Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan (18 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye Hotuba ya Rais ya kufungua Bunge aliyoitoa katika Bunge hili tukufu Novemba pamoja na ile ya kufunga.

Kwa kuwa na mimi ndio mara yangu ya kwanza kuchangia ndani ya Bunge lako hili tukufu, naomba kwa heshima kabisa nitoe shukrani zangu kwa chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa imani yake iliyonipa, hasa kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa utumishi uliotukuka. Pia, nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu kwa wananchi wa Chakechake kutokana na support waliyonipa na imani waliyonipa ili nije niwawakilishe katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ambao nataka niongezee kwenye hii guide book ambayo ni hotuba ya Mheshimiwa Rais ni kwenye suala la utalii. Mheshimiwa Rais vision yake aliyoiweka kwenye guide book hii ya hotuba ni kwamba, anasema ndani ya miaka mitano kutoka 2020 mpaka 2025 anatamani aone watalii wameongezeka Tanzania mpaka kufika milioni tano ambao watachangia kwenye pato la Taifa kwa Dola za Kimarekani bilioni sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwa wasaidizi wa Rais ambao wamepewa kazi ya kumsaidia Rais kufikia hayo malengo ya ku-promote utalii Tanzania ni kwamba, ninavyoona mimi ili hili lengo lifikiwe, la watalii milioni tano ambao watachangia zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni sita, moja katika eneo ambalo tunalikosea ni mawasiliano mazuri baina ya taasisi zinazokuza utalii za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi unahisi inakuwa ni very normal mgeni kutua Zanzibar akatumia zaidi ya siku nane akiwa Zanzibar, katoka ulaya, halafu akaondoka kurudi Ulaya bila kupita Tanzania Bara, hili jambo sio sahihi. Inavyoonekana ni kwamba, hizi taasisi zetu za kukuza utalii au idara za utalii baina ya bara na Zanzibar hazina mawasiliano mazuri. Hakuna juhudi za makusudi zinazochukuliwa baina ya pande mbili hizi kuwasiliana ili kuwashawishi wageni wapate kutumia siku zao wanazokuwa Tanzania kwenye pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtalii ameshakuja Zanzibar au yuko Serengeti anatumia siku nane, unaachaje kutumia fursa hiyo kumshawishi mgeni atumie siku mbili za siku nane zake akiwa Serengeti wakati ameshakuja Tanzania? Kwa hivyo ilivyo sasa haiku vizuri sana. Ushauri wangu kwa kaka yangu Waziri wa Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, ni kwamba anaweza akatafuta namna ya kuzi-link hizi idara za utalii zilizoko Tanzania Bara na zilizoko Zanzibar ili tuwashawishi wageni wanaokuja Tanzania waweze kutembelea pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni kwamba, mwishoni mwa mwezi Desemba, Wizara ya Utalii ya Tanzania Bara ilipata ugeni wa Bwana Drew Binsky alitoka Marekani. Huyu jamaa ni mtu maarufu sana ambaye ametengeneza makala nyingi za utalii duniani. Ni mtu ambaye kwenye face book page yake ana zaidi ya follower milioni 30, video yake moja aliyoi-post akiwa Moshi imetazamwa na viewers zaidi ya milioni 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha hizo fursa watu wameshindwa kuwasiliana baina ya Zanzibar na Tanzania Bara maana yake hata siku moja huyu Drew alishindwa kuwa Zanzibar akapiga picha akiwa Stone Town, ambayo pengine ingeonekana leo na watu zaidi ya milioni 20 duniani watu wangeshawishika kufika Zanzibar nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, ili tumsaidie Mheshimiwa Rais afike hilo lengo la hao watalii milioni tano tuna haja ya kufanya jitihada za makusudi. Watalii wanakuja kutembelea Zanzibar kwenye fukwe pia tuweze kuwashawishi wawe wanakuja kutembelea kwenye mbuga zetu za Serengeti na nyingine zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mchango na ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri anapokwenda kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufikisha vision yake ya kukuza pato la Taifa hasa kupitia utalii kwa kukusanya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 6. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote niungane na watanzania wengine wenzangu waliotoa shukrani na pongezi zao kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo, kwa niaba ya wananchi wa Chakechake, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninatoa ahadi ya kwamba tupo nyuma yake tuna muunga mkono na tutampa kila ushirikiano atakaouhitaji kutoka kwetu Mungu amtie nguvu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni shukrani kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuleta hotuba iliyoshiba, iliyosheheni ambayo inaakisi maono ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hotuba ambayo imechukua mtazamo na mwelekeo wa Mheshimiwa Rais mpya aliyekuwa madarakani Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia kwenye mambo mawili kwenye hii hotuba, jambo la kwanza ni structure ya utoaji wa mikopo iliyopo sasa. Moja katika maeneo ambayo tunajisifia sana I feel very proud ni legacy iliyoachwa na Rais Hayati Dkt. Magufuli kwenye ujenzi wa zahanati zaidi ya 1,198 nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuna idadi ya zahanati zisizopungua 5,900 Tanzania, hili ni jambo zuri na la kuwa mfano kila mahali, tuna vituo vya afya visivyopungua 666 Tanzania nzima, kwenye uhai wa Mheshimiwa Magufuli kulijengwa vituo vya afya visivyopungua 487 Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunachokikosea kama Taifa ni kwenye recruiting ya wafanyakazi au watendaji au wahudumu wa kwenye hivyo vituo vya Afya. Wahudumu walivyo sasa hivi ki-structure tunahitaji ma-clinical officer wengi zaidi na ma-clinical officer ni hawa vijana wenzangu ambao wanasoma diploma za clinical officer kwenye vyuo mbalimbali vya elimu Tanzania ambao ndio hawapati mikopo. Mikopo sera yake ya elimu ya juu, mikopo wanapewa ma-MD ma-medical officers ambao wanaanza degree na kuendelea ambao hao baadae hawataki kwenda kukaa kwenye zahanati na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawawezi kwenda kuishi huko vijijini mtu akishakuwa na degree yake yaani hataki kwenda kuanzisha Maisha kwenye zahanati anajiona kama ni kudogo sana kwake. Kwa hiyo, watu ambao tunawahitaji wakae kwenye zahanati zetu hizi zaidi ya 5900 na vituo vya afya zaidi ya 666 ni ma-clinical officer ambao wengi wao wanaanza na hatua ya elimu ya diploma kwenye vyuo vya afya mbalimbali, ambao ndio hawapati mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu hapa ni kwamba lazima tutengeneze sera sasa. Aidha tubadilishe au tubadilishe sheria ili hawa watu wakopesheke wapewe mikopo ya elimu ya juu ili wasome wawe wengi wakatusaidie kwenye hizo zahanati zetu. Maana yake tukiwa tunajenga zahanati nyingi lakini mwisho zikiwa zinakosa watendaji hiyo itakuja kuwa kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni upande mmoja upande wa pili au jambo langu la pili ambalo nilidhamiria kulichangia ni kwenye sekta ya utalii, wakati nachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyekuja kuitoa hapa madarakani Hayati nilitoa mchango wangu kwenye jambo hili, leo nataka niongeze zaidi. Kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi yenye page 303 kwenye page 207 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ilani inampa task kazi ya kuhakikisha anakuza pato la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia utalii kwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 500,000 hadi 800,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyo sasa hivi wastani wa watalii wanaoingia Zanzibar kwa mwezi ni kati ya 40,000 hadi 50,000 statistic niliyonayo hapa kwa Tanzania Bara kwa mwaka 2020 hadi 2021 kumetembelewa na watalii wasiopungua 620,000, maana yake hiyo ni idadi ya watalii wanaoingia Tanzania kwa mwaka mmoja tu kwa Tanzania Bara, ambao ni task aliyopewa Rais wa Zanzibar kwenye Ilani kwa muda wa miaka mitano kuifikia. Sasa ninachotaka kushauri hapa kuna umuhimu tena umuhimu mkubwa wa kufanya kazi kwa ushirikiano baina ya Wizara ya Utalii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Utalii ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona huwa haiingii akilini na haiko vizuri ikiwa mgeni anafika Zanzibar anakaa siku saba anaondoka kurudi Ulaya hajafika bara, au anafika bara Ngorongoro anatua KIA ana-spend anaondoka baada ya siku saba hajafika Zanzibar. Wakati anakuja Tanzania ilivyo ni kwamba mifumo na ushirikiano baina ya Taasisi hizi ni kama haupo vizuri kidogo labda kuna zile sentiment za kwamba hizi taasisi sio za Muungano lakini sisi tunafanya kazi kama Taifa tunatakiwa tushirikiane ili kusaidia Taifa hili likipata pato lipate kwa jumla yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuunga mkono hoja na huo ndio ulikuwa mchango wangu kwenye sehemu mbili ahsante sana naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nipate kuchangia mawazo yangu na mawazo ya wananchi wa Jimbo la Chakechake kwenye Wizara hii ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza mwanamke wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ametuelezea dira na mwelekeo wa Wizara yake katika mwaka wa fedha 2021/2022 nimpongeze sana kwa kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo sipo vizuri sana kiafya, kifua kidogo na homa homa kwa hiyo utanivumilia, nilipanga kusema mengi lakini inawezekana katokana na hiyo hali nikapunguza kidogo yale ya kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi tunaotoka kwenye majimbo ya visiwani Zanzibar tukisema ile dhana ya local content kwa mfano kwenye maeneo ambayo Mungu amewabariki kuwa na migodi inaweza isiwe inafahamika vizuri kwenye akili za wengi wanaotoka kwenye visiwa. Kwa sababu sisi hatujabarikiwa kupata maeneo ambayo yana uchimbaji wa dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi tumebarikiwa kupata maeneo mengi ambayo yamezungukwa na Kambi za Jeshi, kwa hiyo, ile dhana ya local content inaweza ikatumika mutatis mutandis kutoka kwenye dhana ya wenzetu ambao Mungu amewabariki kupata migodi na sisi ambao tumezungukwa na kambi za Jeshi. Dhana ya local content kwenye kambi za Jeshi ni vile tunavyoweza kutumia uwepo wa kambi za Jeshi kwenye maeneo yetu kama fursa. Kambi za Jeshi zikiwepo kwenye maeneo yetu kwenye majimbo yetu maana yake hiyo ni fursa ya wewe kupata Kituo cha Afya ambacho kitajengwe ndani Kambi ya Jeshi, kupata shule ambazo zinajengwa ndani ya kambi za jeshi na huduma za kijamii nyingine, kwa mfano, mimi kwenye Jimbo langu sina Kambi ya Jeshi lakini jirani yangu Jimbo la Wawi wao wanazo kambi za jeshi zaidi ya moja, ipo hospitali katika Kambi ya Jeshi ya Ali Khamis Camp ambayo imekuwa ina msaada mkubwa kwa wananchi wa Wawi na wananchi wa Chakechake, maana yake nje na zaidi ya Jimbo ambapo kambi ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali imekuwa ikihudumia watu, raia wengi wamekuwa wakienda kwenye hospitali hizo kupata huduma, kwa hiyo rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba hizi hospitali zinatakiwa zipewe uwezo kwasababu sasa zimekuwa ni sawa sawa na hospitali za kiraia kwa jinsi zinavyohudumia hata wasiokuwa wanajeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya nzima ya Chakechake sisi tumebahatika kuwa na hospitali moja ya Wilaya ambayo ndio ina sehemu za kuhifadhia maiti/ majokofu ya kuhifadhia maiti. Ushauri wangu ni kwamba tunaomba kuongezewa uwezo kwa hospitali ya Jeshi iliyoko kwenye kambi ya Ali Khamis Camp ili iwe na uwezo wa hifadhi maiti, kwa sababu Hospitali ya Chakechake haitoshi inakuwa inamezwa na mzigo, inabebeshwa mzigo mkubwa wa kuhifadhi maiti jambo ambalo halina uwezo huo. Kwa hiyo mbadala ni kuiwezesha kambi ili hospitali iliyopo kwenye Ali Khamis Camp ili liwe na Mortuary ambayo itasaidia hii Hospitali ya Chakechake kubwa ya Wilaya pale inapotokea mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nilitaka kuchangia ni suala la uwekezaji wa jeshi kwenye tafiti za kisayansi, hili limesemwa sana jirani yangu Engineer kalisema, Mzee wangu Mheshimiwa Maige kalisema na Wabunge wengi waliochangia mwanzo wamelisema kwa msisitizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo sasa yameshakwenda mbele zaidi kwenye maendeleo ya kisayansi na teknolojia huko duniani ni uwekezaji na utumiaji wa sayansi kwenye majeshi; in terms ya silaha, in terms ya mbinu za kupigana, hizo drones tunazoziona (ndege zisizo na rubani) zimegundulika kutokana na vyuo vya kitafiti vya kijeshi. Kwa hiyo na mimi nataka niweke msisitizo hapa, dunia haipo tena tulipo sisi, watu walishakwenda mbele zaidi, leo watu wanateknolojia za kuzuia makombora kabla ya kufika maeneo yao yakiwa yamelengwa kuelekea kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wana launch rocket za kijeshi, kwa hiyo hatuwezi kufika huko kama hatujawekeza fedha nyingi kwenye maabara za kijeshi za kuweza kufanya tafiti za kisasa ili na wao jeshi letu tulipe uwezo wa kufanya ugunduzi wa silaha mpya na teknolojia mpya za kjeshi ambazo zitalipa uwezo jeshi letu kwenye kulinda mipaka na kufanya ile kazi waliyopewa kikatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 2000-2005 wakati tunamaliza form four kulikuja ile dhana ya mapinduzi ya wasomi ndani ya jeshi, tulikuwa tunashawishiwa kwa sababu mimi wakati ninamaliza muda huo nilikuwa ninasoma shule ya jeshi, kwa hiyo, tulikuwa tunashawishiwa tuingie jeshi tulikuwa tukiambiwa kuna mapinduzi ya kwamba jeshi sasa linataka wasomi kwa hiyo ili hao wasomi wawe na faida ambazo sasa hivi wapo wengi ndani ya jeshi ni wengi wengi wengi wapo, ili wawe na faida ni lazima tuwekeze kwenye maabara za kisasa za kisayansi zitakazowasaidia wasomi wetu kutumia elimu zao ili kulisaidia jeshi letu la ulinzi na usalama kutulinda kisayansi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu pia ambalo nilitaka kulisema ni kuhusiana na suala la ajira; juzi kulikuwa kuna kikao cha kiutendaji baina ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Mchengerwa kilifanyika Zanzibar tarehe 12 Mei, 2021; moja katika vitu walivyovijadili ilikuwa ni nafasi sawa za ajira katika vyombo vya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi ni chombo cha Muungano, kwa hiyo, zinapotoka nafasi za ajira utaratibu tunatakiwa Zanzibar wapewe asilimia 21 ya nafasi hizo za ajira. Kwa hiyo ninasisitiza na hili Mheshimiwa Waziri alichukue na alifanyie kazi zinapotoka nafasi za ajira tunao vijana wengi mimi ndani ya Jimbo langu Chakechake wapo vijana wengi wasomi wamemaliza degree, wamemaliza form six, wamemaliza form four, wapo mtaani na wao wanahitaji hizo ajira zikiwa zinatoka itazamwe Zanzibar kwenye hiyo asilimia 21 ili na sisi tupate nafasi ya kuwa sehemu ya Jeshi la Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema chochote kuhusiana na yale maelezo ambayo uliyasema pale maana yake yale maelezo yalijitosheleza kuhusiana na dada yangu Mheshimiwa Jenista alipotoa utaratibu wa Kanuni ya 71 wa Kanuni za Kudumu za Bunge pamoja na Ibara ya 34 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini cha kushangaza mtu anashangaa kwa nini mwanajeshi anakwenda kwa Mkuu wa Mkoa, lakini mtu hashangai kwa nini mwanajeshi ni daktari anatibu raia wake wenye jamii. Unaogopa mwanajeshi akiwa Mkuu wa Mkoa tu na magwanda…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarrifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramandan kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Ramadhan kwamba kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63(2) na (3) imetoa mamlaka kwa Bunge kuishauri na kuisimamia Serikali na vyombo vyake. Kwa hiyo, pale nillikuwa ninatimiza wajibu wangu wa kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba kama Mbunge. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, humu ndani humu, Kanuni zetu ziwe zinatuongoza vizuri. Nilitoa mwongozo kuhusu utaratibu ulioombwa na Mheshimiwa Jenista na sasa amesimama Mheshimiwa Esther Matiko akieleza kwamba yeye alifanya jukumu lake, nadhani nilieleza kwa kirefu kabisa kwamba Rais hafungwi na ushauri unaotolewa, kwa hiyo wewe umefanya kazi yako na yeye anachangia vile aonavyo bora kama wewe ulivyofanya ya kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan malizia mchango wako.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naendelea, ni kwamba wanajeshi hawa hawa ndio madaktari wetu kwenye hizo jamii zetu na magwanda yao wanatutibu na wala hatuwaogopi, ni walimu mimi kwenye Jimbo langu wapo wanajeshi ni walimu mpaka wa madrasa. Kwa hiyo wamefanya urafiki na jamii kiasi kwamba wao kwa sababu ni ndugu zetu, hao hao wanajeshi baadaye wanarudi kwa sababu ni baba au ni mjomba unamuogopaje mjomba! Hiyo ndio ambayo nilitaka nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka kuishia hapo, ahsante sana kwa kupata hii fursa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Kwa niaba ya watu wa Chakechake na mimi ninaunga mkono hoja hii kutoka mwanzo wa uwasilishaji wangu, lakini nitakuwa na ushauri kidogo kwa Wizara hii kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kwenye ushauri wangu binafsi nichukue nafasi hii kwanza kutoa pongezi kwa bondia Hassan Mwakinyo kutokana na ushindi alioupata juzi baada ya kumpiga bondia Muangola kwa KO. Anaipeperusha bendera ya Tanzania vizuri, Watanzania tuko nyuma yake na tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nitoe pongezi kwa msanii wa kizazi kipya wa Tanzania, Nasib Abdul a.k.a. Diamond Platnumz kwa kuwekwa kwenye nomination ya Best International Act kwenye tuzo za BET. Nayo ni hatua kubwa na ya kupigiwa mfano. Na mimi niahidi kwamba nitampigia kura na kuwashauri Wabunge wenzangu tuungane kwa pamoja na Watanzania wote tumpigie kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, simpigii kura kwa sababu ni msanini tu, Diamond ni icon inayoamsha dreams za vijana wengi walioko nje ya muziki; ndio definition ya hard working, vijana wengi wanapotaka kujifunza kuhusu hard working na commitment kwenye tasnia au fani zao wanaweza wakamuangalia Diamond kama mfano. Kwa hiyo, hiyo inanipa mimi hiyo hamu ya kutaka kupiga kura kumpigia kura, ili apate kushinda imtie moyo kuendelea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu natoa shukrani kwa uongozi mzima wa GSM jinsi unavyoendelea kuishika Yanga na kutushika mkono kwenye kipindi hiki cha mpito, tunaelekea kwenye mabadiliko ya uongozi wa klabu wameendelea kutu- support kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, pongezi pia ziende kwa Mr. Ghalib Salim Said na uongozi mzima wa GSM, Mungu awajalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za nne ziende kwa Azam Media Limited, wameuheshimisha mpira wa Tanzania. Mkataba wa shilingi bilioni 225.6 unaenda kuongeza thamani ya ligi kuu ya Tanzania. Unaenda kuvitendea haki vilabu vyote vinavyoshiriki ligi ya Tanzania, vilabu 16, sio tu timu kubwa za Simba na Yanga. Vilabu vyote vinavyoshiriki ligi ya Tanzania sasa kutokana na mkataba huu vitakuwa vina uwezo wa kupokea shilingi milioni 500 kabla ya msimu, hizi ni nyingi na zitawasaidia vilabu vidogo hasa ambavyo vipato vyao bado viko chini kuweza kujikimu na kuondokana na umasikini wa vilabu vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wameutendea haki mpira wa Tanzania kwa sababu kwa mujibu wa mkataba huu coverage ya uoneshaji wa mpira inaenda kuwa asilimia 99 sasa. Kwa hiyo, tunaenda kuungalia mpira wa Tanzania kwa asilimia 99, hii ni heshima kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niipongeze TFF kwa kukubali hiyo tender na mkataba huu kuingia na Azam ni media ya nyumbani, kodi inarudi nyumbani kwa hiyo, ni heshima kubwa sana kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka mchango wangu nijikite kwenye mpira wa miguu. sisi wengine kileo chetu, hatuna starehe nyingine, kileo chetu ni mpira, aidha tucheze au tuangalie, tuzungumzie, yaani kitu chochote kinachohusiana na mpira, kwa hiyo mpira umekuwa ni sehemu ya maisha yetu tunavyotoka mpaka tulipo sasa. Moja katika kitu kinachotusononesha sana ukikaa ni kuangalia timu yetu ya Taifa, kwa kweli hatufanyi vizuri kwenye football, lakini nakusudia, hatufanyi vizuri. Tunapata progress, lakini haiendi kwa kasi tunayoitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ili tupate maendeleo kwenye mpira ni lazima tukubali kuwekeza kwenye mpira, nakusudia investment kwenye mpira. Hatujawa serious kwenye kufanya investment kubwa kwenye mpira. Wenzetu wa Burundi na Mauritius wanapiga maendeleo makubwa kwenye soka, wanaleta revolution kubwa kwenye soka. Baada ya miaka mitano mbele tutakuja kushangaa watakapofikia na yote ni investment. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpira ni profession, ni fani kama u-engineer, kama udaktari, kama ualimu, tusipowekeza tutakuwa tunajidanganya. Kama tuna uwezo wa kuchukua madaktari wetu kuwapeleka Urusi wakakae miaka mitano tunawalipia kwa pesa za Bodi ya Mikopo, kama tuna uwezo wa kuchukua ma-engineer kuwapeleka Japan, China, kuchukua madaktari kuwapeleka India wakakae miaka mitano ili tuje tubadilishe fani ya udaktari tuwe na ma- professional kwenye fani, the same ina-apply kwenye mpira. Hakuna ubabaishaji, tukitaka shortcut ndio tunapoharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Burundi wanachukua watoto wa miaka 11, wameingia mkataba na nchi za Scandnavia pamoja na Algeria, wanachukua watoto wao wenye talents, vipaji vya mpira wenye umri wa miaka 11 mpaka 14 wanapelekwa Algeria na Scandnavia, wanakaa huko kucheza, wako academy huko na federations ndio zinalipia gharama za kuwaweka huko. Tunalilia hatuna academy, hatujajenga academy, lakini wako duniani watu wanazo academy, tuwachukue hawa vijana wetu tuwapeleke kwenye hizo academy zilizoko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukichukua vijana watano ukawapeleka academy PSG - Ufaransa, watano wenye umri wa kati ya miaka 14, 15, 16, baada ya miaka mitano unapata watoto wasiopungua 30 wacheza mpira professional ambao watakuja kuipa nguvu timu yetu ya Taifa. Na sisi ifike wakati tuwe na timu ya Taifa ukikaa nyumbani kutizama timu ya Tanzania inacheza, una soda, unakunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasahivi moyo, sisi wengine tuna maradhi ya moyo. Sisi wengine tuna maradhi ya moyo, yaani hatutabiriki, mara unapata maradhi. Leo tunacheza vizuri, kesho pasua kichwa. Maana yake sisi tunataka kuziba ma-gap kwa kuweka viraka viraka, mpira ni uwekezaji, ni professional, hakuna shortcut. Ni lazima tuweke strategy za muda mrefu, bora tuumie miaka mitano hii, lakini baada ya miaka kumi tuje kustarehe…(Makofi)

SPIKA: Poleni sana Yanga, ugonjwa wa moyo jamani. (Kicheko/Makofi)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, baada ya miaka kumi tuje tukae tukistarehe tukiiangalia timu yetu ya Taifa. Sasa hivi mpira unachezwa na vijana wenye umri mdogo ndio wenye market. Ukisema mpira duniani sasa hivi unazungumzia uchumi. Wachezaji unalipwa kwa wiki pound laki moja, ni fedha nyingi. Watu ni fulltime job. Soka imekuwa fulltime job za watu hawafanyi kazi nyingine yoyote, ni mpira tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nikiiuliza Wizara wanajua nini kuhusiana na Kevin John? Wanaweza wasiwe na majibu.

Mheshimiwa Spika, Kevin John kapelekwa Genk, alipofika Genk wameshindwa kuingia nae senior contract kwa sababu ya umri. Wamemchukua wenyewe Genk wamempeleka Uingereza, Leicester School, akae Leicester, asome lugha na vitu vingine ajue, apate ile general knowledge, halafu muda ukifika wa kuingia contract atarudi Genk. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapolalamika kwenye mifumo na sera zetu za elimu, baadhi ya wakati na ajira za vijana wetu tunaweza tukaweka academy, sio lazima tusome chemistry, tuwalazimishe watoto wasome physics, wasome, unaweza ukawaweka academy ukawapa general knowledge ya kuyainua maisha tu na lugha. Yaani wakawa wamebobea mtu anajua lugha tano, sita, ikamtosha yeye kuwa aki-fail kwenye mpira anarudi huku kumsaidia kwenye maisha yake ya kawaida hizo lugha sio lazima tung’ang’anie vijana wetu lazima… (Makofi)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ramadhan Suleiman.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hoja ya bajeti iliyoko Mezani. Nichukue fursa hii kumpongeza na mimi kama wenzangu Waziri wa Fedha kutokana na uwasilishwaji wake mzuri wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalamu sio mchumi ni Mwanasheria. Kwenye sheria za uwakala kwa kitaalamu tunaziita Law of Agency, kuna usemi wa kilatini unaosema kuifasi pa alyum fas perse. Tunapompongeza Mheshimiwa Waziri tunampongeza yeye pamoja na timu yake yote walioandaa bajeti hii. Tunampongeza yeye pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa sababu, alichokileta ndani ya Bunge hili sio mawazo yake peke yake, ni yake yaliyochangayika na Mawaziri wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapolipongeza Baraza la Mawaziri tunampongeza Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia. Kwa hiyo, kilicholetwa mbele yetu ni maamuzi ya Serikali n ani maamuzi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanznaia. Mnafanya kazi nzuri kama Serikali, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo 15 ya kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148, kuanzia page ya 28 mpaka ya 31, mapendekezo 15. Moja ya mapendekezo hayo amekuja kuomba kufanyiwe marekebisho ya sheria ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyumba vya ubaridi, cold rooms. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoitazama bajeti hii ni kwamba, kwa asilimia 90 imesikiliza vilio vya Wabunge. Haya ndio ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele kila siku na Waheshimiwa Wabunge humu ndani kwa hiyo, ni bajeti ambayo imesikiliza na kuliheshimisha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani hiki kilio kimeliliwa sana humu na Dada yangu Mheshimiwa Neema Kichiki, mama lishe. Kwamba, inaenda kuongeza thamani ya mazao yetu ya mbogamboga kwenye sekta yake ya lishe ambayo itaenda kusaidia wakulima wanaolima mbogamboga na mauwa kuongeza thamani ya mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madini precious metals Wabunge wa kanda Mungu aliwajalia madini, hasa Kanda za Ziwa, Geita na kwingine, Mheshimiwa Musukuma, wamelia sana. Wakati wa uchangiaji wa jumla tuliyasema haya sana ambayo hiyo inaenda kuongeza thamani kwenye viwanda vyetu vya uchenjuaji wa madini ambapo jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua kiwanda kimoja, inaenda kuongeza fedha za kigeni, inaenda kuongeza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo ya kusamehe kodi kwenye ongezeko la thamani kwenye huduma ya bima ya mifugo. Wabunge Kaka yangu Mheshimiwa Nicholaus Ngasa, wamelia sana kuhusu hili, ndio ambalo Mheshimiwa Waziri kalichukua kalileta ndani ya bajeti kwa sababu, lilikuwa kilio cha Wabunge. Ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyasi bandia; rafiki yangu hapo Mheshimiwa Sanga amelipigia kelele hili, kwa hivyo limechukuliwa likaja likawekwa kwenye bajeti kwamba, linataka utekelezaji. Maana yake ukiiondoa hii inaenda kukuza yale mawazo ya Mheshimiwa Sanga ya kukuza mpira wetu na kuleta viwanja vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kadi za kutengenezea National ID. Haya yamepigiwa kelele sana, upatikanaji wa National ID umekuwa tatizo, labda kutokana na gharama za uzalishaji kwa hiyo, Waziri akaleta mapendekezo, ili tupunguze huko hizi ID zipatikane kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye simu janja, haya aliyasema kaka yangu Mheshimiwa Jerry. Tunataka kutoka asilimia 40 ya matumizi ya mitandao tunaelekea asilimia 86, hatuwezi kufika kwenye hiyo target kama gharama za simu janja, moderm na vishkwambi viko juu. Ndio hayo ambayo Serikali wameyaleta kwetu kwa sababu, hicho ndio kimekuwa kilio chetu cha muda mrefu; dada yangu Mheshimiwa Judith Kapinga haya kayasema sana kwa hiyo, yamechukuliwa mawazo yake yameletwa kwenye bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kaleta mapendekezo ya kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mikebe inayotumika kuhifadhia maziwa. Hapa yamesemwa hatusafirishi maziwa nje ni kwa sababu, kulikuwa kuna gharama za uhifadhi wa maziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Zanzibar ambalo ndiyo limenikuna kweli kweli Waziri ameleta mapendekezo ya kuondosha au kurudisha utaratibu wa VAT kwa bidhaa inazonunuliwa Tanzania Bara na zinazotumika Zanzibar. Wafanyabiashara katika Jimbo langu la Chakechake na Wazanzibar kwa ujumla wafanyabiashara wakubwa kama hardware’s kwa asilimia 80 sasa hivi wanaagiza bidhaa kutoka Tanzania Bara hawaendi tena China, hawaendi tena India, hawaendi tena nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nondo tunanunua Tanzania Bara, saruji tunanunua Tanzania Bara, wire za umeme tunanunua Tanzania Bara, tunanunua Tanzania Bara gypsum board, gypsum powders, bodi za kujengea, misumari, wires na tumekuwa tukililia hili kwa muda mrefu jirani yangu haya Mheshimiwa Abdul-Hafar wakati wa mchango wake alilisemea hili kwa sana kwamba kumekuwa na ukiritimba wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar wakija wakinunua bidhaa zao Bara na kuzirejesha Zanzibar na hiki ndiyo kilio ambacho Mheshimiwa Waziri amekileta na Serikali ya Mama Samia wamelisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lango ni kutaka kuondosha hiyo migongano, watu ambao walikuwa hawapendi muungano wetu walikuwa wanatumia mwaya wa kutubomoa sehemu hii, ya kuonesha hii ni nchi moja mbona mnanyanyaswa mkifika Bara. Sasa haya ndio yanakwenda kuondoka maana yake sasa unaondosha VAT kwa sababu VAT inalipwa na yule mtumiaji wa mwisho mlaji.

Kwa hiyo ukiweka VAT akija Bara analipa halafu akifika Zanzibar analipa mara mbili, anafanya double maana yake anaiongeza thamani bidhaa yake ili apate kufikia ile VAT aliyoitoa mara mbili na bidhaa inapanda bei kwa hivyo haya yanakuja kuondosha tatizo na kupunguza bei na kuwasaidiwa wananchi wetu walioko kwenye maeneo yetu na wafanyabiashara kufanya biasahra bila kusumbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo lilikuwa linatokea pia kwenye umeme tumesema sana kwenye TANESCO walipokuwa wanatuuzia umeme ZEC kwenda Zanzibar walikuwa wanatutoza VAT na ndiyo hayo madeni ambayo yalikuwa yanalalamikiwa na ikishafika umeme Zanzibar kwenda kwa mlaji mimi ili uingie kwenye nyumba yangu nalipa tena VAT, kwa hiyo mapendekezo haya yakishafanyiwa kazi maana yake yanaenda kuondoa hizo double VAT kwa sisi watumiaji wa mwisho wa umeme maana yake hii inaenda kurahisisha maisha ya wananchi watu. Kwa hiyo, nilivyoisoma bajeti hii kuanzia page ya mwanzo mpaka ya mwisho ya 121 hakuna kitu ambacho kilikuwa kinanipa furaha wakati nasoma kama nikiona haya yamesemwa na Mheshimiwa Waziri. Maana yake ndiyo yalikuwa vilio vya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Chakechake, naunga mkono hoja bajeti hii imetuheshimisha sana Bunge, Mungu aibariki sana Tanzania na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye hoja iliyoletwa mezani ya ripoti ya Sheria Ndogo kuhusiana na uchambuzi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mheshimiwa Spika, na mimi kutoka mwanzo wa mchango wangu naomba nieleze kwamba ni mmoja kati ya member ambao wanahudumu katika hii Kamati ya Kudumu ya Bunge Sheria Ndogo, kwa hiyo namimi naomba nichukue fursa hii kukupongeza kwa imani yako kwangu kwa kuniamini na kunichagua na kuhudumia kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu nataka niulekeze kwenye uhalisia ulipo ambao unawekwa katika sheria ndogo mbalimbali zinazoletwa kwetu. Kwa mujibu wa Ibara ya 64(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, mamlaka ya kutunga sheria yamewekwa kwa Bunge, lakini Katiba hiyo hiyo kwenye kifungu 97(5) ikatoa pia mamlaka kwa Bunge kukasimu madaraka yake kutunga sheria kwa vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, kutokana na wingi wa shughuli za Bunge, Bunge likapewa mamlaka kwamba linaweza kukasimu madaraka yake ya kutunga sheria kwa mamlaka nyingine au vyombo vingine ili viweze kulisaidia kwenye kutunga sheria zinazogusa maisha ya watu kila siku huko. Kwa sababu tunajua mchakato wa Kibunge wa kutunga sheria unakuwa ni mkubwa baadhi ya wakati na mahitaji ya sheria kwenye jamii zetu yakiwa makubwa nayo kwa hiyo mamlaka ya Bunge zikapelekwa ziruhusu mamlaka zingine zitunge sheria ili sheria hizo zisaidie kwenye maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, sheria zilizoletwa mbele ya Kamati na tukazichambua, tumebaini kama Kamati kuna sheria 11 zilikosa uhalisia kutokana na vifungu vilivyomo kwenye sheria pamoja na maisha ya Watanzania, kwenye kiingereza tunaita reasonability, vifungu vya sheria havina reasonability ya maisha ya Watanzania na inavyoonekana kuna baadhi ya maeneo ikitokea mtu anafaida ya jambo au interest kwenye kitu fulani kimbilio lake anakimbilia kwenye mamlaka za kutunga sheria ndogo kwenda kuweka sanctions ya hayo anayotaka, anaona kwamba huko ni rahisi zaidi kuliko kuja Bungeni. Kwa hiyo wanatumia mwanya wa mamlaka za kutunga sheria ndogo kwenda kuweka vitu wanavyotikana wao. Kwa mfano, kuna sheria ndogo ililetwa mbele yetu na tukaijadili Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru Halmashauri ya Njombe, sheria imeweka tozo na ada ya ushuru ya shilingi 1,000 kwa pikipiki inayoingia stand pamoja na shilingi 1000 kwa gari zinazoingia stand.

Mheshimiwa Spika, huku ni kuvunja moyo au ku- discourage watu wanaojishughulisha na shughuli za pikipiki hao bodaboda; yeye unamwekea shilingi 1,000 mwenye daladala inayopakia watu 40 unamwekea shilingi 1,000 ni kumuonea. Kwa hiyo hayo ndiyo mambo sisi tuliyaona kama Kamati natukayajadili na tukaishauri Serikali na mamlaka zilizotunga hizo sheria kwenda kurekebisha.

Mheshimiwa Spika, kuna Sheria Ndogo ya Ada ya Ushuru wa Halmashauri ya Kiteto imesemwa hapa kwenye taarifa na msoma taarifa, imeweka ada shilingi 20,000 kwa shughuli za jando na unyago, siyo sahihi hata kidogo. Tumezifanya shughuli za jando na unyago kuwa kama chanzo cha mapato, wakati zilivyowekwa uhalisia wake ni kuwa sehemu ya kufundisha vijana wetu nani shughuli za kijamii zinazokwenda kuwapa madarasa vijana wetu jinsi ya kuja kuishi kwenye jamii pana zaidi.

Kwa hiyo unavyoiweka kwamba lazima shughuli hiyo itoe shilingi 20,000 ni kuwaonea wananchi wasiokuwa na kipato wa kwenye jamii nyingi hasa za vijijini, kwa hiyo hayo ni miongoni mwa vitu ambavyo tumeviona wakati tunajadili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Kanuni ya Filamu na Michezo ya Kuigiza; mchangiaji wa kwanza Advocate Mheshimiwa Swalle alisema hapa, Sheria Ndogo ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Mjini wao wameweka kumiliki na kuendesha shughuli za kuonesha filamu kwenye mabanda ya filamu yale mabanda yetu yale tunaita mabanda umiza kibali kinaanzia shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000; huku ni kuwaonea wajariliamali wadogo waliojiwekeza kwenye hayo mabanda umiza, watu wenyewe ni maskini mtu ana mtaji wake mdogo, kaweka banda lake kwa ajili ya kuonyesha mpira na filamu wewe unamtaka akatoe shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000 hiyo shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000 anaitoa wapi.

SPIKA: Mheshimiwa Ramadhani Suleiman Ramadhani nakushukuru kwa mchango wako.

MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kupata fursa ya kuchangia kwenye itifaki au azimio hili la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalohusiana na usalama wa mimea, wanyama pamoja na usalama wa chakula. Kutokana na maelezo ambayo yametolewa mbele yetu na Mheshimiwa Waziri pamoja na taarifa ya Kamati, kitu ambacho nimejifunza, ni kwamba hii SPS Measure ina component mbili. Component ya kwanza inahusiana na Sanitary Major na component ya pili inahusiana na Phytosanitary Measure.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye component ya kwanza ya sanitary major ni kwamba msisitizo uwekwe kwenye kuweka measures au maana yake ni hatua au vitu vinavyoweza kum-protect binadamu kutokana na maradhi yanayotokana na vyakula. Maana yake ni measure to protect human from born disease. Ndiyo kitu ambacho nimekisoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu na ushauri wangu kwa Serikali utajikita kwenye kwenye usalama wa chakula (food safety) kwenye hii component ya kwanza ya sanitary measure. Ili twende sambamba na itifaki, ni kwamba lazima measures zetu tunazozichukua kama Taifa, moja kati ya vitu vinavyotakiwa tujitahidi ni kuhakikisha chakula tunachokila sisi na Watanzania wote kipo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja hapa za baadhi ya wachangiaji kwamba tumechelewa kwa muda wa miaka nane. Kuchelewa siyo tatizo, lakini tunapokiendea kitu, tuwe na uhakika wa asilimia mia moja kwamba tunakwenda kutekeleza itifaki ikiwa sisi ndani bado tuko salama na tutaji-protect kuingiza chakula kutoka nje ambacho hakiko salama na tutakuwa tuna ulinzi wa vyakula vyetu tunavyokula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu ni kwamba ili hizi measures zichukuliwe na zifanye kazi, mchangiaji aliyepita amezungumzia kwenye aspect moja ya sheria, lakini tunahitaji kuwa na sera ya usalama wa chakula (policy) ambayo haipo. Tukitaka tuende sambamba na wenzetu ni lazima tujitahidi tuwe na Sera ya Usalama wa Chakula. The main and first thing kwenye ile component ya sanitary measure, halafu sera ndiyo ifuatiwe na sheria pamoja na kanuni na miongozo itakayotufanya sisi tuwe salama zaidi kwenye vyakula vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ibara ya 11 ya itifaki hii ambayo inasema, itahusu nchi wanachama kuainisha, yaani kufanya harmonization sera, sheria, kanuni na program ili kufanikisha madhumuni ya itifaki hii, ni ibara imo ndani ya itifaki. Imesema, katika utekelezaji wa itifaki hii, ni lazima nchi wanachama kama blocks za Afrika Mashariki, tuwe au tume-harmonize sera zetu, sheria zetu, kanuni zetu na miongozo yetu kwenye wanyama, kwenye mimea na kwenye usalama wa chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuna-harmonize vipi wakati hata hiyo sera hatuna; na sheria zetu bado ziko scattered zinazohusiana na usalama wa chakula? Hizi zetu za ndani, hazijawa harmonized. Huwezi kupata sheria moja ambayo imesimama kulinda usalama wa chakula. Usalama wa chakula upo kwenye sheria tofauti tofauti, ndogo ndogo; unakuta iko kidogo kidogo kila mahali; kwenye uvuvi kidogo, kwenye kilimo kidogo, kwenye vipodozi kidogo, lakini hatuna sheria mama ambayo inasimama kufanya protections ya aina ya vyakula tunavyokula. Huo ndiyo wasiwasi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama walivyosema wachangiaji, kuridhiwa kwa itifaki hii iwe ni wake-up call kwa Wizara na Serikali kwamba tunahitaji tuchukue hatua za haraka, tena haraka sana ili kama nchi tuwe na sera, sheria na kanuni zitakazotulinda sisi kama nchi kwanza, halafu litakaloilinda block yote ya Afrika Mashariki kutokana na vyakula tunavyozalisha na tunavyotumia kila siku kwenye maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu kwa ujumla. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kupata fursa hii ya kuchangia kwenye hoja iliyoletwa mezani leo kutoka Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kabla ya kutoa mchango wangu napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na uwezo wa kusimama kwenye Bunge lako Tukufu leo kutoa maoni yangu pia nimuombe Mwenyezi Mungu huyo huyo aendelee kumpa nguvu Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassain anapotekeleza majukumu yake ya kitaifa akiwa nje ya nchi muda huu akiwa Misri Mungu ampeleke salama na amrejeshe salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wachangiaji waliopita kama watatu kuanzia Mheshimiwa Ridhiwani, Mheshimiwa Advocate Swalle na Kaka yangu Simai umeshaanza kuona picha kubwa ya jinsi sheria ndogo zinavyoleta changamoto. Bahati sijui niseme nzuri au mbaya kwa utaratibu wa kanuni za nchi yetu sisi Sheria zetu ndogo zinaanza kutumika kabla hazijaja kwenye Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake zinatolewa kwenye gazeti baada ya kutungwa halafu zinaingia mtaani zinaanza kufanya operation ya matumizi yake halafu baadaye zinakuja kwenye Kamati ya Sheria Ndogo kwa ajili ya uchambuzi ya kuona kwamba yale tuliyoelekeza watunga sheria yameendana na maelekezo ya Bunge? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida inapotokea ni kwamba sheria zinaweza zikawa zimeanza kufanya operation mtaani na zimeanza kutumika halafu sisi tunakuja kuona madhahifu yaliyomo mpaka tukiwaambia Serikali wakaribishe baadhi yao tayari zimeshaumiza watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapotoa msisitizo wa kipekee kwa Serikali kuwa makini mara mbili zaidi wanapotunga Sheria Ndogo ndiyo tunatakiwa tuweleweke hapo. Kwamba tunatoa msisitizo kwamba sheria hizi zitaenda kutumika kabla hazijapita kwenye Kamati za Bunge kwa ajili ya kuzi- scrutinize, kuzichunguza kwa makini na sisi kutoa mapendekezo ya yale tunayoyaona yanakosewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawaomba Serikali kwa sababu wamepewa mamlaka na Sheria za Bunge katungeni Sheria Ndogo kwenye mambo haya. Kwa hiyo, wanakuwa Kamati zao Ndogo wanakaa kwanza, wanakaa na wadau zinaandikwa zinapita kwa Waziri anazisoma, anazisaini kwa hiyo tunawaomba makini mara tatu zaidi ya kuhakikisha kwamba Sheria Ndogo hizo zinakuwa, zinapokuja kutumika kwenye jamii haziji kumi za watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikutana na sheria moja ilikuja kwenye kamati yetu kwa ajili ya uchambuzi hii ya uhifadhi wa wanyamapori ni kanuni ya uhifadhi ya wanyamapori ya mwaka 2021. Kwenye kifungu cha 31 cha kanuni hiyo imekuja kuwapa mamlaka hili Jeshi Husu, Jeshi la Uhifadhi la Wanayamapori, mamlaka ya kufanya upelelezi kukamata, kufanya searching za kwenye majumba na watu ku-secure maeneo ya matukio kufanya surveillance kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati tunachambua tulikuwa tuna wasiwasi haya mamlaka kwa mujibu wa criminal procedures yamewekwa kwa vyombo maalum vinavyofanya upelelezi kwa mfano Polisi. Leo tunayachukua mamlaka haya haya tunaenda kuwapa Jeshi Husu wafanye na wao, siyo shida lakini umakini wa kuhakikisha tuna-control behavior za majeshi yetu wakati wa kufanya haya tunatakiwa tuwe makini mara mbili zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wanaenda kuingia kwenye haki za watu, unapopewa haki ya kumkamata mtu na kumfanyia upelelezi maana yeke utakaa naye, utamuoji lakini kwenye criminal procedure utaratibu wa jinsi polisi na vyombo vingine vya upelelezi vimepewa mamlaka kwa kwa mujibu wa criminal procedure na utaratibu mzuri ambao wao wanaufuata na baadhi ya wakati vyombo hivyo vingine vinampaka ma-PGO, wana code of ethics na conduct za kuhakikiha kwamba hawavuki, na hawaharibu haki za watu wakati wakitekeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, moja katika vitu tunavyowaisitiza ni kwamba wahakikishe michakato ya kuwatungia code of ethics iende kwa haraka ili kuhakikisha kwamba hao waliopewa mamlaka sasa haya sasa hawaendi kuya-abuse haiendi kuyatumia kinyume na yanavyotakiwa kutumiwa kwenye sheria zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ulikuwa mchango wangu naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nami kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Kamati ya Sheria Ndogo ambayo imesomwa mbele yetu na Mwenyekiti wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nichukue fursa kama wachangiaji wengine kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi tunaahidi tutashirikiana na wewe.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kwenda kwenye hoja yangu nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, pesa za UVIKO zimefika Zanzibar na tumeanza kuona matumizi ya pesa hizo na zimeanza kuleta faraja na maendeleo kwa wananchi wetu. Miradi sasa ya maji, miradi ya kumalizia mabanda ya shule inafanywa kwa ufanisi mzuri zikisimamiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikijielekeza kwenye hoja, amemalizia mchangiaji aliyemaliza hapa kaka yangu Tarimo ambaye tupo Kamati moja kwamba kuna ugonjwa mkubwa unaendelea ambao ni ucheleweshaji wa kuyatekeleza mapendekezo yanayopendekezwa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, kwenye Bunge lako tarehe 28 Juni, 2021 Bunge lilipitisha Azimio la Kamati hii ya Sheria Ndogo na moja kati ya maazimio yaliyopitishwa na Bunge lako ilikuwa ni kwenda kufanya marekebisho kwenye maeneo ambayo Kamati ilipendekeza na iliona yana dosari, lakini kwa masikitiko makubwa yapo maeneo ambayo toka Mkutano wa Pili, Mkutano wa Tatu bado hayajafanyiwa marekebisho, sasa ni mwaka Serikali hawajafanya marekebisho ya maeneo ambayo Kamati ilipendekeza kwao kufanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Spika, zipo sheria zinaendelea kuumiza watu na Bunge likaziona na likaiambia Serikali wazirekebishe sheria hizo lakini hadi leo wanakuja kwenye Kamati baada ya mwaka sasa kauli ni ile ile ndiyo tunaandaa jedwali la rasimu kupeleka kwa CPD, tunaandaa jedwali la rasimu kwenda kwa mchapaji, kwa tukikaa nao wakija na story hizo hizo inaumiza kwa sababu tunapotoa mapendekezo tunataka wananchi wetu wasiendelee kuumizwa na sheria ndogo ambazo zipo na zinatumika huko kwenye maeneo tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka leo kwa mfano zipo sheria za kwenye Halmashauri yako ya Mbeya za kutoza tozo za bajaji na mpaka leo hazijafanyiwa marekebisho huu ni mwaka sasa na tumesema zifanyiwe marekebisho kwa sababu zilikuwa zimeshaanza kuleta ugomvi kule, lakini hadi leo bado. (Makofi)

Kwa hiyo, bado ninasisitiza na ninaomba na ninaweka msisitizo kwamba yale makabrasha yakishatoka kwenye Kamati yasiende kufungiwa kabatini, yanahitaji kufanyiwa kazi ili tupate weledi mzuri wa jinsi ya kuwasimamia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo nilitaka kuchangia ni hoja ya ushirikishwaji Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD). Hapakuwa na utamaduni wa Serikali wanapokuja kwenye Kamati kujibu hoja za Kamati kuja na mfanyakazi au ofisa yeyote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili kuja kutueleza hatua zilizofikiwa, wakija tu watakuambia kwamba hili lipo kwa CPD, sisi tukawashari kama Kamati sasa mkija kwenye Kamati mje nao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili sasa tujue ukweli ni upi kwamba tatizo lipo kwenu au tatizo lipo kwa CPD. (Makofi)

Sasa hivi hili limerekebishika na tunataka kutoa shukrani kwamba sasa wanapokuja kwenye Kamati yetu wanakuja na Ofisi ya CPD sasa hakuna mtu ambae anaweza kumzulia mwenzake kwamba nimepeleka pale kwangu imeshaondoka kwa hiyo kazi inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo ambayo nilitaka kuchangia kwa leo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya mimi kuchangia au kutoa mawazo yangu kwenye hoja za kamati zilizowasilisha ripoti zao za mwaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Kamati ya Sheria Ndogo. Kwa hiyo zilizoko mezani ni taarifa za mwaka za kamati mbili naomba mchango wangu niuelekeze wenye Kamati ya Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jukumu na mamlaka ya kutunga sheria za nchi hii ni mamlaka ya Bunge. Hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara ya 4 ikisomwa sambamba na Ibara ya 64 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake yote. Kwa hiyo, mamlaka yote ya kutunga sheria za nchi hii yako kwenye chombo hiki cha Bunge ambacho sisi tunakitumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Katiba hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatoa mamlaka ya kukasimu madaraka hayo ya Bunge kwa vyombo visivyokuwa Bunge ili vilisaidie Bunge kutengeneza Sheria kwa ajili ya kuleta mustakabari mzuri wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania. Hiyo ipo kwenye Ibara ya 97(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaratibu unatolewa kwenye sheria za nchi (principal laws), ambapo kwenye Sheria ya Tafsiri ya Sheria CAP 1 kwenye Kifungu cha 37 na 38 kinatoa utaratibu, vipi vyombo visivyokuwa Bunge vitatunga Sheria na vitapita katika utaratibu gani. Kwa hiyo, baada ya sheria kutungwa, kwa utaratibu uliopo, sasa kwa sheria zetu ni kwamba zitaingia mtaani na zinaanza kutumika baada ya kupata sahihi za waliopewa mamlaka ya kutunga sheria; aidha mawaziri au wakurugenzi, kwa zile sheria zinazotoka kwenye taasisi, na baada ya kutangazwa kwenye gazeti rasmi la Serikali, sheria hizo zinaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa utaratibu ni kwamba Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo inakuja kukutana na sheria hizo wakati sheria zikiwa zimekwisha ingia mtaani na zinafanya kazi. Sasa sisi tunatekeleza wajibu wetu wa kisheria wa kuzisimamia na kuzipitia sheria hizo ili kuona kwamba tuliowakasimu madaraka hayo hawayavunji? Hawayatumii wanavyotaka wao? Huo ndio wajibu wetu namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zinavyokuja mbele yetu sisi tunazipitia halafu tunatoa mapendekezo yetu na marekebisho kwa hizo taasisi zilizotunga kanuni hizo. Kwamba tunapoona sheria hizo zimevunja aidha Katiba au sheria mama au haziendani na uhalisia, tunawambia nendeni karekebisheni au nendeni kafuteni hii wekeni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kumezuka tabia ambayo si nzuri kidogo na ni lazima kama Bunge tuikemee. Maazimio ya Bunge kwa Serikali ya kurekebisha baadhi ya kanuni tunazowambia hayarekebishwi. Hilo ni jambo baya sana sana sana sana; kama taasisi hatutakiwi tuliache hata siku moja. Tuiachie Serikali wasirekebishe marekebisho tunayowapa aidha Kamati au Bunge zima linapofanya Maazimio baada ya Kamati kuleta taarifa yake ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo tumeyabaini kwamba tangu kikao cha Bunge la 5, 6, 7 mpaka leo Bunge la 10 hayajarekebishwa; bado yako mtaani na yanaumiza watu. Kuna kanuni hazifai kabisa hata kuziona, ziko mtaani na zinaumiza watu. Kwa sababu hizi kanuni tunazozipitia ndiyo maisha ya watu ya kila siku huko mtaani na wananchi wetu. Kwa hiyo sisi tunaposema zikarekebishwe kunapita zaidi ya miezi 6, 7, 8 hazijarekebishwa hivi tunategemea nini? Ni kanuni zinaendelea kuumiza watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nataka nitoe mfano mmoja. COSOTA walituletea kanuni moja hivi, walikuwa na kanuni yao inaitwa Copyright and Neighboring Right Regulation GN 137. Kwenye kanuni yao hiyo COSOTA walikuwa wana kipengele kwenye Kanuni ya 3 (2) na (3); ya kwamba mikataba yote ya wasanii wa nchi hii wanayoingia aidha na taasisi au ma-promoter au mtu yeyote lazima mikataba hiyo ipite COSOTA. Sasa walivyokuja kwenye kanuni tukawauliza mnataka kutibu nini? Mbona kama vile sheria itashindwa kutekelezeka? Unataka msanii aliyeko Geita Vijijini achukue mkataba wakati Geita hakuna hata Ofisi ya COSOTA aulete Dar es salaam ili wewe uje uipitie wewe nani? Mnataka kutibu nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatuambia malalamiko yamekuwa mengi sana ya wasanii kuwa wanadhulumiwa kwenye mikataba, hawajui, wanasaini mikataba wakiwa hawavijui vipengele. Kwa hiyo sisi tunataka tuwasaidie wasanii. Hata hivyo, behind wameweka kila mkataba watakaoupitia wata-charge asilimia moja ya value ya mkataba huo iende COSOTA ili wao wapate hiyo nafasi ya kutibu. Tukasema hii sio sahihi. Msanii akiona iko haja ya mkataba wake anadhulumiwa atatafuta mwanasheria. Kama ninyi COSOTA kama taasisi ya Serikali mnataka kusimamia msiweke ulazima, anayetaka aje, lakini si lazima. Kuna wengine wameshatoka huko wana wanasheria wao binafsi, unamlazimishaje aje COSOTA? kwa hiyo, toka Mkutano wa Tano jambo hilo halijarekebishwa hadi leo. Lipo hivyo na linaendelea kuumiza wasanii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria tukishasema, tukishatoa maazimio kuna tatizo lingine la kukaa muda mrefu sana kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Zinakaa kwa muda mrefu zikisubiri uhakiki au zikisubiri zipate GN. Ziko sheria za tangu Mkutano wa Sita na wa Saba mpaka leo. Serikali wakija kwenye Kamati yetu tukiwauliza mmefikia wapi kwenye kurekebisha yale mliyoambiwa mrekebishe na Bunge? Wanakwambaia sheria sisi tulikwisha rekebisha zilishapata saini ya Waziri lakini hadi leo zipo kwa Mwanasheria Mkuu hazijapata GN au nyingine zinasubiri uhakiki. Si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kanuni za halmashauri ndogo ya hifadhi ya mazingira ya Itigi. Kanuni hizi kwa mfano zilikuja na mapendekezo kwamba mtu yeyote anayekaa kwenye Halmashauri ya Itigi anayetaka kufuga, atafuga kwa idadi ambayo halmashauri itamwambia afuge. Kwa hiyo, walivyoleta kwenye sheria yetu tukawaambia hii sio sahihi, haiwezejkani kuwa hivi. Kwa nini halmashaurri mumpangie mtu mifugo? Hata kama mnataka ku-control mazingira mnaweza kuweka kwenye kanuni idadi ya mifugo mnayotaka lakini si maamuzi ya Mkurugenzi au Mtu yeyote kwenye halmashauri Kwenda kusema sasa wewe ng’ombe fuga 50, wewe utafuga 30, wewe kuku fuga hivi, si sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukawambia kwamba nendeni karekebisheni. Wamekuja kwenye Kamati ya Bunge hili tunauliza mmefikia wapi? Wanasema sisi tumekwisha saini rasimu ya marekebisho lakini hadi sasa rasimu hiyo Mheshimiwa Mwenyekiti, iko kwa Mwanasheria Mkuu haijapata GN Number. Hili ni jambo ambalo linaendelea kuwaumiza wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifano ipo mingi sana kwa sababu zinakuja kanuni nyingi ambapo kanuni nyingine hazitekelezeki, kanuni nyingine wanaleta masharti ambayo yamepitwa wakati. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni lazima tuchukue hatua kama Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ikishamaliza kufanya kazi yake na taarifa yake ikishasomwa ndani ya Bunge, Bunge linatoa maazimio ya jambo hilo likarekebishwe, likafanywe; sasa wewe unakuja kwenye Kamati kuja ku-negotiate Maazimio ya Bunge wewe nani? Bunge lishasema nenda karekebishe, karekebishe si wakati tena wa kuja kutuambia sisi tulivyoona hii ilikuwa si sahihi. Wabunge wote hawa 396 jambo hilo baada ya kuliazimia waliona si sahihi nyie watu wawili tu wa Wizara mkalione ni sahihi kweli jamani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naunga mkono hoja kwa taarifa zote mbili. Ahasante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya mambo ya Ndani iliyoko mbele yetu. Kabla ya kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya, hasa jinsi alivyochukua hatua za haraka na za makusudi akishirikiana na IGP Sirro kwenye kutatua tatizo la kiusalama lililopo kwenye baadhi ya maeneo ya katika Jiji la Dar-es-Salaam. Wanastahili pongezi kwa jinsi wanavyochukua hatua za kutatua changamoto hizo za kiusalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi katika mchango wangu nataka nijikite kwenye mambo mawili makuu au matatu. Kwa uchache wa muda nataka niende harakahara.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ni kuhusu uhaba wa vituo vya polisi kwenye maeneo yetu. Kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu la Chakechake, Wilaya nzima ya Chakechake ambacho ndicho kitovu na centre ya uchumi katika Kisiwa cha Pemba tuna Kituo cha Polisi kimoja tu. Watu wanafuata Kituo cha Polisi wakitoka masafa ya mbali kwelikweli.

Mheshimiwa Spika, polisi wanapofanya shughuli zao wanatoa huduma kwa kuwa shughuli za kipolisi ni huduma kama vile wananchi wanavyohitaji maji, elimu pamoja na umeme. Kwa hivyo wanavyohitaji ulinzi wa mali zao na wao raia kulindwa ndivyo wanavyohitaji huduma kama huduma nyingine. Kwa hivyo mtu kutoka eneo moja kutembea zaidi ya kilometa 15 ama 20 kufuata Kituo cha Polisi hili ni jambo ambalo sasa linatakiwa lifike mwisho. Watu wanatoka Pojini kufuata Kituo cha Polisi Madungu. Watu wanatoka Ole kufuata Kituo cha Polisi Madungu. Kituo hicho chenyewe ni kidogo, hakitoshi, kuna mlundikano wa mahabusu ambao wanakuwepo kwenye Kituo cha Polisi kabla hawajapelekwa Mahakamani. Kichumba hicho cha mahabusu cha ndani ya polisi ni kidogo, baadhi ya nyakati kinakusanya mpaka watu 40 ama 50 at a time, ni jambo ambalo sio zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi hapa alikuwa anajibu swali Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Sagini, alisema lilishatengwa eneo katika Wilaya ya Chakechake kwa ajili ya kujengwa kituo kingine ili kuondoa huo usumbufu, lakini tuliposoma eneo lote la bajeti hatukuona kwamba kuna jitihada za makusudi za kujengwa kituo kingine cha polisi. Kwa hiyo natoa wito, hali yetu ni mbaya, wananchi wanatembea masafa marefu kufuata huduma za kipolisi. Sasa tuko miaka 58 sasa ya tangu muungano wetu na tangu tulivyounganisha Jeshi letu la Polisi, lakini bado tuna kituo kimoja wilaya nzima. Hii haikubaliki, tunahitaji, na ushauri wetu ni kwamba, polisi waongeze huduma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi walioko kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili utajikita kwenye kubadilika kwa ufanyaji wa makosa. Sasa hivi ufanyaji wa makosa unafanywa sana online, unafanywa kwenye mitandao, lakini uwezo wa Jeshi letu la Polisi kwenye kukabiliana na kufanya upelelezi kwenye mitandao uko nyuma kulingana na ufanyaji wa uhalifu walioko mbele. Teknolojia imewafanya wahalifu wawe mbele zaidi kuliko uwezo wa Jeshi letu la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetunga Cyber Crime Act ili kukabiliana na makosa yanayofanyika kwenye mitandao. Tunayo Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Electronic and Postal Communication Act, lakini kufanyika kwa investigations za kipolisi kumekuwa na changamoto kubwa kwelikweli. Kituo cha Cyber cha Kipolisi kipo kimoja tu, Dar-es-Salaam. Sasa hivi ukitaka kufanya investigation za ki-digital kwa mfano kosa limeanzia kwenye simu, inabidi uchukue hiyo simu uliyoikamata kama kielelezo, uisafirishe, ipelekwe cyber center ikafanyiwe upelelezi. Hata ikirejeshwa ukitaka huyo shahidi atoke Dar-es- Salaam mpaka afike Pemba hilo kosa limeshachukua miaka miwili halijasikilizwa Ushahidi wake; kwa hiyo tuna changamoto kubwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwamba, umefika wakati sasa tupanue vituo vya cyber centers kwa ajili ya investigations za kipolisi kwenye maeneo ya kikanda, hasa Zanzibar. Muda umefika tuwe na kituo cha cyber cha Zanzibar kwenye kufanya investigations za kipolisi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kabla ya kutoa mchango wangu niitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania wananchi wa Zanzibar hawa wa Jimbo la Chakechake, tunaona jitihada na nguvu wanazozitumia kwenye kuiletea maendeleo Taifa hili. napongeza pia jinsi anavyoshirikiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi kwenye kuisaidia Zanzibar kusogea kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mchango kwenye jambo moja tu. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri alivyokuwa akisoma leo hapa, na ukisoma kwenye kishikwambi, kuna ongezeko kubwa sana la idadi ya mifugo kutoka mwaka jana hadi mwaka huu. Kwa mfano kwenye ng’ombe tumetoka milioni 35.3 mpaka milioni 36.6. Kwenye mbuzi tumetoka milioni 25.6 mpaka milioni 26.6, kwenye kondoo tumetoka milioni nane mpaka milioni tisa, kwenye kuku tumetoka miliono 92 mpaka milioni 97. Ukuaji wa sekta umeongezeka kwa asilimia tano, lakini cha kusikitisha moja katika eneo ambalo halifanyi vizuri kwenye kukua na kuongezea Pato la Taifa (GDP) ni eneo hili la sekta ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa National Bureau of Statistics of Tanzania (NBS), statistics zinaonyesha tangu mwaka 2019 GDP haijaongezeka kupitia sekta ya mifugo, yaani sekta ya mifugo haijaongeza tija katika kuongeza growth development product yatu. Kwa hiyo hili ni jambo ambalo Wizara wanatakiwa walichukue kwa uzito na kuona ni jinsi gani sekta italeta maendeleo kwenye kukuza uchumi na kukuza GDP yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamechangia hapa, Mheshimiwa Kamonga ametoka kusema hapa, kwamba Tanzania ni nchi ya tatu kwa idadi ya mifugo barani Afrika. Zipo nchi tunazipita kwa idadi ya mifugo, lakini hizo nchi zinafanya vizuri zaidi yetu kwenye uuzaji wa bidhaa za mifugo, hasa nyama kwenye soko la kimataifa. Kwa mfano South Africa ambao hawapo hata top tena wanauza kwa dola za Kimarekani milioni 89.2 kwa mwaka, sisi ni dola milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sudan wenye idadi ya takriban mifugo milioni 31 tu ambao sisi tunawapita kiujumla, wanauza kwenye soko la dunia takriban Dola za Kimarekani milioni 51, kwenye idara moja tu ya nyama. Misri ambayo nayo haipo hata kwenye top ten tunalingana kwenye uuzaji wa bidhaa za mifugo kwenye soko la kimataifa, hii ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Sasa kinachosikistisha, kuna watu tunawapita kwa idadi ya mifugo lakini wanapofika kwenye soko la kimataifa wao ndio wanatuongoza na wanajipatia fedha nyingi zaidi ya sisi, tunakosea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ambao ni majirani zetu wao wana kuku karibia milioni 21 tu tunawapita mara nne ya idadi ya kuku wetu takriban milioni 92, lakini wao pato lao wanafika Dola za Kimarekani milioni 71 zinazoingia kupitia mauzo tu ya kuku. Sasa kuna mahali tunakosea kama Taifa, kwa hiyo ndio hapo napotaka sasa Wizara watusikilize na wachukue ushauri wetu wakaufanyie kazi kwa ajili ya kutaka kuboresha sekta hii itusaidie kwenye kukuza uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi moja ya jambo lililoahidiwa kwenye sekta hii ni kwamba tutabainisha na kutenga maeneo ya ufugaji kwa kuyatambua na kuyapima, kuyasajili na kuyamilikisha ili kuongeza maeneo yaliyotengwa kutoka hekta milioni mbili na laki saba hadi hekta milioni sita. Moja kati ya mwarobaini wa kukuza pato letu kupitia sekta hii ya ufugaji ni kuwa maeneo tengefu kwa ajili ya ufugaji. Tumeshaingia kwenye migogoro mingi kwa miaka mingi, tumeona ufugaji wa kuhamahama hauna tija. Ilani imetuelekeza tuyatenge maeneo maalum, tuyaweke tuyarasimishe, tuyapime na tuwape wafugaji wetu wapime, tuwawekee miundombinu mizuri tuwape maji ili waongeze tija kwenye uzalishaji wa bidhaa za mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafeli tunapokwenda kuliendea soko la kimataifa kwenye bidhaa zetu za mifugo. Kuna kitu amekisema hapa mchangiaji aliyepita, kwamba tumeshindwa kuwa-label na kuwa-trace wanyama wetu. Soko la kimataifa linataka uwajue wanyama wako tangu walivyozaliwa, umri wao wanavyokuwa, wanachokula, ukienda uwe na hizo kanzidata za kutosha kwenye soko la kimataifa unapokwenda kuuza hizo bidhaa. Sasa zote hizo hatuna, hatuzijui, kwa hiyo inafanya quality ya bidhaa zetu iwe ndogo na hivyo kufanya competition ya kwenye soko la kimataifa pia nayo iwe ndogo. Kwa hiyo moja katika maeneo ninayoishauri Wizara ni kuongeza tija kwenye kufanya hiyo kwa ajili ya kusaidia ubora wa nyama inayotoka Tanzania ilii iwe juu na hivyo soko la kimataifa tuweze kuliendea kwa usahihi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndio mchango wangu naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu kuhusu Bajeti ya Wizara ya Biashara na Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna usemi wa Kiswahili unasema, “Ngoma ikipigwa Tanga, wanademka Pemba.” Kwa geographical location baina ya Tanga na Pemba, asilimia 50 ya bidhaa tunazozitumia Pemba zinatoka Tanga. Kama hazikutoka Tanga, zitatoka Mombasa au Unguja Mjini. Kwa hiyo, bidhaa za chakula tunatoa kwa ndugu zetu wa Tanga, the same kwa bidhaa ya cement au saruji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saruji inapoadimika Pemba, aidha tunaipata kutoka Mombasa au inaagizwa nje ya nchi kwa Zanzibar. Kwa hiyo, nimesikiliza kwa makini sana mjadala wa hoja ya ku-merge Kampuni ya Tanga Cement na Twiga Cement, vizuri sana. Wasiwasi walionao ndugu zangu Wabunge wa Tanga, Mheshimiwa Mnzava na aliposimama kaka yangu Mheshimiwa Kitandula, ndiyo wasiwasi huo huo ukaniingia baadaye mimi Mbunge wa Pemba ambaye nawawakilisha wananchi wa Pemba, hasa wa Jimbo la Chake Chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vile vile wanavyoogopa wao, nami ndiyo naogopa hivyo hivyo. Kwa hiyo, nilikuwa nataka kusema mengi sana kuhusiana na jambo hili kwenye how shares zilivyokwenda, vipi sheria ilivyokuwa, lakini Mheshimiwa Mnzava amezungumza kwa upana na kwa usahihi zaidi, hakuna ambaye hakumwelewa. Hakuna ubishi kwamba yapo maamuzi ya Mahakama kwenye jambo hili ya kuzuia na ku-stop ile merge isiendelee. Hiyo hakuna anayebisha kwamba yapo maamuzi ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnapataje nguvu na mabavu ya kwenda kutaka kuyapindua yale maamuzi ya Mahakama? Maamuzi ya Mahakama kisheria yanapingwa kwa vitu viwili tu; aidha uka-appeal Mahakama ya juu zaidi ya hiyo ikiwa maamuzi tofauti na yale yaliyotolewa na Mahakama ya chini, jambo ambalo baada ya maamuzi yale Serikali haikufanya; au uombe review. Mahakama yenyewe ikae, iyapitie maamuzi yake, halafu iseme kwamba aidha ilikosea au itoe maamuzi otherwise. Sasa hayo yote hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnataka kuendelea na mchakato, jambo ambalo Mahakama walishasema hili linavunja sheria kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 2003 kifungu cha 11, kwamba merging ambayo itazidi asilimia hizo za share market hairuhusiwi. Sheria hizo tumezitunga wenyewe. Kuna mtu kwenye mjadala asubuhi anasema sheria mbovu. Hii ndiyo international standards, unaitaje sheria mbovu jambo ambalo ndiyo kimataifa linakubaliwa liwe hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji akija anayatazama yote hayo ili naye awe salama, asije akawa ameanzisha biashara, katikati ya process biashara yake inakwenda watu wanakuja ku-merge, wanali-monopolize soko, yeye anakufa, anaondoka. Kwa hiyo, vitu vyote hivi tunafanya kwa sababu hizi ndiyo international standards. Kwa hiyo, tunafuata sheria kwa sababu jumuiya hizi za Kimataifa ndizo zinataka sisi tuzifuate. Kwa hiyo, tumeweka utaratibu wetu wenyewe, sheria zinatakiwa zifuatwe. Hicho ndicho nilichotaka kusisitiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari za kwamba nani alikwenda Mahakamani, sijui Chalinze Cement akaenda Mahakamani; wakati Chalinze Cement anaenda Mahakamani alikuwa na locus stand ya kwenda Mahakamani na ndiyo maana akawa part ya kesi. Kama Chalinze Cement angekuwa hayupo, maana yake Mahakama inge-determine kwamba huyu jamaa siyo part ya kesi. Hiyo kesi imemalizika, decision imetolewa, mnatakiwa mtekeleze. Hii tabia ya kuwaachia Serikali maamuzi ya Mahakama wayazingatie, wayakanyage kanyage, wayapige mateke, tutawapa mamlaka ambayo baadaye tutakuja kuyajutia sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Bunge, tunatakiwa tusimamie kwa hali yoyote ile, Serikali waheshimu mhimili wa hizi tribunal zinapotoa maamuzi. Unaweza ukaiona ni Quasi-Judicial Body imetoa maamuzi, lakini anaye-reside pale ni Jaji wa Mahakama Kuu na ile ni binding decision yake. Unataka kuikwepaje sasa hivi? Kama kuna hoja mpya, nilikuwa nimesoma kwenye Gazeti la Citizen, hoja ya watu wa FCC ni kwamba maamuzi yalitoka 2022, sasa hivi 2023 mazingira ya soko yamebadilika. Kuna mazingira mapya, kila kitu kimebadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa, lakini mazingira yakibadilika hayabadilishi maamuzi ya Mahakama. Maamuzi ya Mahakama hayabatilishwi na mazingira mapya. Maamuzi ya Mahakama yanabatilishwa na sheria pia. Kwa hiyo, unatakiwa ufuatwe utaratibu wa kisheria kubatilisha yale maamuzi ya tribunal. Kwa sababu maamuzi yale yanasimama, Serikali chonde chonde, heshimuni sheria kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yale yalishatoka, mnachotakiwa ni kuyasimamia, na kama kuna jambo lingine linatakiwa kufanyika, mnatakiwa mliendee kwa busara zaidi. Hakuna anayezuia merge isifanyike, lakini ikiwa utafuatwa utaratibu wa sheria na utaratibu tuliojiwekea wa kikanuni wetu wenyewe. Kwa hiyo, hicho ndiyo nilichokuwa nataka kusema juu ya wasiwasi wetu tulionao baada ya kusikia kilio cha Wabunge wenzetu majirani zetu ambao kuathirika kwao ni moja kwa moja kunaenda kutuathiri na sisi. Kwa hiyo, hicho ndiyo nilichotaka kuchangia, na ninaomba Serikali wasikilize kilio chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba iliyoko mbele yetu leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa mchango wangu nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na afya na kutujalia kuwa wazima na kuendelea kulitumikia taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za kuendelea kumalizia miundombinu ya barabara na miradi mikubwa ya reli ya SGR na mambo mengi kwa ajili ya kuendelea kuijenga nchi hii. Pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kumwamini Waziri Profesa Mbarawa, kuendelea kuishikilia Wizara hii. Wewe Profesa Mbarawa ni true definition ya maana ya kiongozi. Umeendelea kuwa shupavu, umekomaa kumsaidia Rais, tunakuombea dua Mwenyezi Mungu aendelee kukulinda, kukupa nguvu, wewe ni kiongozi mzalendo wa nchi hii. Kwa hiyo, tunakupongeza kwa juhudi kubwa unazozifanya kwa ajili ya kulitetea na kuliletea maendeleo taifa hili, hasa kwenye suala la miundombinu ya taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa na mambo mawili kwenye mchango wangu. Jambo la kwanza, tuna masikitiko makubwa sisi wakazi wa Tanzania wanaokaa Pemba na Unguja. Shirika letu la Ndege la Taifa (ATCL) ni keki ya taifa. Masikitiko yetu sisi bado hatu-enjoy keki hiyo. Kuna tatizo kubwa sana la safari za ndege kutoka Pemba kwenda Unguja na kutoka Unguja kwenda Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukitaka tiketi ya ndege inabidi uikate kwa wiki mbili kabla la sivyo huwezi kupata tiketi. Kukitokea dharura hakuna usafiri wa anga, usubiri meli na jambo ambalo nalo linasuasua. Kwa hiyo, wito wangu kwa Wizara hii waangalie uwezekano wa kutuwekea route japo mara moja kwa siku ili kutatua tatizo hili. Kama wamefanya tathimini na kuona ndege zao kubwa za Dash 8 - Q400 ni kubwa kwenda Pemba kwa sababu zinahitaji abiria wengi, niwahakikishie abiria wapo au tusubiri hyo ndege yao ambayo iko matengenezoni huko Malta ya Dash 8 Q300 itakapokuja Mheshimiwa Waziri upambane uhakikishe wakazi wa Pemba na Unguja wanpata ku-enjoy na wao keki ya taifa ya kuzitumia ndege hizi za Shirika la ndege la taifa, tunateseka. Kwa hiyo, nafikiria hilo ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri kwa sababu ni mzikivu atali-consider au atalizingatia kwa mapana makubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kwamba, sisi Tanzania Mwenyezi Mungu ametujalia kuwa kwenye nchi kubwa sana kijiografia. Hiyo ni bahati tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Hii nchi tukisubiri tuijenge wote kwa pesa za ndani aidha tutashindwa au tutachelewa. Hayo mambo mawili yanaweza yakatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia imekwisha move huko, hao watu ambao wanatuzidi kila kitu, wanatuzidi per capital income, wanatuzidi makusanyo kwenye revenues, wanatuzidi kwenye GDP, wao aidha wako kwenye PPP au wako kwenye EPC + Finance. Kwa nini sisi masikini bado tunang’ang’ania kutumia kipato chetu kidogo tunachokipata kutaka kujenga miundombinu yote ya nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umefika tuwaachie private sectors waje wajenge baadhi ya sehemu kwenye miundombinu yetu. Viwanja vya ndege, bandari, barabara tunaziweza kuziendeleza tukazijenga kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mtindo wa aidha EPC + Finance au PPP, ule ambao Serikali tutaona unafaa ili kusaidia hizi fedha kidogo ambazo tunazozikusanya au tunazipata zikaenda kusaidia kwenye mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi; elimu Serikali, afya Serikali, welfare ya watu wa nchi hii Serikali, biashara Serikali, sasa tutafanya yote hayo na kipato chetu si cha kutosha? Kwa hiyo, tuwaachie private sector waingie waje watusaidie tuwabane kwenye negotiations ili wasaidie hiyo miundoimbinu ijengwe, hatutoweza kuvifanya vyote. Kama nchi kubwa kama Russia wamebakisha jeshi tu ndilo ambalo bado linahudumiwa na Serikali itakuwa sisi Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vya ndege vyote ni private owned (vinamilikiwa na private) na Serikali wana-joint venture, wanakusanya kodi, wanapata kipato na maisha yanaendelea. Hatutaweza, hii Tanzania ni kubwa, na kila siku watu wanasogea kwenye maeneo ambayo mwanzo yalikuwa hayakaliwi na watu. Wakisogea watahitaji barabara, wakisogea watahitaji wajengewe miundombinu hatutaweza halafu tutachelewa. Kwa hiyo, ushauri wangu tuondoke huku tuondokane na huu uzamani. Tuwaruhusu private sector waje wajenge sisi tuwabane kwenye mikataba na negotiations za kutusaidia sisi wasije wakatubana mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji aliyepita, Mheshimiwa Sangu amelalamika hapa kuhusiana na matrilioni na mabilioni ya fedha zinazokusanya kwenye certificates kwa kuchelewa kulipa riba. Haya yote yanatokana na fedha zetu kuwa ni kidogo, hatuna uwezo wa kuzigawa zote kwa pamoja ukalipa wakandarasi, huku elimu inataka kuhudumiwa, huku hospitali zinataka kujengwa, haiwezekani. Kwa hiyo, tuwaachie watu wajenge sisi tuwakamate tukusanye kodi zetu maisha yaendelee. Huo ndio ushauri wangu na tunaweza kwenda kwenye nyanja zote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ahsante sana kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi nichangie kwenye Muswada huu nilikuwa na mambo matatu tu ya kuchangia. Kwanza kabla ya kutoa mawazo yangu nipongeze Jeshi la Zimamoto kwa kwa kazi nzuri inayofanywa ingawa inatakiwa waongeze juhudi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Tanzania Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya hasa wakati huu anafanya ile royal tour Mungu ambariki sana na amlinde na majanga yote wakati anafanya hiyo royal tour yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niende straight kwenye mchango wangu sasa kwenye Muswada, kwenye kifungu cha 11 nimeona kuna makosa kidogo aidha sijui inawezekana ya uandishi wakati naupitia huu Muswada inawezekana kamati haikuona kwa sababu haikusema kwenye mapendekezo yake na pia haikuonekana. Lakini nimeona kwenye kifungu cha 11 cha Muswada kinaleta marekebisho kwenye kifungu cha 32 cha Sheria Mama, ambacho kifungu cha 32 cha Sheria Mama kina Paragraph (a)-(h), (h) ina (i),

Mheshimiwa Spika, kwenye marekebisho ilivyoletwa kwenye Muswada wanasema kinafanyiwa marekebisho kifungu kwa kuondoa paragraph (h). Sasa haya marekebisho yanapofanywa ya kuondoa Paragraph (h) kifungu kidogo cha (b) kimesema kina rename kimetumia neno ku-rename kifungu cha (h) kuwa (n) na (o).

Mheshimiwa Spika, sasa wakati ninakipitia nimeona kama kime-chopper numbering kwa hiyo Mheshimiwa Waziri aiangalie vizuri ime-chopper maana yake kimeenda (n) na (o) hakijapita (m), na (h) mpaka (I) kipo kwenye marekebisho lakini kwenye sheria mama kuna numbering zimekosewa. kwa hiyo, unaweza kuiona hiyo Mheshimiwa Waziri wakati anapokuja kufanya majumuisho.

SPIKA: Endelea na linalofuata baada ya kuchangia nitakuomba uje hapa utakaa pembeni na Mheshimiwa Waziri au AG hapo mtaona hilo likoja.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, nimuoneshe.

SPIKA: Endelea na linalofuata na linalofuata.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, Sawa ahsante la pili nilitaka kuchangia ukisoma kwenye Sheria Mama hii sura ya 427 na Muswada unaoleta mapendekezo ya Sheria Mama hakuna sehemu nimeona Sheria zinatoa wajibu wa raia kulisaidia Jeshi la Zimamoto wakati wanafanya operation zao za kuzima moto hasa kwenye suala la fire hydrant ki-mantiki baadhi ya wakati Jeshi linapokwenda kufanya kazi ya kuzima moto hizo hydrant maana yake wao wanatumia maji kuzima moto na maji yanaweza yakawa yapo mbali, tuchukulie mfano moto unazimwa Dodoma Mjini na Hydrant pengine ipo Kisasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, alivyosema Mwenyekiti maji yakishamalizwa inabidi fire litoke kufuata maji kisasa lakini hapa kati kabla ya kufika Kisasa kwa mfano kwenye Sheli ya Shabiby panaweza pakawa pana magari ya maji ya private ambayo yanauza maji private, yakawa yanaweza ku-rescuer situation kabla ya gari la fire kufika Kisasa ambapo mbali, hata wakirudi huku moto umeshateketeza.

Mheshimiwa Spika, sasa je, hakuna sehemu sheria inatoa wajibu wa kisheria kwa raia kwenye situation kama hiyo kuisaidia fire maji? Kwa hiyo, nikawa nimeona aidha kama haiwezekani sasa hivi kuwekwa kwenye Mswada Sheria inaweza ikaletwa kwenye kanuni wakati Waziri anafanya kanuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wenzetu wanapopata dharura kama hiyo mpaka nyumba za private kwa mfano zenye ma-swimming pool zinasaidia gari za fire kunyonya maji kwenye yale ma-swimming pool kwenda kusaidia kuzima moto, kwa sababu miundombinu yetu bado ni migumu hizo hydrant wanazosema zipo mbali na ni chache baadhi ya wakati unaweza ukamkuta mtu tu private anayo lakini kama haujamuwekea wajibu wa kisheria huwezi kuja kumwajibisha baadaye akikataa kukupa yale maji yake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, aidha ingewekwa kwenye sheria au kanuni responsibilities au duty ya raia yeyote ambaye anaweza kuisaidia fire kupata maji wakati wa kutoa msaada wa kuzima moto huo ndio ulikuwa ushauri wangu wakati nasoma kwenye hii sikuona.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka niipongeze kamati mimi sio mwanakamati lakini nataka niipongeze kamati kwenye pendekezo lao namba moja wamesema kwamba wameshauri kwanza Bunge liridhie lakini pia kwenye kifungu cha 6 wamependekeza kwamba hii sheria i-act kwenda mbele isirudi nyuma hiyo ni jambo zuri sana ambayo naipongeza kamati hilo wameliona kwamba ha o ambao sasa hivi hawana hiyo miundombinu na wameshajenga hayo majengo tusiwarejee kuwaadhibu kwasababu wao wakati wanajenga sheria ilikuwa haifanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sheria ianze kwa kwenda mbele hiyo ni observation kubwa sana imefanya na kamati yako na niwapongeze sana, ingawa nimesema hapa kwamba sio mwanakamati huo ndio ulikuwa mchango wangu. Naomba nitumie hii kumuonesha Mheshimiwa Waziri kwenye mpangilio huu wa vifungu, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata fursa hii ya kuchangia kwenye hoja iliyoletwa mezani na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenye Muswada huu wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya mwaka 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miongoni mwa wale member ambao waliongozwa na Mheshimiwa Spika kwenda kusaidia Kamati ya Katiba na Sheria kutoa maoni ambayo ndiyo yameletwa hapa mbele yetu leo. Kwa hiyo, tuliujadili kwenye kamati kwa kina sana, tukashauriana na mapendekezo yaliyoletwa mbele yako na maoni ya kamati ndiyo yale ambayo tulikubaliana sote kama wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwenye huu Muswada kuna lugha inatumika kila kwenye kifungu kinachofanyiwa marekebisho ambacho kimeongozwa kwenye sheria zote 14 ambazo zimeombwa kufanyiwa marekebisho kwenye Muswada huu, kumefanyiwa marekebisho zaidi ya vifungu 30 vinafanyiwa marekebisho na kila kwenye kifungu chenye marekebisho kuna lugha imetumika. Hiyo lugha inasema Mkataba unamasharti kama itatokea mkataba una masharti maalum ya utekelezaji wa kifungu hiki na masharti hayo ikiwa yamekubaliwa na Baraza la Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila kwenye kifungu kilichoombwa kufanyiwa marekebisho kwenye Muswada huu kimewekwa masharti yenye maneno haya; ikiwa kutakuwa na mkataba na mkataba una masharti maalum ya utekelezaji wa kifungu hiki, hicho kifungu kinachoombwa kufanyiwa marekebisho na masharti hayo ikiwa yamekubaliwa na Baraza la Mawaziri. Sasa hapa ndipo ninapotaka kushauri; maana yake tunaweka kwenye Muswada huu ambao baada ya kupita Muswada huu itakuwa sheria mandate kwa Baraza la Mawaziri ili lipate kufanya maamuzi yanayogusa kwenye Mamlaka zingine zote ambazo zimeombwa kufanyiwa marekebisho 14. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wito wangu ni kwamba sheria hii haita-apply kwa mikataba yoyote ile ambayo maamuzi yake hayatakubaliwa na Baraza la Mawaziri hicho ndiyo kitu ambacho nataka nikiseme mbele ya Bunge hili, maamuzi yoyote yale ya mikataba yoyote ambayo itafanywa sehemu yoyote na mamlaka yoyote ya Serikali aidha Kuu au Serikali za Mitaa hayatafanyakazi ingawa kwenye mikataba yao hiyo watakubaliana huko kuweka masharti ambayo yataendana na vifungu vilivyofanyiwa marekebisho, mikataba hiyo haitafanya kazi ikiwa mikataba hiyo haikupata maamuzi na baraka za Baraza la Mawaziri, hicho ndicho ambacho nilitaka kukisema mbele ya Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, watu baada ya sheria hii kuanza kufanyakazi wasije wakajitoa ufahamu huko akaenda akafanya mkataba kwa mfano ambao utaathiri Sheria ya Mazingira kwa mfano kwa hiki kifungu cha (6) kilichoombwa kufanyiwa marekebisho, halafu akadhani mkataba huo utafanyakazi kwa masharti ya mabadiliko ya kifungu, lakini kama mkataba huo haukupitishwa na kupata baraka za Baraza la Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ndiyo alert ambayo mimi nilitaka kuisema na ndiyo mchango wangu all in all Muswada huu ni mzuri na ukishakuwa sheria utatusaidia kwenye mradi wa mkakati huu ambao kwa asilimia 90 utatunufaisha sisi Tanzania kwenye kuendelea kukuza uchumi wa nchi yetu hii inayoendelea sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo yalikuwa maoni yangu na ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kutoa mawazo yangu kwenye hoja zilizoletwa mezani leo.

Mheshimiwa Spika, mbele yetu kuna miswada miwili, kuna Muswada wa Haki ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kuna Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania wa mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu naomba niulekeze kwenye Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania wa mwaka 2022. Kwa mujibu wa index ya utafiti ya uwekezaji ya Afrika inayoitwa Deloit Africa Investment Attractiveness Index iliyofanya tafiti kwa kutumia vigezo viwili vya market access au market size pamoja na business environment imeiweka Tanzania kwenye rank ya nane kwa mazingira mazuri na bora kwenye kuwekeza, ikiwa ya tatu kwa East Africa, tukiongozwa na Kenya na Rwanda. Na kwa mujibu wa data ya World Bank ya mwaka 2020 Tanzania ni nchi ya 141 kati ya 190 kwenye mazingira mazuri ya kuruhusu uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 tulipitisha blue print na lengo la blue print lilikuwa ni kutafuta suluhisho la matatizo ya uwekezaji yaliyokuwa yanatukumba kama Taifa. Tulikuwa tunakwama wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukapitisha blue print ikiwa kama regulatory reforms ku-improve business environment ya Tanzania. Sasa kwa masikitiko makubwa sana nimesoma blue print, nikilinganisha na mabadiliko yanayoletwa kwenye sheria yaani huu muswada, nikawa nakosa connection ya vipi muswada huu uta-accommodate, utaunganisha matokeo ya blue print na hoja zilizoletwa na mapendekezo na tunavyoelekea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo mwaka 2022 tunapitisha muswada huu ambao baadae utakuwa sheria, hatujui tutakaa kwa muda gani kuja kupitisha muswada mwingine mpya ambao tutatunga sheria mpya ya uwekezaji. Kwa hiyo, hii ndio nafasi yetu pekee ya kuishauri Serikali ili kuleta mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, Waziri anapokuja kufanya majumuisho atujibu, aseme ni kwa vipi mapendekezo na hoja zilizoletwa kwenye blue prints na effectiveness zilizoonekana zitaleta tija kwenye muswada huu, mimi sijaona, nilivyosoma vyote sijapata kuona. Kwa hiyo, inawezekana yeye anayo majibu yaani kiasi gani blue print imekuwa accommodated ndani ya muswada ulioko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye kifungu cha pili cha muswada wa sheria, kinatoa masharti kwamba sheria hii itatumika kwa taasisi za kibiashara zilizokidhi matakwa yaliyoko kwenye kifungu cha 2(2).

Sasa nilivyokuwa nakisoma kifungu kidogo cha pili kikasema; kwa Mtanzania, kifungu kidogo cha (2)(b), Mtanzania ambaye atapewa favor zilizomo ndani ya muswada huu ambazo tunaziita vivutio na atapata tija na ulinzi unaoletwa kwenye muswada huu ni Mtanzania ambaye ataweka mtaji usiopungua dola za Kimarekani 50,000.

Mheshimiwa Spika, dola za kimarekani 50,000 ukizipiga kwa Tanzania shilling ya sasa ni zinakaribia milioni 115. Ni Watanzania wangapi wana shilingi milioni 115 za kuweka mitaji ya kuanzisha biashara mpya ambazo watakuja kuhitaji incentives na huruma zilizoko kwenye muswada huu?

Mheshimiwa Spika, Watanzania wetu wengi hawawezi, hawana mitaji hiyo. Wanaanza wakiwa underground, mitaji midogo, wanaanza biashara from the grassroot, kwa hiyo, ni vigumu kupata unafuu uliotolewa na muswada wa sheria hii na kuna faida nyingi zinaletwa humu kwenye vivutio, kuna misamaha ya kodi, kuna vitu kwenye jinsi ya usajili, ridhaa, leseni urahisi wake wa kupatikana, zote hizo, lakini sasa leo unaenda kuweka kifungu ambacho unasema ili Mtanzania alindwe na matakwa ya sheria hii ni lazima awe kafikisha mtaji wa dola 50,000. Tunaenda wapi? Kwa nini tusiweke kwa Watanzania tupunguze kiwango cha mtaji ili kuwaruhusu Watanzania wengi wanaofanya biashara, hasa wadogo, wawe accommodated ndani ya muswada huu utakapokuwa sheria kuja kuwalinda na kuwapa unafuu.

Mheshimiwa Spika, moja katika industry inayokuwa kwa kasi sana ni mafundi washoni wa nguo (tailoring). Mimi nataka nikutajie baadhi tu ya tailoring marts zinazofanya vizuri sana sasa hivi; moja ni Shine by Catherine ya dada yangu Mheshimiwa Catherine Magige, nyingine ni Carenitho Smart, yuko dada anatushonea yuko nje hapo tu, nyingine ni Better Design ya dada yangu Mheshimiwa Sylvia Sigula, kuna nyingine JM International Collection ni kijana wa Kitanzania, kuna nyingine inaitwa Suti Bega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya miaka mitano mpaka 10 tutakuwa hatuvai tena suti zinazotoka Uturuki wala China, tutakuwa tunavaa suti zinazoshonwa na mafundi wetu Tanzania, kwa sababu imani ya kuwaamini mafundi wetu inakua siku hadi siku. Hii suti niliyovaa hapa imeshonwa na Mtanzania. (Makofi)

Sasa moja katika maeneo ambayo nahisi bado Muswada wa Sheria za Uwekezaji hauwatendei haki ni wafanyabiashara wanaokuwa, wanaojikwamua, hasa hawa miongoni mwao ni hawa ma-tailoring ambao ni Watanzania wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mwekezaji anayetoka nje akija akianzisha kiwanda cha kutengeneza aidha misumari au mabati atapata unafuu wa kuingiza raw materials ya wire rods kama raw materials, lakini Mtanzania anayeshona anaingiza kitambaa kama bidhaa sio raw material. Kwa hiyo, akiingiza kama bidhaa yeye anakinunua kama bidhaa, anaenda kukikata akishone suti, anaanza kukamatwa anaponunua bidhaa, halafu akishashona suti hiyo ikiingia dukani anaanza kukamatwa tena.

Mheshimiwa Spika, sasa maoni yangu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 kengele ya pili imeshagonga.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, sawa ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu ni kwamba lazima tutengeneze mazingira wakati wetu ni huu. Tukikubali kupitisha muswada ambao bado hautoi nafuu nzuri kwa Watanzania wetu tutakuja kukaa tena zaidi ya miaka 15/20 kusubiri jambo hili litokee tena.

Kwa hiyo, naiomba Serikali ichukue jitihada na maoni yetu kuona wanafanyaje kushughulikia jambo hili ili kuifanya Tanzania iwe sehemu nzuri ya uwekezaji. Hayo ndio maoni yangu. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi ya kutoa mawazo yangu kwenye hoja zilizoletwa mezani leo.

Mheshimiwa Spika, mbele yetu kuna miswada miwili, kuna Muswada wa Haki ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kuna Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania wa mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu naomba niulekeze kwenye Muswada wa Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania wa mwaka 2022. Kwa mujibu wa index ya utafiti ya uwekezaji ya Afrika inayoitwa Deloit Africa Investment Attractiveness Index iliyofanya tafiti kwa kutumia vigezo viwili vya market access au market size pamoja na business environment imeiweka Tanzania kwenye rank ya nane kwa mazingira mazuri na bora kwenye kuwekeza, ikiwa ya tatu kwa East Africa, tukiongozwa na Kenya na Rwanda. Na kwa mujibu wa data ya World Bank ya mwaka 2020 Tanzania ni nchi ya 141 kati ya 190 kwenye mazingira mazuri ya kuruhusu uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 tulipitisha blue print na lengo la blue print lilikuwa ni kutafuta suluhisho la matatizo ya uwekezaji yaliyokuwa yanatukumba kama Taifa. Tulikuwa tunakwama wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukapitisha blue print ikiwa kama regulatory reforms ku-improve business environment ya Tanzania. Sasa kwa masikitiko makubwa sana nimesoma blue print, nikilinganisha na mabadiliko yanayoletwa kwenye sheria yaani huu muswada, nikawa nakosa connection ya vipi muswada huu uta-accommodate, utaunganisha matokeo ya blue print na hoja zilizoletwa na mapendekezo na tunavyoelekea mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo mwaka 2022 tunapitisha muswada huu ambao baadae utakuwa sheria, hatujui tutakaa kwa muda gani kuja kupitisha muswada mwingine mpya ambao tutatunga sheria mpya ya uwekezaji. Kwa hiyo, hii ndio nafasi yetu pekee ya kuishauri Serikali ili kuleta mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, Waziri anapokuja kufanya majumuisho atujibu, aseme ni kwa vipi mapendekezo na hoja zilizoletwa kwenye blue prints na effectiveness zilizoonekana zitaleta tija kwenye muswada huu, mimi sijaona, nilivyosoma vyote sijapata kuona. Kwa hiyo, inawezekana yeye anayo majibu yaani kiasi gani blue print imekuwa accommodated ndani ya muswada ulioko mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye kifungu cha pili cha muswada wa sheria, kinatoa masharti kwamba sheria hii itatumika kwa taasisi za kibiashara zilizokidhi matakwa yaliyoko kwenye kifungu cha 2(2).

Sasa nilivyokuwa nakisoma kifungu kidogo cha pili kikasema; kwa Mtanzania, kifungu kidogo cha (2)(b), Mtanzania ambaye atapewa favor zilizomo ndani ya muswada huu ambazo tunaziita vivutio na atapata tija na ulinzi unaoletwa kwenye muswada huu ni Mtanzania ambaye ataweka mtaji usiopungua dola za Kimarekani 50,000.

Mheshimiwa Spika, dola za kimarekani 50,000 ukizipiga kwa Tanzania shilling ya sasa ni zinakaribia milioni 115. Ni Watanzania wangapi wana shilingi milioni 115 za kuweka mitaji ya kuanzisha biashara mpya ambazo watakuja kuhitaji incentives na huruma zilizoko kwenye muswada huu?

Mheshimiwa Spika, Watanzania wetu wengi hawawezi, hawana mitaji hiyo. Wanaanza wakiwa underground, mitaji midogo, wanaanza biashara from the grassroot, kwa hiyo, ni vigumu kupata unafuu uliotolewa na muswada wa sheria hii na kuna faida nyingi zinaletwa humu kwenye vivutio, kuna misamaha ya kodi, kuna vitu kwenye jinsi ya usajili, ridhaa, leseni urahisi wake wa kupatikana, zote hizo, lakini sasa leo unaenda kuweka kifungu ambacho unasema ili Mtanzania alindwe na matakwa ya sheria hii ni lazima awe kafikisha mtaji wa dola 50,000. Tunaenda wapi? Kwa nini tusiweke kwa Watanzania tupunguze kiwango cha mtaji ili kuwaruhusu Watanzania wengi wanaofanya biashara, hasa wadogo, wawe accommodated ndani ya muswada huu utakapokuwa sheria kuja kuwalinda na kuwapa unafuu.

Mheshimiwa Spika, moja katika industry inayokuwa kwa kasi sana ni mafundi washoni wa nguo (tailoring). Mimi nataka nikutajie baadhi tu ya tailoring marts zinazofanya vizuri sana sasa hivi; moja ni Shine by Catherine ya dada yangu Mheshimiwa Catherine Magige, nyingine ni Carenitho Smart, yuko dada anatushonea yuko nje hapo tu, nyingine ni Better Design ya dada yangu Mheshimiwa Sylvia Sigula, kuna nyingine JM International Collection ni kijana wa Kitanzania, kuna nyingine inaitwa Suti Bega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya miaka mitano mpaka 10 tutakuwa hatuvai tena suti zinazotoka Uturuki wala China, tutakuwa tunavaa suti zinazoshonwa na mafundi wetu Tanzania, kwa sababu imani ya kuwaamini mafundi wetu inakua siku hadi siku. Hii suti niliyovaa hapa imeshonwa na Mtanzania. (Makofi)

Sasa moja katika maeneo ambayo nahisi bado Muswada wa Sheria za Uwekezaji hauwatendei haki ni wafanyabiashara wanaokuwa, wanaojikwamua, hasa hawa miongoni mwao ni hawa ma-tailoring ambao ni Watanzania wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mwekezaji anayetoka nje akija akianzisha kiwanda cha kutengeneza aidha misumari au mabati atapata unafuu wa kuingiza raw materials ya wire rods kama raw materials, lakini Mtanzania anayeshona anaingiza kitambaa kama bidhaa sio raw material. Kwa hiyo, akiingiza kama bidhaa yeye anakinunua kama bidhaa, anaenda kukikata akishone suti, anaanza kukamatwa anaponunua bidhaa, halafu akishashona suti hiyo ikiingia dukani anaanza kukamatwa tena.

Mheshimiwa Spika, sasa maoni yangu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 kengele ya pili imeshagonga.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, sawa ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu ni kwamba lazima tutengeneze mazingira wakati wetu ni huu. Tukikubali kupitisha muswada ambao bado hautoi nafuu nzuri kwa Watanzania wetu tutakuja kukaa tena zaidi ya miaka 15/20 kusubiri jambo hili litokee tena.

Kwa hiyo, naiomba Serikali ichukue jitihada na maoni yetu kuona wanafanyaje kushughulikia jambo hili ili kuifanya Tanzania iwe sehemu nzuri ya uwekezaji. Hayo ndio maoni yangu. (Makofi)