Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Anyigulile Jumbe (3 total)

MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani umewafanya wananchi na wakulima wa kokoa wasipate pesa papo kwa papo kama ambavyo Serikali leo imejibu; na kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ni tofauti kabisa na uhalisia ulioko kule field, je, anachukua hatua gani kwa watu ambao wametoa taarifa ambazo sio sahihi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa zao la kokoa linalimwa na watu kwenye nyumba/kaya zao na siyo mashamba makubwa na wanatumia muda mwingi kukusanya hizo kokoa kidogo kidogo na pesa zinazolipwa zinachukua muda mrefu na kwamba makampuni yanayonunua yanaanza kwanza kukubaliana wao kwa wao pamoja na makato makubwa, je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti haya matatizo yaliyopo kwa wakulima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anaposema taarifa tulizotoa sio sahihi; taarifa tulizotoa ni sahihi, wakulima wamelipwa kutokana na takwimu tulizonazo na uthibitisho tulionao. Kwa hiyo, kama ana kesi maalum ya mkulima ama wakulima ambao hawajalipwa atuletee hiyo kesi na tutaishughulikia kwa wakati na inavyostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kupitia Bunge lako Wabunge wanapoinuka na kusema kwamba, kuna mkulima X hajalipwa na sisi Wizara tunapoomba kwamba, tuleteeni uthibitisho, tunaomba mtuletee uthibitisho, mjadala huu usiishie humu ndani. Mtuletee uthibitisho, ili tuweze ku- resolve tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, taarifa tulizotoa ni sahihi. Hoja iliyoko ya kwamba, mkulima anapovuna, anapokausha, anapopeleka kwenye chama cha msingi mpaka inapoenda kwenye chama kikuu ni vizuri tukaelewa kwamba, cocoa inakusanywa kidogokidogo; mkulima atavuna kilo moja, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa, baada ya siku chache atavuna kilo kadhaa atapeleka kwenye chama cha msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna hoja kwamba, tujadiliane kupunguza muda wa kutoka kwenye chama cha msingi kwenda kwenye mnada, lakini hatuwezi kurudisha mfumo ambao ni maarufu kama njemke ambao wakulima walikuwa wanafuatwa majumbani na wanakusanyiwa cocoa yao na wanapewa bei ndogo na walanguzi hao ndio wanapeleka kwenye mnada, hatutaruhusu huo mfumo. Kama kuna changamoto kwenye mfumo wa malipo, tuujadili huo mfumo wa malipo na kama Waheshimiwa wana maoni watuletee, lakini Wizara sasa hivi tunatengeneza utaratibu wa kuondoa mfumo wa kuhifadhi mazao ya cocoa kwenye maghala binafsi na yatatumika maghala ya Serikali. Tutaanza pia kuuzia katika AMCOS, badala ya kuleta kwenye chama kikuu cha ushirika, ili tuweze kupunguza time kati ya mnada na malipo ya mkulima. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Kyela jengo la mama na mtoto liliungua. Je, ni lini Serikali sasa itamalizia pesa zilizobaki kwa ajili ya jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Kyela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ni moja ya hospitali ambazo nazifahamu sana kwa sababu nimekuwa mganga mkuu wa Kyela kwa zaidi ya miaka tis ana nimekuwa sehemu ya uendelezaji wa miundombinu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela. Ninafahamu kwamba ni kweli wodi ilipata ajali ya moto na Serikali imesha peleka fedha na kazi za ukarabati wa wodi ile zinaendela.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimhakikishie kwamba katika Mpango ujao tumetenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha ukarabati wa wodi ile iliyopata ajali ya moto ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Jumbe kwamba jambo hilo linafanyiwa kazi na mara fedha zitakapopatikana basi ukamilishaji wa wodi ile utafanyika ili tuendelee kutoa huduma kama ambavyo tunatarajia.
MHE. ALLY A. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; Serikali kama kawaida imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kwenye elimu. Sasa hivi imetokea wanafunzi wanaotoka kidato cha nne wanachaguliwa moja kwa moja kwenda kwenye vyuo.

Sasa nilitaka kuuliza na wengine hawana uwezo kabisa na wazazi wao wameshindwa kuwalipia na utakuta ana division one au two. Sasa nilitaka kuuliza je, Serikali inawasaidiaje hawa vijana ambao wanashindwa uwezo wa kwenda huko vyuoni kwa ajili ya kuwasaidia wafike huko vyuoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jumbe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jumbe anazungumza kwamba wapo wanafunzi ambao wanafaulu lakini nafasi za kujiunga kwenye elimu ya juu zimekuwa ni changamoto na suala kubwa hapa ni kuweza kufanya upanuzi. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jumbe na Wabunge wote kwamba tumesaini sasa mkopo kutoka Benki ya Dunia katika mradi wetu wa HIT ambao zaidi ya dola za Kimarekani milioni 425,000 ambazo zinakwenda kufanya upanuzi mkubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu. Tutakapofanya ukarabati huu tunaamini tutaongeza nafasi za udahili na kuondoa changamoto hii ya wanafunzi wengi ambao wamefaulu vizuri lakini kuachwa kwenye vyuo vyetu. Nafasi hizo zitakapoongezeka tunaamini wanafunzi hawa wote ambao watakaofaulu wataweza kupata nafasi ya kwenda kuingia katika vyuo vyetu, asante sana.