Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Abdulrahman Mwinyi (4 total)

MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI aliuliza: -

Je, ni lini Wananchi wa Wilaya ya Mkoani waliosajiliwa kwa muda mrefu watapewa Vitambulisho vya NIDA?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Chambani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa imeandikisha jumla ya wananchi 47,557 ambayo ni sawa na asilimia 94 ya waliokadiriwa kuandikishwa katika Wilaya ya Mkoani. Aidha, Namba za Utambulisho 45,785 zilizalishwa sawa na asilimia 96 ya wananchi wote walioandikishwa.

Mheshimiwa Spika, jumla ya vitambulisho 41,494 ambayo ni sawa na asilimia 91 ya Namba za Utambulisho vimegawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Mkoani. Aidha, mwezi Septemba, 2022 jumla ya vitambulisho 1,000 vimepelekwa Wilaya ya Mkoani ili vigawiwe kwa wananchi. Serikali itaendelea kuzalisha vitambulisho na kuvigawa kwa wananchi walioandikishwa.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi Jimbo la Chambani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdulrhman Mwinyi Mohamed Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Chambani liko katika Wilaya ya Mkoa wa Kusini Pemba. Wilaya hii ina vituo vya polisi vine ambavyo ni Mkoani, Kengeja, Mtambile, na Mkanyageni. Wananchi wa Chambani wanapata huduma ya polisi kwenye vituo vya Mtambile na Kengeja ambavyo viko ndani ya kilometa sita.

Kwa sasa Serikali kupitia Jeshi la Polisi linatarajia kujenga Vituo vya Polisi maeneo ya vitongoji, Pujini, Wesha na Gombani Wilayani Chakechake ambayo ina kituo kimoja tu cha Polisi katika mkoa wa Kusini Pemba.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukijenga upya Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkoani ni chakavu na halifai kwa matumizi ya kutoa huduma za polisi. Mwezi Desemba, 2022 Serikali ilitoa kiasi cha fedha shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga kituo cha polisi kipya cha Daraja B eneo hilo na taratibu za ujenzi zimeshaanza. Ujenzi unafanywa na Kikosi cha Ujenzi cha Polisi na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti, 2023. Nashukuru.
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN. MWINYI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga ofisi ya NIDA katika wilaya ya Mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Jimbo la Chambani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mpango wa ujenzi wa ofisi za usajili za wilaya kwa awamu. Katika awamu ya kwanza Serikali imejenga ofisi 13 na awamu ya pili inatarajia kujenga ofisi 31 kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024. Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa itaendelea kujenga ofisi za usajili kulingana na upatikanaji wa fedha kwa wilaya nyingine nchini ikiwemo Wilaya ya Mkoani, ahsante.