Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda (22 total)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwanza, nashukuru sana kwa majibu yaliyotolewa na Serikali na katika majibu hayo inaonekana kwamba imekadiriwa tani 500,000 ndiyo zitakazokuwa zinapita kwenye bandari hiyo kavu lakini mpaka sasa ni tani 200,000 tu, kwa hiyo, wanasema bandari haijazidiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la msingi ambalo nilitaka Serikali ilifahamu ni kwamba kutokuongezeka kwa mizigo kumetokana na kukosekana kwa mabehewa ya mizigo na ubovu wa reli vitu ambavyo vinakwenda kutengenezwa katika bajeti ya mwaka huu. Je, Serikali haioni kama ni busara kwenda sambamba na kukamilisha bandari hiyo badala ya kusubiri bandari izidiwe wakati ile bandari kavu ya kuhifadhi makasha itakuwa haijakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA W. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba shehena ilikuwa imepungua na mwaka huu wa fedha tunaongeza mabehewa na katika jibu la msingi utaona tayari fidia ya eneo hilo lote hekta 69 imeshafidiwa na mwaka wa fedha ujao tunaanza ujenzi. Kwa hiyo, kwa kadri tutakuwa tunapata fedha tutakuwa tunajenga kwa kadri ya mahitaji yanavyokua. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba bandari hii haitazidiwa na itajengwa kadri tutakapokuwa tunapata fedha. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi wowote ule, tunalifanyia kazi, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nitaomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ni ukweli kwamba tunajua umuhimu wa kazi ya Idara ya Uhamiaji katika kusimamia masuala aliyoyasema Mheshimiwa Waziri ya ungiaji wa wageni ukaaji wao. Hata hivyo, kiwango cha usumbufu wa wananchi unaotokana na doria za uhamiaji kimepita kiasi ambacho sisi tunakifahamu katika historia ya Mkoa wetu wa Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri aniambie kuna jambo lipi jipya ambalo limejitokeza linalosababisha kwa sasa kuwe na misako inayosumbua hata raia halali waliokaa katika mkoa wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; msingi wa kukua kwa tatizo hili ni kuchelewa kwa Wizara yake kutoa vitambulisho vya NIDA kwa wananchi halali wa Mkoa wa Kigoma, jambo ambalo lingekuwa limekamilishwa, haya yote yasingekuwepo. Anieleze ni lini Serikali itakamilisha kazi hii ya kutoa vitambulisho vya NIDA ili kuondokana na usumbufu huu; na kama inawezekana misako hiyo isimame mpaka hapo mtakapokamilisha vitambulisho vya NIDA? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha usumbufu katika kusimamia Sheria ya Uhamiaji, Kifungu cha 12 kama ilivyorejewa mwaka 2016 ambapo Jeshi la Uhamiaji limepewa jukumu la kufanya misako, doria na hata ikibidi kufanya upekuzi ili kubaini nani ni raia na nani sio raia; zoezi hili kama tulivyojibu katika jibu letu la msingi, linafanyika kwa nchi nzima. Usumbufu huu unatokana na mkoa ulivyo na mipaka na majirani zetu ambapo mara nyingi kumekuwa kuna shida katika nchi zao na kwa hiyo wana msukumo mkubwa sana wa kuja katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli kwa muda wa miezi mitatu tumekamata wahamiaji haramu zaidi ya 1,000. Kiwango hiki ni kikubwa na siyo rahisi tusifanye doria, lakini tunafanya hivyo kwa mikoa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anauliza vitambulisho vya NIDA vingetotewa basi usumbufu usingekuwepo. Ni kweli, lakini nataka niseme, kupewa kitambulisho cha NIDA cha uraia wa Tanzania siyo mwarobaini kwamba wewe sasa huwezi ukaulizwa kuhusu uhalisia na uhalali wa uraia wako. Sheria hizi ni mbili tofauti; kuna Sheria ya Uraia, Sheria ya Uingiaji Nchini na Sheria ya Vitambulisho vya Taifa na zote hizi zinashughulikia mambo mawili tofauti. Vitambulisho hivi hata wakazi wasio raia wanapewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna madaraja tofauti tofauti ya kutoa vitambulisho. Siyo kwamba ukipewa kitaambulisho hiki, basi wewe hutaulizwa tena. Tutaulizwa, hata mimi naweza nikaulizwa uraia wangu hata kama nina kitambulisho na hata kama natoka Dodoma; nitaulizwa uraia wangu na uhalisia endapo utajitokeza wasiwasi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo majibu yetu ya Serikali na tunaomba Mkoa wa Kigoma watuelewe hatufanyi kwa Mkoa wa Kigoma peke yake, tunafanya kwa mikoa yote. Hivi sasa kuna oparesheni imeanza tarehe mosi itaisha tarehe 15 ya mwezi huu kwa mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona nilitaka kuulizwa swali la nyongeza kwamba viporo vya barabara zinazounganisha mikoa ni pamoja na viporo vya barabara ya eneo la Malagalasi - Uvinza kilometa 51 na kiporo cha barabara inayotoka Tabora kuja Nguruka kilometa 40; nataka nijue Serikali ni lini ujenzi wa viporo hivi kukamilisha barabara inayounganisha Mkoa wa Kigoma na Tabora vitakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara alizozitaja za Kaliua mpaka Chagu yenye kilometa kama 36 tayari mkandarasi yupo site na amepiga kambi Kijiji cha Usinge, kwa hiyo ujenzi unaanza, lakini katika barabara ambazo zimetangazwa mwezi huu ambazo zinafadhiliwa na Mfuko wa OPEC kutoka Malagalasi hadi Uvinza yenye kilometa 51.3 tayari barabara hii imeshatangazwa kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi kwa kiwango la lami na hivyo Mheshimiwa Kilumbe na wananchi wa Kigoma baada ya muda si mrefu kuanzia Dodoma mpaka Kigoma itakuwa ni kwa lami tu bila kugusana na vumbi, ahsante. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa suala la kujenga uwezo wa halmashauri na hasa katika miradi hii ya kimkakati linakwenda sambamba na suala la kuinua hali za wananchi kiuchumi ili waweze kushiriki vizuri katika miradi hii, nini hatua ya Serikali mpaka sasa katika kilio kikubwa cha wananchi cha kupunguza riba za mabenki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hapa wakati wa mjadala wa bajeti, Mheshimiwa Kilumbe alikuwa miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge ambao walilizungumzia sana tatizo hili la ukubwa wa riba katika mabenki yetu ya biashara. Muda mfupi Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa Serikali kuangalia jinsi gani ambavyo tutapunguza riba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kama ambavyo nilikuwa nimeeleza jana wakati najibu swali, naomba nirudie kuwahakikishia kwamba yale maeneo matano ambayo Benki Kuu ya Tanzania iliyaainisha kuwa kama ni njia ya kuweza kufikia malengo hayo tayari yameshaanza kufanyiwa kazi. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda kwamba, wakati wowote kuanzia sasa mabenki kadhaa tayari yameshaanza kupeleka maombi yao kwenye Benki ya Tanzania kwa ajili ya kutumia fursa hizo zilizotolewa zenye dhamira ya kufikia malengo haya ya kuhakikisha kwamba riba inakuwa nafuu kwa kiwango kisichozidi asilimia kumi.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua kama Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu waliamua kufunga maduka ya fedha za kigeni kwa sababu yalikuwa hayafuati taratibu, na sasa zipo financial institution nyingi mjini humu ambazo zinakopesha kwa riba ya juu na kuumiza walimu na watumishi wengine wa umma. Hivi Serikali inapata kigugumizi gani kuzifunga hizi ambazo zinatesa wananchi na badala yake inakwenda kufunga maduka ya fedha za kigeni ambayo yalikuwa hayalalamikiwi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika ilikuwa ni kuzifuta leseni kwa wale ambao walibainika kuwa wamekiuka taratibu; na hii ipo kwa mujibu wa sheria pamoja na regulation ambazo tumetunga za mabadiliko ya fedha za kigeni, wanaita Foreign Exchange Act, kwa hiyo hii ilichofanyika imefanyika kwa mujibu wa sheria.

Sasa kuhusiana na kwamba kwanini kuna taasisi nyingine ambazo zinaumiza wananchi wa riba kubwa, jana nilimpongeza sana Mheshimiwa Kilumbe hapa, kwasababu nilisema kwamba kama kuna Wabunge ambazo walishiriki katika mjadala wa Bunge la Bajeti lililopita, kuzungumza kwa uchungu na hisia kazi juu ya baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikinyanyasa wananchi kwa kuwakopesha kwa riba kubwa bila msingi yeye alikuwa ni mmojawapo. Nikasema kwamba kwa kusikia kilio hicho hicho kwa Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa hakuchelewa kwa kutoa maelezo ili jambo hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, na nimewahakikishia juzi na jana wakati najibu maswali kwamba kwanza niwapongeze BOT kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, sasa hivi mchakato huu umeshaanza. Kwa hiyo ni matarajio yangu sasa kile kilio cha Waheshimiwa Wabunge akiwepo Mheshimiwa Kilumbe cha kupunguza riba sasa kimepatiwa dawa. Kwa hiyo hoja hizo mbili zote zinachukuliwa hatua kwa utaratibu wake kulingana na sheria na taratibu za nchi yetu.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Ujenzi kwamba katika kazi zilizotangazwa na zilizoanza kufanyika sasa hivi na TANROAD kule Kigoma, nyingi zimekwama kwa sababu GN hazijatolewa. Je, mna mpango gani wa kufanya mawasiliano na Wizara ya Fedha kuhakikisha GN hizo zinatoka kabla mvua nyingi hazijaanza kunyesha katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inafanya mawasiliano na Wizara ya Fedha na tunapoongea hivi nina hakika muda siyo mrefu GN zitakuwa zimetoka ili tuweze kuanza kutekeleza hiyo miradi haraka kabla ya mvua haijakolea. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, labda kama kuna barabara ambayo ni specific ama kuna shida, hiyo haitatoka GN mpaka wajiridhishe kwamba kila kitu kimekaa sawa. Ila kwa barabara nyingine nina hakika siyo muda mrefu zabuni zote zitatangazwa baada ya kutoka hiyo GN. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa na Serikali ni kwamba kampuni iliyokuwa inafanya utafiti ya Beach Petroleum tangu mwaka 2017 imeshindwa kuendelea na kazi hiyo kutokana na kina kirefu cha maji na wenyewe kushindwa gharama hiyo: -

Je, Serikali imetafuta mwekezaji mwingine katika eneo hilo tokea hiyo 2017? Kama hivyo ndiyo, wananchi wategemee lini utafiti huo kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2017 pale ambapo kitalu kilirudishwa na mwenzetu wa beach petroleum mtakumbuka kwamba kulikuwa kuna upiatiaji wa mikataba ya uvunaji na ushirikiswaji (PSA) na hivyo tangu kipindi hicho Serikali haijatangaza vitalu wazi kwa ajili ya wawekezaji kuja kufanya utafiti katika maeneo hayo. Hivyo, baada ya PSA Review kuwa zimekamilika sasa Serikali iko tayari kuanza kutanganza ili watu sasa waweze kuja kuwekeza katika maeneo hayo kwa ajili ya kufanya utafiti na baadaye kubaini uwepo wa mafuta na kuanza kuyatumia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kilumbe Ng’enga kwamba Serikali iko katika hatua za kuhakikisha inakamilisha hiyo taarifa ya PSA Review na baada ya kufanya reviews zikakamilika, itaweza kufungua kwa ajili ya kuweza kukaribisha sasa watu kuja kuendelea na utafiti. Itakapofanya hivyo, basi taarifa ya nini kimepataikana itatolewa. Nakushukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) limetangaza mpango maalum wa ufugaji wa samaki katika maneo mbalimbali duniani ikiwemo Ziwa Tanganyika. Je, Serikali yetu imechukua hatua gani za haraka za kushirikiana na shirika hili katika kufanikisha mpango huo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. FAO ni wadau wetu wakubwa na tunashirikiana nao kama Serikali. Hata hivyo, kwa jambo hili mahsusi alilolisema Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda ninaomba nimkaribishe kula swali mahsusi ili tuweze kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Tatizo la kugawa maeneo ya utawala lililokuwa limetolewa na Mheshimiwa aliyemaliza, linafanana sana na tatizo lililopo katika Jimbo langu la Kigoma Mjini na hasa kugawa maeneo ya utawala ya kata. Maombi tayari yamekwishapelekwq kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo kwenye Wizara husika. Je, ni lini Serikali itafikiria kufanya kazi hii ya kugawa kata. Zipo kata ambazo zina wakazi wengi, zina mitaa mingi, Kata kama za Mwanga Kaskazini, Mwanga Kusini, Buzebazeba na Kibirizi huko Kigoma. Je, ni lini Serikali itachukua hatua hii ili kuwarahasishia watu huduma za kiutawala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe N’genda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri zimeendelea kuwasilisha maombi ya kugawa maeneo mapya ya utawala kwa maana ya kata na nikiri kwamba Serikali tumepokea zikiwepo Kata za Kigoma Mjini, tathmini zinaendelea na baada ya tathmini hizo na kuangalia mazingira hayo, tutashauri mamlaka husika kwa maana ya mamlaka inayoweza kugawa maeneo hayo ili tuweze kufikia hatua ambayo inahitajika. Kwa hivyo nimhakikishie Mbunge kwamba, suala hilo lipo linafanyiwa kazi. Nashukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Kipande cha barabara kinachotoka Uvinza kuelekea Malagarasi ujenzi wake unasuasua sana kwa muda mrefu. Napenda kujua nini tatizo la Serikali kufanya kipande hicho cha barabara kisikamilike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilikuwa inasuasua, lakini sasa nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ya Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51, kasi imeongezeka baada ya kuondoa changamoto zilizokuwepo. Ni matumaini yetu kwamba Mkandarasi huyu ataikamilisha barabara hii ndani ya wakati. Ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kigoma, Wizara ya Ujenzi imetoa taarifa kwamba mna mpango wa kuupanua uwanja huo running way yake kutoka 1.8 kilometa na kuja kilometa 3.1; na wananchi wamepata taarifa hizo, lakini mpaka sasa hawajui ni eneo gani mtalichukua la wananchi.

Je, ni lini Wizara yako itakwenda ku-earmark maeneo ambayo yatayachukua, ili maeneo ambayo hamyachukui wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo?

Je, baada ya kuyachukuwa, mtaweza kulipa fidia kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli ahadi imeshatolewa, lakini pia nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari hata usanifu Wizara imeshafanya tayari, kutoka kilometa 1.8 mpaka kilometa 3.1. Kuhusu fidia, tayari taratibu zinaendelea ili mara taratibu, na hasa tunataka uwanja utakapoanzwa kujengwa kwa awamu ya kwanza kwa uwekezaji wa fedha ndipo awamu ya pili itakapoanza kupanua uwanja.

Kwa hiyo nikuhakaikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuanahitaji sana huo uwanja kuwa mrefu ili kupokea ndege. Serikali imejipanga kulipa fidia kwa wakati na kuanza kujenga, na taratibu zitakapoanza tutakuja kuwajulisha wananchi, wapi uwanja huo utapita. Ahsante.
MHE.KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa hatua ambayo inachukua, hata hivyo ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, uzoefu unaonyesha kwamba wanaponunua mabehewa mapya wanayapeleka katika route nyingine na route hizo mabehewa yaliyochakaa huko ndiyo wanayaunga kwenye route ya Kigoma. Sasa nataka commitment ya Serikali kwamba mabehewa haya 22 mapya yatakayokuja yatawekwa kwenye route hii?

Mheshimiwa Spika, la pili, kwa sababu mabehewa yanayokarabatiwa ni 39 na mapya ni 22 jumla ni mabehewa 59 na bado ni machache na ukizingatia kwamba Serikali ina mkakati wa kuhama kutoka kwenye narrow gauge kwenda standard gauge; je, Wizara ina mpango wa kukarabati mabehewa zaidi ili yaweze kutumika badala ya kununua mapya ambayo tukianza standard gauge tutayaacha?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shaban Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka kujua commitment ya Serikali kwamba mabehewa hayo 22 mapya je, yatakwenda Kigoma. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mabehewa haya 22 yenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 14.9 yatakwenda Kigoma na namwalika siku yatakapofika nchini Septemba mwaka huu awe sehemu ya kuyapokea haya mabehewa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema reli inayotengenezwa ni ya standard gauge na tuliyonayo ni ya meter gauge tunaonaje kwamba hizi reli ziweze kufanya kazi kwa pamoja, lakini pili ziendane na uhitaji wa mabehewa tuliyonayo. Turn worksheet ya Mheshimiwa Mbunge kwamba reli ya sasa ya meter gauge ina meter moja na standard gauge ina meter 1.475 kwa namna yoyote ile reli tuliyonayo tutaendelea kuitumia hadi hapo itakapokuja kukamilika ya standard gauge. Hata ikikamilika, lakini bado hii pia tutaendelea kuitumia. Kwa maana hiyo bado tutaendelea kukarabati mabehewa tuliyonayo kwa sababu tender ya kutangaza kutoka Tabora kwenda Kigoma ili ijengwe standard gauge bado itachukua muda. Kwa hiyo bado tutaendelea kutumia ya meter gauge. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ujenzi wa Vituo vya Polisi unakwenda sambamba na ujenzi wa makazi ya askari ili kuwawezesha Askari Polisi kupata makazi mazuri na kuweza kufanya kazi zao vizuri. Je, ni upi mpango wa Wizara kusaidia suala la nyumba za askari polisi katika eneo la Kigoma Mjini ambazo ziko katika hali mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ng’enda,
Mbunge wa Kigoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba askari wanahitaji makazi hususan yawe karibu na vituo vya polisi, lakini tunajua pia kwamba makazi mengi hasa vituo vya zamani ni mabovu, ndio maana kipaumbele kimewekwa kwenye ukarabati wa majengo yaliyochakaa. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya askari kadiri tutakavyoweza kupata fedha kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninataka kujua kwa sababu viashiria vya uwepo wa mafuta kwenye Ziwa Tanganyika vimeonekana katika utafiti wa awali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha utafiti huo ili kuweza kupata taarifa kamili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni lini wananchi wa Kigoma watarajie kupata taarifa za mwisho za utafiti huo ambao umechukua zaidi ya miaka mitano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika swali la kwanza, mbinu ambazo zinafanywa na Serikali na jitihada zinazofanywa na Serikali kama mnavyofahamu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua sana Tanzania kwa ajili ya wawekezaji, nasi Wizara ya Nishati tumekuwa tukishiriki katika maonesho mengi ya Kimataifa kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kuja nyumbani kufanya kazi pamoja nasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazofuata za utafiti ambazo zimebakia za 3D ni za gharama kubwa na Serikali imekuwa ikitafuta mbia wa kimkakati wa kushirikiana nae kwenye maeneo hayo ili kukamilisha utafiti huo ambao unatakiwa kufanyika. Mara tu baada ya kumpata na taarifa zikapatikana vizuri basi Ndugu zetu wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla watapewa taarifa ya nini kimepataikana na lini uchimbaji wa mafuta katika Ziwa Tanganyika utaanza kufanyika. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mkoa wa Kigoma unaunganishwa katika Gridi ya Taifa, mpaka sasa Wilaya za Kigoma na Uvinza bado hazijaunganishwa. Je, ni lini Serikali itakamilisha kazi ya kuunganisha Wilaya hizi ili kukamilisha Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma umeunganishwa kwa Gridi ya Taifa kwa line ndogo inayotoka katika kituo chetu cha kupoza Umeme cha Nyakanazi na line hiyo ya msongo wa kilovolti 33 iliishia maeneo ya Kibondo, lakini tayari mradi mkubwa wa kilovolti 400 unaojengwa kutoka Nyakanazi kwenda Kidahwe Mjini Kigoma wa kilometa 280 unaendelea, kabla ya mwaka 2025 utakuwa umekamilika na hivyo Mkoa wote wa Kigoma utapata huduma ya umeme wa Gridi ya Taifa.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. nilitaka kuuliza swali la nyongeza kwamba barabara itokayo Malagarasi kwenda Uvinza, kipande cha kilometa 51 kimekuwa na muda mrefu sana na sasa kimeanza kutengenezwa lakini kinasuasua sana.

Nini mpango wa Serikali kuhakikisha wanamaliza maana barabara hiyo ni kipande hicho ndicho kilichobaki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kati ya maeneo ambayo barabara imechukua muda mrefu ni pamoja na kipande hiki
cha Malagarasi – Uvinza ili Mkoa wa Kigoma uweze kuunganishwa na mikoa jirani ikiwemo Tabora.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wote wa Kigoma. Mtakumbuka ziara aliyoifanya Mheshimiwa Rais, alipokuwa Kigoma ni miongoni mwa barabara hizi ambazo alizotoa maelekezo kwamba ni lazima ikamilike. Sisi Wizara ya Ujenzi katika bajeti hii inayoendelea na inayokuja tumetenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilika, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nilitaka ifahamike kwamba meli ya MT Sangara ambayo imefikia asilimia 90.7 ni meli ya mafuta siyo ya abiria wala mizigo, inabeba mafuta tu na kwa maana hiyo haina msaada mkubwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa imekuwa kawaida kwa Serikali kila mwaka kutenga bajeti na kuleta hapa kwenye Bunge lakini hakuna utekelezaji, na kwa kuwa, katika Ziwa Tanganyika kwa sasa hakuna meli hata moja ya Serikali inayofanya kazi. Nataka commitment ya Serikali kwamba bajeti itapungua kwenye eneo lingine lolote la Wizara na siyo kwenye meli hii, kwamba lazima meli hizi zitatengenezwa na kurudi majini, nataka commitment ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri wetu wa Ujenzi na Uchukuzi amesoma bajeti ya Wizara yetu na ameonesha commitment ya kiwango cha juu kabisa kuhusiana na namna ambavyo Ziwa Tanganyika tunakwenda kujenga meli mbili mpya pamoja na chelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi, commitment nyingine ya Serikali ni hizi meli ambazo hazifanyi kazi kwa sasa na tayari kwa mfano, hii MV Mwongozo ambayo tayari Mkandarasi ameshapatikana, ni Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) pamoja na hii meli ya MT Sangara ambayo amesema kweli ni ya mafuta lakini inafanya kazi katika Ziwa Tanganyika na iko asilimia 90. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Katavi, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa fedha ujao inakwenda kufanya haya ambayo imeahidi hapa. Ahsante. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba katika ziwa inaonekana ni njia moja nzuri ya kusaidia kupumzisha ziwa kwa wavuvi kuvua katika ziwa. Nini mkakati wa Serikali kusaidia wavuvi katika Ziwa Tanganyika kupata vizimba vya kutosha vya ufugaji wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bahati nzuri Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda anajua kabisa mkakati wa Serikali sasa hivi, baada ya kuwekeza sana katika Ziwa Victoria sasa tutafanya hivyo katika Ziwa Tanganyika pamoja na Ziwa Rukwa na Ziwa Nyasa. Ziwa Tanganyika tumeshakaa na Wabunge wa eneo hilo, na mwaka wa fedha unaokuja, mpango wetu kwa asilimia kubwa utakuwa katika ziwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kupata commitment ya Serikali kwamba wakati tukisuburi kukamilika kwa mchakato wa Itifaki ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kati ya nchi yetu na nchi ya DRC ambayo ni mdau mkubwa wa kibiashara wa nchi yetu; je, Wizara yako ipo tayari kukaa na wafanyabiashara wa Kigoma ili kuwapa elimu ya Itifaki hiyo kurahisisha shughuli za kibiashara baina yetu na DRC?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kutoa mafunzo na kwa ujumla tayari Serikali imeandaa programu maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo ya wafanyabiashara hao, lakini siyo tu waliopo Kigoma bali nchi nzima.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; barabara ya Bungu kuelekea Kibirizi ambayo inamilikiwa na TANROADS hali yake ni mbaya sana na haipitiki kwa sasa. Je, mna mpango gani wa kukarabati barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri barabara hiyo naifahamu sana, siyo barabara ndefu ni barabara ambayo ipo katikati ya Mji. Naomba nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS aipitie hiyo barabara na iweze kukarabatiwa kwa sababu imetengewa fedha kwenye matengenezo ya kawaida. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge barabara hiyo itakarabatiwa katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninataka kujua, je, ni lini mabehewa 37 yaliyokuwa kwenye karakana ya reli yakikarabatiwa kwa ajili ya safari za Kigoma – Dar es Salaam yataingia kwenye reli na kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mabehewa aliyoulizia Mheshimiwa Mbunge ni kweli tunakarabati mabehewa 37, na kila mwezi tunakarabati mabehewa 22, 20 za mizigo na mbili za abiria. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wasafiri wote kutoka Kigoma kwamba mwezi ujao mabehewa haya yataanza kufanya kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, andiko la TMA kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni latokea mwaka jana mwaka wa 2021; na sasa tunakwenda kukaribia mwaka wa 2022. Nilitaka commitment ya Serikali kujua kwamba hatua hii inaweza ikakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu, jambo hili litasaidia katika kuleta maendeleo ya wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mmejipangaje kuendelea na maboresho wakati mkisubiri maamuzi yale ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shabani Ng’enda, Mbunge Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee kufuatilia Chuo hiki cha Hali ya Hewa pale Kigoma jimboni kwake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anasema maandiko yalianza tangu mwaka 2021; kimsingi maandiko tumeandika mwaka huu na tumepeleka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tarehe 14 Aprili, 2022 lakini mwaka jana tulianza mazungumzo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hivi sasa tunavyosema tulitegemea Seneti itakapokaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndipo tupate mrejesho pengine ndani ya miezi miwili ijayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka afahamu tumejipangaje namna ya kuboresha chuo hiki. Ni kweli kwamba chuo hiki ni mkombozi mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa na chuo ni kimoja na Serikali kupitia bajeti zake mwaka wa fedha 2021/2022 tulitenga kiasi shilingi milioni 450 na tumejenga majengo pale kwa maana ya madarasa, maabara pamoja na computer room ama computer lab. Lakini hata hivyo, mwaka wa fedha na Waheshimiwa Wabunge mlitupitishia hapa tumetenga kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga jengo la utawala, na tunahakika mwakani chuo hiki kitaboresha zaidi.