Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Charles Stephen Kimei (19 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi siku hii ya leo nina afya tele. Pia nishukuru chama changu cha CCM kwa kunipa fursa ya kugombea kwenye Jimbo lile la Vunjo ambapo wananchi wake walitupa kura kwa wingi na CCM ikashinda kwa kishindo, kwa hiyo, CCM oyee.

WABUNGE FULANI: Oyee.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, niseme hivi, mimi niliyesoma hivi vitabu vitatu nasema ni kitabu kimoja ambacho bado kinaandikwa bado hakijaisha na naamini kwamba itakapofika mwezi Juni, 2025 tutaona chapter ya nne na pengine ikimpendeza Mheshimiwa Rais tutaona na chapter ya tano itakayokuwa inatuonesha kwamba dira ya 2025 kwenda 2050 itakuwaje lakini ni kitabu kitamu na utamu wake ni kwa sababu una happy ending, unaishia pazuri.

Mheshimiwa Spika, niliposoma nimeona kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyotoa Novemba 2015 anaanza na mambo magumu sana ya kuunda utawala bora na kutafuta uongozi ambao ungeweza ukapigana na mmomonyoko wa maadili ndani ya Serikali, kurudisha nidhamu na kuhakikisha kwamba mapato ya Serikali yanakusanywa vizuri na yanatumiwa vizuri. Naamini kwamba kwa kile alichokifanya kuunda uongozi ambao aliweza kufanya nao kazi lakini pia akawa anatumbuatumbua mpaka tukaona mambo yamesimama vizuri ndiyo sababu tunasema kwamba kusema kweli ni fundisho kubwa linalosema kwamba maendeleo ya Afrika, maendeleo ya Tanzania yanatokana na uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini uongozi bora siyo viongozi bora ni kiongozi mmoja ambaye anajitokeza, the leader, ana make a big difference katika mambo yote yanayofanyika kwenye nchi au kwenye kampuni inakuwa hivyo hivyo, kama ukiwa na kiongozi bora utaona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nashukuru na nasema kwamba kusema kweli ukisoma kitabu hiki ambacho kinaandikwa hakijaisha natumaini utaona wazi kwamba tumempata kiongozi ambaye anastahili sifa kwa kila Mtanzania. Hata mtiririko wa namna anavyoelezea dira na mkakati wake na malengo yake na milestone za kufikia na namna ya kutathmini utaona wazi kwamba ni kitu ambacho kinaeleweka kwa kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utaona kitu kama hicho hata ukimuuliza bibi yangu pale mgombani kule Moshi wewe ni nani? Anakwambia mimi ni Mtanzania naenda kwenye uchumi wa kati, kipato cha kati na baadaye tutafika kwenye kipato cha juu. Kwa hiyo, kila mtu anaelewa ni kitu gani. Lengo kuu la nchi ni kuinua kipato cha Mtanzania.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake aliyotupa kwenye ufunguzi anasema wazi kwamba sasa amejua kutakuwa na miundombinu lakini hailiwi, lazima sasa tuweze kuwezesha wananchi wetu na wale tunaowaongoza kuongeza kipato chao, wajasiriamali kwa kuwawezesha kupata mikopo na kadhalika ili waweze kuinua kipato chao. Kwa hiyo, nasema kwamba kwa logic ya hiki kitabu kiko vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, nimsifu kwa kitu kimoja, katika nchi ambayo inaenda kwa kasi tunayoona, kasi ya ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia saba kwa wastani, lakini miradi mikubwa inatekelezwa. Utakuta kwamba mataifa mengi yanashangaa kwamba bado tumeweza kuendelea na utulivu wa uchumi mkubwa. Utulivu huo umetokana na umakini wa Mheshimiwa Rais, lakini pia tumpongeze Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wetu wa Fedha na Mipango pamoja na Gavana wa Benki Kuu kwa ushauri mzuri waliotoa. Kwa sababu wangeweza wakachukua njia rahisi ya kufanya inflation finance maana ku-print pesa na kukuza mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wao hawakufanya hivyo, wametumia njia ngumu ya kukusanya mapato kutoka kwa Watanzania, hiyo njia ngumu kuliko ku-print pesa au kukopa tu na ni kweli kwamba hii miradi mikubwa ungekuta kwamba inashawishi watu sana kuchukua mikopo ya ziada, lakini nashukuru kwamba hawakufanya vile wamefanya kitu ambacho ni kigumu, lakini tunaona matunda yake ni mazuri na ndio hapa unasema hapa tunaona kuna happy early.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi tumeona kuna utulivu wa uchumi wa ujumla ndio, exchange rate imekuwa stable, mfumuko wa bei uko chini, riba zimetulia lakini hazijatulia mahali pake kwa sababu ziko juu bado watu wanalalamika riba asilimia 15 inflation asilimia tatu, really interest rate ni kubwa sana. Kwa hiyo, kinachohitajika sasa ni pengine tuhakikishe kwamba tunaendeleza sera hizo za kuhakikisha kwamba riba nazo zinashuka kwenye mabenki yetu. Utaona mabenki yanarekodi faida kubwa sana, mwaka huu kwa mfano, faida za mabenki ni kubwa sana kwa sababu wanatoza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoke hapo niseme hivi, kwa kuona kwamba miundombinu inaboreshwa vizuri, sasa njia ya peke ni kuongeza uwekezaji na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusema kwamba ameunda Wizara ndani ya ofisi yake ambayo inashughulika na uwekezaji. Niseme hivi kwamba private sekta haitaweza kunufaika sana kama blue print aliyoizungumza Mheshimiwa Mwijage haitatekelezwa kwa umakini na kwa haraka zaidi. Inatekelezwa kwa speed tofauti tofauti kwenye kila Wizara, lakini ingetekelezwa kwa speed ile wanayotekeleza kwa mfano Wizara ya Viwanda naamini ungekuta vitu vinabadilika na pengine private sector ingeweza ikaanza kushika hatamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba tatizo kubwa katika sekta binafsi ni kusema kwamba uwekezaji lazima uwe mkubwa sana, kumbe sasa hivi uwekezaji hata kwenye nyumba yako unaweza kwa sababu kuna umeme. Ukishakuwa na umeme unaweza ukawa na kiwanda kidogo cha kuchakata hata ndizi na hiyo ndio njia peke kusema kweli ya kuinua kipato kule kwetu mashambani kwa kuunda viwanda vidogo kwa vikundi au kwa mtu mmoja mmoja ambaye ataweza kuchakata mazao akayaongezea thamani na yale mazao yakauzwa sehemu nyingine ambapo hayapatikani au ambapo yanahitajika kwa wakati ule.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba pengine tuangalie namna gani ya kuwawezesha vijana wetu au wajasiriamali wanawake na wengine na hata akinababa kwa kuwapa exposure. Nikasema exposure haiwezi kutolewa kwa kumpeleka mtu China kuangalia maonesho China hapana, exposure ni kwamba pengine Shirika letu la SIDO lingekuwa karibu zaidi kule kwenye vijiji sasa linashughulika kwa kuona kwamba kweli linaonesha watu kwamba kuna kiwanda kidogo cha shilingi milioni moja au laki tano na hiki kiwanda unaweza ukakitumia mkiwa vijana watano, mkakitumia mkaongeza thamani mkapeleka mkauza. Naamini kwamba hicho lazima kifanyike na naamini kwamba Wizara inayohusika itafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunazungumza mambo ya mikopo, kupeleka watu vyuo vikuu, hii nataka kusema katika uchumi tunaojenga sasa hivi uchumi wa kati, tatizo kubwa ni skills study zile za watu kufanya vitu kwa mkono sio kuwa na degree sio kuwa na ma-Ph.D hayatasaidia sana. Utakuta kwamba unemployment kati ya watu waliomaliza chuo kikuu ni kubwa sana lakini mtu anayetengeneza simu, simu hizi tunazotembea nazo hizi mfukoni ukimtafuta mtaani humpati na wana kazi, mechanic wote wana kazi lakini tatizo moja tunasema tu kwamba elimu yetu inalenga chuo kikuu, hapana! Huko ni kwa zamani, elimu ilenge daraja…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …baada ya kumaliza form six watu wengi waende kujifunza kazi za mikono, study za mikono. Kwa hiyo, vyuo vya ufundi viongezeke…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Lakini na vyenyewe vibadilishe mwelekeo sio kuangalia zile study zilizokuwa zinahitajika zamani tuangalie study za kisasa, electronic base na ambazo…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei pokea taarifa, jitambulishe Mheshimiwa nani.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naitwa Mheshimiwa Musukuma, ningependa kumpa taarifa tu Mheshimiwa Dkt. Kimei kwamba anavyochangia anasema tuache kuamini ma-degree na ma-PhD. Nampa taarifa tu kwamba duniani kote matajiri wengi hawana degree. (Makofi/Kicheko)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa!

SPIKA: Kabla Mheshimiwa Dkt. Kimei hujapokea taarifa hiyo, nisisitize tu Waheshimiwa Wabunge mumsikilize Mheshimiwa Dkt. Kimei hoja yake, ni hoja ya msingi sana. Hii habari kila mwanafunzi anaenda chuo kikuu anasoma vitu vya ajabu ambavyo tumezoea traditionally, sitaki kuyataja masomo, yako masomo yaani ni kama kumpotezea mtoto tu direction. Yalikuwa na maana enzi hizo, lakini leo hii dunia ya sasa, dunia ya uchumi wa kati, ndio hii anayopendekeza Mheshimiwa Dkt. Kimei. Skills na kwa hiyo hata mfuko wa mikopo uelekeze zaidi mikopo yake huko. Mheshimiwa Dkt. Kimei hebu rudia hiyo hoja yako bwana, nakupa dakika tatu. Katibu hebu iweke vizuri. (Makofi)

Waziri wa Elimu amekaa vizuri anakusikiliza sasa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ndio nasema hivyo kwamba, kusema kweli mahitaji ya uchumi wetu wa sasa hivi ni watu wanaoweza kutenda na mahitaji ni kwamba watu wana magari lakini hawawezi kutengeneza, ukitafuta fundi hakuna kwa sababu hakuna mtu anayefundisha vitu hivyo na siyo tena kutengeneza magari ambayo ni ya ajabu, sasa hivi tengenezeni magari ambayo lazima zile shule zetu za ufundi na zenyewe zi-adopt mahitaji ya sasa hivi. Ukienda uka-register wanafunzi utapata wanafunzi utapata wengi sana ukitafuta kwenye electronic base industry na nini utapata, lakini ukienda kwa ile ya zamani kwamba sijui unataka mtu wa kuranda. Tuna chuo cha ufundi pale kwetu Mamba pale lakini hakuna mtu anaenda kwa sababu wana mashine za kuranda wanafundisha kuranda au cherehani za kushona lakini ni zile za zamani sasa hivi kuna cherehani za kisasa.

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema hivi kwa kule kwetu kama anavyosema Mheshimiwa Saashisha, kusema kweli zao la kahawa limedorola sana na nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais aliweka hilo pia katika zao la kimkakati. Hata hivyo, niseme hivi kule Kilimanjaro ile ardhi imeshadidimia haifai tena hata kulima kahawa, utatumia madawa mengi na watu hawajui kutengeneza composite, kwa hiyo unakuta kwamba ile kahawa ukiipeleka kuuza nje tena hupati hata wanunuzi. Halafu bahati mbaya pia vile vihamba vyetu, yale mashamba yetu yamekuwa tragmented mtu mmoja ana robo heka, atalima wapi.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi, sisi Wachaga wengine tunataka tuhamie mahali ambapo kuna ardhi, tukalime huko, mambo ya kusongamana kule haifai na wameniomba wananchi wangu wa Vunjo kwamba jamani ukienda tafuta mahali utakakoweza kutupeleka tukalime tupate eneo tulime na sisi tuwe na tija, tuwe na mabilionea na sisi, lakini kusema kweli kule Uchagani huwezi kuwa bilionea kwa sababu hakuna ardhi. Watu wa kule Vunjo tuna shida hiyo na nitakuja kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, atusaidie.

Mheshimiwa Spika, mwisho, niseme hivi katika rasilimali tuliyonayo sisi kule Kilimanjaro, ni mlima Kilimanjaro na ni kweli wana Vunjo na wengine wote wanaozunguka ule mlima wanapata shida sana. Shida kubwa ni kwamba ajira haipatikani, vijana wengine wanaokuja kupata ajira kule ni kutoka maeneo mengine, lakini hata wale wanavijiji wanaozunguka ule mlima, ile nusu maili hawaruhusiwi kutumia, siku hizi wanapigwa, walikuwa wanasema ni wanawake tu waende huko, sasa wanawake wakaenda wenyewe, baadaye na wenyewe wakanyimwa kwenda huko kutafuta kuni, kutafuta majani ya ng’ombe na mbuzi na kadhalika. Sasa tunamwomba Waziri wa hifadhi naye atuangalizie hilo na ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Spika, mambo ya barabara yameshazungumza sana. Naunga mkono hoja ya kuongeza Mfuko wa TARURA, kusema kweli barabara zetu zina matatizo japokuwa hata zile ambazo zinatakiwa ziwekwe lami zimeahidiwa lami tunazo hizo kama tatu hivi ambazo Mheshimiwa Rais naye alituruhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Naona kengele imelia.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kimei, tunakushuru sana…

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa moyo moja na sisi tutatekeleza kila jambo ambalo liko kwenye hotuba hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa muda huu uliniopa nizungumze. Ninayo mengi kidogo,kwahiyo nitaenda moja kwa moja kwenye mjadala huu. Pia nikupongeze wewe kwa namna ambavyo unatuongoza, kusema kweli inatupa hamasa kubwa sana kuwa Bungeni hapa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba naunga mkono kwa asilimia mia moja Mpango ambao umewasilishwa hasa kwasababu nafikiria kwamba mpango huu una uhalisia kwa kiasi kikubwa. Uhalisia kwamba assumptions zilizotumika kwa mfano ya kusema kwamba tunaweza tukaongeza pato la Taifa mwaka ujao kwa 6.3%,wangeweza wakasema 7%, lakini wamesema 6.3%, naamini ni achievable kwasababu ya misingi ambayo tumeijenga. Naamini kwamba kuna mambo mengi ambayo yanaweza yakatuteteresha kwasababu hatujajua dunia ina kwenda wapi kwasababu ya wingu ambalo bado lipo kuhusiana na corona kwenye nchi za nje, lakini naamini endapo hali itabadilika kidogo tunaweza tukafikia hiyo 6.3% kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana pia wastani wa 8% utafikiwa mwishoni mwaawamu, lakini inawezekana pia hata 7%, ni nzuri sana kwasababu wale wanaojua kanuni ya ukuaji cumulative(limbikizo la ukuaji)wanaita ni the low ofcumulative growth. Kama unaongeza pato lako kwa asilimia 6.0 kwa mwaka unaweza uka-triple hiyo kwa miaka siyo zaidi ya miaka 10. Kwahiyo naamini kwamba tunaweza tukafikia hiyo nanihi yetu ambayo ni pato la uchumi wa kati, kiwango cha juu.Kwahiyo naamini tupo sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nakosa tu kwenye huuMpango, nilikuwa natamani sana nione mipango ambayo imekaa fungamanishi kama kwa mfano ulivyokuwa mpango wa SAGCOT ambao unaeleza vitu vingi ambavyo vinasaidianaili kuhakikisha kwamba ile corridor inatoa kitu. Sasa kuna mipango kama huo wa SAGGOTambao naamini kwamba bado uko unatekelezwa. Nilikuwa nataka tuone kamalogisticsmapaulogistics plan za kufanya Tanzania hususan Dar es Salaam kuwa ni logistichub ya nchi hizi ambazo zinapakana na sisi, lakini sijauona vizuri. Ndiyo tunajenga vizuri infrastructure ile ya kutufungulia mipaka na kupeleka vitu kwenye mipaka na tuweze kupata a lot of value additions, lakini bado naona haijafungamanishwa sawasawa,ili kuona zile corridor tulizonazo zote zitatusaidia namna gani kuongeza kipato chetu bila kutegemea sana vitu vingine ambavyo ni more primary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba wengi wanasema kilimo, kusema ukweli ni kizuri, lakini nataka kuwatahadharisha kwamba Mheshimiwa yuko sahihi anaposema kilimo hakilipi kama hatuna viwanda. Bado watakaoweka bei kama tutawauzia primary product watakuwa bado ni walaji wa kule nje, ni walaji wa Ulaya na wanapoona kwamba tunataka kufanikiwa watazidi kutubana, watasema bei ziko hivi bei zitaanza kutuvuruga, kwahiyo njia tu pekee ya kuweza kuhakikisha kwamba beiya mazao yetu inaimarika ni kuhakikisha kwamba tuna-process, tunauza kitu ambacho kinaweza kikahifadhiwa, kikafika kwenye masoko tofauti tofauti kwa bei ambayo siyo ile inakuwa dictated by the consumers. Kama consumers ata- dictate bado utapata matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kama ninavyosema kilimo lazima tunapokizungumzia tuseme tutafanyaje tukiunganishe na viwanda ili kiweze ku-process. Niseme kwamba tumezungumza mambo mengi kuhusiana naukuaji nakadhalika, lakini ni lazima tuzungumzie strength. Watu wanapotengeneza plan yoyote unaangalia strength zako ni nini na ni sawa tukasema ni uongozi bora, amani, utulivu, mshikamano na vitu vyote hivyo na siasa safi, lakini kitu ambacho hatujakiona ni ile strength tuliyojenga kwa kutuliza uchumi wetu ukawa tulivu ambao mfumuko wa bei upo chini, wenye exchange rate ambayo ni nzuri nakadhalika ambayo inatufungulia milango ya kuweza kuisaidia Serikali yetu kuweza kukopa kwa bei nafuu kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa MWENYEKITI,tunapoangalia mipango hii mara nyingi tunajua tunatumia cash budget, sasa tukianza kuzungumza mpango kwa kuanzia kwenye matumizi kwa kuorodhesha vitu gani tunataka vifanywe, kwanza niseme naomba Mungu ajaalie kwamba pamoja na mafanikio tuliopata kwenye miundombinu, kule Vunjo wamesahau. Naomba wasisahau zile barabara zetu kule Vunjo,lakini kama tutaorodhesha kila mtu aorodheshe vitu, the shopping distance is huge,TARURA inataka pesa,TANROADs inataka pesa, halafu bado wengine wanasema Serikali ijenge viwanda, hili hapana, Serikali haiwezi kujenga viwanda, zaidi Serikali iwezeshe kwenye viwanda vya kimkakati ambavyo tunatakiwa Serikali kama tunavijua kwenye maelekezo ya hotuba za Rais. Hiyo ya kuwezesha viwanda vya kimkakati hata kama ikiingia ubia lakini kuhamasisha, sera ziwe safi,blue print iwepo, mambo yawe sawasawa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,kusema kweli hatuwezi kusema Serikali ikajenge viwanda vya alizeti nakadhalika hatutaweza hiyo, tuwezeshe watu na ndiyo kazi yetu kwenye zile kamati ambazo zinahusika. Kwahiyo nataka kusema hiyo tuwe makini,kwasababu hatuwezi kuorodhesha. Nimejifunza kitu cha msingi sana na nimefurahia sana Wabunge fulani wameanza kusema kwanini tusipate fedha namna hii. Kwasababu cha kwanza ni mapato, je, yanatoka wapi? Kuna Mheshimiwa Shabiby alisema pengine mapato tuongeze tozo kwenye matumizi ya mafuta na tena akatoa pia mawazo ya namna hii, yale ndiyo mambo tunataka tujue kwasababu ukishapata zile fedha ukimpa Rais wetu anazitumia vizuri, anajua kuzisimamia kwa ufanisi,zitazaa vyovyote tunavyotaka, lakini tuangalie na nashukuru wale wanaozungumzia kwamba tuzibe mianya ya pesa kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tax effort yetu we mention kwenye hizi documentis 13%,12.9% ndiyo revenue effort tuliyofanya mpaka mwaka jana na tunaendelea kusema mwaka unaokuja 13.3% ndiyo tax effort, nchi nyingine hata hapo Kenya 23% ya GDP, uwiano kati ya mapato ya Serikali na GDP, pato la Taifa ni 20%, sisi tunasema 13% ni ndogo sana, ina maana kwamba njia tunazotumia kutoza kodi na njia tunazokusanya mapato yetu ni finyu. Aidha, vile vyombo vyetu vinavyoshughulika na ukusanyaji wa mapato vijiunde upya vi-think out of the box, what is happening?Effort yoyote Mheshimiwa Rais aliyofanya kupata hela kwenye madini na nini lakini bado eti revenue effort 13% ofGDP isnothing, tunataka tupate 20% whichmeans tunapata 28 trilioni, tunge- finance vitu gani? TARURA ingepatapesa mpaka tushindwe kuzungumza, lakini ninavyoona ni kwamba kuna kitu kiko hafifu hapo katikati kwenye ukusanyaji, sijui zinaenda wapi hizo hela. Kwanini iwe 13% au sisi tuna overstateGDP yetu pengine I do not know, lakini kama kweli takwimu ziko sahihi 13% ni ndogo toka tukiwa kule sisi miaka ya 1996, kwahiyo tunazungumza kwamba effort yetu lazima ifikie 20%, sasa mpaka leo hii 13%, tuna matatizo lazima tuanzie hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema tuna-demand barabara na vitu vingine, je, mapato yanatoka wapi? Kwasababu hutapata kule kwenye Wizara ya Viwanda wanapata 6%, kilimo wanapata 6% of approved budget, it willnever work. Kwasababu hiyo tuna over state hizi revenue ndiyo sababu tunapanga vitu ambavyo ni hewa,havitatekelezeka,where is the money?The money is the cash budget, sasa niseme hivi kwanini nimeanza kusema kwamba tuna strength moja ya kukopesha. Revenue ya Serikali ya matumizi inatokana na vitu viwili taxrevenueyaani mambo ya kodi na tozo; pili, mikopo. Sasa mikopo inaweza ikatokana kwenye mabenki ya ndani napensionfunds nakadhalika yaani vianzio vya ndani, lakini pia zinaweza zikatoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nje na tunaambiwa kwamba nanii yetu iko chini sana, yaani uhimilivu wetu wa ukopaji bado tunaweza tuka-affordhata mara tano, sasa kwanini tusikope zaidi, tunaogopa nini kukopa kwasababu tunajenga rasilimali, tunajenga mtaji, nchi hii ina balance sheet yake,liabilities and assets. Watu wanaposema sijui deni hili siyo himilivu, deni walikuwa wanapiga ile gross hawaondoi ile rasilimali tuliyotengeneza,assetskwahiyo lazima uchukue asset - liabilities unapata net liability au netasset.

Sasa sisi ukiangalia kwa mfano vitu ambavyo vimejengwa Awamu hii ya Tano thamani yake na deni letu, ni kama hatuna deni yaani ukiangalia kwa uhimilivu watu wa Taifa letu,uhimilivu wa balance sheet ya kwetu,network yetu ni nzuri kwasababu tumekopa tumeweka kule, hata kama tungekuwa tumekopa mara ngap,i tutaingiza kwenye asset inazaa vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie…

MWENYEKITI: Tayari ni kengele ya pili.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Sasa nina mengi sana, lakini...

MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI:Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.(Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na napenda kwanza nimshukuru sana na nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake pamoja na Kamati ya Bajeti kwa namna ambavyo wamewasilisha Mpango huu. Natumaini wote imetufurahisha. Nataka nianze kwa kusema kwamba naunga hoja yake mkono, japokuwa nitakuwa na maoni mawili au matatu ili kuweza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hivi kwamba kusema ukweli kwanza tunawapongeza pia Wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuweza kutuwekea uchumi wetu kwenye hali ya utulivu. Tunajua kwamba ukuaji umekuwa mzuri sana, hata wakati huu wa covid, lakini pia mfumuko wa bei uko chini, uko vizuri, japokuwa namuunga mwenzangu mkono aliyezungumza kwamba pengine asilimia tatu ni ndogo sana, inatunyima fursa fulani ya kuweza kukuza zaidi kwa kuipa Sekta Binafsi na wale wanaouza, nafasi ya kuona faida watakayopata wakiendelea kuzalisha Zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona kwamba hali ya deni la Taifa ni himilivu. Pili, tunaona pia kwamba thamani ya shilingi yetu iko vizuri na pia tuna International Reserves ambazo ni nzuri. Hiyo ina maana kwamba ni strength kubwa sana ambayo tunaweza tukaitumia tukafanya assessment ya nchi yetu kwa athari ya wawekezaji na hivyo tukaanza kukopa kwa riba ya chini sana. Riba ya asilimia tano au sita unaweza ukapata kwa mfumo huo wa infrastructure bond au pia kwa kukopa moja kwa moja kwa direct placement ya bond yetu kwa wale wanaotaka kuwekeza Tanzania kwa sababu Tanzania imekaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwamba hakuna sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi elekezi. Hii miradi tunasema ya vielelezo kama SGR na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere wakati tunaweza tukakopa, tukahamasisha na tukafanya haraka haraka tukaanza kuona matunda kutokana na miradi hii mikubwa ambayo itatoa chachu katika ukuaji wa Taifa letu. Nataka niseme kwamba tutumie hiyo kama fursa, kama ni strength na hiyo strength tuweze kuitumia kuweza kufanya mchakato huo wa kuweza kwenda kwenye soko la Kimataifa na kukopa na tusizingatie sana kukopa ndani kwa sababu tukikopa ndani maana yake tunai-crowd out private sector. Watu binafsi hawawezi kwenda nje kwa sababu hawajulikani, lakini Serikali inajulikana kwa sababu ni Serikali na Serikali is as good as gold.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukihamasika sisi Serikali tukakopa nje, tukaacha resources za ndani zinakopwa zaidi na watu binafsi, kwanza riba zitakuwa chini. Sasa hivi tuliambiwa kwamba riba nashangaa kwamba licha ya vigezo hivi vizuri vya uchumi, riba bado ziko kwenye asilimia 15. Nimekutana na watu wa BOT walituambia kwamba kwa sababu tunakopesha Serikali kwa asilimia 15, sio kweli! Serikali inalipa asilimia 15 kwa bond ya muda kati ya miaka 15 na 20, lakini Benki zinakopesha mikopo ya mwaka mmoja mpaka miwili sanasana pengine ni michache sana kwa miaka zaidi ya hapo. Sasa wakikopesha kwa asilimia 15 ni kubwa sana ambapo Serikali ikikopa kwa kipindi hicho kifupi riba inakuwa ni kwenye asilimia chini ya 10. Kwa hiyo unaona kwamba kuna uwezekano wa kushusha hizi riba kwa kuwezesha Sekta Binafsi kukopa zaidi na hivyo kuwezesha Sekta Binafsi kuwekeza na tukaona matokeo ya Mpango wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kitu kimoja ambacho nimekisikiliza hapa. Tunafanya mambo kimazoea mazoea sana, yaani tatizo la sisi Waafrika pengine ni kwamba tunaanza kuzalisha halafu ndiyo tunatafuta soko. Kumbe uzalishaji unatakiwa uanze sokoni, unatafuta soko liko wapi. Ukishaona soko liko wapi na bei zake zikoje, ndiyo unasema sasa niki-incur au nikitumia gharama hizi kuzalisha nitapata faida, lakini mtu anazalisha ndizi heka 20 halafu zimeshaiva, anasema anatafuta soko liko wapi, hamna soko lolote namna hilo, huwezi kupata na mtu akijua unazo ndizi zinaoza anakupa bei ya chee! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze kufanya biashara kitofauti kwanza tufanye utafiti tujue kwamba ni kitu gani kinauzika wapi. Tunapoendelea kulima, tunazungumzia mazao haya ya asili siku zote, pamba, kahawa, tumbaku. Hivi tumeshajiuliza ni wapi masoko haya yakoje duniani kwa sasa hivi? Bei za huko mbele za kahawa zinaenda wapi, bei za tumbaku zinadidimia na tunaendelea kusema tumbaku na kadhalika. Ukweli tukifanya tathmini sahihi tukajua kwamba ni kitu gani cha kuzalisha hapa kwetu, sio lazima iwe ni mazao haya tunayoona, tumeona kwamba tulivyowaambia Wachaga kule kwamba hawa jamaa wenzetu wa Kyela wanalima avocado halafu wanapata kilo moja shilingi 1,500; kila mtu anatafuta mbegu ya avocado, huna haja ya kumtafutia mbolea, anatafuta mwenyewe kwa sababu anajua kwamba ina faida kulima avocado.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa na taarifa hizo lakini ukweli ni kwamba taarifa hizi hazimfikii mkulima, tunakaa na hizo taarifa, hujui kwamba unaweza sasa badala ya kulima kahawa ukalima avocado, kwa nini? Ukiendelea kulima kahawa kwenye ule udongo wa kule kwetu umeshakwisha kabisa kwa sababu umelima kahawa miaka 40 au 50, kwa hiyo hauna tena rutuba na hauna tija. Kwa sababu hauna tija badilisha uzalishe linguine, baada ya muda mwingine unaweza ukarudia tena kahawa na ndiyo mambo ya crop rotation, wale wanaojua mambo ya kilimo. Kwa hiyo naweza kusema kwamba pengine kuna haja ya kusema kwamba ni eneo lipi nibadilishe zao lile, kama kule Uchagani kahawa haiendi tena, pengine twende upande wa avocado na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine pia unaona kwamba unatumia gharama nyingi kwa sababu ule udongo unatakiwa ufanye rotation, uzalishe kitu kingine. Naamini kwamba tunaposema tutafutiane masoko, cha kwanza ni hizo taarifa na hizo taarifa sasa hivi ni kielektroniki, tufungamanishe masoko yetu. Mtu hajui kwamba kama nina ndizi, Mbeya wananunua namna gani ndizi, Moshi wananunua namna gani, Nairobi wananunua namna gani kwa kutumia hizi gadgets zetu za mawasiliano hizi ambazo zinatupa bei kila mahali duniani virtually unaweza ukajua kila kitu kinauzwa namna gani. Kwa hiyo watu watajua bei zake na sio lazima ukutanishe mtu physically, unaweza ukakutanisha watu kwa mawasiliano haya tuliyonayo na hiyo ni bei nafuu ya kukutanisha watu, ni bei nafuu ya kumpa mtu tija ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi, mimi nafikiri kwamba katika huu Mpango wetu, suala zima la ushirikishi, kujenga uchumi shirikishi na uchumi shindani. Issue iliyopo ni kwamba tutafanyaje vijana hawa wapate ajira na hawawezi kupata ajira bila kujiajiri wenyewe sasa hivi kwa sababu watu ni wengi ambao hawana ajira na hawataki kuingia kwenye kilimo kwa sababu kilimo hakina tija na kwa sababu hawajafundishwa namna ya kulima kwa tija au kwa faida. Kwa hiyo naomba hivi, kwamba pengine umefika muda sasa tujaribu kutengeneza mfumo wa kuwa-organize vijana kwenye vikundi na kuwaonesha namna gani ya kutengeneza mashamba yenye tija, kutengeneza viwanda vidogo vidogo vyenye tija na mtu asifikirie kwamba kiwanda ni kiwanda cha Mchuchuma, hapana. Tena sasa hivi hata kuzungumza mambo ya chuma ni kitu tofauti kidogo kwa sababu dunia haiendi kwenye mambo haya, inaenda kwenye software zaidi sasa hivi, kwa hiyo Sekta ya Huduma ndiyo itakuja kuwa ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Huduma maana yake ni sekta ya kuhudumia viwanda, kwa sababu ukiwa na kiwanda lazima kihudumiwe, maintenance na kadhalika. Sasa kama wewe unakimbizana tu hiki unasahau kule, haitawezekana, lazima tuingize fedha, lakini ili vijana waweze kufanya hivyo wanahitaji mtaji, mtaji unatokana na nini? Tunasema tutawapa vimikopo vidogo dogo kwenye halmashauri, haina kitu hiyo! Tuunde ile Mifuko ya Serikali ambayo imetawanyika kila mahali, tuunde National Credit Guarantee Scheme or Fund au kuwe na misingi ya kibiashara lakini nafuu ambayo itakuwa imewekwa na Serikali ili watu wanaotaka mikopo wanajua tunaenda pale ambapo kutakuwa na kitengo cha wakulima, vijana, vinakaa mahali Pamoja. Pia unaweza uka-leverage ile guarantee scheme ikazalisha maradufu kwa sababu kama default rate kwa mkopo, hiyo iliyotoka kwa vijana pengine ni only ten percent ina maana kwamba ukiwa na mkopo wa ku-guarantee watu 100 unazidisha mara 10, uta-guarantee watu mara 10 yaani kiasi cha fedha mara 10. Sasa hivi unatumia kile unam- guarantee mtu mmoja ambapo tunaweza tukapeleka kwenye guarantee fund tukawapa watu wakaendesha kibiashara, tukaweza kuwezesha watu kupata mikopo kwa wingi na mitaji kwa wingi kwa muda mrefu na muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, mimi ni muumini wa masuala ya kwamba, kilimo cha sasa hivi ni lazima kibadilike na kubadilika kwa kilimo hicho ni lazima tusifanye mambo ya mazoea, tujaribu kuona ni kitu gani kitaoteshwa wapi na wakulima wapewe taarifa za masoko ambayo ni sahihi. Kwa kumalizia niseme hivi, ili tuweze kuongeza lile fungu la kukopesha au kuwezesha watu kupata mitaji, lazima tuunde National Credit Guarantee Fund or Corporation ambayo itashughulika na Mifuko yote na ile fedha inakaa mahali pamoja na inatumika kwa faida ya wengi. Hapa nataka kukuhakikishia kwamba inaweza ikawa ni kubwa kuliko Benki zote hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona na kunipa fursa hii nichangie kwenye mjadala huu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameanza kazi yake vizuri, amerejesha amani na matumaini mapya kwa watu wengi. Lakini pia kwa kuzingatia kwamba ametuambia tunaendeleza yale yaliyoanzishwa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, na tunaamini pia kwamba kwa jinsi ambavyo tunmfahamu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ataongeza hata ile kasi ambayo tunaipokea.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwamba kielelezo kikubwa cha kuonesha kwamba kweli Mheshimiwa Rais wetu anatekeleza kama anavyoahidi ni timu ya Mawaziri aliyoweka kumsaidia yeye, akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye amekuwa ni kichocheo kikubwa na naamini kwamba ataendelea na kasi ileile, ataendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa namna hiyo lakini pia na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliyechaguliwa, naamini wote ni watu poa kabisa, siyo poa, ni bomba kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naamini tukiangalia timu iliyopo mtu anapokwenda kwenye kiwanja cha mpira unaangalia kwamba amebeba timu gani na yeye ameingia kwenye uwanja huu akiwa amebeba timu ya Yanga au ya Simba? Ya Yanga tuseme, lakini itabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hivi; nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uwasilishaji wake mzuri, wa kina na unaoeleweka, ripoti ambayo imeandaliwa kweli kitaalam na ina-cover kila kitu ambacho mtu unataka kuona. Lakini nimpongeze zaidi kwa jinsi ambavyo amesimamia shughuli za Serikali kwa miaka hii yote ya Awamu ya Tano na mwaka huu ambao tumeanza na jinsi ambavyo amejitoa kutembea kwenye maeneo mbalimbali, na nina matumaini kwamba kule kuona kwake kumesaidia sana kusukuma utekelezaji wa miradi na mikakati ambayo ilikuwa imewekwa mbele yake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimpongeze na niseme kwamba tunaamini na mimi naamini kwamba hatasahau kutembelea Vunjo. Na ninaamini pia kwamba Mheshimiwa Rais kule Vunjo hatujaona viongozi wa kitaifa wa kubwa kwa miaka mingi, takribani miaka saba – naamini tutaanza kuwaona pia kule wajue kwamba kule pia sisi CCM tumejipanga vizuri na tumejipanga kwa safu ambayo italeta maendeleo kwa jimbo letu sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe na Naibu Spika kwa jinsi ambavyo mnatuweka pamoja na kutupa fursa na kujua ni yupi aseme saa ngapi na kadhalika. Nawapongeza sana, naamini naona ufahari sana.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kwamba huu utani wa darasa la saba na maprofesa siyo mzuri sana. Kule nilikotoka mtu anajulikana kwa kazi na umuhimu wake na wote tuna kazi moja ya Ubunge, hatujuani kwa elimu tulizonazo na elimu tulizonazo hazina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapofika hapa tupeane heshima kwamba wewe uko darasa la saba au gumbaru umetoka huko we don’t care unajua kusoma na unaweza kuchangia vitu vizuri. Naamini kwamba sisi kila mtu ana nafasi yake lakini tusianze kuingiza utani, utani huo ni mzuri lakini, hasa Mheshimiwa Musukuma akiwepo…

SPIKA: Haya, sasa endelea na hoja Mheshimiwa Dkt. Kimei.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Endelea na hoja iliyopo Mezani.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, niache Mheshimiwa.

SPIKA: Ukiwachokoza nawajua hawa, endelea tu Mheshimiwa Dkt. Kimei. Ukiwachokoza darasa la saba utatafuta mlango wa kupitia.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nawafahamu, nawafahamu sana. Nawafahamu na ninawapenda sana lakini…

SPIKA: Maana yuko Rafiki yangu mmoja, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, alikosa kuona mlango wa kupitia baada ya kuwagusa darasa la saba. Ndiyo maana nasita, usije ukawagusa huko Vnjo watakuvunja mguu, endelea tu na hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, darasa la saba waache.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Niseme hivi; kuna jambo moja ambalo linatakiwa liangaliwe kwa ujumla, hasa kwenye hii nyanja ambayo inahusiana na mambo ya uajiri wa wafanyakazi serikalini na kadhalika. Ni suala zima la kutathmini skimu ya mishahara ili kuiweka bayana ili mtu kama ni profesa atake kukaa kwenye uprofesa wake. Lakini ukweli ni kwamba mtu anafuata pale penye maslahi, lakini kuna wengine tunakuja hapa kwa sababu tunataka kutekeleza mambo fulani fulani kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, na ninataka kusema kwamba ninashauri kwamba skimu ya mishahara iangaliwe ili stadi zile ambazo ni rare professions na kadhalika na ambao tunataka wabaki kule kwenye specialties zao waweze kufanya utafiti, walete innovation, wasaidie nchi hii kwenda forward professionally, tuweze kuwabakiza kule zaidi kuliko kuwatoa na kuwaleta kwenye siasa na kuwavutia kwa sababu huku kuna maslahi mazuri mengine, lakini naamini kwamba tutaangalia hili ili mambo yawe vizuri zaidi na watu wakae kwenye professions. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninataka kuchangia kwenye maeneo matatu; eneo la kwanza kabisa ni eneo la utawla bora, utawala bora unaendana na span of control. Sasa imekuwa kwamba kuna halmashauri nyingine ambazo ni kubwa sana, zinaweza zisiwe kubwa sana kwa maeneo lakini kwa wingi wa watu.

Mheshimiwa Spika, sasa kama halmashauri ni kubwa sana, zaidi ya watu laki tatu, inakuwa ni ngumu sana kusema kweli halmashauri ile kutenda kwa kuwafikia watu ambao tunataka tuwafikie kwa karibu, tuwapelekee elimu ya uwezeshaji na tuwasaidie kwa kuwaonesha kwa vitendo. Lazima halmashauri hizi zinagaliwe ili kama zinaweza zikapangwa kivingine zipangwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais Hayati wetu, mpendwa wetu, JPM, alipokuja kwetu alisema kwa mfano tuwe na Halmashauri ya Himo, alikubaliana na hilo. Na ninaamini kwasababu naunga mkono mambo mengi nasema Mungu atujalie na Mheshimiwa Rais wetu mpya, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aweze kukubali pia twende na Halmashauri yetu ya Vunjo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nataka nizungumzie suala la Kamati ya UKIMWI kudhibiti UKIMWI. Naomba hii ijiongeze kidogo na kuhusu la gonjwa la COVID, ninaomba hii Kamati iingize masuala hayo kwenye mchakato wake ili tuweze kujua tunapoendelea huko mbele na tuweze kudhibiti, siyo tu UKIMWI, kwasababu UKIMWI naamini tumeshaanza kuu-contain na mtu ambaye kweli amejipeleka hovyohovyo natumaini ni... lakini ukweli UKIMWI kwenye rate ya three to five percent siyo mbaya, at least tunaweza tukadhibiti. Lakini naamini kwenye magojwa haya mapya yanayojitokeza, hasa COVID, pia tuangalie.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, niseme kwamba kwenye suala zima la COVID Private Sector Foundation ilitoa mchango wake, ilifanya utafiti wkae kuhusiana na athari na ninaamini kwambs Serikali itaendelea kusoma na kuona mapendekezo gani yalifanyika hususan kwenye sekta ya utalii, kwamba sekta ya utalii iliathirika sana na ukiwaambia kwamba walipe tozo zile walizokuwa walipe NGOs fees ambazo ni fixed, waendelee kulipa wakati hawajawa na watalii, zitakufa. Hawataweza kuendelea. Kwa hiyo, tukasema kwamba wale waangaliwe kwa namba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na siyo sekta ya utalii tu, na sekta nyingine pia zimeathirika lakini ile ripoti najua ilikuja Serikalini na tunaomba kwamba Serikali iisome tena ione kama inaweza ikaitumia ili kuweza kupunguza makali ya gonjwa hili. Kama kwetu halipo limekuwa nje kwa hiyo, limeathiri wale wateja wet, na kadhalika. Lakini nataka kusema kwamba ni lazima tuangalie namna ya kusaidia watu.

Mheshimiwa Spika, suala la uwezeshaji. Uwezeshaji naamini kila Mbunge hapa amejipanga kwa namna moja kwasababu hii miundombinu tunayoijenga haitakuwa na maana kama haitatumiwa kuzalisha, na ndiyo sababu moja nasema lazima tuangalie kwamba tumejenga barabara, ni kitu gani kimetokea hapo kwenye barabara.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na Central Corridor Programme ambayo ilikuwa isaidie ku-develop vitu fulani fulani along the central corridor ya railway na ile railway baadaye iweze kuwa na tija zaidi na watu wengi wanavutiwa na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwezeshaji ni jambo la msingi lakini kuna masuala ambayo lazima tuyaangalie. Kwanza ishu ya finance kama alivyosema mwenznagu, kwamba mtaji ni kitu kikubwa. Sasa mitaji tunayotegemea, kwa mfano ukiwa kwenye halmashauri, haijawa revolving fund, mtu anachukua mkopo lakini ukiuliza ni mingapi imerejeshwa kwenye halmashauri wale waliokopa utakuta kwamba urejeshaji ni very low.

Mheshimiwa Spika, ndiyo sababu inakuwa kila mwaka lazima uingize hela mpya na ukiuliza leo hela ya kukopesha ni ngapi watakwambia ni ile waliyopokea mwaka huu, hawakwambii ukichanganya na ile ambayo tumekopesha mwaka jana ikarudi na hii ambayo leo imetolewa tunaweza tukakopesha mara tano, haijatokea namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, ni kwasababu kuna weakness kwenye level ya halmashauri kutoa ile mikopo, ile mikopo inatolewa na watu ambao kwanza ni wale maafisa maendeleo wako wachache, hawana staff wa ku-follow up, hawashirikishi sana watu wa kwenye vijiji. Kwa hiyo, ikiwa kama mtu amechukua mkopo ijulikane anatumia kwa njia ya uzalishaji na kadhalika, kwa hiyo inatokea kwamba yule mtu anayechukua hela hawezi hata kuitumia vizuri na anakuwa hajaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kwamba ni vizuri hizi hela halmashauri…

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kimei, tunakushukuru sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru sana kwa hotuba nzuri iliyosheheni mikakati mizuri ya kuboresha na kuinua sekta ya kilimo. Naamini wakipata fedha hizi ambazo zinaombwa basi wataweza kutubadilishia sura ya kilimo na pengine tutaona tija ikiongezeka kwa kasi katika sekta hiyo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa mtizamo wa kinadharia kwamba, duniani kote tija kwenye kilimo inaongezwa kwenye nchi zote tija inaongezeka kuliko idadi ya watu, watu wanaongezeka kwa asilimia mbili au chini ya asilimia mbili wakati tija kwenye kilimo, kwenye mataifa takribani yote inaongezeka kwa asilimia siyo chini ya saba.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kwamba kutokana na hilo ni kwamba tunachangamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba bei za wakulima zitapanda, haziwezi kupanda ikiwa kwamba supply inaongezeka kuliko demand. Na pili hili linajitokeza hapa kwetu pia kwamba mwaka ambapo tumepata neema ya mvua zao likawa kubwa, mahindi walikuwa wanasema bei za mahindi zinashuka kwa zaidi ya nusu inashuka by more than fifty percent na nyingine hata thirty percent ya mwaka ule ambapo kumekuwa na changamoto za uzalishaji inashuka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, na kwamba mkulima anajaribu sana anatumia gharama nyingi lakini inapokuja kuuza kwa sababu ni cobweb theory iko hapo inaitwa cobweb theory inakuwa kama mkulima hawezi kuwa tajiri. Kwa hiyo, njia pekee ya kuweza kuwa wakulima wenye kupata utajiri ni lazima tujitofautishe na wengine duniani tujue kwamba ni zao lipi ambalo likizalishwa lina soko. Kwa mfano, tukiweza kuwahamasisha watu kutumia organic crops tukaweza kuotesha bila kutumia nanii sana unakuta kwamba bahati nzuri ndiyo unapata bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, unatofautisha zao lako na la wengine duniani iwe Kahawa iwe chochote kile lakini organic ndiyo kinatafutwa, lakini pia kuna mazao kama maparachichi/avocado hizi ambazo pia na zenyewe zinaweza kupata demand kubwa ni vitu vya kuhamasisha tusing’ang’anie vilevile vya zamani, tusing’ang’anie tu mahindi tung’ang’anie vitu ambavyo tunaweza tukauza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajazungumzia masuala mazima ya horticulture, mboga mboga, matunda na vituo kama hivyo ambayo kweli unaweza ukaotesha mara tatu, mara nne hasa ukiwa na umwagiliaji ukaotesha throughout the year na ukawa tajiri. Lakini nataka kusema kwamba hilo ni jambo ambalo lazima walivalie njuga kwa sababu linahitaji mkakati ambao ni endelevu ili tuweze kulitekeleza hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine watu wameonyesha changamoto sana kwenye ushirika lakini nataka niseme kwamba, nadharia ya ushirika inabakia palepale ni nadharia nzuri hatuwezi kuwasaidia wakulima bila kuwa na ushirika. Tatizo la ushirika ni nini? utawala bora na hiyo lazima sheria hii ya ushirika ibadilishwe ili kuwe na udhibiti zaidi kwa wale wanaochaguliwa kuongoza taasisi hizi, waweze kutoa mrejesho kwa kuwa na financial statements zinazotoka na zinaenda kwa wanachama wake na wanazijadili na wale viongozi wanaoshindwa wanatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri hilo ni jambo la msingi na matatizo yote bila Serikali kujikita na Mrajisi ile Ofisi ya Mrajisi kuwa na uwezo hatutaweza kuleta nidhamu kwenye ushirika na kila wakati tutasema kwamba ushirika ni wezi na nini lakini wataendelea kuiba kama hawana udhibiti wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna issue ya skimu za umwagiliaji, kule kwetu kuna skimu ya Kahe hasa ile ya Mawala kule kunachangamoto sana na naomba kwamba kusema kweli tumeorodheshewa nyingi kwenye kwenye kiambatisho tuliyopewa na Mheshimiwa Waziri, lakini naamini kwamba kuna ambazo ni kubwa na zinahitaji marekebisho makubwa haraka sana na hasa hii ya kwetu za Kahe kule ndiyo tunazalisha, Kilimanjaro hatuna Mpunga isipokuwa sehemu hizi za Kahe.

Mheshimiwa Spika, naomba pia tuangalie mambo mengine kwa mfano kuwezesha wakulima kupitia constituency au ward mechanization centers tusiseme kwamba tunawasaidia wakulima kwa kuwapa mmoja mmoja lazima tuwe na center moja ambayo itachukua na vifaa vile mtu anaweza akakodisha kwa bei nafuu au akakodishiwa bila kuchajiwa mpaka akaja akakatwa wakati anapouza mazao yake.

Mheshimiwa Spika, lakini ni vigumu mkulima kununua trekta na mwisho waziri amezungumzia hili la kuongeza mitaji kwa wakulima. Lakini nafikiri badala ya kuwapa fedha tuwape lease arrangement ambapo yaani wanapewa mashine halafu wanalipa polepole wanapoendelea kuuza vifaa vyao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kufirikia hilo la kwamba financing ni kitu cha msingi na naona amesema anaunda kamati ambayo itamsaidia kufirikia zaidi namna gani wakulima wapate mikopo ya riba nafuu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa nafasi hii. Mimi pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuja na bajeti yake ya kwanza nzuri sana. Nampongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu wake na uongozi wa Wizara kwa ujumla kwa bajeti hii ambayo kusema kweli imezingatia maoni ya Wabunge pamoja na maoni ya wadau wengi na ninaamini kwamba imewafurahisha wananchi kwa ujumla katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu makubwa ambayo siyo sana ya kutaka kuingia ndani in detail, lakini niseme mambo matatu makubwa ya kisera. Kwanza, nikiangalia bejeti hii, kusema ukweli ni contractionary budget. Yaani ni bajeti ambayo haitaweza kukuza uchumi kwa kiwango kile ambacho tungetarajia. Kwenye wasilisho la hali ya uchumi wa sasa hivi tumeambiwa kwamba tumekua kwa asilimia 4.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kwamba tutakua kwa asilimia 5.6 mwaka ujao, 2022. Kwa nini tufikie asilimia 5.6 badala ya kurudi asilimia saba ambapo ndiyo long term trajectory yetu kwa miaka mingi? Wakati tumeshashuka mwaka huu tukapunguza ile kasi, tutawaona kwamba kwenye nchi nyingine ambazo wametekeleza aina fulani ya sera, utaona kama Ulaya zinaanza kurudi na kuwa mara mbili ya ile waliyokuwa wamebajeti mwaka uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tatizo ni kwamba ukiangalia bajeti, sera zilizomo humu ndani za fiscal na monetary utakuta zote ni contraction. Kwa nini? Kwa mfano, ukisoma bajeti ya mwaka jana, 2020 na ukisoma Monetary Policy Statement ya mwaka 2020 na ya miaka mitabo iliyopita kwa ujumla hutaona tofauti. Wanabaki pale pale kwamba tutakua kwa asilimia saba. Naamini kwamba ndiyo sababu tumebakia tunakua kwa asilimia saba kwa sababu hatubadilishi zile sera za ujumla, zinabakia ni zile. Kwa hiyo, kama hubadilishi ile sera uka-promote growth, ni kwamba hutaweza ku-break through out of your long term hiyo ambayo tumekuwa tunaiendeleza asilimia sita au saba kwa miaka zaidi ya 10 toka wakati wa awamu ya nne na ya tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaamini ukweli ni kwamba ukiangalia sekta ya fedha, utakuta kwamba tatizo ni kwamba kama unashikilia inflation kwenye tarakimu kati ya tatu na tano kwa miaka 10 au 20, umejenga fiscal space kubwa sana ya kuweza kukopa na kuongeza fedha za kuendesha miradi katika nchi yetu; ya Serikali in this case, lakini pia inafungua fedha zile zilizo benki ziweze kwenda kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba sera hii ya kushikilia inflation kwenye asilimia tatu, maana yake ni kwamba mikopo isikue. Kwa sababu the only way unavyoingiza fedha kwenye uchumi ni kwa mikopo au kwa kuuza fedha za kigeni. Sasa sisi mikopo yetu tumeishikilia, Serikali inakopa kidogo na sekta binafsi inakopa kidogo, kwa hiyo, kwenye uchumi kunakuwa na ukwasi mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua Marekani ni nchi ambayo the rate of employment kule Marekani ni 5% au 6% na wao inflation yao inakuwa ni tatu kwa sababu wakichochea kidogo uchumi tayari inflation mambo yatakuwa magumu, hawatapatikana watu wa kufanya kazi. Hapa kwetu tuna unemployment kubwa, kwa hiyo, tunaweza tukaweka mkopo kwa sekta binafsi, sekta binafsi ikaajiri na uchumi ukaanza kukua kwa 7%, 8%, 9% au 10%. Ni very easy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba utakuta kwamba riba ni zile zile miaka hii yote. Toka mimi nianze kusoma hii serious, riba zinazotokana na Sera ya Fedha ni zile zile za zaidi ya asilimia 10. Ukiangalia nakisi ya bajeti ambayo sasa ni budgetary policy ni nakisi ile. Ukiangalie, yaani kitu unapotaka kuangalia zaidi kwenye bajeti ni nakisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia nakisi ya bajeti ambayo sasa ni Budgetary Policy, yenyewe Budgetary Policy ni nakisi ile. Uiangalie yaani kitu unavyotaka kuangalia zaidi kwenye bajeti nakisi. Ukiweka nakisi ndogo maana yake Serikali inajinyima kwenda kukopa fedha kwa sababu, maana yake ni kitu ambacho lazima ukipate nje ya mapato uweze kukiingiza kwenye uchumi wako. Na sasa hivi kwa sababu kuna fiscal space ya muda mrefu ya low inflation unaweza ukakopa hata kwenye Benki Kuu, tumeona sasa wameanza kukopa Benki Kuu kwa kasi kubwa kidogo na hiyo ni kitu kizuri kwa sababu, tunaingiza fedha kwenye uchumi, na watu wakishaleta bidhaa zao wanaweza wakaongezea mikopo yao wakazalisha. (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo nasema kwamba, bila kufanya marekebisho hapo na niwakumbushe wale waliosoma kidogo, kuna trade off kati ya inflation na growth. Trade off kati ya inflation na, unaongeza inflation unaongeza na rate of wealth growth mpaka a certain level hapo inflation inapokuwa kwamba, ina cause employment imeshafikia mwisho ndio unasema hapa sasa nikienda zaidi nitajikuta napata hasara kwa sababu hata labor cost inakuwa sasa ni structural inflation imejitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba, hii issue ya contraction monetary policy na fiscal policy tuiangalie, nakisi sasa imeshuka wameishusha kutoka asilimia 3 kwenda asilimia 1.5 maana yake Serikali isikope, isitafute fedha mahali pengine ikaingiza kwenye uchumi uchumi ukakua; uchumi hauwezi kukua bila kuwekeza, sasa hiyo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme pili,nasema kwamba, ukiangalia kwa upande wa mapato ijapokuwa wana-protect ifike kwenye 23 plus, lakini ukweli ukiangalia mapato ya mwaka huu hayatafikia trilioni 18. Mpaka sasa hivi ukichukua takwimu za mwezi Mei ziko itafikia, nimepiga hesabu haiwezi kuzidi trilioni 18, sasa trilioni tano utazipata wapi? Uongeze ufike 23 trillion?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo una over estimate, tumesha-over estimate kwenye hii bajeti, lazima tuangalie ni wapi tupate au tuongeze vipato wanavyoshauri wengine kwenye simu, whatever. Japokuwa wanawema ukiweka kwenye simu au ukiweka kwenye miamala hii watu watarudi kule kwenye matawi ya benki, benki zitafurika watu. Watu watasema kwa nini nikachukue kwenye M-Pesa? Nitaenda kwenye benki kwenye matawi nichukue pesa yangu cash kwa kulekule hudai kwa hiyo, sasa tatizo utaongeza mpaka wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu hivi ambavyo vina alternative ways tukivishika tutapata matatizo. Kwa hiyo, nasema kwamba, ukweli ni kwamba, hilo ni tatizo na niseme hivi kuna hii issue kwa mfano kwenye upande wa mapato unpredictability, again mambo ya policy unpredictability yamejiingiza hapo. Kwamba, unaweka ushuru kwa mwaka mmoja, nasema tumeweka huu kwa mwaka mmoja, hii kwa mwaka mmoja, sasa wewe mtu utafanyaje maamuzi ya kuwekeza wakati wewe unajua kwamba, huu ushuru umepata unafuu wa mwaka mmoja tu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka ushuru ukae kwa miaka mitatu, minne, kabla hujajigusa. Tatizo hapa tunasema tax current kuwe na tax current ya kwamba, nikipandisha mwaka huu nitakaa miaka mingine mitatu kabla sijapandisha. Kwa hiyo, mtu akitaka kutumia ile opportunity anawekeza kweli kama unpredictability tunazidi kuiongeza hapa haitasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu nasema hivi kodi hii ambayo wanakamati wa bajeti wameisema ya LUKU; LUKU, eehee, LUKU ni watumiaji wengi ni wapangaji. Sasa wewe ukaenda kutumia unamtoza mwenye property au unamtoza aliyepanga property?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie vizuri namna ya kukusanya. Ni kodi nzuri ni ubunifu, lakini tuiangalie namna ya kukusanya na kitu kama hicho. Lakini niseme hivi kwenye upande wa ku-allocate resources zetu tunaziweka sana kwenye miundombinu, sawa, lakini tujiulize ni kitu gani tunafanya ili watu waanze kuona opportunities kwenye central corridor kwa mfano kwa sababu sasa SGR is coming, lakini hebu niambie toka tuanze kujenga SGR mpaka Morogoro ni watu wangapi wameenda kuanza kuwekeza au hata kuulizia nijenge kiwanda gani? Niweke kitu gani? Niweke shamba gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hamna watu wamekaa kimya tu kwa sababu, kuna vitu vingine ambavyo havijafanyika kuweza ku-motivate production na investment katika hii nchi. Mwisho, but not the last kwa sababu muda tu. Niseme execution, execution unakuja kuona mwisho wa mwaka, unaona hela nyingi zinaanza kutolewa quarter ya tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, issue ninayoomba ni kwamba, fedha hasa hizi za maendeleo tujaribu kuzipangilia kwa mpango kwamba, zile ambazo tunakopa tuzikope mapema, ili zianze kutekeleza miradi ya maendeleo tusingojee mpaka quarter ya nne ndio tuanze kupata pesa kwa sababu hizi zinakusanywa kwenye kodi mostly for the current purpose, lakini hizi za maendeleo ni fedha ambazo zinatakiwa zipatikane immediately. Tutafute wale watu wanaotukopesha watukopeshe, tutafute donors wazilete mapema tuanze kuzitumia kwenye miradi ya maendeleo, tuanze kuzi-disburse mara moja hasa kule kwenye wananchi zifike mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha mwisho ni issue hii ya ahadi za viongozi. Tuliahidiwa na Wabunge hapa tulipokuja tuliahidiwa kwamba, zile ahadi za viongozi kwa wananchi wetu kule kwenye majimbo zitaorodheshwa ziwekwe kwenye vipaumbele tuambiwe kwamba, hii ya kule Vunjo itatekelezwa mwaka wa tatu. Nikitajiwa hivyo nitasema haleluya, lakini kama hatujajua kwamba, zile ahadi zimewekewa mchakato gani wa kutekeleza itakuwa kwamba, tunabakia tunaenda kule wataanza kutupa mawe wewe ulizungumza hivi, tupeni tuende na hicho kitu. Nimesema hapa kwa sababu najua ni kwenye mambo ya execution. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unisamehe kwa kuzidisha kidogo, lakini nataka kusema naunga mkono hoja hii vizuri sana. Na haya niliyosema ni mambo tu ya kuboresha tunaenda mbele, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nikupongeze kwa namna ambayo unaendesha Bunge hili kwa weledi. Pia nijiunge na wenzangu kutoa pongezi na shukurani nyingi, kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa jinsi ambavyo anaendeleza kazi hii kwa kasi na kusema kweli anatekeleza kwa mafanikio. Sio mafanikio tu, lakini huku akizingatia kile ambacho watu wengi wanakisahau; Katiba, Sheria, Sera na Kanuni. Jambo hili limeanza kuvutia sana wawekezaji kutoka nje na hapa ndani na watu kujisikia wako nyumbani. Naamini hiki kitachangia sana katika ukuaji wa pato letu katika miaka inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa yote ambayo walifanya. Wameleta mapendekezo ya Mpango ambayo yanakubalika. Nimpongeze pia Mheshimiwa Daniel Silo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa namna ambavyo aliwasilisha ushauri na maelekezo fulani fulani ambayo, yametoka kwenye Kamati yake kuhusiana na mapendekezo haya ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajikita kwenye lile ambalo nataka nizungumzie zaidi ambalo ni la mambo ya sera ya fedha, niseme kwamba licha ya mipango mingi na mikakati mingi ambayo inatekelezwa kwa sasa hivi, ikiwepo ile ambayo inaendana na mpango wa kupambana na athari za COVID-19. Utaona kwamba bado Mpango huu umekuja na maoteo ya ongezeko la pato la Taifa ambalo nafikiri ni chini sana asilimia 5.2. Ni ongezeko kidogo sana ukizingatia kwamba mambo mengi yanatokea na yanatokea kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hivyo, naamini kwamba, sisi hatutoki kwenye uchumi ambao ulikuwa kwa hasi, uchumi wetu umekuwa chanya, kwa hiyo tuna kila sababu ya kutegemea kwamba, kile kinachotokea kwenye ground na ukweli ni kwamba maoteo ya ukuaji wa chumi zilizoendelea ni asilimia sita kwa mwaka 2020/2021 na mwaka unaokuja unaotea wakue kwa asilimia 4.9, yote hii itachochea ukuaji wa uchumi wetu. Kwa hiyo, ni lazima pengine tuangalie vizuri kwamba tusiwe-conservative sana bali, tujaribu kuangalia ni namna gani tutachukua hatua na nafikiri kwamba, hatua zitakazochukuliwa zilete matokeo ni hizi ambazo nazungumza sasa hivi ndio hizo zitaweza na ndio kitu kimekuwa kikwazo kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba ukuaji wa pato la Taifa unatokana zaidi na sekta zile ambazo zinanufaika na uwekezaji wa Serikali. Miundombinu, ujenzi ndio utaona hizo sekta ndio zinanufaika na zinakua kwa kasi mpaka asilimia 13 mpaka 14, lakini sekta nyingine hizi za watu binafsi binafsi za kilimo na kadhalika, zinakua kwa kiwango ambacho naamini bado kiko chini. Ukuaji huu mdogo kwenye sekta hizi naamini unatokana zaidi na kile ambacho hakijafikiwa licha ya kwamba tuna uchumi ambao tunasema ni uchumi tulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi tulivu maana yake ni uchumi ambao una-low inflation (mfumuko mdogo wa bei). Hata hivyo, utakuta kwamba, mahitaji kwa uchumi kukua kwa kasi sio tu kwamba uwe na mfumuko mdogo wa bei, wanasema necessary but not sufficient conditions ziko tatu. Moja ni hiyo mfumuko wa bei mdogo; lakini huu mfumuko wa bei mdogo lazima uweze kutupelekea kupata riba zilizo chini. Cha kwanza, riba ziwe chini na tulivu na maana ya riba kuwa chini na tulivu ni riba ziwe chini kwa maana ya kwenye tarakimu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kwamba, thamani ya sarafu yetu iwe nayo tulivu; exchange rate stability. Kwa hiyo, the three ni necessary but not sufficient conditions za rating growth. Sasa niseme hivi, tutaona kwamba uchumi wetu kwa miaka mingi umekuwa na inflation ambayo ni chini ya asilimia 10. Imekua kwenye zaidi ya miaka 10 iliyopita, tuna inflation ambayo iko kati ya tatu sasa na sita au saba, lakini utakuta kwamba bahati mbaya licha ya kuwa na hiyo, bado kuna matatizo ya sera ya fedha haijaweza kutuletea riba ambazo ziko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ni kwamba tujiulize ni kwa nini sera hizo haziji chini? Benki Kuu imefanya mambo mazuri, imeweza kupunguza ile riba ambayo wanatoza mabenki wanakwenda kukopa kwao. Imepunguza fedha ambayo mabenki wanalazimika kuweka kwenye Benki Kuu ambayo haipati riba. Zote hizi zimejaza mabenki ukwasi wa kutosha. Hata hivyo, bahati mbaya hatua hizi zilizochukuliwa siku za karibuni zimesaidia yale mabenki kutengeneza faida kubwa kwa manufaa ya wana hisa wao tu, hazijaenda kwa walengwa, yaani hizi hatua zimguse yule mzalishaji wa sekta binafsi ambaye ili yeye aweze kuongeza uzalishaji au awekeze kwenye uzalishaji mpya, ni lazima apate mkopo ambao ni acceptable kwa riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo haijatokea. Nafikiria kwamba, siku itakapotokea kwamba riba zishuke ziwe kwenye tarakimu moja, ndio utaanza kuona kwamba mahitaji ya mikopo yataanza kuongezeka. Kwa sababu, unajua kwamba unaenda kuzalisha, lakini huhatarishi ile dhamana yako, hawaji kuiuza kwa sababu utaweza kulipa ule mkopo na u-service. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwa hizi riba za asilimia 16 mkopo unaji-multiply mara mbili baada ya miaka mitano. Hebu niambie ni kitu gani duniani hapa utawekeza halafu kiji-multiply mara mbili kwa miaka mitano. Hata nyumba yako wewe mwenyewe miaka 20, 30 ndio unarudisha fedha yako. Kwa hiyo, nasema hiyo haitawezekana mpaka wafanye hivyo. Sasa napenda kutoa hoja kwamba, kitu kinachopelekea mabenki wasishushe riba sio kana kwamba hawana ukwasi, ni kwamba kuna riba ambayo ni bench mark, kigezo ambacho wao ndio wanaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika wao wanaangalia kwamba kwenye soko la dhamana za Serikali, je, riba inayopatikana pale ni kiasi gani? Wakishapata pale wanasema ok, hii ni risk free rate kwa hiyo ile ndio kigezo chetu. Hatuwezi kushuka chini na ukweli ni kwamba fedha hizi zilizopatikana zote kwenye huu mlegezo uliotolewa na Benki Kuu, nyingi zimekwenda kwenye dhamana za Serikali, hazikwenda kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme hivi, ukweli ni kwamba hata deni la Taifa linachochewa zaidi na riba hizi za dhamana za Serikali za muda mrefu ambazo ni asilimia 15, 16. Kwa hiyo, tunaposema deni la Taifa tatizo sio tu kwamba eti wanakopa sana, hapana. Rate service burden inakuwa kubwa kwa sababu riba hizo ziko hivyo. Ukiangalia miaka ya nyuma riba kwa dhamana za Serikali hazikuwa hivi. Kwa hiyo, nasema ule mfumo wa ku-auction dhamana za Taifa, una-auction kwa kutaja bei, kwamba, nauza dhamana za bilioni 400 kwa asilimia 16 nani atashusha bei? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni soko au una-dictate? Nakuapia hazitakaa zishuke hizo riba ilimradi namna ya kuendesha hiyo minada ni hiyo hiyo. Kuna mwanaume anaitwa Dutch Auction natumai wajaribu kuangalia namna gani ya kufanya au waanze kushusha waseme tuta-auction kwa asilimia 10, tuone kama hawatanunua. Mabenki yatakimbilia hata mimi nitanunua kwa sababu asilimia 10 it is a big real interest rate. Real kwa sababu ukitoa hii asilimia tatu, nne ya inflation bado nina real benefit ya six, seven percent. Kwa hiyo, kuna kila haja tumwombe Waziri atekeleze kwa sababu, hiyo itasaidia kwenye kupunguza burden kwa kila mtu na kuanza kuona tena hali inarudi kikawaida, watu kuchukua mikopo, biashara kukua na sisi wote tukafaidi na utakuta hata kwenye kilimo watu watapata mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba, nafikiria hilo ni la msingi na tuseme kwamba pamoja na kwamba mfumuko wa bei umetufaidisha kuhakikisha kwamba exchange rate bado imekuwa stable, lakini bado haujatufikisha pale ambapo, that is the most critical issue ni riba na niseme hivi nazungumza riba kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya fedha sio kitu kingine isipokuwa riba, basi ukienda nje huko duniani kwenye masoko yaliyoendelea, nenda US, nenda wapi kitu cha maana wanaangalia bank rate, that is all, mambo mengine yanaji- set yenyewe kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naambiwa muda umeisha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Ninayo mengi kidogo, lakini nitajaribu kuzungumza machache. Niseme na najiunga na wenzangu kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa mafanikio mengi tunayoyaona na ambayo yameorodheshwa vizuri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pia nimpongeze Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi na Makamu wa Rais wetu Philip Mpango na wewe pia Mheshimiwa Spika nikupongeze jinsi unavyofanya kazi yako.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo, naomba niseme, tumesikia mengi yametekelezwa kwenye uchumi wetu, miradi mikubwa sana, lakini naomba Serikali ielewe kwamba, wakati unapofanya makubwa usahau kwamba kuna vikero vidogo vidogo ambavyo ukiviondoa vitakupa amani na kutekeleza yale makubwa.

Mheshimiwa Spika, ukiingia kwenye mtihani usianze na maswali magumu, anza na yale madogo na yale rahisi ambayo utayamaliza mara moja, halafu uende kwenye makubwa. Hasa ukienda kwenye halmashauri zetu kwa mfano, kuna vijikero kama kwa mfano kule Vunjo, barabara ya kilometa saba toka Mji Mdogo wa Himo kwenda Lotima, kitu ambacho unaweza ukakimaliza kwa fedha utakayoita ni chenji tu.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye barabara tunayoita ni ya Mandaka - Mkirema kilometa saba ni pesa kidogo, ukienda Uchila – Kisomanji - Kikolarii ni kilometa saba au nane, kwa hiyo unaweza ukaviondoa na mimi nisije tena hapa nikiwa naomba kuuliza maswali hapa na pale, nitawaachia na wengine wakiuliza maswali kwa sababu vile vidogo vimetoka, mimi nina amani na Serikali ina-implement vitu vizito itaweza kui-implement bila kusema kule Vunjo kuna matatizo gani mbona huyu jamaa anasimama kila siku. Naomba Serikali ichukulie hilo na iweze kuvikamilisha vile vidogo.

Mheshimiwa Spika, tunaipongeza sana Serikali kwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na tunasema kwamba hii miradi ina maana kubwa sana hasa hii tunayoizungumza ya huduma za jamii, mashule na hospitali na kadhalika. Nafikiri tuangalie vizuri kwamba je, the current costs implications zake zikoje. Unapojenga shule ufikirie OC na mishahara itakayotosheleza ile shule, iende ifanye kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, nafikiri kwamba hilo jambo ambalo kila saa nikiangalia najisikia na-shrink sana. Hivi itakuja kufika mahali kwa mfano leo naamini kama tungesema mahitaji yote ya Walimu, watoa huduma za afya na wafanyakazi wengine wa Serikali ambao wanatakiwa kwenye Wizara ambao hawapo kama wote wangepewa, tungepewa ile ikama kama inavyoombwa, naamini kwamba bajeti nzima isingetosheleza kukidhi mahitaji yale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naamini kwamba ni lazima tuangalie vizuri na tufanye uchambuzi vizuri, tusije tukaishia kukopa ili tule. Nakubaliana na mambo haya mnayosema inflation, kwani hii inflation niseme na ni lazima tujue, leo hii mfumuko wa bei Marekani na nchi za kanda za ulaya imefikia asilimia 7.5 kwa wastani.

Mheshimiwa Spika, ni mfumuko mkubwa kuliko wakati wote kuanzia mwaka 1982. Kwa hiyo hili ni suala la kidunia ni structural na kitu ambacho hatuwezi kuki-address kusema kwamba tunaenda kuomba pesa, ni kufanya nini, ni kukaza mikanda, this is the time to belt tighten, ni wakati kusema kwamba there is no way tutaepuka makali haya, kama ulikuwa unaenda jimboni kila siku nenda mara mbili, mara tatu kwa sababu hela utakayokuwa nayo haitatosheleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba hilo ni jambo ambalo tuliangalie, sio kwamba ni letu na sio jambo la kufanya haraka haraka na sio kitu ambacho Benki Kuu inaweza ikashughulikia mara moja, haiwezi it is not monetary policy ya hapa ndani itafanya hicho kitu kwa sababu kinakuwa given na imported inflation.

Mheshimiwa Spika, sasa turudi hapa, ambacho nimepongeza kwenye hii miradi mikubwa, kuna kwa mfano hili suala la Vyuo vya VETE, naishukuru sana Serikali imeanza kutoa vipaumbele stahiki kwa VETA, vyuo hivi ambavyo vinatupa study na ufundi. Hata hivyo, naambiwa kwa takwimu ambazo sio rasmi, VETA ina upungufu wa Walimu 1400 na ni kabla havijaongezwa hivi vyuo vingine ambavyo vinakamilika kwenye mwezi huu wa Juni na mwaka unaokuja wanaweka vyuo vingine thelathini.

Mheshimiwa Spika, ukiweka pengine upungufu utakuja kuwa ni mkubwa sana wa watu, lakini sio tu upungufu wa Walimu, lakini ni upungufu pia wa vitendea kazi, vifaa vile vya kufundishia. Watu wanataka kujifunza cherehani, wanahitaji kushona kwa sababu sasa hivi tunavaa nguo zimeshonwa hapa, kwa hiyo lazima wawe na basic equipments kwenye hivi vyuo. Kwa hiyo, ni lazima tufikirie tunafanyaje pesa inatoka wapi ili tuweze kuhakikisha kwamba wanajenga ndiyo tusije tukajenga magofu, yaani kuwa na majengo tu it doesn’t help, haitasaidia.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu mkubwa nilitaka kuingiza kwenye uwekezaji ambao Mheshimiwa Rais wetu ameufanyia kazi sana na naamini utaanza kuona miradi mingi inasajiliwa. Wamesajili miradi 294 kutokana na hotuba tuliyopewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na kweli kama miradi hii yenye kubeba thamani ya Dola Bilioni Nane itatekelezwa ajira zitaongezeka, kipato cha Taifa kitaongezeka, tutabakia kwenye kundi lile la watu walioendelea vizuri kipato cha kati na pengine tutaenda juu, lakini miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa, tutafanyaje mimi nataka nishauri mambo matatu, manne.

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka uwekezaji huu wenzetu majirani zetu wameanza kupunguza kodi ya makampuni, kwa sababu tunashindania wawekezaji hawa, wanapunguza kodi ya makampuni kutoka 30 kuja asilimia 25. Hiyo ni kivutio ambacho hatuwezi kukibisha hata tungesema tunafanya nini. Pili; kuna perception kwamba gharama za kuanzisha mradi hapa ni kubwa sana kumbe wala si kubwa sana ukilinganisha na kwingine, tatizo la watu kuona gharama hizi za uanzishaji miradi kubwa ni utitiri wa mamlaka zinazotoza tozo hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakuta kwamba kama tungeweka lamp sum tukasema kuanzisha kitu hiki ni Shilingi Milioni Moja unaenda kulipa kama ni TRA au mahali pengine lakini mamlaka nyingine zikagawiwa na huyo anayekusanya inakuwa ni rahisi mtu anajua kabisa ok, nataka kuanzisha kampuni ya simu ni Shilingi Milioni Tano basi its transparent and open and no need ushauri wa mtu. Kwa hiyo, mimi naomba hilo lifanyiwe kazi ili tuweze kupata wawekezaji hawa waje upesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu; ni suala zima nitalizungumza tena kwa bahati mbaya suala la riba ambalo najua mamlaka imeshatoa amri imeshatoa directive kwamba lishughulikiwe, lakini hatuwezi kupata wawekezaji ambao hawawezi kukopa ndani kwa sababu utakuja na mtaji wako ndiyo mashine na nini, lakini ule mtaji wa working capital lazima utoke kwenye mabenki ya ndani. Hasa huwezi kukopa kwa asilimia 16 wakati kule nje mtu anayezalisha kama huyo anakopa kwa asilimia tano uende ukashindane naye kwenye mauzo ya nje it is impossible! What you need ni kwamba lazima kweli au tuweke special windows na tunajua kwamba kuna watu wanataka kuongeza uzalishaji wao hapa kwa mfano kule NIDA tulikwenda, lakini hawawezi kukopa hapa ndani kwa sababu hiyo tu kwamba riba ni kubwa na wakipeleka kuuza vile vitu nje hawataweza kushindana kwa hiyo inakuwa matatizo, naomba hicho kifanyiwe kazi na tusichukue tu mzaha mzaha kwamba basi tu tuna njia ya kupunguza hizo riba, tunajua zipo! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze kingine ni kwamba mimi naamini pia kwamba miradi mingine kwa mfano Bagamoyo Port, sijui Mchuchuma – Liganga, tunasema kwamba tatizo lililopo ni kwamba wanajadili vitu ambavyo hatuna, wanajadiliana maslahi ya Taifa letu tuyalinde lakini tuangalie maslahi mapana yanatokana au faida nzima zinazotokana na mradi ule kwa muda mrefu, tuangalie tusiangalie kesho utakosa ushuru wa kiasi hiki na hiki, kwa sababu huo ushuru huna anyway haupo kama ile kampuni haitaanzishwa wewe hutapata huo ushuru. Kama Bagamoyo port haitaanzishwa ianze kufanya kazi hutapata hicho kitu, kwa hiyo afadhali tukubali tuangalie tuwe na long term view ya issues badala ya kuwa na short term issues.

SPIKA: Ahsante sana muda wako umeshaisha Mheshimiwa.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kuchangia kwenye mjadala huu ambao ni muhimu sana kwasababu ya jukumu la Wizara hii katika kuendeleza nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako, na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Wizara kwa kazi nzuri kwenye mazingira ambayo ni magumu na kwenye changamoto nyingi.

Mheshimiwa Spika, kwasababu uchumi wowote unapobadilika haraka sana sekta ya elimu inatakiwa na yenyewe iweze kujibadilisha na kuwa bunifu ili iweze kutengeneza wahitimu ambao wanakidhi mahitaji ya wakati huo. Sasa tukiangalia na tukijaribu kufikiria kwamba tuko wapi na tunakwenda wapi katika dunia hii, utajikuta kwamba sekta hii inatakiwa ibadilike sana kwa namna ambavyo tunakwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, sekta ya viwanda ilivyobadilika, industrial revolution ilivyoingia, tija kwenye kilimo iliongezeka sana na hivyo bei za vyakula zikashuka kwa hiyo faida kwenye kilimo ikashuka pia. Kwa hiyo, watu wakaamua kukimbilia mijini wakapata kazi kwasababu viwanda vile vilikuwa vinazalisha ajira.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi viwanda havizalishi ajira. Bahati mbaya ukienda kiwanda chochote kikubwa utakuta kwamba robots wame-automate na artificial intelligence utakuta kwamba pengine ma-robot yanafanya kazi. Hata kule kwenye mabenki yetu sasa hivi unakuta kwamba watu hawaajiri, walikuwa wanaajiri watu 400 sasa hivi hawaajiri kwasababu tunatumia sim banking na vitu kama hivyo ambavyo vina-replace employment ya watu.

Mheshimiwa Spika, sasa tunapokwenda hii karne siyo ya viwanda ambavyo ni labor intensive, ni kadri sasa ya TEHAMA na hii TEHAMA inatupeleka mbali sana tukijifikiria vizuri. Tukijifikiria vizuri tutafanya mambo mengine na ni kweli kwamba vyuo hivi ambavyo tumekuwa tunazungumza toka asubuhi kwamba tuviboreshe, tufanye hiki na kile, tukichunguza vyuo hivi vya ufundi vya kuwasaidia vijana wetu wapate maarifa na ujuzi waweze kutenda kazi na waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, pengine kwanza havifai kwenye karne hii, havina karakana na vifaa vya kufundishia vitu ambavyo vinahitajika kwenye uchumi wa kisasa, kwenye uchumi huu ambao sasa hivi ndiyo tunakwenda. Na mtu akisema kwamba hatujui tunakokwenda ni mtu ambaye haoni kwasababu ukweli ni kwamba tunakokwenda ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta zinazozalisha ajira ni sekta za huduma; mawasiliano, kwa sekta kama za usafiri, uchukuzi, afya itazalisha utalii, itazalisha utawala, sales and marketing, lakini ukiangalia upande huu wa viwanda hawatazalisha kwasababu automation imefika mbali sana na tija imekwenda mbali sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwamba tunapoangalia hivi vyuo kuvipa uwezo lazima na walimu wale wapite kwenye mafunzo tofauti na waweze ku-identify ni kitu gani ambacho watafundisha ili tuweze kuwasaidia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kitu ambacho nakiona ni kwamba vyuo vilivyo kila kata kuna vyuo. Sasa vyuo hivi usipofanya vikawa-specialized hutaweza kuvi-equip na vile vitu ambavyo vinahitajika; hutaweza. Kwa hiyo, lazima viwe specialized na vitangazwe kwa wananchi wajue kwamba nikienda Bukoba ntapata chuo ambacho kinatengeneza watu wanaojifunza kutengeneza simu, au nikienda Lindi kule ntapata watu ambao wanaweza wakatengeneza au kuhudumia mashine za oil and gas, and so forth. Kwa hiyo, ni lazima tuvifanye viwe specialized kidogo angalau kuwe na specialization kidogo ili tujue ni vipi na viko wapi.

Mheshimiwa Spika, lakini nikihesabu kule kwangu kuna Vyuo viwili; Mshiri na kingine kiko kule Mwika, hakina hata walimu, hata hao ambao tunasema kwamba ni wa kale ambao sidhani kama wanaweza waka-cope na skills zinazohitajika, bado hawapo hata hao walimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niombe kwamba pengine, kwanza hiyo kanzidata ya walimu wa vyuo hivi vya ufundi na stadi mbalimbali ijulikane ili waweze kuwa allocated properly. Hayo majengo ambayo yamekaa idle hayaendeshi kozi zozote kwasababu ya kukosa walimu yaweze kutumika lakini cha msingi ni kwamba wapate training, wapelekwe hata nje.

Mheshimiwa Spika, hata tukikaribisha Wachina na Wahindi wakaja wakatuonesha wao wanafanyaje na wanakwendaje kwasababu nchi nyingi sasa zinajikita kwenye upande wa training ya mambo haya ya hudua na kutengeneza vitu vya kisasa, siyo kutengeneza magari ya, hata magari manual siku hizi hakuna kabisa.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi; kwasababu watu wa ku-train ni wengi sana hebu tufikirie wazo moja. Kwa mfano tunasema mambo ya soft skills hizi za watu kuwa na tabia ya kuweza kujituma, kuweza kuheshimu kazi na kadhalika, zinapatikana zaidi kule JKT.

Mheshimiwa Spika, ukienda JKU sasa hivi ukaweza kupiga mark time pale vizuri halafu jioni ukafundishwa skills zozote hizi ambazo tutakuwa tumesema Ruvu wafundishe hiki na hiki, ukifundishwa hivyo ukimaliza pale baada ya miezi mitatu au sita unakwenda unaajiriwa na utakuwa na heshima na utakuwa mwaminifu na utafanya kazi vizuri kwasababu umejifunza discipline na skills kwa namna ambayo itasaidia sana watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri hiyo ndiyo njia ambayo inaweza ikafanya kwa haraka sana watu ambao wanamaliza form six, hata wanaomaliza university wanaambiwa piteni kule mtapata skills kwa ujumla kwa haraka zaidi na kule kuna vifaa vya kufanyia majaribio na kadhalika. Kwa hiyo, hicho ni kitu ambacho mimi nafikiri kingekuwa cha msingi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niseme kwamba tukizingatia kwamba kuna haja ya kuwa wabunifu kwenye hii nyanja ya TEHAMA, kuna haja ya vyuo vyetu hivi vikuu sasa hivi viwe na vitengo. Kila chuo at least kiwe na kitengo cha incubation ambapo mtu akiwa na wazo lake anakwenda kwenye kitivo au kitengo kile cha chuo kikuu, wanamsaidia kuboresha na kumuonesha namna gani anaweza aka-implement.

Mheshimiwa Spika, wanaweza wakamuonesha pia kwamba pengine mashine za namna hii zinapatikana TEMDO, zinapatikana wapi, hebu tukusaidie, wanamsaidia kina-take off wanamuachia anaendelea na watu wataajiriwa wengi.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna hii ambayo tunaona naona kuna shida sana; ijasiriamali haufundishwi darasani, unafundishwa kwenye field. Mtu kama umemaliza kama usipopata on job training hutaweza. Sasa hivi vyuo vina watu, walimu wako wengi ambao wana-retire, maprofesa wana-retire, wajasiriamali wengi nao wana-retire.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tusiwapeleke tukawaombe waanzishe hivi vitengo ili watu waweze kupata skills zao wakajifunza. Kuna mmoja alisema kwa nini akina Dewji hawaandiki vitabu. Watu wamejifunza kutoka kwa akina Dewji waka-implement mambo ambayo yataleta tija katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nafikiri kwamba kule kwenye jimbo letu, na nitafurahi sana kama kweli tutaweza kupata specialization ya mambo ya…

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei, muda hauko upande wako.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Nakushukuru sana, ahsante sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia 100; ahsante. (Makofi)
The Water Resources Management (Amendment) Act, 2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii. Nichukue pia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu anayeongoza Serikali na Wizara hii husika ambayo ameona umuhimu wa kuleta marekebisho haya ya kuboresha usimamizi wa rasilimali ya maji katika nchi yetu. Ninaamini ni jambo muhimu na ninamshukuru sana na kumpongeza Waziri wetu, Kijana wetu Mheshimiwa Jumaa Aweso, Mheshimiwa Maryprisca ambaye ni Naibu wake pamoja na Viongozi wa Wizara hii kwa umakini wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru pia kwamba wameshirikisha, wamepokea maoni ya wadau kuhusiana na masuala haya ambayo yanakwenda kurekebishwa na ninaamini kwamba ukiangalia utaona kwamba siyo masuala ambayo kama wangekuwa sio watu makini sana wangeweza kuyaibua lakini wameweza kuyaibua kwa sababu kweli wanataka ufanisi katika suala hili zima, ambalo mimi nimejiona kama ni sheria ambayo inapaswa kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali ya maji kwa kukabiliana na vitendo vinavyosababisha uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni shughuli ambayo inaenda kudhibiti au kuhakikisha kwamba wanadamu ambao sisi tunahitaji maendeleo tunatumia vyanzo vya maji kwa namna ambayo itakuwa endelevu na ndiyo sababu kwenye hifadhi nyingine, mimi ninafikiri kwamba kwenye mabonde ni kama hifadhi tu hakuna tofauti na hifadhi nyingine wameenda mkondo ule wa kuunda hata majeshi kabisa kule ambako ni hifadhi watu wasitumie ile ardhi kwa namna ambayo itaharibu au kupoteza kabisa utajiri huu ambao Mungu ametupa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba hawa hawajaenda kwa kufuata nadharia ya kuunda majeshi kuhifadhi maji, lakini wanataka kutumia naona nadharia inayotumika na msingi wake ni ushirikishwaji wa wananchi katika kusimamia vyanzo na matumizi ya maji haya tuliyopewa. Tofauti kidogo pia ambayo ninaiona na ninashukuru kwamba Profesa Manya amezungumza mambo mazuri sana sitaki kuyarudia, nayaona kwamba kuna umuhimu wa kufungamanisha usimamizi wa maji kwenye mabonde lakini pia tuangalie pia zile mamlaka ambazo zinasambaza maji, zile mamlaka ambazo zinasimamiwa na Mamlaka za Usambazaji Maji Mijini na Vijijini kwasababu zenyewe ndiyo zinaenda sasa kuona kwamba watu wale wanaoshirikishwa kwenye usimamizi wana motisha na wanajua namna gani na umuhimu gani wanaweza wakapata katika suala hili zima la kusimamia maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri pia ieleweke kwamba maji yanapita kwenye mikondo, maji yanatokea kwenye chemchem mbalimbali na yanapita kwenye mashamba ya watu walikuwa wanazitumia zile chemchem kunywesha mashamba, kule kwetu ni kawaida kabisa chemchem zipo karibu hata kwenye shamba langu kuna chemchem ambayo ninaweza nikatumia, lakini ukweli ni kwamba lazima tuweze kulinda sasa haya maji yanatiririka namna gani yapelekwe kwenye maeneo ambayo yanahitajika na yatatumika kwa ufanisi zaidi katika shughuli za kibinadamu pamoja na ikiwa ni maji safi wa kunywa na pia maji ya kuendeshea shughuli mbalimbali kwenye sekta za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini kuna umuhimu huo na ndiyo sababu ninaamini kuwa hii nadharia ya kushirikiana wale watu ambao wanaweza kwa urahisi sana kufikia hivi vyanzo na kuviharibu inakuwa ni jambo la msingi na ndiyo maana kwamba wenzangu waliozungumza suala zima la elimu, kutoa elimu sana kwa wananchi siyo tu wanaoishi kwenye maeneo ya vyanzo vya maji lakini pia wale ambao wanaweza wakachimba visima na wale wanoatumia. Watu wajue kwamba maji yana umuhimu, kuna maji ya kutumia kuoshea magari na kuna maji ambayo yanaweza yakatumika kunywesha mashamba, lakini siyo yale yale maji yanastahili kutumika kwa kunywa. Kwa hiyo watu wajue kwamba maji yale ambayo wanatumia kufanya shughuli zao siyo maji ambayo yangeweza kutumika kwa shughuli za watu kunywa ambayo ni msingi sana ni maji safi hayapo kila mahali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba kama nilivyosema hatuwezi kuzungumzia suala zima la usimamizi wa rasilimali maji bila kuzungumzia wale wanosambaza na maana yake ni kwamba lazima Kanuni zinazotungwa chini ya vifungu husika au huko baadae tutakapoangalia hii sera ya maji tuone kwamba namna gani wale wanaosambaza maji wanabanwa ili waweze kusambaza maji kwa namna ambayo ni endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatuwezi kuondokana na ukweli kwamba, hatuwezi kutokuzungumzia gharama za kuwafikishia wananchi wetu maji kwenye nyumba zao na katika maeneo yao ya kufanyia shughuli mbalimbali, hizi gharama zimekuwa ni kero na jambo ambalo mimi ninaamini kwamba watu wanaanza sasa kukiuka kutumia yale maji kupitia mikondo husika ambayo tunafikiri kwamba inahifadhi na badala yake wanaanza sasa kutoboa toba ili wapate maji kwa gharama ambayo ni nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naamini kwamba suala la motisha la kuhifadhi kama nilivyosema haliji endapo utasema kwamba mtu ambaye anaweza akafikia maji kwa urahisi pale alipo unaenda kumtoza Shilingi 800 kwa unit ambayo ni fedha kubwa kwao, wanaona kwamba pengine afadhali wapindishe yale maji yaende kwenye nyumba zao bila kulipa chochote. Kwa hiyo masuala ya gharama lazima yaangaliwe, ninaamini kwamba Naibu Waziri husika atachukua hili suala zima la kusema kwamba atafanyaje, atatumia Kanuni gani ili wale wanaosambaza wasambaze maji kwa gharama ambazo ni muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nitoe maoni yafuatayo ya kuzingatia pia, kwamba mabonde haya tumeona hayana vyanzo ambavyo vinatosheleza kwa fedha, kwa hiyo naomba kwamba ili haya mabonde yaweze kutoa elimu kama tunavyosema basi ni lazima yawezeshwe kupata rasilimali ya kutosha ya kuweza kuelimisha kutoa elimu kwenye ngazi zote kuanzia kwenye Vijiji hata kwenye Kata na kwenye Wilaya. Mabonde haya pia yapewe uwezo wa kufanya doria pengine kwa kushirikiana na Kamati za Usalama na Ulinzi kwenye maeneo yetu ili waweze kukagua vyanzo hivi vya maji na kuhakikisha kwamba hivi vyanzo vipo vinatunzwa na vinatumika kwa namna ambayo ni sahihi na maji hayachafuliwi na watu wengine wakawa wakakunywa maji chini ya bonde, maji ambayo yamechafuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jumuiya za Watumia Maji pia nafikiri kwamba watumiaji maji hususani wale wanaomwagilia wasaidiwe kuboresha miundombinu yao ya mifereji ili kuepuka matope kujaa kwenye vyanzo vile na kuhakikisha maji yale hayaendi kwenye mkondo na kwenda kwenye maeneo mengine ambayo yanahitajika maji kufika kwenye bonde hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kwamba Bonde la Mto Pangani kwa mfano, lina matatizo na wanahitaji kweli kuweza kuwawezesha wale wanotumia waweze kuboresha mifereji yao ili maji yaendelee kwenye mikondo inayostahili hata kufika kwenye Bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ifanye maboresho kwenye bei za maji kama nilivyosema kwenye maeneo mbalimbali ili maji yawafikie watu kwa njia ambayo ni sahihi na gharama ambayo inakubalika lakini natumaini kwamba pia kwa sababu suala hili lote ni mtambuka Wizara ya Mifugo ninaamini kwamba na wao wamepitia Muswada huu. Wizara ya Mifugo wasaidie kujenga mabwawa na mabirika ya mifugo kuweza kupata maji katika nyakati zote za mwaka ili mifugo sasa isiwe inafunguliwa kwenda kuharibu vyanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anayefuga akiona ng’ombe wake anakufa kwasababu ya maji anapeleka yule ng’ombe mahali popote, kwa hiyo naomba Wizara ya Maji sasa ijikite na iwezeshwe kutengeneza mabirika ya mabwawa ambayo yanaweza kusaidia sasa ng’ombe na mifugo mingine kupata maji. Pia naamini kwamba Kamati zile ambazo mnasema zitaundwa kwenye vidaka maji, zile kamati ninaomba Wizara ifikirie kuweka vigezo vya wanakamati, kwa sababu tumeona kwenye jumuiya wameweka watu kwenye jumuiya za maji za RUWASA ambao hawana uwezo, hawaelewi hata ni kitu gani kinafanyika, hawafanyi hesabu na hamna vitabu vinavyojitosheleza kutoa hesabu yam aji, bili zile wanazokusanya zimekuwa Shilingi ngapi, mapato na matumizi kiasi gani hela zimepelekwa kwenye Serikali Kuu kusaidia uendelevu wa miradi ya maji ambayo inatekelezwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Muswada huu. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba Wizara ifikirie pia kuweka vigezo vya wanakamati, kwa sababu tumeona wameweka watu kwenye jumuiya za maji za RUWASA watu ambao hawana uwezo, hawaelewi hata ni kitu gani kinafanyika. Hawafanyi hesabu na hamna vitabu vinavyojitolesheleza kutoa hesabu ya kwamba maji, bill zile walizokusanya zimekuwa shilingi ngapi mapato na matumizi na kiasi gani hela zimepelekwa kwenye Serikali kuu kusaidia uendelevu wa miradi ya maji ambayo inatekelezwa hapa kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ninaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Muswada huu. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nami nianze kwa kumpongeza Waziri mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa kuweza kuwasilisha hotuba yake vizuri, hotuba nzuri iliyosheheni ubunifu mkubwa na ninaamini kwamba atakwenda kutekeleza kama walivyoainisha kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba tunamshukuru Waziri kwa sababu ni mtu mnyenyekevu sana. Mimi toka nije hapa Bungeni sijaona Waziri amenifuata akaniambia pale kwako vipi mambo? Kwenye mambo ya mawasiliano yako sawa? Sijaona. Sijaona mwingine aliyenifuata akaniambia vipi maji? Sijaona; lakini yeye ameweza kuja kwetu na kutuuliza kwamba vipi tunaonaje mambo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kwa kuamini kwamba zile Kata zetu za Kirua Vunjo, Marangu, Mwika na Makuyuni ambapo pia tuko mpakani, lakini zaidi ni kwamba vijiji vingi vimepakana na Mlima Kilimanjaro na msitu. Kwa hiyo, kule mawasiliano yanakuwa ni vigumu sana. Naamini tutatafuta mbinu ya kupeleka minara au kupeleka njia nyingine za mawasiliano kwa hawa watu walio kule kwenye mpaka na kwenye vijiji ambavyo kusema kweli hawapati mawasiliano sasa hivi na kidogo wanayopata ni ya Kenya, hata kama ni redio pia zinapatikana za Kenya na siyo sehemu nyingine. Kwa hiyo, nataka niwaombe watekeleze hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kukazia mambo machache. Natumai yanaweza yakawa yamezungumzwa, issue ni kwamba ni lini tutaweza kufungamanisha mifumo yetu ya utambulisho wa wananchi? Utambulisho wa wananchi umekuwa ni tatizo kubwa. Ukitaka kwenda kwenye Passport unaambiwa jaza fomu zile zile ambazo unajaza unapokwenda NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mahali utakapokwenda utajaza; hospitali utajaza, utarudia na bado una kitambulisho chako cha NIDA, lakini bado ukienda hospitali hawawezi kutumia kile kitambulisho waka-access zile data kwa sababu ile database inaonekana kwamba bado haijafungamanishwa ili iweze kuwa accessed na wadau wote wanaotaka kupata taarifa za mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufungamanisha huko pia kunawezesha kabisa hata kuongeza usalama kwa sababu ukweli ni kwamba mtu anapofanya makosa; na kama anajua kwamba namba ya NIDA aliyonayo, yale makosa yataandikishwa kule, basi anakuwa na uwoga zaidi kwa sababu inakuwa ni rahisi kumfuatilia mtu makosa aliyofanya na mazuri aliyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na inakuwa ni rahisi sana hata kwa mabenki kuweza kumfahamu huyu mtu ni wa namna gani wanaku-access katika database ile ambayo itakuwa imefungamanishwa kwa watu wote, iwe ni simu na kila kitu kitakuwa kule. Naamini kwamba kwa zile reference bureau nazo zitaingiza database yao huko. Kwa hiyo, tutakuwa tunaweza kufanya mambo kama hayo. Nchi zote zilizoendelea zinafanya hivyo, mtu anakuwa na namba moja, hawi na namba mbili, na ninaamini kwamba kitambulisho kinakuwa ni kimoja siyo viwili ili mtu yule aweze kutambulika kila mahali anapokwenda na saa yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba sekta ya TEHAMA ndiyo inayokuwa kwa kasi zaidi sasa. Sasa tumeunda Wizara ya Teknolojia na TEHAMA kwa ujumla. Nataka niseme hivi, fursa zilizopo ni nyingi sana, nchi nyingine zimeamua kufanya kwamba TEHAMA ndiyo sekta ya muhimu kuliko zote; nchi kama Rwanda mnafahamu. Nia yake ni nini? Ni kwa sababu wako vijana wengi wanapokwenda shule na kwenye vyuo wanajiunga kwenye hii fani, lakini kuwatumia inakuwa vigumu. Kwa sababu hakuna mitandao inayofanya kazi vizuri kwenye maeneo yale ambayo vijana hao wanamalizia shule zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna mkonga, kwa nini hatuwezi kuwezesha Wifi ikapatikana kwenye maeneo mengi tu hata kwa bure? Nami nakubaliana na mwenzangu aliyesema kwamba TTCL ikiwezeshwa ikatumia mkonga huu ikawekeza vizuri kwenye maeneo mengi ya vijijini, siyo mijini tu, vijijini zaidi kwa sababu kuna fursa. Sasa hebu niulize kwa mfano, masoko sasa hivi hayatafutwi kwa mtu kusafiri kwenda kuangalia soko, mtu anatumia simu, hii simu imekuwa ni ofisi, huhitaji ofisi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nawaambia wapigakura wangu kwamba hii simu ni ofisi yenu, huna haja ya kwenda kutafuta mnunuzi wa ndizi Dar es Salaam wakati unaweza ukapiga ndizi yako picha ukaituma kwa rafiki yako Dar es Salaam akakwambia nitumie kwa shilingi fulani, umeshafanya biashara. Kwa hiyo, biashara unaweza ukaifanya kwa kutumia tu kiganja chako na uwe na simu, lakini iwe janja kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niombe hiyo kwamba kweli tufanye hivyo. Pia Wizara ione namna ya kutoa mafunzo kwenye vyombo vya Habari; kwenye TV na kwenye redio, kueleza watu ni fursa zipi zinafunguliwa kwa kuwa na uwezo wa kuwasiliana nchi nzima na nchi za jirani, hata dunia nzima inawasiliana na hii simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vile vile lazima gharama zipunguzwe. Sasa tutapunguzaje gharama? Nafikiri kwamba tunavyozidi kuongeza mtandao, hasa huu wa TTCL; na tunaamini kwamba wataweza kuleta ushindani ambao utalazimisha wale wengine ambao wanafanya tu biashara waweze kushusha bei zao, lakini ni lazima TTCL ifanye kazi kwa nguvu zaidi. Kwa hiyo, naomba kwamba kuwepo na hivyo vipindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Mheshimiwa alizungumzia kuhusu technology hub. Tuna COSTECH, imeweza kuanzisha incubation centers na hizo incubation centers ndiyo zinachukua na zinashindanisha; unaweza ukatangaza kwamba watu wenye uwezo hasa wale waliosoma IT, ambao wana ubunifu wowote wa teknolojia, waweze kufikisha pale. Hiyo ndiyo njia ambayo itaweza kuwaajiri hawa vijana na pia ku…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kimei kwa mchango mzuri.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru sana kupata fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ambayo inamajukumu makubwa sana hususani katika kipindi hiki.

Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwapata watu makini wanadiplomasia makini kuongoza Wizara hii. Namfahamu sana Mheshimiwa Mama yetu mpendwa Balozi Mulamula, kazi aliyofanya kujenga diaspora pale Washington na Marekani kwa ujumla na ninaamini sasa tutaona tofauti kubwa kwenye suala hili la diaspora kwa sababu ni mtu anayelifahamu, anafahamu uwezo wa diaspora kuchangia kwenye maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaamini kwamba suala linalozungumzwa la dual passport (passport pacha) litashughulikiwa, lakini pia tukijua kwamba hawa watu hawawezi kuja kuwekeza kwenye nchi ambayo siyo raia, hata kuweka akiba tu wakitaka kufungua account kwenye mabenki yetu inakuwa shida. Kwa sababu wanaambiwa onesheni passport ya Tanzania, kwa hiyo, inakuwa kwamba akiba nyingi ambazo tunaweza tukazileta remittances kutoka nje huko, kutoka kwa diaspora, ambako kwa nchi nyingine zinachangia sehemu kubwa ya pato la Taifa, mpaka asilimia tano kwa watu wa Ethiopia inachangiwa na watu wa diaspora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwetu hata ukisema unahesabu haifikii hata 0.1 percent of GDP. Kwa hiyo, ina maana tunapoteza uwezo, lakini pia tunapoteza nguvu kazi ambayo ina uzoefu tofauti na wana-skill tofauti, ambayo wakija hapa wakiwa na uhuru wa kuja na kuondoka wataiacha hapa nchini. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba mimi ninamuamini sana kwamba sasa kwenye Wizara hii tumepata watu Mheshimiwa Mbarouk na Mama Mulamula naamini hawa watatufanyia kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye suala zima la diplomasia ya kiuchumi ambalo limezungumzwa na wengi. Mimi ningesema hivi, hauwezi kuwa na Balozi ambazo hazina wafanyakazi wa kutosha, tunataka Balozi ziwe na wanamasoko, zamani ilikuwa ni trade attachees, wanakaa kwenye Balozi kazi yao ni kuzunguka na kuangalia ni nani anawekeza, nani mwenye interest, nani anauza nini kwenye masoko yale na kuunganisha watu wetu na wale watu kule pamoja na wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nataka niombe kwamba tusiseme tu kwamba tunapeleka mabalozi wazuri tupeleke pia wafanyakazi wa kutosha kwenye Balozi hizi na tusifungue tu Balozi nchi kama China jamani unakuwa na Balozi moja kwa nini usifungue consul nyingi miji mingi kule Thailand, miji hata mitano tukawa na consulars. Tukiwa na hizo ofisi ndogo ndogo za Balozi, zitakuwa na watu ambao sasa sio tu wanadiplomasia, sasa hivi tutawapeleka watu ambao watasaidia kwenye mambo ya masoko, kwa sababu masoko yako Guangzhou yako na sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba nimeona mmefungua Ofisi ndogo kule Mumbai, tufanye zaidi China jamani ni Taifa la kimkakati, lakini yako mataifa mengine kama Marekani, Uingereza pengine Ujerumani na wapi pia ni ya kimkakati basi tufanye mbinu ya kuongeza presence yetu kwenye hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kingine ambacho ningeomba kuzungumzia ni issue ya ushirikishwaji wa wafanyabiashara kwenye safari za viongozi wetu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwamba alivyoenda Kenya juzi hapo alianza kutuonesha mfano mzuri kwamba anachukua watu waliochujwa, wafanyabiashara waliochunjwa kutoka TPSF pamoja na may be CTI pamoja na Mawaziri. Lakini ukweli ni kwamba, wakienda wenyewe hawa wafanyabiashara wanakuwa wanajua na watakuwa wamelenga na wanaunganishwa na watu ambao wataleta uwekezaji haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kila mtu atataka mbia, wewe ukiwa hapa ndani ukitaka kuanzisha biashara kubwa ni lazima uwe na wabia kutoka sehemu hizo na mimi ninaamini hili linakuwa na tija na ninaomba kwamba liendelezwe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni kwamba tumeona pia kwamba mmejaribu na ninawapongeza sana Wizara, kusema ukweli nawapongeza Wizara kwa sababu wamejaribu kuunganisha wajasiriamali kwenye maonesho ya viwanda nimeona kuhusu China na NMB wameweza ku-sponsor, wameweza kutoa ufadhili kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri hili ni jambo la kuomba sana kwamba liendelezwe, lakini na mabenki mengine au na wafadhili wengine hata wabia wenyewe watu wa maendeleo tuwaombe waweze kuchukua vijana wetu kwenda kuona, kwa sababu kuona ndiyo kuelewa na ndiyo kuamini. Kule China viwanda vidogo vidogo vimejaa na bei zake ni bei chee kabisa, unaweza kununua kiwanda kidogo cha shilingi hata laki tano ukaja nacho hapa ukachakata vitu, ukatengeneza fedha, ukawa tajiri, tena tuna umeme. Kwa hiyo naamini kwamba, tukiwapeleka wale vijana kule wakiona hata wale wanaofanya kama mashamba wataunda vitu ambavyo ni demonstration tukiwapeleka wale wachache, lakini watakuja kuwaonesha wenzao kwamba ni possible kufanya vitu vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ni ujenzi wa maofisi ya Balozi ambapo ni vizuri tujenge, nimeona kwamba wanamkakati wa kujenga hizo ofisi, nilikuwa nasema kwanini tusitumie mortgage financing kule? Bei ya mkopo kule Marekani au Uingireza nchi nyingi bei ya mkopo riba ni asilimia mbili na hususan ya mortgage. Tunaweza tukachukua mortgage zile na kwa sababu hatuna mtaji wa kutosha wakati huu kwa sababu tunawekeza kwenye miradi ya kimkakati basi tunaomba mkopo kwenye benki ya kule, tunachukua mortgage ile fedha tunaipeleka Balozi kwa pango ikatumika kama ni fedha ya kulipa mortgage na baada ya miaka siyo zaidi ya 10, 20 mnakuwa mmeshalipa mortgage, nyumba ni yenu na hamjatoa fedha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati mimi nafurahi kwamba NSSF walitaka kufanya vile, lakini ilikuwa pia siyo nadharia nzuri, kule mortgage ni kitu straight forward. Kwa hiyo, tunaweza tukafanya, tukakopa kwenye benki kule balozi ikajengwa wakakaa lakini wanajipa ile mortgage kwa fedha ya pango. Hata wafanyakizi wa balozi wanaweza wakafanya vile. Naomba sana hilo lizingitiwe kwa sababu naamini litaweza kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ninataka niseme kwamba, nimefurahishwa sana na nilivyosoma kwamba kwenye taarifa ya utekelezaji ya mwaka uliopita, wameweza kufanya vitu vingi, miradi mingi ambayo wemeweza kuhamasisha kutoka kule na nikasema kwamba kweli Wizara hii imechangia vizuri na ninawapongeza kwa sababu huu ulikuwa ni mwaka mgumu sana ni mwaka wa ku-survive, lakini bado tunaweza kupata miradi, tunaweza kupata ufadhili wa kutosha kutoka kwenye nchi mbalimbali na tunaweza kupata wawekezaji.

Mimi nawapongezeni na ninaamini kwamba kweli tukitia nguvu kwenye Wizara hii basi uchumi wa kati wa kipato cha juu unaweza ukafikika kwa kipindi ambacho tunataraji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana kwa Jimbo letu na kwa Mkoa wetu wa Kilimanjaro. Nawashukuru na nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu wake kwa kuwa wenye mwamko chanya katika kushughulika na matatizo yetu kwenye mikoa yetu hasa sisi ambao tunapakana na hifadhi na tunasimamiwa na TFS ambayo imekuwa inanyanyasa sana watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuzungumza jambo moja hili la nusu mile na natumaini limezungumziwa vizuri sana, nusu mile ni kitu ambacho kwetu kinatuuma kwa sababu kama mnajua kwamba ardhi yetu kule Kilimanjaro ni ndogo, lakini pia ukiwa unapakana na msitu huu unaozunguka Mlima Kilimanjaro unakuta kwamba fursa iliyopo ni kuokota kuni, kukata majani, kuweka mizinga ya nyuki na kadhalika. Mwanzoni tuliruhusiwa kuingia hadi nusu mile hiyo, lakini baadae TFS wakang’ang’ania kuchukua hata eneo hilo, walikuwa wanaturuhusu hata angalau wanawake waingie kukata kuni na kuchukua majini, lakini sasa hawaruhusiwi. Naomba hilo jambo lifikiriwe na nimeshazungumza pamoja na Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu, naamini kwamba litakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nazungumzia kuhusu stimulus package kwa sekta hii muhimu ya utalii. Naamini kwamba wengi wanaelewa jinsi ambavyo watu wameathirika; mahoteli yameathirika, hayajatengeneza fedha, yametengeneza hasara kwa muda mrefu na hawa tour operators pia wametengeneza hasara. Hivyo nafikiria itafaa kujua ni namna gani ya kuweza kuwanusuru kwa kuwapa muda kama wana mikopo, kama wana tozo wanadaiwa kwenye vitalu au kwenye maeneo yao wanayoshughulika nayo, Serikali iweze kuona ni namna gani ya kuwanusuru kwa kuwapa muda mrefu wa kulipa au kuwasamehe kwa maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme pia kwamba kuna tatizo baada ya hilo na kama ikiwezekana naamini linawezekana kama tukilifikiria vyema, tukijua hii ni sekta muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni issue ya tour operators; niliwahi kuzungumza kuhusu tour operators hapa. Tour operators wameunda jumuiya yao kule kwetu Kilimanjaro kupandisha watalii mlimani. Wameunda hii jumuiya ili kui-serve na kui-regulate; waweze kujiwekea discipline na namna gani wanapandisha watu na nidhamu katika kushughulikia watalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa walikuwa wanafikiri kwamba ni vizuri ili waweze kujadiliana vizuri malipo yao na tour operators waweze kupata au waweze kupewa fursa ya kujadiliana na wawekezaji wa tour operators na pia kujichagua wenyewe nani anapandisha huyu kwa vile anajua Kiswahili, Kifaransa na kadhalika. Kwa hiyo tunaomba kwamba tour operators wapewe mwongozo huo wa kutumia jumuiya hiyo ili waweze kupandisha watu/watalii mlimani wakiwa wamekaa vizuri na mtalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, watalii hawarudi kwa sababu hawawi-treated properly, lakini wakitumia jumuiya hiyo ambayo ni wataalam watawaweza wakawa-treat na wale ambao wanafanya mambo ambayo siyo ya kinidhamu, wakashughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni suala zima la utalii wa vivutio vya kiasilia. Watu wanasema kwamba kivutio cha kiasilia hapa Tanzania ni Mmasai tu, kumbe kuna vivutio vingi, kuna mahandaki, kule kwetu Mamba, Komakundi kuna mahandaki ambayo ukiingia utashangaa, utafikiri upo mahali tofauti kabisa, kule Tanga - Amboni; sio Amboni, watu wamechimba kujificha wakati wa vita, kuna mengi ya namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi pia kuna vivutio kwa mfano, namna watu walivyokuwa wanafua vyuma asilia, uhunzi kule kwetu watu wanafua, wanatumia namna ambayo ni teknolojia ambayo ni ya kizamani lakini watalii wakiona wanashangaa ni kitu gani kinafanyika. Kwa hiyo, nashauri, tusing’ang’anie tu hifadhi ya misitu, hifadhi za wanyama na kadhalika, tuanze sasa kuunda kitengo maalum ambacho kitashughulika na vivutio asilia, vitangazwe na viorodheshwe, ni wapi utaona nini na wapi utafanya nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Waziri na Naibu wa Wizara hii kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa kwenye kutatua matatizo ya migogoro ya ardhi. Ninapongeza pia Katibu Mkuu pamoja na uongozi mzima wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya ya Moshi Vijijini, hususan Mji Mdogo wa Himo, kumekuwepo na migogoro mingi inayosababishwa na Maafisa Ardhi kufanya double allocation kwa nia ya kujipatia rushwa. Aidha, wafanyabiashara wachache wamejirundikia maeneo makubwa na mji ni kama vile umekuwa mali ya matajiri wachache. Tunaomba Wizara iingilie kati na kugawa maeneo yaliyohodhiwa bila kuendelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa kwenye Wizara ni ucheleweshaji wa vibali vya kujenga, pamoja na utoaji wa electronic titles jambo ambalo tuliahidiwa lingefanyika kwa haraka, inachukua muda mrefu na ingekuwa vizuri kuchapisha kwenye vyombo vya habari titles ambazo ziko tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna umuhimu wa kutenga maeneo ya kilimo kwenye kila Halmashauri kwa wawekezaji wakubwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nimewasikiliza wenzangu vizuri sana lakini kabla sijasema hapo, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumpongeze yule aliyekuwa anashikilia Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ambaye aliweza kusimamia Ilani ya CCM tukaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na tukapata ushindi sisi tunaoingia sasa kama Wabunge. Naona ni vigumu sana kujua walifanyaje wakaweza kutekeleza miradi hiyo na hali kwamba deni letu likabakia bado himilivu.

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa najua kwamba bajeti ni sheria, lakini naamini hii ya kwetu siyo sheria, kama inatungwa bajeti tumekaa hapa miezi mitatu tunatunga bajeti hapa halafu tunaambiwa imetekelezwa kwa asilimia 50; nani anashikwa, nani anapelekwa kortini? Nani anawajibika kwa hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri lazima sisi wenyewe tujue kwamba sisi ndio tunatakiwa tuwajibike pengine kwa sababu hatukuweza kuisimamia Serikali ikaja na bajeti ambayo inatekelezeka kwa asilimia mia moja, ahadi zinazotolewa hapa zikatekelezwa kweli. Wewe utaahidiwa mradi lakini mradi hautatekelezeka kwa sababu kama mapato hayatapatikana hatutapata hiyo miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina shaka sana kwa sababu tunajua kwamba kazi kubwa ya Wizara ya Fedha ni kutafuta mapato, matumizi tumeshajua, kwa hiyo ni kutafuta mapato yatakayokidhi utekelezaji wa bajeti ile. Sasa mapato yanatokana na kodi au kukopa.

Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri sana Waziri achakarike aanze kutafuta mikopo, siyo ya ndani. Naona wenzetu alipokuwa Mheshimiwa Msuya alikuwa kila saa yuko nje anatafuta fedha za kuweza kutekeleza bajeti, siyo lazima upate yote ndani, na ukipata yote ndani ndiyo inasababisha haya mambo tunayoona sasa kwamba mwenzangu anasema kwamba riba ziko juu sana.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya amesema kwamba Benki Kuu ndiyo inapangia benki viwango vya riba, lakini Benki Kuu kusema kweli haipangii mabenki viwango vya riba isipokuwa wanakuwa ni waelelezaji kwa zile riba ambazo wanatoa kwa dhamana za Serikali.

Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri hakuna ongezeko la mshahara, badala yake mishahara inapungua… lakini nataka niseme kwamba pengine ni muda sasa wa kufikiria ongezeko la mshahara kwa wafanyakazi wa Serikali. Kwa sababu ni miaka mitano na … tulisikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba ataona namna, lakini kama hatujaingiza kwenye bajeti inakuwa kwamba ni matatizo. Hakuna Wizara hata moja iliyoonesha kwamba kutakuwa na ongezeko la mshahara, na mimi nataka Waziri wa Fedha aliangalie kwa upya aone litafanyikaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kupunguza makali ya utekelezaji wa miradi yetu, naamini kwamba Serikali inatakiwa kuangalia upya msimamo wake wa kurejesha kwa Msajili wa Hazina yale mashirika yaliyokuwa yamebinafsishwa sekta binafsi ikashindwa kuyaendesha halafu Serikali inarudisha. Kitu ambacho kimeshindikana kwa sekta binafsi kwa biashara, Serikali haitaweza.

Mheshimiwa Spika, unless unasema kwamba hiyo ni mkakati kama Air Tanzania. Kama ni Air Tanzania twende kwa sababu tunajua ni mkakati, basi. Lakini lazima tuangalie ni mashirika yapi; ni viwanda au ni taasisi zipi ambazo zilikuwa zimebinafsishwa halafu zikarejeshwa, tuone mkakati wake uko wapi. Kama upo then tuendelee lakini siyo hivyo, tunaona kwamba Msajili wa Hazina ametoa ruzuku na nyongeza kwa mitaji ya mashirika takribani shilingi bilioni 27. bilioni 27 ni hii 500 tumepewa kwenye majimbo yetu mara tatu? Kwa hiyo, naomba hiyo iangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi; mimi nafikiri katika mambo yote ya kukusanya kodi ambayo ni kazi kubwa ya Wizara, mahali penye leakage kubwa ni kule kwenye Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa hawakusanyi, na wakikusanya zinaingia mifukoni mwa watu. Kwa nini tunawaambia kwamba waingie kwenye GEPE, muda mwingi kule kwenye vijiji vyetu kwenye halmashauri hakuna mawasiliano, hawana Point of Sale za kukusanya hayo mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unakuta kwamba ukimpa mfanyakazi Point of Sale akatembea nayo barabarani huko, haina hata risiti ile roll imekwisha, unakuwa ni mtaji kwake na ukimnyang’anya analia machozi ya damu, anakwambia umrudishie hiyo Point of Sale kwa sababu anajua kwamba ni njia rahisi sana ya kupata mtaji wa bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na naomba kwamba ili mradi hatuwezi kusambaza Point of Sale za kutosha kwenye halmashauri zetu, kwenye vijiji kwa sababu na kule wanakusanya kodi, tusiseme kwamba tutakaa tu tuangalie halafu tutakusanya kodi au tutaongeza wigo wa kodi. Naamini kwamba kwa wale walio kwenye wigo wanalipa na wanafuatiliwa lakini kwenye sehemu nyingi watu hawafuatiliwi.

Mheshimiwa Spika, na kitu kitakachotupa mapato kwenye mwaka huu ni usimamizi mzuri. Kwa sababu kwa muda mfupi hatuwezi kuongeza wigo wa walipa kodi, hatuwezi kuongeza kwa siku tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niseme pia kwamba kwenye suala hili la riba za Serikali, kwa sababu unajua kitu kinacho- drive deni la Serikali zaidi ni riba kubwa. Na ninasema kwamba uhimilivu wa hili deni hautakuwepo kama riba zitakuwa kubwa. Na riba zimekuwa ni asilimia 15.9, alisema mwenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanapokea hiyo, mkopo, kama ni mkopo umelimbikiza mwaka mmoja unaongezeka kwa asilimia 15 na zaidi. Kwa hiyo, inakuwa kwamba hutaweza kabisa kulipa. Tunalipa asilimia 25 ya mapato yetu kwenye ku-service deni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri hivi; njia pekee ni kwamba sasa tukubali kwamba inflation au mfumuko wa bei ni asilimia tatu. Na kwa kawaida huwezi kuwa na zaidi ya asilimia nane hapo kwa sababu unaongeza hapo asilimia tano, asilimia tano ndiyo inakuwa ni riba ambayo inakubalika. Inakuwa inflation plus five percent ni eight percent, kwa hiyo, ukiwa juu ya pale ni matatizo, ni majanga kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachowashauri Benki Kuu na Waziri wa Fedha ni kwamba ile coupon rate ya dhamana za Serikali wanayotoa Benki Kuu, kwa sababu wanasema tuna option na riba itakuwa ni asilimia 15.6. Kwa hiyo, kila mtu anakwenda ku-bid, ananunua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ile coupon rate inayotangazwa asitangaze tena sasa ya asilimia 15, atangaze asilimia kumi; mabenki na wawekezaji wengine hawana mahali pa kuwekeza fedha zao salama zaidi ya kuweka kwenye dhamana. Kwa hiyo, ina maana kwamba watakwenda watu watanunua tu, hakuna njia nyingine kwa hiyo watanunua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ni kweli kwamba hiyo faida watakayopata bado ni kubwa kwa sababu ni risk free, hawana gharama yoyote, wanakusanya tu bure. Kwa hiyo, naamini kwamba kama tukisema kwamba, okay, kuanzia minada inayokuja, coupon rate yetu itakuwa ni asilimia kumi, anayetaka aje, asiyetaka asije. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya muda watakuwa na maukwasi yamerundikana wataamua kuja kununua kwa asilimia 10. Na hiyo itasaidia pia kushusha riba za mabenki binafsi kwa sababu riba zimelegezwa kwenye riba hizi za dhamana za Serikali. Kwa hiyo, hakuna njia nyingine ya kushusha riba kwenye mabenki kama siyo kufanya hicho, kwamba hatutauza dhamana kwa juu ya asilimia kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wanauza treasury bills chini ya asilimia tano, za mwaka mmoja. Sasa kwanini na zilikuwa asilimia 14? Sasa ameshusha, inakuaje kwamba wameshusha hizo za na nanii, na tunajua kwamba upeo wetu wa inflation ndiyo hiyo asilimia tatu. Hakuna sababu ya kushindwa hicho kitu. (Makofi)

Niombe kwamba ikiwezekana, hasa kwenye mambo ya ugawaji wa fedha, wenzangu wamesema, lakini ukweli kama hatutagawa fedha kwa vipaumbele au kwa kuzingatia kasma, hatutakwenda mbali…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …kwa hiyo Wizara ipeleke kufuatana na jinsi ambavyo imepitishwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza hotuba nzuri ya Waziri wa Viwanda na Biashara, nampongeza yeye mwenyewe Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Wizara kwa kazi nzuri na ubunifu katika kutekeleza Sera na Ilani ya chama tawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha sana ni Wizara hii inayobeba dira ya Taifa letu kwa sehemu kubwa kutokupewa kipaumbele cha kufikishiwa fedha zilizoidhinishwa kwenye bajeti ya maendeleo. Kwa mwaka 2020/2021 ilipata chini ya asilimia 50 ya bajeti na hivyo kushindwa kutekeleza miradi ambayo ingewezesha kujenga misingi bora ya kuwezesha wananchi wajasiriamali kuanzisha shughuli za uzalishaji na kutengeneza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa majengo/ mabanda ya kuwapangishia wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati ni falsafa nzuri kwani inawezesha pia kuwafikishia wajasiriamali hawa huduma na mafunzo mbalimbali, na pia kuwasimamia wale wanaopewa mikopo na SIDO kutumia mikopo hiyo vizuri. This be Serikali ikubali kutenga fedha nyingi zaidi kwa utekelezaji wa mkakati huu na kwa Mfuko SIDO wa kuwezesha wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashirika ya TIRDO, CAMARTEC, TEMDO yanafanya ubunifu mzuri na unaozingatia uwezekano wa kupeleka kwenye soko letu teknolojia sahihi kwa mazingira yetu na kwa bei nafuu. Hata hivyo taasisi hizi hazipati bajeti za kutosha kujitangaza na kupeleka taarifa sokoni kwa walengwa ili wazijue na wazinunue. Kwa namna hii zinapoteza tija. Wapewe rasilimali fedha na watu wa kueneza kile walichobuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mashirika mengi yaliyo chini ya Wizara hii hayana bodi. Hii inapunguza kiwango cha utawala bora. Tuiombe mamlaka husika ifanye uteuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa blueprints unastahili kuongozwa na Wizara hii licha ya kwamba Wizara nyingine zina maeneo yao. Blueprint inatekelezwa kwa kasi ndogo, lakini kuna haja ya kufanya tathmini mpya kuhusu kero mpya zilizoibuka kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Kero zilizoorodheshwa miaka mitatu iliyopita zimepitwa na uhalisia wa sasa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa Fedha Haramu wa Mwaka 2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa fursa hii. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kukubali kwamba muswada huu uje kwa hati ya dharura. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu wake na timu yake kwenye ile Wizara pamoja na Mwanasheria Mkuu na CPD kwa kuweza kuwa wasikivu sana katika kusikiliza hoja ambazo zimetolewa na ndiyo sababu tukaona kwamba ile draft iliyokuja imebadilishwa kwa namna ambayo inaridhisha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba nimekuwa reporting agent kwa miaka mingi sana, miaka kama 13, kwa hiyo najua namna gani nchi itafaidi kutokana na suala hili la kuweka sheria na sera ambayo najua itakuja baadaye itakayoweza kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu pamoja na ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa proliferation ya weapons of mass destruction (silaha za maangamizi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba mimi ninavyouona na nafikiri kwamba wananchi wataelewa vizuri, kwamba sasa nchi yetu inajiingiza kwenye mfumo wa kimataifa wa malipo (international payment system), tunaingia sasa tukiwa na hadhi tofauti na ile ambayo tulikuwa tunaonekana. Kwa sababu hiyo naamini kwamba itaipa heshima hata passport yetu, ukiwa unasafiri sasa unakwenda mahali popote kwenye nchi nyingine mtu akikuona hakushuku kwamba huyu mtu anaweza akawa amebeba fedha ambazo ni haramu, hutaweza kupekuliwa sana pengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hiyo, ni kwamba inainua hadhi ya mabenki yetu. Mabenki yetu mengi yale madogo na ya kati yamepata shida sana katika kufungua akaunti na mabenki mengine ya nje ili waweze kufanya miamala na akaunti zile za mabenki mengine kwa sababu mabenki mengine huku nje yanahisi kwamba mabenki haya hayajajiweka sawa katika kudhibiti fedha haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo imekuwa vigumu sana kupata correspondent banking relationships ambapo hakuna benki inayoweza kufanya biashara vizuri bila kuwa na mahusiano na mabenki ya nje. Naamini sasa watakwenda kufungua milango ile na mabenki yale ambayo yalikuwa bado hayajaweza kufungua badala ya kupitia milango ya nyuma au migongo ya mabenki makubwa, nazo ziweze kuingiza biashara yake kwenye mifumo ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba of course kuna faida za kiusalama kubwa na naamini kwamba hilo limefanyiwa kazi vizuri na haitakuwa tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi; kwa wale ambao hawajui kitu gani kinafanyika, kushuku miamala ni nini? Unashuku kitu ambacho ni abnormal kwenye mtiririko wa mapato ya mtu au kwenye akaunti ya mtu. Naamini kwamba huu muswada umekwenda mbali sana, kwa nchi nyingine nyingi kwa kiwango cha kimataifa watu wanaofanya ripoti hizi, wanaotoa taarifa hizi ni financial institutions, mabenki na taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumeweka na wengine wengi, kwa hiyo naamini sasa tutaonekana kama vile tuko juu ya kiwango cha kimataifa, kwa sababu tunasema hata customs wataripoti. Of course, customs watakuwa wanaripoti kwa sababu ya fedha zinazopita mipakani lakini naweza kusema kwamba kwa wale wengine, kwa mfano car dealers et cetera pengine hawataripoti kwa sababu hawataona kitu chochote cha kuripoti, hakuna mtu ambaye hataki kuuza halafu uende kwake kuuliza maswali 20 anapotaka kukuuzia gari, lakini itaonekana kwenye akaunti za mabenki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba ultimately the major reporting person itakuwa ni taasisi za kifedha na watu wasiogope kwamba eti kila mtu atakuwa reporting agent, haitakuwa hivyo. In fact, itakuja kugeuga kuwa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja ambalo naliona, hii issue ya elimu; wananchi wanaogopa kwamba ukiweka fedha benki unakuwa reported kila wakati, kumbe hapana. Ile hela yako iliyo kule benki kama ni deposit yako haiwi reported kinachokuwa reported ni ile miamala ambayo inapita kule ambayo inaonekana kwamba haihusiani na kitu unachofanya. Kama wewe ni Mbunge halafu suddenly ukaingiziwa shilingi milioni 50 na hujui zimetoka wapi, lazima benki itaripoti na utatafutwa, lakini siyo ile balance, haina tatizo sana, siyo muamala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kushauri hapa ni kwamba elimu ifanyike kama walivyosema wenzangu, kuwe na elimu kwa wananchi waelewe kwamba ni namna gani haya mambo ya kushuku yanafanyika, inatokea wapi na implementation ya sheria hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho niseme kwamba, ibara ya 12 kifungu cha 15 kwenye ile iliyorekebishwa kinaweka sharti la kufanya tathmini ya viashiria hatarishi vya utakatishaji wa fedha. Sasa haijaweka itafanyika kwa muda gani; itafanyika kila baada ya miaka mitano au baada ya miaka kumi au kila mwaka? Sasa zoezi la kufanya tathmini lina gharama sana na ndiyo sababu halifanyiki hovyohovyo, gharama zake ni za juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba kama pengine kwenye kanuni zitakazozungumzwa na Mheshimiwa Waziri, ziweze kuainisha hilo kwamba hii tathmini haitafanyika hila mwaka itafanyika baada ya miaka mitatu au baada ya miaka mitano au kitu kama hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hilo ni la msingi na naamini kwamba kweli tukipitisha sheria hii ambayo naiunga mkono kwa asilimia 100, basi tutakuwa tumeiweka nchi yetu kwenye hadhi iliyo juu sana katika masuala haya ya fedha haramu pamoja na utakatishaji fedha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, nianze kwa kumshukuru na kumsifu na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa msikivu na kuelekeza baraza lake la mawaziri vizuri.

Nimpongeze pia Makamo wa Rais nimpongeze Waziri Mkuu, nipongeze baraza zima la Mawaziri, pia nimpongeze sana kipekee kabisa Mheshimiwa Dkt. Nchemba kwa hotuba nzuri aliyotoa jana, na kwa kuwa ni msikivu sana, la tatu nisema kwamba ametendea Ph.D yake haki jana, allitoa mada yake alitoa hoja yake vizuri na ninaamini ndio sababu wengi wanapenda kuchangia kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ukiangalia mswada ambao umeletwa Mbele yetu, ni mswada ambao unakidhi matakwa ya kufikia malengo ambayo ni makubwa kwa bajeti yetu ya 2021/2022 pamoja na mpango wetu wa maendeleo ambao nitasema kwamba ni ile miradi ya kielelezo ambayo tunajua itapata fedha, kuendeleza miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii, kujenga mazingira Rafiki kwa wawekezaji, blue prints na hasa jana tukasikia Mheshimiwa Waziri anasema nini, kwamba hata areas au yale madeni ambayo privet sector wa contactors hawajalipwa yanaweza yakalipwa pia kutokana na fedha hii ambayo itapatikana ya ziada, kutokana na ubunifu ambao imejitokeza kwenye kuangalia na kubuni vyanzo vya mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ukijumlisha zile fedha ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha jana alizielezea kwamba ni za ziada na zitapelekwa kwenye maeneo mbali mbali, unaona kwamba sasa tunaweza tukakusanya kitu kama tilion 26, ndio mapato ambayo yanayijitokeza kwa hesabu za haraka haraka, hii inamaana kwamba tunakusanya mapato ambayo ni asilimia 17.5 ya pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakuwa tumefanya tax effort kubwa sana, kwa hiyo tatizo kubwa letu kwenye hii bajeti na kuhakikisha kwamba tunatekeleza tukae mpango wa kukusanya vizuri, inamaana gani? Inamaana kila mtu Serikalini hata sisi wabunge tuhakikishe kwamba ile elimu kwa walipa kodi inakwenda na kwamba tunafanya kila kinachowezekana ili Serikali ipate pato lake na ili hii miradi iweze kutekelezeka na sera yetu na bajeti yetu iwe na muoleleo huo ambayo sasa unaona kwamba itaendelea kupunguza in-quality katika mapato ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapotumia fedha nyingi kwenye huduma za kijamii, na kutumia fedha nyingi kwenye miundombinu ya kiuchumi inamaana kwamba inapunguzia mtanzania, inampunguzia mwananchi wa kawaida mzigo wa kulipa kwa sababu anakuwa amepata bure kama kapata bima ya bure inaama unakwenda kutibiwa bure, inamaana fedha haikuingia mfukoni mwako lakini imekusaidia wewe sasa kuongeza kipato kwa njia ambayo ni in direct. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi kwamba nafikiri katika yote yanayo zungumzwa, jambo muhimu ni kutengeneza ile guideline au mwongozo wa kutekeleza hizi kodi mpya zilizokuja. Kodi ya luku, kodi ya majengo kupitia luku, kama ile program ambayo alikuwa ametueleza Waziri hapa jana, program ambayo inatengenezwa kuweza kukusanya kupitia luku. Kama haijakamilika upesi tutacheleweshwa, na inatarajiwa kwamba wakati huu kodi hii ya mapato imebuniwa kutoa au imekadiriwa kutoa fedha nyingi sana kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kodi inayotozwa kwenye fedha za mobile money na airtime. Sasa niseme kuna wakati ule tulivyoingiza extra duty on financial transition, TRA iliwachukua muda mwingi sana kuja na guideline ya kwamba itatozwa namna gani. Nawaomba watu wa TRA wapo hapa wafanye haraka ili kuwa muongozo uende kwa wale wanaohusika wale wadau wetu ambao ni makampuni ya simu na mabenki waweze kujua kwamba wana-adjust mifumo yao pia kuweza kukusanya hiyo fedha electronical, hiyo ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili ni issue hii ya uwezo wa Tanzania Revenue Authority mamlaka ya mapato, kusema kweli unaambiwa kwamba kwenye majimbo au halmashauri waajiriwa wa TRA ni wachache sana. Sasa kama TRA haitajipanga haitaongezewa rasilimali watu na rasilimali fedha naamini kwamba hatutafika. Kitu kikubwa katika utengezaji wa sheria hii ambayo itakuja kutufinya sisi wenyewe kwa vile tutakuja shindwa kitekeleza na tutashindwa kusimamia Serikali, kikuwa ni kwamba uwezo wa kukusanya hayo mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ni mengi na inaonekana kwamba vianzio ni bunifu sana, naamini kwamba tukikusanya tutafika pazuri na tunaweza kutekeleza malengo yetu ya bajeti na malengo wa mpango wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme hivi kuna mambo ambayo tunaona kwamba yangeweza yakaongeza revenue base yetu au taxi base yetu, moja ni kufanya Dar es Salaam iwe a logistic hub kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa hivyo unfortunately Inakuwa na vikwazo vingi lakini moja wapo ni East African Customs Management Act, inakuwaje hivi, kwa sababu huku kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki axle load inayokubalika ni maximum thirty tonnes huku ambako ziko mizigo mingi inakwenda mizigo inapita sasa hivi Dar es Salaam sasa hivi mingi inaenda SADC, sisi pia ni watu wa SADC ni jumuia ya SADC. Sasa hatuwezi kubeba mzigo iende Kongo inazidi au iende Zambia au iende huko kusini kwetu Mbeya inazidi tani 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utakuta kwamba watu wengi na tunaambiwa na watu wa TPA kwamba meli nyingi hasa zinaenda Beira kwa sababu kule wanaruhusu axle load ya 50 tonnes. Sasa mimi nataka niseme hivi tujaribu nataka pale wenzetu kwenye jumuia ya wenzetu partners wajue kwamba sisi iyo inatuzuia maendeleo, hiyo ya kuzuia mzigo mkubwa wa tonne 50 kupita kwenye barabara zetu ni jambo ambalo haliwezi ku-facilitate industrialization kwetu kwenye zone ya kusini au hata kuwasaidia wenzetu kupitisha mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri hiyo ikitokea inaweza kuwa njia pekee au njia kubwa ya kutupa mapato siku za Mbele. Sasa niseme pia kwamba hili la ushuru wa bidhaa ya pombe tamtam hizi kali, nafikiri hivi ukweli ni kwamba miaka mitatu au zaidi huku nyuma bei hazikuwa zinaongezwa kwa kasi ya mfumuko wa bei, sasa ukichukua compound rate ya three point of inflation kwa miaka mitatu tu inakuja 3x3x3 ni 27, kwa hiyo wazee wa fedha inakuja na 30 it was within. Sisi tukasema hapana kuja kwenye Kamati ya Bajeti ikasema hapana punguza kidogo ikashushwa ikawa 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kwamba hawakuwa nje ya sheria, wako ndani ya Sheria hasa baada ya kushuka kwenda 20. Kwa hiyo, napenda kinywaji changu lakini hiyo hainitishi sana laizima tulipie mfuko wa Serikali ili Serikali ipate mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niseme kuna suala la hizi fedha ambazo zimeongezewa kwenye maeneo mbali mbali. Sasa kuna pendekezo la bajeti escalating inasema kwamba ile wakati bei za mafuta zina fluctuate, zikishuka ile asilimia 50…

MWENYEKITI: Ahsante, Dkt Kimei mda wako umekwisha.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …kutokana na hiyo inakwenda kwenye kilimo, kwa hayo naomba niunge mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Fedha wa Mwaka 2022
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii na nianze pia kwa kujiunga na wenzangu kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu anayeongoza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuanza kuchukua hatua madhubuti na za kimkakati za kuongeza uwekezaji na kasi ya uwekezaji katika uchumi wetu, kwa vile mimi naona kwamba Muswada huu una maudhui ya kimkakati kabisa na siyo tu kwamba, tunaona kwamba kuna kupunguza hapa na pale lakini utaona kwamba ni Muswada au ni marekebisho ambayo yanaenda kumpa Mheshimiwa Waziri wa Fedha uwezo wa kufanya maamuzi ya haraka ili kuweza kuruhusu miradi ile mahiri na ya kimkakati kuanza hapa nchini upesi bila kusubiri bureaucracy ya kupeleka kwenye Bunge kwa sababu sheria za kikodi mara nyingi zinahitaji zirudi huku Bungeni, na naamini kwamba Mheshimiwa Rais ameruhusu Muswada huu uje ili uweze kufupisha ule mchakato wa Mwekezaji kuweza kufika na kuanza mradi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sisi tunaofahamu ni kwamba, Wawekezaji wote na miradi mingi inakuwa na mahitaji tofauti tofauti ili iweze kuonesha kwamba itakuwa na faida katika kipindi ambacho yule Mwekezaji amejiwekea. Bila yale masharti au zile athari ambazo yeye anaziona kwenye mradi ule, hazijawa addressed kwa namna ambapo yeye na Bodi zake, kama ziko nje ya nchi au ziko hapa hapa nchini, basi inakuwa vigumu sana kuchukua hatua ile ya kuanza kutekeleza mradi.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi watapita kwenye maeneo mbalimbali, wataanza TIC ambapo baadaye wataishia hata kwenye National Investment Steering Council - Kamati ya Uwekezaji ya Taifa, lakini kama hawana uhakika kwamba yale wanayojadili, yale yanayojadiliwa na taasisi hizi hayatatekelezwa haraka, ni lazima pengine yaje Bungeni yaulizwe maswali mengi, pengine yasipite, basi inakuwa ni vigumu sana miradi ile kuanza.

Mheshimiwa Spika, nami naamini kwamba hili mkakati wake unatokana hilo; kwamba sasa Waziri wa Fedha, na niseme kwamba sio tu Waziri wa Fedha; na tumeridhika sana kule kwenye Kamati yetu kuona kwamba Waziri wa Fedha atatekeleza haya baada pia ya kupitia kwenye cabinet kwenye maeneo fulani fulani; lakini ni miradi ile ambayo imepita kwenye Kamati ya Taifa ya Uwekezaji ambayo inasimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Siyo tu Waziri Mkuu, pia ndani yake kuna kuna watu ambao ni mahiri, ni watu ambao ni wazalendo ambao tunajua kwamba wanaongoza taasisi ambao zinaelewa masuala ya uwekezaji kwa mapana kama vile Benki Kuu na wengine. Kwa hiyo ninaamini tutakwenda mbali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunajua kabisa kwamba, tena tumeambiwa, kuna congress man mmoja kule Marekani ambaye ame-trend sana; natumaini wengi wameona; anatoa changamoto. Kwamba ukweli tatizo kubwa la uwekezaji huku nchini linatokana na kodi nyingi na kubwa. Ile corporate tax, ukienda kwenye VAT ziko juu. Na nini, mimi ninakubaliana naye kwa namna fulani. Ni kweli kwamba tusipoangalia vizuri na tusipoweza ku-treat kila mwekezaji kwa namna fulani ambayo inampa au kinampa uhakika; kwamba zile gharama zisipoweza kupunguzwa, zikafanywa hivi kwa kupunguza VAT kwa muda fulani tutakaa muda mrefu bila kuona uwekezaji ukiongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na huu uwekezaji unashindaniwa. Kila nchi inashindania uwekezaji kwasababu inajulikana kwamba capital discuss duniani ni taji, haipo tu hovyo hovyo, ni taji inashindaniwa na nchi mbalimbali na shughuli mbalimbali, na kila nchi inajaribu kutoa kwa namna fulani vivutio ambavyo vinaweza kuwezesha wawekezaji wakaingia. Kuna nchi nyingine sasa hivi zimeanza, na natumaini ni nadharia mpya ambayo inakuja; kwamba the only way ya kuongeza tax base ili kuongeza government revenue bila kuongeza viwango vya kodi ni kuongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, kama hatuwezi kuongeza uzalishaji kwa namna hii ya kuvutia wawekezaji, kitu ambacho hatuna uzalishaji ambao haupo lakini tukiwavutia watakuja tukawapa dispensations fulani, tukawapa misamaha fulani kwa kipindi ambacho kinakubalika hawa wawekezaji wakaja wakaongeza uzalishaji tukaanza kuvuna Pay as You Earn, tukaanza kuvuna vyote vile vingine vinavyotokana na uzalishaji kuongezeka katika nchi hii hakutafika mbali. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwasababu naona kwamba hii nadharia ameweza kuiona. Kwamba njia pekee sasa ya kuweza kuongeza taxbase yake si tu kuchukua from kilichopo lakini tuongeze uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, na hata tusipowakaribisha kwa kuwapa hizi dispensations wanazoomba hatutakuwa nao, uzalishaji hautakuwepo; lakini tukifanya vile kwa muda mfupi watakuwepo, tutaona uzalishaji utaongezeka na taxbase yetu itakuwa ina-grow na itakuwa inakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa kwamba Muswada huu umebuniwa vizuri. Kwa mfano tumeona kuna vingi vinalenga mwenye kiwanda hiki cha kuzalisha mbolea, utaona kila mtaji ukija utakuwa hivyo hivyo, utakuwa na vitu vingine vinahitajika, si kupunguza tu bei ya phosphate au kutoa mrahaba kwenye phosphate, mwingine atakuja na ombi lingine kutokana na jinsi ambavyo anawekeza. Kwa hiyo ni vizuri tukampa Waziri wa fedha na pia tukahakikishiwa kwamba kwa vile hivi vitu sio yeye anafanya mwenyewe, vitaenda hadi kwenye Cabinet ambayo Mheshimiwa Rais mwenyewe atakuwepo; hivyo haiwezi kuwa abuse. Mimi ninaamini kwamba tutakwenda vizuri, na hiyo ndiyo inaonesha wazi kwamba miradi mingine ili iweze kwenda fast na iweze kutekelezwa kwa kipindi kifupi ni lazima tutoe uwezo kwa Serikali kuweza kufanya hayo mambo bila kupoteza muda mrefu sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia ninachelea kusema kwamba naungana na Kamati na nilikuwepo, na ninashukuru kwamba Kamati imeshauri pia kwamba kwa baadhi ya misamaha inayotolewa iwe inachapishwa na Serikali kwenye gazeti ili watu wajue, kwamba katika kipindi hiki Serikali imetoa misamaha hii na watu wataona mahudhui kwasababu gani misamaha hiyo imetolewa na hakuna mtu atalalamika kwamba kuna misamaha ambayo imetoka kienyeji enyeji. Kwa hiyo ninaamini ikichapishwa itakuwa imesaidia, lakini pia ni transparence na ndio dhana zima ya uendeshaji wa Serikali (good governance) sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu pia ninaamini kwamba huo ushauri ambao umetolewa, kwamba Serikali iwe inafanya tafiti za mara kwa mara, kufanya tathmini ya ile misamaha iliyotolewa au zile punguzo zilizotolewa kwenye maeneo fulani fulani ya kodi kama ni VAT whatever kwamba imeleta matokeo chanya yanayoendana na mahudhui ya marekebisho yaliyofanywa na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeshauri pia kwamba kuwe na timeframe ya hiyo …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa malizia.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, … time flame iwepo. Kwamba wakati unapotoa ile misamaha ijulikane inaisha ndani ya utekelezaji wa mradi na pia ndani ya muda mfupi baada ya mradi kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa fursa hiyo, nataka niseme kwamba naunga mkono hoja iliyoletwa na Mheshimiwa Waziri ya kurekebisha hizi sheria lakini pia naomba Wabunge wenzangu waweze kona maudhui haya kwa u-chanya wake ili waweze kupitisha hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Ahsante sana. (Makofi)