Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Samweli Xaday Hhayuma (7 total)

MHE. SAMWELI H. XADAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha kupooza umeme Mjini Katesh kwani kuna line ndefu ya Km 780 hivyo kusababisha umeme kukatika mara kwa mara Wilayani Hanang?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI aljibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samwel Hhayuma Xaday, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) limeanza taratibu za ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo kidogo (switching yard) cha kilovoti 33 kutoka njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 inayoendelea kujengwa kutoka Singida hadi Namanga katika Kijiji cha Mogitu Wilayani Hanang.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kituo hicho utaboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya Wilaya ya Hanang na maeneo jirani utaanza mwezi Julai, 2022 na kukamilika Juni, 2023. Gharama ya mradi ni takribani shilingi bilioni 2.6. Utekelezaji wa mradi huu utagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.
MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi ya mabasi ya Mji wa Katesh?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma Mbunge wa Hanang kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ni miongoni mwa mwa Halmashauri zilizokidhi vigezo vya kupatiwa fedha za ujenzi wa stendi ya mabasi kupitia Mpango wa Mradi Mkakati katika Halmashauri. Lengo la Serikali kuanzisha Mpango huu ni kuziwezesha Halmashauri kubuni miradi itakayoziongezea mapato ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Stendi ya Mabasi ya Katesh wenye gharama ya shilingi bilioni 5.60 ni miongoni mwa miradi 20 ya kimkakati nchini ambayo utekelezaji wake ulisitishwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye hatua za mwanzo za utekelezaji. Serikali ilizifanyia kazi changamoto hizo kupitia timu ya wataalam iliyoundwa na kutafuta namna bora ya kutekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, timu ilitoa maoni kadhaa yaliyotakiwa kutekelezwa na Halmashauri ya Hanang ikiwa ni pamoja na kupitia upya vipengele vyote vya mkataba, hususan muda wa mkataba na masharti ya dhamana ya awali kwa maana ya advanced payment guarantee. Hadi Machi, 2021 Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imekamilisha taratibu zote kama ilivyoelekezwa na timu ya wataalam tayari kwa kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Hivyo, mradi utaendelea baada ya Wizara ya Fedha kupitia nyaraka hizo na kujiridhisha.
MHE. SAMWEL X. HHAYUMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Kondoa – Gisambalang – Nangwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Samwel Xaday Hhyuma, Mbunge wa Hanang’, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kondoa - Nunguri - Mtiriyangwe - Gisambalang - Nangwa yenye urefu wa kilometa 81.4 ni barabara inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini TANROADS baada ya kupanda hadhi mwaka 2010 kutoka barabara ya wilaya na kuwa barabara ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya ukarabati ili ipitike kwa mwaka mzima. Katika mwaka wa fedha huu 2020/2021, barabara hii ilitengewa jumla ya milioni 888.8 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali na ukarabati na Shilingi milioni 60 kwa ajili ya usanifu wa Daraja la Mungurwi. Serikali itaiweka barabara hii katika mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii kuhakikisha kuwa inapitika vizuri majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Katesh – Hydom kwa kiwango cha lami ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za afya katika Hospitali ya Hydom pamoja na usafirishaji wa mazao hasa ngano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Hanang, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Katesh – Hydom yenye urefu wa kilometa 67 ni sehemu ya barabara ya mchepuo wa Mbuga ya Serengeti (Serengeti Southern Bypass) ambayo inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu wa Barabara ya Mchepuo ya Mbuga ya Serengeti (Serengeti Southern Bypass) yenye urefu wa kilometa 575.6 inayojumuisha barabara ya Karatu – Hydom – Lalago hadi Maswa yenye kilometa 446.6, Katesh – Hydom yenye kilometa 67 na Kolandoto – Lalago yenye kilometa 62 inatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Ujerumani. Upembuzi yakinifu unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, mwaka huu 2021. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Katesh – Hydom utaanza pindi usanifu wa kina utakapokamilika na kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Makao Makuu ya Tarafa za Basotu, Endasak na Balangdalah kunajengwa Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang’, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga vituo vya afya katika Tarafa na Kata za kimkakati ambapo, katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 58.25 zimepelekwa kujenga vituo vya afya 233 kote nchini.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 Halmashauri ya Hanang’ ilipokea shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Tarafa ya Simbalay Kata ya Gisambalang na ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Hanang’ kupitia mapato ya ndani wametenga na kutoa kiasi cha Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuendelea na upanuzi wa Kituo cha Afya Bassotu. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 500 kimtengwa katika mwaka 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Endasak.

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa vituo vya afya katika Halmashauri unajumuisha fedha za mapato ya ndani na maelekezo mahususi yametolewa kwa halmashauri zote nchini kutenga fedha za ujenzi wa vituo ili kuboresha huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti wa kujua sababu za kusambaa kwa maji ya Ziwa Bassuto na kuhama kwa samaki kwenye Ziwa Eyasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujiibu swali la Mheshimiwa Samweli Hhayuma, Mbunge wa Hanang kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeona hakuna haja ya kufanya utafiti wakujua sababu ya kusambaa kwa maji na kuhama kwa samaki ziwa Bassuto. Sababu kuu ni kujaa maji wakati wa mvua nyingi, ziwa hilo ni dogo halina uwezo wa kuhifadhi maji mengi yanayosababishwa na mvua nyingi. Aidha, maji hayo hutawanyika na kuingia Ziwa Eyasi na kwa kuwa Ziwa Bassuto lina viumbe mbalimbali ikiwemo samaki, maji hayo yanapoingia kwenye Ziwa Eyasi huingiza na viumbe mbalimbali wanaoishi kwenye Ziwa Bassuto ikiwemo samaki. Hali hii inasababisha wananchi wanaotegemea samaki wa Ziwa Bassuto inawabidi kupata samaki hao kwenye Ziwa Eyasi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa viongozi wa Wilaya ya Hanang kuendelea kuhamasisha wananchi kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo Maziwa ya Bassuto na Ziwa Eyasi.
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga vyumba vya kujifungulia akina Mama kwenye Zahanati za Dirma, Laghanga na Getanus?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Samweli Xaday Hhayuma, Mbunge wa Jimbo la Hanang, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vituo vya kutolea huduma za afya kutoa huduma ya kujifungua, zikiwemo zahanati za Dirma, Laghanga na Getanus zilizopo Halmashauri ya Hanang. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Halmashauri ya Hanang itatenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kujifungua katika jengo la Zahanati ya Laghanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, upanuzi wa vyumba vya kujifungua katika zahanati za Dirma na Getanus utafanyika katika mwaka wa fedha 2024/2025. Ahsante.