Supplementary Questions from Hon. Samweli Xaday Hhayuma (21 total)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naitwa Eng. Samweli Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji lililopo Butiama lipo pia kwenye Mji wa Katesh kwenye Jimbo langu; na kwa kuwa Serikali imeshawekeza shilingi bilioni 2.5 kuleta maji mjini na maji yale sasa yapo tayari kutumika. Je, Wizara iko tayari kuongeza fedha kidogo ili maji yaweze kusambazwa kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuongeza fedha katika miradi ambayo ipo katika hatua za utekelezaji ni jukumu la Wizara. Hivyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge fedha zitakuja kwa awamu kama ambavyo imekuwa kawaida yetu kuhakikisha mradi huu unafikia lengo la kupata maji bombani. Lengo la Wizara siyo tu kujenga hizo structures ambazo zipo tayari, tutaleta fedha kuhakikisha maji sasa yanafika bombani.
MHE. SAMWELI H. XADAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, kwa kuwa kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kufuata mipaka ya kiutawala katika kutoa huduma za umeme, kwa mfano, Kata ya Masakta iko kwenye Wilaya ya Hanang kiutawala lakini inahudumiwa na TANESCO Babati na hii imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi kufuatilia huduma. Je, Serikali ina mkakati gani kurekebisha tatizo hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imefanya kazi kubwa kwenye mradi wa REA kupeleka umeme vijijini lakini kwenye vijiji husika maeneo yanayofikiwa au watu wanaopata umeme ni wachache. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanapata umeme na kufika kwenye hatua ya vitongoji hasa kwenye Jimbo langu la Hanang? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Samweli Xaday, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya maeneo ambapo mikoa au wilaya za ki-TANESCO haziendani na mikoa au wilaya za kiserikali na nia kuu ya Shirika la TANESCO chini ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wananchi katika maeneo ambayo yanafikika kirahisi. Kwa kutoa mfano katika Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Kiteto inahudumiwa na Mkoa wa Dodoma lakini tunayo wilaya ya ki-TANESCO inaitwa Simanjiro na wilaya nyingine inaitwa Mererani. Wilaya ya Simanjro ki- TANESCO inahudumiwa na Mkoa wa Kilimanjaro lakini wilaya ya ki-TANESCO ya Mererani inahudumiwa na Arusha.
Mheshimiwa Spika, kwa wanaofahamu ni rahisi sana kutoka Simanjiro kwenda Kilimanjaro, ni rahisi sana kutoka Mererani kwenda Arusha kuliko kurudi Makao Makuu ya Mkoa wa Manyara ambapo ni Babati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nia ya Serikali ilikuwa ni kuhakikisha kwamba huduma zinawafikia wananchi kirahisi wanapohitaji kwenda ofisini kupata huduma lakini pale ambapo TANESCO inatakiwa iende kuwafuata wananchi kuwahudumia au kwenda kufuata vifaa katika bohari.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepiga hatua kubwa sana ya kuhakikisha miundombinu inafika karibia kila sehemu na hivyo ni rahisi sana kufikisha huduma kwa wananchi mbalimbali kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, kila inapowezekana Serikali imeamua sasa ipeleke utawala wa ki-TANESCO sawasawa na utawala wa kiserikali ili kuhakikisha mtu anapata huduma kutoka kule ambako anategemea kuipata na maendeleo hayo ataendelea kuyaona kadri muda unavyozidi kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ni kweli na kama tunavyofahamu maendeleo ni hatua. Kwa harakaharaka tu mwaka 2007 wakati REA inaanza ilipita vijiji 506 ndio vilikuwa na umeme lakini taarifa zinaonyesha kufikia 2015 tulikuwa tuna vijiji 2018 vyenye umeme na kufikia mwaka huu 2021 taarifa zetu zinaonyesha tuna vijiji 1950 kati ya 12,268 ambavyo viko Tanzania kwa ujumla wake. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba maendeleo ya kupeleka umeme ni endelevu na kadri Serikali inavyoendelea kupata pesa kwa kujibana na kwa kujihamasisha yenyewe inaendelea kuepeleka huduma hii na tutahakikisha inamfikia kila mwananchi anayehitaji kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SAMWEL X. HHAYUMA: Ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali yenye kutia matumaini, nina maswali mawili madogo. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii inategemewa na wananchi, upande wa Hanang’ tu zaidi ya 100,000 wa Kata za Gisambalang, Bilmaa, Simbai, Isilo, Wareta na Nangwa yenyewe na kulikuwa na Daraja la Mungurwi B. Daraja lile limechukuliwa na mafuriko ya mvua iliyonyesha 2019/2020. Ni kwa nini Serikali daraja lile lilivyochukuliwa halikuwekwa kwenye mpango wa dharura wa kulirudishia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa daraja lile la Mto Bubu limekuwa likigharimu Maisha ya watu na kupoteza mali kwa kusombwa na maji. Je, Serikali ina mpango gani wa dharulra ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kijamii pamoja na biashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Samwel Hhayuma, Mbunge wa Hanang’, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba daraja la Mungurwi B lilisombwa na maji na ni daraja ambalo liko sehemu ya bonde ambapo baada ya kusombwa lilitengeneza umbali wa mita zaidi ya 200 na hivyo ilikuwa ni ngumu sana kulijenga kama lilivyokuwa na badala yake, daraja hili linafanyiwa usanifu kutoka ilipokuwa kupanda eneo la juu ambalo tunaamini litakuwa ni eneo fupi, lakini pia hakutakuwa na changamoto ya mafuriko. Kwa hiyo linafanyiwa usanifu na baada ya kukamilika tutaanza kulijenga daraja hilo. Hiyo ndio sababu kubwa ambayo hatukuweka daraja la dharura.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la huo Mto Bubu nadhani nimelijibu pamoja na swali la kwanza kwamba baada ya fedha kupatikana na baada ya usanifu kukamilika, basi hilo daraja litakamilika ili kuunganisha wasafiri kutoka upande wa Kondoa kwenda upande wa Mkoa wa Manyara. Kwa sasa tunawashauri wananchi waendelee kupita kutoka Kondoa kupitia Babati kwenda Katesh na kutoka Sambalang kwenda Babati bila kupita kwenye huo mto. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Changamoto ya barabara iliyopo Mbinga ni sawa sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo langu la Hanang hasa Mji wa Katesh. Ule ni Mji ambao una umri zaidi ya miaka 30 na kitu ukiwa ni Makao Makuu ya Wilaya lakini hakuna kilometa hata moja ya lami :-
Je, Wilaya ina mpango gani angalau kuweka kilometa 10 za lami ambayo pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuainisha hapa barabara ambazo ni ahadi za viongozi na sasa hivi nikuhakikishie tu kwamba Serikali ipo katika Mpango wa Kukusanya ahadi zote na kuziweka pamoja, kuzifanyia tathmini pamoja na kuzitengea bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hicho ambacho amekieleza katika Mji wa Katesh ambapo mahitaji yao yapo, nimhakikishie kuwa ahadi zote za viongozi tutaziainisha, tutazitenga katika bajeti kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo katika mji wake wa Katesh.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa, swali la msingi nami pia nina wakulima kwenye jimbo langu la Hanang wanasumbuliwa vivyo hivyo; na malalamiko makubwa ya wakulima hawa ni ubora wa matrekta ambayo wamepewa na pia kukosa usaidizi pale ambapo matrekta haya yanaharibika, kwa maana ya matengenezo na matengenezo kinga na vipuri:-
Je, sasa Serikali iko tayari kuwasimamia hawa NDC pamoja na URSUS, kampuni iliyouza matrekta kuhakikisha kwamba matrekta haya yanahudumiwa kadri ya mikataba ya wakulima?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto kidogo kwa baadhi ya wakopaji kwa wakulima ambao walikopa matrekta haya ya URSUS katika suala la ubora. Kweli suala la teknolojia ambayo ilikuja na matrekta haya kulikuwa kidogo kuna changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara kupitia NDC tulishaligundua hilo na hivyo tumeshaanza kulifanyia kazi kuona namna gani tunaweza kuwa na utaratibu mzuri wa kuwasaidia ili matrekta hayo yanayopata changamoto ya ubora kwa maana ya utekelezaji wa dhana nzima ya kuhakikisha trekta lile linafanya kazi, tumeshaanza kuainisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba wenzetu wa NDC wameshaweka utaratibu mzuri wa kuwa na mafundi maalum ambao watapita kuwasaidia wakulima wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na vipuri, ni kweli matrekta haya kidogo yalikuwa na changamoto ya vipuri kwa sababu ni mapya na ile kampuni ya URSUS ilikuwa bado inaendelea kuleta baadhi ya spare. Kwa hiyo, hili nalo tunalifuatilia kuhakikisha kwamba matrekta haya yanaendelea kuwa na vipuri ili pale ambapo yanapata hitilafu au yanaharibika, basi angalau vipuri vya kurekebisha hitilafu hizo vinapatikana.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi naomba kufahamu Serikali lini itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa Manyara ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wakulima wafugaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge la nyongeza juu ya uwanja wa Manyara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali nililoulizwa na Mheshimiwa Phillip Mwanyika kutoka Njombe Mjini, nimesema kwenye jibu la msingi kwamba viwanja 11 vimefanyiwa tathmini na upembuzi yakinifu, tunajua gharama zilizopo, uwanja wake Mheshimiwa Mbunge na Mkoa wa Manyara kwa ujumla upo kwenye mpango huu, tunatafuta fedha na zikipatikana wakati wowote uwanja wake wa Manyara, pamoja na viwanja vingine 11 ambavyo nimevitaja hapa vitajengwa ili ndege iweze kutoa huduma katika mikoa hiyo. Ahsante.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa Serikali imesema upembuzi yakinifu wa barabara ya Katesh – Hydom unakamilika Juni, yaani mwezi huu; na kwasababu mfumo wa sasa ni wa kusanifu na kujenga. Je, baada ya mwezi wa sita ambapo upembuzi utakamilika Serikali iko tayari kuanza ujenzi mara moja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye barabara hiyo kuna maeneo mawili korofi moja ni daraja ambalo lipo Njia Panda ya Dawar kwenye hiyo barabara ya kwenda Hydom, lakini lingine ni ule Mlima Chavda ambao unakwaza usafiri na usafirishaji kwa kata za Bassodesh, Garawja, Hirbadaw, Getanuwas, Bassotu, Murbadau, Dawar yenyewe na Mogitu na mara nyingi wananchi wamekuwa wakipoteza maisha yao na kupoteza mali.
Je, Serikali itakuwa iko tayari sasa kuweka lami wakati tukitarajia ujenzi uanze kwenye eneo la Mlima Chavda na kujenga daraja imara pale kwenye ule mto uliopo kwenye njia panda ya Dawar?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Samwel Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna aina mbili, ya usanifu na kujenga ama kusanifu halafu baadaye kujenga. Kwa kuwa tayari tunafanya upembuzi yakinifu, itategemea na upatikanaji wa fedha kama utaruhusu tufanye utaratibu wa kusanifu na kujenga. Lakini kama fedha itakuwa haipo, kwa maana ya bajeti ya mwaka tunaoanza kutekeleza baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu tutafanya usanifu wa kina ili barabara hiyo sasa iwe tayari kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa hela hiyo ya mfadhili kutoka benki ya Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu daraja na maeneo korofi tayari tulishatoa taarifa kwa mameneja wote barabara zote ambazo zina maeneo korofi waweze kuyaainisha ili tuweze kuyafanyia mkakati wa kuyatengeneza si tu kwa barabara hii ya Hydom – Katesh bali ni pamoja na barabara zote ili tuweze kuyatengeneza, hata ikiwezekana kuweka lami nyepesi ili yaweze kupitika kwa kiwango chote. Kuhusu madaraja wataalamu wako barabarani wakiwa wanaangalia uharibifu wa madaraja hayo yote na kuweza kuyatengeneza ili baada ya kipindi hiki cha mvua kukatika basi barabara zote ziweze kupitika bila kuleta bugudha. Ahsante.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi.
Naomba kufahamu, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji wa Ziwa Basutwa ambao utasambaza maji kwa vijiji tisa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hhayuma Mbunge wa Hanan’g kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote ambayo inapatikana kupitia maziwa makuu, mito na vyanzo vikubwa vya maji vyote vimepewa kipaumbele na Wizara. Na kama tulivyowahi kumsikia hapa ndani Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ameshaji-commite kwa Serikali, kwamba lazima tutajitahidi kutatafuta fedha ili tuweze kuona maziwa makuu na vyanzo vikubwa vya maji vyote tunakwenda kuvitumia kadri fedha tutakakuwa tunazipata.
MHE. SAMWEL X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Changamoto ya maji inayoikumba Jimbo la Mwibara ni sawasawa na ambayo tunaipata kwenye Mkoa wetu wa Manyara na sehemu kubwa huwa tunapata changamoto kubwa hasa kwenye eneo la kuchelewa kwenye suala la manunuzi. Pale Mkoani hatuna Afisa Manunuzi.
Je, Wizara iko tayari kwa kushirikiana na Utumishi kupeleka Afisa Manunuzi pale Mkoani ili kuharakisha manunuzi? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Hanang kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Jimbo lake. Sisi kama Wizara ya Maji tutaendelea kumpa ushirikiano katika kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji katika Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la Maafisa Manunuzi ni kweli tumeanzisha Taasisi yetu ya (RUWASA) Wakala wa
Maji Vijijini, hii ni mahususi kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji vijijini. Lakini tumekuwa na changamoto ya watumishi hususani katika eneo la manunuzi. Tumeshafanya mazungumzo na wenzetu wa Utumishi na hivi karibuni tutapata Maafisa hao katika kuhakikisha tunakwenda kutatua matatizo ya maji. Eneo ambalo tutalipa kipaumbele kabisa ni Mkoa wa Manyara katika kuhakikisha hii changamoto tunaifanikisha kwa haraka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza; baada ya ujenzi wa Kituo cha Afya Bassotu, Endasak na Gisambalay kukamilika bado tutakuwa na upungufu wa vituo vya afya 25 kwenye Wilaya ya Hanang’. Je, Serikali iko tayari kutufanyia upendeleo mahususi, ili tupate vituo vya afya viwili kwenye bajeti hii tunayoenda kuianza ya 2022/2023?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili; Serikali imetupatia fedha milioni 300 kwa ajili ya kujenga jengo la magonjwa ya dharura kwenye hospitali ya wilaya, lakini wananchi pia, wamehamasishana tumechanga vifaa vinavyokaribia milioni 200. Je, bado tuna upungufu mkubwa wa majengo; Serikali iko tayari kutupatia fedha ili tujenge jengo la wodi kwa ajili ya wanaume? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Hanang’, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Hhayuma kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya kwa ajili ya Jimbo la Hanang’ na nimhakikishie kwamba, Serikali tutaendelea kushirikiana nae kuhakikisha wananchi wa Hanang’ wanapata huduma bora za afya.
Mheshimiwa Spika, upungufu wa vituo vya afya hivi sasa tumeweka mkakati badala ya kujenga kituo cha afya kila kata, tuna kata zaidi ya 3,500 kwa hivyo, kwa sasa tunajenga vituo vya afya vya kimkakati kwenye tarafa, lakini pia kwenye kata zile ambazo zina uhitaji mkubwa kwa maana ya idadi kubwa ya wananchi, umbali mrefu zaidi kutoka kwenye kituo cha karibu, lakini na idadi ya magonjwa.
Mheshimiwa Spiika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutafanya tathmini ya mazingira yale ambayo kimsingi pale Hanang’ tunaweza kujenga vituo vya afya ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, pili; ni kweli Serikali yetu imefanya kazi kubwa ya kupeleka fedha ya ujenzi wa miundombinu ya majengo ya dharura, ikiwepo Hanang’ wamepata milioni 300 na kazi ya ujenzi wa wodi na miundombinu mingine tutaendelea kuitekeleza kwa awamu, ili hospitali ile ya Hanang’ iwe na miundombinu yote inayofanana na hospitali ya wilaya. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka 2021 alifika kwenye Barabara ya Haydom - Katesh na amejionea hali ya ile barabara ambayo inategemewa na wananchi kwa shughuli za kilimo pamoja na huduma mbalimbali: -
Je, ni lini wananchi wa Jimbo la Hanang na Mbulu watawaona wakandarasi wakiwa kwenye kazi kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tutafuatilia na kuona kwamba wakandarasi hawa wanakuwepo site haraka inavyowezekana. Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Hanang, Kata ya Basutu, tuna mgodi wa dhahabu, lakini uzalishaji wake uko chini sana. Je, Serikali iko tayari kushirikiana na mwekezaji ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu kwenye eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara, tunashirikiana na wawekezaji na wachimbaji wadogo. Vilevile sisi kama Wizara lengo letu kubwa ni kusimamia upande wa sera, kanuni na sheria, lakini pia kutoa elimu na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata fursa za kufikia taasisi za kifedha ili waweze kukopeshwa vifaa ama fedha baada ya kukidhi vigezo ili uzalishaji uweze kuendelea na waweze kupata tija kwa juhudi ya uchimbaji wa madini.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wilaya ya Hanang tunachangamoto kubwa sana ya umeme kukatika mara kwa mara, na suluhu ya tatizo hili ni kujengwa kwa kituo cha kupooza umeme pale Mogitu. Serikali iliahidi kutoa zaidi ya shilingi bilioni mbili ili ujenzi huo ufanyike.
Je ujenzi huo utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hhayuma kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye maswali mengine, Serikali imefanya utafiti na kubaini maeneo yanayohitaji kujengwa vituo vya kupooza umeme kwa ajili ya kuhakikisha huduma inawafikia wananchi, na eneo hilo ni mojawapo kati ya maeneo ambayo yametengewa na muda utakapofika huduma hiyo itatekelezwa kwenye jimbo lake.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara ya kutoka Bashineti – Lukumanda – Seche – Basodeshi – Ibadalu – Zinga, kutoka TARURA Kwenda TANROADS? Kwa sababu barabara hii upande wa Singida iko TANROADS na upande wa kutoka Babati kwenda Mbulu iko upande wa TANROADS.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maelekezo yetu katika halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Hanang na mikoa yote, ni kuhakikisha zile barabara ambazo zinaunganisha kati ya halmashauri moja na nyingine, mkoa mmoja na mwingine ambazo zinaangukia katika upande wa TARURA ili ziunganishe mkoa, ni kuanza mchakato wa kuhakikisha sasa zinakuwa na vigezo vya kupandishwa hiyo hadhi.
Mheshimiwa Spika, maelekezo yangu kama katika swali la msingi na kwa Waheshimiwa Wabunge ni hayo na tutafuatilia maelekezo hayo kwa nia moja tu ya kutaka kuwasaidia wananchi katika maeneo yenu.
MHE. ENG. SAMWEL X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Haidong - katesh imeshatengewa milkioni 300 kwa ajili ya ujenzi na milioni 280 kwa ajili ya usanifu wa kina. Je, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pilli, Barabara ya Nangwa – Kondoa ina daraja ambalo limekuwa likikwamisha wananchi, daraja la Munguli, ilitengewa milioni 600. Je, ujenzi wake utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Xaday, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Hydom – Katesh ipo kwenye mpango na imepangiwa fedha. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa utekelezaji ni mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Daraja la Munguli linalounganisha Kondoa na Hanang pia limetengewa fedha kwa ajili ya kulijenga Mwaka huu wa fedha. Ahsante.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu kwa kuwa mashamba ya Murujanda, Sechet ambayo yako chini ya Mwekezaji kwa sasa uzalishaji uko chini ya kiwango na aliahidi kwamba ndani ya mwaka mmoja ataboresha.
Wizara ina kauli gani katika kuhakikisha kwamba tunapata Wawekezaji ambao wako makini au kuwapatia wana Hanang’ maeneo hayo?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Hanang’ kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna mashamba yalichukuliwa na Wawekezaji mojawapo ni Ngano Limited katika Mkoa wa Manyara Wilaya ya Hanang’ na uwezo wake wa kuyatumia hauzidi asilimia 30. Aliingia makubaliano nasi kama Wizara ya Kilimo na kutuambia kwamba tumpe span ya mwaka mmoja, ataweza kufanya matumizi kwa kiwango cha asilimia 100 mpaka sasa amefeli.
Mheshimiwa Spika, hivyo, Wizara sasa hivi tunawasiliana na wenzetu wa TIC na kuwasiliana na wenzetu wa Hazina ili tumuite Mwekezaji huyu, tukae naye aweze ku- offload hekari zaidi ya 30,000 ambazo ameshindwa kuzitumia mpaka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninatumia Bunge lako Tukufu kuwaambia Halmashauri ya Hanang’ kwamba eneo la Basutu lisibadilishwe matumizi litabaki kuwa eneo la uzalishaji wa ngano. Hili ni jambo muhimu sana na Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani, wahakikishe hawabadilishi eneo la Basutu kulipelekea matumizi mengine isipokuwa kwa ajili ya matumizi ya ngano. (Makofi)
MHE. SAMWEL X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Barabara ya Nangwa- Gisambalang-Kondoa inayotegemewa na Kata ya Gisambalang, Dirma, Simbai, Sirop na Wareta ina daraja ambalo limekatika toka mwaka 2019.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga hilo Daraja la Muguri B?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, daraja alilolitaja ambalo liko sasa hivi kwenye usanifu na tunategemea kwenye mwaka wa fedha ujao daraja hilo lianze kujengwa. Ahsante.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itahamisha barabara ya Bashnet – Bassodesh – Hirbadaw - Singida kutoka TARURA kwenda TANROADS kwa kuwa upande wa kutoka Bassodesh - Hirbadaw ipo TANROADS na Singida ipo TANROADS matengenezo yake huwa yako tofauti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Xaday Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nizielekeze tu halmashauri zenye mahitaji hayo zifuate taratibu na utaratibu unaeleweka unaanzia ngazi za halmashauri baadaye zinaenda katika Bodi ya Barabara Mkoa halafu zinapelekwa Wizara ya Ujenzi kwa ajili ya uthibitisho. Kwa hiyo sisi tunapokea tu kama ombi ili hizo taratibu ziweze kufuatwa, ahsante sana.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, changamoto ya ufinyu wa maeneo ya kutolea huduma ya afya ya mama na mtoto hasa eneo la kujifungulia ipo maeneo mengi ndani ya Wilaya yangu ya Hanang.
Je, sasa Serikali haioni ni wakati muafaka kufanya tathmini ya jumla wakati tukiendelea kupanga mpango wa kujenga kituo cha afya kila Kata ili kufanya maboresho katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili fedha zilizotengwa kwa zahanati ya Laghanga, milioni 10. Je, Serikali haioni kwamba hizo fedha ni kidogo haiwezi kutosheleza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba zahanati zile ambazo zilijengwa miaka ya nyuma zilikuwa ndogo na vile vyumba vya kujifungulia vilikuwa finyu lakini kwa sasa Serikali imeboresha sana ramani zetu, ramani zetu ni kubwa zina vyumba vya kutosha vya kujifungua, lakini pia vya kupumzika wakina mama baada ya kujifungua. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba kwa ramani za sasa tutajenga zahanati zenye nafasi za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujenga vituo vya afya kila Kata utaratibu wa Serikali tutajenga vituo vya afya vya kimkakati katika maeneo ya kimkakati ambayo yana idadi kubwa ya watu lakini umbali mkubwa kutoka kituo cha huduma cha Jirani zaidi. Lakini hii shilingi milioni 10 imetengwa kutoka mapato ya ndani na chumba kinakwenda kuongezwa katika jengo lile ambalo linatumika kwa sasa, kwa hiyo tunaamini itatosha na kama haitatosha basi Serikali itaongezea kuhakikisha kwamba chumba hicho kinakamilika. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Mogitu - Hydom kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, barabara aliyotaja Mheshimiwa Hhayuma, ni link kati ya Barabara ya Babati - Hydom kwenda Sibiti. Kwa hiyo itakavyoanza kujengwa, hicho kipande kitakuwa ni sehemu ya hiyo barabara.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba nifahamu ni lini Serikali itakamilisha usambazi wa maji Ziwa Basutu ambako imefikia tu eneo moja kwa sasa na maeneo yaliyotarajiwa ni 12?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kwanza anafanya kazi kubwa nzuri na nimekwishafika katika Jimbo lake. Kikubwa ahadi ni deni, Serikali na dhamira ya Rais wetu tutahakikisha kwamba tunakwenda kuyatumia maji yale ya Ziwa Basutu na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.