Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Anania Tadayo (10 total)

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na juhudi za Wizara ambazo tunaziona, lakini kwa kuwa mipaka ya hifadhi hii iliwekwa mwaka 1954 na idadi ya watu imezidi kuongezeka kiasi kwamba sasa hivi Makao Makuu ya Mji Mdogo wa Same yapo kilometa nne tu kutoka kwenye mpaka wa hifadhi.

Je, Serikali haioni kwamba suala la eneo hili la Same Magharibi lichukuliwe kama special case ili kuwapa watu nafasi ya kuweza kufanya kazi zao kwa sababu mpaka upo karibu sana na Makao Makuu ya Mji Mdogo wa Same? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Malisisli na Utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba Same ipo kilometa sita kutoka maeneo ya makazi ambayo wanaishi wananchi mpaka kwenye eneo la hifadhi. Kama ambavyo nimeelezea kwamba sasa hivi tuna changamoto ya tembo na hawa tembo wanarudi kwenye maeneo yao ya zamani, kwa hiyo, kuendelea kumega hili eneo ni kuendelea sasa kuongeza migogoro kati ya wananchi na wanyama.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati Serikali inaangalia utaratibu mwingine basi wananchi waendelee kuishi kwenye maeneo hayo kuliko kuendelea kuwasogeza kwenye hatari zaidi kuliko ilivyo sasa, ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa hitaji la stendi lililoko Jimbo la Geita Mjini ni sawa kabisa na lile lililoko katika Jimbo la Mwanga; na kwa kuwa mwezi Novemba mwaka jana Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Kilimanjaro aliwaahidi wananchi wa Mwanga stendi ya kisasa pale Mwanga.

Swali langu je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais kwa wananchi wake wa Mwanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Tadayo, Mbunge wa Mwanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan tayari tumeshaipokea Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumeshaifanyia tathmini na tunatafuta fedha wakati wowote ahadi hiyo itatekelezwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kazi imeanza kwa ajili ya kujenga stendi ya kisasa pale Mwanga. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huduma ya utengemao na mazoezi ya viungo ni muhimu sana kwa wagonjwa wanaopata matatizo yanayohusika na viungo, na kwakuwa Wilaya nzima ya Mwanga kuanzia Hospitali ya Wilaya mpaka vituo vyake vya afya hatuna matalaam hata mmoja wa huduma hiyo.

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kutupatia physiotherapist katika Wilaya ya Mwanga hasa ukizingatia ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi juu ya ajira lukuki zinazokuja kwa ajili ya afya. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwapigania wananchi wa Mwanga, lakini yeye mwenyewe anajua sasa Rais wetu amepeleka fedha pale Mwanga kwa ajili ya kujenga Idara ya Dharura na ujenzi unaendelea. Wakati ujenzi unakamilika na kuweka vifaa na ajira 32,000 ambazo zimetokea hayo mambo yatakwenda kuzingatiwa kuhakikisha tunapomaliza huduma ya magonjwa ya dharura na watalaam wa aina hiyo uliowasema wanakuwepo vilevile kwenye eneo hilo. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa baadhi ya watu wenye ulemavu wanapata changamoto ya kufanya biashara wakiwa peke yao pengine kutokana na nature na ile hali ya ulemavu wao na kwa kuwa imejidhihirisha kwamba Halmashauri nyingi zinakosa wakopaji wa kutosha katika kundi hili la walemavu na hivyo kupelekea zile fedha kukopeshwa kwenye makundi mengine au hata kurudishwa. (Makofi)

Je, Serikali ina mpango gani basi wa kuwarahisishia zaidi hawa watu wenye ulemavu ili waweze kutumia ile asilimia mbili yao ambayo wamewekewa kwa mujibu wa sheria? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Anania Tadayo, Mbunge wa Jimbo la Mwanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kasi ya ukopaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa kundi la watu wenye ulemavu bado hairidhishi na Serikali tumeona hilo na moja ya sababu ni kwamba walio wengi hawana ile confidence ya kukopa wakiamini kwamba hawawezi kurejesha. Lakini ni hatua ambazo Serikali imechukua kwanza ni kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa watu wenye ulemavu; lakini pili kuwarahisishia kwamba hata mtu mmoja mwenye ulemavu anaweza akapata mkopo wa asilimia 10 akafanya biashara yake baada ya Kamati ya Mikopo kujiridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitumie fursa hii kuhamasisha wananchi, lakini kuwaelekeza watendaji kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa makundi ya watu wenye ulemavu ili wapate mikopo ya asilimia 10, ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii, kwa kuwa ipo ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa stendi ya kisasa katika Mji wa Mwanga, swali langu ni je, ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa kwa wananchi wa Mwanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Tadayo aniruhusu niweze kupata maelezo sahihi ya kuhusu utekelezaji wa hii ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa TANROADS kujenga hii stendi ya kisasa katika Mji wa Mwanga baada tu ya kutoka kwenye kipindi hiki. Ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninapenda kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo la magugu maji katika Ziwa Jipe limedumu zaidi ya miaka 20 sasa, na imekuwa ni ahadi ya Serikali kila wakati ya kuondoa magugu maji hayo. Pamoja na shukrani kwa Mheshimiwa Rais kupitia kwa Mheshimiwa Waziri alimtuma Naibu Waziri akaja kuwapa ahadi hiyo wananchi, lakini Serikali haioni sasa kwamba umefika wakati kwa vile tatizo hili limekuwa kwa muda mrefu sana, ziko mashine hizi aquatic wild harvesters nyingi sana China na kila mahali ambazo thamani yake haizidi hata dola laki tano, ambazo zinaweza zikafanya kazi hii kwa namna endelevu kidogo kidogo ili kuzuia kuendelea kwa uharibifu wa mazingira na pia kuwawezesha wananchi wa Mwanga kuendelea kufaidi matunda ya lile Ziwa wakati Serikali inaendelea na mpango mkubwa huo wa mabilioni ya fedha ambao tunausubiri kwa hamu, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Joseph Tadayo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kushukuru sana Mheshimiwa Mbunge amekuwa akielezea hoja hii mara nyingi sana na ndiyo maana takribani wiki nne zilizopita nilimtuma Naibu wangu, Mheshimiwa Chilo alienda kule kwa ajili ya kuangalia uhalisia ulivyo. Kama nilivyosema ni kwamba tunaendelea na mchakato huu na andiko letu hili ni kwa ajili ya Ziwa Jipe na hali kadhalika Ziwa Chala lakini maoni ya Mheshimiwa Mbunge naomba niseme kwamba Ofisi yetu imeyachukuwa, lengo letu ni kwamba kuhakikisha tunatumia mbinu zote zinazowezekana, hili itaangalia fursa zote zinazopatikana hata tukipata mradi kidogo wa muda mfupi, nini kifanyike lakini jambo kubwa la pale litaendelea kufanyika katika mradi huu lakini lile wazo la kwanza lakini wazo lako tunalichukua kwa ajili ya kulifanyia kazi Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kupata nafasi hii. Ziwa jipya lililoko Wilayani kwangu Mwanga mpakani na Kenya, upande wa Tanzania unakaribia kupotea kabisa kwa ajili ya magugu maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza ahadi yake ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Jipe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali hii ni kuhakikisha kwamba tunaondosha changamoto zote zinazogusa kwenye eneo la mazingira ikiwemo changamoto ya kuenea kwa magugu maji. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuzitafuta fedha kokote ziliko ili kuhakikisha kwamba tunaondoa magugu maji katika maeneo yote. Pia nimwambie kwamba siyo hili tu, yapo maziwa mengi yana changamoto hii. Hivyo, nimwambie tu kwamba hata katika Ziwa Jipe tutahakikisha tunakwenda kuondosha kabisa changamoto ya magugu maji, nakushukuru.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa, tarehe 7 Agosti, 2022 Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea pale Rungwe Serikali ilitoa ahadi kwamba mradi huu ungekamilika mwezi Oktoba, 2023; na kwa kuwa, tarehe hiyo imepita sasa; je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawaeleza wananchi wa Tukuyu kwamba ni lini sasa mradi huo utakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mradi wa Maji uliopo Wilaya ya Mwanga, Kata ya Kileo, sehemu inaitwa Mnoa, ambao unakusudia kuwahudumia wananchi wa Vijiji vya Kileo, Kituri na Kivulini, wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3; je, ni lini sasa mradi huu utakamilika ili wananchi wa vijiji hivi vitatu vya Kileo, Kituri na Kivulini, Kata ya Kileo waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Albert Anton Mwantona, kwa niaba yake limeulizwa na Mheshimiwa Joseph Tadayo, lini mradi huu utakamilika; kipande ambacho tulimwahidi Mheshimiwa Rais kukamilika, kilishakamilika. Ni hizi kilometa tisa kutoka kule kwenye chanzo cha Mto Mbaka mpaka pale kwenye tanki. Ni mimi mwenyewe kabla ya ule mwezi wa Kumi nilikwenda pale Tukuyu na tukahakikisha maji yameweza kuingizwa kwenye existing line.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limebaki kama nilivyosema, kufikia mwezi Aprili tunatarajia tanki liwe limekamilika lijazwe na kuongeza uzambazaji kwa existing line na kuongeza line mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye swali la pili la kutoka Mwanga, Mradi wa Moa, huu mradi umekamilika kwa asilimia zaidi ya 95 na tayari maeneo ambayo yanapitiwa na mradi huu yanaendelea kukamilishwa, na mwezi huu Februari tunatarajia maji yaweze kufika kwenye vijiji hivi alivyovitaja vya Kileo na Kivulini. Kwa watu wa Kituri, wenyewe kwa sasa hivi wanapata maji kutoka kwenye Mradi wa Kifaru. Kwa hiyo, wapo kwenye mpango wa kuongezewa extension kutoka kwenye huu Mradi wa Mnoa, baada ya hawa ambao hawana maji kabisa kupata, nao watapelekewa maji vilevile. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja tu la nyongeza. Andiko la mradi liliwasilishwa tarehe 28 Desemba, 2021. Mwaka 2022 nilikumbushia kwa njia ya swali la nyongeza, nikapewa majibu kwamba mchakato unaendelea.

Mheshimiwa Spika, mwezi Julai, mwaka huu 2023 Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri, TAMISEMI, alitembelea Jimboni kwangu, tulipomkumbushia hilo ndiyo akashauri kwamba tufanye wasilisho la kukumbusha. Kwa hiyo, wasilisho analoli-refer Mheshimiwa Waziri hapa ni la kukumbusha ambalo limewasilishwa mwezi Agosti mwaka huu 2023 na ninalo hapa, limefanya reference kwa andiko la msingi ambalo ni la mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, swali langu: Kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ni ya muda mrefu: Je, Mheshimiwa Waziri sasa yuko tayari kutuambia ni lini kazi hii itaanza ili wananchi wa Mwanga waanze sasa na wao ku-¬play their party kwa kuanza kukusanya material site kama sehemu ya mchango wao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni kweli kwamba Halmashauri ya Mwanga iliwasilisha andiko awali mwaka 2021, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipitia na kuwarejeshea kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yalihitaji maboresho zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa, ahadi za Mheshimiwa Rais ni kipaumbele chetu na ndiyo maana tayari tumeingiza kwenye mpango, tunafanya tathmini ya mwisho wa vigezo na wakati huo huo tunatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi katika Halmashauri hiyo ya Mwanga.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mwanga wawe na imani kwamba Serikali kuna hatua za mwisho za tathmini na mara fedha zikipatikana tutakwenda kuanza ujenzi wa stendi hiyo, ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa, tarehe 7 Agosti, 2022 Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea pale Rungwe Serikali ilitoa ahadi kwamba mradi huu ungekamilika mwezi Oktoba, 2023; na kwa kuwa, tarehe hiyo imepita sasa; je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawaeleza wananchi wa Tukuyu kwamba ni lini sasa mradi huo utakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mradi wa Maji uliopo Wilaya ya Mwanga, Kata ya Kileo, sehemu inaitwa Mnoa, ambao unakusudia kuwahudumia wananchi wa Vijiji vya Kileo, Kituri na Kivulini, wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3; je, ni lini sasa mradi huu utakamilika ili wananchi wa vijiji hivi vitatu vya Kileo, Kituri na Kivulini, Kata ya Kileo waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Albert Anton Mwantona, kwa niaba yake limeulizwa na Mheshimiwa Joseph Tadayo, lini mradi huu utakamilika; kipande ambacho tulimwahidi Mheshimiwa Rais kukamilika, kilishakamilika. Ni hizi kilometa tisa kutoka kule kwenye chanzo cha Mto Mbaka mpaka pale kwenye tanki. Ni mimi mwenyewe kabla ya ule mwezi wa Kumi nilikwenda pale Tukuyu na tukahakikisha maji yameweza kuingizwa kwenye existing line.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limebaki kama nilivyosema, kufikia mwezi Aprili tunatarajia tanki liwe limekamilika lijazwe na kuongeza uzambazaji kwa existing line na kuongeza line mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye swali la pili la kutoka Mwanga, Mradi wa Moa, huu mradi umekamilika kwa asilimia zaidi ya 95 na tayari maeneo ambayo yanapitiwa na mradi huu yanaendelea kukamilishwa, na mwezi huu Februari tunatarajia maji yaweze kufika kwenye vijiji hivi alivyovitaja vya Kileo na Kivulini. Kwa watu wa Kituri, wenyewe kwa sasa hivi wanapata maji kutoka kwenye Mradi wa Kifaru. Kwa hiyo, wapo kwenye mpango wa kuongezewa extension kutoka kwenye huu Mradi wa Mnoa, baada ya hawa ambao hawana maji kabisa kupata, nao watapelekewa maji vilevile. (Makofi)