Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ravia Idarus Faina (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kwanza nataka kupata ufafanuzi juu ya Serikali kwa nini haijajenga Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Zanzibar na hii inapelekea kwamba Waziri na Naibu Waziri wanapofika Zanzibar wanapata tabu sana, wapi watafikia. Kwa hiyo naiomba Serikali ilete ufafanuzi juu ya suala hili.

Mheshimiwa Spika, kwa vile muda ni mchache…

SPIKA: Hebu fafanua hilo likoje.

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Spika, hadi hii leo Zanzibar hakuna Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwa hiyo ni lini Serikali itajenga hiyo Ofisi hili Waziri na Naibu Waziri wanapokuja Zanzibar wawe na sehemu maalum ambayo wanafikia.

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba Serikali itupatie Ofisi ya NIDA pamoja na Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Kusini Unguja ambayo tunakosa huduma hiyo, ukizingatia wananchi wa Wilaya ya Kusini wanakosa huduma nzuri ambayo wanaihitaji kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kuhusu Jeshi la Polisi; hapa nisipopata ufafanuzi mzuri natarajia kushika shilingi.

Kwanza naomba nipate ufafanuzi, ni kwa nini askari polisi anasoma na ahahitimu degree yake ya kwanza na anapomaliza degree yake anapelekwa kozi ya sergent na anapata cheo cha sergent. Je, huyu ambaye kasoma diploma na form six yeye atapewa cheo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeweka utaratibu mzuri tu wa PGO, lakini PGO inatumika katika baadhi ya maeneo, baadhi ya maeneo haifanyi kazi. Inakuwaje Askari Polisi anakaa miaka 15 hajapata rank. Jeshi la Polisi linawapeleka askari, rank pamoja na faini, lakini cha kushangaza mpaka kufikia mwaka 2013 hawana stahiki zao ambazo wanazipata.

Mheshimiwa Spika, vilevile Askari Polisi wanapewa jukumu la kuwachukua watuhumiwa kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine lakini hakuna stahiki zao ambazo wanapata, wanaishia kujaza fomu na hizo fomu zinabakia kwenye mafaili hadi leo hawapati stahiki zao. Hii inaleta usumbufu kwamba huyo ambaye anaenda kumchukua mtuhumiwa ni yeye mwenyewe amuhudumie mtuhumiwa, sijui pesa anaitoa wapi.

Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kumalizia kwa suala ambalo alichangia Mbunge mwenzangu kwamba, Askari Polisi wanahitaji kupatiwa vitendea kazi, haipendezi kuona documents muhimu za Jeshi la Polisi zinapelekwa kwenye vibanda vya kawaida tu kutolewa photocopy ili ifanyike hiyo kazi, hiyo haipendezi kwa kweli. Photocopy machine thamani yake sio kubwa kwamba askari apate tabu kwenda kutoa yeye hiyo photocopy.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa mzima na kusimama mbele ya Bunge lako na kutoa mchango wangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi limeanzisha Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa Jeshi la Polisi, Mfuko huo kwa ajili ya ustawi wa askari, lakini cha kushangaza mpaka sasa hivi hakuna kanuni za kusimamia uendeshaji wa Mfuko huo, hivyo inapelekea kuwa na wasiwasi wa matumizi ya Mfuko huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi limeweka vizuri sheria na miongozo yake kwenye PGO. Kwa nini hawataki kufuata taratibu hizo walizojipangia hasa kwa askari wadogo. Kwa mfano, posho za maaskari wadogo haziendani na vyeo vyao, kama vile posho za mavazi, udereva, kibaka chekundu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, posho za safari, wanapofuata watuhumiwa kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine hawalipwi. Sasa, naishauri Serikali kwa vile katika ripoti ya CAG imebainisha kuwa fedha zinazokusanywa kwenye Mfuko wa Polisi ambazo ni tuzo na tozo, hazipangiwi sheria na kanuni za matumizi yake. Sheria na matumizi yake yaratibiwe kwa mujibu wa Sheria ya Fedha iliyokuwepo nchini ili ziweze kuondoa hizo changamoto za maaskari wadogo na stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nashauri fedha hizo aidha zitumike kwa ujenzi wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za askari ambazo zimechakaa sana. Mashirika na taasisi za umma ziache mara moja kujiingiza kwenye shughuli zinazoweza kufanywa na vijana wetu na akinamama ambao wanataabika na ukosefu wa ajira kama vile usafishaji wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama salama hapa, na kuchangia Wizara ya Habari.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Katiba ya TFF kifungu 2.7 inaeleza TFF itashirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar kwa yale mambo ya kimataifa na ndio kipengele pekee ambacho kipo katika Katiba ya TFF, yenye page 64 lakini cha kushangaza kifungu hiki hakifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakifanyi kazi kwa sababu kunako mwaka 2017 Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar lilijiunga na uanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika CAF. Kwa muda mfupi Shirikisho la Miguu Zanzibar likaondolewa uanachama huo, lakini chakusikitisha na chakushangaza Chama cha Mpira wa Miguu - TFF hakikushiriki lolote juu ya kadhia hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili FIFA inatoa mgao kwa wanachama wake kila mwaka usiopungua dola milioni mbili, lakini miradi hiyo yote ipo Tanzania Bara tu kwa mfano Kigamboni Dar es Salaam na Tanga; Zanzibar hakuna mradi wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika,…

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimwa Ravia kuna taarifa, Mheshimiwa jitambulishe.

T A A R I F A

MHE. SIMAI HASSAN SADIKI: Mheshimiwa naitwa Mheshimiwa Sima Hassan Sadiki, Mbunge wa Jimbo la Nungwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa ndugu mchangiaji kwamba wakati wa uongozi wa Mheshimiwa Tenga alipokuwa Rais wa TFF Zanzibar iliwahi kunufaika na huo mradi ambao anazungumzia kwa kujengewa uwanja wa Gombani, Pemba kule kuwekewa nyasi bandia, lakini toka kipindi hicho si chini ya miaka minane hakuna mradi mwingine wowote wa kimaendeleo uliwahi kufanyika kwamba kwa kutumia fedha hizo. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Ravia unaipokea taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Sadiki.

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo na niunge mkono hoja na huo uhalisia ulivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile Zanzibar haiwezi tena kuwa mwanachama wa CAF wala FIFA, kwa hiyo naomba niishauri Serikali mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, zikutane Wizara mbili za michezo kati ya Zanzibar na Tanzania Bara hili kulijadili mustakhabali mzima wa kadhia hii kwa wakati huu; pili, yafanyike marekebisho ya Katiba ya TFF na ndani ya Katiba ya TFF isomeke Zanzibar kitu ambacho kipo mstari mmoja; Makamu mmoja wa Rais TFF atoke Zanzibar; kuwe na Wajumbe wa Kamati Tendaji wa TFF ambao wanatoka Zanzibar; kuwe na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF watoke Zanzibar na isiwe kama sasa hivi Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar na Makamu ni mwalikwa tu wa Mkutano Mkuu, aende pale akasinzie tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia turejeshe ligi ya Muungano ili tupate wawakilishi sahihi wa Tanzania na tupate kutengeneza timu ya Taifa ya Tanzania Bara yenye ushindani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kama haya hayatekelezeki naomba Bunge lako Tukufu liridhie na liwaruhusu Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar wawaarifu FIFA kipengele cha 2.7 cha Katiba ya TFF hakitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa mzima na kunijalia kuchangia katika Wizara hii na mimi najielekeza katika mpira wa miguu.

Mheshimiwa Naibu Spika, TFF ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ambalo limejipa madaraka ya kuongoza mpira Tanzania kama ilivyo katika Katiba yake Ibara ya Kwanza. Lakini katika Ibara ya 12 imeorodhesha wanachama wake, la kusikitisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar halijaorodheshwa katika orodha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, akija Naibu Waziri nataka anielezee kwa nini TFF inavunja Katiba yake na Baraza la Michezo halichukui hatua yoyote. Kwa nini hadi leo Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake hawajafanya uchaguzi? Wakati Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake ni mwanachama halali kama alivyoorodheshwa katika Katiba Ibara ya 12. Hapa nisipopata maelezo ya kuridhisha nakusudia kuchukua shilingi ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi wa Machi, 2017 Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar kilipata uanachama wa CAF, lakini mwezi Julai, 2017 kiliondoshewa uanachama wake baada ya kukosa sifa za kuwa mwanachama wa FIFA. Mnamo mwezi Machi, 2021 CAF ilifanya mabadiliko yake ya Katiba Ibara ya 4(1) na Ibara ya 4(4); kwa mantiki hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar haliwezi tena kuwa mwanachama wa CAF. Sasa naomba niishauri Wizara ikae na Baraza la Michezo (BMT) na Baraza la Michezo la Zanzibar (BMZ)... (Makofi)

MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba nimpe taarifa mzungumzaji, wakati umefika sasa kurejeshwa kwa Ligi Kuu ya Muungano ili tupate wawakilishi halali wa vilabu Tanzania. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ravia, taarifa umeipokea?

MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa naipokea na ninaiunga mkono kwa asilimia zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naishauri Wizara ikae na Baraza la Michezo (BMT) na Baraza la Michezo la Zanzibar (BMZ); washauriane namna ya kubadilisha Katiba ya TFF na Katiba ya ZFF ili ziendane na uhalisia uliokuwepo kwenye Katiba ya CAF na Katiba ya FIFA ikiwezekana waangalie Katiba ya TOC. Iwapo hili halikufanyika Mwenyezi Mungu akitujaalia mwakani nitalizungumza tena na kuwaomba Wizara waruhusu kuwaeleza CAF na FIFA kwamba TFF na ZFF hawashirikiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nimepunguza naunga mkono hoja. (Makofi)
MUswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. RAVIA IDARUS FAINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kusimama hapa, vilevile nikushukuru wewe kwa kunipa fursa ya kuchangia muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ushauri kwa mambo kama mawili, kwa vile Zanzibar hakuna Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi na walio wengi wahasibu wa Zanzibar ni wanachama wa NBAA, kwa hiyo ningeshauri Serikali mbili zikakaa; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka harmonize ya Muungano hii sheria ikatumika kwa Tanzania nzima ili wahasibu wapate kufanya kazi zao kwa ufanisi mzuri, lakini pili kuna wahasibu ambao wana CPA na wao waweze kufanya kazi zao kwa muongozo uliokuwa sahihi.

Kwa mfano unapofungua kampuni ya ukaguzi wa mahesabu Zanzibar iweze kufanya ukaguzi Tanzania Bara na vilevile utapofungua kampuni ya ukaguzi Tanzania Bara ifanye kazi Zanzibar. Vilevile nipende kutoa ushauri kwamba niziombe tena Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakae na wazipitie Sheria za Fedha ambazo zinaathiri taaluma ya uhasibu ziwekwe sawa kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na kinachonishawishi kuunga mkono hoja ni kwa sababu tu itafungua maslahi makubwa kwa kada hii ya wahasibu na niwaombe Wabunge wenzangu tuupitishe muswada huu wa sheria ili ulete maslahi makubwa kwa wahasibu. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)