Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan (7 total)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa kulisaidia kwa kulijengea uwezo Jeshi la Kujenga Uchumi la Zanzibar (JKU)?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mashirikiano kati ya JKT na JKU yalianza mwaka 1975, kuanzishwa kwa JKU kutoka mfumo wa kambi za vijana ulioanzishwa tarehe 3 Machi, 1965 kwa sehemu kubwa kulitokana na mashirikiano hayo. Tangu wakati huo JKT na JKU wameendelea kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya kiutawala na uzalishaji mali na ndiyo maana JKU ina sura ya JKT. Mwaka 2001 iliundwa Kamati ya Mashirikiano yaliyopelekea kuwa na Katiba ya Mashirikiano ya mwaka 2007. Katiba hiyo pamoja na mambo mengine imeainisha vikao mbalimbali vya mashirikiano ikiwa ni pamoja na ratiba za vikao vya wakuu wa vyombo hivyo.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, Programu za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mfuko wa Taifa wa kuendeleza Wajasiriamali (NEDF) na Mfuko wa kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali wadogo (SMF) zimewasaidiaje Vijana, Wanawake na Wajasiriamali wa upande wa Zanzibar katika kujikwamua kiuchumi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Program ya Mifuko yote hiyo iliyotajwa ya kuwaendeleza vijana, wanawake na wajasiriamali, inafanya kazi Tanzania Bara na haitekelezwi upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, mifuko hiyo ilikuwa ni Mfuko wa YDF, WF na NEDF. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na mamlaka inayohusika na mifuko hii kwa upande wa Zanzibar ambayo ni Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuona namna ya bora kuwasaidia vijana, wanawake na wajasiriamali wa Zanzibar. Ahsante sana.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kituo kipya cha Polisi katika Wilaya ya Chakechake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge Wa Chakechake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi lina eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Shehia ya Vitongoji lenye ukubwa wa mita za mraba 1,496. Mpango wa Serikali ni kutenga fedha katika bajeti ya mwaka ujao 2023/2024 ili ujenzi uanze. Nashukuru.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, mgawanyo wa mapato ya tozo za miamala upoje kwa pande za Muungano na vipi yataboresha huduma kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Seleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha tozo ya miamala ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu kwa lengo la kugharamia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na madarasa. Utaratibu wa mgawanyo wa fedha za tozo ya miamala kwa pande zote mbili za Muungano unasimamiwa na Kanuni ya saba ya Kanuni ya Tozo za Miamala ambapo fedha zinatoka na miamala inayofanyika Zanzibar huwasilishwa Bodi ya Mapato ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari, 2022 jumla ya shilingi bilioni 231.54 zilikusanywa kwa Tanzania Bara na shilingi bilioni 2.96 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa upande wa fedha zilizokusanywa Zanzibar, mchanganuo wa matumizi yake utatolewa ufafanuzi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, kwa Tanzania Bara, fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na madarasa katika tarafa ambazo hazikuwa na miundombinu hiyo. Ahsante sana.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Mpango wa TASAF kwa Zanzibar umenufaisha kaya 216, Unguja Shehia 204 na Pemba Shehia 78 ambapo ni sawa na 70% ya Shehia zote Zanzibar.

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Shehia zote 388 Zanzibar zinanufaika na mpango wa TASAF kwa 100% badala ya 70%?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chake Chake, kama ifuatavyo: -

Mgeshimiwa Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoanza utekelezaji mwaka 2013, rasilimali zilizokuwepo zilitosheleza kufikia asilimia 70 ya Vijiji, Mitaa na Shehia ambavyo kwa hesabu ni maeneo 9,960. Kipindi cha kwanza cha Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kilidumu kwa miaka sita na kilikamilika mwezi Desemba 2019. Katika awamu hiyo, idadi ya maeneo ambayo hayakufikiwa ni Vijiji, Mitaa na Shehia 5,590 nchini kote zikiwemo Shehia 388 za Zanzibar (Unguja ikiwa ni Shehia 259 na Pemba Shehia 129).

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF kilianza rasmi mwezi Januari, 2020. Sehemu hii ya Pili inatekelezwa katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, kwenye Vijiji, Mitaa na Shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza. Utambuzi na uandikishaji wa walengwa katika maeneo yote 5,590 ambayo hayakufikiwa katika kipindi cha kwanza tayari umeshafanyika.

Mheshimiwa Spika, utambuzi ulitanguliwa na semina za uelimishaji kuhusu TASAF na taratibu zake, vigezo vya walengwa na majukumu ya wadau katika ngazi za jamii, shehia, Halmashauri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar. Aidha, kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza, taratibu za utambuzi wa walengwa zimeboreshwa ili kutambua kaya zinazokidhi vigezo. Aidha, tathmini ya hali ya walengwa waliodumu kwenye Mpango katika kipindi cha kwanza itafanyika kwa lengo la kubaini wale ambao wameshaimarika kiuchumi ili kusitisha utoaji wa ruzuku kwa kaya hizo. Naomba kuwasilisha.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wa Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetoa kibali cha kuajiri askari wapya wa Jeshi la Polisi 4,103. Kwa sasa askari hao wapo kwenye mafunzo ya awali katika shule ya Polisi Moshi. Watakapomaliza mafunzo yao, watagawiwa kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa askari ikiwemo mkoa wa Kusini Pemba. Nashukuru.
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Ghati la Kisasa la Abiria kwenye Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. DAVID M. KIHENZILE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha huduma kwa wananchi wake katika maeneo mbalimbali ya nchi, likiwemo Jiji la Dar es Salaam. Ili kuendeleza juhudi hizo, Serikali kupitia TPA inakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa gati la kisasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ambao hadi sasa upo katika hatua za mwisho na unatarajia kukamilika mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Ramadhan Suleimani Ramadhan na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwa kuendelea kufuatilia kero za wananchi katika maeneo yao. Serikali itaendelea kuboresha huduma hizo ili kuwawezesha wananchi kufanya kazi zao bila kikwazo chochote.