Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka (1 total)

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kwanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia Maazimio yote mawili yaliyopo mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu Afrika na dunia nzima imeshuhudia upendo usio na mfano ulioonyeshwa na Watanzania walipojitokeza kumsindikiza, kumuenzi na kumuombea Hayati mpendwa wetu Dkt. John Pombe Joseph magufuli. Upendo waliouonesha Watanzania katika maeneo ulikopitishwa mwili wa Mheshimiwa Dkt. John Pomba Joseph Magufuli na maombi na dua yaliyofanyika nchi nzima katika maeneo ambapo mwili wa mpendwa wetu haukuweza kufika ni ushahidi tosha kwamba Watanzania walikuwa na imani kubwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais wetu wa Awamu ya Tano alifanikiwa kujijengea uhalali wake mara alipochaguliwa na Watanzania kuwa Rais wa nchi yetu. Rais hayati Mzee Benjamin William Mkapa aliwahi kusema: “Kazi ya uongozi ni kuonyesha njia na watu wanakufuata si kwa sababu wanakuogopa ila kwa sababu wanakuamini na imani ya kweli haitokani na maneno bali matendo”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matendo ya hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yalimjengea heshima, imani ya Watanzania kumfuata. Kazi aliyoifanya kwa miaka mitano akisaidiana na Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan amekijengea chama chetu na Taifa letu uhalali wa kuendelea kuheshimika Barani Afrika na duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi nyote ni mashahidi na Watanzania ni mashahidi kwamba ukiacha kufanya maombolezo tuliyofanya kwa kujitokeza kila mmoja wetu lakini siku ya kumuaga Afrika ilileta Rais wapatao 16 na Mabalozi wasiopungua 51 waliotoka kote duniani. Pia nchi zote dunia ambazo hazikuweza kuleta Mabalozi na Rais walituma salamu kwa Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kufuatia kuondoka kwa shujaa wa Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba maisha ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli siyo tu yaliwagusa Watanzania yaligusa Afrika na dunia yote. Kinachosikitisha ni kwamba wakati mataifa haya yakitupa pole na kuomboleza pamoja nasi bado kuna Watanzania wenye passport za Tanzania wanaobeza kazi iliyofanywa na hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kazi yetu ni kuendelea kuwaombea msamaha kwa Mungu awafunulie ili siku moja waweze kuijua kweli na warudi kuungana nasi katika kuweka Utanzania mbele hata kama kwa sasa wanalishwa na hao wenye nia ovu na Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii tena kueleza bayana kwamba tunamuenzi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri aliyofanya na tunampongeza mama Samia Suluhu Hassan kwa kupokea kijiti cha kuendelea kuongoza Taifa letu. Wote wawili hawa wamepata uongozi bila ya kuwa na makundi, bila kutoa hata shilingi. Dkt. John Pomba Joseph Magufuli alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa bila kuhonga hata shilingi moja naye alimteua mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza na hatimaye wakaongoza jahazi la nchi yetu kwa muda wa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya miaka hiyo mitano mmeshuhudia kiwango cha kura ambacho CCM imeweza kupata katika uchaguzi wa mwaka 2020. Huu ni ushahidi tosha kwamba tulitekeleza Ilani ya Uchaguzi chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Mgufuli na mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tu uhalali wa uongozi wowote na hasa kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama cha Mapinduzi wa mwaka 1981, ibara ya 107 unatokana na uongozi huo kuendelea kuwa tetezi wa kuaminika kwa maslahi ya makundi au kundi lililokuwa kubwa katika nchi yetu. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba kijiti kinapokabidhiwa kwa mama Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kiongozi kutoka kwenye ngazi za msingi hadi ngazi ya Taifa ya chama chetu na ameongoza Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano na hatimaye Makamu wa Rais, tuna uhakika kabisa nchi yetu ipo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme la mwisho kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nina hakika kabisa miaka hii iliyobaki katika ungwe hii ya miaka mitano itakuwa ndiyo miaka mitano ya kwanza ya mama Suluhu Hassan na miaka mitano mingine itakuwa miaka ya ungwe yake ya pili kwa mujibu wa Katiba yetu. Hili tujiandae kifikra na kimtazamo kwa watu ambao walikuwa wanafikiri 2025 uongozi utabadilika. Ni zamu yao, sisi Bara tuliongoza miaka 23 ya Mwalimu, tukaongoza miaka 25 tena mingine siyo dhambi…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, siyo dhambi sasa kwa Mzanzibar mmoja aliyejipambanua na mwenye sifa kuendelea kuwa Rais katika miaka hii iliyobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)