Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda (17 total)

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali kwa ajili ya kuingiza Wilaya ya Manyoni katika mpango wa kujenga Chuo cha VETA mwaka huu, lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa tuna vijana wengi wanamaliza kidato cha nne hawaendelei kidato cha tano na vijana wengi wanamaliza kidato cha tano na sita hawaendelei vyuoni; je, nini mpango wa Serikali kuifanya elimu ya ufundi kuwa basic education yaani elimu ya msingi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa sasa hivi tuna uhitaji mkubwa sana wa elimu ya ufundi hasa hasa kwa ajili ya uzalishaji viwandani; nini mpango wa Serikali na Wizara kutoa mikopo kwa vijana ambao wanaenda kusoma elimu ya ufundi? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inakusudia kama nilivyosema kujenga vyuo vya ufundi katika Wilaya zote hapa nchini na sasa hivi zimebaki wilaya hizo 62. Kwa hiyo, ujenzi utaendelea na kuhakikisha kwamba vyote vinafanya kazi kwa ajili ya wanafunzi kuweza kusoma humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa sababu sasa hivi tunapitia mitaala na kazi mojawapo kubwa ya kupitia mitaala ni kuongeza elimu ya ujuzi, ujuzi ikiwa ni pamoja na ufundi, tunaamini tutakapokamilisha kazi hii rasimu zitakamilika mwisho wa mwaka huu maamuzi mwakani, tunaamini kwamba tutakuja na mkakati ambao utaongeza mafunzo ya ufundi na ujuzi katika shule zetu kuanzia darasa la kwanza kwenda mpaka elimu ya kidato cha sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili kuhusu mikopo. Kwa sasa hivi kwa kweli Serikali haitoi mikopo kwa ajili ya kwenda kwenye vyuo vya VETA, lakini tumefanya mazungumzo na Benki ya NMB kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaweza tukatoa mikopo kwa wale ambao wana miamala inayopitia kwenye benki hiyo kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kusoma kwenye vyuo vyote ikiwa ni pamoja na vyuo vya ufundi.

Kwa hiyo, tunaamini kwamba itasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kutopata mkopo lakini tutaendelea kutafuta mikakati mizuri zaidi kuhakikisha kwamba tunatoa fursa ya mikopo.
MHE. BENEYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Wilaya ya Mbinga hatuna Chuo cha VETA na tulipata ahadi ya Serikali kwamba awamu hii tutaingia kwenye mpango wa kujengewa Chuo cha VETA, tayari tuna eneo. Ni lini sasa chou hiki kinaenda kuanza kujengwa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema Wilaya zote ambazo hazina Vyuo vya VETA tunaanza kujenga VETA mwaka huu tumekubaliana kwenye hizo bilioni 100 ambazo tumezipata kutoka Hazina tutaanza ujenzi mwaka huu na mwakani tutapata bilioni 100 nyingine na kumalizia ujenzi. Kwa hiyo, tutafanya hivyo pamoja na Wilaya ya Mbinga na ujenzi utaanza siku za karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwa Wabunge wote ni kwamba kuhakikisha tunapata maeneo mapema, tunapata hati miliki ili tuweze kujenga kwa sababu hatuwezi kwenda kujenga chou mahali ambapo hatumiliki ardhi chini ya utaratibu wa VETA. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshiiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali.

Mheshimiwa Spika, swali hili niliwahi kuuliza likiwa linafanana hivi kwenye maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Majibu yaliyotolewa na Serikali na haya yanayotolewa sasa hivi yanapishana. Sasa napenda kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu shule hizi, kwa mfano shule ya Mshara, Sare na Mroma. Shule hizi zina majengo, vifaa na walimu: Je, Serikali inatoa msimamo gani kuhusiana na shule hizo?

Swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi VETA ndani ya Jimbo la Hai ilhali tayari tumeshapanga eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna shule za msingi 123 hapa nchini ambazo zilikuwa zinatakiwa zitoe mafunzo ya ufundi pamoja na elimu ya msingi, lakini shule zote hizo sasa hivi hazitoi mafunzo hayo kwa sababu ya uhaba wa walimu. Vyuo ambavyo vilikuwa vinatoa mafunzo kwa mfano Chuo cha Ualimu cha Mtwara ambacho kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwafundisha walimu elimu ya ufundi kwa ajili ya shule za msingi, imeacha kufanya kazi hiyo kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika kujibu swali la msingi, sasa hivi tunapitia mitaala yote ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi na lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaingiza ufundi na ujuzi katika shule zote ikiwa ni pamoja na hizi shule 123 na hizi shule za Jimbo la Hai kama alivyoeleza Mheshimiwa Saashisha. Tunatarajia kwamba tutamaliza shule za mitaala mwisho wa mwaka huu, hivyo tutaweza kuanza sasa kuhakikisha kwamba tunafundisha wanafunzi katika ngazi zote hizo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu VETA, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba tunajenga vyuo vya VETA kila Wilaya hapa nchini na juhudi hizo zinaendelea. Kwa yale maeneo ambayo tayari Wilaya zimeshatenga maeneo na hasa maeneo yale ambayo Wilaya na Halmashauri na Wabunge wameanza juhudi za kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi, tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunaenda kuongeza nguvu za Serikali ili kukamilisha azma hii ya kuwa na VETA katika kila Wilaya ikiwa ni pamoja na Jimbo la Hai kwa Mheshimiwa Saashisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Swali langu ni: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na nchi nyingine ambazo zimeendelea katika sekta hii ya ufundi stadi hasa kwa masuala ya Exchange Program kuwapeleka watoto wetu Internship ili waweze kujifunza zaidi ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa swali la Mheshimiwa Jesca kwa sababu pamoja na swali alilouliza hapa, tunafanya jitihada pamoja kuhakikisha kwamba tunaunganisha nguvu kupeleka vijana kwenda kusoma nchi za nje ikiwa ni pamoja na nchi ya Uturuki ambapo wameendelea vizuri sana katika masuala ya ufundi stadi na elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuhakikisha kwamba tunaanzisha taratibu kwanza za kuwa na staff exchange ya walimu wetu wa ufundi kwenda nchi nyingine kuangalia wanafundishwa vipi na kuleta walimu kutoka nje kuja kukaa kwa muda katika vyuo vyetu ili kuboresha elimu ya ufundi. Vile vile kupeleka wanafunzi wetu katika nchi ambazo zimeendelea vizuri zaidi katika elimu za ufundi ikiwa ni pamoja na Uturuki. Namwahidi Mheshimiwa Jesca kwamba jitihada ambazo ameshazianza tutazifanya pamoja mpaka tutazikamilisha. Ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa imethibitika pasipo shaka kwamba maendeleo sio miujiza. China wana Vyuo karibu 7,294 vya shule za ufundi. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Sera ya kuwa na vyuo kama ilivyokuwa kwenye Sera ya Afya kwamba kila Kata, sasa Sera hii iende kwenye kila jimbo na hasa majimbo ya vijijini ili tuwafundishe sasa watu wetu kulima katika maeneo madogo, tija kubwa pia ili waweze sasa kubadilisha udongo badala ya kuchoma majani wawe wanafukia? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua sana umuhimu wa elimu ya mafunzo ya amali ambayo mara nyingi tunaita mafunzo ya ufundi stadi na ndio maana sasa hivi tume-register vyuo takribani 809, vya Serikali 77 na vingine vilivobaki ni vya watu binafsi na bado vile vile Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi stadi 65, kimoja cha Mkoa wa Songwe na Vingine 64 kwa ajili ya kila wilaya. Pamoja na hivyo kama ambavyo tutakuja kulieleza Bunge lako katika Semina ambayo tutakuja kukuomba, Mabadiliko ya Sera na Mitaala ambayo yanafanyika yataongeza ufundishaji wa elimu ya amali (ufundi stadi katika Shule za Serikali) ili kuhakikisha kwamba kweli tunaongeza ujuzi kwa wanafunzi wetu wanaohitimu, ahsante.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuwa kwenye majibu ya Waziri katika ukarabati wa awali nimesikia baadhi ya Vyuo Vikuu ambavyo vimekarabatiwa, lakini sikusikia Chuo Kikuu cha UDOM na kwa kuwa Chuo Kikuu cha UDOM kina changamoto sugu ya uhaba wa maji kwa miaka kumi na sita sasa toka 2007, ambayo inapelekea uchakavu wa majengo yale. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali inakwenda kuondoa changamoto ya miundombinu ya maji katika Chuo Kikuu cha UDOM? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa Chuo Kikuu cha UDOM kilikuwa kinajengwa kwa phase na kwa kuwa ujenzi wake bado haujakamilika, kuna uhaba wa madarasa na hakuna kabisa nyumba za watumishi. Je, Serikali imejipangaje sasa kwenda kumaliza phase za ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDOM?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilitaja baadhi ya Vyuo ambavyo tayari Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati na ku–improve miundombinu chakavu lakini sikutaja vyuo vyote ambavyo vimenufaika na fedha za Mradi wa HEET. Chuo Kikuu cha UDOM ni kati ya vyuo ambavyo vimenufaika na fedha za mradi huu wa HEET na tayari fedha zimeshapelekwa kwa ajili ya ujenzi. Suala la maji UDOM kwa ujumla wake tunaendelea kulishughulikia kwa kushirikiana na Wizara husika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata utatuzi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake tunaongeza jitihada kuhakikisha kwamba vyuo vyote ikiwa ni pamoja na UDOM tunamaliza ujenzi na ukarabati katika maeneo ambayo yalikuwa hayajakamilika ili wanafunzi wetu waweze kupata huduma nzuri ya elimu ya juu.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Naomba kuuliza Swali dogo la nyongeza. Wakati ambapo wenzetu wanazungumzia kuboresha Vyuo Vikuu chakavu, Mkoa wa Njombe hauna Chuo Kikuu hata kimoja, mara kwa mara tumekuwa tukiomba na kwa kuwa Wilaya ya Makete tuko tayari kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu chochote kile ambacho unaweza kuona kinafaa;

Je, ni lini Serikali na ipi ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Jimbo la Makete na Mkoa wa Njombe kwamba mtajenga Chuo Kikuu?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hakuna Mkoa hapa nchini ambao hauna Tawi la Chuo Kikuu Huria, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Sanga kwamba Njombe siyo kati ya Mikoa ambayo inayo au itanufaika sasa hivi kwa mradi wa HEET kwa kuwa na kampasi ya Chuo Kikuu kwa jitihada ambayo Serikali imefanya kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tumesambaza kampasi katika Mikoa kadhaa. Mipango iko mbioni ya mazungumzo na Mkoa wa Njombe kuhakikisha kwamba tunapeleka kampasi kule. Ningeomba details tuzitoe baada ya kukamilisha mikakati hii, lakini tunatambua umuhimu huo na tunajua kwamba kulikuwa na ahadi ilitolewa pale Njombe kwamba Njombe na yenyewe itapata kampasi ya Chuo Kikuu.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Je, Serikali ina mpango gani kujenga au kuboresha vituo atamizi katika vyuo vyetu vikuu au taasisi za elimu ya juu, kwani hivi vituo ndio chachu ya kutengeneza viwanda hapa nchini?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba vituo atamizi ni muhimu sana kwa ajili hasa ya kuunganisha juhudi za taaluma na maendeleo ya viwanda na maendeleo ya nyanja nyingine mbalimbali hapa nchini, nguvu kubwa tunazielekeza huko. Naamini hata baadhi ya Wabunge watakuwa wamepata fursa ya kuangalia wiki ya ubunifu ambayo inaendelea kwenye viwanja vya Jamhuri leo na juhudi ambazo tumezifanya na baadhi ya matokeo ambayo tayari tumeshazifanya. Kwa hiyo, tunalichukulia suala hili kwa umuhimu mkubwa na tutajitahidi sana kuongeza juhudi ya kuwa na vituo vyakutosha atamizi katika vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kesho tunazindua Industrial Advisory Council ya Sokoine ambayo vilevile ni kwa ajili ya kuunganisha juhudi za maendeleo ya viwanda na Chuo Kikuu cha Sokoine na vyuo vingine vyote hapa nchini.
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tunatambua kwamba lengo la Serikali kuweka utaratibu huu ni pamoja na kutambua uwezo wa kiakili wa watoto wetu pamoja na uwezo wao wa kusoma kwa muda fulani. Tunavyozungumza, kuna shule za primary hasa za watu binafsi ambazo mwanafunzi wa kutwa anaenda shuleni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na moja na wa bweni anasoma tena kuanzia saa moja mpaka saa tatu au saa nne usiku, zaidi ya muda ambao umepangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Je, Serikali inatambua kwamba kuna shule ambazo zinafanya utaratibu huu ambao ni kinyume kabisa na utaratibu na inahatarisha afya za akili za watoto wetu? Kama inatambua, inachukua hatua gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa ajili ya umuhimu wa afya za akili za watoto wetu: Je, Serikali haioni haja kwenye marekebisho haya yanayofanyika ya utaratibu wa elimu na mfumo wake kuliingiza suala hili katika mfumo? Ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kwamba ziko shule ambazo wanafunzi wanakaa muda mrefu zaidi shuleni na vile vile wanatumia muda mrefu sana kwenda shuleni na kuna aina mbili ya changamoto katika jambo hili. Kwanza, sio wanafunzi wote wanatumia mitaala ile ile. Ziko shule ambazo zinatumia mitaala tofauti na ile ambayo imetolewa na Serikali. Kwa mfano, kuna wale wanaotumia mitaala ya Cambridge na muda wao wa kusoma siyo lazima uwe sawa na muda wetu. Pili, kwa kuchagua shule, hasa hizi binafsi na umbali wa shule na nyumbani, baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanaondoka mapema sana nyumbani na wanarudi kwa kuchelewa sana, kwa sababu tu ya choice ya wazazi kwamba pengine wanaishi Mbezi Beach lakini mtoto wako anaenda kusoma Kimara tofauti na kusoma eneo lile lile la Mbezi Beach.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili suala ni changamoto kweli kwa sababu tungependa watoto wapate fursa vile vile ya kucheza na kuwa watoto na kuwa na makuzi mazuri na wasitumie muda wote tu kwa ajili ya shughuli za darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutajitahidi kuendelea kukaa na wadau wa shule binafsi kuangalia namna bora zaidi ya kutatua changamoto hii. Vile vile tunaendelea kuhimiza ujenzi wa shule mbalimbali za watu binafsi ziwe karibu zaidi na makazi ya watu na kuhimiza wazazi wachague shule ambazo ziko karibu zaidi na nyumbani ili watoto wasitumie muda mrefu sana barabarani wakati wanaenda shuleni.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Shule ya Msingi Bupandwa, Kasisa, Ruhama, Mwabasabi zina uhaba mkubwa sana wa walimu na hivyo kuwafanya walimu kufundisha kwa masaa mengi kuliko kawaida na watoto kushindwa kuelewa: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuwasiliana na Waziri wa TAMISEMI ili aweze kututafutia walimu wa kutosha watoto wetu waweze kujifunza kwa urahisi na kuelewa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shigongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna maeneo yana uhaba mkubwa wa walimu, mtawanyiko wa walimu siyo sawia kama ambavyo tungependa. Bahati nzuri kuna nyongeza, walimu wataajiriwa hivi karibuni na tunazungumza na wenzetu wa TAMISEMI ili kuhakikisha kwamba walimu wale wanatawanywa maeneo yale ambayo yana uhitaji mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, sasa hivi tuna utaratibu wa kuweza kutumia walimu wa kujitolea kwa ajili ya kuendelea kupunguza uhaba wa walimu na tutaendelea na jitihada hizi ili kuhakikisha kwamba kweli wanafunzi wote popote pale Tanzania wanapata huduma ya kufundishwa kama inavyotakiwa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tunatambua na tunajua kwamba elimu ni haki ya msingi kwa mtoto na kwa mwanadamu; na amesema kwamba kuna ile ratiba ambayo imepangwa elimu ya awali, elimu ya msingi mpaka elimu ya Sekondari; sambamba na hilo, kuna suala zima la watoto wenye mahitaji maalum hasa autism: Je, ratiba hii inaenda sambamba na hayo ambayo Mheshimiwa Waziri ameyasema?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tuna wanafunzi wenye mahitaji maalum na ambao wanahitaji muda mrefu zaidi kusoma kwa ajili ya kuweza kulingana na wenzao darasani. Njia mojawapo ambayo inatumika sasa hivi wakati wa kufanya mitihani kulingana na changamoto ambayo inafahamika, wanafunzi wanapewa muda tofauti wa kufanya mitihani. Vile vile katika mitaala mipya hii, hili suala limeangaliwa kutokana na maoni ya wadau ili kuhakikisha kwamba kweli tunatoa unyumbufu wa kutosha kuweza kuwa-commodate wale wanafunzi wenye mahitaji maalum hasa wakati wa kufundisha darasani.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna ongezeko kubwa la thamani ya bidhaa zinazotokana na ubunifu, kwa mfano, kutoka mwaka 2002 kulikuwa na shilingi bilioni 208, kufikia mwaka 2020 zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa takwimu za Umoja wa Mataifa. Je, Serikali imejipangaje kulinda hakimiliki za wabunifu wa Kitanzania ili washiriki kikamilifu katika uchumi bunifu wa dunia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa uchumi bunifu na bidhaa bunifu ni utajiri wa kibiashara na kiutamaduni. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa Wizara ya Elimu kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Wizara ya Fedha na taasisi nyingine za kibiashara kuona kwamba Tanzania inashiriki kikamilifu katika uchumi bunifu katika dunia yetu? Nashukuru.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Londo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kwanza kuchochea bunifu mbalimbali hapa nchini na kuanzia mwaka 2019, Serikali imekuwa ikiendesha Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama KISATU kwa ajili ya kualika watu mbalimbali walete bunifu zao, washindanishwe, zitambuliwe na ziendelezwe. Baada ya kuendelezwa ziweze kulindwa kwa kupata hakimiliki. Tangu tuanze mashindano hayo tayari bunifu 283 zimeshahakikiwa, 38 tayari ziko sokoni nazo hizo zinalindwa kwa ajili ya kuingia sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake Serikali inaona umuhimu sana wa kuchochea bunifu kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, ndiyo maana vile vile tunasaidia vijana wetu ambao wanaenda na bunifu mbalimbali katika mashindano ya Kimataifa na baadhi yao wameshinda tuzo mbalimbali na sisi tunachochea waingie sokoni kwa ajili ya kubiasharisha bunifu zao.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, Serikali ina mpango gani wa kutambua na kuendeleza ubunifu unaofanywa na wanafunzi kwenye vyuo vyetu hapa Tanzania kikiwepo Chuo cha DIT ambapo kuna mwanafunzi mmoja anaitwa Angella Cliff Nkya ametengeneza mfumo wa ku-control makosa ya barabarani ili waweze kuendelezwa na Serikali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua bunifu zote za wanafunzi na watu mbalimbali hata watu walioko vijijini na wanafunzi wamechangia vile vile katika baadhi ya bunifu ambazo sasa hivi zimeanza kuingia sokoni. Zipo bunifu ambazo tayari zimeshaanza kutambulika, zinafahamika na hatua iliyobaki kwa kweli sasa hivi ni kuhakikisha kwamba bunifu hizo zinaingia sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe mfano mmoja tu, bunifu ya kuweza kulipia bili ya maji kwa kutumia simu janja ambayo imegunduliwa na Mtanzania, sasa hivi inafanyiwa majaribio kwa ajili ya kununuliwa na Mamlaka ya Maji Tanzania na kutumika.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri mno ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa sababu mradi wa HEET ume-fund vyuo vya umma pekee ambavyo viko 15 kati ya 47 vilivyopo nchini: Ni upi mkakati wa Serikali kuona namna wataweza kuviwezesha vyuo vya private ambavyo kimsingi ni vingi kwa idadi hii ili na vyenyewe viweze kufanya mapitio ya mtaala ili viendane na dira na mwelekeo wa Serikali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna terms of reference zipi ambazo Serikali wameshavipatia vyuo vya private ambavyo waliamua kuanza wenyewe kufanya mapitio, ili sasa kuona namna gani bora tunaweza tukafungamanisha dira na mwelekeo wa Serikali kwenye elimu ambayo inatolewa katika mtaala wa vyuo vikuu nchini? Ahsante.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nusrat Hanje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza pamoja na kwamba, fedha nyingi zaidi za Mradi wa Higher Education for Economic Transformation zimepelekwa katika vyuo vya umma, bado fedha zimetengwa vilevile kwa ajili ya sekta ya vyuo binafsi kwa mfano, kutoa scholarship, lakini na mafunzo ambayo yanaendeshwa kwa ajili ya kubadilisha mitaala yanachanganya vyuo vyote bila kujali kama ni binafsi ama vya umma.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TOR; vyuo vyote, kama nilivyosema katika kujibu swali la msingi, vinatengeneza mitaala yao kwanza kwa kupitia kwenye seneti zao, baada ya kukamilisha ndio zinapelekwa kwenye Commission ya Elimu ya Juu kwa ajili ya kupata ithibati. Chuo kinapata kibali cha kuwa chuo kikuu kwa sababu, tunaamini seneti yao ina uwezo mkubwa wa kuidhinisha mitaala. Sasa sisi maelekezo yetu ni kwamba, sasa hivi tuanze kuongeza elimu ya mali na kuzingatia vipaumbele vya nchi, hilo tumeshazungumza na ma-vice chancellors wote wa vyuo vyote na wakati wa kupitisha kwenye ithibati kuna fursa ya sisi kuangalia ni kiasi gani wameji-align na muelekeo huo wa kitaifa.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipatia fursa hii kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kujenga vyuo vya VETA sehemu mbalimbali. Je, Serikali ina mkakati gani kufungamanisha mitaala ya vyuo vya VETA na sehemu vilikojengwa? Kwa mfano Kagera tumepata Chuo cha VETA, tunaishukuru Serikali, kufungamanisha mtaala wa VETA na uchumi wa Mkoa wa Kagera kama kusindika kahawa, uvuvi na maeneo mengine kama madini? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba, Vyuo vya VETA vinawaandaa watu kwa ajili ya ajira na kuweza kumudu mazingira ambayo wapo. Na mkakati wa Serikali ni kwamba, pamoja na zile kozi mbalimbali za VETA ambazo kwa kweli zina-cut across kwa mfano kusoma wiring, electrical wiring au mechanics, n.k., lakini kila Chuo cha VETA kinashauriwa kufanya kazi na maeneo yale pale, ili kuchagua baadhi ya masomo ambayo yanakidhi matakwa ya eneo lile ambalo wanafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, najua kwa mfano, chuo ambacho kinajengwa pale Mkuranga kutakuwa na mazungumzo na wanaojenga viwanda katika eneo lile kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, mafunzo yanayofanyika pale yanaendana na mahitaji. Kwa hiyo, kadhalika hata cha Kagera na sehemu nyingine tutaendelea kufanya hivyo.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuuliza swali kwamba, zamani tulikuwa na vyuo kama Sokoine kinahusika na kilimo, IFM kilikuwa kinahusika na fedha, Mzumbe inahusika na sheria na utawala, ardhi kinahusika na ardhi, lakini siku hizi kumekuwa na kozi mbalimbali zinazoingia ambazo zinatofautiana na asili ya vyuo hivi. Ni upi mkakati wa Serikali kuona vyuo hivi vinabaki kwenye asili yake, ili tuendelee kuzalisha wataalamu bora zaidi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Sanga kwamba, kuna wakati vyuo vilipoanzishwa vilikuwa vina-specialize katika maeneo mbalimbali na vingine kwa kweli, vilikuwa ni taasisi ya elimu ya juu, lakini sio vyuo vikuu kwa tafsiri ambayo tulikuwanayo kwa mfano Mzumbe kilikuwa kinatoa Advanced Diploma badala ya kutoa Degree. Baada ya mageuzi ambayo yalitokea hapo kabla vyote vilipewa vibali vya kuwa vyuo vikuu na hivyo walikuwa wanaweza wakaanzisha programs mbalimbali na wakipata kibali walikuwa wanaendelea kwa hiyo, maana yake hata vyuo kama Sokoine vimeongeza baadhi ya programs nje hata ya eneo ambalo mwanzoni walikuwa wamelizingatia.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hivyo tuna-insist na tutaendelea kufanya jitihada kuhakikisha kwamba, kila chuo kikuu kinajaribu kuwa na eneo ambalo wame-specialize, ili kuwa na competence kubwa zaidi. Kwa hiyo, kama Sokoine tutatarajia kwamba, waongeze nguvu sana kwenye kilimo, kuna chuo kama Nelson Mandela ambacho kime-specialize kwenye sayansi na teknolojia tungependa wa-focus zaidi kwenye sayansi na teknolojia na kadhalika.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri; huko nyuma imezoeleka mara panapotokea mabadiliko ya mtaala, hizi competence base kwenye madarasa, Serikali inachukua walimu wa Serikali kwenda kuwapa mafunzo kwa ajili ya mabadiliko ya teknolojia, lakini shule za private wanachajiwa na wanalipia. Je, katika huu mtaala mpya unaoendelea sasa Serikali iko tayari kuanza kuunganisha walimu wa private na Serikali ili wawe wanakwenda pamoja kwa sababu, watoto wote ni wa kitanzani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mulugo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kila mitaala inapobadilika Serikali hutenga bajeti kwa ajili ya kuwafundisha walimu kujiandaa kwa ajili ya utekelezaji wa mitaala mipya. Ni kweli kwamba, wakati mwingine fedha ambazo zimekuwa zikitengwa zilikuwa zinakidhi tu kuweza kuwaandaa walimu wa sekta ya umma kwa ajili hiyo na sekta binafsi wanapohudhuria wakati mwingine walikuwa wanachangia au wanajigharamia wenyewe, lakini huduma nyingine wanapewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, tunaongeza jitihada za kuhakikisha kwamba, mabadiliko ya mitaala ambayo yanakuja tutajitahidi kukusanya walimu wote bila kujali wanatoka sekta binafsi au sekta ya umma. Lakini kwa kadiri bajeti itakavyoruhusu tunaweza tukawalipia hata wale wa sekta binafsi. Kama hairuhusu tutawaalika wahudhurie katika semina na mafunzo haya bila kuchajiwa chochote kwa sababu, wale wanaoandaa mafunzo haya na kumbi na gharama za chakula na kila kitu ni ruzuku ya Serikali kwa ajili ya kusaidia vilevile shule binafsi kuandaa walimu wao. Nashukuru.