Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Omar Ali Omar (9 total)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri, kwanza naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutupa majibu ya uhakika ya kupata ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, suala la ajira kwa vijana wa Jeshi la Polisi, hasa wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Serikali ina mpango gani wa kupeleka askari 150 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo ndiyo tatizo kubwa kwa sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba; Jeshi la Polisi linapoajiri vijana kupitia Jeshi hili kuna tatizo/ changamoto moja kubwa kabisa; vijana wengi wanaondoka kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kuomba ajira ya Jeshi la Polisi,

Je, changamoto hii wamejipangaje kuhakikisha kwamba vijana wa Mkoa wa Kaskasini Pemba ndio wale wanaohusika hasa kutokana na sifa walizonazo kajiriwa katika Jeshi la Polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie fursa hii kwanza kumpongeza kwa kuwa Mheshimiwa Omar siyo tu amekuwa mwakilishi ama Mbunge wa Jimbo la Wete, lakini pia amekuwa anafanya kazi na kuusemea mkoa wake kwa ujumla katika mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya siasa, uchumi na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie Mheshimiwa kwamba nafasi hizi zimekuja na zitakwenda katika kila mkoa. Na zitapita katika kamati za ulinzi na usalama kama utaratibu ulivyokuwa umepangwa. Lakini kikubwa nimwambie kwamba idadi ya nafasi alizozitaja zinaweza zikaenda mahali ambapo patakuwa pana uhitaji zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yana uhitaji zaidi. Kwa mfano kuna maeneo yana idadi kubwa ya watu (wananchi), kwa sababu utaratibu ulivyo ni kwamba askari mmoja analinda raia kuanzia 350 mpaka 400, kwa hiyo ikiwa mahali pana watu wengi panaweza pakapelekwa idadi hiyo. Lakini pia tutaangalia na crime rate (hali ile ya vitendo na matukio ya uhalifu ya mara kwa mara) pia yatatupa sisi impetus ya kuona wapi tuangalie itakavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa nimwambie Mheshimiwa, kwamba katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, nafasi hizi zitakwenda na vijana wataomba na Serikali itaendelea kutekeleza azma yake ya kuwaahidi wananchi na kuwatekelezea. Asiwe na wasiwasi wananchi/vijana wake wataajiriwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu changamoto ya vijana kutoka mkoa mmoja ama wilaya moja kwenda nyingine kuomba hizi nafasi. Kiutaratibu sifa inayokuja anatakiwa awe Mtanzania, haikusema kwamba atoke Pemba au Unguja au wapi. Kwa hiyo anaweza akatoka sehemu moja akaenda nyingine.

Mheshimiwa Spika, lakini kikubwa tuwaambie kwamba watakaosimamia nafasi hizi wahakikishe vijana ambao wako katika mkoa husika wapate hizi nafasi ili lengo na madhumuni vijana waweze kupatiwa ajira kama ambavyo Serikali iliwaahidi wakati wa kampeni. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba posho ya shilingi 100,000 ambayo ilikuwa inatolewa kwa ajili ya kuwawezesha askari wetu waweze kukidhi haja ya kuweza kujenga, tukiangalia kwa mtazamo ni kwamba posho hiyo ilikuwa ni ndogo na hata askari wakipewa miaka 100 hawawezi kufanya ujenzi kwa posho hiyo.

Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwawezesha askari wetu kuwaongezea posho hii ili iendane na utaratibu wa kuweza kujenga kwa askari wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili; je, sasa Serikali haioni kwamba kuna haja kwa Wizara kuhakikisha kuona kwamba pamoja na kwamba askari wetu wanaintelijensia ya hali ya juu, hatuoni sasa kwamba kuna haja sasa ya ule utaratibu wa mwanzo kuweza kutumika ili kwamba askari wetu tuweze kuwaweke katika mazingira mazuri waweze kulinda nchi hii, raia pamoja na mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Ali Omar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari ama ina utaratibu gani sasa wa kuongeza hii posho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo dhamira kwa sababu kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba vyombo vyetu vya ulinzi hasa Jeshi la Polisi wanafanya kazi nzuri na kwa kweli tunayo kila sababu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuendelea kufanya kazi vizuri, katika hili tunawapongeza sana. Kikubwa ni kwamba utaratibu wa kuongeza hizi posho upo, tumeshaupanga/tumeshaufikiria maana hata katika bajeti ambayo tuliiwasilisha juzi tulilizungumza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa awe na stahamala kwa sababu hii mipango inahitaji fedha na tupo mbioni kuhakikisha kwamba tunatafuta hizo fedha ili tuweze kuwaongezea kwa sababu hatuwezi tukasema kwamba kesho tutawaongezea, kwa hiyo, kesho watazipata lakini the way ambavyo kasungura ketu kananenepa ndivyo ambavyo tutakapokuwa tunawaongezea na wao hii posho ili sasa waendelee kufanya kazi nzuri zaidi ya kulinda raia na mali zao. Kwa hiyo, hiyo nia ya kuwaongezea posho ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini je, hakuna haja ya kurejesha ule utaratibu wa mwanzo, mimi nadhani Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tuende tukakae na wenzetu tukalifikirie hili, tukapange halafu tutaona sasa namna bora ya kuboresha haya mambo ili sasa kuweza kurejesha ule utaratibu wa mwanzo ambao kama yeye Mheshimiwa Mbunge ameuzungumzia. Nakushukuru. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Khamis, lakini nataka nikubaliane na muuliza swali la msingi Mheshimiwa Lambert pamoja na maswali yake ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ni kweli tunakubaliana kwamba vijana hawa askari polisi wanafanya kazi nzuri kwa nchi na Taifa lao na pengine wanafanya hivyo katika mazingira magumu na wengine kulingana na vyeo vyao ni vigumu sana kujikomboa na kupata hata maisha mazuri baada ya kumaliza utumishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lililosemwa katika swali la msingi ni kama je, Serikali haioni haja ya kuwapatia vijana hawa viwanja kwa bei nafuu? Nataka niseme sisi kama Wizara tunalichukua hili, tutajadiliana na wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone uwezekano huo kwa sababu ni jambo jema kabisa na wengine kweli wanamaliza/wanastaafu wakiwa kwanza na umri mdogo kulingana na Kariba ya ajira yenyewe ya Jeshi la Polisi, mtu ana miaka 54 anastaafu, halafu hana hata nyumba wala kiwanja. Nataka nikubaliane kwamba acha tulifanyie kazi, tuone kwa mfumo ambao uliopo kama tunaweza tukawapatia vijana hawa angalau viwanja, angalau kwa wale wa vyeo fulani fulani ambao unajua wapo kidogo underprivileged. Nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri, mmezungumzia upande wa viwanja nafikiri pia Serikali mtajipanga na hoja ya pili ya muuliza swali ameuliza mambo mawili; msamaha wa kodi katika vifaa vya ujenzi pamoja na viwanja kwa bei elekezi. Kwa hiyo, nafikiri…, karibu.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa na utaratibu wa duty free shops kwa ajili ya hawa askari. Maduka haya yalitumika na ukatokea ukiukwaji mkubwa sana wa taratibu za kikodi na kutokana na mazingira hayo mambo mengi mabaya yalitokea, Serikali ikaona bora kuondoa ile kwa sababu waliokuwa wananufaika ni watu fulani, fulani tu hata walengwa pengine walikuwa hawanufaiki, tukaona bora waingiziwe fedha zao na kwa utaratibu wa sasa wanalipwa shilingi 300,000 kila baada ya miezi mitatu, ni kitu fulani kuliko wengine ambao walikuwa vijijini huko hata duty free shops hizo hawazioni. Na utaratibu huo wa ku-institutionalize leo ni vigumu sana. Kwa hiyo, utaratibu wa fedha kuingizwa kwenye akaunti zao umekuwa ni bora na wanaufurahia sana. (Makofi)
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza ni kwamba kutokana na gharama ya fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo ambalo alisema kwamba ni chakavu lakini jengo hilo ni bovu kabisa.

Je, haoni Mheshimiwa Waziri kwamba kuna haja sasa ya kuambatana na mimi kwenda katika jengo hilo kwenda kujionea na kuona uhalisia wa gharama zinazohitajika katika kutengeneza jengo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti swali langu la (b) ni kwamba kutokana na ongezeko la vitendo vya udhalilishaji na vitendo mbalimbali vya unyanyasaji wa wanawake na watoto katika eneo la Mkoa wa Kaskazini Pemba na magari ambayo yanatumika ni magari matano tu. Haoni kwamba kuna haja sasa ya kuweza kuongeza magari ya dharura kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vitendo hivi vinakomeshwa muda mfupi ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar, Mbunge wa Jimbo la Wete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya miongoni mwa wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kuona kila jengo ikiwa nyumba za makazi, Kituo cha Polisi, mradi wowote ambao unashughulika na masuala ya Jeshi la Polisi ni wajibu wetu kwenda kuukagua. Nimwambie tu Mheshimiwa Omar kwa kushirikiana na wananchi wa Jimbo la Wete tupo tayari kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kukagua na kuona na sio Wete tu, lakini maeneo yote ya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla. Ni sehemu ya wajibu wetu na tuko tayari kufanya hivyo na mimi niko tayari kuambatana na yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine je, sasa si tupate hata gari kwa ajili ya doria na vitendo vya uhalifu? Nimuambie tu Mheshimiwa katika bajeti ambayo tumeisoma ya mwaka 2021/2022 tulisema kwamba tuna jumla ya magari zaidi ya 300 ambayo yatakuja kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Wete tutaliangalia kwa jicho la huruma sana kuhakikisha kwamba gari hizo zinakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza.

Kati ya wanafunzi 1,492 ni wanafunzi wangapi wenye mahitaji maalum ambao walipatiwa mkopo huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda sasa kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Omar Ali Omar Mbunge wa Wetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa vigezo ambavyo vinatumiwa na Bodi ya Mikopo yetu ya Elimu ya Juu ni pamoja na ulemavu, kwa maana ya wenzetu wenye mahitaji maalum pamoja ya uyatima. Kwa hiyo nitatoa takwimu tu za jumla za wenzetu hao kwenye makundi hayo kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2021 wanufaika wote wa Bodi ya Mikopo walikuwa ni 149,389; kwa upande wa Zanzibar wale waliokuwa na mahitaji maalum walikuwa ni 100; na mwaka 2021/2022 yaani mwaka huu tunaoendelea nao jumla ya wanufaika wote ni 177,892 na wale wenye mahitaji maalum kwa upande wa Zanzibar peke yake walikuwa ni 181. Nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza ni kwamba pamoja na juhudi kubwa za Serikali za kuangalia hifadhi ya mazingira lakini swali la kwanza ni kwamba Serikali ina mpango gani wa kuviwezesha vikundi vinavyojishughulisha na upandaji wa mikoko pamoja na matumbawe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika visiwa vidogovidogo vilivyopo Pemba Kisiwa cha Mtambwi Mkuu ni moja kati ya visiwa ambavyo vinaathirika kwa hali ya juu kabisa.

Je, Serikali ina mpango gani kukihami kisiwa kile ili kisipotee katika sura ya dunia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA
MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Omar kwa kazi nzuri anayoifanya kutuwakilisha katika suala zima la utunzaji na uhifadhi wa mazingira hasa katika suala la uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo juhudi mbalimbali ambazo tumezichukua katika kuhakikisha kwamba tunawasaidia hawa watu wa vikundi, cha kwanza ni kuelimisha. Tumegundua kwamba changamoto kubwa iliyokuwepo ni kwamba watu wengi taaluma kwao imekuwa ni changamoto. Kwa hiyo, tumekuwa tukichukua juhudi ya kuwaelimisha kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira pia tunawahamasisha juu ya upandaji wa miti na kuishughulikia, kwa sababu kuipanda ni suala moja na kuishughulikia ni suala jingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitoe wito kwa jamii hasa Waheshimiwa Wabunge tushirikiane, kila mmoja apande mti lakini kila mtu ashughulikie mti wake, kuipanda tu miti haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi kwa kushirikiana na Wizara ya Uvuvi tunahakikisha kwamba tunapambana dhidi ya uvuvi haramu ambao unaharibu hayo masuala ya mazingira.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni viwanda vingapi vya wazawa ambavyo vimepata msamaha huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, vimewasaidiaje viwanda hivyo? ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli swali la kwanza ni suala la takwimu naomba hili tulichukue tutampelekea kwa maandishi. Swali la pili, ni hakika kabisa viwanda vyote vya wazawa nchini vinapata misamaha kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; nami nataka niulize swali moja la nyongeza.

Mkoa wa Kaskazini Pemba kituo cha polisi kiko katika hali mbaya; je, Serikali inampango gani wa kukitengeneza kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli nilitembelea Pemba na nilibaini kituo kile kweli ni chakavu. Kinachotia faraja ni kwamba mkoa umeshabaini eneo la kujenga kituo kipya cha ngazi ya mkoa. Katika bajeti yetu ya mwaka ujao ni mpango wa Serikali kuanza ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi cha Mkoa wa Kaskazini Pemba.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa taarifa nilizokuwa nazo kwamba magari ya polisi yaliyoko Mkoa wa Kaskazini Pemba ni mawili tu. Je, hili gari moja limekwenda sehemu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Jeshi La Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba lina magari machakavu mengi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyatengeneza magari haya au kuyapiga mnada?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa alizonazo yeye ni magari mawili, lakini taarifa nilizopewa na IGP ni magari matatu. Tutafuta hilo la tatu liko wapi, kama limepelekwa mahali fulani tutahakikisha linapelekwa Pemba ili magari matatu yaweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa magari, tutafanya tathmini kama kawaida ilivyo kwa mali za Serikali, magari yaliyochoka yanafanyiwa tathmini, yanayoweza kufanyiwa ukarabati au matengenezo yakarejea barabarani yanafanyika, yale yanayoshindikana huuzwa kwa utaratibu unaosimamiwa na Wizara ya Fedha. Kwa hiyo, tutafanya tathmini ya haraka ili yale yaliyo machakavu kabisa tuyaondoe kwenye daftari kwa kuyauza na yale yanayoweza kutengenezeka yafanyiwe matengenezo, yasaidie usafiri wa vijana wetu, nashukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ni masomo gani ambayo yalisahihishwa katika kipindi hicho alichokitaja Mheshimiwa Waziri 2021/ 2022?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, Wizara imejipanga kusahihisha mitihani mingapi katika mwaka 2023?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Omar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa usahihishaji wa mitihani kila kituo kawaida huwa kina sahihisha mtihani mmoja na kwa miaka hiyo niliyoitaja ya 2021/2022 katika kituo hiki cha Zanzibar ni somo la civics ndilo ambalo lilisahihishwa katika kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anataka kufahamu ni mitihani gani ambayo itasahihishwa. Masuala ya mitihani na masomo gani yatasahihishwa ni jambo la siri. Kwa hiyo, hatuwezi ku-disclose hatuwezi kufungua hapa sasa hivi ni mitihani gani utakwenda kusahihishwa kwenye kituo hiki na ni mapema Sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tarehe 26 Juni, tutaanza kufanya ukaguzi wa vile vituo ambavyo tunalenga sasa mitihani itakwenda kusahihishwa lakini somo gani kwamba linapelekwa katika kituo hicho litaendelea kuwa siri mpaka baada ya kazi hiyo kumalizika, nakushukuru sana.