Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salum Mohammed Shaafi (6 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia leo kuwepo katika Bunge hili Tukufu. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru wale wote waliosababisha kwa namna moja ama nyingine nami kuwa Mbunge wa kuchaguliwa Pemba. Nawashukuru sana wananchi wangu wa Chonga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kujadili hotuba ya Mheshimiwa Rais. Miongoni mwa mambo aliyoyajadili Mheshimiwa Rais ni suala zima la kudumisha Muungano. Muungano huu umeunganisha nchi mbili; ulikuwa ni Muungano uliounganisha Tanzania Bara na Tanzania Visiwani Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wanzanzibar, sisi Watanzania tunahitaji Muungano wa haki, usawa na wa kuheshimiana. Naomba ifahamike sisi Zanzibar tunayo Mahakama Kuu ambayo ina mamlaka ya kusikiliza kesi zinazohusu masuala ya Zanzibar. Nilikuwa najiuliza maswali na kupata ukakasi mkubwa sana iweje leo kesi inayopaswa kusikilizwa Zanzibar ihamishiwe Tanzania Bara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukirudi tuna kesi kadhaa, natolea mfano kesi ya uamsho. Hili dai liko mahakamani linaendelea, sipendi kuingilia Mhimili wa Mahakama, lakini najiuliza sasa ni takribani miaka nane, kesi hii bado iko kwenye upelelezi, bado haijakamilika ushahidi wake. Je, hakukuwa na mamlaka kwa Mahakama Kuu ya Zanzibar kusikiliza kesi hii mpaka iletwe Tanzania Bara? Hebu tunaomba Serikali mtuambie nini shida watu hawa hadi leo; tunahitaji tuwatendee haki Wazanzibari wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumwomba Rais huyu, Rais msikivu, Rais mtetea wanyonge, Rais anayesema aombewe, nimwombe Mheshimiwa Rais; kama walivyoachiwa wale Waethiopia na hawa Wazanzibari na wao tuwaachie. Kama walivyoachiwa Waethiopia wale, Wazanzibari hawa na wao Mheshimiwa Rais awahurumie, atumie nafasi yake ya Urais kuhakikisha Wazanzibari hawa na wao tunawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende katika suala la mchakato wa Katiba Mpya, ni sehemu ambayo Mheshimiwa Rais aligusia. Katiba hii tutakapoipata tutatatua changamoto na matatizo mbalimbali yanayotuhusu Wazanzibari na yanayotuhusu Watanzania.

Leo najiuliza, iweje referee anachezesha ndani ya uwanja halafu yeye huyo huyo anakuwa ndiye mchezaji wa mpira, anakuwa ndio muamuzi; kweli tutakuwa tuna Tume huru? Tunahitaji Tume huru ili tuwaaminishe Watanzania chaguzi hizi zinavyofanywa ni uchaguzi huru na haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, humu leo sote kila mmoja anafahamu ni namna gani alivyoingia humu. Sote tunajuana humu; waliongia kushoto wanajua, waliongia kulia wanajua, kila mmoja na siri yake. Uchaguzi ulikuwa ni uchaguzi wa shida, ulikuwa ni uchaguzi mtihani. Leo humu wengine ukiwauliza, aah kwani bado mimi ni Mbunge? Ni mtihani mtupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme Taifa hili tunasema tuliombee, hatuwezi Mungu akatupa mafanikio makubwa kama dhuluma inatawala ndani ya nchi hii. Dhuluma ni adui wa haki. Tutakuwa tunadhulumu lakini mafanikio hatuyapati.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa, Kanuni.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Naomba niendelee kusema. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa uliyekuwa unataka kutoa taarifa uniwie radhi, sikuona uko upande gani, kwa hiyo kengele imeshagonga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunajadili Wizara ya Katiba na Sheria ambayo ndiyo msingi wa Taifa letu. Nchi yetu inaongozwa na misingi ya Katiba na Sheria ambayo kila mmoja wetu anapaswa kuifuata na kuiheshimu. Hii ni Katiba ambayo sisi sote humu ndani tuliapa kuilinda na kuiheshimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu kuna mambo ambayo binafsi nadhani sio sawa kuendelea kufanyika. Nikaanza kujiuliza, je, ni watu gani au chombo gani ambacho kina mamlaka ya kuzitumia sheria na kutoa hukumu? Wapo baadhi ya viongozi wa Serikali wanatumia sheria, wanatoa hukumu mikononi mwao pasi na kuheshimu Katiba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona namna gani baadhi ya watu wanavyodhalilishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali. Tunaona kuna baadhi ya viongozi wa Serikali wanawadhalilisha kwa kuwapiga bakora watumishi wengine wa Serikali. Sidhani kama viongozi hawa wamepewa mamlaka, ni kwa sababu wameshindwa kuheshimu Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kwenye mitandao, tuliona Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mmoja…

MBUNGE FULANI: Wa Wilaya.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nazungumzia Mkuu wa Mkoa kule Zanzibar, acha huyu Mkuu wa Wilaya huku, anampigisha pushup mtumishi wa Serikali mbele ya vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi halafu tunakaa tunasema tunaheshimu Katiba wakati wao ndiyo wanaoivunja Katiba hii. Mimi nitoe rai kwamba ipo haja kwa viongozi hawa kupewa elimu juu ya Katiba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema tuna kila sababu sisi Wabunge kuhimizana na kuheshimu mihimili mikuu ya Serikali. Mhimili Mkuu wa Bunge sisi lazima tuwe na kazi moja tu ya kutunga sheria. Mhimili mwingine ambao ni wa Mahakama, tuipe kazi yake ya kutafsiri sheria na Serikali kwenda kutekeleza sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu Serikali ilione hili juu ya watu hawa wanaowadhalilisha wananchi jambo ambalo halikupaswa kuwa hivyo. Walitakiwa wawachukue wapeleke polisi na polisi ifuate taratibu nyingine za kisheria. Ndiyo utaratibu kwa mujibu wa Katiba hii, tukiiangalia ukurasa wa 92 Ibara ya 107A inasema: “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muunganoo itakuwa ni Mahakama na siyo Mkuu wa Mkoa wala Mkuu wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Tunafahamu kwamba utaratibu na mwenendo wa kesi umeandaliwa sheria zake lakini tuna kundi kubwa la watu ambao kesi zao ziko ndani ya upelelezi. Sasa tufike mahali uletwe Muswada wa sheria Bungeni tubadilishe baadhi ya mambo. Hatuwezi kila siku tukasema upelelezi unaendelea, miaka nane, tisa hadi kumi wakati hao ambao upepelezi wao unaendelea wameacha familia, tunawaathiri kisaikolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tufahamu sasa Taifa letu leo linapiga vita chokoraa, wana Watoto, nini faida yetu, wale watoto watakuwa chokoraa. Wameacha wake, wale wake watakuwa wajane. Taifa linahitaji uchumi, wale ambao tumewaweka ndani upelelezi wao unaendelea Taifa litakosa mapato kwa sababu baadhi yao walikuwa ni wafanyabiashara na kila Mtanzania anachangia mapato ndani ya Taifa hili. Naomba sana tutumie fursa tuliyonayo kupitia Bunge hili na vyombo vyenye mamlaka ya kubadilisha sheria, tulete Muswada tubadilishe sheria tuweke ukomo wa upelelezi, tusiende tu kama tunakata kamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kuchangia, tuna Katiba mbili; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar. Ibara ya 93 ya Katiba ya Zanzibar imeeleza kwamba Zanzibar ina Mahakama Kuu na tukirudi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeelezea kwamba nako kuna Mahakama Kuu, kila Mahakama inajitegemea, inafanya kazi pasi na kuingiliwa na Mahakama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kusikitisha, hali ya maajabu tunaidhalilisha nchi yetu na tunaonekana si watu wenye kufuata Katiba. Leo Mahakama upande mmoja inaingilia Mhimili wa Mahakama nyingine. Wako baadhi ya watu wametoka upande mmoja wa Zanzibar wameshtakiwa, kesi zao wamehamishiwa Mahakama Kuu ya Bara. Naiomba Serikali ikija hapa ieleze Bunge hili na Watanzania ni mamlaka gani ambayo imepewa Mahakama Kuu ya Bara kuingilia Mhimili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar watuhumiwa wa Zanzibar kushtakiwa Mahakama Kuu ya Bara. Tuelezeni kwa ufanisi kabisa ili tufahamu na wananchi wetu wajue kwamba kumbe Mahakama Kuu ya Bara ina uwezo wa kusikiliza kesi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nishukuru sana kwa kunipa nafasi hii na niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Chonga kwa kuniamini kwamba naweza kuwatumikia. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia bajeti hii muhimu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia kuweza kukutana hapa na kujadili jambo muhimu ambalo ndiyo msingi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuri Wizara kwa namna walivyoweza kutuwasilishia bajeti hii nasi kuweza kuichambua na kuijadili na kuitolea maoni yetu na kama hatuna la kushauri basi tumepata nafasi hiyo. Mimi leo sina mengi ya kusema lakini naomba niseme machache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza binafsi nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza kwa kipekee kabisa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenye macho haambiwi tazama. Sote tunaona namna Mama yetu anavyoongoza Taifa hili na niseme Mheshimiwa Rais wetu Mwenyezi Mungu kamjaalia kipaji cha hekima na busara. Namuomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema, ampe umri mrefu wa kuzidi kutuongoza Watanzania kusimamia haki na kujali utu wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii kuna mambo mengi yamezungumzwa. Mimi leo naomba nitoe rai na kuishauri Serikali. Mara baada ya kupitisha bajeti hii siku ikifika tunaenda kuwapa fedha Wizara au mamlaka husika. Naomba niishauri Serikali iende ikazisimamie fedha hizi katika yale maeneo yote ambayo yamepangiwa kupewa hizi fedha. Wawasimamie ili tuondokane na ile kadhia ya watu kuhujumu uchumi, watu kuiba fedha za Serikali, watu kuiba fedha za walipakodi wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya tukifanya haya tutakuwa tumedumisha nidhamu Serikalini lakini tutakapoziacha tu hizi fedha ziende ile nidhamu ya fedha Serikalini itakuwa haipo, lakini mara baada ya kuwapa fedha hizi naishauri Serikali sasa iwakumbushe watumishi hawa wajibu na majukumu yao katika kazi zao. Jeshi la Polisi likumbushwe wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mengi yanatokezea wananchi wanalalamika juu ya kadhia ya baadhi ya Wanajeshi la Polisi, yapo mitaani! Leo tukiangalia tu Taifa letu linapita katika hali ya usalama na amani ya kutosha kabisa ni kwa sababu wanasiasa ndiyo walioleta amani hii. Ni wanasiasa ndiyo walioleta amani hii katika nchi hii. Nani anasema haya? Mengi yalipita, kule kwangu Zanzibar mengi yalifanyika kupitia Jeshi hili la Polisi pamoja na vikosi vya SMZ, watu walipigwa, watu walinyanyaswa, walipigwa risasi, yale makovu Wazanzibari wameyafunika, wanaamini sasa tumekuwa kitu kimoja tunasonga mbele, tumesahau yaliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yaliyopita yasije yakarejea tena. Ili yasijirudie lazima Serikali muende mkawakumbushe sasa hawa watumishi wajibu wao katika utekelezaji wa kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niwasemee wenzetu wastaafu. Hawa wastaafu wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu sana, wamejitoa kwa hali na mali, wamejitoa kwa kila hali kuhakikisha kwamba wanatumikia nchi yao. Naomba bajeti hii iwe ni sababu ya kwenda kumaliza kero za wastaafu hawa, isiwe kila mwaka wa bajeti katika Bunge hili tunawajadili hawa wastaafu kwamba bado posho zao hawajazipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wastaafu wengi na wana miaka mingi bado hawajapata posho zao. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kijana mwenzangu, muonekano wa sura yako inaonekana ni msikivu na mtiifu, nenda kalisimamie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu niendelee kusema Serikali hebu nendeni TFF. Wizara husika nendeni TFF mkaangalie kuna nini TFF? Kuna shida gani TFF? Manung’uniko haya yaweze kuisha, niishauri Serikali nendeni huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kikubwa tu na cha mwisho ambacho naomba nikiseme ni kudumisha Muungano wetu na ninachukia sana wanapojitokea baadhi ya watu kuunyoshea vidole upande wa pili kwamba hawaupendi Muungano, sio kweli, wao wanaonyosha ndio ambao hawaupendi Muungano. Hakuna aliyesema hataki Muungano. Sote tunataka Muungano, lakini tunataka Muungano wa haki na usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya nikiamini hapa Wabunge wengi wamesimama, wamesema na ninaishukuru Serikali kwamba wameingiza hizo shilingi milioni 500 ili kuweza kusaidia maendeleo katika majimbo yao, lakini leo, jana na juzi, baadhi ya Wabunge wanahoji fedha hizi je, na kule Zanzibar zitapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa muono wangu mimi naamini sisi sote ni Watanzania. Kama tutabaguliwa Wazanzibari katika fedha hizi sasa hapa ndio tutaanza kuhoji kuhusu suala la Muungano, kwa sababu Serikali yangu ni sikivu, Serikali yangu nawaelewa ni wasikivu, sidhani kwamba ikifika Jumatatu jambo hili litajadiliwa tena humu kwa sababu mimi nafahamu Serikali yangu ni sikivu na jambo hili italisikia na Wazanzibari nao ni sehemu ya Muungano. Hapa Bara Wazanzibari wapo wanafanya biashara, wanalipa kodi, sasa leo iweje eti Wazanzibari wasipewe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siamini; mimi siamini, mimi naamini tutapewa, zitatumika Zanzibar na ile fedha ambayo inajenga shule ya sekondari kila kata na Zanzibar kila jimbo tutajengewa shule ya sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nimalizie kwa kusema naishukuru Serikali. Waziri Mheshimiwa Mwigulu unanisikia sana rafiki yangu, shilingi milioni 500 hii ni haki ya Watanzania, hatuna Mbunge wa Bara wala hatuna Mbunge wa Zanzibar; ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sote tuliomo humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, nami nitumie fursa hii kukushukuru wewe. Pia kipekee niipongeze Kamati yangu ya Katiba na Sheria kwa namna ambavyo inasimamia na kutekeleza majukumu yake ya Kikamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende katika mchango wangu mfupi kwa taarifa ambayo imewasilishwa mbele yetu. Mimi nitajadili mfumo wa utoaji wa haki nchini. Kwanza naomba niipongeze Mahakama kwa namna ya kipekee wanavyojitahidi katika masuala mazima ya utoaji wa haki na uendeshaji wa kesi Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali ya pongezi hizi, bado zipo changamoto, bado yapo malalamiko mengi kwa wananchi juu ya mhimili wetu huu wa Mahakama katika masuala mazima ya utoaji wa haki na usimamizi wa kesi ama uendeshaji wa kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, wananchi hawawezi wakalalamika tu juu ya Mahakama hii, maana yake ni kwamba kuna sababu za msingi ambazo zinawafanya wailalamikie Mahakama. Mimi kama Mbunge naomba nichukue fursa hii kuiomba Serikali sasa, ipo haja na sababu za makusudi za kuongeza watendaji katika Mahakama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tutakapotumia nafasi hii ya kuongeza watendaji katika Mahakama, itakuwa ni sababu ya kupanua wigo, itakuwa ni sababu ya kurahisisha usikilizaji wa kesi na utoaji wa hukumu kwa kipindi kifupi baada ya kesi kusikilizwa. Kama tutafanya hivyo, tutawasaidia na kuwapunguzia kero wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike kuna watu wanatoka masafa ya mbali kwenda katika Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na katika Mahakama za Mikoa kusikiliza kesi ama hukumu za kesi zao, lakini wanapofika katika Mahakama zile wanaambiwa leo Jaji ama Hakimu ana kesi nyingi, kwa hiyo, warudi wanapangiwa tarehe nyingine. Hiyo tarehe ikifika, wanapangiwa tarehe nyingine. Mwananchi yule maisha yake ni duni, maisha yake ni magumu, anatoka masafa ya mbali, anakuja bila mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nadhani ili kutatua changamoto hii, ipo haja Wizara ya Katiba na Sheria sasa kufikiria upya namna ya kuwaongezea maslahi Mahakimu hawa. Utakapowaongezea maslahi Mahakimu hawa tutapunguza kero na malalamiko kwa wananchi. Itakuwa ni sababu ya kuepuka vishawishi kwao na watafanya kazi kwa ufanisi, weledi na watatenda haki kiukweli kabisa na wananchi hawatalalamika. Katika hilo, naamini vishawishi vipo na zipo namna za kutatua vishawishi hivi na njia pekee, tuwaongezee maslahi watendaji wa Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi, ni moja tu; kwenye Magereza zetu kumejaa mahabusu. Mahabusu ni wengi mno! Sasa kama Mahakama, kama Wizara au kama Serikali itafanya jambo la kusudi, kwenda katika Magereza yale kutafiti na kuhakiki ni mahabusu wangapi ambao wamo ndani ya Magereza yale, halafu wakafanya utaratibu; wale ambao wanaona kwamba ipo haja ya kuwatoa, wakawa wapo uraiani na upelelezi wa kesi zao unaendelea, basi nadhani ipo haja ya kufanya hivyo ili kupunguza mzigo kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale mahabusu wakiwemo mle Magereza Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kuwalisha; na wale wanapotoka baadaye Serikali ama Mahahama inapowaambia ninyi mmetoka, hamna kesi. Wamekaa miaka mitatu, minne, nane. Wakija uraiani, maisha kwao yanakuwa ni magumu, wanakosa uaminifu na ushirikiano na jamii inayowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, wafanye jitihada za makusudi na za kipekee kabisa, kufanya uhakiki Magerezani. Ambao tunaona wanafaa tuwatoe nje, wakati wa wako nje upelelezi wao unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Moja kwa moja naomba niende katika hoja ambayo iko mezani kwetu. Huu ni mwaka wa 58 wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kihistoria muungano huu ulikuwa ni baina ya nchi mbili huru; Nchi ya Tanganyika na Nchi ya Zanzibar, lakini nchi zote hizi zilikuwa ni Wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, wakati tunaungana tulikubaliana mambo 11. Katika mambo haya naomba nisiyaseme, lakini yako mambo ambayo si ya Muungano lakini Zanzibar imekosa nafasi kama ni sehemu ya Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar. Naomba niseme masuala ya michezo siyo sehemu ya Muungano, masuala ya afya siyo sehemu ya Muungano, lakini leo yapo mambo tumeambiwa yamepatiwa ufumbuzi, yako mambo ambayo tumeambiwa haya tayari tumeyapatia ufumbuzi na sasa hatuwezi kuyajadili tena badala yake tunaenda katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, masuala ya Afrika Mashariki, masuala ya kikanda pamoja na kimataifa. Leo Zanzibar tuna ZFF Tanganyika tuna TFF lakini TFF inabeba nembo ya Muungano ambayo sasa inakuwa ni member wa FIFA na inaleta misaada TFF. Je, naomba kujua Mheshimiwa Waziri atakapokuja, tunafahamu mgao ambao unatoa FIFA Zanzibar tunakuwa ni sehemu ya manufaiko katika mgao huo?

Mheshimiwa Spika, naomba niseme ukienda katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuna mahali, kuna sehemu imetutaka kwa mujibu wa makubaliano yetu tutakuwa na account ya pamoja na fedha. Katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri amesema haya ni mambo ambayo sasa tunaendelea kuyashughulikia. Sasa ni mwaka wa 58, bado tunaendelea kushughulikia matatizo yale yale, kitu ambacho kwa Wazanzibar hatuoni kwamba sasa kuna nia na dhamira njema katika Muungano huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme wazi, hakuna mtu ambaye hautaki Muungano huu, sote tunautaka, lakini tunataka Muungano wa haki na tunataka Muungano wa usawa. Naomba sasa ufike muda Serikali ituambie ni lini Akaunti ya Pamoja ya Fedha itafunguliwa, itaanzishwa? Kwa sababu zimekuwa ni danadana za muda mrefu na sasa tumefika mahali tunaona kwamba Muungano huu ni jambo ambalo linatunyonya Wazanzibar. Tufike mahali kinia safi tu tuseme yapo mambo ambayo tuseme, haya tuyatatue kwa maslahi ya Taifa letu hili la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nataka nitoe rai na naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa ifike mahali atuambie sasa ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na nia ya dhati kuulinda Muungano huu kwa kufungua akaunti hii ya pamoja.

Mheshimiwa Spika, la pili, nimwombe Mheshimiwa Waziri na niiombe Serikali sasa ituambie ni lini Serikali ya Jamhuri ya Muungano itaipatia Zanzibar…

SPIKA: Mheshimiwa Salum kuna taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza kwamba Muungano wetu una manufaa makubwa kushinda changamoto. Kwa hiyo analipotosha Bunge na Watanzania kusema kwamba muungano unawanyonya, ziko faida nyingi za Muungano ambazo tunazo hata kuwepo hata ndani ya Bunge hili ni faida za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

SPIKA: Mheshimiwa Salum Shaafi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Spika, siipokei na sina haja nayo. Hakuna mimi sijasema naukataa wala naupinga, bali uhalisia ulivyo hakuna asiyejua kama Muungano huu una changamoto nyingi hususan kwa upande wa Zanzibar. Hili ni jambo ambalo naomba litambulike kwa sababu katika lile jambo ambalo kwamba Zanzibar ni sehemu ya Afrika Mashariki leo tunachagua Wabunge wa Afrika Mashariki, Zanzibar…

(Hapa kuengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji )

SPIKA: Mheshimiwa Shafi muda wako ulikuwa umeshaisha nilikuwa nimekupa muda ili umalizie hoja yako.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Ilishapigwa kengele.

SPIKA: Kengele ilishagonga.

MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Moja ya jambo ambalo binafsi linanipa ukakasi ni suala la mgawanyo wa fedha za Muungano. Wazungumzaji wengi waliopita walimsifu Waziri na timu yake na wakamtaja Waziri kwamba ni mchumi aliyebobea, maana yake kwamba ni msomi, lakini sifa moja ya wasomi ni wale wenye kutumia taaluma yao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linanipa mashaka makubwa. Tukiangalia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya Saba inazungumzia masharti ya kukusanya fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ibara ya 133 naomba ninukuu: “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatunza akaunti maalum itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na ambayo itakuwa ni sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambamo kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili…”

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hata hivyo, hadi leo hii bado Serikali haijataka kuweka wazi, je, hii akaunti ya fedha ya pamoja ipo? Je, hii akaunti ya fedha ya pamoja, kwa sababu hapa tuna ushirika, tumekubaliana tunachanga, tutakachokipata tunakiweka sehemu moja, baadaye tunafanya matumizi, tunaambiana tumetumia kiasi fulani cha fedha na kitakachobaki tunakigawa kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa makubaliano tuliyokubaliana katika hii Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza, hatuna akaunti ya fedha ya pamoja. Hatujui ni mahali gani fedha hizi zinawekwa. Ni namna gani ambazo fedha hizi zinatumika. Leo kama haitoshi, katika ibara hiyo ya 134 pia ilipendekeza kuweko na Tume ya Pamoja ya Fedha, lakini hadi leo hatujui ni namna gani tume hii inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea tume hii iweze kukusanya fedha, lakini kutupa taarifa ni namna gani fedha wamekusanya kiasi gani, ni namna gani fedha hizi wametumia, ni namna gani fedha ambazo zimebaki na mgawanyo sasa tunagawaje kati ya Zanzibar na Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii inapelekea mgogoro na malalamiko makubwa juu ya suala zima la Muungano hususan kwa upande wa Zanzibar. Naomba ikumbukwe mwaka 2006 iliundwa tume iende ikafanye utafiti, ione namna gani ya mapato na matumizi ya fedha hizi za Muungano. Tume ile ikiitwa PWC ilianza kufanya kazi kuanzia mwaka huu 2014 hadi 2020, ilionesha ni kwa namna gani Zanzibar hatupati stahiki ya fedha zetu kwa mujibu wa Katiba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hiki hadi 2014, zaidi ya Shilingi Trilioni 11.2 Zanzibar tukidai Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa naamini Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atatuambia sasa ni kwa asilimia ngapi Zanzibar tulipata fedha hizi kwa mujibu wa taarifa ya Tume hii ya PWC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme. kwa sababu ya muda, mgawanyo wetu ni asilimia 4.5 lakini kwa report hii tulipata asilimia 1.1 kwa nini? Tumekuwa kama ni uhisani tunafadhiliwa wakati sisi ni washirika katika tume hii. Naomba nitoe rai au nitoe ushauri kwa Serikali. Kwanza, naomba Serikali kufuata Katiba na Nchi kwa kuanzishwa Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria ya mapato yote ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naiomba Serikali ifanye utafiti mpya wa mapato ya Muungano na matumizi kwa shughuli za Muungano tu ili kutoa takwimu sahihi kwa kipindi tulichonacho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, naiomba Serikali igawe ziada ya mapato ya Muungano kwa washirika wa Muungano kwa mujibu wa mgao na kanuni za mgao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, naiomba Serikali kumtaka CAG kufanya ukaguzi ili kubainisha mgao sahihi na fedha ambazo Zanzibar inaidai Serikali ya Muungano kwa kipindi chote toka kuanzishwe kwa jambo hili la Akaunti ya Pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)