Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan (8 total)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri yaliyojibiwa na Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, jibu lake linaonesha kwamba hii mifuko haifanyi kazi Zanzibar na inafanya kazi Tanzania Bara, lakini wapo Watanzania Bara wanaoishi Zanzibar ambao nao walipaswa kunufaika na mifuko hii; ambao hawana sifa ya kunufaika kwenye mifuko kama hii wakiwa Zanzibar. Hawa wananufaikaje? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la rafiki yangu sana Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan. Ni kwamba kwa wote wanaoishi Bara na kufanya shughuli zao huku Bara, kwa zile fursa zinazohusika na mambo ya Bara zinawagusa huku upande wa bara na wale wote wanaoishi kule Zanzibar na fursa zinazohusika katika mifuko mbalimbali ya Zanzibar, wanapata fursa hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika jambo hilo halina shida yoyote, kwa sababu siyo suala la kimuungano. Kwa hiyo, turidhie tu utaratibu wa sasa. Bahati nzuri kule kuna Wizara Maalum inafanya michakato hiyo. Ninaamini, kama kuna maeneo kidogo yanataka uboreshaji, basi inawezekana kwa ushauri mzuri wa upande wa pili, kufanyika uboreshaji wa ziada. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali iliyopo sasa.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hoja yake ni nzuri, inachochea kuona pande zote za Muungano zikiwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaweza vikasaidia wananchi katika maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ingawa, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri kwenye swali la msingi, lakini naomba niulize swali la nyongeza. Serikali imeshafanya jitihada za makusudi kwenye kupunguza ukali kwenye bidhaa ya mafuta. Je, Serikali haioni haja ya kufanya jitihada hizo hizo ili kupunguza ukali kwenye bidhaa za vyakula?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kwamba tayari Serikali imeshatoa ruzuku kwa upande wa mbolea na tayari Serikali imeshusha kodi ya uingizaji wa mafuta ya kula. Kwa hiyo, Serikali imeshachukua hatua ya kupunguza ukali wa mfumuko wa bei za mafuta.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ingawa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri kwenye swali lake la msingi, naomba nimwulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba, wakati tunasubiri fedha zitengwe kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kikubwa.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga vituo vidogo vya Polisi (Police Post) kwenye maeneo tofauti ya Mji wa Chakechake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami twende kwenye eneo la Chakechake akaone jiografia na kama ujenzi wa Kituo cha Vitongoji ndiyo ingekuwa suluhisho la wananchi kufuata huduma za kipolisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, ni kweli kwamba pale ambapo pana umuhimu Serikali inaweza ikasaidiana na wananchi kujenga Police Post kwa maana ya vituo vidogo vya Polisi panapohitajika. Hata hivyo, kwa sababu Kituo cha Chakechake kwa sasa kimechakaa, kinahitajika kujengwa kituo kipya, kipaumbele tumeweka kwenye kujenga kituo kipya katika mwaka wa fedha ujao. Namwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane nasi tulitekeleze hilo kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili juu ya umuhimu wa kuongozana naye kwenda vitongojini, niko tayari, hakuna kikwazo chochote. Wakati utakapofika tukaambiana basi tutaongozana. Nashukuru. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina masuala mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; nje ya utoaji wa rasilimali fedha kwa kaya maskini je, ni mambo gani mengine Mpango huu wa TASAF unafanya kuzinufaisha kaya maskini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, mpango huu unategemea kuisha lini ili kaya maskini zinazonufaika zipate kujiandaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, kwamba TASAF imefanya nini kingine cha ziada kwa walengwa? TASAF imefanya mambo mengi ikiwemo kuingia MOU na Bodi ya Mikopo Tanzania ili kuweza kutoa mkopo wa asilimia 100 kwa wale wote ambao wanakwenda kwenye elimu ya juu kutoka kwenye kaya hizi za walengwa wa TASAF. Vilevile TASAF imewawezesha walengwa hawa kuwa na bima ya afya. Bima ya afya hii inawawezesha wao kupata matibabu wakati wowote hata pale ambapo wanakuwa hawana pesa. Vile vile mradi huu umejenga miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye madarasa, vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, mpango huu kwanza nilijulishe Bunge lako tukufu ulikuwa unaisha mwaka huu 2023. Hata hivyo, kwa jitihada zake Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa mapenzi yake kwa Watanzania ameweza kutafuta fedha na kuongezea mradi huu fedha na sasa utakwenda mpaka 2025.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Baada ya majibu mazuri ya Wizara kuhusiana na swali nililouliza, nina swali moja la nyongeza. Ni kwamba kumekuwa na uvumi wa muda mrefu kwamba VAT inayotoka kwenye miamala ya mtandao ya simu inakusanywa na mamlaka moja tu ambayo ni ya TRA. Halafu TRA ndio wanakisia kiwango ambacho wanawapa Zanzibar. Wizara wanasemaje kwenye uvumi huo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la taaluma tu katika nchi yetu kwa jamii yetu kwamba TRA ndio wanakusanya mapato ya pande zote mbili katika suala la miamala. ZRB wanakusanya kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara ni TRA. Kwa hiyo nichukue fursa hii kuwaagiza TRA na ZRB kuendelea kutoa taaluma kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wajue makato haya yanakatwa vipi kwa mujibu wa sheria. Ahsante.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye swali langu la msingi nina swali moja la nyongeza.

Kwenye jibu lake la msingi amekiri kwamba upo uhaba wa Askari Polisi katika Mkoa wa Kusini. Je, ni ahadi gani ya Serikali kwamba watatoa kipaumbele kwenye hizo ajira 4,103 alizozitaja maalum kwa ajili ya Mkoa wa Kusini Pemba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan Mbunge wa Chakechake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ahadi yetu ni kwamba hawa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Polisi 4,103 watagawiwa maeneo yote yenye upungufu ikiwemo Mkoa wa Kusini Pemba. Kama tulivyokubaliana Mheshimiwa Ramadhan nitakwenda huko baada ya Bunge hili ili kuangalia pamoja na mambo mengine upungufu huo na kiwango kinachohitajika kusaidiwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; kwenye majibu yake Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wapo kuandaa mwongozo utakaoruhusu wawekezaji kuja kuwekeza kwenye kupunguza makali ya hewa ya ukaa; ni lini mwongozo huo utakamilika?
WAZIRI WA NCHI. OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ni kwamba kwanza nimshukuru Mheshimiwa Ramadhan na nilijua kama ni miongoni wa vijana machachari na hata mwaka huu wanawezekana wakaenda kutuwakilisha kule Misri katika ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi.

Mheshimiwa Spika, katika upande huo Serikali ni kama nilivyosema ni kwamba mwongozo huu uko katika hatua za mwisho, takriban mwezi mmoja uliopita tulikuwa katika kile kituo cha Carbon Tanzania ambacho sisi tumeki-center pale University of Sokoine Morogoro, tulikuwa na kikao hicho imani yetu ni kwamba mwanzoni mwa mwaka wa fedha unaokuja maana yake kuanzia Julai kwenda hapa mbele si muda mrefu mpango huo utaweza kukamili ili mradi kwamba watu waweze kushiriki katika ajenda hii kubwa ya kibiashara.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba, upembuzi yakinifu utakamilika Desemba, je, ni lini ujenzi utaanza rasmi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, ujenzi huo utazingatia kwa kiasi gani kuweka vifaa vya kisasa ili abiria wasikaguliwe na mbwa kama inavyofanyika sasa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. DAVID M. KIHENZILE): Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan kama nilivyosema hapo awali. Hatua ya kwanza ambayo Serikali inafanya ni kufanya uthamini au upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao utaweza kutusaidia kujua nini kinapaswa kufanyika. Pia, mara baada ya kukamilisha hatua hiyo, hatua itakayofuatia itakuwa ni kuanza kufikiria au kuanza mchakato kwa ajili ya ujenzi. Kwa sababu, Serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa sana kwenye bandari zetu nchini ikiongozwa na Bandari yetu kubwa ya pale Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili; kama nilivyojibu swali la kwanza, katika usanifu huu unaoendelea kwa ajili ya ghati letu jipya la Dar es Salaam, utaambatana pamoja na ufungaji wa mashine ya ukaguzi wa kisasa ambao utatumia teknolojia ya kisasa ya ukaguzi kwa ajili ya abiria na mizigo.