Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omar Issa Kombo (15 total)

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamona na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini je, kwa vile tunafahamu kwamba, vijana hawa wanaokwenda JKT takribani wengi wao ni kutoka katika familia maskini na wanatumia gharama kubwa mpaka kufikia kwenye makambi. Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu pindi inapotokea dosari kama hii kuwarejeshea gharama ambazo wanatumia kwa ajili ya safari hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema kwamba, lengo la kuwarudisha vijana ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, tunaweka utaratibu mzuri. Nafikiri Mheshimiwa Mbunge akubaliane na mimi kwamba na kwa haraka utaratibu ukikamilika tutawahitaji tena vijana kwa sababu, yako manufaa makubwa sana kwa mafunzo ambayo yanatolewa kwa vijana kwa sababu, hawa vijana tunawaandaa, kuna mafunzo ambayo yanawasaidia pia kwenda kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba, tutoe ushirikiano kwa Serikali, tutoe ushirikiano kwa Wizara kama wazazi. Kama anavyosema hata tulivyowarudisha tulizingatia kuona kwamba, vijana hawa wanarudi kwa kufuata utaratibu ambao tumeuweka. Tutaendelea kuona namna nzuri ya kuwasaidia vijana kupitia utaratibu ambao nilikuwa nimeutoa katika jibu langu la msingi.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumeona jitihada mbalimbali za wananchi wakizichukua kwa makusudi katika kupanda mikoko kwa lengo na madhumuni ya kuhifadhi mazingira, kuongeza mazalia ya samaki lakini kuzuia maji ya bahari kupanda nchi kavu. Mfano mzuri ni wananchi wa Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini Wilaya ya Micheweni. Swali la kwanza, je, Serikali inawapa matumaini gani wananchi hawa wa Mjini Wingwi na Sizini kwa kuwapatia misaada ya kifedha na vifaa kama boti kwa ajili ya patrol kama sehemu ya kuhamasisha na kuwapa moyo kuendelea na jitihada hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana nami baada ya Bunge hili mpaka kwenye Kijiji cha Mjini Wingwi na Sizini kwa lengo la kwenda kuona jitihada za wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu maswali haya, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Omar Issa kwa juhudi yake ya kutunza mazingira katika maeneo yake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anauliza Serikali itawapa matumaini gani wananchi? Serikali kwa sababu inasikiliza na inathamini juhudi za wananchi, naomba hili tulichukue na baadaye tutakaa pamoja naye na wataalamu wetu tuone namna gani tunawapatia motisha wananchi ambao wanajitahidi kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili mimi niko tayari kabisa kufuatana naye baada ya Bunge hili kwenda kuona na kutafuta njia sahihi ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu, lakini pamoja na majibu mazuri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine Wabunge kutoka Zanzibar, pamoja na majukumu mengine tunatakiwa kuwaeleza wananchi wa Zanzibar juu ya umuhimu na faida za Muungano wetu. Kwa kujua hilo, je, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haioni ipo haja ya kuwashirikisha Wabunge kutoka Zanzibar katika uibuaji wa vipaumbele vya miradi inayotokana na fedha za Muungano?

Pili, Mheshimiwa Waziri katika Mkutano wa Nne aliniahidi kwenda Jimboni kwangu kutembelea vijiji vya Mjini Wingwi na Sizini.

Je, ananiahidi ni lini tutakwenda kutekeleza ahadi hiyo?Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nikiri wazi kwamba kwa kweli Wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa na kipaumbele sana cha kushughulikia changamoto za wananchi wa Zanzibar akiwemo ndugu yangu Omar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba niliahidi kwenda ni kweli, bahati nzuri nilishafika Zanzibar mpaka Jimbo la Nungwi, Jimbo la Amani na maeneo mengine, lakini nikuhakikishie kwamba ahadi yangu ya kufika katika eneo lako la kazi lipo pale pale tutaenda kuchapa kazi ondoa hofu katika hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kushirikisha Wabunge wa Zanzibar naomba niwashukuru, hata hii ajenda ukiangalia fedha za Covid, Wabunge wa Zanzibar mlileta fedha mahsusi hapa wakati mchakato wa barabara ulipokuwa ukifanyika ndiyo maana hata suala zima la fedha za Covid unaona kwamba zaidi ya shilingi bilioni 231 zimeenda upande wa Zanzibar lengo ni kuona kwamba hisia za Wabunge wa Zanzibar zimeonekana kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba yale Wabunge wanayoyachangia humu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo lazima iwe shirikishi.

Mheshimiwa Spika, hiyo, hilo jambo ni zuri, tutaendelea kuboresha zaidi jinsi gani Wabunge watashiriki vizuri katika kuibua hoja mbalimbali. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia na kukarabati ujenzi wa nyumba za polisi katika kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha jibu katika swali langu la msingi, Micheweni ambako kunahitajika pia ujenzi wa nyumba na kuboresha kituo ni miongoni mwa vituo ambavyo vitaimarishwa kulingana na mpango wetu wa kukarabati nyumba na vituo chakavu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni nimeona baadhi ya wananchi wakifutwa kwenye mpango wakati bado hali zao ni mbaya sana, na naomba nimtaje mwananchi ambaye ni mfano, anaitwa Ndugu Hamad Faki Hamad maarufu Fofofo kutoka Shehia ya Mjini Wingwi, hali yake ni mbaya sana lakini amefutwa.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa kauli gani kwa TASAF dhidi ya hali kama hizi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya taarifa ambazo zinasambaa kwa wananchi ambazo zinaleta wasiwasi kwamba wanakwenda kufutwa kwenye mpango wakati hali zao bado ni mbaya. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya taarifa hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza yeye mwenyewe Mheshimiwa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kwa sababu pia ni mjumbe wa Kamati ya USEMI ambayo inasimamia Wizara yetu hii Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na amekuwa akifuatilia sana masuala haya ya TASAF hasa jimboni kwake kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikienda kwenye maswali yake anauliza ni vigezo gani ambavyo hata huyu amemtaja Mzee Hamad Faki vimemuacha. Sijui hasa kwenye kesi hiyo kama individual na nitakaa naye Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujua kwa nini Mzee Faki alitoka katika mpango wa TASAF, tukitoka hapa nitakutana naye ili tuweze kulijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja katika mradi huu awamu hii ya pili imekuwa ina component mbili; component ya kwanza ni ile ambayo tulikuwa tumeizoea kwenye awamu ya kwanza ya mradi huu wa TASAF, ni ule wa cash kwenda kwenye kaya hizi, lakini component ya pili ni public works. Kwamba kaya huenda ina watu watano, na mkuu wa kaya anaweza akawa ni mtu mzima labda ana miaka 70 lakini ndani ya kaya ile kuna watu wenye uwezo wa kufanya kazi. Basi watafanya kazi na kulipwa ujira kutoka kwenye mradi wa TASAF, kwenye miradi ile ambayo wameibua wao wenyewe katika maeneo yao husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, ya taarifa hizi kwamba wanufaika wanaenda kufutwa. Niseme taarifa hizi si za kweli, walengwa hawa hawaendi kufutwa, na tulifanya uhakiki kabla ya kuingia kwenye awamu ya pili ya mpango huu na kaya zimeongezwa. Serikali hii ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake mwenyewe alielekeza tuongeze idadi ya kaya kwenye mpango huu wa TASAF, na kaya zimeongezwa na hauendi kufutwa.
MHE. ISSA OMAR KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, kwanza naomba nikumbushe tu kwamba kwa Zanzibar tunatumia Wadi siyo Kata. Kwa hiyo, hii ni Wadi ya Kiuyu.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza kama ifuatanyo; ni miaka miwili sasa tumekuwa tukipata matumaini haya ya Serikali kwamba tutajengewa ofisi, lakini kiukweli hali ni mbaya. Kwa NIDA Micheweni wanatumia vyumba viwili walivyoazimwa na Wizara ya Afya ambapo vyumba hivyo viwili wanatumia Ofisi ya DRO, Ofisi ya Picha, store na jiko. Kwa kweli hali mbaya sana, hata ufanisi unakuwa ni mdogo sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba commitment ya Serikali; je, ni quarter gani ya mwaka wa fedha husika tutaanza kujengewa ofisi hii wananchi wa Wilaya ya Micheweni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kweli narekebisha, badala ya kuita Kata ya Kiuyu, ni Wadi ya Kiuyu, ahsante sana.

Kuhusu kuwapa matumaini na kwamba hali ya ofisi hizo ni mbaya sana, nakubaliana naye. Ndiyo maana tunasema katika mwaka 2023/2024 tutaweka fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hii.

Mheshimiwa Spika, commitment ninayoitoa, ni kazi ndogo tu. Bunge lako tukufu likiidhinisha bajeti hii ambayo itakuwa imebeba pia dhima ya kujenga hizo ofisi 31, ni kwa uhakika kabisa jimbo lake litanufaika na ujenzi huo, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kweli nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kweli ni matumaini yangu kwamba wananchi wa Micheweni watafarajika pindi watakaposikia majibu haya ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo nina swali moja la nyongeza. Mara nyingi imezoeleka katika Shirika la Posta wakati wanapotoa ajira wanachukua waajiriwa kutoka katika maeneo mengine. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishiaje, pindi watakapofungua ofisi hii katika ajira ambazo watatoa watazingatia kipaumbele au wataweka kipaumbele kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo anaifanya kwa ajili ya wananchi wa Wingwi. Lakini vilevile ameendelea kuhakikisha kwamba anatupatia changamoto zinazoendelea ndani ya jimbo lake. Sisi kama Serikali tunaendelea kuzipokea na kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini pili suala la ajira linafahamika kabisa kwamba mashirika yetu haya yanaajiri kwa kupitia utaratibu wa utumishi wa umma. Hivyo basi, tunaamini kabisa kwamba mfanyakazi yeyote, au yeyote ambaye ni Mtanzania ana haki sawa kuomba kazi na kupatiwa kazi kulingana na vigezo ambavyo vitakuwa vimewekwa.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina swali dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni awamu ya pili hii kuambiwa tumetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki. Na kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kwa kweli uchakavu ni wa hali mbaya sana. Tunaomba commitment ya Serikali; kama ni kweli kituo hiki kitajengwa kwenye bajeti ya mwaka unaokuja, ni quarter ipi wamepanga kufanya ukarabati wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, atakumbuka Mheshimiwa Kombo kwamba nilitembelea Kituo hiki cha Micheweni nikajionea hali halisi; na kwa msingi huo tukakubaliana ndani ya Wizara na Jeshi la Polisi kutenga fedha. Atakumbuka kwamba miaka iliyopita hata kama alipewa ahadi hakuna fedha iliyotengwa lakini mwaka ujao namhakikishia fedha imetengwa na tutahakikisha tutakapopata fedha za maendeleo basi kituo hiki tutakipa kipaumbele, nashukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Hadi sasa katika Wilaya ya Micheweni hakuna nyumba za askari ambazo ujenzi unaendelea. Pamoja na hili sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo cha polisi Wilaya ya Micheweni ndiyo Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Micheweni. Je, Serikali ina mkakati gani wakujenga nyumba za polisi katika Wilaya ya Micheweni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Micheweni kuna hanga la Jeshi la Polisi ambalo lilijengwa kutokana na nguvu za wananchi miaka kumi iliyopita hadi sasa hanga hili kutokana na kwamba halikumaliziwa tayari limeanza kuharibika ikiwemo paa kuvuja na saruji kuharika. Je, Serikali haioni haja kuunga mkono jitihada hizi za wananchi kwa kumalizia jengo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati nimeusema ni kuendelea kutenga fedha kujenga nyumba za askari na maofisa kutegemea upatikanaji wake hata hivyo alichosema kwamba ujenzi umesimama kule Micheweni Mheshimiwa Mbunge ni kweli ndiyo maana kwenye jibu la msingi nimesema zinahitajika milioni 60 ili kumalizia jengo hilo na fedha hizi zinatengwa kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo. Kwa hiyo, Mheshimiwa eneo hilo litakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uendelezaji wa ujenzi wa nyumba, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi tutaendelea kujenga nyumba za askari kadri tunavyopata pesa kwenye bajeti yetu au pale tunaposhirikiana na wadau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Waziri, swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba uko mdaki mmoja utafungwa katika eneo la Azam Sea Link, tunataka kujua, ni lini mdaki huu utakwenda kufungwa ili kuondoa adha kwa wananchi wanaotumia eneo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa vilevile Mheshimiwa Waziri amesema kwenye bajeti ya mwaka huu, wametenga fedha kwa ajili ya kununua midaki mingine. Je, ni midaki mingapi itakwenda kunuliwa kwa ajili ya eneo la Azam Sea Link ili kuendelea kuboresha eneo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu lini, ni ndani ya Mwaka huu wa Fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu ni midaki mingapi itajengwa kwenye eneo hili ni kwamba hakuna mpango wa kuongeza kwenye eneo la Azam Link kwa sababu tayari umeshapatikana mmoja na kama kutakuwa na uhitaji tutakwenda kwenye maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa vile Waziri amekiri kwamba kituo hiki kutokana na uchakavu tayari kimeondoka; na tayari kutokana na mahitaji na eneo lile ni kubwa, kuna miradi mikubwa ya Serikali ambayo ipo sasa: -

a) Je, Serikali haioni haja ya kuweka kituo cha dharura katika eneo hili la Tumbe?

b) Je, Wizara iko tayari kwenda kukaa na ofisi ya mkuu wa wilaya pamoja na halmashauri kuangalia eneo kubwa au kupatiwa eneo ambalo litatosha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi, ni kweli kabisa kwamba eneo hili lina matumizi makubwa kwa kuwa pia kuna miradi mikubwa ambayo inahitaji kituo cha polisi. Lakini kituo cha polisi cha dharura kinaweza kikapatikana endapo tu mamlaka za halmashauri husika zitatenga jengo ambalo litakuwa na sifa ya kutumika kama kituo cha polisi.

Mheshimiwa Spika, suala la eneo; kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni jukumu la halmashauri sasa kutafuta eneo ambalo tunakwenda kujenga kituo kipya. Na Wizara iko tayari kutoa ushirikiano kwa mamlaka za halmashauri hiyo ili kituo hicho kiweze kujengwa haraka sana.
MHE. OMAR ISSA. KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante je, ni lini Serikali itawajengea nyumba za kuishi Jeshi la Polisi Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kadri ambavyo tutapata fedha tutaendelea kuimarisha na kujenga Vituo vya Polisi na Makazi ya Askari. Kwa hiyo, Micheweni ni moja ya eneo litakalozingatiwa katika ujenzi wa nyumba za askari, ahsante. (Makofi)

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali ingawa hayaleti matumaini kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na hali ya kituo kilivyo hali ni mbaya sana mpaka paa zake kuvunja. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa dharura kukarabati Kituo hiki cha Micheweni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi mpaka Micheweni kwenda kujionea hali halisi ilivyo kwa sababu hanga hili la polisi limejengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka minane iliyopita na sasa hivi tayari limeanza kuvuja. Je, uko tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea hali halisi ilivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kombo kama ifuatavyo:-

Kwanza nakubaliana naye kwamba hali ni mbaya ndiyo maana tathmini yetu imefanyika na kubaini gharama zinazohitajika. Kwa kuwa bajeti ya mwaka huu imepita, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo yatakayopewa vipaumbele katika mwaka ujao basi tutazingatia hili eneo pia la Micheweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kuambatana naye niko tayari na mara nyingi natekeleza ahadi baada ya Bunge hili tutapanga tuone lini kuweza kuitembelea Micheweni kubaini kiwango cha uharibifu na nakubaliana naye pamoja namna ya kutekeleza ukarabati huo, nakushukuru.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali ilifanya tathmini kwa kuzingatia vigezo hivi sambamba na mgawanyo wa fedha za majimbo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunashuhudia baadhi ya majimbo yakipata fedha kidogo ukizingatia kwamba vigezo alivyovieleza Mheshimiwa Waziri ni vikubwa zaidi ukilinganisha na Majimbo mengine na hata hali ya umaskini ni kubwa zaidi. Mfano mzuri ni Jimbo langu la Wingwi: Je, Serikali haioni iko haja ya kufanyia tathmini vigezo hivi, kwa kuzingatia sensa ya mwaka 2022? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kwamba Serikali inafanya tathmini ya vigezo hivi mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba vinakidhi uhitaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo katika Majimbo yetu na pia kuona namna nzuri ya kuendelea kuboresha formula za hivi vigezo ili kuweza kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Mfuko wa Jimbo kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kufanya tathmini mara kwa mara, na mara itakapoona kuna maeneo ambayo vigezo vinahitaji kuongezwa au kupitiwa upya, basi suala hilo litafanyika.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba fedha za Mfuko wa Jimbo zinatofautiana kutoka Jimbo moja na Jimbo lingine kwa kuzingatia vigezo hivi. Kama nilivyosema, asilimia 45 ya idadi ya watu katika Jimbo husika; kwa hiyo, Majimbo yenye idadi kubwa ya watu automatically yatakuwa na fedha nyingi zaidi, lakini kiwango cha umaskini kwa asilimia 20 pia na ukubwa wa eneo la kijiografia kwa asilimia 10, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenye majibu Serikali imesema itavifanyia tathimini vijiji vilivyobakia je ni lini tathimini hii itaanza?

Mheshimiwa Spika, vilevile asilimia kubwa ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni hutumia mitandao ya simu ya halotel na tigo lakini huduma zake zimekuwa ni hafifu mitandao hii. Je, Serikali inachukua jitihada gani kuwaondolea usumbufu wananchi wa maeneo ya vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza ni lini tutafanya tathimini? Tayari tumeishamaliza kufanya tathimini katika vijiji 2,116 na hivyo naelekeza timu ya wataalam kutoka Wizarani kwetu wakishirikiana na UCSAF waende wakafanye tathimini mara moja katika kata ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziomba.

Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili ni cha kiufundi na kibiashara, pia ni cha kisheria, kwa sababu kinaangukia katika upande wa sheria kwa mujibu wa Sheria Namba 12 ya Mwaka 2003, na kwa kanuni zetu za mwaka 2018 inampatia TCRA mamlaka ya kuhakikisha kwamba inaangalia ubora wa huduma ya mawasiliano. Hivyo, basi nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuwaelekeza TCRA kwenda kufanya tathmini na kujiridhisha na quality of service katika maeneo hayo ili tujue ni hatua gani tunazichukua kulingana na majibu ambayo watayaleta, nakushukuru.