Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Amour Khamis Mbarouk (9 total)

MHE. AMOUR K. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza sijajua kwa nini mikoa ya Zanzibar haijaorodheshwa hapa, lakini pia sijajua Serikali inawezeshaje makundi haya 157 ili kumudu kazi hii ngumu sana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kwa kuwa zipo dini ambazo zinajinasibu na kujitahidi kusema kwamba kila kitu kitakachotokea duniani kwenye vitabu vyao wameeleza: Je, Serikali imeshaona umuhimu wa kuwashauri viongozi wa dini katika kuondoa tatizo hilo ambalo ni gumu sana hata pale Zanzibar ambapo visiwa ndiyo vinaondoka?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khamis Amour Mbarouk kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Amour kwa juhudi yake ya kufuatilia masuala ya mazingira kule visiwani Zanzibar. Suala lake la kwanza ni kweli kwamba ipo haja ya kuhamasisha vikundi mbalimbali katika sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na tayari tumewasiliana na wenzetu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kule Zanzibar kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wa Kanda za Pwani ili kusudi kuanzisha vikundi kama hivi kwa lengo la kutunza mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kwa kweli tunachukua hoja yake hii kwamba upo umuhimu wa kushirikisha taasisi za dini. Tumeanza kuwaita viongozi wa dini na kuzungumza nao kuhusu suala la utunzaji wa mazingira. Kwa mwelekeo ambao tunakwenda nao sasa, ni lazima tuzishirikishe taasisi za dini kuhusu suala la utunzaji wa mazingira, kwa sababu wao kwa asilimia kubwa wanakaa na wananchi. Kwa hiyo, tutawaomba viongozi wa Makanisa ama Misikiti iwe ni sehemu ya mahubiri yao ya utunzaji wa mazingira ili mazingira yetu yawe salama kwa maslahi ya Taifa letu. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri au majibu ya Serikali.

Kimsingi majibu ni mazuri sana, ila uhalisia ulivyo ni kwamba, abiria anaweza kuwa na mzigo akatakiwa kulipa, lakini akiuliza alipie ofisi gani, akakosa hiyo ofisi na akatakiwa kumpa fedha mkononi mchukuzi ambaye ndiye atamlipia itakapofika saa 1.30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya nyongeza; kwanza, naomba kujua ni mzigo wenye uzito kiasi gani ambao mtu akipita nao hapo bandarini atatakiwa kulipa? (Makofi)

Pili, je, Serikali haioni umuhimu wa kupunguza au kuondoa kabisa ushuru wa wafanyabiashara wadogo wadogo wanaotoka Zanzibar kuja kuchukua biashara zao hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee shukurani za Mbunge kwa niaba ya Serikali. Pili, naomba kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza amezungumzia suala la uzito; anataka kufahamu ni uzito kiasi gani ambao anastahili ama anapaswa kulipa anapopita pale bandarini? Ieleweke kwamba Mamlaka yetu ya Bandari nchini inaongozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2004 na miongozo mbalimbali ikiwepo Mwongozo wa Mwaka, 2003 na Aya ya 12(1) na aya ya 71(1). Miongozo hii inatuelekeza kwamba mzigo wa abiria yeyote anayetoka Bara ama kwenda Visiwani au Visiwani kuja Bara inatakiwa atozwe ukiwa hauzidi kilogram 21. Hilo la kwanza kupitia Mwongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, inaelekeza kwamba inatakiwa ujazo wa huo mzigo kwa maana ya cubic measurements usizidi moja, kwa maana ya ujazo wake ama nafasi inayochukua huo mzigo wako ni kiasi gani? Kuhusu wafanyabiashara wadogo kupunguziwa gharama pale bandarini; nataka nimhakikishie Mbunge ya kwamba kama wewe una bidhaa, kwa mfano, una baiskeli au TV ya matumizi yako binafsi, haitakiwi utozwe ushuru pale bandarini. Ila kama una zaidi ya hivyo, hii sheria itatuhusu sote. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali ya nyongeza, lakini kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana mimi namuombea dua Mwenyezi Mungu amuongezee katika elimu yake hii. Ninayo maswali mawili.

Swali la Kwanza; Serikali inatumia sheria gani kuweka vigezo vya kuwatambua hawa wavumbuzi?

Swali la Pili; amesema kwamba kati ya wavumbuzi waliotambuliwa ni 2,735. Je, katika hawa Zanzibar wapo wangapi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amour, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Serikali imekuwa ikifanya mchakato wa kuibua hawa wabunifu, wabunifu hawa wanaibuliwa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 1986 ambayo ilianzishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kati ya wabunifu hawa 2,735 tumesema wabunifu 376 wanaendelezwa na Serikali, kati ya wabunifu hawa ni wabunifu 11 wanatoka upande wa Zanzibar. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nilikuwa naulizia iwapo Serikali inaweza kuthibitisha au inaweza kutuhakikishia kwamba huyu mbwa kwa namna walivyom-train hataweza kupata hicho kichaa cha mbwa, ahsante. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo hili ambapo kuna meli kubwa za mzigo zinazotoka huku Bara kwenda Zanzibar na kwenda Comoro hususan eneo la Azam Sealink na Lighter Key linahitaji kufungwa mzani mkubwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayokwenda na inayoingia pia Dar es Salaam. Serikali ilikwisha tangaza tenda tangu mwaka jana mwezi wa kumi na bahati mbaya hakuna aliyeweza kukidhi vigezo vya tenda hiyo kwa maana ya scanner ama mdaki ambao tunahitaji kama Serikali. Maana tunahitaji scanner iwe kubwa na kwa maana hiyo sasa, tutatangaza tenda upya tarehe 3 ya mwezi wa pili tuweze kufunga midaki miwili katika eneo hili la Azam Sealink na Lighter Key kwa ajili ya meli kubwa za mizigo zinazokwenda Zanzibar pamoja na Visiwa vya Comoro, ahsante.. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina swali moja la nyongeza; kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari baada ya Bunge hili kwenda kukitembelea kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza kwamba niko tayari ratiba itakavyoruhusu tutatembelea eneo hilo ili kuona kiwango cha uchakavu hicho kilichofikiwa.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru majibu ya Mheshimiwa Waziri ila nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa, wapo watalii wanaokuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta matibabu na tunao waganga wa jadi ambao wanaweza kutibu COVID kama vile Mheshimiwa Shekilindi. Swali langu ni kwamba Serikali ina mpango gani kwanza kuwawezesha waganga wa jadi kama hawa wenye ujuzi wa hali ya juu na kuwatangaza pia ili Pato la Taifa liongezeke? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nafikiri kama nimelisikia ni kwa namna gani tunaweza tukawasaidia waganga wa asili. Moja ni kwamba na kwa sababu kuna ushirikiano kweli na Wizara ya Maliasili kwa sababu baadhi ya vitu ambavyo vinatumika na watu wetu kama mizizi na vingine vipo kwenye maeneo ya maliasili.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ni kwamba tunaanza kuiweka rasmi na kuna tafiti zinazofanyika kuthibitisha hivyo vitu ambavyo waganga wa asili lakini tunajenga ukaribu na Wizara ya Maliasili kwenda kwa pamoja ili tuweze kuwasaidia. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika,ahsante sana, na nimpongeze Waziri kwa niaba ya Serikali kwa majibu mazuri sana, ila nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, hizi kilometa 25172.42 zilizo bakia ambazo zimejengwa kwa changarawe zitajengwa lini kwa lami na zitatumia muda gani?

Swali la pili bajeti hii ya bilioni 1.8 ninavyoamini ni pamoja na kujenga michirizi au mifereji ya maji sasa kuna maeneo ambayo mifereji hii haijajengwa hata hapa Mjini Dodoma; je, ni lini mifereji hii itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo : -

Mheshimiwa Spika,kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, fedha inayokadiriwa kukamilisha mtandao wa barabara ambazo zinahudumiwa na TANROADS ni takribani tirioni 45; na bado barabara zingine zinaendelea kupandishwa daraja kuja, kwa hiyo zitaendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Spika,na Serikali kusema ni lini tunaweza tukakamilisha ujenzi wa barabara zote kwa kiwango cha lami hii itaendelea kuwa ni kazi endelevu kadri fedha inavyopatikana. Kwa sababu, Mbunge atakubaliana nami kwamba bajeti tu ya nchi kwa mwaka ni zaidi ya tirioni 40 kwenda 41 kwa bajeti tunayoitekeleza sasa barabara hizi ni tirioni 45 kwa hiyo Serikali inajitahidi kujenga barabara kadri ya uwezo lakini hasa barabara zile za kipaumbele. Kwa hiyo kadri tutakavyoendelea tunahakikisha tutaendelea kupunguza idadi ya barabara za changarawe.

Mheshimiwa Spika,kuhusu swali lake la pili, ni kweli barabara zinajengwa lakini zingine hazina mitaro, lakini kipaumbele za kuweka mitaro hasa ni barabara ambazo ziko kwenye miji na maeneo ambayo wananchi wako wengi kwa ajili ya usalama. Na changamoto kubwa ambayo tunaipata kwenye uzibaji wa mitaro ni pale ambapo huduma za kijamii zinasababisha ile mitaro inaziba na basi maji hayo yanapanda kwenye barabara na kuharibu zile barabara.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nampongeza sana Waziri kwa majibu yake mazuri sana, Mwenyezi Mungu awawezeshe ila nina maswali mawili ya nyongeza.

Moja, hiyo mobile app ambayo iko asilimia 90 itakamilika lini ili kupunguza vifo vya wavuvi ambao wanakwenda kutafuta bila kujua wanatafuta nini na wapi? (Makofi)

Swali la Pili; hivi Serikali ilishawaeleza wavuvi wajibu wao kuhusiana na mobile app ambayo wanaingeneza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, hii application tayari imekwishakamilika, iko katika asilimia 90. Asilimia 10 hiyo ni ile ya kuangalia ule mfumo unaweza kufanya kazi kwa usahihi kiasi gani. Halafu, hatua ya pili itakuwa inajibu swali lake la pili kwamba, wavuvi kama wamekwishakujulishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mfumo huu kuwa umekamilika, tutaanza hatua ya kuwajulisha wavuvi wote ili kuweza kunufaika na utaratibu huo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi katika makundi mbalimbali. Ahsante.
MHE. KHAMIS MBAROUK AMOUR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri, kimsingi nina swali moja tu la nyongeza.

Je, Serikali ipo tayari kuwatambua hawa wajasiriamali wamachinga, nakusudia wa Tanzania nzima, wawe wa Tanzania Bara na Visiwani, halafu wakawaandalia mazingira ya kukopesheka benki? Je, Serikali ipo tayari kufanya hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khamis Mbarouk Amour, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshaanza kutambua wamachinga Tanzania nzima ikiwemo Visiwani, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anafuatilia sana suala hili, tutaongeza juhudi na kuweka mipango stahiki ya kuwatambua na kuwawezesha wamachinga wote ikiwemo upande wa Zanzibar ambao tunaamini wanatakiwa kupewa fursa sahihi ili waweze kuendelea kufanya biashara zao kwa ukamilifu na kwa ufanisi. Nakushukuru.