Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maryam Omar Said (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kwanza katika kipindi hiki cha pili cha leo cha kujadili hoja ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, nichukue fursa hii kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa makundi matatu ambayo yalishiriki katika kuhakikisha leo Maryam nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee ziende kwa familia yangu kwa jumla. Pia nikishukuru Chama cha Wananchi CUF kupitia Mwenyekiti wake shupavu, Mheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba kwa kuweza kunisimamisha nikawa mgombe katika Jimbo la Pandani kule Pemba. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa wananchi wangu wa Jimbo la Pandani kwa kunipa ushindi wa asilimia
56.6 ambazo zimenifanya leo hii nasimama kifua mbele ndani ya Jimbo huku nikijidai kuwa ni mwanamke pekee katika majimbo 18 ya Pemba niliyepata nafasi ya jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo, naomba nichangie hoja ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikisimama zaidi katika miundombinu ya viwanja vya ndege pamoja na bandari kwa upande wa Pemba. Nilifurahi sana pale Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliposema atashirikiana na Rais wetu wa Zanzibar bega kwa bega katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Naamini tumepata majembe mawili, tunamuamini Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa sababu amelelewa na Rais wetu ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaamini yale yaliyoko Tanzania Bara basi na Tanzania Visiwani yatafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa kumtaka Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aongeze kasi zaidi katika kushirikiana na Rais wetu wa Zanzibar katika suala la miundombinu hususan viwanja vya ndege pamoja na bandari, Wapemba wanalalamika, wananung’unika. Tufahamu kwamba Pemba imo katika sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini tupo nyuma. Leo hii nikitaka kusafiri nikiwa Pemba basi nianze kuweka booking ya ticket ya ndege siku mbili kabla nikikosa hapo ndege ya asubuhi ama jioni naikosa. Wapemba wanaomba pia ndege ya Air Tanzania kama jina lilivyo Air Tanzania kiwanja cha ndege kiboreshwe na iweze kufika Pemba pia, wana ndoto, wanaota kila siku ndege ya Air Tanzania ipo Pemba lakini bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa bandari tumechoka wananchi wa Pemba kutumia saa kumi na mbili tukiwa ndani ya Bahari tu tunaitafuta Unguja. Tunahitaji tuboreshewe miundombinu ya bahari kwa kupata boti za kisasa kwa hali yoyote ile kama ambavyo Unguja na Bara ama Unguja na Dar es Salaam inaunganishwa kwa saa kadhaa tu unatoka Unguja unafika Dar es Salaam. Ni ndoto zetu na sisi Wapemba, tunataka tutumie saa chache kutoka Pemba kuja Unguja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais tunakuamini, ni jemedari mzuri, unaweza kuleta maendeleo kwa kiasi fulani lakini tunaomba umshauri vizuri Rais wetu wa Zanzibar hususan atuangalie kwa jicho la hurumu Pemba kwa miundombinu ya usafiri. Wapemba bado tuko nyuma, wananchi wanalalamika na ndiyo maana ukakuta kwamba siasa kali inahamia Pemba, kimaendeleo bado tupo nyuma. Tunahitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu wananchi wa Pemba mbali na mawili, tuangaliwe kwa jicho la tatu, tuko nyuma katika sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na nikaweza kuchangia katika sehemu ya Bajeti ya Wizara ya Muungano na Mazingira. Zaidi nitajikita katika sehemu ya Mazingira lakini nitaenda zaidi katika sehemu ya Mazingira ya nchi kavu. Namshauri kwanza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, tusiangalie tu mazingira ya bahari bali tuende zaidi na mazingira ya nchi kavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye mazingira ya nchi kavu, ni vizuri kwamba tunasema tunashajihisha sana kwamba tupande miti, lakini naomba tushajihishe kupanda miti lakini pia tushajihishe kuitunza miti hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwenyewe binafsi ni mtu ambaye kwamba jimbo langu lipo katika mazingira hatari sana la miti ambayo kwamba ni mashamba ya Serikali. Mashamba haya ya Serikali yenye kilimo cha miti ya mipira, zamani ilikuwa ni mazuri yana faida kubwa kwa wananchi wangu wa Jimbo la Pandani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa imekuwa ni changamoto kubwa sana ndani ya Jimbo langu la Pandani. Yale mashamba zamani yalishughulikiwa vizuri, yakafyekwa vizuri, kiasi ambacho kwamba ulikuwa unauona mti uliopo mwanzo wa kwenye heka mpaka mwisho wa heka. Lakini sasa mashamba yale yamevamiwa na miti ambayo kwamba, si rasmi na kufanya sasa mashamba yale yamegeuka kuwa mapori na kuwa sasa, yanahatarisha maisha ya wananchi wangu ndani ya Jimbo langu la Pandani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitendo vingi vya uhalifu vinafanyika ndani ya mashamba hayo ya Serikali kutokana na mazingira yaliyopo. Tunaona sasa imefika hadi hata mwanafunzi akitoka kwenye Shehia moja kwenda kwenye Shehia nyingine, ambapo kwamba anafuata huduma ya elimu inakuwa ni mtihani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wabakaji hutumia maeneo hayo kwa kutimiza matakwa yao, kitu ambacho kwamba sasa wananchi wangu wanaishi wakiwa roho juu. Namuomba sana Waziri pamoja na Naibu Waziri. Naibu Waziri analijua hili kwasababu, ni mtu ambaye kwamba yupo jirani yangu ndani ya Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, afike katika maeneo yale na aniangalie kwa jicho la huruma, lakini pia ayasimamie mazingira ya Jimbo lile, katika mashamba yale ili kuondoa changamoto zile. Yale ni mashamba ya Serikali leo kama Serikali tunashajihisha kupanda miti, lakini miti yetu wenyewe hatuitunzi, hivi tunafikiria kipi ambacho kwamba kitaendelea hapo baadaye? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hiyo miti inayopandwa inaweza kuja baadaye ikawa changamoto pia kwa wananchi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri hebu tuliangalie hili. Tuangalie mazingira ya bahari lakini pia tuje katika mazingira ya nchi kavu. Katika mashamba haya kumeshawahi kufanyika mauaji makubwa yaliyolitikisa Jimbo na Taifa kwa ujumla. Kijana mdogo tu, aliuliwa ndani ya mazingira haya, mara nyingi sana vinatokea vitendo vya ubakaji ndani ya mazingira haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitaki kuzungumza mengi na sitaki nipoteze muda, niliona kama sikulisema hili hapa sitopata nafasi kulisema pengine na wananchi wataniandama kwa hili. Wataniuliza, ulipata nafasi kwa nini hukulichangia? Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, nakuombeni mfike katika mazingira yangu ya Jimbo na muweze kuniwekea mazingira sahihi kwa mashamba yale. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia bajeti iliyopo Mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniamsha mzima wa afya na kuweza kusimama hapa leo. Pia niipongeze Serikali kwa kuleta bajeti nzuri ila bado ninahofu na wasiwasi mkubwa, kila ninapoisoma bajeti hii nikiangalia na bajeti zilizopita, kiukweli Napatwa na wasi wasi mkubwa mno, kwa sababu ni tayari mara nyingi sana wananchi kubwa wanalolalamikia ni kupitisha bajeti zetu, ikisha baadaye zikatushinda njia tukawa hatufikii kile kiwango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nitachangia katika maeneo mawili makubwa. Niishukuru bajeti hii ama nimshukuru mama yetu Samia, kwa kutufanyia kazi kubwa katika sehemu ya VAT ya Jamhuri wa Muungano ya Tanzania. Kiukweli tulikuwa katika hali mbaya sana kule Zanzibar kiasi ambacho ilifikia hatuwezi kuutaja Muungano kabisa, ilikuwa tukiutaja Muungano kwa mwananchi wa kawaida anavyokuja juu, unashindwa unafikia hadi unanyamaza kimya. Tumefikia hatua nzuri lakini bado, ni wakati muafaka sasa wa kwenda kumaliza zile kero za Muungano zilizobaki hususan kwenye VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazanzibari tunataka tukitoa bidhaa zetu kutoka Zanzibar kuja Tanzania bara basi tusiwe na vikwazo kama vile tunavyotoa Tanzania bara tukapeleka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nije katika sensa. Naishukuru bajeti hii imezungumzia vizuri na imetenga pesa ya bajeti kwa ajili ya sensa. Nitakacho kiomba hapa ama nitakachoshauri hapa, ni Serikali kuzipeleka haraka fedha za bajeti ya sensa ya watu na makaazi kwa sababu, mara nyingi sana tunapokwenda kwenye sensa kutekeleza majukumu ya sensa changamoto moja tunayokutana nayo ni elimu ndogo, inafika hadi siku mdau anakwenda kukamilisha yale mahesabu ya sensa unatakiwa uanze na elimu kwanza, unamkuta mwananchi hakuna elimu yoyote aliyopatiwa juu ya sensa, vinginevyo analiingiza suala la sensa katika masuala ya dini na tamaduni, jambo ambalo haliko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali tujitahidi sana kuzifanyia kazi pesa za bajeti ya sensa zipatikane haraka na elimu ifike kwa usahihi kwa walengwa wahusika zaidi hususan kwa upande wetu wa Zanzibar. Kule kuna changamoto mnajua fika dini ilivyotanda kule Zanzibar, kwa hiyo kila kitu kinaingizwa katika dini, ni wakati muafaka Serikali kutoa elimu kabla ya kwenda kufanya mahesabu ya sensa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo mawili niipongeze tena Serikali kwa kuleta bajeti nzuri hii, nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, nataka uwe mfano Bunge hili la Kumi na Mbili, tukitoka tutoke na kipaumbele kizuri bajeti yetu ifikie kiwango, kile ambacho kwamba tumekipanga. Naamini kabla ya kupitisha hii bajeti ulishazungusa jicho lako Tanzania nzima na ukajua fedha ya bajeti itatokea wapi. Sitaki kwamba nikupe twakimu za kilimo za wizara moja moja hapana, ninachokiomba nataka utuwekee historia ndani ya Bunge hili la Kumi na Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii iende ikakamilike kwa asilimia 100, tukirudi kule majimboni tuwe tunatemebea vifua Mbele kwa ajili ya bajeti hii. Sikupi pongezi nikupongeza niatakaporu Mungu akiniweka hai, baada ya mwaka huu mmoja nikaiona bajeti hii imefikia wapi, hapo nitakuja kuleta pongezi kwa kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kupata nafasi hii niweze kuchangia hoja zilizopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi moja kwa moja nitakwenda kwenye miradi ya maendeleo ambayo bado ni changamoto kubwa kwa miradi yetu kusuasua na kuchukua muda mrefu na kwa upande huo nitakwenda moja kwa moja kwenye miradi ya Muungano ambapo nitazungumzia Mradi wa Mabadiliko ya Tabianchi uliopo Kaskazini A, Unguja.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi ulianza mwaka 2018 na tulitegemea mwaka 2022 mnamo mwezi wa saba tuwe tayari tumekamilisha mradi huu, lakini mpaka sasa huu ni mwezi wa pili tuna miezi mitatu tu mbele tuwe tumemamaliza. Mpaka sasa katika eneo lile kinachoonekana ni nyasi tu, hakuna chochote kinachoendelea, jambo ambalo ni changamoto kubwa, hivi Serikali hebu tujitathmini kwa nini tunakwama? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuseme labda ni wawekezaji wetu, kama hawana uwezo si lazima tumng’ng’anie mtu mmoja, wawekezaji ni bora tutangaze kwa tender kwa watu wengi, halafu tumuangalie ni nani mwenye uwezo kuweza kukiendesha kitu na kikafikia kwa wakati. Hatupati tija, tunawazuia wananchi maeneo kwa maelezo kuwa tunafanyia kitu fulani. Inafikia muda, muda unamalizika; mwananchi alikuwa akilima pale halimi tena anakaa nyumbani, anakufa njaa, hatumlipi mafao yoyote na bado tunakaa na lile eneo hatulitumii kwa kazi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani Serikali ni muda sasa wa kukaa chini tukatafakari tunapokwama na tukaendelea na miradi yetu jamani. Haya mambo ya kila siku miradi yetu kuwa wimbo wa Taifa humu ndani si sahihi. Wimbo wa Taifa ndio kila siku ni ule ule haubadiliki, mpango kila unapopita ukija miradi ni ile ile, mpango mwingine ukija miradi ni ileile, sio sawa, si haki hii, Serikali kaeni chini tutatue tujue kwamba, tukiendesha mradi hata kama ni mmoja sawa. Sekta tunamaliza muda wetu lakini tunajua kitu hiki kimefikia hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitoa mfano, Liganga na Mchuchuma ni mwaka wa ngapi? Toka enzi za mababu zetu, wamekuja wazazi wetu, tumekuja sisi, watakuja watoto wetu bado tunaonesha tu mlima uko pale, faida yake ni ipi kwetu sisi? Wote tuliowazuwia kwamba shughuli zote pale zisiendelee, tumemaanisha nini kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtatukosesha kura zetu tusirudi humu ndani, Mbunge akitoka huko anaahidi kwamba, ndani ya miaka yangu mitano nitahakikisha jambo hili limemalizika, tunamaliza miaka mitano hakuna chochote, tunarudi kwenda kusema nini kwa wananchi? (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tulifikirie hili, tusaidiane ifikie mahali tufanye jambo moja lionekane kwamba tumefanya hiki kuliko kwamba, kila mahali, kila mahali, tunaacha mapengo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye Kiwanda cha Viuadudu; nimesikia hapa taarifa ya Mwenyekiti, ameelezea kiwanda cha viuadudu, lengo kilipoanzishwa kile kiwanda; kilianzishwa kwa madhumuni ya kumaliza malaria nchini kwetu. Leo hapa kumeelezewa nchi takribani saba hizi zinachukua dawa kutoka kwenye kiwanda chetu hiki, lakini Tanzania bado, kitu ambacho kwa tathmini ya mwisho huku walisema kwamba zilinunuliwa lita 560,308 tena ziliponunuliwa hizo wameweka msisitizo ni kwa maelekezo ya Rais wa Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tujiangalie, malaria nchini kwetu bado ni tatizo tena ni tatizo sugu. Sisi kule Zanzibar tulikuwa na mradi wa kupigiwa dawa majumbani kila miezi mitatu, ikaja mpaka sehemu igundulike na malaria ndio inakuja kambi tunapigiwa dawa, ikafikia muda tukaambiwa mradi umeisha, sawa, malaria imerudi tena upya. Kama tukishirikiana hii ni nchi moja, kwa nini tusitumie rasilimali zetu zilizomo ndani na tukamaliza malaria? Hiki kiwanda kimeelekea kabisa madhumuni yake ni kumaliza malaria Tanzania, tunakwama wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ni zetu, pesa ni zilezile za Serikali, hivi kwa nini tusizoshawishi hizo Halmashauri kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakanunua hizi dawa na tukamaliza malaria nchini, lakini pia kiwanda kikawa kina- survive vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)