Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda (10 total)

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Manyoni?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mia moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi. Aidha, Wilaya ya Manyoni ni miongoni mwa Wilaya hizo 62 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ambapo Serikali inaendelea na hatua hizi, nashauri wananchi wa Wilaya ya Manyoni wakiwemo wa Jimbo la Manyoni Mashariki waendelee kutumia Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Singida, na Chuo cha Wilaya ya Ikungi, Pamoja na Vyuo vya Singida vya FDC na vyuo vingine vya ufundi stadi vilivyopo hapa nchini. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafufua Shule za Msingi za Ufundi Wilayani Hai na kurejesha mfumo wa wanafunzi kufanya mitihani na kupewa vyeti?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elinikyo Mafuwe Saashisha, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali iko katika mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na uboreshaji wa Mitaala ya Elimu ili iweze kuwajengea wanafunzi stadi na ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi utakaowawezesha kuhitimu na kuhimili ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi. Mara baada ya mitaala tajwa kukamilika ikiwa ni pamoja na manunuzi ya vifaa na mashine mbalimbali za ufundi, Elimu ya Ufundi itatolewa katika Shule za Msingi na Sekondari. Aidha, utaratibu wa kufanya mitihani ya Elimu ya Ufundi na kupata vyeti utaandaliwa kwa kushirikiana na mamlaka husika kama vile Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Mheshimiwa Spika, pamoja na mapitio ya Sera na Mitaala, Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Chuo cha Ualimu Kleruu pamoja na Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Morogoro (MVTCC) kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kwa lengo la kuongeza fursa ya mafunzo kwa Walimu wa masomo ya Ufundi.

Mheshimiwa Spika, pia Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya kimeanza maandalizi ya utoaji wa mafunzo hayo katika ngazi ya Stashahada katika Elimu ya Ufundi, (Diploma in Technical Education na Postgraduate Diploma in Technical Education). Kwa sasa mitaala ya masomo hayo inafanyiwa kazi na Tume ya Vyuo Vikuu ili kuidhinishwa na kuanza kutumika katika Chuo hicho. Ahsante sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, ni vijana wangapi wa Tanzania wamepata nafasi za masomo nje ya Nchi kwa mwaka 2015-2020 na wangapi wanatoka Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi za ufadhili wa masomo unaotolewa na mashirika au nchi rafiki zinazopitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, huratibiwa kwa ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano. Idara za elimu ya juu zina jukumu la kubaini sifa za waombaji na kupendekeza wanufaika wa ufadhili kwa kuzingatia vigezo bila kujali mwombaji anatoka upande upi wa Muungano. Aidha, zipo baadhi ya nafasi za ufadhili wa masomo ambazo huratibiwa moja kwa moja na nchi au shirika linalotoa ufadhili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 - 2020, Wizara ya Elimu, Sayani na Teknolojia kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliratibu ufadhili wa masomo katika nchi za Uingereza, Hangaria, China, Morocco, Misri, Algeria, Urusi, Ujerumani, Msumbiji, Thailand, Mauritius, Iran na Indonesia. Watanzania walionufaika na ufadhili huo ni 873 ambapo kati yao wanaume ni 587 na wanawake 286.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italifanya somo la kilimo kuwa la lazima kwenye Vyuo vya Ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi kutoa mafunzo yanayozingatia shughuli za kiuchumi za maeneo husika na Taifa kwa ujumla ili kuwawezesha wananchi kutumia kikamilifu fursa na rasilimali zilizopo nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imekuwa ikifanya upembuzi yakinifu kabla ya uanzishaji wa fani za ufundi ili kubaini mafunzo yanayofaa kutolewa katika vyuo hivyo kulingana na fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo husika. Kozi ya kilimo ni miongoni mwa Kozi zinazotolewa katika Vyuo vya Ufundi Stadi vya Kihonda, Dakawa, Katavi, Arusha na Manyara. Aidha, katika Vyuo vipya 64 vya Wilaya vinavyojengwa, kutakuwa na karakana moja kwa kila

chuo kwa ajili ya kutoa mafunzo yatakayozingatia shughuli za kiuchumi katika eneo husika ikiwemo kilimo, nashukuru.
MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa miundombinu chakavu katika Vyuo Vikuu?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika Vyuo Vikuu vya Umma hapa nchini. Ili kutatua changamoto ya uchakavu wa miundombinu vyuoni Serikali imefanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na Chuo Kikuu cha Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inaendelea na ukarabati wa miundombinu chakavu na ujenzi wa miundombinu mipya katika Vyuo Vikuu vyote vya Umma 14

na Taasisi tano (5) za Elimu ya Juu zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji vyuoni. Aidha, Taasisi hizi zimekwishapokea fedha kwa ajili ya kuendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu kupitia Mradi wa Mageuzi ya Uchumi katika Taasisi za Elimu ya Juu (HEET).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, kwa nini ukomo wa saa za kufundisha Wanafunzi haujawekwa kisheria kama ilivyowekwa kwa saa za kazi kwa Waajiriwa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Elimu haijaweka ukomo wa saa za kufundisha wanafunzi ili kutoa fursa ya mtaala kuwa nyumbufu kulingana na mahitaji maalumu ya ujifunzaji wa wanafunzi wote pamoja na mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mitaala ya Elimu ya Msingi na Sekondari imeweka bayana Muda (duration) unaopaswa wanafunzi kusoma. Mtaala wa Elimu ya Msingi unaeleza kuwa muda wa kusoma Elimu ya Awali na Darasa la I - II ni masaa matatu tu kwa siku na kipindi kimoja ni dakika 30. Aidha, Muda wa kusoma kwa darasa III - VII ni masaa sita kwa siku na kila kipindi ni dakika 40. Aidha, kwa upande wa Elimu ya Sekondari muda wa kusoma ni masaa matano na dakika 20 na kipindi kimoja ni dakika 40. Aidha, kwa mwaka wanafunzi hutakiwa kusoma kwa siku 194.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) K.n.y WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inao mpango wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini kwa lengo la kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wanafunzi viziwi na katika jamii. Aidha, katika mchakato wa mapitio ya sera ya mitaala unaoendelea somo la Lugha ya Alama limependekezwa liwe la lazima kwa walimu wote tarajali katika vyuo vyote vya ualimu na vyuo vikuu nchini.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mpango na mapendekezo hayo, tayari Serikali imeandaa na kusambaza kamusi ya lugha ya alama ya Tanzania ya kidijitali katika shule na vyuo vinavyopokea wanafunzi viziwi. Aidha, kozi ya lugha ya alama ya Tanzania inatolewa katika Chuo cha Ualimu Patandi na Kabanga na katika Vyuo Vikuu vya Dodoma, Dar es Salaam na Archbishop Mihayo University College Tabora kwa lengo la kumudu darasa jumuishi. Aidha, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa walimu maalum na wasio wa elimu maalum 3,650 wa shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwafundisha na kuwahudumia wanafunzi viziwi ili kujenga jamii jumuishi ya viziwi shuleni.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza:-

Je, ubunifu una nafasi gani katika kuleta mageuzi ya kiuchumi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ubunifu ni nyenzo na kichocheo cha kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali za uzalishaji na kutoa huduma nchini. Matumizi ya ubunifu yameongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma. Aidha, maeneo yaliyonufaika zaidi ni pamoja na: mawasiliano, huduma za fedha, utawala, masoko, afya, tafiti na usimamizi wa fedha za umma, mitambo inayojiendesha, kompyuta na roboti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ubunifu wa teknolojia mpya ikiwemo mifumo ya TEHAMA katika undeshaji wa shughuli za Serikali (e-Government) na kukusanya mapato ya serikali kwa njia ya kielektroniki (GePG) kwa kiasi kikubwa zimechangia katika mageuzi ya kiuchumi tunayoshuhudia nchini. Mathalan ubunifu uliowezesha kutuma na kupokea fedha kupitia simu za mkononi, umeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini hasa kwa wafanyabiashara na wananchi mijini na vijijini.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, lini Serikali itapitia Mtaala wa Vyuo Vikuu ili kufungamanisha elimu sambamba na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu. Katika ngazi ya Vyuo Vikuu, kikanuni, mitaala huandaliwa na Vyuo Vikuu vyenyewe kisha kuidhinishwa na Seneti na kuwasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu kwa ajili ya uhakiki na ithibati. Hata hivyo, tayari Wizara yangu imeshatoa maelekezo kwa Vyuo Vikuu kuhuisha na kufanya maboresho ya mitaala yote ili iendane na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa ambayo kwa sasa inalenga kutoa Elimu itakayompa kijana wa Kitanzania elimu na ujuzi kwa mujibu wa mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Spika, Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) vimepata mafunzo mbalimbali ya kuandaa programu zinazoendana na vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira. Aidha, Vyuo vimeunda Kamati za Ushauri wa Insia (Industrial Advisory Committees) zenye Wajumbe kutoka Sekta za Waajiri kwa ajili ya kuzishauri Taasisi za Elimu ya Juu kutoa programu zinazoendana na soko la ajira. Kupitia utaratibu huu, zaidi ya programu 300 zitaanzishwa au kuhuishwa ili kuendana na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa sambamba na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira, ahsante sana.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa inatekeleza azma ya kujenga Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali ilitenga shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwamo Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe kimetengewa fedha shilingi bilioni 6.53 kwa ajili ya ujenzi wa jumla ya majengo 25 ikijumuisha jengo la utawala, karakana, madarasa, maktaba, bwalo la chakula, vyoo, stoo pamoja na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshapeleka shilingi bilioni 1.14 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe ambapo kwa sasa ujenzi umefikia hatua ya kukamilika kwenye baadhi ya majengo na kazi ya ujenzi wa kuta inaendelea. Ahsante.