Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Anania Tadayo (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa sehemu ya Bunge lako hili la Kumi na Mbili kwa mara ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, nikishukuru sana chama changu Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini niweze kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Niwashukuru sana wananchi wa Mwanga kwa ushindi mkubwa walionipa wa kura za kishindo.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mwenyezi Mungu anijaalie mimi lakini atujalize sisi sote tuweze kuwatumikia wananchi ipasavyo kwa kuwa utendaji wa Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza pamoja na ushindi huu wa kishindo umeamsha shauku kubwa sana ya wananchi na matarajio makubwa ambayo wanayo. Kwa hiyo Mungu atujaalie tuweze kuyatimiza.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii ya hotuba ya Mheshimiwa Rais na sababu kubwa ni kwamba hotuba hii ni mwendelezo wa hotuba ya 2015 ambayo ilitekelezwa ikatutoa na kutupeleka kwenye uchumi wa kati. Ni dhahiri kwamba tukitekeleza hotuba hii mafanikio yatakayopatikana ni makubwa mno na yatatupeleka mbele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeitazama hotuba hii nikaona pamoja na mambo mengine lakini kwakweli inatusababishia kwenye kushusha chini yale mafanikio makubwa ambayo yalipatikana kwenye miradi mikubwa ya kitaifa yaende yawaguse wananchi na kugusa uchumi wa mtu mmoja mmoja, jambo ambalo ndilo hasa wananchi wanalolitamani na kulitarajia. Naipongeza sana Serikali kwa sababu imeshaanza kutekeleza. Kwenye Jimbo langu la Mwanga tulikuwa na tatizo sugu la maji ambalo matumaini ya kuliondoa yalikuwa yanafifishwa na utendaji ambao ulikuwa hauridhishi wa mkandarasi ambaye kimsingi alikimbia site kwenye ule mradi mkubwa wa maji. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa maana alisikia kilio chetu akachukua hatua za haraka za kuweza kusaidia na ule mradi sasahivi unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba iwajali wale wafanyakazi waliokuwa chini ya mradi ule kwa sababu baada ya mkandarasi yule kuususa au ku- repudiateule mkataba na kuondoka wako wafanyakazi ambao stahiki zao hazijalipwa. Naamini kabisa kwamba kwa sababu mkandarasi amekimbia basi endapo kuna chochote anachodai Serikali inayo mamlaka ya kumkata na kuwalipa wale wafanyakazi nahata kama hakuna anachodai bado Serikali inaweza ikawalipa wafanyakazi pamoja na watu wengine waliokuwa wana mikataba na mkandarasi yule na ziko taratibu za kisheria za Serikali ku-recover fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwamba kwa kasi hiyo hiyo ambayo imeonekana kwenye miradi hii, basi miradi mingine ambayo iliahidiwa wakati wa kampeni ambayo wananchi wa Mwanga wameiomba sana itekelezwe. Kwa mfano, liko suala la mradi wa hospitali ya wilaya ambayo Mheshimiwa Rais alituahidi, kiwanja kipo tayari hekari 54, kwa hiyo tunaiomba Wizara husika basi iweze kulitekeleza jambo hilo kwa sababu litakidhi kiu na matamanio makubwa sana ya wananchi wa Mwanga. Pili, iko miradi ya umaliziaji wa vituo vya afya hasa Kituo cha Afya cha Kigonigoni ambacho kwa kweli kiko kwenye mkwamo. Tunaomba Wizara husika ilitazame suala hili.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru Wizara ya Ujenzi kwa niaba ya Serikali kwamba kasi ya ujenzi wa barabara katika Jimbo la Mwanga inaendelea vizuri lakini bado ziko barabara, iko barabara ya Lembeni – Kilomeni mpaka Lomwe kilometa 31 ambayo tayari iko chini ya TANROADS tunaomba sasa barabara hiyo nayo itazamwe. Iko barabara ya Kisangara – Ngujini – Shingatini kilometa 25.9 na barabara ya Mgagao – Pangaro – Toroha kilometa 35 ambazo katika ngazi ya road board na RCC zimeshaombewa kuingia TANROADS. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri husika basi atusaidie barabara hizi ziingie TANROADS ili pia ziweze kupata matengenezo kama barabara zingine.

Mheshimiwa Spika, ukienda ukurasa wa 15 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais amezungumzia mkazo juu ya uwekezaji katika sekta ya nyama. Jimbo la Mwanga ni wadau wakubwa pia wa sekta hii ya nyama kwa sababu tunayo mifugo mingi na pia eneo letu location yetu iko mahali pazuri kwa ajili ya viwanda vya nyama kwa sababu kuna Bandari ya Tanga iko karibu, kuna Uwanja wa Ndege wa KIA na pia tuko mpakani. Nafahamu kabisa kwamba nyama ya Tanzania hasa nyama ya mbuzi ina soko kubwa sana middle east huko na nafahamu kabisa kwamba ziko nchi za jirani ambazo huwa zinachukua mbuzi wetu na kuwachinjia kwao na kutoa certificate of origin wale mbuzi waonekane wanatoka kwao, lakini ukweli wa mambo wale mbuzi wanatoka Tanzania na wanapata soko zuri nje kwa sababu ya ladha yake. Kwa hiyo, tunaomba Waziri anayehusika kutukumbuka katika uwekezaji kwenye sekta hii ya nyama hasa katika eneo la Kata ya Mgagao ambapo tayari kuna mnada mkubwa unaovuta watu kutoka hata nchi za jirani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ombi hili, ningependa pia niseme kwamba wafugaji katika Jimbo langu kwa sababu wako wanapakana na Mbuga ya Mkomazi wanakabiliwa na changamoto zinazokabili wafugaji wengi wanaopakana na maeneo ya hifadhi. Ni vizuri Serikali ikahakikisha kwamba mipaka kati ya maeneo ya wafugaji na hizi mbuga inaeleweka na wafugaji wapewe elimu inayotosheleza na kwa kweli ni vizuri wakaongezewa maeneo ya kulisha mifugo yao. Ziko faini ambazo wanatozwa pale ambapo mifugo yao imekosea ikaingia kwenye maeneo ya hifadhi. Zile faini ni kubwa mno na kwa kweli zinakuwa ni kama zinawakomoa hawa wafugaji. Wafugaji wanaishi maisha ya mashaka sana katika mipaka na hifadhi ikiwa ni pamoja na wafugaji wa Jimbo langu la Mwanga.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa niaba ya Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kudhibiti suala la…

Mheshimiwa Spika, nasikia kengele imelia. Nakushukuru kwa nafasi hii.

SPIKA: Hapana ni kengele ya kwanza.

MHE. JOSEPH A. TADAYO:Ni kengele ya kwanza, ahsante.

Mheshimiwa Spika, basi kwa haraka nizungumze tu kwamba suala la kudhibiti uwindaji haramu limefanikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Hii imesaidia wanyamapori kuongezeka, lakini baraka hii ya wanyamapori kwa baadhi ya maeneo imesumbua sana.

Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo kubwa sana la tembo ambalo limefanya maeneo ya karibu kata tano za jimbo langu yawe magumu sana au yasifae kabisa kwa masuala ya kilimo. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu akizungumzia juu ya kuweka kambi za hawa Askari wa Wanyamapori katika maeneo ya changamoto kama hizo. Naomba hilo liharakishwe kwa sababu ziko kata tano za jimbo langu ambazo kwa sasa hivi maisha ni magumu na wako watu kadhaa ambao wameshapoteza maisha kwa ajili ya wanyama hawa tembo.

Mheshimiwa Spika, naomba kurudia kwamba naunga mkono hoja kwa dhati kabisa na tuko pamoja katika kutekeleza haya yaliyomo humuna kuisukuma mbele nchi yetu kwenda kwenye uchumi wa kati wa juu sasa. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia Mpango huu. Nianze kwanza kuipongeza Serikali yetu chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kutuletea Mpango huu mzuri. Naipongeza pia Wizara kwa kazi nzuri ambayo wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja nilikuwa nasoma journal moja ambayo imeandikwa na Royal Irish Academy ikizungumzia juu ya vyama vikongwe kubakia madarakani. Walifanya uchambuzi mzuri sana, walipofika kwenye CCM wakaeleza kwamba CCM ipo madarakani na ina uwezo wa kuendelea kuwa madarakani kwa sababu baada ya uchaguzi huwa wana-stick kwenye kutekeleza Ilani, hawafanyi manipulations na kufanya mambo mengine mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nasoma Mpango huu, kikubwa nilichokuwa najaribu kukitazama ni hicho kwamba umeendana vipi na ilani yetu? Mimi nimeridhika kabisa kwamba Mpango ulioletwa uko sambamba na Ilani na kwa hiyo, kama ilivyo kawaida kwamba kwenye Mfumo wa Vyama Vingi, chama kinachoshinda kwenye uchaguzi Ilani yake inageuka kuwa sera, basi tuungane kwa pamoja tutekeleze Mpango huu, tuutungie sheria, bajeti ikija tupitishe mafungu tukatekeleze kwa pamoja na kwa umoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu mambo machache. Suala la kwanza ni elimu. Endapo kweli tutataka kama ambavyo tunataka kwamba vijana wetu washiriki katika uchumi wa viwanda na waweze kufaidi matunda ya nchi kufikia katika uchumi wa kati, basi suala la VETA ni lazima tulitilie mkazo sana kama ambavyo imezungumzwa kwenye Mpango. Vipo Vyuo vya VETA ambavyo vilianzishwa na wananchi kwa kushirikiana na marafiki na wafadhili mbalimbali; kwenye Jimbo langu viko viwili; kuna kimoja kiko Tarafa ya Usangi na kingine kiko Tarafa ya Ugweno, ni muhimu hivi vikafufuliwa viweze kufanya kazi kwa sababu huduma yake bado inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunahitaji Vyuo vya VETA katika kila wilaya ambavyo vitaendena na uchumi wa eneo husika. Kwa mfano, Kanda ya Kaskazini tuko kwenye utalii na madini; basi Vyuo vyetu vya VETA viendane na kutengeneza vijana watakaoshiriki kwenye uchumi huo. Halikadhalika, Kanda ya Ziwa kama kuna uvuvi na madini, basi twende hivyo hivyo ili tuhakikishe kweli vyuo vyetu vinawafaidisha vijana wa maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunahitaji kuendelea kutilia mkazo elimu ya juu. Dhana kwamba kwa sasa hivi elimu ya juu imeanza kuwa irrelevant, hiyo mimi sikubaliani nayo kabisa, kwa sababu mbili. Kwanza, huwezi kupigana vita ukawa na Askari wa chini peke yao bila Majenerali. Halikadhalika, liko suala kwamba dunia imekuwa kijiji, tunahitaji ku-export hata grains. Kama tunavyopeleka wachezaji akina Mbwana Samatta wakacheze nje huko, pia tunahitaji wasomi wetu waende wakafanye kazi za kibingwa huko nje. Wako wengi mpaka sasa hivi ambao wanafanya kazi hiyo, hata waliotoka kwenye Jimbo langu, lakini tunahitaji succession plan kwamba hawa wanapostaafu, wapatikane wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo, tutilie mkazo pia elimu ya juu, kwenye Jimbo langu tuna ardhi kubwa sana, kwa hiyo, ninaalika kabisa Serikali ije kuwekeza hata kwenye vyuo vikuu. Tuna ardhi ya kutosha, tufanye kazi hiyo, pamoja na Vyuo vya VETA lakini pia tuendelee kutengeneza akili kubwa kwa ajili ya kuingia kwenye Soko la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni kwamba wataalam wetu wa elimu watutengenezee mitaala ambayo itawafanya wahitimu wasiabudu vyeti. Kuna nchi jirani tu hapa, kuna kijana ame-graduate International Relations and Diplomacy lakini akaenda kuanzisha car wash. Sasa yeye kwa sababu amefikia level hiyo, anaenda kwa Mabalozi na Mashirika ya Kimataifa, anasaini mikataba ya kuwaoshea magari, analipwa dola. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana mwingine atakuja akuambie naomba mtaji wa kuanzisha car wash shilingi milioni tano, sijui nitanunua hoover na hiki na hiki; akishaanzisha car wash anakaa hapo anasubiri wateja wamfuate, yeye anaongea habari ya Arsenal na nini akisubiri wateja waje, badala ya kwenda kuwagongea mlango. Bora hata angezungumza Simba na Yanga maana ni za kwetu. Kwa upande wa elimu napenda nisema hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, naungana na wote ambao wamesema kabisa kwamba kilimo ni moja ya vitu ambavyo vitatutoa kiuchumi, lakini lazima twende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nchi yetu ina vyanzo vingi sana vya umwagiliaji kiasi ambacho hata suala la greenhouse linaweza likaja kama second option.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa sababu kengele imelia, ipo miradi kwa mfano kwenye Jimbo langu, naishukuru Serikali kwamba…

(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Nami pia kwa nafasi yangu kama Mbunge na Mjumbe wa Kamati iliyoleta hoja, naunga mkono hoja ambayo imeletwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipewa kazi hii na wewe ili kuwapa haki wenzetu hawa ambao kwa mujibu wa kanuni tunawaita mashahidi, kuwapa ile haki yao ya kikatiba ya kuwasikiliza. Tuliwasikiliza chini ya kiapo na wakakubali kwamba kweli hizi kauli ni wao walizitoa. Inakuja sasa kuangalia juu ya uhalali wa kauli hizi kisheria kama ambavyo ripoti imezungumza kwamba unasimama, unasema kwamba viongozi wamepewa fedha ili kuruhusu chanjo ambayo si salama iingie. Kwamba kila anayetetea chanjo, kila anayechanjwa ikiwa ni pamoja na mimi kwamba ni hela, ni hela, ni hela. Halafu unafika mahali unajigamba kuwa juu ya kila mtu, kuwa juu ya Bunge, kuwa juu ya Spika kwamba mimi naweza nikafyatua mtu ndani ya Bunge, naweza nikafyatua mtu nje.

Mheshimiwa Spika, sasa ni wazi kabisa kwamba hata bila kusoma sheria, kila mtu anapaswa kuthibitisha yale mambo ambayo anayasema dhidi ya wenzake, kwa sababu kila mtu anastahili jina lake liwe safi kama lilivyo. Kwa maana ya kwamba mimi nimeajiriwa, nafanya kazi ni Waziri wa Sekta au nafasi yeyote ile. Kazi yangu naifanya kwa mujibu wa sheria, sasa kama unasema kwamba mimi nimepewa hela ili nifanye hivi, basi unao wajibu wa kuthibitisha jambo ambalo shahidi wa kwanza, Mheshimiwa Gwajima alishindwa kabisa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kwa shahidi wa shauri la pili, Mheshimiwa Jerry Silaa, dai lake kubwa kwamba mishahara ya Wabunge haikatwi kodi. Sasa waraka wa msingi, primary document ya kuthibitisha mshahara wa mtu huwa ni salary slip ile ambayo inatumika kukulipa wewe mshahara. Mmiliki wa ile document ni yule anayekulipa, sasa Mhasibu Mkuu wa Bunge ameshakuja, ameshatoa ile, ametenga ile salary slip ni hii hapa, inakatwa kodi na amesema inakatwa kodi na ametueleza kwamba hata wakusanyaji kodi wenyewe waliwahi kuja wakatazama hili jambo, wakaridhika nalo. Hata hivyo, bado mtu unasisitiza kwamba upo sahihi. Maana yake sasa huu kwa kweli ni uvunjaji sheria wa makusudi tu ambao ndiyo maana Kamati ikafikia hapo kutoa adhabu hizi ambazo mimi naziunga mkono kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri sisi Wabunge tukakumbuka kwamba baada ya kuchaguliwa tuliapa kuilinda, kuitetea na kuhifadhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba hii ndiyo iliyoweka hii mihimili ambayo tunazungumzia habari ya kuigonganisha na kuidhalilisha. Katiba hii ndio inayogawa mamlaka na madaraka ya watu kufanya kazi. Pia Katiba hii imetupa nafasi hasa sisi Waheshimiwa Wabunge namna ya kuhoji au namna ya kurekebisha mambo ambayo tunafikiri hayaendi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 63, kwamba tunayo mamlaka ya kumhoji Waziri yeyote juu ya suala lolote lile ambalo tunaona haliendi sawa. Sasa endapo basi tunadhani kwamba Serikali inakwenda ndivyo sivyo hatuna mamlaka ya kwenda kuwahojia huko kwenye maeneo yetu, kwenye vikundi vyetu vya ngoma au kwenye Makanisa au mahali pengine popote pale. Sheria inatuongoza na kutupa wajibu kabisa wa kuja kuihoji mahali ambapo ni stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, endapo basi mtu ameona kwamba sheria inayotulipa sisi mishahara kama ilivyo kwenye kifungu cha 20 cha ile National Assembly (Administration) Act, haipo sawasawa, basi unataka kuanzisha mchakato wa marekebisho, basi sidhani kama mchakato unaanzishwa hivyo. Sisi ni Wabunge, tunafahamu utaratibu wa kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Katiba ili hata ile posho ya mafuta ambayo ukienda kununua mafuta tayari kodi imeshakatwa, kama unataka na yenyewe ikatwe tena sijui mara ya ngapi, basi mchakato wa kisheria upo wa kufanya hivyo, sio kwenda kuchochea wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi, hizi kauli za wenzetu hawa wote wawili effect yake pia ni kuwachochea wananchi kuichukia Serikali. Kwa sababu kwa upande mmoja ya Mheshimiwa Gwajima ni kwamba anawachochea wananchi waone kwamba Serikali haijali afya zao, Serikali haijali usalama wao. Kwa hiyo watu wanapokea tu fedha huko wanaleta machanjo ambayo sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii nyingine ni kwamba Serikali ina upendeleo kwamba wengine wanakatwa kodi, wengine hawakatwi kodi. Kwa hiyo kauli zote hizi mbili zinakwenda zaidi hata ya makosa yetu ya kikanuni, kuna uchochezi hapa pia. Kwa hiyo ni vizuri kabisa Azimio hili la Bunge likapita kama ambavyo Kamati imelileta. Naliunga mkono, twende hivyo, turekebishane ili tuweze kwenda sawasawa katika kuwatumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa mara ya pili. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kutuletea Muswada huu katika wakati huu ambao ni muafaka. Naomba nieleze kabisa hapo kwamba mimi nimekuwa Wakili wa Kujitegemea kwa takribani miaka 25 sasa, kwa hiyo, nimeshuhudia hizi changamoto zinazozungumziwa juu ya ugumu wa kupata haki au wa kufikia haki kwa kutumia lugha ambayo si ya mhusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakimu wetu na Majaji na Waendesha Mashtaka wamepata taabu kidogo katika kuendesha mashauri wakati ambapo sheria inataka yawe kwa kiingereza. Kwa hiyo, wanasikiliza kwa Kiswahili, wanaandika kwa Kiingereza baadaye wanaandika hukumu kwa kiingereza, lakini wanapata taabu tena kuanza kuwatafsiria watu na mtu anasomewa shitaka inabidi litafsiriwe kwanza. Kwa hiyo, kwa kweli imekuwa ikileta changamoto kubwa. Niwapongeze Mahakimu wetu, Majaji na wadau wengine wamejitahidi sana katika kwenda katika ugumu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka 2007 Mahakama za Kazi zilishatutangulia, ziliundwa zile Labour Court Rules (Kanuni za Sheria za Mahakama za Kazi za mwaka 2007) ambazo ziliruhusu matumizi ya Kiswahili. Kwa hiyo, Mahakama zetu zimefanya juhudi kubwa, na zipo hukumu nyingi za kuanzia wakati wa Mheshimiwa Marehemu Jaji Mwaipopo, Jaji Rweyemamu na hata Jaji Samatta katika hukumu ile ya Kesi ya Dibagula, ile kesi maarufu iliyotokea Morogoro, walijitahidi kufanya hivyo. (Makofi)

Sasa tunapofikia mahali pa kuwatungia sheria nadhani tunairahisisha hii kazi, itafanyika vizuri na ninaamini sasa Serikali itawekeza, kwa hiyo, hata ile shida, changamoto walizokuwa wanapata zitapungua na haki itatendeka kwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandikwa kwa Kiswahili na Kiingereza, lakini kwa kutambua umuhimu wa Kiswahili kama lugha ya wengi, imeelekezwa kwamba panapokuwa na mgongano basi ile tafsiri ya Kiswahili ndiyo ambayo itazingatiwa. Sasa umefika wakati kwa sheria zetu ambazo zinatungwa chini ya mamlaka ya Katiba hiyo hiyo nazo pia zitungwe kwa Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tukumbuke kwamba katika mihimili mitatu ambayo inaundwa chini ya Katiba yetu; Serikali, Bunge na Mahakama, mihimili miwili tayari inatumia lugha ya Kiswahili, umebakia Mhimili mmoja tu wa Mahakama. Nadhani sababu ya kutumia Kiswahili katika mihimili hii miwili ni kuwezesha huduma yake kufika kirahisi na wale wahudumiwa/wananchi, waweze kuifikia hii mihimili. Mahakama imebaki peke yake, wakati umefika sasa mahakama nayo itumie Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taarifa ya Kamati ilivyoeleza ni kwamba kile kifungu cha 84(1) kinaelekeza kwamba lugha ya Mahakama zetu na vyombo vingine vya kutoa haki iwe Kiswahili na hiyo ni kwa sababu ya kuwahudumia walio wengi. Lakini kifungu hiki cha 84(2) kinazungumzia sasa haki za wale walio wachache kwamba endapo watu watakuja Mahakamani na wanapenda kesi yao iende kwa Kiingereza basi wanaruhusiwa pia kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipofanya hivyo tukakamilisha huu Muswada kama ulivyoletwa nadhani tutaingia kwenye tatizo, wanaharakati wanaweza siku moja wakajitokeza hata wakatushtaki kwamba tunaingia kwenye lile kosa, sasa unisamehe kwamba lazima nitumie Kiingereza kuna kitu wanaita class legislation, kwamba tunatunga sheria ambazo zinahangaika na tabaka moja tu.

Lakini katika kutibu hilo kuna kitu wanaita reasonable classification ambacho ndicho kilichofanyika hapa; kwamba tunawahudumia wale walio wengi lakini pia wale walio wachache nao pia wanapata nafasi ndani ya sheria hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu ni wa kihistoria, kwa hiyo ni vizuri tukaupitisha kwa umakini wote. Lakini pia naamini Serikali itawekeza ipasavyo katika ku- manage hiki kipindi cha mpito ili sheria hizi zitafsiriwe vizuri na tufikie mahali ambapo tutaendesha mashauri yetu kwa lugha ya Kiswahili bila kuathiri haki za watu na bila kuwapa ugumu utakaokwamisha utoaji haki wale ambao wanahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukienda kwenye mpango ambao tumemaliza kuujadili siku ya leo, unasisitiza juu ya suala la utawala bora. Utawala bora utafikiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya mwisho kuchangia. Hoja ya Wakili Msomi au sio msomi siku nyingine ukinipa nafasi nitaizungumzia vizuri kwa sababu Mheshimiwa Jaji Barnabas Samatta aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania aliwahi kutoa definition nzuri sana ya who is a learned person ambayo sijaona mahali pengine popote, siku nikipata nafasi hiyo tutayasema. Hatujiiti wasomi ila watu wanatuita wasomi, inaonekana wanatuona tumesoma. Ahsante sana.

SPIKA: Kesho tutakuwa na muda wa kutosha, mjiandae mawakili wasomi kuna sheria tutakuwa tunajadili na hiyo nayo tutapenda mlisomeshe, siyo Wabunge tu lakini mlisomeshe Taifa pia. (Makofi)

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, ataanza Mwanasheria Mkuu kwa sababu yeye ndiye Advocate Number One.

SPIKA: Ahsante endelea Mheshimiwa na dakika zako tunakulindia. (Kicheko)

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, kwanza mimi nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada huu katika wakati huu muafaka na hasa Muswada wa Marekebisho unaohusu Sheria ya Makampuni Sura 212 ambayo ndiyo sana nitakayozungumzia pamoja na kwamba nitazungumza kidogo kama muda utaruhusu juu ya Sheria ya Mahakama za Mahakimu.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu umeletwa kwa wakati muafaka kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua wazi kabisa kwamba inaweka sekta binafsi mbele kama engine ya maendeleo na Sheria hii ya Makampuni inahusu zaidi Sekta Binafsi. Kwa hiyo, ni muhimu kabisa sheria hii ipitiwe vizuri na ifanyiwe marekebisho kila wakati na ije tu tutaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na timu yake walikuwa na ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati. Tumejadiliana na kama ambavyo imesemekana hapa ni kwamba maeneo mengi tulikubaliana na yamekuja vizuri tu kama ambavyo tuliweza kufikia muafaka, hiyo ni kazi yetu na wala hatuhitaji kupongezwa au kuona kwamba mtu mwingine hakufanya kazi yake wakati tumewekwa kwa ajili hiyo ya kushirikiana ili tupate document ambayo inafaa kwa manufaa ya nchi yetu. Kwa hiyo, nitakazia tu marekebisho ya ile Ibara ya 30 ambayo imeitwa hapa kwamba ni hatari, ukasema tu-sanitize kwanza lakini mimi sijaona hatari mpaka sasa hivi kama ambavyo nitaeleza. Nitazungumzia pia Ibara ya 36 pamoja na ile Ibara inayohusiana na Sheria ya Mahakama za Mahakimu.

Mheshimiwa Spika, nikianza na Ibara ile ya 30 iliyoitwa kwamba ni ya hatari, labda nianzie mwisho ndiyo nirudi mwanzo. Mimi sioni tatizo linakopatikana kwa sababu Kamati yako kwa umakini wake ililiona hili, tukalizungumza na Serikali, tukawashauri na wakakubali kuondoa kile kifungu. Hata ukienda kwenye schedule of amendment (f) pale, kama utaniruhusu kusoma inasema ‘in clause 30 by deleting the proposed subsection 5’ sasa kama Serikali ilishakubali ikafuta, hiyo hatari sasa sijui inatoka tena wapi.

SPIKA: Unajua Mbunge mwingine anapokuja, anakuja ana ile Bill, zile amendment labda za Serikali au nini hajaziona. Kwa hiyo, mengine tunasameheana tu. Endelea Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, hata kama basi zile amendment hazikuonekana, hoja iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hapa ukurasa ule wa Tisa kama utaniruhusu pia kurejea ‘aidha, kufuatia maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Serikai kupitia jedwali la marekebisho imefanya marekebisho kwa kufuta mapendekezo ya Kifungu (5) kilichokuwa kinazuia watu waliowahi kutiwa hatiani katika makosa fulani kuanzisha makampuni ili kuondoa uwezekano wa watu hao kuadhibiwa mara mbili kwa kosa moja’ (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba hii hatari ambayo imesemekana hapa tukajichanganya changanya haipo na tusipate hiyo impression kwamba kuna hatari yoyote. Tulizungumza kwenye Kamati vizuri na Serikali, wakatuelewa. Schedule of amendment imekuja, wameondoa kile na hoja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imesema wazi. Kwa hiyo, sioni hapa kama kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo tu kwamba Serikali iliamua kukiondoa tu kwa sababu imekiondoa lakini ziko sababu kama ambavyo tumezungumza kwamba suala la kuanzisha kampuni linahusiana na haki ya mtu kumiliki mali ambayo ni haki ya Kikatiba. Sasa ile haki tunailinda kwa sababu tunataka Watanzania wa-enjoy hiyo haki na hata wawekezaji wa nje wanaokuja waweze kufurahia hiyo haki. Mtu akishahukumiwa akatumikia adhabu yake, akaimaliza anabakia kuwa mtu msafi tu na ndiyo maana kuna utetezi kwamba ukinifungulia kesi ambayo nilishahukumiwa nayo ule ni utetezi tayari. Sasa naogopa tena hili neno la wasomi lakini kuna lugha ya kilatini hiyo defense inaitwa autrefois acquit kwamba nilishafunguliwa hii na nikaachiliwa huru kwa hiyo, huwezi tena ukanifungulia kesi hiyo hiyo ukanitia hatiani. Sorry, hiyo ni autrefois convict kwamba ulishanifungulia hiyo, ukanitia hatiani, nika-serve sentence yangu nikamaliza sasa huwezi tena kunishtaki mara ya pili au nipate madhara yoyote yanayotokana na ile hukumu hilo halipo na Serikali ililizingatia vizuri ndiyo maana wakafuta hiki kifungu. Kwa hiyo, nadhani tupate amani katika hilo.

Mheshimiwa Spika, pia lazima tukumbuke pia kwamba mtu anapokwenda gerezani kwa mfano kwenye ile adhabu anaenda kule kurekebishwa. Magereza yetu yanafanya vizuri, anarekebishwa akitoka kule ni mtu salama anaweza akafanya kitu. Kama kuna muda wa uangalizi kwa mfano katika mambo ya kugombea wanayosema kwamba labda baada ya miaka fulani hiyo ni sawa, unaweza ukawekewa muda wa probation wa kutazamwa lakini siyo kukatazwa milele na milele haikuwa hivyo na ndivyo ambavyo sheria hii inakuja.

Mheshimiwa Spika, pia kabla sijazungumzia Kifungu kingine cha Sheria ya Makampuni niongelee pale kwenye Sheria ya Mahakama za Mahakimu kwa sababu pia kama nilisikia vizuri nilizungumza hapa kwamba wale Wazee wa Baraza (Assessors) wameondolewa hata hilo naona siyo sahihi kwa sababu ukienda kwenye jedwali la marekebisho ile schedule of amendment Ibara ya 54 labda nisisome yote kwa sababu ni ndefu lakini wale Wazee wa Baraza wameondolewa bado wapo katika kesi zote ambazo zinahusiana na Sheria za Kimila na sheria za Kiislam na haya ndiyo mambo yanayohitaji Wazee wa Baraza kwa sababu mimi naweza nikaenda Tadayo Mpare hapa na digrii yangu nakwenda kule Mwanza, natakiwa kuhukumu hata kama nina digrii lakini natakiwa kuhukumu kesi katika sheria za kimila za Wasukuma, nahitaji Mzee wa Kisukuma pale aje aweze kunisaidia juu ya zile mila na mimi niangalie sasa kama kwenye sheria za kimila zinazokubalika haikinzani na Katiba niweze kuamua nimeshauri, hivyo hata hilo pia sioni kama kuna tatizo hapo labda tu watu walikuwa hawajajielekeza vizuri kwenye jedwali hili la marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nirudi tena kwenye Sheria ya Makampuni ile Ibara ya 36 ambayo imepunguza umri wa watu kuruhusiwa kuwa Directors na imeondoa ule ukomo wa juu. Hili niipongeze Serikali kwa sababu kwa kweli tulikuwa tumechelewa. Maeneo mengi sana ambayo nimepitia Sheria hizi za Makampuni, age of majority mtu anaruhusiwa ni miaka 18 na umri wa juu hakuna haja, mtu ana kampuni yake, anataka Mkurugenzi anaona mtu ana miaka 75 lakini ana busara, akili kiwembe kinakata, muacheni aendelee kufanya kazi, aendelee kupata haki yake ya kipato na pia tuendelee kufaidika na ile akili yake ambayo anayo.

Mheshimiwa Spika, labda hapa wito tu ni kwamba marekebisho kama haya yanapofanyika basi ni vizuri sasa wataalam wetu wa elimu nao katika mifumo na mitaala basi wajielekeze hivyo sasa. Wasomi wetu wanaandaliwa kuhakikisha kwamba vijana wetu wanaandaliwa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa!

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, ni kengele ya pili.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, basi naunga mkono hoja. (Makofi)