Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka (7 total)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona.

Kwa kuwa mgogoro unaoendelea kati ya askari wetu wa uhifadhi na wananchi wanaozunguka katika msitu wa Marang unafanana kabisa na mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya wananchi wa vijiji vya Kimotorok kwa upande wa Simanjiro na Kijiji cha Kiushiuborko kwa upande wa Kiteto dhidi ya pori la Mkungunero Game Reserve askari wanaoishi Mkungunero Game Reserve na kwa kuwa mgogoro huu ni wa muda mrefu na ulifikia Serikali kukubali kurudisha eneo ambalo walipima kwa makosa kinyume na GN iliyotakiwa Mkungunero Game Reserve imebaki Kondoa sasa imevuka mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaamua sasa kuja kukaa na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Mkungunero Game Reserve kumaliza mgogoro huu ili kuepusha maisha wa watu na vitendo vinavyofanana na hivi ambavyo Waziri akihitaji, hata hapa ndani nitoe ushahidi wa vitendo vya kinyama walivyofanyiwa wananchi wa Kimotorok na wahifadhi, nitakupa kwenye simu yangu hii? Nitakupa nashukuru sana naomba swali langu lijibiwe. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi ambao aliutoa awali, lakini pia niweze kumjibu Mheshimiwa Ole-Sendeka kwamba tunapotaka kutatua tatizo lazima twende kwenye kiini cha tatizo. Wote tunajadili hapa na hakuna siri ni kweli yanatokea mapigano kati ya askari wa Maliasili pamoja na wananchi, lakini mapigano haya yanatokea ndani ya maeneo ya hifadhi.

Kwa hiyo kwanza Mheshimiwa Ole-Sendeka na Waheshimiwa Wabunge wote tusaidiane kuelimisha wananchi wetu kwanza tusiingie, na endapo wananchi wanaingia kwa bahati mbaya na akatendewa visivyo tutoe taarifa, tupate huo ushahidi, tuwawajibishe askari hawa ambao hawafanyi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshawawajibisha askari kadhaa, nilitoa takwimu hapa, askari 61 tumewafukuza kazi kwa sababu ushahidi umeletwa. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge pale wananchi wetu ambapo wanafanyiwa ndivyo sivyo tuletewe ushahidi ili tuwashughulikie askari hawa, lakini na sisi tuna wajibu wa kuwashauri na kuwaelekeza wananchi wetu tusiingie kwenye maeneo haya yaliyohifadhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili ameongelea suala la Mkungunero, tulifanya kikao mimi Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Mheshimiwa Olelekaita kuhusiana na Mkungunero kuhusiana na dispute ya mpaka wa Mkungunero na tukakubaliana tunapeleka wataalam kwenda kuhakiki mpaka huo kwa mujibu wa coordinates ambazo zimewekwa kwenye GN. Niseme hapa kuna tatizo moja, katika maandishi katika maneno imesema ni Wilaya ya Kondoa lakini coordinates zimefika Wilaya ya Kiteto, sasa kitaalam zile coordinates zina prevail, kwa hiyo, wataalam waende wakatuoneshe coordinates hizi zinatakiwa kuvuka au zisivuke ili tutatue mgogoro huo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara inayotoka Arusha, Simanjiro, Kiteto, Kongwa umekamilika na ni ahadi ya muda mrefu ya ilani za uchaguzi kadhaa. Je, ni lini Serikali Sikivu ya CCM itaanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sendeka Mbunge wa Simanjiro kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii aliyoitaja ni barabara muhimu sana hasa kwa mikoa ya Arusha Manyara na Dodoma na nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kati ya barabara ambazo ziko kwenye mpango na kwa kuwa usanifu umeshakamilika Serikali inatafuta fedha ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami katika awamu ambayo ime...

MWENYEKITI: Ahsante ameshakuelewa barabara inajengwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza nia yake ya kuendelea kurejesha imani ya wafanyabiashara na kujenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wafanyabiashara. Na kwa kuwa sasa hivi Serikali inaendelea kujadiliana na watu hawa wa maduka ya kubadilisha fedha.

Je, Serikali itakuwa tayari kuweka bayana kiasi cha fedha kilichokusanya wakati wa operation hiyo, na kiasi cha fedha ambazo zitakuwa zimerudishwa kwa wale wasio na hatia na sababu zitakazopelekea wale ambao fedha zao zitachukuliwa na kwamba zitakuwa zimechukuliwa kwa misingi ipi? Naliweka hili na naomba swali langu lijibiwe. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ole-Sendeka, Mbunge wa Simanjiro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni sahihi kabisa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria sana kuhakikisha kwamba imani ya wafanyabiashara inaimarika Zaidi. Na kama ambavyo Mheshimiwa Rais mwenyewe amekuwa akisema kwamba Serikali yake itahakikisha kwamba itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inaibua vyanzo vya mapato. Jtihada mbalimbali mmeshaziona ambazo Mheshimiwa Rais mwenyewe binafsi amezifanya katika kuhakikisha kwamba anahamasisha uwekezaji nchini ili tuweze kupata wawekezaji wengi wakubwa waweze kutupatia kodi katika nchi hii; na amesema mara kadhaa kwamba hataki kuona kodi ya dhuluma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wizara ya Fedha na Mipango tutakuwa watu wa mwisho sana kuona kwamba kama kuna mwananchi yeyote anadhumumiwa kupitia utaratibu wa kodi na tukalifumbia macho jambo hilo.

Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba katika hoja hii hawa ambao wanahusiana na maduka ya fedha za kigeni tumefuatilia kwa kina na tumebaini kulingana na taarifa ambazo tunazo na vielelezo kadhaa ambavyo tunavyo, kwamba walihusishwa wenyewe mara kadhaa katika mchakato mzima wa mgogoro uliojitokeza. Imani yetu ni kwamba kama nilivyozungumza, kwamba wengi wao wamekubaliana na hali halisi baada ya kupewa ushahidi juu ya matukio mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini kama kuna wale mnadhani bado, basi bado nafasi hiyo ipo kwa sababu Serikali hii imetoa mwanya na nafasi kwa yeyote ambaye anadhani bado hajatendewa haki kuweza kufuata taratibu za kudai haki yake ili aweze kuipata.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya nyongeza. Kwa kuwa janga la mwaka huu na mwisho wa mwaka jana inalika nguvu za ziada za Serikali katika kutenga fedha za kutosha kuchimba mabwawa katika maeneo ya nyanda kame. Je, Serikali itaweka bayana idadi ya mabwawa yatakayoweza kujengwa ili kunusuru hali iliyotokea juzi isirejee kabla ya bajeti ya mwaka 2022/2023 kuanza?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba jambo hili la idadi hasa liwe ni jambo la utendaji kazi. Kwa hivyo, sisi tutawasiliana halmashauri yake tupate namba halisi ili tuweze kulifanyia kazi.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, utekelezaji wa agizo la Rais la kupeleka maji katika Kata Nne za Mererani, Endiamtu, Naisinyai, Shambarai na Oljoro Na. 5 umeanza katika Kata Mbili za Mererani na Indiamtu.

Je, ni lini sasa Wizara itatekeleza agizo hilo la Rais katika Kata zilizosalia kupitia Mradi ule Kabambe wa bilioni 400 wa Jiji la Arusha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maagizo ya Mheshimiwa Rais kinachofuata ni utekelezaji, ndiyo maana katika Kata Nne tayari Mbili zimeshaanza kutekelezwa na Kata hizi Mbili pia lazima tuje tuzitekeleze ndani ya muda ambao Mheshimiwa Rais ametuagiza.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Wizara ya Mifugo ikiongozwa na Waziri na wewe Mheshimiwa Naibu Waziri, mlikuja wakati wa janga la mwaka 2020 la ukame Wilayani Simanjiro na kushuhudia vifo vya mifugo mingi, mliahidi kutokana na upungufu wa majosho tuliokuwa nayo mtatujengea au mtatoa fedha ya majosho 20; kinyume chake, bajeti iliyofuata mwaka 2021 mmetupa majosho mawili.

Je, lini sasa Serikali itatoa hizo shilingi milioni 400 ili kukamilisha majosho yale ambayo yataungana na nguvu za wananchi ili kuepusha vifo vya mifugo katika nyanda hizo kame?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ole-Sendeka Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika maeneo ambayo yamekuwa yakiathirika kwa kiasi kikubwa na ukame ni pamoja na Mkoa wa Manyara hasa Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Kiteto. Katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa majosho na mabwawa.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Ole- sendeka atupatie vile vijiji ambavyo wamekubaliana viende vikajengewe majosho ili kusudi Serikali iweze kutekeleza kazi hii ya kuhudumia wafugaji, ahsante.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Naomba tu nimuulize Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma awali ulikuwa unaipa Serikali ya Tanzania 20% na 80% ilikuwa inakwenda kwa mwekezaji wakati uwekezaji wake ulikuwa ni dola milioni 600 tu kati ya dola bilioni tatu zilizokuwa zinahitajika. Je, Serikali imeweka mkakati gani wa dhati wa kuhakikisha kwamba sisi tunanufaika zaidi ukizingatia kwamba chuma cha Liganga ni jiwe ambalo liko juu wala huchimbi unafanya kukata tu kama keki ya harusi? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli mradi huu gharama yake jumla kwa tathmini za wakati ule ilikuwa ni bilioni tatu, mwekezaji huyu katika mkataba ule wa awali alikuwa awekeze kwa maana ya fedha kianzo dola milioni 600.

Mheshimiwa Spika, tunaamini katika majadiliano ambayo tunaendelea nayo sasa tutaona namna gani sasa kuhakikisha mwekezaji huyu anaweka fedha au mtaji wa kutosha ili sisi kama nchi tuweze kunufaika, zaidi katika mkataba huu hatuweki fedha yoyote lakini zaidi kupitia sheria zetu tutakuwa wanufaika wakubwa kwa sababu zile asilimia 20 ni interest ambayo sisi kama nchi hatuwekezi fedha bali kutokana na utekelezaji wa mradi huu sisi hizo ni asilimia ambazo tayari Serikali tunapata bila kuingiza mtaji wowote katika mradi huu.