Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Geophrey Mizengo Pinda (2 total)

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii nami kama Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nipate nafasi ya kuchangia kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote, kwanza ndugu zangu ambao ni Wawakilishi wa Wananchi, kama kuna eneo ambalo tulikuwa tumeliacha likiendelea kutawaliwa ni hili la utoaji haki. Kwa sababu mwanzo wa matumizi ya Kiingereza katika utoaji haki ulianzia kwa Wakoloni. Nchi yetu imepata uhuru kamili na sasa tuna miaka ya kutosha kabisa katika uhuru wetu. Kwa hiyo, utaona namna ambayo kuchelewa kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji haki ilikuwa ni kuendelea kukandamizana katika maeneo ya maisha yetu ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itambulike tu kwamba sheria ndiyo msingi wa maisha. Sheria ni makubaliano ya jamii kuishi katika mfumo fulani na kuuheshimu. Sasa huwezi kuleta zile sheria na miundo hiyo kwa lugha ambayo wewe mwenyewe huijui. Waingereza walileta lugha hii kwa sababu ndiyo walikuwa wanatutawala. Sasa hata baada ya kutawaliwa, tuendelee tu kusimama kwenye eneo lao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kusema ni nini? Kiswahili kinaheshimika sana kote duniani na mtakublaiana nami kwamba kwa sasa hivi Mataifa mengi sana yamefungua TV za Kiswahili. Ukienda Ujerumani, Korea, Japan, BBC wote hawa wanatuenzi Watanzania ambao hatujajitambua thamani yetu. Sisi tunathaminika sana duniani, lakini sisi wenyewe hatujajithamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ufike na kila jambo linahitaji uthubutu. Mheshimiwa Rais asingekuwa mthubutu tungeendelea kuimba wimbo wa kuhamia Dodoma hata miaka 500 ingepita bila kufika hapa Dodoma. Sasa ifike wakati, tunataka kubadilisha miundo ya maisha yetu ili wananchi wetu ambao ndiyo wanufaika wakubwa waweze kunufaika na lugha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingi sana nimeshuhudia akina dada, akiwa mjamzito Tanzania anataka kwenda kuzalia Ulaya ili aandikishe uraia wa Ulaya. Sasa sijui ni mawazo tu ambayo mtu anakuwa nayo ya kuathirika kisaikolojia, lakini ukweli Tanzania yetu ni Tanzania ya Kiswahili. Kwa hiyo, sheria zetu zikibadilika zitawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi migogoro ni mingi. Hapa nina judgment zilizotolewa kwenye Mahakama karibia sijui copy ngapi, wananchi hawajui namna ya kuzitafsiri, wanatafuta Mkalimani awatafsirie. Acha hao Waingereza watafute mtafsiri wa Kiswahili, siyo kazi yetu sisi tulio wengi kutafuta watafsiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini wazi mawazo ya Waheshimiwa Wabunge ambayo yamelenga katika kukubaliana na wazo la Wizara, ni vizuri mkayapa nguvu ili muweze kufika mahali tuweze kukubaliana na hii hoja iliyowasilishwa na Wizara ili tuweze kufikia muafaka wa lugha ya Taifa kutumika mahali popote pale kwa ujasiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuniona, dakika saba hazitafika kwa kweli. Kwa sababu mtoa hoja atakuja kutoa maelezo yote. Nilitaka nirekebishe usemi fulani ambao usije ukanukuliwa vibaya.

Mheshimiwa Spika, hakuna sheria ambayo ilishakuwa sheria halafu ikakatwa. Serikali inachofanya ni kupeleka mapendekezo kwenye Kamati, na Kamati inapopitia yale yanayokuja hapa sasa hayana sura ya Serikali yana sura ya Kamati ya Bunge ambayo imechakata na sasa inaleta kwa ajili ya ridhaa ya Waheshimiwa Wabunge; na sasa Wabunge ndio Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria. Kwa hiyo hapa napo tunapata ule mchakato na mapendekezo then tunafikia kwenye muafaka wa kuitunga ile sheria ambayo inapelekwa kwa ajili ya kusainiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka tu nirekebishe hilo, kwa sababu wananchi wasije wakafikiri kwamba kuna sheria ambayo inatungwa na Serikali halafu inapelekwa Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya aina yoyote. Kwa hiyo yale mapendekezo yanapita kwenye vyombo ambavyo kimojawapo ni Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, inapitia mawazo ya Serikali juu ya kutunga ile sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nilisemee tu hilo, lakini vinginevyo niwapongeze wajumbe wote ambao wametoa mawazo yao. Na kimsingi kwa sehemu kubwa sana nimeona mengi ni yale ambayo vilevile kamati imependekeza yafanyiwe marekebisho.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.