Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mohamed Abdulrahman Mwinyi (4 total)

MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wananchi ambao wamejisajili mwaka 2018, 2019 na 2020 na baadhi yao mpaka leo hawajapata vitambulisho hivyo: Nini kauli ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza wakati najibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kuhusu changamoto hii ya upatikanaji wa vitambulisho nilizungumza kwa ujumla wake na majibu yale yale yanaweza kusaidia kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Mwinyi kuhusu changamoto hii ya upatikanaji wa vitambulisho kwa nchi nzima ambayo inakumba majimbo yote likiwemo jimbo la Chambani.

Mheshimiwa Spika, nilieleza hatua gani Serikali imechukua ili kukabiliana na jitihada hizo. Hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Mbunge aridhie na majibu yale yale ambayo nimeyajibu ambayo yaliainisha hatua ambazo Serikali inachukua kukabiliana na changamoto ya upungufu wa upatikanaji wa kadi kwa wananchi wa nchi nzima wakiwemo wananchi wake wa Jimbo la Chambani.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa kuna vitendo vya uhalifu vinavyojitokeza katika Jimbo langu la Chambani, kama vile uwingizaji na utumiaji wa madawa, wizi wa mifugo na mazao.

Je, nili Serikali itaanza doria kwa kupambana na wahalifu hao?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdulrahman Mwinyi Mohamed, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Abdulrhman Mwinyi kwa kujali utulivu usalama na amani kwenye Jimbo Lake la Chambani. Hata hivyo, kwa kuwa ujenzi wa vituo hivi utachukua muda nitoe maelekezo kwa RPC Mkoa wa Kusini Pemba kuimarisha doria kwenye maeneo korofi ambayo ni pamoja na Dodo, Chambani Pamoja na eneo la Chonga ili wenye vitendo vya wizi wa mifugo na mazao waweze kukoma. Ahsante.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza niipongeza sana Serikali kwa hatua ambayo wamechukua na nina masuala mawili tu ya kuuliza.

(a) Kwa kuwa fecha zilitolewa Desemba, 2022 na mpaka leo imefika hatua ya kusafisha kiwanja hicho, je, ni tatizo gani ambalo linasababisha hilo?

(b) Ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda kuangalia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohabed Mwinyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuhusu tatizo la kuchelewa, ni kweli umetokea uchelewaji baada ya kubaini kwamba utaratibu uliokuwa umewekwa wa kutumia force account ulikosewa na baadhi ya watekelezaji wa jukumu hili. Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alianza mfumo wa kuwaelimisha Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa juu ya mfumo huo unaofanya kazi ili wauzingatie wakati wa utekelezaji, kwa hiyo ndio sababu ya kuchekelewesha. Sasa hivi wote umeshapitishwa ndiyo maana utekelezaji unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kuhusu lini nitakwenda, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunao utaratibu wa kufatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na maofisa wetu lakini na sisi viongozi wa kisiasa tunapata nafasi tunaenda huko. Kwa hiyo itakapokuwa pengine Bunge hili linamalizika kabla ya mwezi Agosti Mbunge akiwa tayari niko tayari kuongozana nae kuangalie maendeleo ya ujenzi huo. Nashukuru sana.
MHE. MOHAMED ABDULRAHAMAN. MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Ofisi ya NIDA ya Wilaya ya Mkoani ni kichumba kidogo sana ambacho akiingia mteja mmoja wengine wanabakia nje wanapigwa na mvua, wanapigwa na jua…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa swali.

MHE. MOHAMED ABDULRAHAMAN. MWINYI: Je, Serikali haioni haja ya kuwatafutia jengo jingine kuondoa adha hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kuna wananchi ambao wamejisajili mwaka 2018, 2019, 2020 mpaka leo hawajapata vitambulisho vya NIDA na wanaojisajili sasa hivi wanapata vitambulisho vya NIDA; je, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwatafutia jengo lingine kwa kweli tunatambua kwamba zipo wilaya zenye changamoto ndiyo maana tumesema zitaendelea kujengewa ofisi baada ya hizi 31 zitakazofanyika kwenye mwaka wa bajeti ujayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwa hali ambayo ameieleza Mheshimiwa Mbunge niombe uongozi wa Wilaya ya Mkoani kule Mwinyi Pemba waone uwezekano wa kuwatafutia, kwa sababu wananchi wanaosajiliwa ni wananchi walewale walio chini ya Mkuu wa Wilaya, chini ya mamlaka zao za serikali za mitaa. Lakini nimuahidi pia tutatembelea huko baada ya bajeti hii ili kuona namna ya kutatua hilo tatizo alilolisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi waliojisajili muda mrefu na hawajapata vitambulisho, tuliahidi hapa Mheshimiwa kwamba mwaka huu tunashukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kutupatia 17,000,000,000 ambazo zilikuwa zinadaiwa na mkandarsi na tumeshamlipa, kinachoendelea ni kuanza kutekeleza kadi ghafi ambazo zilisimama uzalishwaji wake kutokana na masuala ya UVIKO. Lakini tunayo matarajio kwamba ndani ya miezi sita ijayo tunaweza kuanza kupokea na wananchi wake watapokea vitambulisho kama ambavyo vitagaiwa kwa wananchi wengine, nashukuru.