Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kilumbe Shabani Ng'enda (17 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga na wenzangu wote….

SPIKA: Kwa wale wengine wasiomfahamu huyu ndio Mbunge wa Kigoma Mjini eeeh! Si mnaelewa.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naungana na wenzangu waliotangulia kuutambua utukufu wa Mungu katika kutuweka hapa, naungana pia na wenzangu kukishukuru Chama cha Mapinduzi na wapiga kura wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mjadala unaohusu hotuba ya Rais wetu ni mjadala wenye kusudio kubwa moja la kutafsiri dira hii aliyoitoa Rais wetu katika utekelezaji wa kazi za Serikali na Taifa kwa ujumla. Kama ulivyosikia wazungumzaji waliotangulia na wengine hakuna anayekosoa wala kupinga, maana yake wote tunaikubali kwamba hii ni dira ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepata bahati kuanza kazi za uongozi wa siasa toka kipindi cha mwisho cha Mwalimu alipokuwa anamalizia nafasi yake ya uongozi.

Kwa hiyo, nimepata nafasi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu, kwa Mzee Mwinyi, Hayati Mzee Mkapa na Mzee wetu Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hiyo, wazee wote hawa kwa kweli walikuwa na vipawa mbalimbali ambavyo vimelifikisha Taifa letu mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme juu ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, huyu mtu amepewa uthubutu wa aina yake haogopi, hakuna mtu alifikiri kwamba unaweza ukawa Rais usiende nje kupiga magoti kwa wakubwa hawa halafu ukaongoza nchi vizuri, lakini ametufikisha hapo na sasa tunaamini unaweza ukaongoza Taifa la Tanzania bila kwenda kupiga magoti huko nje na shughuli zikaenda. Ni Rais ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kutafsiri nadharia katika vitendo katika muda mfupi, anaamua jambo hili lifanyike na muda mfupi wananchi wanaona jambo limefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuna jambo kubwa katika haya tunayozungumza zaidi ya kuonesha kwamba hotuba yake ni dira kwa Taifa letu. Katika kipindi cha miaka ya 1990, Chama chetu cha Mapinduzi kilijikita katika sera ya kutaka kulitoa Taifa letu kuwa Taifa lenye uchumi tegemezi na kulileta kwenye uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Tumekwenda hivyo katika kipindi chote, lakini sasa tunauona mwanga, mwanga huu tunauona hapa tulipofikia kwenye hatua ya kuwa kwenye uchumi wa kati kwenye kipindi kifupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachokusudia kusema hapa ni kwamba sekta ya viwanda ambayo sasa imetupiga tafu (imesaidia) kubwa ni lazima tuiongezee kasi na katika kuiongezea kasi ni kuiongezea kasi katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji, wenzangu wengi wameshalieleza. Lakini niseme kwa upande wa Mkoa wetu wa Kigoma, sisi tunaweza tukasaidia sana Taifa letu kuondokana na fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje na Serikali imeanza na Waziri Mkuu huyu Mheshimiwa Kassim Majaliwa amekuwa ndio askari wa mstari wa mbele wa kuhakikisha zao la michikichi linalimwa, linakuzwa na ikiwezekana linavunwa na kusaidia kuondokana na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto tuliyonayo, kulima ni mchakato mrefu, na mabenki yetu mengi si rafiki kwa mkulima, miaka mitatu ya kutunza mchikichi mpaka uanze kuzaa ni changamoto kwa wakulima wetu. Kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano wa kutumia fedha, mfuko sijui wa kilimo kwanza kuwapa kama ruzuku wale wakulima ili waweze kusaidia kulima na tuweze kuondokana na tatizo la kuagiza mafuta kutoka nje. Mafuta ambayo siyo tu ni gharama, lakini ni hatari kwa maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka niliseme ni lile ambalo Mheshimiwa Rais amelisema katika ukurasa wa 27 wa hotuba yake nalo linahusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nimesikia kengele naunga mkono hoja mengine tutachangia katika mpango ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini niseme kidogo sisi Wabunge ambao tumeingia kwa mara ya kwanza tunatumia njia mbili hapa kujifunza namna shughuli za Bunge zinavyoendeshwa. Ya kwanza ni hii ya kusoma kwenye Kanuni na nini na nyingine ni kuwaangalia wale wazoefu waliokuja hapa siku nyingi namna wanavyoendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme kwamba ninayo masikitiko. Wapo baadhi ya wazoefu wanachangia Mpango hapa wanasimama tangu ameanza mpaka anamaliza anakosoa tu halafu hasemi tufanyeje. Nilitaka kusema hilo kwa kweli sioni kama ni jambo jema ambalo sisi tunajifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa maono yangu mimi Serikali ya CCM na inawezekana Serikali ya nchi nyingine yoyote duniani ingependa kuwafanyia wananchi wake kila jambo wanalotaka, kinachozuia kufanya hivyo ni uwezo. Ndiyo maana tuko hapa leo kupitia mipango kuona kupanga ni kuchagua, lipi litangulie lipi lisubiri kutokana na uwezo wetu. Kama tunataka tuongeze zaidi lazima tuseme tunapataje uwezo wa kufanya zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nishauri kidogo kwenye eneo la ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP). Nimeangalia katika Mpango huu, ni miradi nane tu ambayo imewekwa katika Mpango wa PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa kwanza ni Kiwanda cha Dawa; mwingine ni Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi; Hoteli ya Nyota Nne; Uwanja wa Mwalimu Nyerere; usambazaji wa gesi asili; Reli ya Standard Gauge Tanga – Arusha – Musoma na Mtwara – Mbambabay; Mwingine ni hosteli ya Chuo cha Biashara Kampasi za Dar es Salaam na Dodoma; na Chuo cha Uhasibu Kampasi ya Dar es Salaam na Mbeya; na wa mwisho ni mradi wa Kiwanda cha Kutengeneza Simu. Hii ndiyo miradi katika mpango mzima wa mwaka ambayo imeingia kwenye PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na PPP ndilo eneo ambalo lingeweza kutusaidia kushirikisha sekta binafsi katika kutekeleza mambo mengi ya Serikali. Kwa mfano leo hii usafiri wa Reli ya Kati kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam, wasafiri wanaotakiwa kusafiri kila siku ya treni wanaoondoka ni asilimia 25 tu, asilimia 75 ya wasafiri wote wanabaki kwa ajili ya kukosa mabehewa. Kwa nini katika mpango huu tusingeingiza mabehewa kwenye PPP, wapo Watanzania wafanyabiashara ambao wangeweza kununua mabehewa ya treni yakafungwa. Sasa hivi injini hizi zinakokota mabehewa chini ya uwezo wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda pale Stesheni ya Kigoma zaidi ya mara nne, mara tano. Injini inaondoka imefunga mabehewa nane yenye capacity ya kubeba mabehewa 30, mabehewa hakuna na mabehewa ya mizigo vilevile tatizo. Wakati mwingine yanakosekama mabehewa mpaka yanasababisha mfumuko wa bei ya saruji na bidhaa nyingine za viwandani zinazotoka Dar es Salaam kuja maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango atakapokuja hapa atueleze namna anavyoweza kuongeza wigo kwenye PPP. Naamini kabisa wapo Watanzania kama watu wanaweza wakanunua mabasi 115 wanashindwaje kununua behewa mbili, tatu au nne za treni akaingia katika utaratibu huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya afya vilevile bado tunaweza tukaingia kwenye utaratibu wa PPP. Nimeangalia sasa hivi kwenye hospitali zetu, tuna wodi za kawaida zile za msongamano na kuna wodi ambazo zimepewa grades; grade one na grade two. Wodi zile kukaa wodini siku moja acha huduma nyingine, unachajiwa kati ya shilingi 25,000 mpaka shilingi 40,000. Hiki ni kiwango cha lodge za kawaida za mjini ambazo mtu anaweza akakaa. Ukiwaambia wafanyabiashara wakujengee majengo hayo kwenye hospitali, watajenga tutaigia kwenye utaratibu wa PPP…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe, naona hii kengele bwana sijui ina matatizo gani. (Kicheko)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ina hiyana, lakini hakuna shida. Ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nataka niseme kwamba sina kawaida sana ya kuzungumzia mambo hasa ninayoona yananitia uchungu kwa watu ninaowafahamu vizuri na hasa Wabunge wenzangu, lakini mnapofika mahala mnataka kutengeneza chombo ni lazima mkubali kwamba, kama yuko mtu anapasua mtumbwi ili mzame, basi bora azame yeye lakini chombo kiendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tuliomo humu tumeletwa na vyama vyetu kupitia kura za wananchi, vyama vyetu vina katiba na miongozo, chama kikongwe kama CCM kina mpaka Kanuni za Maadili na Uongozi, zinazoonyesha miiko, zinazoweka makatazo na utaratibu. Kwa bahati mbaya, niseme kwa mfano Shahidi Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Gwajima, labda muda wake wa kuwepo kwenye CCM umekuwa ni mfupi sana, labda mambo haya hajapata nafasi nzuri ya kuyasoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hilo tu, tukishachaguliwa tukifika hapa, hatuanzi kazi mpaka tubebe Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tuape kuitii, kuitetea kwa mujibu wa sheria. Katiba hiyo inayo mambo ambayo yanatutaka lazima tuyafanye kwa sababu tumeapa, unashangaa na unajiuliza na unapata shaka, hivi hawa wenzangu wanapata nafasi ya kupita hii miongozo. Kama wangefahamu vizuri nadhani tusingefika huku tulipofika. Alipoanza Mbunge mwenzetu Mheshimiwa Gwajima, alianza kama anatoa ushauri hivi, akaeleza kuhusu hizo chanjo na nini, halikuwa jambo baya na wakati huo Rais wetu mpendwa alikuwa ameunda Kamati ya Wataalam kumshauri kuona namna ya kuliendea jambo la kupambana na COVID. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kama unaamua kumshauri Rais, Katiba ulioapa nayo Ibara ya 37 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoeleza majukumu ya Rais, inaonyesha kwamba Rais yuko huru katika kazi yake, halazimiki kufuata ushauri, ukimpa anaweza akauchukua au asiuchukue na atatimiza wajibu wake. Kama Rais alikua ameshaunda Kamati ya Wataalam hana lazima ya kusikiliza ushauri wa Askofu, maana jambo lenyewe la ugonjwa ni la kitaalam.

Mheshimiwa Spika, tuache Katiba na miongozo ya chama, ndugu yetu huyu ni mtumishi wa Mungu, Askofu, imeshafika mahali jambo liko kwenye mamlaka ya Rais analishughulikia, unawezaje kufika mahali ukaanza tena kuhoji, kwenda mbele kuchochea watu, hasomi hata Biblia yenyewe inasemaje? Kwamba mtii mamlaka maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya ya Kanuni, ya Katiba yamempita na ya Biblia yamempita? Si hilo tu hata sisi tunaoamini katika Uislamu imeandikwa atwiu-Allah, waatwiu rasuli wauli-l-amri minkum, kwamba tumtii Mwenyezi Mungu, tumtii Mtume na tuwatii wenye mamlaka miongoni mwetu. Huu aliouonesha mwenzetu siyo utii kwa mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya, tunapokuwa hapa ni vizuri tujue viwango vyetu, umeingia siasa jana, Ubunge una miezi sijui sita au tisa, lakini hata huko kwenye Biblia, si tuyaishi maneno ya Bwana Yesu. Ukialikwa kwenye harusi usikae viti vya mbele, maana mwenye harusi anaweza akaja na watu muhimu akakupeleka nyuma, kaa viti vya nyuma ili kama yeye atakuona wa muhimu akulete mbele maana ajikwezae hushushwa na ajishushae hupandishwa na haya maneno hayajui? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa amekuja hapa Mheshimiwa Gwajima amekaa viti vya mbele, hata sisi tuliokaa siku nyingi humu kwenye chama hiki tunamwangalia, lakini basi umefika mahali umekaa viti vya mbele, unaanza tena kupiga mawe kiti cha bwana harusi na sisi tukuangalie tu haiwezekani. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge karibu wengi ambao tumekutana huko nje tunazungumza juu la tukio hili la mwenzetu, kila mmoja anasema kwa kweli huyu bwana kafanya vibaya. Sasa ukiwauliza mbona hamkemei, wanasema hapana tunaogopa, atapanda madhabahuni kwenda kutuchapa pale kutukashfu. Mheshimiwa Gwajima, Mbunge mwenzangu, mimi nimejitoa kama dhabihu, nipeleke kwenye madhabahu siku ya jumapili, nichape ujuavyo, lakini mwachie Mama Samia na Serikali yake wafanye kazi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, narudia tena nimejitoa, nikwambie kwa nia ya kukurekebisha kama Mbunge mwenzetu, twende pamoja, ukiamua kwenda kutumia jukwaa la Mungu badala ya kuongoza kondoo kuanza kuwasema watu, endelea hivyo ila ujuwe Mungu anakupa muda. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja.

SPIKA: Haya malizia.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, mimi nimechukulia wito wa mama yetu na juhudi alizozifanya Mheshimiwa Rais wetu, tena nimenukuu maisha ya Nabii Nuhu, alipoona watu wake wanatenda makosa mengi kwa Mungu na Mungu akamletea ufunuo kwamba, mimi nataka kugharikisha, alikwenda akawasihi watu wote, jamani tutengeneze safina tupande, Mungu analeta gharika kutokana na makosa tuliyofanya, sasa tujisalimishe tukae kwenye safina. Wako baadhi ya watu mpaka ya wa familia yake walimpinga. Kilichotokea gharika ilikuja na wote waliompinga waliangamia. Mama ametutaka tuchanje na akatuomba kwa hiari anayetaka achanje, asiyetaka aache, sisi tulioamua kuchanja tunasubiri safina iwe tayari, wale ambao wamekataa litakapotokea gharika ya Mungu shauri yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kweli angekuwa Mheshimiwa hayati Magufuli ndiyo Rais leo, Mheshimiwa Gwajima angeweza kusema hayo aliyoyasema? Wakati wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka wa 1979, alikuwepo Mjumbe mmoja wa Halmashauri tena Mjumbe wa Kamati Kuu na alikuwa Mkuu wa Idara ya Organization, namkumbuka alikuwa mtu wa kwetu, mzee wetu, ameshatangulia mbele ya haki, Mungu amuweke mahali pema, alikua anaitwa Tuwakali Karangwe. Iliwekwa karantini ya kipindupindu alipokwenda kule Kigoma akakuta ma- barrier watu wanazuiwa wasiende huku kwa imani tu ya kutaka watu wala sio kwa kiburi, akawaambia fungueni watu waende wakapate huduma, kipindupindu kikaathiri watu wakafa, alilazimika kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu anachochea watu wasichanjwe na kushambulia wale wanaohamasisha na wanaoleta chanjo, katika CCM hii ninayoijua adhabu bado.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, nakitaka chama kiangalie vizuri adhabu hii. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naungana na waliotangulia kukushukuru sio tu kwa kunipa nafasi lakini kwa kuendesha Bunge lako vizuri kama walivyopongeza wengine katika siku hizi za karibuni tunajifunza kitu kipya kutoka kwa Ndugai tuliyemzoea, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na wananchi wangu wa Kigoma Mjini unapozungumza habari ya uvuvi, unazungumza kiwanda kinachoajiri watu wengi na ambacho ni tegemezi kubwa la wananchi wa Kigoma Mjini. Hii inatokana na kwamba tunazo malighafi nyingi ambazo tungeweza tukaweka viwanda lakini kwa sababu hatujapata umeme wa grid ya Taifa bado malighafi hizo zinachukuliwa kwenda sehemu nyingine na nyingine hazijatumika kabisa na kwa maana hiyo uvuvi ndiyo eneo pekee ambalo tunalitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitamshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya uvuvi na Wizara yake kwa ujumla. Hivi karibuni mimi na yeye tulifanya ziara Kigoma, ilikuwa mwezi jana Aprili na tukaongea na wavuvi. Napenda kutumia nafasi ya Bunge hili kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi, kwa namna ambavyo ametatua matatizo ya wavuvi baada ya kupata ukweli na hali halisi ya manyanyaso wanayoyapata ambayo yana maeneo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ni eneo la Kanuni zilizotungwa zinazoongoza shughuli za uvuvi. Pili, ni utendaji wa ofisi yake kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa hawana huruma kwa wavuvi. Siwezi kurudia mambo ambayo naona Mheshimiwa mwenzangu Aida ameyasema na wengine, lakini niseme, uzalishaji wa uvuvi uko chini karibu maeneo yote ya nchi yetu. Ukitafuta sababu kubwa ni mbili, sababu ya kwanza ni zana duni, lakini sababu ya pili, ni kanuni ambazo si rafiki kwa wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hili la Kanuni Waziri ametusaidia na namuomba aendelee kutusaidia. Kaja Kigoma pale katoa tamko la Serikali la kutaka wavuvi wa samaki wa migebuka watumie wavu wa inchi mbili, ply mbili badala ya maelekezo yaliyokuwa kwenye Kanuni ya wavu wa inchi tatu ply nne mpaka sita, ambao kwa kweli muda mrefu umewasumbua wavuvi kutokuvua. Kwa hiyo, nashukuru sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri asiishie hapo, kuna jambo pale tulisahau kuliweka sawa la tundu au macho ya wavu. Kanuni ya zamani ilikuwa inasema macho 144 kwa sababu wavu ulikuwa wa inchi tatu ulikuwa upana wa wavu sasa unakuwa mita 12.5. Sasa ukishapunguza upana wa macho yale kuwa ni ya inchi mbili ukiacha macho 144 ina maana kwamba wavu ule unakuwa sasa kina chake kwenda chini ni mita saba tu hauwezi kuvua. Kwa hiyo, wavuvi wanasema wanataka waende kwenye ile ile mita 12 kwa hiyo, lazima uongeze macho kwa sababu umepunguza ukubwa. Hili tulikwishalizungumza na Waziri akalielewa vizuri kwa hiyo, wameomba macho angalau
yafike 300 yawawezeshe kuvua vizuri na hasa katika ziwa hili lenye kina kirefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la zana duni za uvuvi, mimi nashangaa sana kwenye nchi yetu, tunapiga kelele ya mambo mengi lakini tunajizuia sisi wenyewe, tunasukuma gari halafu tunaweka gingi sasa itakwendaje? Ipo kampuni ya uvuvi ya wazawa wa Kigoma tangu mwaka 2015 maombi yao yako Wizarani, wametimiza vigezo vyote hamuwaruhusu kuingiza boti za kisasa za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, baba yangu alikuwa mvuvi, kulikuwa na vyombo pale vya Wagiriki vinaitwa Angella wengine Yorobwe na kulikuwa hata na chombo cha Kibwedeko. Tulikuwa tunavua samaki mmoja wa nonzi na sangara anabebwa na watu nane leo hii hatuvui kwa sababu ya zana duni za uvuvi. Hata hivyo, urasimu uliopo wa kupata vibali vya zana za uvuvi, bora uombe kibali cha kwenda peponi utaingia haraka kuliko kupata zana za uvuvi. Haiwezekani lazima tubadilike Mheshimiwa Waziri tutoe hapo, hatuwezi kupata tija kwa zile zana zilizopo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni ushuru katika mazao ya uvuvi. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri umelizungumza kidogo. Ushuru huu umekuwa tofauti sana katika mazao ya uvuvi ya Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Kwa mfano, kilo moja ya dagaa inayotaka kusafirishwa kwenda nje inadaiwa Dola 0.5 ambapo ikifika mahali unasafirisha kilo 100 ni zaidi ya Dola
50. Sasa hii kwa kweli unafika mahali unawakatisha tamaa hao wanaotaka kufanya biashara hii. Lazima tuangalie, ushuru uwe kidogo unaovutia biashara kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muda mfupi hapa ulipokuwa unatambulisha wageni, umetambulisha wageni wangu na wako mpaka sasa kwenye gallery pale. Hawa walikuwa wananisubiri, tunakwenda nao Kigoma, wamewekeza kwenye kuchakata samaki Mwanza na tunataka kwenda nao Kigoma. Ila katika mazingira haya ya urasimu wa miaka mitano watu hawajapata vibali, haitawezekana.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kitu kimoja, uwekezaji huu lazima tuujue uko wa aina mbili. Wapo wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza katika nchi yetu, lakini soko lao wanategemea ndani ya nchi yetu. Wapo wawekezaji wanakuja kuwekeza katika nchi yetu, soko lao wanategemea nje. Hawa ndiyo wawekezaji bora zaidi. Kwa mfano, hawa nilionao mimi, Wachina wamefika mahali wamewekeza kule Mwanza. Wenyewe wanachukua yale matumbo ya samaki ambayo zamani yalikuwa yanatupwa. Wanachukua minofu, mapanki wanachukua Waswahili wenzetu wanakula, matumbo yalikuwa yanatupwa. Wenyewe wamechukua yale matumbo (fishmonger), wanafika mahali wanasafirisha huko nje na tunapata pesa nyingi. Huu ndiyo uwekezaji mzuri zaidi maana wanatoa hela nje kuingiza ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikoni mtu ambaye ameleta material zake hapa anafika mahali anawekeza marumaru ambazo zinanunuliwa na Watanzania wenyewe humu humu wanachukua hela zetu. Kwa hiyo, nataka nisisitize lazima tutengeneze mazingira mazuri. Leo hao wawekezaji wa Mwanza…

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe, kumbe matumbo ya samaki nayo ni chakula!

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ohooo! Tena kina soko kubwa kuliko hata minofu ya samaki. Wapo hapa (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza hao hao wawekezaji ambao wapo hapa, wameomba vibali vya wafanyakazi wao wawili, leo miezi sita hawajapata na wameshalipa. Kila mmoja wamemlipia kama Dola 1,000 na risiti wamenipa wanazo hapa, lakini mpaka leo vibali vya wafanyakazi hao ambao wanakuja kuwekeza kwa ajili ya kuchukua matumbo ya samaki ambayo sisi hatuyatumii, wanayapeleka nje, sisi tunapata fedha. Mambo ya ajabu kabisa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niseme kwenye Sekta hii ya Uvuvi sisi tunategemea Mheshimiwa Waziri na ndugu yetu Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri, mlete mapinduzi makubwa yaongeze pato la Taifa. Katika mapinduzi haya makubwa tunayotaka myatazame, kwanza ni hizi kanuni ambazo namshukuru Mheshimiwa Waziri ameanza kushughulika nazo. Pili, ni kuruhusu uwekezaji mkubwa kwa sababu mnaona leo tunalaumu hapa NARCO.

Mheshimiwa Spika, nami naungana nawe, jamani mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 1990 ni kutuondoa katika Sekta ya Umma kutupeleka kwenye Sekta Binafsi. Sekta Binafsi iweze kuchangia pato la Taifa kwa kiasi kikubwa. Sijui kwa nini hatuelewi hili? Kwa hiyo, leo Sekta Binafsi, tuisukume, tuitengenezee mazingira, sisi tukusanye kodi ili kodi zile zisaidie wananchi wetu. Mnakazana na Sekta ya Umma ambayo inafika mahali kila wakati inawekewa ruzuku na ruzuku zile zinayeyuka, kinachoendelea hakuna, mapori yamekaa. Hatuwezi kuendelea hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka kwenye uvuvi Sekta Binafsi imeonesha, hivyo viwanda vyote unasikia viko Mwanza, ingawa Mwanza kuna viwanda leo vya minofu mpaka hivi vya matumbo ya samaki, viko kama vinane tu, lakini nenda Uganda, viko 30 kwa sababu, Uganda wametengeneza mazuri ya uwekezaji.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe, subiri. Mheshimiwa Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa mchangiaji. Siyo matumbo ya samaki. Yanaitwa mabondo kwa lugha nzuri.

SPIKA: Mheshimiwa Ng’enda unapokea Kiswahili hicho?

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, yaani hiyo taarifa ni sahihi na kama unavyojua Kiswahili kimepanuka sana katika hivi vitu vya kisasa, maana hicho nilichotumia mimi ni cha Kigoma zaidi. Lugha sahihi ni mabondo na kwa kizungu wanaita fish maws. Kwa hiyo, nakubali taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala zima la ushuru, kutazama ushuru. Nimeshalizungumza na ushuru usiwe na tofauti kubwa. Leo Ziwa Victoria, dagaa wa kilo
100 ushuru wake ni shilingi 38,000/=, lakini Ziwa Tanganyika 116,000/= kwa kilo 100. Tusiweke hii tofauti kubwa kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo limelalamikiwa na wavuvi na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi, Mheshimiwa Waziri tukiwa pale Kigoma unakumbuka, dagaa zina grade kama ilivyo tumbaku. Sasa sijui hakuna classifiers wa ku-classify hii ni class gani na hii ni class gani? Haiwezekani classes zote ziwe bei moja tu ya ushuru. Kuna dagaa wanaitwa nyamnunga, walipigwa na mvua, hao ni kwa ajili ya chakula cha kuku…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutupa afya ili tuendelee kulitumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukuwe nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, Naibu wake, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutafuta uwezo na kuuweka katika utaratibu wa kuwezesha miradi ya Serikali ambayo inategemewa na Umma wa Watanzania kutelekelezwa kutokana na makusanyo ya kodi. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa nikiwa na nia ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Fedha kwenye suala zima la riba za mabenki. Mwelekeo wa sasa wa uchumi wa Taifa letu unategemea sana mchango wa sekta binafsi. Sekta binafsi inatutegemea sana kufanya mambo mawili makubwa; la kwanza ni kutengeneza sera ambazo zinaitambua sekta binafsi na kuiwezesha kufanya kazi zake. Sera bahati nzuri tunazo nzuri, sheria tunazo nzuri na taratibu tunazo nzuri na tunaendelea kuzirekebisha kila inapoonekana inastahili kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa katika hii sekta binafsi ni uwezeshaji; kuiwezesha kuchangia pato la Taifa. Katika uwezeshaji huu, chombo kikubwa cha kuwezesha sekta binafsi ni mabenki yetu. Nasikitika kusema kwamba mabenki yetu hayajawa katika mwelekeo mzuri wa kusaidia sekta binafsi na hasa kwa riba kubwa zilizopo kwenye mabenki ambazo zimekuwa mzigo mkubwa kwa sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, benki zetu kwa sasa zinatoza riba kati ya asilimia 13 mpaka 21. Kiwango hiki cha riba ni kikubwa sana, lakini ukiacha riba unakwenda kuomba mkopo kwenye benki, unaambiwa kuna kitu kinaitwa processing fee. Hiyo processing fee, wanakwenda kwenye computer wanabadili majina kutoka kwenye mkataba wa mtu mmoja kwenda mtu mwingine wanabadili figure, maandishi ni yale yale halafu wanakutolea hiyo copy ya mkataba wa wewe na benki, unaweza ukafika mahali ukailipia mpaka shilingi milioni tatu au milioni nne. Huo ni mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara wetu, na hatuwezi kusaidia sekta binafsi kwa stahili hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa insurance. Sasa unashangaa, insurance hii wakati mwingine anatozwa anayekwenda kuomba mkopo wakati risk za mkopo ziko sehemu mbili; risk ya kwanza ni ya benki inayotoa fedha kumpa huyo mkopaji na risk ya pili ni ya mkopaji ambaye ameweka kitu chake collateral ili apate mkopo, lakini wanakwambia wewe nenda kalipe insurance. Hata ukimaliza hiyo mikataba wanakwambia peleka kwa mwanasheria. Ukipeleka kwa mwanasheria, gharama za mwanasheria unalipa wewe, lakini unakuta kuna processing fee, unalipa hapo.

Mheshimiwa Spika, kubwa ninalotaka kulieleza ni kwamba benki zetu bado riba zake ziko juu, haziwezi kusaidia sekta binafsi kukua. Hili nalisema kwa sababu nafahamu kwamba Wizara ya Fedha kupitia BoT ndiyo wanaopitisha hizi riba za mabenki. Maana siku moja nilikuwa na kiongozi mmoja wa Serikali, kasimama kwenye function moja analaumu mabenki kwa riba, mimi nikamwandika kameseji, lakini zimepitishwa na BoT.

Mheshimiwa Spika, hakuna benki hata moja inayojipitishia riba yenyewe, lakini BoT wanatufanyia kama hadithi ya kilio cha mti. Mti uliona mashoka yanapita yametoka dukani, wakawa wanasema yanakuja kutumaliza. Mti ukamwambia hapana, hayawezi kutumaliza hayo mashoka mpaka ifike mahli yawekwe mpini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi chombo chetu cha Serikali ndiyo kinachoshirikiana na mabenki kuwakandamiza hawa watu wa sekta binafsi. Kitu hiki hakiwezekani. Nataka Waziri atakapokuja hapa atueleze kwa kweli vizuri na kwa kutulia, ni namna gani watasaidia sekta binafsi kukua kwa kupunguza riba za mabenki?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, hili lina mifano mingi tu…

SPIKA: Ndiyo Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuzungumza kwamba kitendo cha Serikali kupitia Benki Kuu yetu, kukopa kupitia bond kwa asilimia 15.95, hiyo inayahamasisha mabenki kuikopesha Serikali badala ya kukopesha wananchi. Ahsante sana.

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea?

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naipokea vizuri sana kwa mikono miwili. Naomba niendelee na mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, ninayo mifano midogo ninayoweza nikaitoa hapa, maana hata sisi wengine tumeamua kuingia kwenye mikopo. Unaweza ukafika mahali ukajiuliza katika hali ya kawaida, mikopo kama ya asilimia 20, 18; mikopo yenye asilimia ndogo kama ya kwetu yenye government quarentee asilimia 13; unaweza ukajiuliza, hivi mtu unaweza ukampa shilingi milioni 200 au 300 halafu akafanya biashara, akakulipa wewe shilingi milioni 69 naye akapata faida? Kwa biashara gani kubwa ya namna hiyo? Hilo ndilo jambo kubwa la kujiuliza. Unafika mahali unamkopesha mtu, halafu ujiulize, huyu akitoa hii riba yangu, halafu naye atajilipa mshahara, halafu atatengeneza faida awe ameendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii nimesikia kwenye vyombo hapo kwamba Benki ya NMB inakwenda kugawana faida ya shilingi bilioni 60. Ni jambo la kushukuru na kufurahi benki kwamba yetu imetengeneza faida, lakini jambo la kujiuliza Serikali ni kwamba hao waliotengeneza hiyo faida wamebakije? Hao ambao hiyo Benki ya NMB inawakopesha ambao ni wateja wake wamebakije? Au inafurahia kusikia benki imetengeza faida bila kujali kwamba wale wateja wa benki hiyo nao wamebaki katika hali ambayo imewaendeleza au imewadidimiza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnaweza mkawa mmeitengeneza faida ya benki lakini mmewauzia watu majumba, mmefika mahali mmewaacha wananchi wenu taabani. Halafu kubwa zaidi tunalokuja kuambulia ni kugawa neti kwenye hospitali wodi mbili, mnagawiwa neti. Wanasema benki imerudisha faida kwa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, katika kipindi hiki ambacho tunataka kuinua sekta binafsi, isaidie kukuza uchumi wa Taifa, ni namna gani mabenki yameandaliwa kushusha riba ili kuwezesha sekta binafsi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka kulizungumza ni hizi microfinance institution. Kuna vikampuni vimetengenezwa vya kukopesha wananchi, sijui hata nani anaye-control? Sijui ni BoT, sijui vimeachwa huru? Unaweza ukakopa shilingi milioni tano, unakalipa shilingi milioni 12.

MBUNGE FULANI: Kweli!

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Wana kitu kinaitwa compound interest. Kadri unavyochelewa, inaenda inazaa na hii deni na hii inazaa, yaani ni matatizo makubwa, watu wamenyang’anywa vitanda. Ukienda kwenye ofisi za hizo microfinance, utakuta vitanda, mafriji, magodoro, sijui nini? Wizara ya Fedha iko kimya, watu wake wananyonyolewa.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: …BoT iko kimya.

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe, upokee taarifa. Ndiyo.

T A A R I F A

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninampa taarifa mzungumzaji kuwa siyo tu kwamba wanachukua vitanda na magodoro, wanachukua ATM cards za hao watu wanaowakopesha na walioathirika zaidi ni walimu. Kwa hiyo, ATM cards zinakaa kwenye hizo ofisi, mishahara ikiingia wao wanatumia kuchukua pesa. Kwa hiyo, ni hali mbaya sana.

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe, pokea hiyo taarifa, na ninakuongezea dakika moja ufafanue hili jambo vizuri kwa sababu ni tatizo kubwa. Hata kule Kongwa walimu wangu wana hali ngumu kwa sababu ya hawa watu. (Makofi)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza naipokea taarifa hii, ni taarifa nzuri na inaendana na mchango wangu. Lakini vilevile nakushukuru kwa kuniongeza dakika hiyo, na nilitaka kuzungumza kidogo jambo la mfano kwa ajili ya Timu ya Wananchi, sitazungumza tena. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli jambo hili lazima niseme wote sisi tunalifahamu maana sisi ni wawakilishi wa wananchi, lazima Waziri atakaposimama hapa atueleze hizi microfinance institutions zinazozaliwa kama uyoga. Umefanya vizuri kwenye mabenki, mabenki mengine mitaji ilikuwa inadondoka na nini, mabenki mengine umeyafungisha ndoa yamekuwa pamoja; sasa tuambie kwenye hizi microfinance institutions unafanyaje. Kwa kweli ni msalaba mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ninataka niseme baadhi ya wazabuni kama alivyokuwa anasema dada yangu, Mheshimiwa Halima hapa, baadhi ya wazabuni wa Serikali wamekopa kutoka kwenye mabenki. Mikataba yao na mabenki iko palepale, Serikali haijawalipa, huku riba zinaendelea. Wengine wamefika mahali wamekuwa taabani.

Mheshimiwa Spika, sitaki kusema kama dada yangu, Mheshimiwa Halima, maana yeye ana lugha zake; anauliza, hii ni akili? Kwa sababu sisi tuliolelewa vizuri ukisema siyo akili maana yake unasema yule anayefanya hivyo hayuko sawasawa, na naamini wote hao wanaofanya hivi wana akili nzuri sana. Isipokuwa nauliza; ni busara? (Makofi/Kicheko/ Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, narudia kuuliza; hivi ni busara kweli kufika mahali mtu kawapa huduma, amekopa benki anakuja na karatasi yake, jamani naendelea kudaiwa, na ninyi ama hamuhakiki deni lake au hata mkihakiki hamumlipi, anaendelea kudaiwa, riba inaendelea kuchajiwa. Hata mkija mkimlipa hana tena cha kurudisha mfukoni mwake. Kwa hiyo, ninataka niseme…

SPIKA: Wizara ya Fedha, Mbunge anauliza tu, ni busara kweli hii? (Makofi)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, la mwisho nataka nimalizie hapa ni utaratibu wa kutoa fedha za miradi kwenda mikoani na katika wilaya. Atanisaidia Waziri wa Fedha; kulikuwa na utaratibu kwamba tukishapitisha bajeti hapa kwamba tumetenga kifungu hiki cha fedha kwa ajili ya mradi fulani, pesa hizo zinapelekwa mkoani. Sasa hivi mpaka mchakato uanze kule, kazi itangazwe, BOQ zitengenezwe, huko wakati mwingine wataalam wenyewe hatuna, BOQ zinachelewa kutengenezwa, pesa zinachelewa kuombwa.

Mheshimiwa Spika, ninauliza; kwani kuna tatizo gani la kufika mahali tukazingatia kasma iliyokwisha pitishwa na Bunge tukapeleka fedha hizo huko?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu Waziri amemteua dada yangu pale kuwa balozi wa… mimi sitaki aniteue, najiteua mwenyewe kuwa balozi wa kutetea kupunguza riba kwa wananchi. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia, na zaidi namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuendelea kuwa na afya ya kutumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema yale ninayokusudia kuwa ni mchango wangu katika eneo hili, napenda nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ziara nzuri yenye matumaini na iliyotutia nguvu sisi wawakilishi wa wananchi pamoja na Watumishi wa Serikali katika Mkoa wa Kigoma. Ametufungua katika mambo mengi, ameelekeza mambo mengi ambayo kwa kweli yanakwenda kuipa Kigoma sura mpya ya maendeleo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunamwombea afya njema yeye pamoja na wanaomsaidia ili waweze kutimiza matarajio ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizishukuru sana Kamati zote tatu zilizowasilisha hoja zake hapa Bungeni. Katika kuzishukuru, nipeleke shukurani vilevile kwa CAG kwa ofisi yake ya kufanya kazi nzuri ya kutupa miwani ya kutazama mambo mengine ambayo yanafanyika kwenye utendaji na sisi huwa hatuyaoni mpaka tuletewe na yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujielekeza katika kuzungumzia hasa mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya LAAC na PAC. Nianze na LAAC. Ushauri na mapendekezo haya yametolewa katika ukurasa wa 19 hadi 24 wa taarifa yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia uwekezaji wenye tija. Uwekezaji wenye tija maana yake Halmashauri zetu zinapowekeza, ziwekeze katika maeneo ambayo zinakwenda kupata tija, zinaongezea mapato na mapato yale yanasaidia hata halmashauri zenyewe kuweza kufanya miradi ya maendeleo kutokana na fedha wanazokusanya kwa makusanyo ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana hapa kuna miradi mingine watu wanafuata mkumbo tu, kwamba madhali halmashauri fulani wana stendi na sisi stendi; madhali wana soko, na sisi soko; basi ni miradi kama hiyo. Kwa ujumla niseme, kwenye eneo hili napenda kuishauri Serikali kwamba zipo halmashauri ambazo zinakuwa na matatizo ya kubuni miradi na kuisimamia kutokana tatizo la wataalamu.

Mheshmiwa Mwenyekiti, nichukue Manispaa yangu ya Kigoma Ujiji. Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa Manispaa ambazo zina makusanyo madogo, kiasi kama cha Shilingi bilioni tatu kwa mwaka, kiasi ambacho unaweza ukasema ni kidogo sana. Halmashauri hii ina tatizo kubwa la wataalamu. Ukienda kwenye wahasibu ni tatizo, ukienda kwenye wakaguzi; Manispaa nzima ina mkaguzi mmoja, yaani afanye kazi zote za ukaguzi zinazotakiwa kufanywa, wahandisi ni tatizo, valuer ni tatizo. Kwa hiyo, tuiombe Serikali iwezeshe halmashauri zetu kupata wataalamu ili waweze kubuni miradi na kuisimamia vizuri, hapo tutaweza kusaidia kuongezeka kwa mapato ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine, wamesema hasara zitokanazo na taasisi za Serikali. Zipo hasara ambazo Halmashauri zinapata kutokana na taasisi za Serikali. Moja ya taasisi iliyotajwa ni MSD. MSD inatajwa kwa sababu inalipwa fedha kwa ajili ya kuleta vifaa vya hospitali; vitanda vya hospitali na madawa, baada ya kulipwa fedha wanachukua miezi mitatu, minne, mitano, sita hawajaleta vifaa hivyo. Kwa hiyo, wanaitia hasara halmashauri.

Mheshiniwa Mwenyekiti, kuna taasisi kama TEMESA, hawa yaani sijui niseme, ingekuwa ni mamlaka yangu, ningeweza kuangalia: Je, inastahili kuendelea kuwepo au isiwepo? Yaani hawa ukienda, unataka kukagua magari, unataka kutengeneza gari, hawana wataalamu, hawana vipuri, waende tena kwenye maduka ya watu binafsi wakatafute vipuri hivi, gharama ya TEMESA inakuwa gharama kubwa kuliko gereji za watu binafsi. Kwa hiyo, lazima serikali iangalie eneo hili. Tumeweka kwa nia njema, lakini tusipoangalia litakuwa mzigo kwa Serikali na mpaka sasa TEMESA ni mzigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, GPSA; yapo malalamiko ya Idara za Serikali chungu mzima, zimeingiza pesa GPSA, kwa ajili ya kulipia magari, mwaka mzima mpaka leo hawajapata magari. Mwezi Novemba kuna taasisi zimeingiza pesa, mwezi Novemba huu hawajapata magari. Magari hayo yalitakiwa kuja kufanya kazi kwa ajili ya kuongeza tija kwenye Serikali, lakini GPSA wamepewa, hivi Serikali wanakwama wapi Ukienda gereji TOYOTA ukiwapa oda miezi mitatu wamekuletea gari, mwaka mzima GPSA hawajaleta gari.?

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi nyingine iliyoyatajwa ni NHIF. NHIF imetajwa kwa maana ya kwamba uko mfumo ambao nataka niishauri Serikali waone jinsi ya kuubadilisha. NHIF inaingia mkataba na hospitali za Serikali na binafsi kwa ajili ya kuhudumia wateja wao ili wao waweze kuwalipa. Wanapokwenda kuhakiki malipo, NHIF wanaamua haya tutalipa haya hatulipi labda kuna kasoro fulani fulani na wakishaamua wao ndiyo wa mwisho. Haiwezekani, tukawa na mamlaka ambayo yenyewe inaingia mkataba na watu na wakitofautiana yenyewe ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuamua, nikulipe au nisikulipe. Hata mikataba mbalimbali, hata ya Serikali, mnaambiwa kwamba tukitofautiana, tutatafuta arbitration kabla ya kwenda Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa arbitration ya hawa NHIF na zahanati zetu za Serikali na zahanati za watu binafsi, ni nani? Kwa hiyo lazima kitafutwe chombo hapa ambacho kitakuwa kati, iwapo NHIF watasema mimi siwezi kulipa, basi huyu aliyetoa huduma akimbie kwenye chombo hicho aseme NHIF wananionea, nimetoa huduma hawataki kunilipa. Hilo ndilo wazo langu ambalo ningependa kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Kamati ya PAC ukurasa wa 28, kuna suala la Polisi, kutoandaliwa kwa hesabu na kufanyika kwa ukaguzi wa hesabu za Mfuko wa Tuzo na Tozo wa Polisi. Kamati imelieleza vizuri, huu Mfuko upo kwa mujibu wa sheria ‘The Police Force and Auxiliary Service Act, Cap No. 322’, lakini CAG amebaini kwamba, kwenye Mfuko huu kuna pesa zimewekwa kwenye Benki Kuu, bilioni 35.3, lakini pesa hizi hazikaguliwi wala haziletwi taarifa yake katika ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo hivi sisi tunaviheshimu sana, vyombo vyetu hivi vya ulinzi. Tungependa viwe clean, wanafanya kazi nzuri, wasichafuliwe na mambo haya madogo madogo. Mimi niombe sana kwamba utaratibu usimamiwe chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kuhakikisha mifuko kama hii ambayo nia yake ni njema inakaguliwa na utaratibu unafanyika. Mzee wangu, mzee Yusuph Makamba aliwahi kusema, ukiumwa na nyoka utatibiwa na mzizi, sasa ukiumwa na mzizi unatibiwa na nini? Maana hawa polisi ndio kazi yao kukamata wezi na wahalifu, sasa kama wao ikitokea uhalifu tunafanyaje, kwa hiyo hivi ni vyombo vya kuviangalia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna Idara ya Uhamiaji, kwenye idara hii ukaguzi maalum ulifanywa kwa mujibu wa kifungu cha 93, Idara ya Uhamiaji imekuwa ikitoa stika bandia za visa. Hizi DCI alibaini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Vitendo hivi na stika hizi zimekuwa zikiingia kupitia KIA. Sasa CAG baada ya kufanya ukaguzi kwa kipindi cha miezi sita tu, CAG amebaini kwamba kuna upotevu wa kiasi cha Shilingi bilioni 2.4 na kuna Maafisa 32 wa Idara ya Uhamiaji ambao wanahusika na wamefika mahali wakacheza na kanzidata na kufuta kwenye kanzidata watu ambao walilipa visa, ambao ni wa nje watu 21,208.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni mapato makubwa sana ya Serikali na vitendo hivi vimekuwa vikifanyika huko zamani. Hata huko Kigoma waliwahi kiwajibishwa Maafisa Uhamiaji kwa kugonga muhuri wa entry halafu ile nanii ya visa hawakukata au dola hamsini wanachukua dola 30 wanaacha dola 20, waliwajibishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nashukuru Mungu Kigoma mambo ni mazuri, tunaye Afisa Uhamiaji na Mkuu wa Mkoa ambaye wanasimamia mambo vizuri, yanakwenda vizuri. Uzoefu ule wa Kigoma ungeweza ukatumika kuangalia maeneo mengine yote na huu uliojitokeza KIA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutuwezesha kufanya kuendelea kufanya kazi ya Taifa letu ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningependa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote ambao wanamsaidia, Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao kazi hizi nzuri ambazo tunaziona zimefanywa kwa juhudi zao. Ukimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu bila kumshukuru Mheshimiwa hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli unakuwa hujakamilisha shukrani, maana huyo Waziri Mkuu ni matunda ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyezi Mungu amuweke mahali pema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata bahati sana ya kufanya kazi muda mrefu kwenye chama chetu. Nimeanza kazi ya uongozi mwaka 1988 na sasa nina miaka 33 nikiwa mjumbe wa NEC. NEC yenyewe nimekaa miaka 15 lakini nimeshika vyeo mbalimbali kwa muda wote wa miaka 33. Hata hawa baadhi ya makada na Wabunge wenzangu wanaosema hapa wengine walio wengi wamenikuta humo, wengi wote akina Kibajaji, akina Msukuma, akina January Makamba na wengine walio wengi. Niliowakuta ni akina Mheshimiwa Lukuvi hapa, kwa hiyo kwenye chama chetu nimekaa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niseme jambo moja. Nakijua sana chama chetu, naujua uwezo wa chama chetu katika kusimamia mambo yote ya msingi ya uongozi wa Taifa na hata ndani ya chama chenyewe. Kunapofika kuna jambo lolote ambalo wewe ni kama Mbunge, au ni mwana CCM au ni mwananchi una mashaka lipeleke kwa CCM litapata majibu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipopata msiba wa kiongozi wetu, wengi tulihuzunika sana, kwa sababu kwanza hatukuamini na pili, tulihuzunika kwa sababu bado tulikuwa tunamhitaji, lakini la tatu, tulihuzunika kwa sababu tulijiuliza nini hatima ya Taifa letu baada ya kuondoka kwake. Sisi makada tuliobobea vinenoneno vingine tunavyoviona vinapita tulivitarajia. Ninachokiomba, sisi wenye mapenzi mema wenye kujua kazi ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tutumie busara sana katika kusema jambo lolote tunaloliona linatokea. Inawezekana akatukana mtu halafu wewe ukasimama kusema, ukawa wewe unatangaza tusi badala ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama naeleweka vizuri? Umesikia neno huko, ulipime, hili ni la kwenda kusema au ni la kuliacha, maana chama chetu kinao uongozi imara kinaweza kupata majibu ya matatizo yote tuliyonayo. Naomba niseme kama mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini nimo ndani ya Bunge; tabia ya mtu kujipa ukaka wa Taifa, kujipa udada wa Taifa, kujipa ushangazi wa Taifa, unakemea, unaweza ukakosea unaweza uka-overdo, tuache. Kama unaona jambo fulani lina shida, lipeleke kwenye chama chetu, litapata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge ningependa sana tuishi kwa kuheshimiana, kustahiana, hiki ni chombo kikubwa Watanzania wanatuangalia, wanarushiana vineno visivyokuwa na maana na wakati mwingine kama mwenzako hujaelewa vizuri alichokisema, pata muda wa kujifunza, hakuna kitu kibaya kama kumtafsiri vibaya mtu aliyesema vizuri, halafu umeshamchafua unajiuliza utarudije kumsafisha. Kwa hiyo nimesimama hapa kwa kweli kusema jambo hilo, chama chetu kina majibu yote ya nchi yetu juu ya matatizo ya wananchi na chama. Mtu asijipe jukumu lolote kubwa, ajue chama kipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ningependa niseme hivi, nimepongeza kazi nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na nimesikiliza hapa mchango wa ndugu yangu Mheshimiwa Shabiby juu ya TARURA, niseme nami nataka kuongezea jambo moja kwenye TARURA. TARURA haina tatizo tu kwenye bajeti au kwenye mahusiano na Councils bali ina tatizo hata la kimuundo ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye TARURA kuna mtu anaitwa regional coordinator yupo mkoani, huyo ndie anayetangaza tenda, ndiye anayetoa kazi, ndiye anayelipa, ndiye anayeweza kuvunja mkataba, hawa District Manager wa TARURA wamekaa kama sijui nitasemaje, yaani nitafute neno gani, lakini wanafanya supervision ambayo hawana nguvu nayo. Kwa hiyo, tunapokwenda kuipa nguvu TARURA kwa kuiongezea fedha, lazima tuangalie muundo wake, tugatue madaraka kutoka juu tuyarudishe chini, kwa Mameneja wa Wilaya wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa nilizungumze, sisi wa Kigoma tulivyosikia Standard Gauge inaanza Mwanza, tukanung’unika nung’unika, unajua sisi hapa ndio ingekuwa na impact ya kiuchumi na nini, lakini kupanga ni kuchagua, tulikwisha chagua Mwanza, hakuna tena kurudi kuangalia huku na kule. Hata hivyo, inakuwaje huku mnapelekea standard gauge, halafu hii narrow gauge ambayo ilikuwepo huku ya mkoloni inaachwa hivyo. Hali ya reli yetu ni mbovu sana hasa kutoka Dodoma kwenda Kigoma. Maeneo mengi ni mabovu. Nimemwona Waziri Mkuu amekuja na mpango wa kununua mabehewa na vichwa vya treni, tunashukuru sana hilo ni moja ya tatizo, lakini na ile reli ikarabatiwe katika kiwango cha kufanya wanaosafiri wawe na uhakika na maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali si nzuri na niwaambie katika hali ya kawaida, unajua watu wakiwa wanalalamika mbona standard gauge imeanza huku, basi hii ya kwao mbovumbovu mnawatengenezea na wenyewe ili kuwafuta machozi kulikoni waendelee kubaki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeisha! Naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nami naungana na Wabunge wenzangu waliotangulia kuonesha imani yetu kubwa sana kwa viongozi wa Wizara hii ya TAMISEMI, Waziri, Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu na wasaidizi wote. Tuna matumaini makubwa sana katika utendaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijazungumza mambo ya kijimbo, nilitaka nizungumze haya ya kisera kidogo na hasa ni utaratibu wa kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri zetu. Tulipokuwa kwenye vikao vya RCC tumekutana na tatizo kubwa sana na tatizo lenyewe ni utaratibu mpya nafikiri uliotolewa na Hazina wa kutaka fedha za maendeleo zitolewe baada ya kuwa kandarasi za kazi zinazotaka kufanyika katika mpango kazi zimetangazwa na wataalamu wameandikia na kwenda Hazina. Sasa utaratibu huu umechelewesha sana miradi mingi ya maendeleo kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha wa 2019/2020 katika Mkoa wa Kigoma ni asilimia 78 tu ya fedha za maendeleo ndiyo zilizopelekwa lakini mwaka huu ndiyo hatari zaidi maana mpaka tunakwenda kumaliza robo ya tatu ya mwaka ni asilimia 23.3 ya fedha zote za maendeleo ndiyo zimeletwa. Tatizo kubwa limetokea wapi? Ni uhaba wa wataalamu hasa wahandisi ambao wanashughulika na kuchakata miradi hii ili ipelekwe Hazina kwa ajili ya kuombewa fedha.

Kwa hiyo, labda kama tunaona kuna ugumu wa kuwapata hawa wataalamu kwa wakati kwenye halmashauri zetu na kwenye Sekretarieti ya Mkoa basi turudi kwenye utaratibu wa zamani ambapo pesa zilikuwa zinatolewa Hazina kupelekwa mikoani na kwenye halmashauri kwa kuzingatia mpango kazi. Kama mpango umeshatoka na kasma imeshapitishwa na Bunge, pesa zipelekwe mchakato wa miradi ufanyike huko kuliko huu utaratibu wa sasa unachelewesha sana fedha kufika kwenye maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda nilizungumze, mimi natoka Manispaa ya Kigoma Ujiji. Sisi ambao tunatoka katika miji tuna maeneo yetu ya mapato na wale wanaotoka katika vijiji wana masuala ya mazao, mifugo na kadhalika, wanakuwa na maeneo mapana ya mapato. Moja ya eneo kubwa tunalolitegemea katika mapato kwenye halmshauri zetu ni masoko. Nimeona Serikali imefanya kazi nzuri katika baadhi ya maeneo ya kujenga masoko ya kisasa lakini Manispaa ya Kigoma Ujiji bado eneo lake la kukusanya mapato hili la masoko halijaboreshwa.

Mheshimiwa Spika, tungeomba Wizara ya TAMISEMI waone uwezekano wa kusaidia ili tuweze kupata masoko yaliyopangiliwa na yaliyokaa kisasa na ambayo ni rahisi kudhibiti mapato yake. Nasema hili hasa ukizingatia kwamba Manispaa ile iko mpakani, meli zinakuja pale za kutoka Kongo, Burundi, waone hata nchi yetu unajua wengine hawajui Dar- Es-Salaam hawajui Dodoma, akifika pale akiona soko la hovyo anasema hivi Tanzania tunavyowaona walivyo soko lao ndiyo hili? Wenyewe wanasema ndiyo soko la Tanzania. Sasa mnatupa kazi ya kuanza kujieleza aah, kuna Kariakoo, kuna wapi, wenyewe hawajui. Kwa hiyo, tunaomba mtusaidie sana katika suala la kupata soko la kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Kigoma Ujiji ni miongoni mwa Halmshauri ambazo hazina hospitali ya wilaya na mpaka sasa tunatumia hospitali ya Shirika la Dini la Babtist. Kwa sababu Serikali ni moja nilitaka niseme hili kwamba tumekwishakubaliana kule na sasa hivi tumepata eneo la kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa, najua hii iko Wizara ya Afya, lakini ni kwamba hospitali hii ikipatikana hospitali ambayo inatumika sasa kama hospitali ya rufaa ya mkoa inaweza ikawa hospitali ya wilaya ikasimamiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji. Kwa hiyo, niombe tu Wizara hizi zinaweza zikafika mahali zikafanya mashauriano ya kusaidia kuharakisha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa ili hospitali iliyokuwa inatumika kama hospitali ya rufaa ya mkoa ya Maweni iweze sasa kubaki kama Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu kwa kuzungumzia suala la upandishaji wa vyeo watumishi. Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji lipo tatizo kubwa sana, Watendaji wa Kata na Mitaa walioajiriwa Julai 2005 sasa wana takribani miaka 16 hawajapandishwa vyeo. Naomba mlitazame suala hili.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza, naomba radhi kidogo, uliniita hapo mapema, nilikuwa na mataizo kidogo ya kifamilia, nikatoka nje kuyashughulikia mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla naungana na wote waliotoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Elimu. Ni ukweli usiopingika kwamba unapotafuta wanawake wa mfano wanaofanya kazi nzuri ya Taifa letu, huwezi kuacha kumtaja Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako. Niseme kwa kweli anatujengea heshima hata nasi tunaotoka katika Mkoa wa Kigoma kwa kazi nzuri anayoifanya kwa Taifa letu na sisi wengine tunajitahidi kuiga mfano wake ili tukipewa kazi kama hizi tuzifanye kwa uhaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia mapitio ya utekelezaji wa bajeti wa 2020/2021, nimeona yapo maeneo ambayo Wizara imeonyesha kabisa kwamba yanahitaji msukumo, maana huko nyuma katika mapitio yalikuwa hayafanyi vizuri sana. Moja ya eneo ambalo nataka nilizungumze tena kwa mfano mzuri hata katika jimbo langu, ni hivi vituo vya Teachers Resources Centre (TRC). Hivi vituo kwa ujumla vimekuwa kama havipo. Kwa mfano, mimi katika Jimbo langu la Kigoma Mjini, kulikuwa na vituo hivi katika Shule ya msingi Bungu, eneo la Mnarani, Shule ya Msingi Muungano na eneo la Rusimbi, Shule ya Msingi Rusimbi; lakini vituo vyote hivi vimefungwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, alitokea Afisa Elimu mmoja tu akaamua akasema ninyi walimu mliopo hapa nendeni mkafundishe, ondokeni nendeni madarasani, basi vile vituo vimekuwa kama vimefungwa. Hata hivyo, ukipitia mapitio ya Wizara na Taarifa yake ya 2020/2021 inaonyesha kwamba asilimia kama 54 wamevitembela, vinafanya kazi kwa takribani kipindi cha miaka mitatu sasa, lakini moja ya tatizo kubwa ambalo linakutana na vituo hivi ni kukosa mfumo wa TEHAMA. Unapozungumza katika dunia ya sasa ya Sayansi na Teknolojia, unakuwa na vituo vya maarifa ya walimu ambavyo havina mfumo wa TEHAMA, maana yake unaendelea kuwarudisha nyuma hawa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme katika utekelezaji wa bajeti ya 2021/2022 Waziri ajaribu kuangalia uwezekano, kwanza kuwepo na hao walimu, lakini zaidi ya yote kuwepo na vifaa hivi vya TEHAMA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri, atakapokuwa anatazama bajeti yake hii angalie VETA. Tumetoa msukumo mkubwa sana wa kuanzishwa VETA kule ambako hakuna, lakini pale kwangu ipo VETA, lakini inakabiliwa na changamoto nyingi. Moja, ni tatizo kubwa la bweni. Mabweni yaliyoko hayatoshi na kwa maana hiyo wanachukua wanafunzi wachache kutokana na kukosa mabweni na vijana wengi wanaomba nafasi. Kwa hiyo, hili ulitazame.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba, sasa hivi eneo moja kubwa linalofundisha vijana taaluma ya udereva ni VETA, lakini ukienda VETA ya Kigoma hiyo gari wanayofundishiwa wanafunzi ni kama wanafundishwa matatizo badala ya kufundishwa udereva. Maana mara isimame njiani, mara imekwama na iko gari moja. Sasa madhali eneo hili limetoa ajira ya kutosha; kuna boda boda, madereva wa magari na kadhalika, lazima VETA viwepo vifaa vya kutosha vya kufundishia ikiwa ni pamoja na pikipiki na magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nataka niliseme katika mchango wangu wa leo ni huu uhusiano wa Wizara moja na nyingine katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Hili nalisema kwa maana Wizara ya Elimu bado yapo mahitaji makubwa ya vijana wa Kitanzania ya kupata Elimu za Taaluma na Elimu za Juu. Vipo vyuo vya kitaaluma ambavyo, kwa mfano, pale Kigoma kipo Chuo cha Hali ya Hewa. Chuo hiki kina eneo kubwa, kina miundombinu mingi, lakini kinatoa taaluma moja tu ya hali ya hewa. Taaluma ambayo hata ajira yake ni ndogo sana katika nchi, muone uwezekano wa kuchukua kile chuo mwongeze taaluma nyingine ili kiwe hata Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vijana waweze kupata nafasi za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo hivi mbali na kusaidia elimu, vile vile vinasaidia eneo ambapo kunakuwa na vyuo vingi, kama vile mfano Mkoa wa Iringa, mzunguko wa fedha unakua mzuri. Mimi nimekaa Iringa pale nimeona, kuna vyuo vitatu pale; kuna Tumaini, kuna Mkwawa na Ruaha University. Hivi vyuo vina wanafunzi pale zaidi ya 3,000. Kwa hiyo, mzunguko wa fedha katika mji ule wa Iringa unaona hata unachangamka kutokana na vyuo vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika miji hii ya kwetu kama Kigoma ambayo kidogo mzunguko wa fedha ni mdogo, mnapoleta vyuo hivi, basi mnatusaidia na sisi mzunguko wa fedha unaongezeka. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kwa kuanza tu ninataka nikushukuru kwa kutukumbusha kuzingatia misimamo ya nchi yetu na sera za chama chetu ambazo zimeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nilipokuwa nimejipanga kuchangia nikaenda kuangalia sera zetu za mambo ya nje, nisije nikasema jambo ambalo liko kinyume na sera za chama kuhusu mambo ya nje, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa imani yangu mimi nchi yetu imepata hifadhi kubwa sana ambayo haitoki kwa mtu mwingine yeyote wala Taifa lingine lolote, inatoka kwa Mungu mwenyewe kutokana na namna ambavyo sisi kama Taifa tumeji-address siku zote kwamba ni Taifa linalosimamia haki na linaloheshimu utu na haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo ni toka Taifa letu lilipoasisiwa na Mzee wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume. Tumeji-address hivyo, duniani kote wanatufahamu kwamba Tanzania ni nchi ambayo inaheshimu haki za binadamu na inatetea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenzangu ametoka kusema muda mfupi uliopita juu ya msimamo wetu kama Taifa kuhusu hali inayoendelea Mashariki ya Kati, na ukisoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hakuligusia. Amegusia diplomasia ya uchumi, Mashariki ya Kati tunauza nyama Qatar, Oman, Kuwait; ni jambo jema, lakini ninachotaka kusema ni kwamba tusirudi nyuma, wala tusione woga, wala tusione aibu kusema sisi kama Taifa jambo hili hatulioni sawa, tunawaomba wakubwa kaeni muone jinsi ya kutatua matatizo haya. Si jambo baya wala si dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa ninakumbuka maneno ya Askofu Desmond Tutu wakati wa harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika; alisema hivi; If you are neutral in situations of injustice, you have chosen the side of the oppressor. Kama unakaa kimya katika jambo ambalo wengine wanakandamizwa, maana yake wewe umechagua upande wa wale wakandamizaji ndiyo upande wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi hatuwezi kuwa upande wa wakandamizaji, tunataka Mungu aendelee kutoa baraka kwenye Taifa hili. Msimamo wetu toka wakati wa Mwalimu na mpaka leo haujabadilika, ni kwamba Wapalestina wamefika mahali wamekaliwa katika ardhi yao na kwamba ni lazima waachiwe ardhi yao. Huo ni msimamo ambao tumekuwa nao na hatujawahi kurudi nyuma katika msimamo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba hao wakubwa huko watafute namna ya kufanya mambo huko Mashariki ya Kati yaende vizuri badala ya kushuhudia dunia watu wanakufa kwa maelfu halafu sisi tunasema tunakaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, tulikuwa na msimamo mkali hata juu ya Morocco ambayo ilikuwa inaikalia Sahara ya Magharibi, na huo msimamo wetu hatujawahi mahali popote kuuondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba katika jambo hili lazima tupaze sauti na tusione vibaya kama Taifa kusema kwamba hili hatuoni vizuri. Hatumshutumu yeyote, hatukai upande wowote, lakini hatuoni vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze sasa kuzungumzia hasa masuala yanayohusu diplomasia ya uchumi. Katika ukurasa wa 23 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia ushirikiano wa Tanzania na nchi za Afrika, na akaeleza kwa mtiririko; Kenya, Burundi, Msumbiji na nchi nyingine amezitaja nyingi. Lakini kwa bahati mbaya sikuona DRC Kongo ikiwa imetajwa, inawezekana zipo sababu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilichotaka kusema mimi natoka Kigoma Mjini, sisi jirani zetu pale ni watu wa DRC na hawa watu wa DRC wamechangia sana mzunguko wa fedha katika Mkoa wa Kigomana hii inatokana na nanii, inatokana na ukweli kwamba watu wa DRC hasa Mkoa wa Kivu ambao tunapakana nao, huduma nyingi wanazipata kutoka nchini kwetu. Na hili ni eneo na fursa kubwa sana kwa sababu Mkoa wa Kivu una population ya watu karibu milioni sita, lakini umbali kutoka Mkoa wa Kivu kwenda Kinshasa ni zaidi ya kilometa 1,900 maana yake unatokana Kigoma, unapita Mtwara unaingia mpaka Msumbiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya nchi ile bado haijawa mizuri sana, kwa hiyo huduma nyingi bado wanazitegemea katika nchi yetu, fursa hii tumeipoteza kwa sababu ya kutokutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara ya sisi na DRC. Na hapa ningependa Mheshimiwa Waziri unisikilize vizuri, moja ya jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa ni pamoja na visa kubwa kwa wafanyabiashara wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna visa ya dola 50 ambazo ni hela nyingi kwa mfanyabiashara mdogo anayetoka DRC Kongo kuja kufuata bidhaa ambazo anajua atazipata kutoka Kigoma, lakini sasa hivi kimeongezeka tena kitu kingine mbali na hiyo visa kila Mkongo anayeingia anatakiwa apimwe covid na kupimwa covid dola 25 sisi ndiyo tuna kiwango kikubwa cha kupima covid kuliko Kenya, kuliko Uganda, kuliko DRC yenyewe. Wenzetu wengine ni dola tano sisi dola 25 halafu tunasema tunataka tuvutie uhusiano wa kibiashara, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka Mheshimiwa Waziri utakapofika mahala unafanya majumuisho unisaidie, nini mkakati wenu katika soko kubwa hili la watu karibu milioni sita ambalo tunalitegemea, nini, mkakati wenu wa kupunguza gharama ya visa ili tuweze kufanya nao biashara vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hilo nilitaka kuzungumzia tumekuwa sisi ni mafundi wa kuanzisha uhusiano, nilitaka kuuliza hivi uhusiano wa sisi na Msumbiji tukaanzisha mpaka ile TAMOFA imekwenda wapi? imekufa au ipo na hawa Msumbiji ni ndugu zetu naweza nikasema ni ndugu zetu wa damu, tukishirikiana nao tunakuwa tuna uhakika tupo katika mikono salama, uhusiano huu umekwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kuzungumzia diaspora na uraia pacha; ibara ya 132 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imezungumza namna ambavyo tutawashirikisha diaspora katika kusaidia suala la diplomasia ya uchumi na kusaidia uwekezaji katika nchi yetu, tumeeleza, siwezi kunukuu hapa nitachukua muda mrefu, lakini ipo kwenye ibara ya 132.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tunazungumza kuwashirikisha sijui tunapata kigugumizi wapi cha uraia pacha na katika hili nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya majumuisho unisaidie nini kigugumizi cha uraia pacha? Tuna ndugu zetu, tena hawa mbali na kuwa na wana mitaji kama alivyosema dada yangu hapa Mheshimiwa Ng’wasi muda mfupi, wengine wana-technology, wana maarifa, wakiyaleta hapa nchini tutanufaika, kigugumizi kinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba sana, sana wakati tunazungumza diplomasia ya uchumi tuone jinsi ya kuwatumia diaspora kutusaidia katika suala la uwekezaji na maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, narudia kukushukuru, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kunikumbuka na kuniona na hasa baada ya kuzungumza ndugu yangu Mheshimiwa Kavejuru.

Mheshimiwa Spika, suala la umeme wa Gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kigoma ni ajenda ya mkoa, ni ajenda ya Wabunge wote hata wengine ambao ni Mawaziri hawawezi kusema lakini ni ajenda yetu. Hii ni kwa sababu kama mnavyojua Kigoma ni miongoni mwa mikoa ya pembezoni na ambayo imechelewa sana katika maendeleo na moja ya jambo lilituchelewa ni kukosa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunapozungumzia changamoto za umeme tunazungumzia mafanikio makubwa yaliyofanyika kutokana na kazi iliyofanywa na Wizara hii. Kwa hiyo, nimpongeze sana Waziri, Naibu Waziri pamoja na watumishi wote wa Wizara hii na mashirika kama TANESCO na watu wa REA, kwa kweli tunazungumza changamoto zinatokana na mafanikio. Sisi zamani huko Kigoma ilikuwa umeme ukiwaka maana unaweza ukawaka hata mara moja kwa wiki ukiwaka unasikia watu wote eee, utafikiri labda Timu ya Wananchi imeingiza goli kwenye nyavu za Simba. Yaani wala hili sikudanganyi... (Makofi/Kicheko)

MBUGE FULANI: Rudia.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, yaani ukisikia kelele wakati ule ilikuwa sababu ni mbili; ni Yanga kafunga goli kwenye lango la Simba au umeme umewashwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kumshauri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwamba pale Kigoma mmeingia mkataba na wale wawekezaji wa solar ili wazalishe umeme wa megawatt 4.8 mpaka sasa wanazalisha megawatt 2. Tatizo la wale wawekezaji ni kwamba ule mradi wao ulichelewa kuanza ukakumbana na misukosuko mingi hata mlipokuja kukubaliana na kuingia mkataba baadhi ya vifaa vilikuwa vimeibiwa. Kubwa kuliko yote hizo megawatt 2 zinapatikana mchana tu ikishaingia saa moja jioni ni zero, umeme haupatikani kabisa kutoka kwa watu wale wa solar. Kwa maana hiyo wanachosaidia pekee ni kupumzisha mashine za TANESCO mchana ili ziweze kuwaka usiku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo la pale inaonekana vifaa vyote; panel, inventor, step-up transformer vipo sawasawa lakini hawana zile betri kubwa za ku-store energy, kwa hiyo, inapofika usiku hawezi kuzalisha chochote. Kwa sababu mmeingia mkataba na mnawalipa naomba wapeni hata government guarantee wakope benki waweze kuweka mradi wa vizuri. Sisi tukipata ile megawatt 4.8 tatizo letu sisi Wilaya ya Buhigwe na maeneo mengine linakwisha kabisa kabisa. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri muone jinsi ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hebu chukueni utaratibu kama wanaouchukuwa TAMISEMI au Wizara ya Afya, wanapofika mahali wakaamua kuna hospitali ya shirika la dini wanaitumia kama Hospitali ya Wilaya basi hupeleka madaktari wa Serikali kusaidia supervision na kutoa huduma. Hebu kwenye kituo hiki kwa vile mmeingia mkataba na wale watu peleka mainjinia wako wa TANESCO wasaidiane na wale watu pale kuhakikisha kwamba kazi inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kwenye nishati ya mafuta, tofauti ya bei kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Leo hii asubuhi nimefuatilia Dar es Salaam lita moja ya petrol shilingi 2,249, lita ya diesel ni shilingi 2,073 lakini Kigoma leo hii lita ya diesel ni shilingi 2,481 tofauti ya shilingi 232 na Dar es Salaam sasa hapa ukinunua lita 1,000 tu kuna tofauti ya shilingi 232,000, gharama za uzalishaji lazima zitakuwa kubwa kwa Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mtu ambaye namuamini sana Mheshimiwa Waziri, hebu ajaribu kuangalia hivi hatuwezi kuwa na bei moja ya petrol na diesel kwa nchi nzima. Ni jambo ambalo linawezekana, mkaona wapi pakufidia tukawa na bei moja, ukienda Kigoma, Mbeya au sehemu nyingine kila sehemu iwe moja.

Mheshimiwa Spika, la mwisho limezungumzwa suala la vinasaba hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Bahati mbaya muda hauko upande wako.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana lakini kwenye vinasaba nilitaka tu kumsaidia ndugu yangu pale aliyekuwa anaomba ulinzi kwamba mimi nimeshamuandalia ulinzi kule Kigoma asiwe na wasiwasi. (Kicheko/Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchukua nafasi hii kwanza, kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi. Pili, kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuamka salama na kuanza kufanya kazi za kutumikia tena Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote nitoe pongezi maalum za sura ya bajeti. Nasema za sura ya bajeti kwa sababu, kwa hakika bajeti hii imetudhihirishia mambo mawili makubwa. Kwanza, imetudhihirishia kwamba, Serikali hii ya CCM ni Serikali sikivu. Pili, imetudhihirishia kwamba, Serikali inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wetu ni Serikali ambayo imekusudia kabisa kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa hizi hazipatikani kwa kusema tu, zinapatikana kwa mambo tunayoyaona kwa sababu, Serikali sikivu inazo sifa zifuatazo: Moja ni Serikali inayowasikiliza wananchi; Pili, Serikali inayowasikiliza Wabunge; Tatu, Serikali inayoshaurika; Nne, Serikali ambayo ipo tayari kujikosoa; na Tano, Serikali inayotekeleza mambo kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo yakiwepo ndio unasema hii Serikali sikivu na katika bajeti hii unaweza ukayaona haya mambo katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kitendo cha kupunguza faini za makosa ya barabarani kwa bajaji na bodaboda, kutoka Sh.30,000/= mpaka Sh.10,000/= ni kuwa Serikali hii ni sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kitendo cha kuhakikisha kwamba, katika bajeti hii posho za Waheshimiwa Madiwani, ambao ni wasaidizi wa karibu wa sisi Wabunge, zitakuwa zinalipwa sasa kutoka TAMISEMI badala ya Halmashauri zao. Hiki kitendo kinaonyesha Serikali hii ni sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kitendo cha kuweka posho maalum kwa Watendaji wa Kata na Makatibu Tarafa,


ili waweze kupata uwezo wa kuzifanya kazi zao vizuri, kinaonyesha Serikali hii ni sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, kitendo cha kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya barabara zetu zinazosimamiwa na TARURA, maji na kushughulika na maboma ya shule zetu, haya yote yanaonyesha Serikali hii ni sikivu na kwamba, lazima tutoe pongezi maalum kwa Rais wetu na Serikali kwa ujumla, kuonyesha kweli kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, ningependa kuwatoa wasiwasi Wabunge wenzangu, hasa ambao wamekuwa na wasiwasi au wakiwa na maoni tofauti kuhusu kodi ya majengo, kwamba, itozwe wapi na mahali gani? Nataka niipongeze kabisa Serikali wamelenga, wametafuta mahali pazuri ambapo kodi itapatikana na ambapo hapawezi kuwa na maumivu kwa mtu mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri katika hili tukafahamu kwamba, kodi zote na hasa zilizo nyingi, lazima mwisho wake zilipwe na mtumiaji, maana hata ukisikia kodi imewekwa kwenye mafuta, unaweza ukafikiri analipa mwenye gari, si kweli hiyo. Mwenye gari ataenda kununua mafuta tu, lakini baadaye abiria akipanda gari hilo atalipa hiyo kodi ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kodi zote hatimaye hulipwa na mtumiaji kwa hiyo, kama nyumba imejengwa na mwenye nyumba yupo, aidha, anakaa kwenye nyumba hiyo ina umeme au hakai kwenye nyumba hiyo kuna mtu mwingine anakaa na huyo ndiye anayelipa kodi hiyo ya majengo, iko sahihi, wala hakuna tatizo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni niliungana na Rais wetu, kushuhudia utiaji saini wa mikataba mitano kule Mwanza ya ujenzi wa meli ambazo zitatoa huduma na kuchochea uchumi katika Taifa letu. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi katika Ziwa Tanganyika ni wanufaika, maana kuna meli mbili; moja ya abiria ambayo itabeba abiria 600 na mizigo 400 ipo katika mkataba huu ambayo itaanza kujengwa; na nyingine ni ya mizigo. Hapa narudia kuipongeza Serikali, maana nimesema hapa Bungeni katika Mpango na hata katika Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, nilisema kuhusu suala la kuhakikisha tunachangamkia fursa ya soko kubwa la DRC Congo. Kwa hiyo, meli hizi zitakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi cha kufungua mlango na kuongeza wigo mkubwa wa biashara baina ya sisi na DRC Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mniruhusu vile vile baada ya kusema Serikali hii Sikivu, niwakumbushe mambo ambayo hamjayasikia vizuri. Maana ingekuwa ni binadamu ungeweza ukasema, kama mtu ana masikio mawili labda ungesemea sikio la kushoto, la kulia labda liliingia maji hakusikia vizuri. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia haya mambo, nimeshayasema na sasa nataka niyarudie. Uchumi wa nchi yetu unategemea sana uimara wa sekta binafsi. Sekta binafsi sasa hivi imebeba mizigo mikubwa miwili; tukiitua mizigo hii sekta binafsi itatusaidia sana katika kukuza uchumi. Mzigo wa kwanza ni riba za mabenki. Maana ilisababisha hapa mpaka nijiteue mwenyewe kuwa balozi wa kutetea riba za mabenki. Riba za mabenki endeleeni kulitazama jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzigo wa pili ni ulipaji wa madeni ya Serikali kwa wakandarasi wa ndani. Nataka nikwambie, hali ni mbaya. Kuna watu sasa hivi hapa wakipiga simu napata shida kupokea. Mmojawapo ni mpiga kura wangu mmoja anaitwa Raymond Dabiegese, yupo kule Kigoma, anaidai TBA (Tanzania Building Agency). Amewa- supply vifaa, duka lenye thamani ya mtaji kama wa shilingi milioni 100, unakwenda kuchukua vifaa vya shilingi milioni 40, halafu unafika mahali miaka miwili hujalipa. Unamuua huyu mtu. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa kupitia nafasi hii niseme, tumesaini mikataba na hawa wakandarasi kwa ajili kutengeneza meli hizi. Naiomba Serikali ichukue tahadari sana katika kuwasimamia hao wakandarasi kufanya kazi zetu. Najua Serikali kabla ya kutoa kazi, inafanya kitu kinaitwa due diligence, kuangalia uwezo wa kitaaluma na kifedha wa haya makampuni kufanya kazi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa tunalo tatizo, kampuni iliyopewa kandarasi ya reli yetu ya kisasa, inakabiliwa na madeni makubwa ya wazabuni wa ndani wadogo iliyowapa kazi. Sijui hili kama mnalijua! Serikali inawalipa wao kwa wakati, lakini wao wale watu waliowa- sub-contract kazi ndogo ndogo hawawalipi. Sasa hivi wanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 14. Baadhi ya wadeni walikuwa hapa niliwaunganisha na Naibu Waziri wa Ujenzi ili waone jinsi ya kuwasiaidia. Ndugu zangu imetokea baadhi ya makampuni haya yamefanya kazi kwenye nchi nyingine yakamaliza mikataba yake, yakamaliza miradi, yakawaacha watu wa nchi hizo, Wakandarasi wadogo wadogo wa nchi hiyo, wazabuni wadogo wadogo wanadai madeni; nchi mojawapo ni Ethiopia. Wametekeleza miradi lakini wameacha makovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali na hasa Hazina mnapotoa fedha, ikiwezekana hata katika mikataba yenu, hawa wakandarasi wa kutoka nje mnapowapa kazi, waoneshe wao wanaingia mikataba na wazabuni wadogo wadogo wa ndani ya nchi; mikataba ile mwenayo na mjue kama wale wazabuni wanaowapa, wanalipwa kwa wakati. Vinginevyo ninyi mnawalipa lakini wao hawawalipi. Hilo jambo litafika mahali litasaidia miradi kutekelezwa lakini litarudi tena kuwabebesha mizigo watu wa sekta binafsi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla nataka niseme kwamba sisi Wabunge naamini kama nilivyowasikia wenzangu wengi wanasema, tumeridhishwa sana na bajeti hii na kwa kweli napenda kutamka rasmi kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa nafasi ya kuendelea kufanya kazi ya kulitumikia Taifa letu kupitia Bunge lako hili na pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi, na zaidi ya yote, kuniteua na mimi kuwa miongoni mwa Wabunge wanaounda Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipata shida kidogo, mimi taaluma yangu ni mwandishi wa habari, nilipopelekwa kwenye sheria ndogo nikasema sasa inakuaje hii? Lakini kumbe ulikuwa unanipeleka shule nyingine ya kujifunza ili niweze kujua mambo mengi zaidi, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya Wanakamati wenzangu wametoa hoja nyingi za mambo ambayo tuliyapitia na kwa kweli niseme waraka huu ulioletwa na Kamati yetu mbele ya Bunge lako, tumefanya uchambuzi wa kutosha na kusaidiwa vya kutosha na wataalam tuliowashirikisha na wadau tuliowaita kwenye vikao vya Kamati na kwa maana hiyo nataka niseme tulijikita kwelikweli kuangalia na kufanya uchambuzi ili tuone namna nzuri ya kulishauri Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, nifanye mapitio madogo tu katika baadhi ya mambo ambayo wengine inawezekana wamekwishayataja; kwa mfano, tumejadili sana kuhusu sheria ndogo zinazoongoza masuala ya filamu. Na katika kujadili sana, kwa sababu yalikuwa ni mambo ambayo katika sura na tamaduni za kwetu bado ni mambo ambayo hayajazoeleka sana kwa Watanzania, hii tasnia ya filamu haijachukua kasi kubwa sana kama nchi za wenzetu. Kwa maana hiyo kuna mambo ambayo tuliyakuta yamewekwa kwenye mapendekezo ya sheria ndogo ambayo yalikuwa yananyima uhuru tasnia yenyewe kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ni kwamba kama mtu anataka kuonesha kitu juu ya tatizo la dawa za kulevya, lazima aoneshe, lazima awepo mtu anayeonesha hizo dawa za kulevya yanatumiwaje na yanaathiri vipi. Lakini mwisho lazima matokeo yake yaoneshe madhara.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, haiwezekani filamu ioneshwe mtu anaiba mali ya umma halafu baadaye inaonekana ametajirika, maisha yake yanamekuwa mazuri, anaendelea na maisha yake. Uta-entertain watu wengi kufikiria kuiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani filamu ioneshe mtu anatumia dawa za kulevya halafu ionekane huyu amekuwa mchezaji bora mpaka akapata tuzo kwa sababu alikuwa anatumia dawa za kulevya. Lakini tunategemea hiyo filamu itakapoonesha mtu iruhusiwe kuonesha mtu anatumia dawa za kulevya, lakini matokeo ya mwisho ya filamu hiyo yaoneshe jinsi alivyoathirika na ambavyo amekuwa siyo wa msaada kwa Taifa. Kwa hiyo, hayo ndiyo mambo ambayo tumeyaelekeza katika maoni yetu kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo vilevile tuliyaona ambayo umeyaeleza hapa kidogo, juu ya utungaji wa kanuni, sheria mama inatoa loophole kwamba Waziri mwenye dhamana atatunga kanuni zinazosimamia sheria hii. Sasa anapokwenda kutunga zile kanuni unakuta kwenye kanuni kule kuna sehemu inasema, katika jambo hili uamuzi wa Waziri utakuwa wa mwisho. Tukasema hapana, lazima useme kwamba asiyeridhika atakwenda mahakamani, Mahakama ndiyo kiwe chombo cha mwisho cha kuamua juu ya watu. Usiseme uamuzi wa Waziri katika jambo hili utakuwa wa mwisho. Mambo hayo nayo tuliangalia katika baadhi ya sheria ndogo na tukafika mahali tukayaweka katika mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mimi nirudie kusema kwamba nakushukuru sana kwa kunipanga kwenye Kamati hii. Bado ninaendelea kujifunza, lakini kwa ujumla ni kazi kubwa na muhimu, na niseme muda siku zote umekuwa hautoshi kwa sababu mpaka tunachambua sheria zote hizo unazosikia, bado kuna nyingi hazijafanyiwa uchambuzi, na bado kuna nyingi zinazolalamikiwa. (Makofi)

Kwa hiyo ni busara yako na Bunge lako kuona namna ya kuiongezea Kamati hii muda ili tusiendelee kuwa na sheria ndogo ambazo zinalalamikiwa huko mtaani. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania na kwenda maeneo mbalimbali duniani, kutafuta nusura ya Watanzania hasa katika mambo ya msingi yanayotukabili. Nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa tunaanza kupokea huu Mpango ulituongoza ukatueleza na kutusomea kanuni, nami nimezingatia sana. Ukasema Mpango huu ni mwongozo wa bajeti ijayo, lakini ukasema vile vile tushauri vyanzo vipya vya mapato; na la tatu, ukasema tushauri vipaumbele vya bajeti. Nami nitajielekeza huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kwenda huko, katika maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, ukurasa wa saba ameelezea utekelezaji wa baadhi ya miradi katika kipindi hiki, lakini nataka kuzungumza moja ya jambo kubwa ambalo nimekuwa nikilizungumza hapa Bungeni na ambalo nilijiteua kuwa balozi mimi mwenyewe, nalo linahusu suala la riba za mabenki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mzee Kimei, Mbunge mwenzangu ambaye ni mbobezi kwenye masuala ya mabenki alilizungumza vizuri sana kwa lugha ya kitaalam zaidi, mimi nitalishusha katika lugha ya kawaida ambayo kila mmoja anaweza akaielewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa 2019/2020 watu waliokopa katika mabenki walikuwa asilimia 8.1, lakini mwaka wa 2020/2021 waliokopa katika mabenki walikuwa asilimia 4.3 yaani wakopaji wameshuka. Riba za mabenki kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, zimeshuka kutoka asilimia 16.8 mpaka asilimia 16.6. Yaani kushuka kwenyewe ni kwa 0.2 percent. Napenda kuipongeza sana Kamati ya Bajeti, sana sana; Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya Bajeti, wamekokotoa jambo hili vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati riba za mabenki zimeshuka kwa 0.2%, riba za mikopo inayotolewa na Benki Kuu kwa mabenki ya biashara imeshuka kutoka 12% mpaka 7%. Maana yake imeshuka kwa 5%. Kilichotokea ni nini? Ni kwamba Benki Kuu imeshusha kwa 5%, mabenki ya biashara ambako ndiko yanakwenda sasa kwa watu wetu, hao ambao tunasema tunataka kuinua sekta binafsi, wameshusha kwa 0.2%. Hapa kushusha kwa Benki Kuu kumeenda kunufaisha mabenki badala ya kuwanufaisha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ukiliangalia kwa sura ya kawaida, unaweza ukaliona tu; lakini ukiingia ndani zaidi, unaweza ukasema hapa kuna ufisadi. Kwa nini nasema hivyo? Maana Serikali yenyewe, Benki Kuu yake inatoa kuyapa mabenki ya biashara kwa 7%, lakini Serikali yenyewe inakwenda kukopa kwenye mabenki ya biashara kwa 15% ya riba. Najua kwa mujibu wa sheria Serikali haiwezi kukopa Benki Kuu, lakini huu ni mzigo mkubwa sana kwa wananchi, asilimia 15 ya riba kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imeishauri Serikali na ninataka kuiomba Serikali yetu sikivu, izingatie ushauri huu. Isipozingatia ushauri huu, siku moja kwenye ukumbi huu tutaikataa bajeti. Imeishauri Serikali isikope kwenye mabenki ya biashara kwa zaidi ya asilimia 10. Msingi wake ni nini? Kuwapunguzia mzigo walipa kodi Watanzania wa kulipa asilimia kubwa ya riba ya mabenki. Isikope kwa zaidi ya asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili mnalitazamaje? Ni kwamba kama Benki Kuu inakopesha kwa 7% halafu wanatoka watu wa benki za biashara wanakopesha Serikali kwa asilimia 15 inawezekana wapo watu kwenye Serikali yetu, wana hisa kwenye haya mabenki, wanapiga hela kutoka huku Benki Kuu wanaleta huku, wanaikopesha Serikali, ikirudishwa wenyewe wanapata gawio kubwa. Ndiyo maana yake. Jambo hili ndiyo nasema, sitaki mimi nijipe kazi ya kuanza kuangalia kuna wakubwa gani kwenye Serikali wana hisa kubwa kwenye mabenki, kwa hiyo, wananufaika na mchezo huu? Sitaki kujipa kazi hiyo, lakini itoshe kusema busara ituongoze katika hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa, nikamwuliza Waziri wa Fedha na kwa bahati mbaya haya maneno yetu huwa tunazungumza hapa wakati mwingine huwa yanageuka kama ngonjera tu, kwamba wayachukue wasiyachukue, sawa sawa. Ni kwamba, hivi ni nani anaye- control hizi microfinance institutions? Kampuni hizi za kukopesha wananchi ambazo zinapiga riba na wananchi wetu wanateseka, wamenyang’anywa ma-fridge na nini? Sikupata majibu mpaka leo na kazi hiyo inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha hata hii taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha inayosema, riba zimeshuka kutoka asilimia 16.8 mpaka asilimia 16.6, bado haina usahihi sana na hali ya sasa. Mimi nimekopa benki mwezi jana (Oktoba), na mwezi huu nimeanza kulipa mikopo ya kibiashara. Siyo mikopo yetu hii, hapana, ni mikopo ya kibiashara, maana mimi ni mfanyabiashara vilevile. Nimekopa kwa riba ya asilimia 21, akitaka mikataba yangu nitampa aione. (Makofi)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, nimekuruhusu Mheshimiwa.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: nikubaliane na mchangiaji na nimwongezee tu kwamba mfanyabiashara unapokopa kama una hati ya nyumba kwa maana ya dhamana ni asilimia 21 na kama hauna hati ni asilimia 24.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ni sahihi sana na naipokea taarifa….

MWENYEKITI: Na bado mnakopa Waheshimiwa? Asilimia 24?

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ni sahihi kabisa.

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, una kitu kinaitwa letter of offer asilimia 24, kama una tittle deed asilimia 21. Kwa hiyo asilimia 16 inayozungumzwa hapa haipo, sijui labda kwenye baadhi ya mabenki, Kamati ya Bajeti inatueleza nini? Kamati ya Bajeti inatueleza kwamba BOT imeshindwa kuwasaidia wananchi katika kupunguza riba za mabenki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, katika mambo yanayohusu utumishi wa wananchi sina urafiki. BOT siku moja inaweza ikamrudisha Waziri wa Fedha viti vya nyuma, asipoiangalia BOT siku moja itamrudisha viti vya nyuma. Hatuwezi kwenda hivi, wananchi wanapiga kelele, hali mbaya ya uchumi, tunasema, tunasema lakini hakuna linalokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wenzangu wametangulia kusema hapa na naomba niseme, narudia kumpongeza sana Raisi wetu mpendwa. Jana kuna lugha ilitoka hapa, ni vizuri katika mambo haya kuwekana wazi, Mheshimiwa mwenzetu Mheshimiwa Mpina, alisema lugha ambayo wengi haikutufurahisha. Haikutufurahisha kwa sababu mama au kiongozi wa nchi anapokwenda kutafuta manufaa kwa ajili ya watu wake, akija hata kama na uji, onyesheni kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Raisi amekuja na trilioni 1.3, kuna kazi inafanyika ambayo haijawahi kufanyika ndani ya kipindi kifupi kama hiyo kwenye majimbo yetu; Mheshimiwa Mpina anachotueleza nini kwamba wameacha pesa nyingi huku, pesa gani anazosema? Pesa ambazo zipo katika Mahakama ya Usuluhishi wa Kikodi baina ya Barrick na Serikali kuhusu masuala ya kodi zinazotokana na madini, yaani zipo kwenye Mahakama, yeye ndio anatuambia ndio pesa zimeachwa. Ikihukumiwa kwamba nyie hamna kitu maana yake hamna kitu. Sasa huo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe nikuhakikishie…

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Ndio.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mpina huwa analewa togwa, kwa hiyo msamehe tu, asikupotezee dakika zako. (Kicheko)

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kusema habari ya kutuambia kwamba tunapiga makofi mpaka mikono inataka kuchubuka kwa sababu ya trilioni 1.3, kama yeye amezipuuza nashauri ile miradi ya maendeleo iliyopelekwa Jimboni kwake iletwe Jimboni kwangu mimi nazithamini sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia na nilitaka nijielekeze moja kwa moja katika yale tuliyoyaona kwenye Sheria Ndogo hizi. Wenzangu waliotangulia wameeleza vizuri juu ya tatizo linaloonekana la Sheria Ndogo kuanza kutumika kabla ya kupita kwenye mamlaka ya Bunge na wanataka, mamlaka zinazotunga Sheria hizi ndogo ziwe makini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuongeza neno jingine kwamba lazima Bunge lifikirie kubadili utaratibu huu uko mbele na kwamba Sheria ndogo zote ziwe kwanza zinadhibitishwa na ndiyo zinakwenda kutumika. Maana inawezekana umakini wengine wakaukosa na mkazusha malalamiko. Kwa hiyo, huko mbele mpaka sasa Sheria bado inatoa mamlaka ya kutunga kwa Sheria Ndogo na kuanza kutumika lakini huko mbele tunaweza tukafikiria kwamba mpaka ifike kudhibitishwa na kukubaliwa na Bunge ndiyo ianze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo tuliyo experience kwenye masuala ya Sheria Ndogo ipo vile vile Sheria Ndogo ya Uhifadhi na Usambazaji wa Madawa yaani The Tanzania Medicine and Medical Devices Good Storage and Distribution. Hapa napo tumekuta kuna tatizo na changamoto, moja ya changamoto tuliyoiona kwamba Sheria hii Ndogo kwanza inampa mamlaka mhifadhi na msambazaji wa dawa yeye mwenyewe kupokea malalamiko ya dawa zinapokuwa na matatizo, na wakati yeye ni mdau katika jambo hilo, wakati mwingine manufacturer wa hiyo dawa yuko nje ya nchi lakini huyu aliyepokea na kuzihifadhi katika uhifadhi na ushasafirishaji dawa inaweza ikapoteza ubora na baadaye ikaenda kuleta madhara yeye mwenyewe Sheria Ndogo ilikuwa inampa nafasi ya kusikiliza malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni tofauti na Sheria nyingine, leo hii ikifika mahali ambapo kuna malalamiko ya mamlaka za kutoa mawasiliano kama vile vyombo, Voda sijui Airtel na wengine kuna regulatory authority ya kwao ambayo ni TCRA ndiyo itapokea malalamiko. Kwa hiyo, tulitaka mamlaka haya ya kupokea malalamiko ya juu ya storage ya madawa yanayopoteza ubora ya baki TMDA na yasiende kwa wale ambao ni owner wa premises za kuhifadhi. Kwa hiyo hilo ni moja la tatizo tuliloliona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jingine ni suala la dawa kupoteza ubora wakati zikiwa katika maeneo ya storage na usafirishaji. Na kwamba lazima huko mbele hizi Sheria Ndogo zifikirie kuwe na utaratibu wa ku-recall yaani ambao unaweza ukafika mahali kukawa na utaratibu maalumu wa kuzirudisha dawa zilizoharibika kutoka kwa hawa ambao ni owner wa premises na wale ambao wana- distribute hizo dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika jambo jingine ambalo tume-experience ni kwamba utungaji wa hizi Sheria Ndogo vilevile wakati mwingine unakumbana na changamoto za kiutafiti. Kwa mfano; Sheria za Uvuvi hizi Sheria Ndogo za Uvuvi zimeweka mambo mengi ambayo yanakinzana na hali halisi ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, lakini unachunguza unakuta Wizara yenyewe ya Uvuvi na Mifugo inapewa bajeti ndogo sana. Kwa hiyo, katika masuala ya utafiti wanapata shida. Kwa hiyo, wanatunga kanuni kwa kuzingatia jinsi ambavyo wao wanavyofikiria zaidi kulikoni kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Ziwa Tanganyika ambalo lina kina cha zaidi ya mita elfu moja na kidogo, lakini eneo la oxygen ambalo linaweza linakaa viumbe kama Samaki ni mita 150. Lakini ukiangalia katika kanuni walizozitunga wanamkataza mvuvi kuvua kwa zaidi ya mita 20. Kwa hiyo, kuna mita 150 nzima ambayo ipo pale ambalo ni eneo linaweza likavuliwa na hao wakapata mazao ya uvuvi na ambalo lina oxygen, lakini kanuni ile wala haifikii mita 20. Sasa hivi ndiyo tulikuwa tunafikiria wafikie mita 20, lakini kanuni ile ilikuwa inataka nyavu ziwe na macho 144 ambayo ni sawa sawa na mita 16. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunaona yanakinzana na mahitaji ya wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo tuliliona hili si la kiutafiti ni la kimlamlaka tu kwenye suala la uvuvi, wavuvi wameongezewa mzigo sana chombo chenyewe cha uvuvi kinalipa leseni. Lakini mvuvi mmoja mmoja anayeingia kwenye uvuvi naye kwenye kanuni hizi amewekewa leseni kila mvuvi awe na leseni. Na mbaya zaidi wavuvi hawa wanahama kutoka chombo kimoja kwenda chombo kingine akihama kutoka chombo kimoja kwenda chombo kingine ile leseni yake haitambuliki akifika kwenye chombo kingine lazima akate leseni nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeona katika utungaji wa Sheria hizi Ndogo kuna maeneo ambayo yanakinzana na hali halisi na kwa maana hiyo yanaleta ugumu katika kupata tija kwa watu wanaofanya shughuli kwenye sekta hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweke mchango wangu kwenye mpango huu wa maendeleo wa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama uelewa wangu uko pamoja na wenzangu ni kwamba, kadiri tunavyojadili mpango huu tunajaribu kuona vipaumbele katika mpango wetu vitakavyosababishia kuweka sura ya bajeti yetu inayokuja ya 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma, miaka mitano iliyopita, ukiangalia maendeleo ya Taifa letu yalijielekeza katika kuwekeza nguvu kubwa kwenye viwanda na suala zima la madini. Na sasa ukiangalia mwelekeo tulionao sasa na hasa ukiangalia bajeti tuliyoipitisha ni kwamba muelekeo mkubwa sasa tumejielekeza katika kilimo, na hili ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme, hata tulipokuwa tumeamua kujielekeza katika viwanda na kuweka nguvu kubwa katika viwanda, viwanda tulivyovikusudia si vingi vilivyowekwa. Viwanda tulivyovikusudia ni viwanda vya kuchakata mazao ya wakulima na wafugaji ili kuyaongezea thamani ili tuweze kuwatoa watu wetu katika umasikini. Hata hivyo viwanda vilivyoibuka vingi vikawa ni vya kutengeneza nondo, saruji, kutengeneza malumalu, sijui kutengeneza nini, mambo chungu nzima ambayo kwa kweli, haya add value ya mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa hiyo, ulikuja msemo wa wenzetu ambao wako nje, yaani maana ya nje ya Serikali, wana-challenge wakasema tumejielekeza katika maendeleo ya vitu kuliko maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msemo huu ulichukua nafasi kubwa sana ya mijadala, lakini tulikuwa right. Maendeleo ya vitu waliyokuawa wanayasema, kwamba tulijielekeza katika kutengeneza barabara, kujenga shule, hospitali na viwanja vya ndege. Tulifanya hivi kwa sababu, hata kama ukitaka kuwasaidia watu kuwainua kiuchumi kama miundombinu si rafiki basi hao wakulima wako hawawezi kupata soko zuri la mazao, hao watu wako kama hawana hospitali hawawezi kuwa na afya nzuri na kuweza kumudu uhindani kwenye uchumi, kwa hiyo tulikuwa tuko right.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nafikiri sasa ni lazima tujielekeze sasa katika maendeleo ya watu. Kazi tuliyoichukua kwa kipindi kirefu, ya miundombinu, shule, sijui hospitali na nini, kwa kweli naweza kusema tumepiga hatua kubwa sana tukijilinganisha na nchi nyingine za Afrika, hatua ni kubwa sana. Nchi zote za jirani zetu hapa hakuna nchi inayoweza ikajilinganisha na sisi katika miundombinu. Tumekopa, tumefanyaje tukasema tutengeneze mazingira yatakayowafanya watu wetu, wakulima wetu waweze kufikisha mazao sokoni, watu wetu waweze kufika mahali kupata huduma za afya nzuri, waweze kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huko tunakotaka kwenda kusaidia maendeleo ya watu ni kupi? Ndio kitu ambacho nataka nikizungumzie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja. Tunataka wakulima wetu wapate bei nzuri za mazao ili kipato chao kiongezeke maendeleo ya watu yainuke. Kwa hiyo, mpango huu lazima utuelekeze katika namna gani tutawatoa wananchi katika kuwahimiza limeni, baada ya kulima halafu kufika mahali mazao yanaoza hayapati soko. Lazima mpango huu utueleze tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile mpango huu utueleze namna gani tunawasaidia wasomi wetu ambao wamesoma, hawajapata ajira lakini wanataka kuchangia katika uchumi wa Taifa, mpango huu ni lazima utueleze. Na huu katika kutueleza ni kwamba, watu wengi wanayo mipango mizuri ya kukuza uchumi na kuendeleza Taifa lao lakini hawana mitaji. Wakienda benki si rafiki katika kutoa mitaji kwa watu wanaoanza. Kwa hiyo ni lazima tufike mahali tuseme ni namna gani tunaelekeza benki zetu na vyombo vya fedha kuwezesha watu wetu ambao wana elimu, wana ujuzi, wana maarifa, lakini hawana mitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu mikopo nafuu. Tumeweka mikopo ya vijana wanawake na walemavu asilimia 10 ya Halmashauri. Ni kiasi kidogo sana. Leo tunataka tuone kwenye bajeti yetu itakayokuja tuweke fedha kwa ajili ya kuongeza mfuko wa wanawake na vijana, tusitegemee asilimia 10 za Halmashauri tu, haziwezi kututoa mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeona Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamekuja na mpango mzuri sana wa kusaidia kuinua watu na hasa kwenye uvuvi. Wamekuja na mikopo isiyokuwa na riba ya maboti za uvuvi, mashine, vifaa vya kuhifadhia samaki na rada. Mimi naomba sana tunapokwensa kwenye bajeti inayokuja hebu tuweke fedha za kutosha hapa, uvuvi unaweza ukasaidia kuongeza Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa sana. Tunayo maziwa makubwa kama ziwa letu ya Tanganyika pale lakini imefika mahali ambapo uvuvi hauchangii pato la Taifa kwa kiasi kikubwa, ni kwa sababu hatujawawezesha na hawawezi kwenda benki. Hata hivyo fedha hizi zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya boti na vifaa hivyo ni chache sana, tunaomba kwenye bajeti hii inayokuja tutazame namna ya kuongeza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafanyabiashara. Wafanyabiashara nao lazima tuwasaidie; na katika kuwasaidia ni kwamba, hivi kweli jamani bado tunafikiri ni muhimu kuwa na VAT ya asilimia 18? Mbona huu ni mzigo mkubwa sana? Hebu tuweke VAT kidogo iweze kulipika sana. vilevile mfumo wa VAT, kama ni watu wote wafanyabiashara wawe VAT registered kwa sababu gani; wale waliosajiliwa kule kwenye VAT wanaumia kuliko wale ambao hawakusajiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri… aah, muda umeisha?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia sentensi yako.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ambalo ningemalizia katika hilo ni kwamba, Halmashauri zetu zimeonesha, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG zimekusanya vizuri fedha asilimia 94 kuliko hata Serikali Kuu kupitia TRA ambapo kwenye malengo wenyewe walifikia asilimia 86.6. Katika hali hii tuwaongezee nguvu, na katika kuwaongezea nguvu bajeti inayokuja Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa tuwaongezee fedha wapate namna ya kusimamia vizuri Halmashauri zetu. Ahsante sana. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Sura ya 427 kama Muswada ulivyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri na mapendekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda niipongeze Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na pia kumpongeza Mwenyekiti na Kamati nzima ya Bunge ya Ulinzi na Usalama. Kwa kweli, jambo hili limekuwa ni jema na limekuja kwa wakati ambapo majanga ya moto yanachukua kasi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nilikuwa natazama wakati ndugu yangu Mheshimiwa Zahor anatoa ufafanuzi juu ya suala zima la kuwa jeshi kamili, maana zamani ilikuwa inajulikana kama Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, sasa ni Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri wenzetu wanaosimamia jeshi hili watazame changamoto moja kubwa ya kuitwa jeshi, tusitazame tu haja ya kuitwa jeshi. Vitendo vya matukio ya moto yanatokea halafu wanakwenda pale wakiwa hawana maji, siyo vitendo vya jeshi, ni vitendo vya kikosi. Sasa mnakwenda kwenye jeshi, ni lazima myaangalie mambo hayo. Hakuna jeshi linaweza likawa linafanya uzembe wa kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujielekeza katika Kifungu Namba 11(a)…

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda. Watu wengi wanashindwa kuelewa. Vyombo hivi vinapokwenda kuzima moto, vinakwenda vikiwa vimekamilika na vina maji ndani ya magari yao. Changamoto inapatikana, pressure inayotumika ku-discharge maji kwenye magari haya ni kubwa mno. Inachukua muda mchache sana maji yale kuweza kwisha na baadaye kuonekana gari imekuja bila maji. Ndiyo maana sheria hii sasa inaweka kipengele cha kulinda fire hydrants ambazo ndiyo sehemu sasa ya kuweza kupata rescue ya kuchukua maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo kwamba magari haya yanakwenda kuzima moto bila maji, hiyo, siyo kweli. Magari yanakwenda na maji na ukakamavu upo wa kutosha, tatizo yana-discharge maji kwa pressure kubwa yanakwisha upesi. Nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kilumbe.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mwenyekiti nimeipokea ingawa haiendani na taarifa halisi zilizoko kwenye Umma wa Watanzania. Tunaarifiwa na vyombo vya Habari hivyo, nasi hatuendi kwenye matukio yote; na sijamsikia Mwenyekiti anasimama kupinga taarifa hizo za vyombo vya Habari. Kwa hiyo, haisaidii sana hapa Bungeni. Marekebisho haya ya sheria hayahusiani na hilo; hilo nilikuwa nimeweka tu kwamba, tunapozungumza jeshi, tutazame dhima ya jeshi badala ya ilivyokuwa kikosi.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu hasa inaanzia kwenye Kifungu cha 11(a) ambacho kimeongezwa kwenye Muswada huu ambacho kinawapa nafasi sasa Askari wa Zimamoto kutumia silaha. Katika hoja hii, kutumia kwao silaha kumeelezwa humu kwenye Muswada huu kwamba ni kwa lengo la kulinda miundombinu ya jeshi ambayo ni hayo magari, sehemu za kuhifadhia maji na maeneo mengine. Sasa lazima niseme kwamba iwe wazi au iongezwe zaidi kwamba hata kulinda mali za wananchi maeneo wanapokwenda kufanya uokoaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele hiki kilichoko kwenye Muswada kinazungumzia miundombinu ya jeshi. Kwamba, wanapewa silaha kwa ajili ya miundombinu ya jeshi. Nataka pale ikiwezekana waongeze, “pamoja na kulinda mali katika maeneo yanayofanyiwa shughuli za ukoaji wa moto.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nataka nilichangie katika hili ni suala la Kifungu Namba 22 ambacho kinataka sasa majengo yote yenye urefu kutoka usawa wa ardhi kwenda juu mita 12 yanayojengwa, michoro yake ipitishwe kwenye Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kuzingatiwa kwa vifaa vya zimamoto katika majengo hayo. Jambo hili naona ni jema na zuri, lakini kitu kimoja tu ambacho nataka niombe, tumekuwa na tatizo la urasimu katika ofisi zetu. Kuna watu wanataka kujenga majengo haya, watapeleka zimamoto, anaambiwa acha hapa, utarudi wiki ijayo uje uchukue. Huyu mtu anatakiwa aende Mipango Miji, anatakiwa aende kwa Bwana Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawazo yangu ambayo nataka kushauri ni kwamba, Jeshi hili la Zimamoto lihusike katika kuangalia mambo haya, lakini lihusike pale ambapo Kikao cha Kamati ya Mipango Miji kinapokaa kupitisha building permit, ndipo nao waalikwe kuhudhuria. Kwa sababu wakati mwingine kunatokea mpaka upotevu wa nyaraka. Unapeleka michoro yako ya jengo, unataka kwenda kuichukua, wanasema hiki hakionekani, hiki hakionekani kwa sababu, kimekaa muda mrefu kwenye ofisi mojawapo. Sasa wote wakutane kwenye Kikao cha Mipango Miji kinachotoa building permit watazame michoro hapo na wakubaliane au kutokukubaliana na mchoro huo wakiwa kwenye kikao cha pamoja badala ya mwananchi kuzunguka ofisi moja moja anatembeza nyaraka hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndio mambo ya msingi niliyoyaona.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda. Mita 12 ndiyo ghorofa tatu? Mita 12!

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Kuanzia ghorofa tatu.

SPIKA: Inafika hapo eeh! Maana tusije tukasema mita 12 halafu kumbe ni hapa karibu karibu tu.

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, kwenye sheria humu wamesema mita 12, hawakusema ghorofa ngapi.