Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Omar Issa Kombo (12 total)

MHE. OMAR ISSA KOMBO Aliuliza:-

Je, ni kwa nini Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewarudisha nyumbani Vijana ambao walishafika Kambini kwa ajili ya kuanza mafunzo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, JKT ilisitisha mafunzo ya vijana wa kujitolea kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kutokana na sababu zifuatazo:-

(1) Kutoa nafasi kwa JKT kutathmini mafunzo yaliyofanyika na kuandaa utaratibu wa kuwa na mitaala bora ya mafunzo ya vijana itakayowawezesha vijana hao kujitegemea wanapomaliza mafunzo badala ya kutegemea kuajiriwa.

(2) JKT kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kufanya mawasiliano na taasisi zingine kama, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Tume ya Vyuo Vikuu na Baraza la Mitihani (NECTA) kuandaa utaratibu wa kuongeza muda wa mafunzo ya vijana wa mujibu wa sheria kuwa mwaka mmoja badala ya miezi mitatu ya sasa na kuchukua vijana wengi zaidi wanaomaliza kidato cha sita huku idadi ya vijana wa kujitolea ikipunguzwa.

(3) Kutoa fursa kwa JKT kukamilisha mpango wa kuwawezesha vijana kupata mitaji wanapohitimu mafunzo kwa kushirikisha taasisi nyingine ambazo ni Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Kazi na Vijana na TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mkakati huu utasimamiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, JKT itaendelea kutoa elimu kwa umma na kwa vijana wanaojiunga na JKT kujitolea kuelewa kwamba, lengo la mafunzo ni kuwawezesha waweze kujitegemea baada ya mafunzo hayo badala ya kutegemea ajira.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaweka matumbawe bandia na kupanda mikoko katika bahari ili kurejesha mazalia na makulia ya samaki yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuweka matumbawe bandia katika maeneo kadhaa ya mwambao wa Dar es Salaam, Unguja na Pemba. Katika eneo la Sinda Pwani ya Dar es Salaam eneo la mita za mraba 2000 limepandikizwa matumbawe bandia. Vilevile, kwa upande wa Unguja na Pemba jumla ya matumbawe bandia 90 aina ya reef ball yalipandikizwa katika Kijiji cha Jambiani; na matumbawe bandia 46 na mapande maalum 6 katika Kijiji cha Kukuu. Matumbawe hayo yalifuatiliwa ukuaji wake kitaalam na matokeo yameonyesha mafanikio makubwa kwa kuimarika kwa mazalia ya samaki na hivyo kuongezeka kwa kiwango cha samaki katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na upandaji wa mikoko, Serikali imekuwa ikiongeza jitihada zaidi katika upandaji wa mikoko katika fukwe mbalimbali nchi nzima kwa kushirikiana na asasi binafsi na washirika wa maendeleo. Takribani hekta 7 za mikoko zilipandwa Unguja na hekta 10 zilipandwa Pemba kwa mwaka 2020/2021. Upandaji wa hekta 13.5 unaendelea mpaka sasa na matarajio ni kupanda hekta 15 kwa mwaka huu. Aidha, kwa upande wa Tanzania Bara, hekta 105 zimepandwa katika Delta ya Rufiji na matarajio ni kupanda hekta 2000 kwa pwani yote ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatunza, tunahifadhi na kusimamia matumbawe na mikoko pamoja na mifumo ya ikolojia inayopatikana ndani ya bahari zetu. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, Serikali inatumia utaratibu gani wa kugawa miradi ya maendeleo kama shule, barabara na afya inayotokana na Muungano na ina mkakati gani wa kuyapa kipaumbele maeneo ya vijijini ikiwemo Jimbo la Wingwi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

(a) Serikali zetu zote mbili Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa utaratibu wa kugawa miradi ya maendeleo ya Muungano kama shule, barabara na afya unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizokubaliwa na pande zote mbili za Muungano. Vipo vigezo vinavyotumika katika kutoa fedha za kugharamia miradi ya Muungano kama vile Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo na Sheria nyinginezo zinazotumika kwa pande mbili za Muungano.

(b) Sambamba na hilo, Serikali kupitia misaada ya kibajeti (general budget support) hugawa fedha hizo kwa kigezo kilichokubalika kutumika cha asilimia 4.5 kwa Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar. Aidha, fedha hizo hugawanywa kwenye miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ya Mapunduzi ya Zanzibar.

(c) Kwa upande wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania (TASAF) Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliozinduliwa Februari, 2020, shilingi bilioni 112.9 zimepangwa kutumika Zanzibar ikiwemo katika miradi ya kijamii ambapo kipaumbele ni kwenye maeneo yenye mahitaji zaidi.

(d) Serikali itaendelea kutekeleza vigezo na tatatibu zilizokubaliwa na pande mbili za Muungano pamoja na kuimarisha majadiliano na mashirikiano kwa lengo la kuhakikisha kuwa miradi inayokubaliwa inatatua changamoto zinazowakabili wananchi waliopo maeneo ya vijijini wakiwemo wa Jimbo la Wingwi. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wenye sifa wa Shehia ya Njuguni, Majenzi na Chomboni – Micheweni wataunganishwa na TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF iliyoanza rasmi mwezi Januari, 2020 unaendelea katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar kwenye vijiji, mitaa na shehia zote ikiwa ni pamoja na zile ambazo hazikufikiwa wakati wa utekelezaji wa kipindi cha kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika shehia ya Njuguni, Kaya 352 ziliandikishwa, Shehia ya Majenzi Kaya 312 ziliandikishwa na Shehia ya Chamboni Kaya 584 ziliandikishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kaya ambazo hazikutambuliwa na kuandikishwa kwa sababu mbalimbali katika kipindi hiki cha pili utaratibu umeandaliwa kwenda kwenye vijiji, mitaa na shehia zote kwa maeneo yote ya utekelezaji ili ziweze kuandikishwa na kuingizwa kwenye mpango ikiwa zimekidhi vigezo na sifa stahiki.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi ya NIDA katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kujenga ofisi 31 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa gharama ya dola za Kimarekani 84,924,918 sawa na fedha za Tanzania shilingi 197,094,598,943.58. Fedha hizo zinajumuisha mchango wa Serikali wa jumla ya dola za Kimarekani 14,924,918 na mkopo nafuu wa dola za Kimarekani 70,000,000 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea ya Kusini. Wilaya ya Micheweni iliyopo Mkoa wa Kaskazini Pemba ni mojawapo ya Wilaya zitakazonufaika kwa kujengewa Ofisi ya Usajili na Utambuzi wa Watu. Ofisi hiyo itajengwa kwenye Kiwanja Na. 10, kilichopo Shehia ya Maziwang’ombe, huko Micheweni, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Ofisi ya Posta katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukuaji wa teknolojia ya TEHAMA na mabadiliko yanayoendelea ndani ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) katika utoaji wa huduma kwa njia za kielekitroniki kupitia mawakala, Shirika halijapanga kujenga Ofisi ya kutolea huduma bali litatumia mawakala katika kutoa na kufikisha huduma zake kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Shirika la Posta Tanzania limepanga kutumia Kituo cha TEHAMA kilichopo Micheweni kinachomilikiwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kutoa huduma za Posta kwa wananchi wa Wilaya ya Micheweni kwa kutumia wakala. Shirika tayari limewasilisha maombi ya kupatiwa nafasi katika Kituo hicho na kukubaliwa. Shirika linakamilisha taratibu ili huduma za posta zianze kutolewa kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilika.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo kipya cha Polisi cha Wilaya ya Micheweni pamoja na kupeleka samani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la mheshimiwa Omar Issa Kombo Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Micheweni ina kituo cha Polisi daraja B ambacho kinakidhi mahitaji ya kutoa huduma ya Polisi eneo hilo. Tatizo pekee la kituo hiki ni uchakavu unaohitaji kufanyiwa ukarabati. Tathmini ya uchakavu wa kituo imefanyika mwezi Januari 2023, na kubaini kuwa jumla ya shilingi 65,000,000 zinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, dari, milango na madirisha, mfumo wa maji safi, maji taka, umeme, kuziba nyufa na kupaka rangi. Fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kiasi cha fedha shilingi 17, 870,000 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisi zinatarajiwa kuombwa kutoka kwenye mfuko wa tuzo na tozo kwa mwaka 2023/2024 mara ukarabati wa kituo utakapo kamilika.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi katika Kituo cha Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba za makazi ya kuishi askari Polisi katika Wilaya ya Micheweni. Mpaka sasa ujenzi unaoendelea ni wa hanga la kuishi familia 18 za askari na uko kwenye hatua za umaliziaji. Kiasi cha shilingi milioni 60,000,000 kinahitajika ili kumalizia na fedha hizo zinatarajiwa kuombwa kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Serikali itaendelea kujenga nyumba za maofisa na askari kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaweka Mdaki katika Bandari ya Dar es Salaam kwa meli za abiria na mizigo za Azam Sea Link ili kuondoa usumbufu na kero kwa abiria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TPA imenunua midaki mitatu kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi katika eneo la Azam Link na eneo la kuhifadhi mizigo (Baggage room) ambapo midaki miwili imeshafungwa eneo la kuingia na kutoka katika eneo la kuhifadhi mizigo (Baggage room) na mdaki mmoja utafungwa katika eneo la Azam Link. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitIa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imetenga fedha kwa ajili ya kununua midaki mingine, kwa ajili ya eneo la Lighter Quay na yadi ya magari (RORO Yard), ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakifanyia matengenezo Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Micheweni na ujenzi wa nyumba za askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya tathmini ya uchakavu wa Kituo cha Polisi Micheweni na kubaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 51,000,000 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho. Aidha, ujenzi wa jengo la hanga la kituo hicho umefikia kwenye hatua za kumalizia na kiasi cha fedha shilingi 57,000,000 zinahitajika. Ukarabati wa kituo pamoja na umaliziaji wa ujenzi wa jengo la hanga utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, Serikali inazingatia vigezo gani kugawa fedha za Mfuko wa Jimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Jimbo umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 16 ya mwaka 2009 kwa lengo la kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge kuchochea maendeleo ya Jimbo. Aidha, vigezo vinavyotumika kugawa fedha za mfuko wa Jimbo ni pamoja na idadi ya watu Jimboni asilimia 45, mgao sawa kila Jimbo asilimia 25, kiwango cha umaskini asilimia 20 na ukubwa wa eneo asilimia10, ahsante.
MHE. OMAR ISSA KOMBO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya mawasiliano ya simu Micheweni, vijiji vya Sizini, Dodeani, Michungani, Mapofu, Msuka na Makangale?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolijia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Sizini kipo katika mradi wa awamu ya sita ambapo mnara katika kijiji hicho unajengwa na mtoa huduma ambaye ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL). Mnara huo upo katika hatua mbalimbali za ujenzi, ambapo utakamilika na kuwashwa ifikapo Aprili, 2024. Aidha, Serikali imetekeleza ujenzi wa mnara katika kijiji cha Dodeani kupitia mradi wa awamu ya nne ya UCSAF ambapo mnara ulijengwa katika Shule ya Dodeani.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali itavifanyia tathmini vijiji vya Michungani, Mapofu, Msuka na Makangale kuangalia mahitaji halisi ili kuvifikishia huduma ya mawasiliano.