yetu hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta mbalimbali hapa nchini pamoja na sekta yetu hii ya maliasili na utalii. Lakini niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima, kwa kazi kubwa na dhamira nzuri mliyo nayo katika kuiboresha sekta hii ya maliasili na utalii hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwenye hili suala la The Royal Tour, limekuwa na mafanikio makubwa katika nchi yetu. Na moja kubwa ni kuitangaza nchi yetu kimataifa, la pili kuongeza idadi ya watalii hapa nchini na la tatu ni kuongeza fedha za kigeni katika uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo ni pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa iliyofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) yako malengo ambayo tulijiwekea. Moja ni idadi ya watalii kufikia milioni tano kwa mwaka; la pili, mchango wa sekta hii ya utalii kuwa asilimia 15.5 kwenye Pato la Taifa; tatu sekta hii kuchangia asilimia 27 ya mapato yote ya kigeni. Ili kuyafikia malengo haya lazima kazi kubwa ifanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na la kwanza mimi napendekeza, ni kuongeza vitanda kwa ajili ya watalii. Katika eneo hili ni kushirikisha sekta binafsi. Kwa taarifa ya mwaka 2022, Tanzania tuna vitanda 132,684 lakini nchi jirani ya Kenya ina vitanda 1,200,000. Kwa hiyo kuna kazi ya kufanya katika eneo hili kuongeza vitanda kwa kushirikisha sekta binafsi, kujenga hoteli za nyota mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tuna vitanda vya kutosha kwa ajili ya watalii wanafika katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika eneo hili ni kuboresha miundombinu yetu kwenye masuala mazima ya utalii. Jambo la tatu ni kuboresha huduma (customer care) kwa watalii wetu. Jambo la nne utakumbuka wakati tulivyogawa fedha za UVIKO-19 sekta hii ya utalii tuliipa bilioni 90.2. Kazi ilifanyika nzuri sana na Kamati yangu ya Bajeti ilipata ziara katika maeneo mbalimbali, tumeona mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napendekeza kwenye dirisha hili la ECF ambalo lilikuwa na nia ya kupunguza matatizo ya urari wa malipo kwa nchi zetu basi Serikali itenge fedha pia kwa sekta hii ya maliasili na utalii ili kuboresha sekta nzima ya utalii ambayo inachangia katika uchumi wetu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuendeleza na kumaliza migogoro mbalimbali kati ya hifadhi na maeneo yetu mbalimbali hapa nchini. Katika eneo hili niendelee kuipongeza Serikali kwa sababu kazi kubwa imefanyika. Iko timu ya mawaziri nane ambayo imezunguka katika nchi yetu, wamefanya kazi kubwa, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna baadhi ya maeneo yetu bado kuna migogoro. Nitatoa mfano wa Jimbo langu la Babati Vijijini; kuna Vijiji nane ambavyo vinapakaa na Hifadhi nzuri sana ya Tarangire; Vijiji vya Gedabung’, Ayamango, Gedamar, Mwada, Sarame, Sangaiwe na Vilimavitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna dhamira nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri ya kumaliza migogoro hii. Tumesikia hotuba yake, ameongea masuala mazuri sana. Mheshimiwa Waziri, twende kama timu pamoja, liko jukumu la kwangu kama Mbunge na wananchi wangu, liko jukumu la Serikali, twende kwa pamoja tukamalize miigogoro hii ya muda mrefu ili kuwe na uhusiano wa ujirani mwema kati ya hifadhi na wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri umejipanga vizuri, nami nakuhakikishia kabisa ntakuunga mkono katika suala zima la kumaliza migogoro katika maeneo haya yote ya Babati Vijijini ili wananchi waendelee kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la kifuta jasho wananchi wanapoharibiwa mazao na wanyama wakali. Tunaipongeza Serikali kwanza kwa kuwakumbuka wananchi, walau hata kwa hicho kidogo wanachokipata. Lakini kifuta jasho kinachelewa, hakiji kwa wakati. Kwa hiyo tuombe sana Serikali basi kile kifuta jasho kije kwa wakati lakini pia walau kiakisi ule uhalisia wa uharibifu uliofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana katika eneo hili kuwe na tathmini ya uhakika ili wananchi wapate walau kifuta jasho kitakachosaidia familia zao na kisaidie uchumi katika maeneo hayo. Pia viwango vifanyiwe mapitio, ni vya muda mrefu. Kwa hiyo niishauri Wizara iangalie namna ya kupitia viwango hivi vya fidia kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, otherwise nashukuru sana kwa kupata nafasi hii, na mimi naiunga mkono hoja hii kabisa, na Mheshimiwa Waziri nakutakia kila la heri katika mafanikio yako. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara yetu hii ya Fedha na Mipango. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu. Tunamwombea afya njema ili aendelee kututumikia. Pia niwapongeze Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri pamoja na Timu nzima ya Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya kusimamia fedha na sera za fedha za kikodi katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti pamoja na Wajumbe kwa kazi kubwa tuliyofanya katika kukamilisha taarifa hii ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia mambo machache. La kwanza ni mfumo wa TEHAMA wa ukusanyaji wa mapato ya TRA pamoja na TPA. Sisi wote ni mashahidi kwamba mifumo ya ukusanyaji mapato ni ya muhimu sana katika kukusanya mapato ya Taifa letu. Mifumo yetu hii ina changamoto zifuatazo:-

(i) Mfumo wa kodi za ndani bado haujakamilika, unasuasua;

(ii) Mfumo wa kodi za ndani kutokusomana na mfumo wa kodi za forodha; na

(iii) Mfumo wa forodha kutosomana na mfumo wa TOS wa TPA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokamilika kwa mfumo wa kodi za ndani ni risk kubwa sana katika kupotea kwa mapato ya Taifa letu. Kwa hiyo niombe sana Wizara ya Fedha kuhakikisha inasimamia kukamilisha mfumo wa kodi za ndani ili kuweza kuimarisha mapato yetu ya ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote ni mashahidi kwamba asilimia 40 ya mapato yote ya TRA yanakusanywa kwenye Idara ya Forodha, lakini kutokusomana kwa mfumo wa kodi ya forodha na Bandari ni changamoto kubwa sana ya upotevu wa fedha hapa nchini. Kwa hiyo nishauri sana Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango wahakikishe mifumo yetu ya mapato inasomana ili kuboresha mapato ya Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano wa Mwaka 2021/2022-2025/2026 yako mambo ambayo yameainishwa. Kwanza, mchango wa kodi kwenye pato la Taifa kufikia asilimia 13, lakini bajeti yetu ya Serikali karibu asilimia 60 inategemea mapato ya kodi zetu hapa nchini, lakini Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2025 ukisoma ukurasa wa 16 imezungumzia kuboresha mapato ya Taifa letu. Ili kufikia malengo haya ni lazima kuwekeza katika mifumo ya ukusanyaji mapato hapa nchini ili nchi yetu iweze kufikia hatua hii ya asilimia 13 ya pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu kwenye nchi zinazotuzunguka, mchango wa kodi kwa Nchi ya Kenya kwa pato la Taifa ni asilimia 16.9, mchango wa kodi pato la Taifa kwa Nchi ya Rwanda ni asilimia 14.1, lakini sisi Tanzania asilimia 11. Kwa hiyo kama nchi tuna kazi ya kufanya kuhakikisha kwamba tunaimarisha mifumo yetu ili tufikie malengo haya kwa manufaa makubwa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni mikataba ya kutokutoza kodi mara mbili, yaani double taxation agreement na nchi yetu na nchi mbalimbali. Mwaka jana nilichangia jambo hili pia na narudia tena. Nchi yetu iliingia mikataba ya kutotoza kodi mara mbili na nchi mbalimbali kwa lengo la kuondoa vikwazo vya kibiashara lakini na kuongeza biashara baina ya nchi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mikataba ilikuwa ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Nchi yetu na Canada kwenye income and capital tax treatment ya mwaka 1995, Finland na Tanzania Income tax and Capital tax ya mwaka 1976, Denmark na Tanzania Income and Capital Tax ya mwaka 1976, India na Tanzania Income Tax Treaty ya Mwaka 1979, Italy na Tanzania Income Tax Treaty ya mwaka 1973, Norway na Tanzania Income and Capital Tax Treaty ya mwaka 1976, South Africa na Tanzania Income Tax Treaty ya mwaka 2005 na Sweden na Tanzania Income and Capital Tax Treaty ya mwaka 1976 na Zambia na Tanzania Income Tax Treaty ya mwaka 1968.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba hii tunajua ni muhimu lakini ya muda mrefu sana. Aina ya biashara leo zimebadilika, mazingira ya biashara yamebadilika, teknolojia imekua na tuko kwenye digital economy. Kwa hiyo kutokana na mazingira niliyotaja hapo juu ni muhimu sana mikataba yetu hii ya kikodi ikarejewa ili kuona nchi zetu zote zinapata manufaa ya mapato yanayostahili ya kikodi katika nchi zetu hizo. Kwa hiyo naomba jambo hili, Wizara ya Fedha walichukue kwa umakini mkubwa. Mikataba hii ni ya muda mrefu, mikataba ya miaka 50. Tuna kila sababu ya ku-review kuangalia ni namna gani nchi yetu inanufaika kupata kodi stahili katika mikataba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu. Ndani ya uongozi wa miaka miwili imesaidia mikataba hii ya kikodi ya tozo mara mbili ya Nchi za Falme za Kiarabu pamoja na Oman, kwa hiyo hatua hii ni muhimu, itaongeza uwekezaji hapa nchini lakini itapanua wigo wa kodi na kwa kukuza uchumi wa Taifa letu. Kwa hiyo tunaipongeza Serikali kwa hatua hii nzuri na Wizara ya Fedha waendelee kusimamia jambo hili kubwa la kukuza uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kuboresha Kitengo cha Ukaguzi wa Kodi (Tax Audit). Tax Audit ni kitengo ambacho kinasaidia sana:-.

(i) Kuimarisha ulipaji wa kodi ya hiari (voluntary tax compliance);

(ii) Kuongeza mapato ya Taifa letu; na

(iii) Inatoa elimu kwa walipakodi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lazima liende sambamba na hawa wakaguzi wenyewe, lazima wapate exposure kwa maana ya kupata mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo. Leo hii tuko kwenye teknolojia ya hali ya juu. Elimu imebadilika biashara zinafanywa kidigitali, kwa hiyo ni lazima na wataalam wetu tuwafundishe, wapate ujuzi wa kutosha. Ziko nchi zilizoendelea zaidi katika eneo hili la ukaguzi. Waende kule wakajifunze kwa ajili ya manufaa makubwa ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja na nashukuru sana ka kupata nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwa kidogo kwenye Wizara hii ya Kilimo, Wizara muhimu sana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayofanya, pia pamoja na kuondoa vikwazo vya kufanya biashara na nchi jirani, kufungua fursa za uwekezaji pamoja na Royal Tour ambayo itapanua sekta ya utalii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kaka yangu Bashe, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanayofanya lakini pia kwa sura ya bajeti hii tunayoiona, ya kutoka bilioni 298.1 mpaka bilioni 751; ni mwanzo mzuri sana wa kuleta mapinduzi ya kilimo katika Taifa letu, tunawapongeza sana. Tuwaombe Wizara isimamie vizuri. Bajeti hii muhimu sana tunaamini kwamba itaongeza tija na faida kwa wakulima wetu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo machache; eneo la kwanza ni eneo la umwagaliaji. Naipongeza Wizara, nimesoma bajeti hii imeongeza fedha kwaajili ya kuwekeza katika maeneo ya umwagiliaji. Sote ni mashahidi, kwamba kumekuwa na upungufu wa mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na upungufu wa mvua. Kwa hiyo, ni vema kabisa wizara ikajielekeza kwenye umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kufanya kilimo kwa msimu wa mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza maeneo machache eneo la Babati Mjini kwenye jimbo langu kuna Kata za Madunga, Nar na Kameyu, pamoja na Ziwa ambalo halikauki maji katika msimu mzima wa mwaka lina maji ya kutosha niombe sana wizara ijielekeze iwasaidie sana watu wetu hawa waweze kujenga miundombinu ya umwagiliaji maana kuna kilimo kizuri sana cha vitunguu maji pamoja na vitunguu saumu. Naamini kabisa Wizara ikijielekeza huku wananchi wetu hawa watazalisha vya kutosha na kutosheleza soko letu la vitunguu na vitunguu saumu ambalo ni muhimu sana hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata za Magugu, Magara, Kiru pamoja na Kisangaji kuna bonde zuri sana la kilimo cha miwa na Kilimo cha Mpunga. Najua wengi mmepita eneo la Magugu, mkipita pale mnanunua mpunga, mchele mzuri sana. Kwa hiyo, niombe sana Wizara hii ya Kilimo; na ninajua Mheshimiwa Bashe ameshafika pale Magugu amejionea milimo cha miwa kwenye shamba pale la Manyara Sugar. Kwa hiyo niombe sana Wizara yetu ya Kilimo iwekeze miundombinu ya umwagiliaji ili tuweze kulima miwa ya kutosha na tuweze kuzalisha sukari kwa manufaa ya wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la umwagiliaji niombe sana Wizara ya Fedha iiwezeshe Benki ya Kilimo (TADB) ili iweze kukopesha wakulima wetu kwa riba nafuu; ninaamini sana hii italeta tija kubwa sana kwa wananchi wetu atafanya kilimo chao na kitawasaidia sana katika kuwainua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, enelo lingine ni eneo la masoko ya mazao. Kutokuwa na masoko ya uhakika ni changamoto kubwa kwa wakulima wetu. Mkulima anahangaika mwaka mzima anafikia kuvuna hajui pakuuza. Naomba sana wizara ifanye utafiti wa kutosha kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata masoko ya mazao yao hasa wavijijini ambao wanategemea kilimo kuendesha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata za Galapo, Qash, Ufana, Secheda, nakadhalika kuna wakulima wazuri sana wa mazao kama mahindi, dengu, maharage, mbaazi na mazao mengine lakini kuna tatizo kubwa la masoko. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iwasaidie wananchi wetu hawa wanaopambana mwaka mzima; wapatiwe masoko ili wajikwamue kiuchumi na kusaidia familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu eneo la upatikanaji wa pembejeo; naomba sana Wizara ya Kilimo iwasaidie wakulima wetu wapate pembejeo kwa wakati, kama mbegu bora na mbolea, ili waweze kufanya shughuli zao za kilimo na kurahisisha kilimo kufanyika kwa wakati; lakini pia kuna dawa za kuua wadudu. Kumekuwa na dawa nyingi sana kwenye maduka lakini haziui wadudu. Kwa hiyo, naomba sana kufanyike utafiti wa dawa bora ya kuua wadudu ili wakulima wetu waweze kuvuna mazao ambayo wanatarajia kuvuna katika msimu mzima wa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache nikushukuru sana kwa fursa hii naninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara ya Fedha na Mipango kwa bajeti hii ya mwaka 2022/2023. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimpongeze mtani wangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba - Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri - Mheshimiwa Hassan Chande, Katibu Mkuu na timu nzima kwa kazi kubwa wanayofanya katika Wizara yetu ya Fedha na Mipango, lakini pia kwa ushirikiano mkubwa sana katika Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti kwa kusoma taarifa vizuri, lakini na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano mkubwa sana sana wanaonipa katika kuongoza Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo; eneo la kwanza ni eneo la utendaji kazi kwa TRA. Niipongeze TRA kwa kazi nzuri, mwaka 2019/2020 tulikusanya wastani wa shilingi trilioni 1.5 kwa mwezi, lakini 2020/2021 tuna wastani wa shilingi trilioni 1.89 ni kazi kubwa tunayofanya. Tunawapongeza sana wenzetu hawa wa TRA pamoja na changamoto zote walizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha ukusanyaji huu wa mapato ya TRA kuna mambo kadhaa ambayo nitayashauri; la kwanza, ni kuimarisha Block Management System; hili ni eneo ambalo wafanyakazi wa TRA hutembelea wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu na katika eneo hili kuna mambo mawili; jambo la kwanza, ni kuwabaini wafanyabiashara wapya ambao bado hawajaingia kwenye mfumo wa kodi na hili likifanikiwa basi tutakuwa tumepanua wigo wa walipakodi katika Taifa letu na hatimaye kuongeza mapato ya TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye eneo hili kuna wafanyabiashara wengi sana wadogo na wa kati ambao bado hawapo kwenye mfumo na ninaamini TRA wakati huu imeajiri sasa wafanyakazi wa kutosha, hii itasaidia sana kuwabaini wafanyabiashara wa kati na wadogo ambao pia hawa hawana access za mikopo katika benki zetu. Kwa hiyo, niwaombe sana Wizara ya Fedha iwabaini hao wafanyabiashara wa kati na wadogo na pia iwajengee mazingira mazuri ya kupata mitaji katika benki zetu za biashara, kwa maana ya kupata mikopo yenye masharti nafuu na riba nafuu ili kubaini wanaolipa kodi katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili katika hii Block Management ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara ambao tayari wamesajiliwa. Tukitoa elimu ya kutosha kwa walipa kodi wetu itaongeza voluntary tax compliance, itaongeza umahiri wa kulipa kodi, lakini bila kutumia gharama kubwa kwa maana kwamba ulipaji wa kodi wa hiyari. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Fedha iwezeshe TRA katika eneo hili ili waweze kutoa elimu ya kutosha na hatimaye kupata kodi katika maeneo yetu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni kufanya marejeo katika mikataba ya kutotoza kodi mara mbili yaani Double Taxation Agreement. Nchi yetu iliridhia mikataba na nchi mbalimbali katika kutotoza kodi mara mbili na nchi hizo ni kama ifuatavyo na naomba noisome; Mkataba wa kwanza ni Tanzania na Zambia mwaka 1968; Tanzania na Italy mwaka 1973; Tanzania na Norway 1976; Tanzania na Sweden 1976; Tanzania na Finland 1976; Tanzania na Denmark 1976; Tanzania na India 1979; Tanzania na Canada 1995; na Tanzania na nchi ya Afrika Kusini mwaka 2005. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mikataba hii yote ilikuwa na nia njema kabisa ya kuvutia wawekezaji (Foreign Direct Investment), kubadilishana teknolojia pamoja na huduma mbalimbali. Lakini mikataba yote hii ni ya muda mrefu sana mkataba wa kwanza wa mwaka 1968 ni miaka mingi karibia miaka 50 na kitu lakini hata wa mwaka 2005 ni miaka 17. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naliomba sana kwa kuwa suala hili ni la kisera naiomba sana Wizara ya Fedha, ni muda muafaka wa kufanya marejeo katika mikataba hii. Katika eneo hili kuna uwezekano mkubwa sana wa kupoteza mapato, kwa hiyo, niishauri sana Wizara ya Fedha iridhie ifanye marejeo ya mikataba hii ya muda mrefu ili tupate mapato ambayo tunastahili katika maeneo hayo ya mikataba ya kodi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni mafunzo kwa watumishi wa TRA. Mafunzo kwa watumishi wa TRA ni jambo la msingi sana hasa kwenye mawanda ya ukaguzi wa kodi, natambua kule kwa Idara ya Walipakodi Wakubwa kuna Kitengo cha International Taxation Unit. Naomba sana bila kuwekeza kwenye elimu na mafunzo kwa watumishi wa TRA itakuwa ni jambo gumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna International Taxation Unit kama nilivyosema, lakini kuna mambo ya digital economic sasa, kuna transfer of pricing, kuna base oration and profit shift. Kwa hiyo, kuna haja kubwa ya kuhakikisha watumishi wa TRA wanapata mafunzo ya ndani na pamoja na nje ya nchi. Sio vibaya pia wakaenda hata wakafanya field attachment kwenye nchi ambazo zimefanya vizuri kwenye maeneo ya ukaguzi ili na sisi kama Taifa tuwe na wabobezi wa kodi waweze kukagua maeneo mbalimbali ikiwemo na maeneo hayo ambayo nimesema ambayo ni ya kwenye biashara za Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili linakwenda sambamba pia na ukaguzi wa kodi za ndani, najua wanafanya kazi nzuri, lakini bado kuna haja ya kuongeza mafunzo kwa wafanyakazi wa TRA katika ukaguzi wa ndani. Tax Audit huwa ni a very good tool ya Voluntary Tax Compliance, kwa hiyo, ni vizuri wenzetu hawa wakapata elimu ya kutosha, ili waweze kuwafikia walipakodi wetu na hatimaye waweze kukagua kodi mbalimbali katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, nitazungumza kwa ufupi eneo la mfumo wa kodi za ndani; tunaipongeza TRA kwa kuwa na mfumo imara sana wa Kodi ya Forodha unaitwa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) unafanya kazi nzuri ya kuonesha mizigo bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye kodi za ndani kuna changamoto ya mifumo, mara nyingi utaona mfumo haufanyi kazi. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Fedha iwezeshe TRA kupata mfumo wa kisasa kabisa wa kodi za ndani kama alivyosema Mheshimiwa Tarimba. Ule kama nilivyosema ni mfumo mzuri, lakini ni lazima iwezeshwe ili tuwe na uhakika mfumo huu kufanya kazi, masaa yote na walipakodi wetu waweze kupata urahisi wa kulipa kodi kama ambavyo inatarajiwa.

Mimi baada ya kusema hayo nishukuru sana niipongeze tena Wizara na niiombe tu Wizara iiwezeshe TRA, ili iweze kukusanya makusanyo ya kutosha ili kuweza kufadhili miradi yetu ya maendeleo na huduma kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Bajeti hii Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, bajeti hii ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Shilingi Trilioni 41.48 kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 inaleta matumaini makubwa sana, italeta mapinduzi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa maono haya makubwa ya kuwaletea Watanzania bajeti inayoleta matumaini makubwa. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri na timu nzima kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara hii kwa kusimamia sana sera za kifedha na za kiuchumi, pamoja na changamoto ya mfumuko mkubwa wa bei hapa duniani, kwa kweli kwa nchi yetu mfumuko wa bei upo katika wigo wa Afrika Mashariki, kwa hiyo wanafanya kazi kubwa wenzetu hawa tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ukiangalia imejielekeza sana kwenye sera za uzalishaji. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo tumetenga bajeti kuanzia Bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi Bilioni 954 kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 ni hatua kubwa sana tuwapongeze sana wenzetu upande wa Serikali. Wizara ya Uvuvi na Mifugo bajeti imetoka Bilioni 168 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi Bilioni 268 ongezeko la Bilioni 100 ni hatua kubwa sana na hii sekta muhimu sana katika nchi yetu. Hatua mbalimbali za kikodi zilizopendekezwa pia zinaonekana kabisa kupanua wigo wa walipa kodi na kupunguza mzigo kwa walipa kodi wachache hapa nchini. Ili kufikia makusanyo haya tunayotarajia Bilioni 41.48 naomba nishauri katika maeneo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni mifumo ya ukusanyaji mapato iliyoko chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), eneo la pili nielekeza kwenye coordination ndani ya Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Dunia ya leo ni dunia ya TEHAMA na Tanzania siyo kisiwa lazima tukubaliane uhalisia kwamba sasa mawasiliano na biashara zote ziko kwenye TEHAMA. TEHEMA imerahisisha maeneo mbalimbali kwenye ulipaji na ukadiliaji wa kodi ni lazima tuelekeze kwa kutumia mifumo, ili kutokupoteza makusanyo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TRA ina mifumo ya high tax ambayo iko ndani ya kodi za ndani, kuna mfumo wa TANCIS ambao upo Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa, lakini kuna e-filing ambayo inatumika kwenye kodi la ongezeko la thamani (VAT). Changamoto iliyopo kwenye mifumo hii yote ni kwamba haisomani, ndani ya taasisi moja muhimu ya kukusanya mapato ya nchi mifumo haisomani, kwa hiyo niombe sana Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania ili mifumo yote iweze kusomana kusiwe na mwanya wa kupoteza mapato ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo ni muhimu sana ikasomana ili endane na wakati, lakini manufaa ya mifumo bora inayosomana ni kama ifuatayo: -

Moja ni kupunguza muingiliano baina ya Maafisa wa Kodi, na Wafanyabiashara na hivyo kupunguza mianya ya rushwa katika nchi yetu. Faida ya pili ni kupunguza mapingamizi ya kodi yanayotokana na ukadiliaji tukiwa na mifumo bora hata assessment zinatoka kwa ubora kwa hiyo utapunguza mapingamizi ya kodi kwenye Bodi za Rufaa pamoja na Mahakama za Rufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kurahisisha ulipaji wa kodi, kwa hiyo tukiwa na mifumo bora inayosomana itarahisisha ulipaji wa kodi na kupunguza usumbufu wa Watanzania na Wafanyabiashara, wetu kwa hiyo kuna haja kubwa sana ya mifumo hii kuwezeshwa ili makusanyo yetu yakusanywe kwa manufaa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunganishe hili na Idara ya Forodha na Ushuru, Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa inachangia zaidi asilimia 40 ya mapato yote ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini changamoto kubwa iliyoko kwenye idara hii sasa ni kukosekana kwa Cargo Scanners. Kamati ya Bajeti ilifanya na ziara katika mpaka wa Namanga tumekuta hakuna Cargo Scanners lakini ukienda Tunduma, Holili, Sirari kwenye eneo hili tumepoteza mapato makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipata hii bila kuwa na Cargo Scanners ni vigumu kutambua bidhaa gani zinaingia nchini kwa hivyo kutokupata makadirio sahihi ya kodi katika maeneo haya. Kwa hiyo niombe sana upande wa Serikali wawekeze kununua Cargo Scanners kwa mikakati mikubwa ili tuweze kuboresha makusanyo ya kodi katika Taifa letu. Tunalenga kupata hiyo bilioni 41 bila kuwa na mifumo sahihi itakuwa ni ngumu sana kufikia malengo haya. Kwa hiyo niombe sana wizara iweze kufanya nguvu kubwa ili tuweze kukusanya makusanyo makubwa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni uratibu wa bajeti za Wizara, tunapanga mipango mizuri sana na bajeti nzuri sana, lakini bila kuwa na Wizara zetu kusomana itakuwa ni vigumu sana katika kuteleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Taifa yetu. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo kwa mfano inapoandaa miradi mbalimbali ya umwagiliaji na kadhalika je inahusisha Wizara ya Ujenzi ambayo itahusika na ujenzi wa barabara kufikia maeneo haya ya uzalishaji, je, inahusisha Wizara ya Nishati, inayohusika na miundombinu ya umeme? Kwa hiyo, tunapoandaa mipango na bajeti yetu ni muhimu sana kukawa na coordination baina ya Wizara zetu ili kuweza kuweka tija na kuweza kutekeleza miradi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili bila coordination ama tunachelewa au tunakwamisha kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi wetu kwa hiyo niombe sana wenzetu upande wa Serikali kuwe na coordination ili tuweze kutekeleza bajeti zetu kwa pamoja. Tunapokosa coordination baina ya Wizara idara na Taasisi inachelewesha miradi lakini tungekuwa tunawasiliana tungepunguza gharama na pia tungerahisisha utekekelezaji wa miradi mbalimbali na kuwa na tija katika Taifa letu, kuna umuhimu mkubwa sana wa coordination ndani ya Serikali ili mambo haya yaweze kufanyika kwa wakati na kwa manufaa makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nashukuru sana kwa fursa, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia kwenye Muswada huu wa marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji Fedha Haramu wa Mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuja na Muswada huu ambao ni muhimu sana kwa Taifa letu. Taifa letu siyo kisiwa, tuko ndani ya dunia hii, kwa hiyo, ni muda muafaka kabisa wa kuleta Muswada huu wa kupambana na fedha haramu pamoja na ufadhili wa ugaidi pamoja na ufadhili wa silaha za maangamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa ushirikiano mzuri kwa Kamati wakati wote wa kuchambua Muswada huu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Omari Kigua kwa kusoma vizuri taarifa ya Kamati mbele ya Bunge lako Tukufu. Aidha, nawapongeza Wanakamati wote wa Kamati ya Bunge la Bajeti kwa umakini wao mkubwa kabisa wakati wa kuchambua Muswada huu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, CPD, pamoja na Kamishna wa FIU kwa ushirikiano mkubwa sana aliouonesha kwa Kamati wakati wote wa kuchambua Muswada huu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye mambo ya jumla tu. Moja, Muswada huu au mapendekezo haya ya Mabadiliko ya Sheria yatatufundisha dhamira ya sheria na utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa kwenye sheria zetu ni dhamira iliyopo kwenye sheria na utekelezaji wake. Hii nayo kwa Muswada huu kwa jinsi tulivyouchambua, kwa kweli unaondoa ombwe kubwa kabisa la kisheria katika utekelezaji wake. Kwa hiyo, ninaamani, Serikali ikisimamia vizuri Muswada huu ambao utaongeza vita dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi utakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa letu. Kwa hiyo, naipongeza Serikali na tunaiomba sana isimamie vizuri ili dhamira itofautiane katika utekelezaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kuongeza mapambano dhidi ya rushwa. Sheria hii itaondoa sana utakatishaji wa fedha. Wale wote wanaopokea rushwa za fedha taslimu nje ya mfumo wa benki na baadaye kuzihalalisha kwa kununua viwanja, nyumba au mashamba, sasa tumeongeza wigo wa watoa taarifa. Kwa hiyo, naamini kabisa, kwa wigo huu basi, mapambano dhidi ya rushwa ambayo pia ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa itaongeza kasi kubwa na ninaamini kwamba rushwa itapungua katika Taifa letu. Kwa hiyo, sheria hii itakuwa na manufaa makubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kudhibiti mapato ya Serikali. Kati ya changamoto ambayo ilikuwa inapata Serikali, hasa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ni baadhi ya Mawakala wa Forodha au Washauri wa Masuala ya Kodi kushiriki ama kutakatisha fedha au kukwepa kodi. Kwa hiyo, naamini kwa wigo huu tunaongeza watoa taarifa. Sasa jambo hili litakomeshwa kabisa maana yake ni kwamba sasa mapato ya Serikali yatakuwa yamedhibitiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linakwenda sambamba na mabadiliko haya pia ni mabadiliko ya sheria yaliyogusa mabadiliko ya taasisi mbalimbali. Moja ni sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Sura 197, Sheria ya Bima Sura 364 na Sheria ya Masoko ya Mtaji na Dhamani Sura 79.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo haya ni muhimu sana kwa sababu taasisi hizi zinashughulika sana na transactions nyingi. Kwa hiyo, ni rahisi sana kutambua miamala shuku. Kwa hiyo, sheria hii ni muhimu sana.

Waheshimiwa Wabunge, naomba niwashawishi kabisa kabisa kwa nia ya dhati ya Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, tuunge mkono Muswada huu upite, una manufaa makubwa sana kwa Taifa letu na pia Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Muswada huu wa Mabadiliko ya Sheria ya PPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Naibu Waziri, na timu nzima, kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia sera ya kifedha na ya kikodi katika nchi yetu. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Jonas Mbunda, Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, pamoja na Wajumbe wengine wa Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa waliyofanya katika kuuchambua Muswada uliokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia maeneo matatu. Eneo la kwanza ni umuhimu wa miradi ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. Naipongeza Serikali yetu, imeendelea kufanya kazi kubwa sana ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutoa huduma za kijamii katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho haya yanayofanywa ya Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yatasaidia sana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, hasa miradi ya maendeleo ya kimkakati na kuipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa hujihusisha na shughuli za kibiashara, hivyo ili kuipunguzia Serikali yetu mzigo wa kibajeti, basi ile miradi yote ambayo ina sura ya kibiashara ni vyema sasa sekta binafsi na sekta ya umma ikaungana katika kutekeleza miradi yote yenye sura ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu ijielekeze katika ku-finance ile miradi ya huduma za kijamii na hii itasaidia sana kupunguza mzigo wa Serikali wa kufanya kila jambo. Kwa hiyo, kwa kuhusisha sekta binafsi, kwa maana ya miradi hii ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, basi ichukue na sekta hii. Pia Serikali yetu ijielekeze kwenye miradi isiyo na mvuto au sura ya kibiashara ili ijikite zaidi katika kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni bajeti ya Mfuko wa Kuchochea Miradi ya Ubia, yaani ya PPP ambayo ni PPP Facilitation Fund. Mfuko huu una jukumu kubwa sana la kuwatafuta na kuwandaa wadau watakaoshiriki katika miradi ya PPP. Miradi hii ya PPP siyo ya muda mfupi, kwa hiyo, mfuko huu lazima uwe na uwezo mkubwa ili kuandaa utaratibu mzima wa kuwapata wadau wa kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mfuko huu kwa mwaka wa fedha huu tunaokwendanao 2023/2024, umetengewa Shilingi bilioni 2.8. Kwa kuzingatia majukumu ya mfuko huu, na kwa kuzingatia kuwa miradi mingi ya PPP inachukua muda mrefu, naiomba sana Serikali iongeze bajeti katika mfuko huu ili basi wapate muda wa kutosha wa kuandaa wadau mbalimbali watakaoshiriki katika miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2021/2022 - 2025/2026, yako malengo ambayo tumeweka, kwamba miradi hii ya PPP iweze ku-mobilize asilimia 17 ambayo ni sawasawa na trilioni 21 katika kutekeleza mpango mzima wa miaka mitano. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa sana wa Serikali kuona namna bora ya kuongeza bajeti katika mfuko huu ili iweze kupata miradi ya kutosha katika kutekeleza majukumu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni mitaji ya miradi ya PPP. Kabla ya marekebisho ya sheria hii iliyoletwa leo na Serikali, kanuni za awali zilikuwa zinataka, ili mbia aweze kushiriki katika miradi ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi, alikuwa lazima awe na miradi minimum ya 20 million dollars ambayo ni sawasawa na Shilingi bilioni 45. Kiwango hiki kilikuwa kinawatenga Watanzania wengi sana kushiriki katika miradi hii ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali, katika marekebisho yaliyofanyika sasa imefanya kazi nzuri sana, kwamba sasa Mtanzania mwenye mtaji chini ya dola milioni 20 atashiriki kwenye miradi midogo ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, lakini kwa miradi mikubwa basi ni kuanzia dola milioni 20 na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa sana na jambo hili litaunganisha Watanzania wengi kushiriki katika miradi hii ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi. Vile vile jambo hili litachangia sana katika kukuza uchumi wa Taifa letu, kukuza pato la Taifa na kupunguza matatizo ya nchi ya balance of payment au balance of trade na nchi ambazo tunafanyanazo biashara hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kupata fursa. Naunga mkono hoja. (Makofi)