Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juma Usonge Hamad (11 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo hii kuhudhuria kwenye Bunge lako Tukufu salama usalimini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sina budi pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri wa Fedha kwa uandaaji mzuri wa mapendekezo haya ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi pia kipekee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa mno aliyoifanya kwa ajili ya kulisimamia Taifa hili la Tanzania kusonga mbele kimaendeleo. Ingawa wapo watu wachache ambao ndiyo wanaomrejesha nyuma Mheshimiwa Rais, lakini bado anaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Waziri wa Fedha, uchambuzi na ushauri wangu utajikita katika maeneo makuu matatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza nitajikita zaidi kuhusiana na kupanda bei kwa vifaa vya ujenzi. Sasa hivi tumeshuhudia upandaji bei wa holela. Tokea kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2020, bei ya cement imepanda mno. Kwenye hili halijaathiri tu sekta binafsi, lakini hata sekta ya umma pia imeathiriwa mno. Sasa hivi tumeshuhudia cement inauzwa kwa shilingi 17,000/= mpaka shilingi 20,000/=. Kwa kweli Watanzania wanaumia sana. Haiumizi tu kwa huku Mainland, lakini hata kwa upande wa Zanzibar pia wanaumia. Wapo wafanyabiashara ambao wanachukua cement kutoka Bara kupeleka Zanzibar; kwa bei hii ya shilingi 17,000/= ikifika Zanzibar ni bei kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika kuja kufanya majumuisho atupe majibu, amechukua hatua gani, au atachukua hatua gani kwa ajili ya kudhibiti upandaji holela wa bei ya cement? Siyo cement tu, nondo nazo zimepanda sana; gypsum powder nayo pia imepanda sana; misumari na bati, halikadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana atakapokuja Mheshimiwa Waziri atupe majibu na mikakati ambayo ipo kwa ajili ya kudhibiti huu upandaji holela wa hii cement ambayo imemuathiri sana Mtanzania katika pato lake la kawaida. Siyo kuathiri tu katika sekta binafsi, hata sekta ya umma, kwa maana ya Serikali. Sasa hivi Serikali inapoendesha miradi yake ya kimaendeleo, hununua cement kwa bei ghali sana, inasababisha kukwamisha utendaji mzuri wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo la pili ambalo ni muhimu sana kwa sasa hivi katika nchi yetu ambayo tayari tunaendelea kwenye uchumi wa kati. Bado hatujajipanga na hatuna mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba Serikali inakusanya mapato kupitia digital economy. Kwa sasa hivi, nadhani sote ni mashuhuda, Waheshimiwa Wabunge tunatumia mitandao ya kijamii. Wapo wafanyabiashara wengi sasa hivi hawanunui bidhaa zao kuingiza madukani, wananunua bidhaa ile kuweka kwenye stoo na wakauza biashara yao kupitia mitandao ya kijamii. Wanatumia WhatsApp, Instagram, Facebook na mitandao tofauti tofauti. Hata hivyo, bado sijaona wazi kabisa Serikali kusimamia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wafanyabiashara wanawasiliana na mteja moja kwa moja kwa maana kwamba seller na customer wanashirikishwa kwa pamoja wanawasiliana wapi nikuletee mzigo, nikikutumia mzigo Dodoma utatoa pesa ya usafiri shilingi 1,000, lakini Serikali bado haijatambua hizi technic ambazo sasa hivi zinatumiwa na wafanyabiashara. Hii inasababisha Serikali kupoteza gharama kubwa sana kwa ajili ya kuwachaji hawa wafanyabiashara. Hivyo, naiomba sana Wizara hii pamoja na wataalam wetu wa Serikali kuhakikisha sasa wanaweka mipango madhubuti na mikakati ili mradi fedha za Serikali zisipotee kupitia uchumi huu wa digital economy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi tuna wasanii, tuna watu mashuhuri kwenye nchi hii ya Tanzania na wanatumia mitandao ya kijamii, kwa mfano, tunao wasanii wakubwa wanapata fedha kupitia you tube; msanii analipwa pale ambapo ana watazamaji wengi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Usonge.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu leo hii kutujaalia tuko wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa leo tunaendelea na Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi mimi nitajikita zaidi kwenye suala la uvuvi. Kwenye suala la uvuvi kuna watu ambao wanajishughulisha na suala la Mwani, ingawa wachangiaji wengi hawajalizungumzia suala hili, lakini ni suala ambalo ni muhimu sana na suala ambalo ni nyeti. Ukiangalia kuna baadhi ya Mikoa Tanzania Bara na kule Zanzibar kuna Mikoa Tanzania Bara isioyopungua mitano upo Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Tanga ndiyo mikoa ambayo imeshamiri sana katika kujikita kushughulika na suala la uvuvi huu wa mwani.

Mheshimiwa Spika, lakini bado sijaona mipango mikakati kupitia Wizara hii mbali na ripoti ambayo imewasilishwa hapa mezani, bado sijaona fungu la fedha au mikakati yoyote ambayo Wizara imejikita kwa ajili ya kunusuru hili zao la mwani. Miaka ya nyuma mnamo mwaka 1980 zao hili la mwani lilishamiri sana lilipoletwa Zanzibar na tukafanikiwa kwa muda wa miaka 10 na ikaonekana Zanzibar ambayo kiujumla ndiyo Tanzania ikaonekana kama nchi ya Tatu katika kufanikiwa katika kulipanda zao hili la mwani.

Mheshimiwa Spika, lakini mnamo mwaka 1990 na kuendelea zao la mwani hili likaendelea kulimwa huku Tanzania Bara, na wengi wao walikuwa wanapanda huu mwani ni wakinamama. Ukiangalia asilimia 90 ya kinamama ndiyo washughulikaji wakubwa sana wa zao hili la mwani, miaka hiyo ya nyuma mwani ilikuwa ina value kubwa sana na ulikuwa una faida kubwa sana, lakini cha kushangaza baada ya mwaka 2010 na kuendelea zao hili la mwani halina thamani hata kidogo, mbali na gharama kubwa sana za wavuvi hawa wa mwani waliotumia kwa ajili ya kulikuza hili zao la mwani na matokeo yake kupata faida gharama kubwa sana ambazo wanazitumia, sijaona mpango mkakati wa kunusuru zao hili mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa Tanzania inatajwa ni nchi ya tatu baada ya Uphilipino na Indonensia katika kuongoza zao hili la mwani. Kwa hiyo naiomba sana Wizara, naiomba sana kupitia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi iende ikaangalie na kunusuru zao hili la mwani, tukiangalia Zanzibar wamejaribu kutumia mbinu tofauti tofauti kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani, wameanzisha makongamano mbalimbali, kutafuta wawekezaji bado changamoto kwenye soko, lakini bado kwa Tanzania Bara inaonekana kwamba zao hili halijapewa mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana ndugu yangu Naibu Waziri ingawa ni mmoja ambaye unafuatilia sana suala hili la mwani na kufuatilia sana, lakini bado sijaona mikakati ingawa mwaka jana mlitenga zaidi ya shilingi milioni 41, lakini fedha mlizozitowa ni shilingi milioni 14 kwa ajili ya kununua kamba, lakini mwaka huu sijaona kabisa, sijaona kabisa fungu la fedha ambalo limetengwa kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara hii mtenge fedha kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia la pili tutafute wawekezaji kutoka nje, tusing’ang’anie wawekezaji hawa tuliokuwa nao sasa hivi, lazima tufungue forum ya kuwavutia wawekezaji kwa ajili ya kunusuru zao hili; asilimia 90 ya kinamama ndiyo wanajishughulisha na zao hili la mwani. Najua tukisema tunaendelea pia tunawadharau na bei ndogo ya soko tunaenda kulididimiza zao hili la mwani.

Mheshimiwa Spika, nadhani tukiweka mpango mikakati mizuri zao hili linaweza likainuka na tukarejea kwenye top one ile ambayo tayari kidunia zao ili la mwani Tanzania miaka hiyo, basi tukaweza kuirejesha ndani ya miaka hii. Mimi ninaamini ndugu yangu Abdallah Ulega bado ujachelewa na ninaamini maarifa mengi na unauwezo mkubwa sana kwa ajili ya kunusuru zao hili la mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tusiishie hapa tu tunao ndugu zetu wa Zanzibar, kwa nini tusishirikiane kwa pamoja kwa sababu ni suala la kutafuta soko nje ya nchi ni suala la Muungano, Katiba imezungumzia ibara ya kwanza na ya pili kwamba tunapokwenda nje kule tunakuwa kitu kimoja tukaazisha angalau japo makongamano kwa mfano kama tukianzisha masuala ya Seaweed Vast Value Tanzania tunaweza tukanusuru zao hili la mwani na mwisho wa siku tukavutia wawekezaji na zao hili likaleta tija …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Juma Usonge Hamad.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia leo hii tupo wazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita zaidi, mara nyingi sana Wabunge wote waliosimama hapa wanazungumzia suala la vijana na mimi kama rika ya vijana bado ninayo haki ya kuzungumzia suala la vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii, imebeba taswira kubwa na dhana kubwa sana ya kumkomboa kijana wa Kitanzania sasa hivi. Ukweli usiopingika idadi kubwa sana ya vijana wa Tanzania ndiyo ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali, lakini ndiyo wanaochangia pato kubwa sana la Taifa hili la Tanzania. Ripoti ya dunia kwenye Benki Kuu inaonyesha kwamba Tanzania kila mwaka vijana milioni moja wanaingia kwenye suala la ajira, lakini vijana 200,000 tu ndiyo wanufaikaji wa ajira, lakini vijana 800,000 ndiyo ambao hawapati ajira mpaka muda huu tuliouzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukizungumza kama miaka mitano ijayo bado tunatengeneza wimbi kubwa sana la vijana ambao watakuwa hawana ajira. Sasa wazo langu, kwenye Wizara hii, lazima tuweke mipango mikakati namna gani tunaweza tukawasidia vijana kwenye Wizara hii. Isiwe Wizara hii kazi yake kubwa sana, kazi yake kufanya mipango mikakati kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, lakini hatuangili vijana namna gani tunaweza tukawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mipango mahsusi ya kuweza kuwasaidia vijana, tunao vijana wa vyuo vikuu wanamaliza vyuo vikuu, lakini mwisho wa siku wanabakia hawana ajira, ni vijana tu wachache ambao wananufaika na ajira, lakini vijana wengi hawanufaiki na ajira. Kama Wizara imejipanga vipi na namna gani kuwasaidia vijana hawa ambao wanahitimu vyuo vikuu? Kwa nini tusitengeneze exemption at least miaka kama mitatu, minne tukawapa mikopo ya fedha ilimradi wakaanzisha makampuni wao wenyewe binafsi kama vijana ambao wamehitimu vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wapo wanafunzi ambao wamemaliza kada ya sheria, wanaweza wakaendesha kampuni zao za kisheria tukawa tuna mawakala wa-law wakawa wanatetea wananchi, leo hii Tanzania tunaweza tukajikuta hata mtu wa kawaida mkulima anawakili wake wa kuweza kumtetea kwenye mahakama. Leo hii tunaweza tukawa na mvuvi, lakini pia akawa na wakili wake wa kuweza kumtetea kwenyea mahakama endapo kutatokea matatizo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado hatujaona fursa ya kuweza kuwasaidia vijana wanaohitimu chuo kikuu, lakini wapo wanafunzi ambao wanamaliza kwenye kada ya IT ndiyo hawa hawa mwisho wa siku wanaweza wakaanzisha makampuni makubwa ya kufungua masuala ya website, ya kufungua masuala ya computer technician na mambo mengine kadhaa wa kadhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kufungua kwa kampuni hizi nazo zitawasaidia wao wenyewe vijana kupata ajira, lakini pia wapo ambao tayari hawakufikia level za vyuo vikuu nao watapata kufanya angalau ajira, japo kufanya usafi kwenye maofisi na kazi nyingine ndogo ndogo. Lakini bado hatujaenda kuwaangalia kuwasaidia vijana, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye ukurasa wa nane hii ambayo tayari tunaizungumzia ya mwaka 2020/2025 imezungumzia kwamba namna gani Serikali inaweza ikatengeneza ajira kwa vijana milioni nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hatujaangalia mkakati wa kuwasaidia vijana, bado kwenye Wizara hii hatujakaa kabisa. Tusiwe na dhana ya kuweza kuvutia wawekezaji, lakini pia tuwe na dhana ya kuwasaidia vijana wetu ndani ya Tanzania. Najua bado hatujawa na fedha na capital na wala hatujawa na wimbi kubwa sana la wawekezaji kuja ndani ya nchi. Lakini namna gani tunawasaidia vijana, kwa mfano wapo vijana ambao wamemaliza masuala ya business administration ndiyo hawa hawa wanaweza wakaandika ripoti tofauti tofauti kwa ajili ya investment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anaweza akaja mwekezaji, lakini akatafuta ripoti tunao vijana ambao tumeshawapa exemption ya kodi na tulishawapa fedha kwa ajili ya kujikwamu, lakini vipi wanaweza kutengeneza ripoti tofauti tofauti wakaja wazungu, wakaja ma-investor wakachukua ripoti baadaye zikawa applicable. Bado hatujawa tukafikiria lazima Wizara ya Viwanda na Biashara ifikirie namna gani sasa ya kutengeneza fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana kwa ajili ya kujikwamua na huu unyonge na umaskini ili uweze kuisaidia familia zao la sivyo hatuwezi kuwasaidia vijana kwa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutabaki tuna propaganda za kisiasa tuna wasaidia vijana tunatengeneza, tunaandaa ajira kila mwaka, tutaandaa manifesto, tutaandaa Ilani, tutaandaa ripoti tofauti tofauti namna gani ya kuwasaidia vijana, lakini bado hatujawa practical kwa ajili ya kuwasaidia vijana, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakuomba sana wafikirie vijana bado vijana wanateseka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo usishangae kumuona kijana ambaye amehitimu chuo kikuu anaendesha boda boda, usishangae kumuona kijana wa chuo kikuu yupo kwenye michezo ya ku-bet, usishangae leo kumuona kijana yupo kondakta ni muhitimu wa chuo kikuu. Serikali imetumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kumsaidia kijana ili aweze kufika chuo kikuu, lakini mwisho wa siku akimaliza miaka yake mitano au miaka mitatu ya kuhitimu degree anabakia mitaani anaendesha bodaboda. Unadhani kijana kama huyu mwisho wa siku tumemsaidia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukae kama wizara kuweza kuwasaidia, ingawa tunasisitiza siku zote sisi hapa Bungeni kwamba Serikali itenge fedha kwenye Halmashauri asilimia kumi kwa ajili ya kuwasaidia vijana, sawa inafanya hivyo, lakini kwa nini tusitenge angalau asilimia kadhaa ambayo inatoka kwenye Wizara hii kuwasaidia vijana kuanzisha makampuni au kuanzisha shughuli yoyote ya kibiashara? Bado hatujakaa tukafirikia Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Juma.

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii nami kuweza kuzungumza kwenye Bunge lako hili Tukufu. Nitoe pongezi zangu za dhati kwa Waziri Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Hamad Masauni, bila kuwasahau Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na wataalmu wote wa Wizara hii ya Fedha na Mipango kwa uandaaji na uwasilishaji mzuri wa taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, niende moja kwa moja. Kwenye wasilisho langu nitazungumzia zaidi kuhusiana na uchumi. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina uchumi wa Muungano. Uchumi huu unajumuisha na uchumi ule wa Zanzibar, ndiyo maana kila taarifa ya mwezi kutokea BoT inatambua uchumi wa Zanzibar, lakini utaratibu huu hautumiki pale ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapowasilisha taarifa zake za kifedha kule nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye mataasisi ya kifedha, kwa mfano IMF na World Bank, taarifa hizi haziendi moja kwa moja kwa sura ya kipekee ya kuitambua kama Zanzibar, isipokuwa inatambulika kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utaratibu huu unaleta madhara makubwa sana kwa uchumi wetu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, hivi karibuni tu tulitoka kwenye janga kubwa la Corona, Tanzania nayo pia imeathirika kwenye janga hili la Corona, lakini Zanzibar nayo imeathirika zaidi kwenye janga hili. Ukiangalia Zanzibar, uchumi wake mkubwa sana asilimia 82 pato lake la Taifa inategemea kupitia utalii, lakini Bara ni asilimia kama 17 hivi na kidogo ndiyo inategemea utalii. Kwa hiyo, madhara haya yanakuja kutokezea endapo hizi taasisi za kidunia; World Bank, IMF yanapotoa fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi ambazo zimeathirika kifedha, inaleta madhara makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna nchi zetu za karibu hapa kwa mfano Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika, zimepata misaada kifedha, lakini Zanzibar haijaonekana. Kwa sababu uwasilishaji wa taarifa za kifedha kupitia World Bank pamoja IMF, Zanzibar haitambuliki. Hivyo Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri, nawaomba sana, tunapopeleka taarifa zetu za kifedha, basi lazima tutambue Zanzibar nayo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii makusanyo ya fedha ambayo yamepatikana Zanzibar kwa miaka miwili ambapo Zanzibar imeathirika zaidi na Corona, ndiyo maana kufikia kile kiwango cha fedha kwenye bajeti ni asilimia kama 70 tu, mpaka sasa hivi Zanzibar ndiyo ishaanza kupitia tozo tofauti tofauti. Kwa hiyo, hali hii ina athari kubwa sana.

Kwa hiyo, naiomba sana Wizara, tunapowasilisha taarifa zetu za kifedha nje, basi tupeleke taarifa zetu ambazo zitakuwa na sura ya Kizanzibar. Hii itasaidia sana. Naiomba sana Wizara tuzingatie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye eneo lingine la wafanyabiashara. Kuna wafanyabiashara wapo Tanzania Bara na wengine Zanzibar. Changamoto ambayo tunayo, tuko kwenye nchi moja; wapo wafanyabiashara ambao wapo Bara ambao tayari wame invest kwa eneo kubwa, lakini wapo pia Wazanzibar ambao wame-invest kwa eneo kubwa. Changamoto inayopelekea Mzanzibar au Mtanzania wa kutoka mainland kwenda kuwekeza bara au wa labda wa Zanzibar akija bara wa bara akienda Zanzibar kunakuwa na changamoto namna ya kupata leseni. Akienda Mzanzibar, Mtanzania anaonekana kama foreigner. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara, hii ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanapokuwepo wafanyabiashara ambao wamekuwa interested na kuja ku- invest aidha pande hizi mbili za Muungano, basi kuwe kuna exemption ya kuweza kumtambua kama Mtanzania; iwe baadhi ya kodi asikate, asirejee tena kwa ajili ya kukata leseni. Akija Zanzibar, basi apate exemption ndogo au hata atambulike. Isipokuwa anaweza akachangia kodi kutokana na mazingira gani ambayo anafanyia biashara. Hii itasaidia sana; mojawapo linaweza likakuza uchumi wetu wa Tanzania pamoja na kuu-boost.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, itatengeneza ajira kwa vijana wetu; na tatu, itatengeneza variety commodities pamoja na production. Hii itasaidia sana. Leo hii Mzanzibar akija Bara, anaanza process upya kwa ajili ya kupata leseni. Tuondoe hivi vikwazo ili tutanue wigo wetu sasa wa kukusanya kodi, lakini pia angalau tuonee huruma wafanyabiashara wetu waweze kuwekeza wanapokuja upande wa pili wa Muungano. Hii itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, naipongeza sana Wizara kwa kulitambua hili kwamba sasa hivi makusanyo ya visa ya pande zote mbili za Muungano, basi upande ambao utapata fedha, itasaidia sana. Hii itainua uchumi wa Zanzibar, ambao kwa asilimia kubwa sana tunategemea uchumi wa vitu vidogo vidogo. Sasa tukiweka mwanya huu, itasaidia sana ku-boost ule ukusanyaji wa pato kupitia hii visa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi zetu hizi mbili, huko nyuma tulikuwa tunakusanya zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya visa, lakini sasa hivi Mheshimiwa Rais ameliona hili jambo. Kwa hiyo, kutawanya hizi visa itasaidia kwa upande wetu Zanzibar na pia kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana kwamba huku Bara nao pia wataweza kukusanya fedha vizuri kwa kupitia hii visa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia kwa kuidhinisha pesa kila Jimbo kwa ajili ya Mfuko wa TARURA. Naiomba sana Wizara hii ilichukue jambo hili, ituangalie na upande wa pili wa Zanzibar, isiwe wenzetu tu, Watanzania Bara ndio wanaonufaika na huu mfuko wa fedha, bado na sisi kwa upande wetu wa Zanzibar tuna changamoto kubwa. Shilingi milioni 500 ukinipatia kwenye Jimbo langu, utaenda kunisaidia sana na kuwasaidia akinamama ambao sasa hivi wanatembea masafa marefu kwa ajili ya kupata huduma ya afya, akina mama ambao wanabebwa kwa vitanda kama Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba alivyozungumza hapa, watatusaidia sana sasa hivi kusafirishwa kutoka sehemu walipo kwenda hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, machache naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kunipatia fursa hii ya kusimama kwenye Bunge lako yukufu. Lakini pia na mimi niungane na wenzangu kukupongeza kwa kushinda kwa kura nyingi sana. (Makofi)

Baada ya kusema hayo naomba nijikite zaidi kwenye ripoti ambayo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, lakini zaidi nitajikita kwenye maeneo ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mjumbe katika mifuko ya kimataifa yanayohusu masuala ya mazingira duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nitaje baadhi ya wadau ambao wanachangia sana kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzania ikiwemo list of Development Countries Fund, kuna mfuko wa Adaptation Fund, kuna Global Environment Facility ambayo ni ikolojia hiyo kuna mfuko ambao unaitwa Green Climate Fund, kuna mfuko ambao unaitwa UN Environmental Program.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifuko hii inapofadhili nchi zetu hizi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maana kwamba Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Tanzania ambayo ni Tanzania tatizo linakuja kwenye ugawaji wa fedha. Zanzibar miaka yote fedha hizi hazifiki ipasavyo, kwa mfano na nikupe mfano mzuri kuna mradi ambao unatekelezwa wa Global Environment Facility wa ikolojia ambayo kwa ajili ya kunusuru hizi kaya maskini pamoja na vijiji ambavyo viko hatarini kwa ajili ya kuharibika na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fedha ambazo zimetoka zaidi ya bilioni 17 lakini cha kushangaza Zanzibar tumepata 18% na miradi hiyo mpaka hii leo haijakamilika na mradi huu ukomo wake ni ifikapo mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza miradi mingine ambayo tayari inafanyika huku Tanzania Bara miradi hiyo inafanyika kwenye Wilaya nne na yote tayari ishakamilika na fedha zote zimeenda lakini changamoto zile za Zanzibar mpaka leo hii miradi haijakamilika na zimetoka shilingi 402,792,000 basi hizo ndiyo ziliotoka utashangaa nini tatizo; ukiwauliza Zanzibar wanasema fedha zimeganda huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima tuwe wa wazi kabisa Mheshimiwa Waziri nakuomba sana na Serikali yako hii miradi ya fedha zinapokuja Zanzibar tuzisimamie kwa pamoja. Leo hii kuna blah blah nyingi, leo hii tumechonganisha wananchi kati ya Serikali na wananchi wenyewe, leo hii wananchi tumewaambia fedha hizi tunaenda kununua maboti, tunaenda kuwasaidia wajasiriamali, lakini kuna miradi ambayo tayari tumeikita pale kwa ajili ya kupanda miti ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Lakini leo hii miradi hii imefanyika asilimia moja asilimia 90 bado haijakamilika ukomo wa mradi huu uanenda kukamilika kesho kutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tunaenda wapi? Tukae tujitafakari hii mifuko wenzetu wanatusaidia kwa Imani. Leo hii miradi hii haikamiliki kwa muda upasavyo, tunaweka picha gani huko mbele? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii inatekelezwa kwenye Wilaya ya Kaskazini A - Unguja kwenye vijiji zaidi ya vine, wananchi wa kule sasa hivi wameweka kasumba kubwa dhidi ya Serikali yao, Serikali ya Zanzibar ukiwauliza Zanzibar...

MHE. SOUD MOHAMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SOUD MOHAMED JUMAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Juma Usonge uratibu kama alivyozungumza wa fedha ambazo zinakwenda Zanzibar ambao Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo masuuli kwa kweli haliko vizuri; kuna mradi ambao ulikuwa wa African Development Bank na ulikuwa na pesa kidogo tu just dola 350,000 lakini kutokana na uratibu mbaya mradi ule muda umemalizika na zimetumika fedha kama 30% tu na zilizobakia fedha zimeenda halijojo yaani fedha hazikutumika tena mradi umefungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tungeliomba tu uratibu huu tukaupitia na ingewezekana ukaunda tume maalum ya kuweza kuratibu hizi fedha ambazo zinakwenda Zanzibar na mifuko yote hii matumizi yakoje na changamoto ziko wapi? Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante endelea Mheshimiwa; taarifa umeipokea?

MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nimeipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Kwa hiyo, kama alivyozungumza mtoaji taarifa Mheshimiwa Waziri nakuomba sana kwenye fedha hizi ambazo zinaenda Zanzibar tuzisimamie ipasavyo lakini siyo hilo tu pia kuna Mifuko hii ya Jimbo ambayo mnayotupa kila siku tukiwaulizia wenzetu wa Tanzania Bara fedha tayari zimeshaingia, kwa Zanzibar kule kuna urasimu ambao tayari hauna majawabu. Hii ni tatizo tunaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Zanzibar kama tunafanya tathmini Zanzibar ndiyo inahitajika zaidi kupeleka zile fedha. Kuna visiwa sasa hivi vinaanza kupotea, kuna miradi mbalimbali haifanyi kazi sababu ya fedha haiziingizwi, juzi Mheshimiwa Waziri ulikuja Zanzibar umefika mpaka eneo Nungwi umeona maeneo ya beach kule yanavyoharibika na maji kupanda juu. Lakini siyo hilo tu almost Zanzibar nzima kisiwa kinapotea, fedha tunazipata lakini mwisho wa siku urasimu ndiyo ambao tayari unaofanya kazi. Kwa hiyo hatuwi wa wazi, wala hatuwi active kwa ajili ya kuisimamia hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache naunga mkono ripoti ya Kamati. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa hii ya kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kuimarisha muungano wetu, lakini pia kuweka mazingira yetu sawa ili sisi kama binadamu tuwe tunaishi kwa amani kabisa.

Mheshimiwa Spika, nitajielekeze zaidi kwenye maeneo makuu mawili. Eneo la kwanza nitazungumzia suala la muungano nae neo la pili nitazungumzia suala la mazingira.

Mheshimiwa Spika, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa nchi mbili, kati ya Zanzibar pamoja na Tanganyika. Jana tu ndiyo tumehitimisha miaka 58 ya muungano wetu wa Tanganyika pamoja na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huwa kila mwezi tunapata taarifa kupitia BOT ambazo zinatambua uchumi wa Zanzibar pamoja na uchumi wa Tanzania Bara, lakini la kustaajabisha taarifa zinapokwenda nje ya nchi kwa maana ya kwenye taasisi za kifedha, World Bank pamoja na IMF taarifa hizi haziendi kwa sura ya kuitambua Zanzibar. Naomba sana, uchumi wa Zanzibar ni mdogo na ni uchumi ambao ni wa Kisiwa, naomba sana kupitia Wizara hii lazima iangalie ihakikishe kwamba, tunapopeleka taarifa za kifedha lazima kuwe kuna figure sura ambayo tayari itaonekana Zanzibar na uchumi wake.

Mheshimiwa Spika, kila mwezi, kila mwaka, IMF pamoja na World Bank wanatoa taarifa namna ya uchumi, wenyewe wanaita Economic update, kwa Zanzibar haitambuliki. Zanzibar ni sehemu ya kisiwa, lakini pia ni nchi ambayo tayari imeunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naiomba sana Wizara yako Mheshimiwa Jafo kuhakikisha kwamba, Zanzibar zinapokwenda taarifa basi uchumi wa Zanzibar unatambulika kwa sura ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende eneo la pili, eneo la mazingira. Niwapongeze sana watendaji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwa upande wa Tanzania Bara. Ikumbukwe kwamba, eneo la mazingira ni eneo ambalo linajumuisha upande wa pili wa Zanzibar. Tunashangaa sasa hivi kuna miradi ambayo inatekelezwa Zanzibar kwa muda wa zaidi ya miaka mitano, lakini fedha Zanzibar hazifiki kwa wakati. Ukiulizia Zanzibar wanalalamika kwamba, fedha zinaganda Tanzania Bara, Tanzania Bara na huku wanasema kwamba, fedha zinafika Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri, leo hii kuna mradi ambao unatekelezwa Wilaya yangu ya Kaskazini Unguja kwenye vijiji zaidi ya vitatu. Kuna Kijiji ambacho kinaitwa Mbuyutende, kuna Kijiji ambacho kinaitwa Matembwe Kijini, kuna Kijiji ambacho kinaitwa Juakuu. Fedha zimetengwa nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ikolojia, lakini cha kuchangaza mpaka leo hii zaidi ya miaka mitano miradi ile bado haijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tulienda na Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, kuna baadhi ya vifaa vimenunuliwa, kuna ununuzi wa boti, boti limenunuliwa zaidi ya Milioni 46. Ni jambo la kustaajabisha na la kushangaza kabisa, boti moja limenunuliwa zaidi ya Milioni 46 haiwezekani hata siku moja, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tathmini ya sisi ambao tayari tumezaliwa kandokando ya bahari, lakini pia ni wavuvi, boti moja linanunuliwa zaidi ya Milioni 12 siyo Milioni 46. Naiomba sana Wizara yako, Wizara ya Muungano kuhakikisha kwamba, kwenye matumizi ya fedha lazima tuende tukaangalie vizuri. Fedha zinapotea kwa upande wa Zanzibar, lazima tukae tuhakikishe kwamba, fedha zinaenda kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia jambo la pili, kuna ujenzi wa majiko sanifu, jiko moja limejengwa zaidi ya shilingi Laki Saba kwa gharama ya kawaida. Kiuhalisia ukiliangalia jiko moja ni sawasawa na Shilingi Laki Mbili. Upotevu wa fedha ni mkubwa sana, fedha ambazo zinaenda Zanzibar hakuna usimamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Wizara yako Mheshimiwa Waziri, kwenye fedha ambazo zinaenda Zanzibar za Muungano, zinapoenda Zanzibar Wizara yako ihakikishe ndiyo inasimamia ile fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefika Zanzibar tumewahoji watu wa Wizara ambao wanashughulika na masuala ya miradi hii hawana majibu. Tunajiuliza nani msimamizi wa fedha hizi ambazo zinakuja Zanzibar? Majibu hakuna kuhusiana na fedha ambazo zinaenda Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa vile muda ni mdogo naomba niishie hapo. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana na mimi kunipa fursa hii ya kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuimarisha biashara zetu ndani ya nchi, pia niwapongeze sana Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Katibu Mkuu kwa uandaaji mzuri wa taarifa hii na kuwasilisha hapa leo Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki nizungumze sana lakini zaidi nataka nijikite kwenye zao kuu la mwani. Zao kuu la mwani ni zao la kibiashara ambalo sisi kama Taifa tunategemea soko kubwa sana kupitia wenzetu wa Zanzibar pia kupeleka nje ya nchi zao hili la mwani. Pia kuna asilimia kadhaa ambayo tayari inabakia hapa kama malighafi kwa ajili ya utengenezaji na uchakataji wa sabuni, viyoyozi, cosmetic product pamoja na masuala ya kula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la mwani ni kama mazao mengine kwa mfano karafuu zao la korosho, ufuta na mazao mengine tofauti tofauti lakini ni jambo la kushangaza kuona kwamba zao la mwani halijapewa kipaumbele Zaidi. Naweza nikasema kwamba zao hili linaonekana kama labda wakulima wa mwani ni watu ambao wako kwenye hali duni ya kipato chao ambacho wanachokiendesha kwa ajili ya kulivuna zao hili la mwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba zao hili la mwani kupitia Wizara hii bado halijapewa kipaumbele zaidi mbali na jitihada kubwa ambazo zinazofanywa kupitia na wenzetu wa TANTRADE lakini pia kuna wenzetu wa TIRDO wamefanya intervention kubwa na hivi juzi tu mwezi wa tatu tulienda pale TIRDO Dar es salaam, tukaona kuna sample zaidi ya 99 wamezichukuwa kwa ajili kufanyia utafiti, lengo hasa na madhumuni ni kuona kwamba hili zao la mwani linakuwa na soko lakini pia lina toa product ambazo tayari zitatumika ndani ya nchi lakini pia zitatumika ndani ya nchi lakini pia zitatumika nje ya nchi, hivyo nawapongeza sana TIRDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hilo pia niwapongeze sana TIRDO na kuwapa salamu za akina Mama kule Kisiwani Pemba kwa kuwajengea majokofu kwa kiingereza tunaita seaweed dryer majokofu ambayo especial kwa ajili ya ukaushiaji wa ule mwani ili mwani ukishakaushwa ukitoka pale utatoka mzuri lakini hautakuwa na vimelea vyovyote ambavyo vinaweza vikaathiri kwa hiyo niwapongeze sana ndugu zangu wa TIRDO kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze sana ndugu zangu wa TANTRADE kwa kuona kwamba kuna umuhimu mkubwa sana ndugu zetu hawa akina Mama ambao ndiyo asilimia 90 wanajishuhulisha na zao hili la mwani wanawapatia fedha pia wanawapa elimu. Wamefanya kazi kubwa ingawa bajeti yao tunafahamu ni ndogo lakini wanafanya kazi kubwa mno kwa ajili ya kuwasaidia hawa akina Mama, ndiyo maana leo hii ukipita kwenye maonyesho ya Biashara kama utaenda Zanzibar ama utakuja Tanzania Bara bidhaa ambazo zinaonekana kushamiri kwa wingi kwenye maonyesho ya biashara ni bidhaa ambazo zinatokana na hizi za mwani, hivyo ninawapongeza sana ndugu zangu wa TIRDO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji nguvu kazi kubwa kwa ajili ya kulinusuru zao hili la mwani. Zao hili la mwani tukilisafirisha nje tunaingiza pesa nyingi za kigeni na tukizibakisha hapa tunaingiza fedha nyingi za Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia zao hili la mwani limetengeneza fursa za ajira hususani kwa kinamama ambao wako kando kando ya bahari, tunayo mikoa i zaidi ya minne kwa Tanzania Bara, lakini kwa Zanzibar kuna mikoa mingi sana ambayo tayari inashamiri kwenye zao hili la mwani, lakini jitihada za Serikali bado zinaonekana ndogo kwa ajili ya kutafuta masoko. Zao hili la mwani miaka ya nyuma lilikuwa na thamani kubwa, katika matajiri ambao tayari utakaowazungumza kando kando ya bahari, basi ni wakulima wa mwani, lakini sasa hivi zao letu hili la mwani limedharaulika, limedharaulika kupita maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara iliangalie tena zao hili la mwani. Zao hili la mwani linanusuru asilimia 90 akinamama ambao tayari wako kando kando za bahari, hawana shughuli nyingine yoyote ya kufanya isipokuwa kulima zao hili la mwani. Kama Serikali kuna umuhimu mkubwa sana tukakaa kwa pamoja kuangalia masoko ya nje na ya ndani ili mradi zao hili la mwani kuliongezea thamani ili akinamama wale wasikate tamaa na kuweza kumudu familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kupitia zao hili la mwani ili sasa lizidi kupata soko, pia tuweze kupata fedha za kigeni. Jambo la kwanza; tuna makampuni machache ambayo tayari yananunua mwani. Kwa hiyo, Serikali lazima tuangalie makampuni haya kunaonekana kuna urasimu wa hali ya juu, wanajipangia bei wanayoitaka wao wenyewe, hali ya kuwa kwamba ukiangalia kwenye soko la kidunia mwani una value kubwa lakini pia una fedha ndefu, lakini makampuni ambayo tayari yamepata accreditation kwa ajili ya kununua huu mwani ni makampuni machache. Hivyo naiomba sana Serikali iangalie namna ya kuruhusu makampuni mengine yote duniani yaje kununua mwani Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakinunua mwani hapa nchini kwetu naamini kwa asilimia 100 mwani utapanda bei na wananchi wetu ambao tayari wako hali duni za kiuchumi, basi wanaweza wakauza huu mwani kwa bei iliyokuwa ni nzuri. Kwa sasa hivi makampuni mawili kununua mwani, ni sawasawa na kufanya biashara ya monopoly, si sahihi kwa nchi yetu ya Tanzania wakati value of money ni kubwa, lakini mwani unanunuliwa kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niwaombe sana ndugu zetu wa TANTRADE tunao ma-expert, tunao wataalam, tuwatumie hawa kwa ajili ya kushuka chini kwa wakulima wetu kwenda kuwapa elimu namna gani ya kuchakata huu mwani ilimradi kwamba tupate bidhaa bidhaa ambazo tayari tutaziuza kwa thamani iliyokuwa nzuri ili mradi kwamba sasa wakulima wetu waweze kuuza huu mwani, wapate fedha na kuendesha familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; elimu ya ujasiriamali ya hali ya juu nayo pia itolewe, bado wakulima wetu elimu yao ni ndogo sana kwa ajili ya uchakataji wa huu wa mwani ili mradi kutoa bidhaa ambayo tayari itakayouzika. Kwa hiyo naomba sana watumie taaluma ya hali ya juu, watafute watu wa marketing, kisha warudi kwa wakulima wetu, bidhaa ambazo tayari wanazizalisha kule mitaani, basi wazifanyie marketing, wazi brand. Pia zipate national identity, zijulikane hizi bidhaa zinatoka nchini Tanzania. Tukifanya hivyo zao letu hili la mwani litapata value kama mazao mengine kama vile yalivyo mazao ya korosho, karafuu na mazao mengine yaliyokuwepo duniani.

Mhehimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, kuna mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umejikita zaidi kwa mazao haya ya biashara. Zao la mwani pia ni zao la biashara, hivyo naomba sana mfumo wa stakabadhi ghalani nao utumike kwa ajili ya kununua mwani, lakini mwani ukishanunuliwa, lazima uwekwe stoo ili mradi wanunuaji lazima waje kununua mwani kwenye stakabadhi ghalani. Tukifanya hivyo, naamini kwa asilimia 100 zao hili la mwani litakuwa kubwa, lakini pia wakulima wetu watashukuru sana kupitia haya mambo ambayo tumeyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana na naunga mkono.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa ya kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Uvuvi na Mifugo.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa hotuba yao hii ambayo moja kwa moja imeenda kutafsiri maono pamoja na mawazo ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan namna ambavyo anataka Taifa letu liendelee kiuchumi, kimaendeleo na mambo mengine zaidi.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama samia Suluhu Hassan kwa kweli Mama anafanya kazi kubwa mno, anajitahidi sana kufanya kila means kutengeneza diplomasia ndani ya nchi ili kuhakikisha Taifa linasonga mbele kwa maendeleo zaidi. Pia kupitia Wizara hii nitakuwa nina dhambi kubwa nisipompongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hususan kwenye Wizara kama hii kwa kule Zanzibar tunaita Wizara ya Uchumi wa Bluu, kwa kweli Mheshimiwa Rais ameonesha wazi namna ya kutaka kuifumua Zanzibar kwenye uchumi, hususani ambao utaenda kwenye masuala ya uvuvi kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na nimtie moyo aendelee kuchapa kazi na Watanzania tunaona kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa iliyowasilishwa hapa takribani zaidi ya miaka Kenda tunaposimama hapa kwenye Bunge tunakuwa tunashauri, hususani Wabunge ambao tunatokea upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna ya kitoweo ambacho kinaitwa nyama. Nyama ya ng’ombe kwa upande wa Zanzibar ni very expensive ukilinganisha na huku Bara, ingawa nyama ya ng’ombe kwa asilimia 100 kwa upande wa Zanzibar tunategemea soko kubwa kutokea huku Bara, lakini kuna tozo lukuki ambazo bado Wizara haijataka kusema kwamba sasa kwa vile sisi ni nchi mbili, tunawaachia wenzetu kwenye suala la kodi hizi nyingine ndogondogo ambazo zinatuumiza kwa upande wa pili wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, huwezi kuamini sasa hivi bei ya nyama ukilinganisha Bara na Zanzibar ni tofauti sana. Upande wa Bara nyama inanunuliwa kwa kilo moja shilingi 6,000 hadi shilingi 7,000 lakini upande wa pili wa Zanzibar nyama kilo moja sasa hivi unanunua shilingi 13,000 na kuendelea, hii yote inasababishwa kwamba bado Wizara haijaamua kabisa kusamehe baadhi ya tozo.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nizitaje baadhi ta tozo ambazo zimekuwa kichefuchefu kwa uapande wa pili wa Zanzibar na inapekea bei ya nyama kuwa nzito kwa upande wa pili wa Zanzibar. Mfano mzuri bei ya nyama, ng’ombe anapotoka Bara kumpeleka Zanzibar kuna tozo ambazo zinachajiwa, ipo tozo ambayo Wizara ya Mifugo inatoza ng’ombe ambaye anaenda Zanzibar, ambayo hii tunaweza pia tukaisamehe kama Wizara ili Zanzibar aweze kununua kilo ya nyama kwa bei nafuu, hii nayo iangaliwe Mheshimiwa Waziri ikiwezekana ifutwe kabisa na isamehewe, sote ni nchi moja, sote tunafanya kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, ipo tozo ya Halmashauri nayo pia inachajiwa, yule ng’ombe ambaye anapelekwa Zanzibar lazima achajiwe tozo ile ambayo inatoka huku Bara, Halmashauri ya Tanzania Bara. Pia ipo tozo ya Kijiji ambayo inachajiwa kwa ng’ombe yuleyule ambaye anaenda Zanzibar. Pia ipo tozo ambayo inachajiwa na wenzetu wa TRA yule ng’ombe mmoja ambaye anaenda Zanzibar. Tozo ya TPA watu wa bandari nao pia wanamchaji ng’ombe yule anayeenda Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, pia ipo tozo ambayo inaitwa export levy ambayo hii hata mtu wa Kenya akija kununua ng’ombe Tanzania anampeleka Kenya hii anachajiwa ambayo inaitwa export levy, na Mzanzibar hivyo akinunua ng’ombe huku Bara kumpeleka Zanzibar na wao pia inachajiwa. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, ili kulinusuru soko la Zanzibar pia kuwanusuru Watanzania wa Zanzibar tuziangalie hizi tozo na ikiwezekana mkae Wizara zote mbili ili kuweza kuzifuta hizi tozo na bei ya nyama ikawa rafiki kama ya Zanzibar na bei ya Bara zote zikawa sawa. Tukifanya hivi tutakuwa tayari tumewapunguzia wenzetu kule wa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naliomba sana hili jambo kupitia Wizara yako Waziri Mheshimiwa Abdallah Ulega, naamini ni kijana una uwezo mkubwa wa kuweza kufanya lobbying ya kuzungumza na baadhi ya taasisi nyingine hizi ambazo zinashirikiana na wewe kwa ajili ya kufuta kabisa hizi tozo.

Mheshimiwa Spika, niende upande wa pili wa uvuvi. Imekuwa kila mwaka kipindi cha bajeti nalizungumzia suala la zao la mwani, mara hii kwenye bajeti yako Mheshimiwa Waziri umelizungumza zaidi ya mara tatu suala la mwani, lakini kuna taarifa imewasilishwa na Kamati ya Viwanda Biashara na Mazingira ambayo inashughulika na suala hili pia imezungumzia zaidi ya mara nne. Suala la mwani bado hatujaona mpango mkakati, bado mmezungumzia suala la elimu, kutoa vifaa, sijui kuwezesha wakulima wa mwani, lakini ninachotaka kuwaambia mwani hasa changamoto yake ni soko siyo issue ya kuzalisha. Wakulima wetu bado hawajakatishwa tamaa, zao hili takribani zaidi ya miaka 20, 30 linalimwa na wakulima bado hawajakata tamaa, bado hali zao ni duni bado najua hawakopesheki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali bado hamjaandaa mpango mkakati wa kulisaidia hili zao la mwani. Leo wakulima wengi wa mwani wanalalamika suala la bei, bado Serikali haijawa wazi kabisa, haijawa na mpango wa kuwasaidia wakulima kuweza kupata soko rafiki na ikapatikana bei nzuri ya mwani ili mkulima aweze kufurahia zao lake la mwani. Mfano mzuri, Mheshimiwa Waziri tunalo zao la korosho, kuna parachichi, kuna mazao mbalimbali yote tumeona Serikali imeweka mpango mkakati na mazao haya yote yanauzika huko nje na wakulima wanafurahia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini zao la mwani bado hatujaona kabisa Serikali kulizungumzia hili, hasa kuwatafutia soko la mwani? Kwa hiyo, nawaombeni sana, Mheshimiwa Waziri unaufahamu mwani, unawafahamu wajasiliamali wa mwani sasa hivi wanavyopata shida, lakini suala la soko bado. Tuliangalieni, karibisheni wawekezaji wakubwa waje kuwekeza hapa nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naiomba sana Wizara kwa ushauri tengenezeni Bodi ambayo itakuwa inashughulika na masuala ya mwani tu kwenye suala la bei, kwenye suala la upandaji, kwenye suala la dawa na masuala mengine mbalimbali itasaidia sana na naamini kwa kipindi kifupi zao la mwani litapata value kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nakuona umeshabonyeza kengele yako, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii na mimi kuweza kusimama kwenye Bunge lako pia kuchangia kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Ninamshukuru sana pamoja na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa taarifa yako hii iliyopo mezani pamoja na Naibu wako Waziri. Pia niwapongeze sana Watendaji wako wa Wizara kwa uandaaji mzuri na kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya ya kuifanya Wizara hii iwe Wizara nzuri ambayo inachangia Pato kubwa la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo lakini pia nitakuwa nimefanya makosa makubwa sana nisipompongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya hususan kwenye Wizara hii. Hatujawahi kuona tokea dunia iumbwe Rais kufanya kazi kubwa mno kwa kipindi kifupi hususan kwenye Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa kweli Mheshimiwa Rais anahitaji pongezi kubwa mno na anahitaji kila pongezi, kila namna kwa namna ambavyo Rais alivyojitoa muhanga kuitangaza nchi yetu Kimataifa lakini ndani ya nchi kwenye Wizara hii ya Utalii.

Mheshimiwa Spika, leo tumeona wimbi kubwa la wageni ambao wanatoka nje, international kuja nchini kwetu Tanzania. Miaka ya nyuma tumeshuhudia kipindi kama hichi mwezi wa tatu mpaka mwezi wa sita ni kipindi cha low season lakini leo hii tunaona ndege nyingi sana ambazo zinatua ndani ya nchi kana kwamba ni kipindi cha high season. Kwa kweli anastahiki kila pongezi Mheshimiwa Rais. Ameifanya low season sasa hivi kuwa high season. Ni season nzuri tuna wageni wengi sana sasa hivi nchini kwetu namna ambavyo tayari wanavyokuja, namna ambavyo mama alivyoitangaza nchi, namna ambavyo wageni ambavyo wanavyoingia ndani ya nchi kwa ajili ya kuja kutembelea ndani ya nchi lakini pia kujifunza mambo mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi nitajikita zaidi kwenye utalii wa fukwe. Ingawa nchini kwetu tuna fukwe nyingi lakini bado hatujazitumia vile ambavyo inatakiwa ukilinganisha na nchi nyingine. Utalii wa fukwe sasa hivi duniani ndiyo utalii ambao unatembelewa na wageni wengi nchini duniani. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara lazima tuweke mikakati madhubuti ili kuinua Wizara hii kwenye Sekta hii ya Utalii wa Fukwe. Mfano mzuri nilipoangalia kwenye mtandao wa BBC hivi karibuni wametoa taarifa yao 31 Machi, 2023, watalii wengi ambao wametembelea duniani ni watalii ambao wameenda kwenye fukwe ukilinganisha na maeneo mengine yoyote yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri nchi ya kwanza ambayo inaongoza kuwa na wageni wengi lakini wote wameenda kwenye fukwe ni nchi ya Brazil kwenye eneo la beach ambalo linaitwa Santos lakini pia nchi ya pili ambayo imeongoza pia kuwa na watalii wengi wameenda kutembelea kwenye fukwe ni Accra lakini pia kuna nchi ya Australia lakini kwenye tathmini yote overall Marekani ndiyo inaongoza kutembelewa na wageni wengi kwenye eneo la beach. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni wazi sasa lazima tuweke mipango mikakati ili kuhakikisha sasa tunakuwa na utalii wa fukwe. Kwenye nchi zaidi ya 30 zilizotajwa kwenye ripoti ya BBC Zanzibar imetajwa kweye eneo la Nungwi na eneo la Nungwi ni eneo ambalo limeshamiri kwenye utalii wa fukwe. Ni fursa pekee sasa hivi lazima tuwekeze huko kwenye eneo la fukwe. Watalii wengi duniani ndiyo wanakuja kwenye eneo la fukwe ukilinganisha na maeneo mengine, yote ni mazuri hayo, yote ni mazuri lakini kwenye fukwe zaidi ndiyo wanapendelea zaidi, wanapendelea zaidi ku-pleasure, kustarehe, kutembelea beach, kuota jua na mambo mengine hali kadhalika ukilinganisha na maeneo hayo ya wanyamapori pamoja na milima. Kwa hiyo, naiomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingawa huku kwa upande wa bara ardhi upande wa beach kwenye fukwe wameachiwa wenzetu wa Halmashauri na Serikali za Mitaa. Naiomba sana Wizara mtumie technique yoyote ile ili kuhakikisha sasa Wizara ndiyo inahodhi maeneo yale na hii Halmashauri pamoja na Serikali za Mitaa mnaweza mkatengeneza sheria na utaratibu mzuri ili ziweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Wizara ikitengeneza Tume kwa ajili ya kuchukua maeneo ya beach na kuyaendesha basi tuhakikishe kwamba tunaweka sheria na kanuni za Corporate Social Responsibility (CSR) ili vijiji ambavyo vitatoa ardhi yao kwa matumaini kwamba watahisi Serikali itaweza kuwasaidia basi mahoteli yale au wawekezaji hao wawe wanakumbuka kutoa gawio la faida kwa vijiji ambavyo vipo karibu, vitapata faida ya kujengewa mahospitali, vitapata faida za kujengewa mashule lakini pia vitapata faida vya kujengewa transportation. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niwapongeze sana baada ya kuzindua hiyo filamu yetu lakini pia tuna tv yetu inaitwa Safari ambayo hiyo inamilikiwa na Maliasili, kwa hiyo niwapongeze sana kwa hiyo, lakini pia niwaambie kitu kimoja, mbali na tv sasa hivi mambo yetu haya yamehamia kwenye mitandao ya kijamii sasa hivi, tunao vijana wetu ambao wanatangaza sana kwenye utalii na ninaamini tukiwatumia vizuri nina uhakika tunaweza tukaongeza mara dufu watalii kupitia nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao vijana wetu naomba uniruhusu niwataje, yupo kijana ambaye anaitwa Yasini Jamal ni kijana ambaye ukifungua kwenye mitandao ya kijamii ana followers wengi na anauwezo mkubwa sana wa kuitangaza Tanzania kwenye issue ya kiutalii. Pia tunaye kijana wetu anaitwa Ally Jape ni vijana ambao wote wana uwezo mzuri wa kuutangaza utalii. Kwa nini tusiwachukue vijana hawa tukawafanya kama mabalozi wa kuweza kuutangaza utalii wetu ndani ya nchi? Ninaamini tukiwapa fursa hawa vijana wataitangaza sana nchi yetu kwenye sekta ya kiutalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo sasa niende kwenye eneo la pili. Watalii wengi nao wanaokuja ndani ya nchi wanavutiwa na vyakula. Kwenye eneo la vyakula bado hatujaweka mikakati madhubuti ili watalii wengi wanaokuja nchini basi wa-recognize kwenye issue ya chakula. Mfano mzuri tuna nchi nyingi sana kama India, watalii wengi wanaoenda India wanafuatilia masuala ya chakula. Ukienda Japan watalii wengi nao wanaenda Japan kwa ajili ya kufuata taste ya chakula lakini pia kwa upande wa Zanzibar, watalii wengi wanaenda Zanzibar na wao pia mbali na beach lakini pia wanafuatilia masuala ya chakula. Kwa hiyo naamini tukiweka hasa utalii wa chakula tutafanikiwa kwa asilimia 100 na ndiyo fursa yenyewe pekee hiyo tunaweza tukaitengeneza watalii wakaja wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri leo hii Zanzibar kuna tamasha ambalo linaendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja anaitwa Ayoub Mahmud. Huyu anastahiki pongezi za hali ya juu, tarehe 25 Juni, kuna tamasha Zanzibar linaitwa Zanzibar Seafood Festival. Tunaanza na tamasha mwisho wa siku matamasha kama haya yanakuwa ni sehemu ya kichocheo cha kuvutia wageni wengi nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo nchi nyingi sana zimefanikiwa kwenye matamasha haya ya kiuchumi kwenye suala hili la vyakula. Kwa hiyo nawaomba sana, naiomba sana Wizara tuangalie kwenye suala la chakula. Leo hii kuna ma-chef wengi Afrika Mashariki wamekutana walikuja kushangaa Tanzania tunapika ndizi kwa nyama ambayo duniani kote hakuna. Tukilifanya hili jambo kama ni fursa ya kiutalii tumetengeneza uchumi wetu, tumetengeneza ajira kwa vijana wetu, pia kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache ninakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii na ninaunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na mimi kunipatia fursa hii ya kuweza kusimama na kuweza kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kwanza nikupongeze sana kwa umalidadi wako wa kusimama kwenye kiti, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu kwa kazi nzuri ambayo wanayoifanya lakini pia kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hususan kwenye filamu ambayo tayari ameizundua hivi karibuni ya Royal Tour ambayo imetuletea matokeo makubwa sana ambayo na faida kubwa sana kutuletea wageni katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo sisi ambao tayari tunatokea upande wa pili wa Zanzibar jana napiga simu naambiwa kuna wimbi kubwa na wageni ambao wanaingia Zanzibar, kumbe faida kubwa ambayo inapatikana kupitia Royal Tour haipo tu kwa Tanzania Bara bali ipo mpaka Zanzibar, kwa kweli tunampongeza sana mama. Hii imetengeneza fursa kubwa sana vijana wetu kule ambao tunaita beach boy pamoja na waongozaji wa kitalii kufurahia matunda ya nchi yao, lakini pia matunda haya yanatokana na mama yao Mama Samia Suluhu Hassan, kwa hilo nampongeza sana Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbali na hilo sasa nijikite kwenye mchango wangu, mbali na sekta hii ya kiutalii ambayo ina umuhimu mkubwa sana kukuza uchumi wetu na maendeleo ya wananchi wetu moja kwa moja, lakini yapo maeneo ambayo bado hatujaangalia kiujumla. Ingawa Tanzania tumebarikiwa katika maeneo yasiyopungua zaidi ya saba ambayo ndio tumejikita zaidi kuleta watalii nchi kwetu likiwemo eneo la hifadhi ya wanyamapori, lakini kuna eneo la maporomoko ya maji, kuna eneo la milima, kuna maeneo ya misitu, mazingira na maliasili, kuna utamaduni, utalii wa mali ya kale, lakini pia kuna utalii wa fukwe. (Makofi)

Mimi nataka niishauri zaidi Wizara hii mbali na kuangalia na wanyamapori lakini kwenye eneo la fukwe bado hatujawekeza zaidi. Tathmini inaonesha nchini kwetu Tanzania tuna hekari zisizopungua 1,428 kandokando ya bahari pamoja na maziwa makuu, lakini bado hatujaangalia kwenye eneo hilo. Ukweli usiopingika watalii wengi ambao tayari wanakuja kutembelea nchini kwetu Tanzania pamoja na Afrika kiujumla wanapendelea zaidi kuangalia katika maeneo ya fukwe. Leo hii mgeni anapata likizo kwenye mwaka wa miezi 12 anapata likizo ya mwezi mmoja mtalii yule ukimuuliza anakwambia maeneo ambayo nitapendelea zaidi kwenda kutembelea ni eneo la fukwe na eneo la hifadhi ya wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo hayo tunafanya vizuri hususani kwenye eneo la wanyamapori, lakini kwenye eneo la fukwe hasa bado hatujawekeza zaidi. Rai yangu kwa Serikali tuangalie namna gani tunaweka mpango mkakati either wa muda wa miaka mitano, either miaka kumi kwenye eneo hili la fukwe tunawekeza zaidi, inawezekana eneo la fukwe maeneo yale yanaonekana very expensive kwa wawekezaji kununua, lakini ninaishauri Serikali tuanzishe mfumo wa PPP (Private Public Partnership) hiii itatusaidia sana kama Serikali, akija mwekezaji kama Serikali inatoa asilimia 50 na asilimia 50 anatoa mwekezaji. Hii itasaidia kujenga mahotel makubwa pembezoni mwa fukwe, lakini sio fukwe tu za bahari tunayo maziwa makuu, mito na maeneo mengine mbalimbali hii itavutia sana kuleta wawekezaji na ndiyo tathmini ambayo inaonesha duniani kote huko watalii wengi ambao wanakuja wanaangali huko katika maeneo ya fukwe. Kwa hiyo, naamni tukifanya hivyo vizuri zaidi tunaenda kuongeza idadi kubwa sana ya watalii katika nchi yetu kila mwaka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbali na hilo pia kuna eneo lingine ambalo kwenye suala la chakula bado hatujawekeza vizuri zaidi. Watalii wengi ambao tayari wanakuja nchini tunawalazimisha kuwalisha vyakula ambavyo havieleweki. Lakini miongoni mwa vitu ambavyo watalii wengi wanaokuja nchini kwetu wanavutiwa na chakula wengi wao na ndiyo maana ukifanya tathmini watalii wengi, mtalii akija mwaka huu mwakani ni nadra sana kurudi. Lakini bado hatujaangalia maeneo gani ambayo tayari tunaweza tukamvutia ili aweze kurudi miaka na miaka ni eneo la chakula tu peke yake. Na ndiyo maana ukiangalia kule kwetu Zanzibar kuna eneo la Forodhani ambalo ni eneo ambalo limeshamiri kwenye vyakula tunaita local food ambavyo vinatokana na bahari. Lakini bado hatujaangalia kwenye eneo hilo.

Kwa hiyo, mimi rai yangu nashauri kwamba tuanzishe hata matamatasha kila mwaka kwenye eneo la uwekezaji kwa mfano kama Dar es Salaam, Arusha, kwenye maeneo yote ambapo watalii wanakuja kwa wingi tuwawekee chakula. Chakula ni taste pekee ambayo inamvuta mtalii kuja nchini na kurudi mara kwa mara tofauti na wanyamapori na fukwe. Kwenye wanyamapori anaweza akaja mwaka mmoja, lakini mwakani akasema hakuna kitu kingine chochote, tembo walewale, simba walewale. Lakini kwenye chakula, tukiweka sasa chakula kizuri zaidi, tukiwawekea vyakula ambavyo tayari tumevifanyia taste zote naamini watalii wale watarudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri tuaangalie Mother Africa hapa tunayo nchi yetu ya South Africa wanalo zao la zabibu kwenye utalii sisi Tanzania tuko vizuri zaidi kuliko hata wao. Lakini wanalo zao la zabibu, zabibu ile ina zaidi ya vinywaji sita, saba na kuendelea. Lakini wao wamefanya kama ni tamasha kwa wao, kwa mwaka wanafanya matamasha zaidi ya 30 katika nchi yao na watalii wanakuja kwa ajili ya ku-taste ule mvinyo na ku-taste kwao inakuwa ni free zaidi. Hata mzungu akienda kwao basi ile taste ya mvinyo aliyoipata South Africa mwaka jana anaipata tena na watalii wengi wanarudi Afrika ya Kusini kwa ajili ya mvinyo.

Kwa hiyo, sisi kama Tanzania bado hatujawekeza tunayo naturally, ardhi yetu ni nzuri, hali ya hewa nzuri na matunda pia ambayo tayari tunayozalisha ni mazuri naya na taste nzuri, huwezi kuyapata dunia yoyote ile. Kwa hiyo, bado hatujaangalia kwenye eneo hilo. Kwa hiyo sisi tuangalieni sisi kama Serikali. Tumsaidieni mama, mama ameonesha rai kubwa, lakini mama ameonesha nguvu kubwa kwenye sekta hii ya kiutalii haijawahi kutokea duniani, Rais kama mama amefanya kazi kubwa sana kwenye hii kwa ajili ya kuitangaza Tanzania. Kwa hiyo, lazima tuweke mipango mikakati kuweka mazingira mazuri watalii wakaanza kuja nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia kwenye Muswada huu wa Sheria wa Finance.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu sasa hivi tuko kwenye harakati za kurudi majimboni. Mimi kama Mbunge ambaye natokea Zanzibar kwenye Jimbo la Chaani naamini kwamba kutakuwa kuna maswali kwa wapiga kura wangu, lakini sio tu kwa wapiga kura wangu hata wafanyabiashara au watu ambao wataguswa na Muswada huu wanaweza wakauliza. Zanzibar ni ndogo, kwa hiyo, naamini kufikika kwangu ni rahisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye Muswada huu kwenye Amendment ya Value Added Taxes, Cap. 148, amendment ya Section 3, kuna kipengele namba 2, 3 na 4 ambapo tunazungumzia suala la ongezeko la VAT kwa wafanyabiashara kuchukua bidhaa kutoka Tanzania Mainland kwenda Zanzibar na Zanzibar kuja Tanzania Mainland. Sasa hivi kuna mapendekezo mapya ya sheria kwa mfanyabiashara kutoka Zanzibar akichukua product Bara kupeleka Zanzibar au wa Zanzibar akichukua product kuleta Bara atatozwa asilimia 18, naona hatujaenda in deep zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Zanzibar ipo sheria ambayo inatambua mfanyabiashara akitoa bidhaa aidha import au consumption anatozwa asilimia 15 kule Zanzibar. Hata juzi tu Baraza la Wawakilishi limemaliza sijaona Muswada huu wa Sheria na leo hii Muswada wa Sheria umekuja huku, sijajua mantiki ya hii itakuwaje. Maana Zanzibar ukichukua bidhaa kule ukisema utokenayo unatozwa asilimia 15, Bara tunaambiwa asilimia 18, sasa akitokea mtu ambaye anasafirisha bidhaa anatozwa asilimia 18, sijui sheria ipi kwa kule kwetu Zanzibar itakuwa inamruhusu kwamba ZRB au TRA atamkata huyo mfanyabiashara asilimia 18 kwa sheria ipi? Maana ni kwamba tunawaongezea Mamlaka ya Mapato ya Zanzibar asilimia tatu ya ziada.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi juu ya suala hili ili tuondoe mkanganyiko na zisije zikaibuka changamoto za kusema kwamba Muungano huu una shida ingawa Muungano wetu ni mzuri na Mama ameonesha nia njema kabisa ya kuimarisha Muungano huu ambao unatupa fursa sisi kama Watanzania kutembeleana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, Zanzibar kuna Bodi ambayo inashughulika na masuala ya kukagua bidhaa ambayo tunaita ZBS na huku Bara kuna mamlaka nyingine ambayo inaitwa TBS. Kuna changamoto nyingi ambazo zimeshajitokeza, kuna bidhaa ambayo inazalishwa kule Zanzibar inapewa logo ya ZBS (Zanzibar Bureau of Standards) na huku Bara ipo. Kwa hiyo, nina wasiwasi inawezekana kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa interested kuja Zanzibar kuchukua bidhaa lakini mwisho wa siku wakaja kukutana na kikwazo hiki cha Shirika la Viwango. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nahitaji pia maelezo kidogo ili mradi tuondoe huu mkanganyiko baina ya nchi zetu mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, kwenye kipengele namba 4 tunaambiwa fedha zitakazopatikana zitaenda moja kwa moja kwenye Hazina ya Zanzibar; zitakazopatikana huku Bara kwa wale wafanyabiashara ambao watatozwa hiyo asilimia hiyo 18 zitaenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Katika sehemu ambayo wafanyabiashara wengi wanalalamika ni kuhusiana na fedha ambazo zinakwenda Hazina kurejeshwa Zanzibar zinakuwa na changamoto kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara iweke angalau sheria ambayo itaweka wazi na time limit ili kama kuna fedha ambazo zinatakiwa zirejeshwe Zanzibar basi kuwe kuna muda ambao fedha zinatakiwa zirejeshwe, ile returning ya fedha nadhani itakuwa ni jambo zuri Zaidi. Hapa tunaambiwa kwamba fedha ambazo zimepatikana Zanzibar zirejeshwe Bara na za Bara zirejeshwe Zanzibar lakini hakuna muda, inaweza kuja kuibua hoja nayo ikaleta shida kabisa. Kama nilivyotangulia kusema kwamba Muungano huu ni mzuri, utaendelea kuwa mzuri. Mama ameonesha nia njema kabisa, nadhani Tanzania tunaenda kupiga hatua nzuri na uchumi wetu utaimarika vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne, kuna suala linazungumziwa sana kuhusiana na sukari ya Zanzibar, lipo hilo, ingawa VAT hii nayo pia imeenda kugusia zaidi. Itaenda kufungua mwanya wafanyabiashara kule au kile Kiwanda cha Sukari cha Zanzibar nacho kitaweza ku-supply huku Bara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kutokana na tozo hii mpya ya asilimia 18 nina wasiwasi mkubwa sana kwa sababu huyu mfanyabiashara, yule manufacture wa sukari wa Zanzibar akifanya deduction yote ya kutoa gharama za malighafi alizotoa nje kwa ajili ya import, inaweza ikasababisha mfanyabiashara kutoka Bara akiwa interested na kuja kuchukua sukari Zanzibar gharama ya sukari ya Zanzibar inawezekana kuwa kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza tukaja kufungua mianya ya wafanyabiashara sasa waache kununua kwenye soko la Zanzibar au la ndani ya nchi zetu hizi wakaenda kuhamia soko la nje. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara inipe maelezo mazuri, lakini pia mapendekezo nimetoa Wizara iangalie sheria hii ili baadaye isije ikaleta vikwazo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, nashukuru kwa kunipa fursa. (Makofi)