Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo (15 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wetu Dkt. John Joseph Magufuli. Pili, niunge mkono hotuba mbili zote alizozitoa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda ukurasa wa 12 wa hotuba ya kufungua hili Bunge, Rais alisema: “Nataka Watanzania wote washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao.” Tunapoongelea uchumi jumuishi hii ndiyo falsafa yenyewe ambayo Rais anatuelekeza katika hotuba yake. Hata hivyo, hatuwezi kuwajumuisha Watanzania wote katika kujenga uchumi wa nchi yao kama hatujawawekea miundombinu ya kutosha. Ili kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanashiriki katika uchumi wa nchi yao, lazima tuangalie sekta za kimkakati ambazo ni pamoja na kilimo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongelea kilimo, nchi yetu bado inategemea kilimo katika kuzalisha mazao ambayo tunauza nje. Tunayo mikoa ya kimkakati ambayo ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo na biashara. Hatuwezi kuwa na kilimo chenye tija kama tunaendelea na kilimo cha jembe la mkono na cha kutegemea mvua, jua na kiangazi, lazima twende kwenye kilimo cha umwagiliaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Muleba Kusini tunayo miradi miwili ya umwagiliaji maji. Tunao mradi wa Kyamyorwa ambao Serikali yetu Tukufu imeugharamia kushirikiana na wadau wengine, tekeo tayari, mfereji umejengwa, tumebakiza banio. Niiombe Wizara ya Kilimo ikamilishe mradi huu ili wananchi wa Kyamyorwa na Muleba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla wake waweze kufaidi na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi mwingine wa Buhangaza ambao umejengwa lakini haujakamilika. Hii miradi imetumia fedha za walipa kodi, niisihi, kuiomba na kuishauri Wizara ya Kilimo, miradi hii ikamilishwe ili iweze kuzalisha kulingana na pesa tulizoziwekeza pale ili wananchi wanufaike na miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera unapakana na nchi nyingi jirani kama Rwanda, Uganda na Burundi. Tukitumia fursa tulizonazo katika Mkoa wa Kagera ambaapo tunalo bonde la Mto Ngono ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo na uzalishaji mkubwa wa chakula, tukiweza kuwekeza katika bonde hilo Mkoa wa Kagera unaweza ukawa soko la chakula kwa ajili ya nchi zote zinazozunguka mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye sekta ya uvuvi. Sekta hii inaajiri vijana wengi na nitajikita katika Ziwa Victoria ambako mimi natoka. Ukiangalia kazi zinazoendelea katika Ziwa Victoria sisi kama Tanzania tunamiliki asilimia 51 ya ziwa lile, wenzetu wanamiliki asilimia 49, Uganda wana asilimia 43, Kenya wana asilimia 6 lakini ukiangalia mauzo nje ya nchi inaonekana sisi tunauza kidogo kuliko wenzetu ambao wanamiliki eneo dogo la Ziwa Victoria. Kwa nini inakuwa hivyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, jana kuna Mbunge hapa alichangia kuhusu sekta ya mifugo, ukiangalia kwa nini hatufanyi vizuri katika mauzo ya nje kama Rais anavyotuambia biashara ni vita, mfumo wa tuzo zinazotozwa kwenye mazao yanayotokana na uvuvi na ukilinganisha na nchi za jirani, sisi tozo zetu ziko juu sana. Niishauri Wizara ya Uvuvi kuhakikisha kwamba tunapitia tozo zote ambazo zinatozwa kwenye mazao ya samaki. Tuhakikishe kwamba zile tozo aidha zinalingana na nchi jirani au kwa kuwa tuna eneo kubwa la ziwa tunaweza tukafanya ujanja tuka under cut tuwe na tozo za chini ili tuweze kuvuna na kuuza nje mazao mengi ya uvuvi. Vinginevyo tutabaki nyuma, tutabaki kulalamika lakini jambo la msingi tupitie tozo kama nilivyoshauri ili tuweze kupata pesa za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye sekta ya uvuvi, Wilaya yangu ya Muleba ina visiwa 39 na visiwa 25 vinakaliwa na wavuvi. Ilipokuja hii ya sera ya kukamata wavuvi haramu, siwaungi mkono lakini nawaomba na nishauri Wizara ya Uvuvi, busara itumike tunapokwenda kwenye zoezi la kuwakamata wavuvi haramu. Kinachoendelea sasa imekuwa kama kukomoana na kuna kesi nyingi ambazo zinaendelea watu wanakamatwa, wanafunguliwa kesi na wakati mwingine kesi zenyewe ukiziangalia hazina hata ushahidi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bukoba tumejengewa Chuo cha VETA. Nimshukuru Rais wetu na Serikali yetu Tukufu. Nategemea Waziri wa Elimu, kati ya mitaala itakayoendeshwa kwenye Chuo kile cha VETA tuwe na mtaala ambao unawafundisha vijana wetu kutengeneza nyavu na vifaa ambavyo tunavitumia katika sekta nzima ya uvuvi kwa sababu Mkoa wa Kagera na Mikoa ya Kanda ya Ziwa inategemea sana uvuvi katika uchumi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga hoja mkono hotuba zote mbili na hotuba zote zilizotangulia kabla ya hizo. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wabunge wenzangu kumshukuru Rais wetu, hasa kwa pesa ambayo imeletwa kwenye majimbo yetu. Wakati unatoa takwimu za wanafunzi ambao wako darasa la nne nikawa naangalia kwenye Wilaya yangu ya Muleba, tunao zaidi ya wanafunzi 19,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwaka huu kabla Mheshimiwa Rais hajasema neno lolote, tulikuwa tunajiuliza Muleba kule hivi tunafanya nini na watoto ambao wamemaliza darasa la saba. Tukawa tumeanza ujenzi wa vyumba vya madarasa. Nashukuru kwa pesa ambayo ametuletea sasa tunao uhakika kwamba vijana wetu wa darasa la saba watapata madarasa wote na tuendelee kumshukuru Rais wetu kwa kazi nzuri anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango kwa hotuba yake. Pamoja na pongezi hizo, zaidi niwapongeze Kamati yetu ya Bajeti. Nimesoma maandiko yao yote na nipende kuwapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza zaidi kwenye sekta ambazo zinachochea uchumi katika majimbo yetu, hasa sisi tunaotoka vijijini. Mimi naomba nitoe ushauri wangu; kwa vipaumbele ambavyo napendekeza kwenye bajeti ijayo naomba tuangalie sekta ya kilimo, tuangalie sekta ya mifugo, tuangalie sekta ya uvuvi na usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamechangia sekta ya kilimo na wengi wamesema inachukua zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania ambao ni karibia milioni 22 ya Watanzania, wanajihusisha na masuala ya kilimo. Na tumeona mchango wa sekta ya kilimo kwenye uchumi wetu. Lakini ukiangalia bajeti ambayo tunaipatia kilimo, nadhani hatukitendei haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imependekeza kwamba bajeti tuliyonayo ya mwaka huu tuiongeze mpaka ifike zaidi ya bilioni 400. Kama tunataka kutoka hapa tulipo, sikubaliani na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, mimi napendekeza twende zaidi ya trilioni moja kwenye sekta ya kilimo ili tuweze kunusuru uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia uzalishaji wa mazao mengi per hector, mazao mengi tunazalisha chini ya kiwango kwa sababu hatujawekeza vya kutosha kwenye sekta ya kilimo. Ukiangalia mpango wa miaka mitano ambao tulijadili hapa mwaka jana tulikubaliana kwamba tunakwenda kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka ekari 500,600 kwenda milioni moja na laki mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia tulipo leo, tuna miaka mitatu kufikia mwaka 2025 ambako ndiyo target yetu, bado tunaekari 569,000 lakini lengo letu ni kufikia ekari milioni moja na laki mbili, kwa miaka mitatu iliyobaki tunakwenda kufanya muujiza gani ili tuweze kufikia hilo lengo letu. Tusipoongeza bajeti ya kilimo tutabaki tunaimba wimbo uleule, tutabakia hapohapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia uzalishaji kwa mfano wa mafuta ya kula. Mpaka leo tunapoongea ni aibu kwa nchi hii ambayo tunasema wakulima ni zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wote, bado tunaagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Naomba kwenye mpango huu Waziri wa Fedha atupatie mkakati wa nchi ili kuinusuru nchi hii kutokana na kuagiza mafuta kutoka nje wakati tunalima na wakati nchi hii tunasema ni nchi ya wakulima na ni nchi ya wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mikoa wamekuja na mazao mapya. Kwa mfano Kagera kule tuna mazao mapya ya vanilla, kwa mfano. Wakulima wamejitahidi wanalima lakini hatuna masoko. Na Wabunge wengi hapa wamesema tunapowekeza kwenye kilimo tuhakikishe kwamba tunawekeza kwenye utafiti, tunawekeza kwenye kutafuta masoko tusije tukatumbukia kwenye janga ambalo tulinaswa nalo hapa juzi wakati tunahangaika kutafuta pesa ya kununua mahindi kutoka kwa wakulima. Naomba tunapohamasisha wakulima wetu wazalishe kwa wingi na Serikali ihakikishe kwamba inatafuta masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi; mwaka jana wakati nachangia hapa nilisema nchi yetu imebahatika kuwa na maziwa na bahari, lakini ukiangalia mchango unaotokana na mazao ya uvuvi na yenyewe bado ni aibu. Ni aibu kwa nchi kama Tanzania tunapoagiza samaki kutoka nje ya nchi kwa kutumia pesa ya nje ni aibu kwetu. Naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri kwenye mpango tutakaokwenda kutunga sasa kutengeneza bajeti, atuambie tuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba sekta ya uvuvi na mazao ya uvuvi yanachangia kwenye pato la Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea mwaka jana hapa, na ninaomba nirudie niliyoyasema; tumejifunga na kanuni na sheria ambazo zinarudisha uchumi wetu nyuma. Ukiangalia tozo tulizonazo kwenye sekta ya uvuvi, ukilinganisha Tanzania na nchi jirani, hasa zile tatu ambazo tuna-share Ziwa Victoria kwa mfano, kodi zetu hazikubaliki na hazibebeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache tu, ukiangalia tozo ambazo sisi Tanzania tunatoza na wenzetu, majirani zetu, kwa mfano ukiangalia VAT Tanzania tozo yetu ni shilingi 552 wakati jirani yetu Uganda anatoza 115, mwenzetu Kenya anatoza shilingi 34. Matokeo yake ni nini; mazao mengi ya uvuvi yamekuwa yakielekezwa upande wa pili na sisi tumekuwa tukikosa kazi, na hasa vijana wetu ambao wame- invest kwenye sekta ya uvuvi hawawezi kufanya kazi kwa sababu hawawezi kushindana na wenzao ambao wako nchi jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata viwanda vya kuchakata minofu ya samaki. Miaka ya nyuma Tanzania tulikuwa na viwanda vingi lakini kutokana na hizi sheria tulizojiwekea, tozo, sheria mbalimbali, vibali na nini, viwanda vyote vimehamia nchi za jirani, tumebaki na viwanda vichache hapa. Ni lazima tujiulize tumejikwaa wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapoongea tumebaki na takribani viwanda nane. Uganda wana viwanda zaidi ya 20, Kenya wana zaidi ya viwanda vitano, na vyote vimehama vimekimbia kutoka hapa kwa sababu ya mfumo tulionao wa biashara, mfumo wa tozo na mfumo wa sheria tuliyojiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza kwa nini mpaka leo tunapoongea unapotaka kusafirisha mazao ya uvuvi lazima yasafirishwe kupitia Viwanja vya Ndege vya Entebbe na Viwanja vya Jomo Kenyatta, Kenya, mazao ya uvuvi yanayotokea Tanzania. Tuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba sasa badala ya kusafirisha kwenda Entebbe na Nairobi, kwa nini tusitumie Viwanja vyetu vya Mwanza, Dar es Salaam au KIA? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mwanza tumejenga facility kwa pesa ya walipa kodi, facility nzuri hata inazidi Jomo Kenyatta International Airport, lakini hatuitumii. Na sote tuko hapa tumekaa hatujishughulishi na hatujiulizi kwa nini hiyo facility ambayo tumeigharamia haitumiki. Na mwaka jana niliongekea hapa lakini tumemaliza tumerudi nyumbani, kila kitu kimeendelea business as usual. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tubadilike, kama tunataka kuingia kwenye soko la ushindani na kwenye mpango tumesema tunakwenda kujenga uchumi shindani na uchumi shirikishi, tunaujengaje kama hatuwezi ku-strain our minds tukafikiri nje ya boksi ile tuweze kunusuru nchi yetu na kuhakikisha kwamba hii sekta ya uvuvi ambayo tumebarikiwa, ni mali ya Watanzania, ili iweze kutusaidia kuchangia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo kundi la vijana, sijaona kwenye mpango. Ukienda huko vijijini tunakundi la vijana ambao wakiamka asubuhi hawana kazi ya kufanya, mchana hawana kazi ya kufanya, mpaka jioni hawana kazi ya kufanya. Naomba kwenye mpango huu Serikali ije na mkakati hawa vijana tunawafanyaje.Vinginevyo tunatengeneza bomu ambalo miaka kumi, sihirini ijayo, litakuja kutulipukia wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mpango uangalie kama ni mikopo ambayo tunaitoa kwenye halmashauri zetu ya kuwasaidia hawa vijana, hii asilimia nne ambayo tumejipangia haitoshi. Lazima tuangalie mkakati wa kuwanusuru hawa vijana na kwa kufanya hivyo tuweze kuwashirikisha kwenye uchumi wetu…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii nami nichangie hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa nikupongeze wewe kwa kazi unayofanya ya kuliongoza Bunge letu. Vile vile nimpongeze Rais wetu kwa kuliongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana wachangiaji wengi waliongelea mambo makubwa ambayo Taifa letu linayapitia. Sisi kama Kamati ya PIC, kazi tunayoifanya ni kupitia uwekezaji wa mitaji unaofanywa na Serikali yetu kwenye mashirika yetu ya Umma. Katika mashirika ambayo yako chini ya TR yanafika zaidi ya 237 na haya yote Serikali inawekeza pesa ya walipakodi kwa lengo la kuboresha hayo mashirika na kutengeneza fedha.

Mheshimiwa Spika, katika uchambuzi wetu tumepitia mashirika na baadhi ya ripoti za TR na ripoti ya CAG, takwimu zinaonesha kwamba mashirika yetu yanafanya vizuri. Mpaka mwaka 2021 mitaji ambayo imewekezwa na Taifa letu kwenye hayo mashirika inanafikia Shilingi trilioni 67.95. Huo ndiyo utajiri ambao uko chini ya mashirika ya Umma.

Mheshimiwa Spika, ukisoma takwimu, thamani ya uwekezaji wetu katika mashirika haya umekuwa ukipanda lakini ongezeko hilo limekuwa likipungua. Kwa mfano, mwaka 2016/2017 thamani ya mashirika yetu ilikuwa ni Shilingi trilioni 49.6, imeendelea kupanda mwaka 2017/2018 imekwenda Shiligi trilioni 57.79, mwaka 2018/2019 imekwenda Shilingi trilioni 60.3, mwaka 2019/2020 Shilingi trilioni 65.19, na mwaka 2021/2022 Shilingi trilioni 67.79.

Mheshimiwa Spika, kwenye ukuaji wa ongezeko la thamani ya mifuko imekuwa ikishuka. Tunayo sababu ya kujiuliza, kwa nini uwekezaji unaongezeka lakini ongezeko au ukuaji wa ongezeko unashuka? Mwaka 2016/2017 ongezeko lilikuwa ni 63.8%, mwaka 2017/2018 ilishuka ikaja kuwa 13.6%, mwaka 2018/2019 ilishuka mpaka 8.1%, mwaka 2019/2020 ilibaki pale pale 8.1%, na mwaka 2021 ilishuka ni 4.2%. Tunao wajibu wa kujiuliza kwa nini inashuka hivyo? Tusipojiuliza leo, baada ya miaka miwili au mitatu inawezekana tukaja zero tukaanza kwenda kwenye hasi tusipochukua hatua leo.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia haya mashirika yote, yako chini ya usimamizi wa Treasure Registrar (TR). Ukiangalia sheria inayomwanzisha wa Treasury Registrar ya Tanzania ni ya mwaka 1957, ni ya zamani sana, ni sheria kongwe. Imefanyiwa marejeo chini ya Miscellaneous Amendments Act, 2010. Ila yaliyofanyiwa marekebisho hayampi TR wetu uwezo madhubuti wa kusimamia haya mashirika. Ukiangalia, TR anatoa vigezo vya utendaji wa haya mashirika ya Umma lakini haimpi nafasi; haya mashirika ya Umma yasipotekeleza vile vigezo anavyoviweka, TR hana mamlaka ya kuwajibisha haya mashirika ya Umma. Hicho ni kikwazo kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukirejea hiyo sheria ambayo nimeiongelea, ni kongwe, ni ya zamani, na ukiangalia umuhimu wa uwekezaji kwenye haya mashirika, TR anapaswa kuwa na nguvu madhubuti ya kuyasimamia haya mashirika. Taasisi yoyote ambayo inashindwa kutekeleza hivyo vigezo alivyoviweka, lazima ayawajibishe ipasavyo, vinginevyo yataendelea kushuka na tutaendelea kupoteza mitaji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mashirika ambayo tusipoyaangalia vizuri ni cash cow ya Taifa hili. Mashirika kama TPA; mashirika mengi ambayo tukiwekeza vya kutosha, tutaweza kutengeneza mitaji na Taifa litaweza kujitegemea kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viko vikwazo vingi ambavyo vinafanya mashirika yetu yasifanye vizuri. Mojawapo ya hivyo vikwazo ni sheria yenyewe. Napendekeza Bunge hili liitishe hiyo Sheria ya TR, Tuifanyie marekebisho. Kwa upande wangu ningependa tuifute kabisa hiyo sheria tuanze upya, TR apewe mamlaka kwenye haya mashirika ambayo anayasimamia, awe na nguvu kiasi kwamba bodi ambazo zinashindwa kufanya vizuri, wakurugenzi ambao wanashindwa kufanya vizuri awawajibishe yeye mwenyewe, akisubiri mamlaka za uteuzi kuteua bodi mpya na kuteua wakurugenzi wapya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mamlaka nyingine, kwa mfano, Ofisi ya TR Malaysia, TR ana uwezo uwezo mkubwa sana kusimamia mashirika ya Malaysia. Ukiangalia performance ya mashirika hayo yanafanya vizuri kiasi kwamba TR ana uwezo wa ku-suspend mamlaka yoyote ambayo iko chini yake bila kuuliza mtu yeyote. Ana mamlaka ya kufanya hivyo, baadaye anaandika ripoti kwa mamlaka za uteuzi, zinachagua mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Spika, ripoti yetu imebaini pamoja na mambo mengine, kuzorota kwa utendaji wa mashirika ya Uumma kunasababishwa na mambo kadha wa kadha. Mojawapo, limetokea kwenye ripoti ya CAG ukurasa wa 13 kwamba mashirika mengi uteuzi wa bodi unachelewa. Baadhi ya mashirika yanafanya kazi chini ya wakurugenzi ambao hawana bodi na baadhi ya mashirika yametajwa. Kwa mfano, Mfuko wa Kulinda wanyamapori Tanzania; Hospitali ya Rufaa Mbeya, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Hayo ni baadhi ya mashirika ambayo yametajwa na ripoti ya CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukijiuliza kwa nini tunakuwa na mashirika ambayo hayana Bodi za Wakurugenzi? Mnajua fika, kama taasisi haina Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi na Watendaji wote hawawezi kufanya maamuzi ya kuliendeleza hilo shirika, watabaki tu ku-suspend maamuzi kwa sababu hawana chombo cha kuwa-guide. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine ambalo limebainika ni mwingiliano wa majukumu kwenye baadhi ya taasisi. Jana nadhani Mheshimwia Dkt. Chaya aliyasema hapa. Baadhi ya taasisi zetu zinaingiliana kimajukumu. Jana ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Chaya alisema, TANROADS na TAA, kwamba tuna mamlaka mbili; tuna TANROADS ambayo kazi yake kubwa na ya msingi ni kutengeneza barabara. Ila hapo nyuma tumefanya maamuzi tukaipa TANROADS kutengeneza viwanja vya ndege, lakini tuna Mamlaka ya Kutengeneza Viwanja vya Ndege ambayo ni TAA.

Mheshimiwa Spika, utengenezaji wa viwanja vya ndege na usafiri wa anga kwa ujumla, kwa wataalam mnajua, usafiri wa anga unaendeshwa kwa misingi ya Kimataifa pamoja na miundombinu yake TAA na ujenzi wa viwanja vya ndege uko chini ya mamlaka ambayo inaitwa ICAO, ni mamlaka ya Kimataifa. Hii ndiyo inatoa viwango na vigezo. Kama unavyojua TAA inakuwa regulated na Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Sasa unashangaa, ukijiuliza huyu TANROADS anajenga viwanga vya ndege kwa mamlaka ipi na kwa vigezo vipi?

Mheshimiwa Spika, nimesikia wakati tunaongea kwenye Kamati, TANROADS walikuja pale, wakasema wamechukua wataalam wote kutoka TAA wamewapeleka TANROADS. Najiuliza, kwa nini uchukue wataalamu kutoka TAA uwapeleke TANROADS? Kwa nini hiyo kazi ya kujenga viwanja vya ndege ambayo kisheria ipo chini ya TAA, wewe unafanya kazi ya kuhamisha watumishi na kuwapeleka kule. Hii inatupa wakati mgumu na inawapa mamlaka za udhibiti wakati mgumu hasa TCAA ambayo imekasimiwa jukumu la kuhakikisha kwamba viwanja vya ndege vinajengwa kulingana na mikataba ya Kimataifa ambayo inatolewa na ICAO kupitia Chicago Convention Annex 14 ambayo inakwambia viwanja vya ndege vijengwe kwa viwango vipi na ubora upi? Sasa hii tumeikasimisha TANROADS.

Mheshimiwa Spika, naomba ujenzi wa viwanja vya ndege urudi TAA na TANROADS wafanye kazi yao ya msingi ya kujenga barabara, siyo viwanja vya ndege. Kuna maeneo wanasema pale kwamba uwanja wa ndege ni sawasawa na kujenga barabara, siyo hivyo. Kila mwaka tunakuwa na ukaguzi ambao unafanywa na ICAO, tutakwenda mbele, tutafika wakati ICAO itatu-blacklist, ndege za Kimataifa zitashindwa kuja hapa na tutakuja kufanya marekebisho tumechelewa.

Mheshimiwa Spika, nadhani wakati wa kufanya marekebisho ni sasa, ujenzi wa viwanja vya ndege urudi TAA na TANROADS iendelee na majukumu yake ya kisheria. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, zao la kahawa mkoa wa Kagera limegubikwa na tatizo la mfumo wa soko. Soko linaua zao la kahawa Kagera. Mfumo wa AMCOS ni hatari kwa ustawi wa zao la kahawa Kagera. Nashauri tufungue milango kwa wafanyabiashara, turuhusu wafanyabiashara binafsi kwa ajili ya kukuza ushindani wa zao hili. Stop protectionism ya AMCOS. Serikali kupitia Tume ya Ushindani iweke mazingira shindani kwa ustawi wa soko na uchumi wa nchi yetu.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. Kwanza kabisa nitamke tu kwamba naiunga mkono hoja, lakini mimi ni muumini wa uchumi wa soko na ninashukuru kwenye mpango tulioletewa sura ya tatu unaongelea ushiriki wa sekta binafsi kama chachu ya uchumi shindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kidogo nitaongelea sekta ya kilimo. Kilimo kama tunavyosema ni uti wa mgongo wa nchi hii au Taifa letu, lakini ukiangalia maendeleo ya kilimo chetu hayaoneshi kwa vitendo kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa hili, nikiangalia kwenye mpango wenyewe tumeambiwa kilimo mpaka sasa kinachangia asilimia 27 ya GDP, lakini pia kinachangia asilimia 24 ya mauzo nje ya nchi. Nikilinganisha na nchi jirani nchi nyingine ndogo ambazo ukiangalia ukubwa wa Taifa lenyewe wao kilimo kinachangia asilimia 35 ya GDP na asilimia 40 ya mauzo nje ya nchi. Tunayo kazi kubwa ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo chetu kimebubikwa na mambo mengi ambayo nadhani katika mpango huu lazima tuyapatie wajibu, mojawapo ya haya matatizo tuliyonayo Taifa letu limekumbwa limekumbwa na ugonjwa wa kanuni na tozo nyingi kwenye sekta hii, kanuni zetu zimekuwa mnyororo zimekuwa broke ya kutufanya tusonge mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ninayotoka zao kubwa tulionalo ni zao kahawa, lakini zao hilo wakulima wanalima, wanajitahidi, wanakwenda kuuza na kanuni tuliyonayo mpaka leo kwamba mkulima akishalima lazima auze kwenye vyama vya msingi/ vyama vya ushirika na anapokwenda kuuza anayo matatizo yake, lakini awezi kulipwa pesa itabidi asubiri mwezi moja, wa pili, wa tatu na wakati mwingine miezi minne, lakini wakati huo huo tunavyo viwanda vinavoongeza thamani ya kawaha.

T A A R I F A

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO:Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea zao la kawaha Wilaya Muleba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla kwamba kulingana na kanuni tulizonazo kwamba mkulima hawezi kuuza kahawa yake moja kwa moja kwa wafanyabiashara katika mkoa huo, lakini wakati Naibu Waziri wa Kilimo akijibu swali baadhi ya mazao wanaruhusiwa na pale Muleba wapo wafanyabiashara ambao wamewekeza kwenye kusindika zao la kahawa, lakini hawaruhusi kuuza kahawa hiyo moja kwa moja kwenye vile viwanda na kama tunavyofahamu kilimo na viwanda lazima tuvioanishe, matokeo yake wenye viwanda wanalazimika kununua kahawa hiyo kutoka vyama vyetu vya msingi kwa bei ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inayo madhara makubwa sana kwa uchumi, kwanza bidhaa wanayozalisha kutokana na kupata malighafi kwa bei ya juu haiwezi kushindana kwenye soko, lakini pia wakulima ambao wanauza bidhaa yao kwenye vyama vya msingi hawapati bei nzuri na wakati mwingine inawachukua muda kulipwa pesa yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni muda muafaka sasa kuruhusu wafanyabiashara ambao wamewekeza kwenye viwanda ambavyo vinasindika mazao yanayopatikanika katika maeneo mahalia badala ya kufungwa na kanuni ambazo zinazorotesha na kuumiza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taasisi ambazo zinashughulika na masuala ya ushindani, tuziruhusu kampuni binafsi zishindane na vyama vyetu vya ushirika na vyama vyetu vya msingi ili kuleta tija katika masoko yetu na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine na lamsingi na nzuri tukiwaruhusu wafanyabiashara hao kununua mazao moja kwa moja kutoka kwa wakulima ambao ni zao la kahawa, watahakikisha kwamba wanawapa pesa nzuri lakini pia wanaweza kuwafuatilia wakulima wale kuhakikisha kwamba wanazalisha na wanapatia msaada kuhakikisha kwamba mazao yao na mashamba yao yanakuwa bora muda wote na kilimo kinakuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipatia fursa hii niweze kuchangia kwa dakika tatu kwenye hoja iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuja hapa Bungeni nilimueleza Mheshimiwa Waziri kwamba katika Jimbo la Muleba na Wilaya ya Muleba kwa ujumla tunayo changamoto kubwa ya mawasiliano na kwa heshima kubwa nilimpatia maeneo yote ambayo yana matatizo ya mawasiliano. Hata hivyo, leo wakati nasoma hotuba ambayo ameiwasilisha mbele yetu nimeshangaa sana, hakuna hata kata moja ambayo imezingatiwa kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kati ya kata zote ambazo nimempatia, kama mchangiaji aliyetangulia kusema Mkoa wa Kagera tunalo tatizo kubwa la mawasiliano, naomba chonde chonde atusaidie. Kata zote ambazo tumekupatia na sisi kama Mkoa wa kagera tunapaswa kuwa na usikivu wa mitandao, redio ambazo zinachangiwa na walipa kodi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo unakwenda ukipotea tu huwezi kupata msaada. Tunapoongelea Kata za Karambi, Mmbunda na Buhigi hakuna mawasiliano hata kidogo. Nilikuwa na dhamira ya kushika shilingi lakini najua Mheshimiwa Waziri ni msikivu nakuomba utakapokuja kuhitimisha bajeti yako useme neno ili wakazi wa Mkoa wa Kagera roho zao zitulie kwamba tunakwenda kuwawekea mitandao au mawasiliano ili na wao wajisikie wanaweza kuwasiliana na Watanzania wenzao na dunia nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupewa fursa hii ya kuchangia Mpango huu. Nitajikita kwenye maeneo mawili; nitaongelea kilimo na uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango, umeongelea kwa kina suala zima la kilimo. Kama Wabunge wengi walivyochangia, kilimo ndiyo sekta pekee ambayo inaakisi uchumi jumuishi; inaajiri Watanzania zaidi ya asilimia 65. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyosema, kilimo hatujakipatia msukumo ambao kinastahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea zao moja. Kama Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma wanavyosema, kwa Mkoa wa Kagera zao la kahawa ni siasa, zao la kahawa ni elimu, zao la kahawa ni kila kitu. Miaka ya 1970 Mkoa wa Kagera ulibahatika kuwa na wasomi wengi kwa sababu ya zao hili la kahawa. Leo tunapoongea, Kagera zao la kahawa limekuwa kama laana. Bei imeshuka na wanapouza hata bei kama ni ndogo, bado kupata hela zao inawachukua zaidi ya miezi mitatu kama dada yangu Mheshimiwa Conchesta alivyosema pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa kwa Mkoa wa Kagera linahusisha kaya nyingi kama ilivyo kwa Taifa zima. Nilikuwa naangalia takwimu hapa. Zaidi ya 90 percent ya kahawa inazalishwa na wakulima wadogo wadogo. Hawa wakulima wadogo wadogo ndio wazazi wetu, kaka zetu, wadogo zetu, ambao wanahangaika usiku na mchana kuhakikisha kwamba wanapata pesa ya kusomesha watoto wao, kutunza familia zao na kuhakikisha kwamba wazazi wao wanaendelea kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo liko wapi? Naishukuru Serikali, kwa miaka mitano iliyopita walifuta tozo karibia 20 kwa zao la kahawa, tunawashukuru kwa hilo, lakini walipofuta hizi tozo, hatujatafuta suluhisho la bei na mauzo ya zao la kahawa, tumeviachia vyama vya msingi vinunue kahawa kutoka kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sekta binafsi, tunaihusishaje kuhakikisha kwamba na wao wananunua kahawa kwa Mkoa wa Kagera ili kuleta ushindani? Tumeviachia vyama vya msingi peke yao, vinafanya kazi vinavyotaka vyenyewe, vinalipa wakati vinapotaka vyenyewe. Hata hivyo, kuna wazawa wa Tanzania ambao wamewekeza kwenye viwanda vya kusindika kahawa, tunawaambia hao kama unataka kununua kahawa, kanunue kwenye vyama vya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atuambie, tunaoanishaje kilimo na Sekta ya Viwanda? Unapowaambia wanunue kwa vyama vya msingi, watanunua kwa bei ya juu kuliko wangekwenda moja kwa moja kununua kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna maneno hapa yanasemwa, eti watakwenda kuwalangua wakulima. Ndiyo! Wakalangue kule, lakini Serikali ihakikishe kwamba inaweka mazingira sahihi na mazingira huru kuhakikisha kwamba vyama vya msingi vinanunua na wafanyabiashara wananunua bila kuwaathiri wakulima wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango namshukuru Waziri, amesema tunakwenda kujenga uchumi shirikishi na uchumi shindani. Tunayo Sheria ya Ushindani hapa nchini, tuweke mazingira huko kwenye vijiji vyetu kuhakikisha kwamba hata huyu; vyama vya msingi na vyama vya ushirika vishindanishwe na wakulima na wanunuzi binafsi ili kuleta uwiano na ushindani kwenye masoko yetu. Tusimlinde huyu. Mnajua madhara ya uchumi hodhi? Mnajua matatizo ya protectionism? Tumevilinda kwa muda mrefu vyama vya ushirika na vyama vya msingi na tunajua matatizo yake kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaporuhusu ushindani, tunakaribisha ubunifu, tunakaribisha teknolojia na tunakaribisha wakulima wapate a fair deal kwa mazao yao wanayoyalima huko kwenye majimbo yetu. Nawaomba ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane kuhakikisha kwamba baadhi ya sheria na Mashirika ambayo hayatuongezei ufanisi kwenye maeneo yetu tunakotoka, aidha, sheria zao wazilete hapa tuzipitie upya kuona kama zinatuongezea ufanisi au tufute. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nilikuwa nasoma kitabu kimoja wachumi wanakifahamu vizuri sana, “Why Nations Fail? The Origins of Power, Prosperity and Poverty.” Mwandishi anatuambia na kutushauri, kama tuna mashirika ambayo hayana ufanisi, tunakaribisha umasikini kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, nishauri kwenye hili, Wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi tuhakikishe suala la zao la kahawa Mkoa wa Kagera lipatiwe ufumbuzi wa haraka, watu wapate bei nzuri na sekta binafsi ihusishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, tatizo tulilonalo kwenye hili zao lenyewe la kahawa kutoroshwa kuuzwa nchi za nje litakwisha. Pia, tutakuwa tumeboresha Sekta ya Viwanda; kwenye jimbo langu tunavyo viwanda viwili vinasindika mazao ya kahawa, lakini wanalazimika kununua tu kwenye vyama vya msingi kwa bei ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni uvuvi. Tunalo Ziwa Victoria ambalo linazalisha, lakini ukiangalia takwimu za uvuvi na faida tunayoipata kutoka katika ziwa hili ni aibu. Sisi kama Tanzania, niliwahi kulisema hapa mwezi wa Pili. Tunamiliki eneo kubwa zaidi ya kilomita za mraba 35,000 ambazo ni sawa sawa na asilimia 51 na wenzetu asilimia 43; lakini ukiangalia tunachokipata na tunachokiuza nje, hakuna uwiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa nilikuwa nasoma ripoti moja, tumeambiwa sisi tunauza nje kwa asilimia 51 ukilinganisha na majirani. Kwa uchumi wetu tunachangia only two percent ya GDP, Uganda 3%, Kenya 2% na wenyewe. Ukiangalia viwanda ambavyo vimejengwa, Uganda wanaongoza, wana viwanda zaidi ya 20; sisi ambao tuna asilimia 51 tuna viwanda vinane tu na Kenya wana viwanda vitano. Tunaambiwa viwanda vinazidi kuporomoka kwa upande wetu na vinazidi kuongezeka Kenya na Uganda wenye eneo dogo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunafanya hayo na sisi tuko hapa? Kazi kubwa tunayopaswa kuifanya kama tunataka kuchochea uchumi, ni kuhakikisha tunavuna hizi fursa ili wananchi wetu waweze kuchangamkia uchumi wetu. Hata mazao tunayoyapata kutokana na uvuvi ili yasafirishwe kupelekwa kwenye masoko ya nje, yanapitishwa Uganda na Kenya; Entebe na Jomo Kenyatta International Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma tulifanya maamuzi mabaya, tuliweka a five percent surcharge kwa total consignment ya minofu ya samaki kutoka Mwanza. Ilifikia mashirika yote ya ndege yakakimbia. Mpaka leo ili tusafirishe minofu ya Samaki, lazima twende Entebe au Jomo Kenyatta International Airport. Kwa nini, Mheshimiwa Naibu Waziri? Ukiangalia chanzo chake ni tozo tulizojiwekea sisi wenyewe na tulizipitisha hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea tu, mabondo; ili usafirishe mabondo tuna tozo ya shilingi 7,500/= kwa upande wa Tanzania; Uganda ni shilingi 436/= na Kenya ni shilingi 34/=. Ukipitia tozo zote kwa upande wa samaki na mazao ya uvuvi, sisi tuna tozo ambazo hazibebeki na hazihimiliki na matokeo yake tunapoteza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitachangia zaidi kwenye sekta.

Mheshmiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami nichangie kidogo hii hoja ambayo iko mbele yetu. Niwapongeze Mawaziri kwa kazi yao nzuri, lakini ninazo hoja mbili. Nitaongelea Sheria ya Bima, tunapoisoma pamoja na Sheria ya Usalama Barabarani. Sheria ya Bima hasa inapokuja kwenye makosa yanayotokana na ajali za barabarani, inayo matatizo makubwa sana na ukiisoma hii sheria ya bima, ajali inapotokea barabarani, Jeshi la Polisi watakwenda watapima, kesi itapelekwa mahakamani, tutasubiri hukumu itoke na wote tunajua, ni mashahidi hukumu zetu zinachukua muda gani! Hukumu ikishatoka yule muhanga wa ajali ya barabarani ndio anaweza akaambatanisha ile hukumu kwenda kudai fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ni kwamba anapokwenda kudai ile fidia, Sheria ya Bima iko kimya anakwenda kulipwa kiasi gani, ni maamuzi ya kampuni ya bima. Tumeshuhudia ndugu zetu wengi wakipoteza maisha yao kwa sababu, ajali inapotokea baadhi ya familia zetu tunazijua ni masikini, hawana hata pesa ya kumtibia huyu muhanga wa ajali ya barabarani. Wanaanza kuchangishana ukoo mzima ili kupata hela ya kumpeleka hospitalini. Anapokwenda sasa kudai ile fidia/compensation ambayo inalipwa na kampuni ya bima, anakwenda pale wanamwambia tunakupa shilingi laki tano. Ni maamuzi ya kampuni ya bima ndio inaamua amlipe kiasi gani, mtu ametoka Kagera na tunajua makampuni makubwa ya bima yapo Dar es Salaam au hapa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anatoka Kagera analipa nauli anakwenda Dar es Salaam anaambiwa tunakupa shilingi laki tano, hatuwatendei haki watu wetu. Niwaombe Sheria ya Bima ya Tanzania itoe kima au kiwango cha chini, ambacho mtu anapopoteza maisha katika ajali ya barabarani anapaswa kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria nyingine si kwamba hatuna mifano, tunayo mifano. Usafiri wa anga mtu anapokufa akiwa kwenye ndege, sheria zetu pamoja na kanuni za TCAA za usafiri wa anga za mwaka 2008 zinatoa kima cha chini ambacho mtoa huduma anapaswa kumlipa muhanga wa ajali anapokuwa kwenye ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma regulation 24 ni 120,000 USD tunajua hiyo hatuna shida nayo. Lakini usafiri wa majini, nayo ukisoma Shipping Merchant Act kipengele cha 352 kimetoa kima cha chini ambacho muhanga wa ajali ya usafiri wa majini anapaswa kulipwa endapo atapata kifo au ajali au kupoteza mali zote akiwa kwenye meli.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hiyo Sheria ya Usafiri wa Majini (Merchant Shipping Act), ukiisoma ni kichekesho tu, haitekelezeki. Niwaombe Tume ya Kurekebisha Sheria; twenda tukaipitie hiyo Sheria. Unaposema mtu akifa kwenye meli anapaswa kulipwa units wanasema laki 333 units of account nikalifuatilia kuangalia hizi laki 333 units of account maana yake ni nini? Nikaenda kupata kwamba hizo ni sawasawa na one special drawing like the SDR. Na SDR moja ni sawasawa na Euro moja, ni kampuni gani ya Kitanzania inayoweza ikalipa hizi fedha? Haipo!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, na Sheria hiyo tunayo, likitokea la kutokea, hatuwezi kuya-enforce kwasababu ya ugumu wake. Lakini tunajua kwamba hii Sheria ukiisoma na Sheria ya Australia ni cut and paste. Kwa hiyo, niiombe Tume ya Kurekebisha Sheria ipitie hii sheria iweze kuiweka katika viwango ambavyo ni vya kitanzania ambavyo ikitokea ajali hii inaweza ikalipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudi kwenye masuala la ajali za barabarani. Naomba niishauri wizara, twenda tukapitie Sheria ya Bima tuioanishe na Sheria ya Usafiri wa Barabarani Road Traffic Act, tuje na mapendekezo au kiwango ambacho kinahimilika ili watanzania wenzetu wanapopata ajali waweze kulipwa kama sheria inavyosema to compensated adequately lakini sheria ilivyo hatuwatendei haki Watanzania. Tusiyaachie Makampuni ya Bima yaamue juu ya maisha ya Watanzania wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri mwingine kuhusiana na hii, wananchi wetu wanapopata ajali wakati wanasubiri kesi iende mahakamani ihukumiwe, hapa katikati hatuna chombo cha kuwahudumia tunajua wengi hawawezi kujihudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri wizara tuunde chombo ambacho kitachangiwa na makampuni yote ya Bima mtu anapopata ajali leo, kile chombo kitoe fedha zikamuhudie huyu mhanga wa ajali wakati tunasubiri Shirika/ Makampuni ya Bima kumlipa, atakapolipwa zile fedha ambazo tutakuwa tumempatia kumuhudumia basi tutazikata kurudisha kwenye mfuko ambao nashauri na kupendekeza uundwe chini ya sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo janga lingine, tunayo Sheria ya TASAC. Tulitunga hapa Bungeni lakini ukiisoma leo katika mazingira ambayo leo tunasema tunakwenda kujenga uchumi shindani; ile sheria ni janga la Kitaifa. Nashauri hii sheria tukaipitie upya, haileti ustawi wa sekta binafsi kwenye usafiri wa majini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema TASAC ni mdhibiti na tunajua udhibiti tulionao Tanzania tuliochagua kuuchukua ni udhibiti wa pamoja; lakini TASAC yenyewe ukiiangalia imeunganisha shughuli za kiudhibiti na shughuli za kutoa huduma. Huwezi ukawa referee wakati huo huo unacheza mpira uwanjani ni makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza na kushauri, shughuli za kiudhibiti ambazo ziko chini ya hii sheria zitenganishwe tuwe na mamlaka na chombo ambacho kinaangalia masuala ya udhibiti wa usafiri wa majini na tuwe na kampuni ambayo itatuangalizia kwa nia ileile ambayo tulikuja na hii sheria ya TASAC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua zamani tulikuwa na NASACO, turudishe mfumo uleule lakini tuwe na chombo ambacho kinafanya kazi ya udhibiti peke yake na chombo ambacho kinafanya biashara. Na misingi ya udhibiti, mdhibiti ana hadhi ya kimahakama na hawa wengine wote ambao wanafanya zile shughuli wanapokuwa na matatizo wanakuja kwa mdhibiti ili akawapatie suluhu ya matatizo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapokuwa na Taasisi ambayo kimsingi ni mdhibiti, ni mahakama, lakini na yeye anafanya zile shughuli inakuwa ni kinyume na utawala bora inapokuja kwenye kusuluhisha matatizo yanayojitokeza kwenye hiyo sekta. Niiombe Tume ya Kurekebisha Sheria, iiangalie hii sheria; badala ya kuleta ustawi nadhani maoni yangu inakwanza ustawi wa sekta hii ya usafiri wa majini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache naomba niunge hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupewa nafasi hii kuchangia Wizara yetu muhimu ya Elimu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nipeleke salamu kwa Waziri, Wilaya ya Muleba inakupenda na inakupongeza sana, kuna shule yako inaitwa Profesa Ndalichako; wamenituma nikuambie usiwasahau. (Makofi)

SPIKA: Imekuwa ya ngapi kwenye matokeo? (Kicheko)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, anajua mwenyewe Waziri wa Elimu. (Kicheko)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, lakini hizo salamu ni kwamba bado wanamhitaji sana na wanahitaji ulezi wake wa kimama na wa kiuwaziri.

Mheshimiwa Spika, nitajikita kwenye COSTECH. Jana kwenye mjadala hapa liliibuka suala la gongo na konyagi kwamba hao watu wanaotengeneza gongo na konyagi mara nyingi wanakimbizana na polisi kwamba ile ni bidhaa ambayo haitakiwi.

Mheshimiwa Spika, tunao vijana wengi wa Kitanzania ambao wamevumbua vitu vingi. Miaka mitatu iliyopita tulikuwa na maneno hapa, kuna vijana ambao walivumbua helikopta, sijui wako wapi leo? Kuna vijana ambao walivumbua magari, wako wapi leo? Serikali yetu kupitia Wizara hii imewapa msaada gani? Tumewaacha hawa vijana wanahangaika wao kwa wao, wanatumia pesa yao na muda wao na ile end product, kama Serikali, hatui-own. Tunawaacha tu na haya mambo yanapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna kipindi nilisoma siku za nyuma Mwalimu Nyerere alikuwa na wazo la kuanzisha vijiji vya sayansi ambavyo vingewasaidia vijana ambao wana ubunifu wa aina yake waende kwenye vijiji vile wakapate muongozo na ku-shape yale mawazo yao tuweze kupata wabunifu ambao wanaweza kutengeneza vitu. Tunavyoviona vinaelea Ulaya; ndege tunaziona zinatembea na magari, yalibuniwa na kuasisiwa na vijana ambao walikuwa na ubunifu kwenye mioyo yao. Huu ubunifu haufundishwi vyuoni wala shuleni, ila ni mtu anazaliwa ni mbunifu haijalishi amesoma kiwango gani, ana elimu kiasi gani, lakini anao ubunifu ule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kazi yetu kupitia Wizara ya Elimu, hasa ile Taasisi ya COSTECH nadhani ndio kazi yake hiyo. Mwalimu alikuja na wazo la vijiji vya sayansi tukaja na COSTECH, lakini sasa ukiangalia pesa wanayopewa COSTECH hawawezi kuendeleza ubunifu ambao mbele ya safari ungeweza kusaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudi kwenye jimbo langu. Tunayo kazi kubwa mbele yetu. Nilikuwa naangalia maoteo kwenye jimbo langu tu, mwaka huu vijana ambao wamesajiliwa kidato cha kwanza walikuwa 9,041. Mwaka 2023 watakuwa 21,159, mwaka 2024 tutakuwa na vijana 30,025, lakini ukiangalia miundombinu ya shule tulizonazo ni ileile. Naomba Wizara ijipange, vinginevyo kufika mwaka 2025 tutafukuzana kwa sababu wanafunzi walio kwenye shule za msingi ambao tunatarajia waingie kidato cha kwanza ni zaidi ya mara tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu ihakikishe kwamba mikoa ambayo iko pembezoni mwa nchi kama Kagera na mikoa mingine waiangalie kwa jicho la pekee. Ukienda kwenye mikoa mingi ya pembezoni walimu hawapo, unakuta shule ya msingi au shule ya sekondari ina wanafunzi 1,200 ina walimu sita halafu tunaongelea ubora wa elimu, tunajidanganya. Naomba Wizara ya Elimu tujipange kuhakikisha kwamba mikoa ya pembezoni tunaipatia kipaumbele na kuhakikisha ina nyumba za walimu otherwise walimu wote wanaopelekwa kule wanakimbia kwa sababu ya mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, lakini nipendekeze, kwa mikoa ambayo iko pembezoni mwa nchi tuangalie kuwapatia motisha au allowance, ile wanaita hardship allowance iweze kuwa-sustain kule kwenye mazingira magumu ambako hakuna umeme, wakati mwingine hakuna barabara na ukienda kule kwa kweli wengi wanakataa kwenda maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono na nawapongeza Mawaziri wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya, ila Mheshimiwa Waziri asisahau Ndalichako Secondary School. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi nami nichangie hoja ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na jambo moja dogo. Asubuhi wakati Mbunge mmoja anachangia, aliongelea Wizara kutaifisha mifugo wa watu wetu. Katika wilaya yangu ninakotoka, natumaini Mheshimiwa Waziri ananisikia, kuna mwananchi tangu mwaka 2017 ng’ombe wake 111 na kondoo tisa walitaifishwa kwa kisingizio kwamba wameingizwa kwenye Hifadhi ya Burigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi ilikwenda Mahakamani, akafunguliwa Kesi Na. 155 ya 2017 akashinda. Huyo mwananchi siku hiyo hiyo akakamatwa tena akafunguliwa Kesi Na. 56 ya mwaka 2017, akashindwa. Akakata rufaa Na. 35 ya 2019 Bukoba, Mahakama ikaamuru arudishiwe mifugo wake. Mpaka leo tunavyoongea, tangu mwaka 2017 hadi leo anafuatilia ng’ombe wake 111 na kondoo tisa, hajapewa mifugo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waziri anatoa majumuisho, nitaomba kauli ya Serikali, hiyo mifugo iko wapi? Kwa nini Wizara haitaki kumrudishia mwananchi ng’ombe wake?

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar, subiri. Taarifa Mheshimiwa Silaa.

T A A R I F A

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kama mwaka 2017 walikuwa ng’ombe 111 watakuwa wamezaa. Kwa hiyo, madeni ya huyo mwananchi wake aweze kuyaongeza na wale ndama watakaokuwa wamezaliwa kwa muda huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar, unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea na huko ndiko nilikotaka kuelekea. Mheshimiwa Waziri huyu mwananchi anaitwa Dunstan kutoka Kata ya Kyebitembe. Naomba wakati unatoa majumuisho utupe kauli ya Serikali. Whether Serikali iko juu ya sheria au utatuambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mjadala wa asubuhi ilikuwepo hoja ya NARCO. Wakati Mheshimiwa Spika anasitisha shughuli za Bunge asubuhi, naye ametoa maoni yake kuhusu NARCO.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar, subiri. Taarifa; Mheshimiwa Esther.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hoja anayoiongea ni valid sana; na siyo mwananchi wake tu. Tukitaka kusimama hapa kila mmoja, kuna wananchi wengi sana ambao wanapitia hiyo adha. Kwa hiyo, Serikali tu labda ije na mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba wale walioshinda kesi warudishiwe mali zao, ikiwezekana na fidia juu. Siyo kwa Muleba tu, ni karibia nchi nzima kuna matatizo kama haya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni suala la kisera na Kitaifa, naipokea taarifa yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Spika anasitisha shughuli za Bunge asubuhi, naye alitoa maoni yake kuhusu NARCO na Mheshimiwa Rweikiza amesema asubuhi. Katika Wilaya ya Muleba tunao mgogoro mkubwa na shirika letu la NARCO. Katika Wilaya ya Muleba pekee, katika Kata ya Rutoro, tuna mgogoro na NARCO wa hekta 50,000. Katika kata zipatazo sita katika Jimbo la Muleba Kusini; Kata za Kyebitembe, Karambi, Mbunda, Kasharunga, Kakoma na Ngenge, tuna mgogoro na NARCO, mgogoro wa Mwisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu, tumeliongelea hili kwa muda mrefu, lakini kutokana na remarks alizotoa Mheshimiwa Spika leo asubuhi, namwomba Mheshimiwa Waziri, hii ardhi hekta 50,000 ukiongeza hekta 70,000 ambazo tuna mgogoro nazo, atuachie Wilaya ya Muleba tukapange matumizi bora ya ardhi. Wao kama NARCO wabaki kama regulator watupe regulatory oversight tukapange matumizi bora ya ardhi yetu, tukalete wafugaji ambao tunao katika Wilaya ya Muleba, wanatosheleza. Hatutaki wafugaji kutoka nje, tunao wa kutosha na tutafuga…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar, pokea taarifa.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kikao pia cha Waziri Mkuu cha tarehe 26 Februari, 2016 pale Kagera alitoa maelekezo kwamba NARCO wabainishe mpango bora wa matumizi ya ardhi na kama NARCO imeshindwa kuendesha waweze kuipendekeza Serikali wananchi waweze kugawiwa, hasa hilo nilikuwa naomba kumpa taarifa mzungumzaji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Oscar.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba ulinde dakika zangu ninaona nina taarifa nyingi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wizara na kwa maana hiyo tunaiyomba Serikali suala la Mwisa II kwa Mkoa wa Kagera watuachie, uwezo tunao, watu tunao, na ng’ombe tunao. Wakatupatie utalaam na uangalizi kidogo na ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Muleba inazungukwa na Ziwa Victoria, nashukuru mzungumzaji wa mwisho amesema Kagera, Ziwa Victoria tumepewa pesa kwa ajili ya mikopo kwa wavuvi wetu, niishukuru Serikali kwa hilo. Lakini Waziri wa Fedha yupo hapa Tanzania tumebarikiwa kuwa na fursa nyingi kwa upande wa bahari, maziwa, lakini ukiingalia tunavyotumia hizo fursa ni aibu ni aibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bahari tuna fukwe yenye urefu wa zaidi ya kilometa 1424 zenye kufaa kwa uvuvi ni kilometa 854 ambayo ni sawasawa na asilimia 60 zinafaa kwa ufugaji wa Samaki. Kwa upande wa Ziwa Victoria ninakotokea, tuna ufukwe wa kilometa 3450 ambapo kilometa 2587 sawasawa na asilimia 75 zinafaa kwa ufugaji wa Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia shughuli za uvuvi zinazoendelea na mazao tunayoyapata ni aibu, mahitaji ya Samaki kwa upande wa Tanzania kwa mwaka tunahitaji kati ya tani 700,000 mpaka 800,000 kwa mwaka. Lakini pamoja na fursa tulizonazo, pamoja na bahari tuliyonayo, pamoja na maziwa tuliyonayo tunazalisha tani 389,455 hata hatutoshelezi soko la ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walichukua dakika zangu, naomba niongezee mbili.

MWENYEKITI: Dakika moja na nusu nakupa.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaagiza Samaki kutoka nje mpaka sasa na tunalo tatizo la vijana kukosa ajira, sasa tunaomba wizara ituambie ina mkakati gani kuhakikisha kwamba hilo gap la Samaki tunaoagiza kutoka nje kwa pesa ya kigeni tunalipunguzaje na kuhakikisha kwamba tuna-involve vijana wengi zaidi ili tuweze kwanza ku-create ajira, wakati huo huo kupunguza uagizaji wa Samaki nje wakati tuna maziwa, tuna bahari ambavyo vipo, tumepewa tu na Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameongezea suala la kanuni na tozo, niliongelea hapa wakati nachangia Mpango wa Tatu, nimuombe wizara wapitie tozo zote ambazo tunatoza kwenye mazao ya uvuvi wa Samaki. Lakini tunapoongelea tozo tuangalie tunalinganisha na nchi jirani za Kenya na Uganda ambao wote tuna-share kwa mfano Ziwa Victoria kwa upande wa bahari tuna-share na Kenya na wenzetu Msumbiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiishi kama tunaishi kwenye kisiwa, tunapotengeneza kanuni tuangalie na wenzetu, mchangiaji aliyemaliza kusema, amesema kina cha Ziwa Victoria na kina cha Ziwa Tanganyika vinatofautiana, kwa hiyo tunapotengeneza kanuni, tusitengeneze kanuni kwa nchi nzima tuangalie na mazingira ya maziwa yetu, tuangalie mazingira ya bahari, havifanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, lakini naomba Waziri atakaposimama atuambie hatma ya ng’ombe wa wampiga kura wangu 111 na Kondoo 9 wapo wapi? na wameshazaa wangapi? na faida yake ni nini? na anamrudishia huyo mpiga kura lini hao ng’ombe wake. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia Wizara hii. Niungane na wenzangu Wabunge kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameongea mazao mapya ambayo wameyaongeza kwa ajili ya kuongeza chachu na ufanisi katika Wizara ya Utalii, nayo ni utalii wa uvuvi na kujiburudisha, utalii wa kula Wanyama pori, utalii wa kula chakula porini na utalii wa kupiga makasia. Nawapongeza sana kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani wengi tumetembea katika nchi za wenzetu. Kwa mfano ukienda Misri, pamoja na kuangalia zile pyramids lakini jioni mkitoka kuangalia yale ma-pyramids mtakwenda Mto Nile, mtapiga ma-cruise, kuna ngoma za asili, mtakula chakula, inaongeza value kwenye package ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tanzania tutumie na sisi akili zetu jamani, tusibakie kwenda kuangalia wanyama sijui wapi, kuangalia sijui Tarangire, sijui Serengeti, tuongeze value kwenye kuangalia wale Wanyama, jioni hawa watalii wanaangalia nini, wanafanya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Hongkong pale ile Hongkong ilivyokaa ina vilima mithili ya Mji wa Mwanza, lakini vile vilima wamehakikisha wamevitunza na ni sehemu ya vichocheo vya utalii, ile jioni mnapanda kwenye mlima mnaangalia Hongkong pale chini. Angalia Mji wetu wa Mwanza tunautumiaje kwenye sekta ya utalii, tumebaki na sekta ya utalii ambayo hatujaijumuisha na mazingira ya maeneo ya utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna ziwa Victoria pale na maziwa mengine tunayaunganishaje kwenye sekta ya utalii kwa mfano Ziwa Victoria, Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi yupo pale, kuna kipindi pale Bukoba walikuwa wameandaa kuwa na cruising party kipindi cha mwisho wa mwaka, lakini ukienda kuazima meli ile ya Victoria wanakwambia hii siyo kazi yetu, siyo kazi ya utalii hii, ni kana kwamba Wizara ya Utalii inajitegemea, Sekta ya Uchukuzi inajitegemea lakini tunapaswa kuwa holistic approach tunapokuja kwenye sekta ya na masuala yote ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Burigi Chato, nawashukuru Serikali ile hifadhi ilikuwa ni majanga miaka ya nyuma, tusingepita mle, lakini kwa kuanzisha hii hifadhi imetuongezea usalama watu wa kanda ya ziwa. Nimwombe Waziri Burigi ndiyo imebeba maana ya ile hifadhi. Tuna Ziwa Burigi pale ambalo kwa bahati nzuri kama hawajawahi kufika, lakini najua hawawezi kufika kwa sababu lile eneo la Burigi halifikiki, hakuna barabara nzuri, lakini pili kama mchangiaji mmoja alivyosema hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, wakati anakuja ku-wind up atuambie wana mkakati gani kuhakikisha kwamba lile Ziwa Burigi linafikika. Watalii watakapokuja na nina uhakika, watalii wengi watatokea Bukoba kwenda kwenye Hifadhi ya Burigi Chato, tuhakikishe upande wa Muleba tunakuwa na gate kubwa la kuhakikisha kwamba watalii watakapotoka Bukoba kwenda Burigi Chato wanapata sehemu ya kuingilia, badala ya kuzunguka kwenda Biharamulo kwenda sijui Chato, waingilie eneo la Muleba. Mheshimiwa Waziri atatupa maneno yakeo atakapokuja kuhitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, wakati nachangia Wizara ya Mifugo, niliongelea hili suala la kuchukua mifugo. Bahati nzuri wewe mwenyewe ni Mwanasheria, Waziri ni Mwanasheria, wanajua maana ya sheria. Inapokuja katika Wizara hii, mifugo imeingizwa kwenye Hifadhi mwananchi wangu nilimwongelea katika Wizara ya Mifugo…amekamatwa, amefunguliwa kesi ya kuingiza mifugo kwenye hifadhi, ameshinda. Siku hiyo hiyo amekamatwa kwa kosa lingine eti ameharibu uoto wa asili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mahakama imesema arudishiwe mifugo yake kwa nini watu wa Wizara hii wanakaa na mifugo ya wananchi jamani! Wanafanya wananchi wachukie Serikali yao kana kwamba Serikali imewaibia mifugo yao, lakini ni watu wachache. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie wanatupatia wakati mgumu kwenye majimbo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga hoja
mkono. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja hii. Nampongeza Rais wetu kwa bajeti hii nzuri, pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na Watendaji wote wa Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye kushauri. Nilikuwa naangalia hizi sekta zetu za kiuchumi na mchango wake katika pato la Taifa. Ukizipitia zote, kwa kweli bado tunayo kazi kubwa ya kufanya. Ukiangalia kilimo kinachangia asilimia 26.9 kama takwimu zangu ziko sahihi; fedha na bima zinachangia asilimia 3.5; madini asilimia 6.9; viwanda asilimia 8.4; umeme asilimia 0.3; ujenzi asilimia 14.4; uchukuzi asilimia 7.5; na biashara asilimia 8.7. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia jiografia ya nchi yetu, mimi nadhani sekta nyingi kwa kweli tuko chini pasipo sababu yoyote ya msingi. Kwa mfano uchukuzi, kwa jiografia ya nchi yetu, bandari zetu, nchi tunazopakana nazo, napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri, tujipe mkakati wa kukatisha baadhi ya sekta mchango wake katika pato la Taifa uende zaidi ya asilimia 10. Tupende tusipende lazima tuwe na mkakati wa namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya uchukuzi tuna viwanja vyetu vya ndege, lakini kanda ya ziwa tuna uwanja wa ndege wa Mwanza. Zamani mazao ya uvuvi yalikuwa yanasafirishwa kwa ndege kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza kwenda nchi za nje, lakini hivi sasa tunavyoongea, mazao yote ya uvuvi ili yaende kwenye masoko ya nje, lazima tuyasafirishe kwa malori tuyapeleke Entebe au Nairobi. Ukijiuliza, kwa nini mazao yetu ya uvuvi yaende Entebe au Nairobi? Hatuna sababu yoyote ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani uwanja wetu wa ndege haukuwa na facility ya kuhifadhi hii minofu ya Samaki, lakini hivi tunavyoongea, Serikali yetu kupitia TAA wamejenga facility nzuri sana ambayo ukilinganisha na nchi jirani actually facility tuliyonayo pale Mwanza ni nzuri na bora kuliko facility zote za Afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Tatizo tulilonalo, hatujaisajili kupata FOB Mwanza na ndiyo maana mashirika ya ndege kama Air Rwanda walipojaribu kusafirisha minofu yetu ya samaki kutoka Mwanza, wameshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, kwa kuwa tumeshawekeza pesa yetu pale Mwanza, tumejenga facility, tutafute registration, tupate FOB Mwanza ili mazao yetu ya uvuvi yasafirishwe moja kwa moja kutoka Mwanza kwenda nchi za nje. Hii kwanza itaongeza chachu kubwa ya kuwekeza viwanda hapo Mwanza au Kanda ya Ziwa. Pili, zile pesa ambazo tunazilipa Entebe na Nairobi zitabaki kwenye nchi yetu, tutaongeza pato kwa sekta ya uchukuzi na sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu kilimo. Ukiangalia sekta ya kilimo, mchango wake ni mdogo. Wachangiaji wengi wamesema hapa, tuna vijana wengi huko mitaani hawana kazi, lakini hawawezi kwenda kwenye kilimo kwa sababu ukiwaambia wanasema hawana mitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu kitengo cha JKT wanafanya vizuri sana kwenye kilimo. Nashauri tuwaongezee pesa wakajikite kwenye kuzalisha mazao ya kilimo. Kwa sababu wana uwezo, watazalisha, watayaongezea thamani na wanaweza kupata masoko kirahisi kuliko mkulima mmoja mmoja. Hata kilimo ambacho tunakizalisha, hapa tunaongea lakini nadhani hatuna mkakati wa madhubuti kuhakikisha kwamba tunaongeza tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu Kagera tunazalisha kahawa. Tumepiga kelele sana hapa, tumesema hebu ruhusuni wafanyabiashara wakanunue hizi kahawa. Kuna watu wamewekeza kwenye viwanda pale, lakini tunawawekea figisufigisu hatuwapatii vibali. Msimu wa kahawa ulianza mwezi wa Nne, lakini tunavyoongea leo, vyama vyetu vya msingi havijafungua masoko, hata wafanyabiashara binafsi ambao wangenunua kahawa, hawajapewa vibali. Ukijiuliza wakati mwingine, tunadhamiria nini? Tunalenga kufanya nini? Ndiyo maana sekta nyingi kama hizi kutokana na kanuni zetu tulizojiwekea, hatufanyi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwamba hizi posho ambazo walikuwa wanalipwa Madiwani sasa Serikali inazibeba. Hata hivyo nikiangalia hizi posho zao hawa Madiwani wenzetu, pamoja na kwamba naishukuru Serikali kwamba imezibeba, itazilipa kwa wakati, lakini tuziangalie hizo posho, bado ni kidogo mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Madiwani wenzetu ndio tunawaachia majimbo yetu, ndio wanafanya kazi kwenye kata zetu, ndio wanafanya kazi ya kuhamasisha kukusanya mapato ya Halmashauri zetu. Napendekeza kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake, tuiangalie hii posho ya Madiwani, tuwaongezee angalau kidogo nao wakajisikie na wakafurahie kazi wanayoifanya huko kwenye Halmashauri zetu na waweze kutulindia majimbo yetu ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa posho zilizopendekezwa kwa ajili ya Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa. Nawashukuru sana. Hata hivyo, kuna kundi ambalo tumelisahau; kundi la wazee. Nimefurahi kule upande wa pili wa nchi yetu, Zanzibar wanawalipa wazee posho ya shilingi 25,000/= kila mwezi; wanafanya vizuri. Ila kwa upande wa Tanzania Bara tuna makundi ya watu wenye mahitaji maalum; tunaongelea watoto, wanawake na vijana ambao wanapewa mikopo, lakini tumesahau hili kundi muhimu la wazee na ambalo katika maisha yao wamelitumikia Taifa hili na kwa kweli wanaishi kwa kusononeka, baada ya kuingia kwenye hili kundi la wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yetu na tujuwe kila mmoja wetu tunaelekea kwenye uzee, tuwatengee na wenyewe posho kidogo ambayo itawapatia furaha katika maisha yao. Hii inawezekana. Baadhi ya taasisi kwa mfano ninakotoka kwenye jimbo langu, kuna NGO tu; kuna mzee mmoja Mswisi, ameishi pale zaidi ya miaka 10. Aliamua yeye kwa pesa yake kuwaletea raha wazee wenzake, kila mwezi anatumia zaidi ya shilingi milioni 16 kuwapa posho hawa wazee. Anawalipa posho zaidi ya wazee 1,000; na kwa mwaka anatumia zaidi ya shilingi milioni 195 kwa pesa yake na pesa ambayo anaitafuta nje. Huyu mzee amekaa hapa muda mrefu sana, lakini alijaribu hata kuomba na uraia tukamnyima. Naona Waziri wa Mambo ya Ndani yuko hapa. Huyu mzee amefanya mambo mengi mazuri na anawasaidia wazee na anawapa raha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema kuwalipa posho wazee siyo suala la pesa unawalipa kiasi gani? Kinachofanyika ni kwamba, wanajiona wamethaminika, wanajiona wanapendwa, wanajiona wana thamani katika nchi yao, hata tukiamua tuwepe shilingi 10,000/= tu, watafurahi, wataishi maisha marefu zaidi na watafurahia nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili tuliangalie, tulitafakari na tulitathmini. Sasa hivi wazee tunasema ni wachache lakini tuendako zaidi ya miaka 10 ijayo, wazee tutakuwa wengi, tunazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga hoja mkono, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami niungane na Wabunge wengine kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Katika ripoti yetu tumeangalia mashirika mengi, lakini nasikitika kusema mashirika yetu mengi hayafanyi kazi vizuri. Tatizo mojawapo, katika ripoti yetu tumeainisha, ukosefu wa mtaji ni tatizo kubwa kwenye mashirika yetu na nijikite kwenye TPA.

Mheshimiwa Naibu Spika, TPA kwa uchumi wa nchi yetu na kulingana na jiografia yetu na nchi zinazotuzunguka, kusema kweli ni cash cow yetu. Hata hivyo, ukiangalia mtaji walionao na uwekezaji wetu na jiografia yetu, nchi zilizotuzunguka zinazohitaji huduma yetu, kulingana na ripoti yetu ambayo tumewasilisha hapa, tumesema TPA utendaji kazi wake ni mdogo kwa sababu hawana mtaji wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia vifaa walivyonavyo ni vya karne iliyopita, siyo vya karne hii. Tanzania siyo peke yetu; au Bandari ya Dar es Salaam siyo peke yake katika ukanda huu. Tunazo bandari nyingi ambazo tunashindana nazo. Kama tuna vifaa hafifu ambavyo vina teknolojia hafifu, hatuwezi kushindana na bandari za nchi zilizo karibu kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Tutaachwa nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza, Serikali i- commit hela ya kutosha kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili tuweze kuhudumia mizigo ambayo nchi jirani wanapitisha kwetu. Vinginevyo washindani wetu watatuacha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, bandari hiyo ina upungufu mkubwa wa wafanyakazi. Ikama yao ni wafanyakazi 3,196, lakini waliopo mpaka leo tunapoongea ni wafanyakazi 2,512. Wanao upungufu wa wafanyakazi 1,404 tunashindwa wapi? Kama hiki ndicho kitega uchumi cha uhakika tulichonacho, tukiwekeza vya kutosha, tuna uhakika wa kutengeneza fedha za kutosha kutusaidia kupunguza matatizo kwenye bajeti yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukishakuwa na wafanyakazi wachache, ukawa na mtaji mdogo, madhara yake ni kwamba tunatumia muda mwingi kuhudumia meli na matokeo yake hawa tunaowachelewesha kupakua mizigo yao, tunawalipa fidia na hizo gharama zote zinapelekwa kwa mlaji na matokeo yake ni nini? Bidhaa inayopitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam haiwezi kushindana na bidhaa nyingine. Itakuwa ni ya bei ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie na Taasisi inayoitwa TASAC. Wakati Sheria ya TASAC inapitishwa hapa, wengi tuliipigia kelele, lakini tukaipitisha kama Bunge. TASAC anafanya kazi ya udhibiti, lakini wakati huo huo anafanya kazi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani hii. Kwetu huku tunasema ni sawa sawa na kuchukua rubisi ukachanganya na konyagi, haiwezekani. Kama ni mdhibiti, afanye kazi ya udhibiti na tuunde taasisi nyingine ya kufanya biashara ambayo inafanywa na TASAC. Mdhibiti afanye kazi ya udhibiti na tuwe na kampuni nyingine tofauti na TASAC ambayo itafanya kazi ya clearance, kazi za kusafirisha kidogo kidogo na kutoa mizigo, lakini hizi kazi mbili lazima tuzitenganishe, hatuwezi kuendelea hivi. Vinginevyo tunabaki kama kichekesho tu katika uchumi wa soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia muda huu nami niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru hoja ambayo ilitolewa na Waziri Mkuu. Zaidi namshukuru Waziri Mkuu kwa mkutano wake alioufanya Mkoani Kagera, Wilaya ya Karagwe kutoa suluhu na mweleko wa zao la Kahawa Mkoani Kagera. Nadhani tunakoelekea ni kuzuri, hasa sisi ambao tunatoka katika mikoa inayolima zao la kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajikita kwenye migogoro ya ardhi. Ninavyoongea leo kuna watu wamelala nje jana. Tuna Kampuni yetu ya ranchi kwa jina mashuhuri, NARCO. Kama kuna kitu ambacho wamefanikiwa Mkoa wa Kagera, ni kutengeneza migogoro mikubwa baina ya wakulima na wafugaji. Kwa kweli, NARCO ni mtambo wa kufyatua migogoro kuliko ufugaji ambayo ni kazi ya msingi waliopewa na sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kagera, hususani Wilaya ya Muleba, NARCO wana ranchi mbili. Wana ranchi Rutoro na Mwisa, lakini wamepata hizo ardhi katika Wilaya ya Muleba kwa njia ambayo mimi kama Mwanasheria sijui walipataje. Bahati nzuri Mheshimiwa Spika ni Mwanasheria, na ninamwona Waziri wa Ardhi yupo hapa. Upatikanaji wa ardhi ya Mwisa ambayo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, hawa watu walivyoipata tuna mashaka makubwa. Nimepitia GN zote, tangu mwaka 1960 mpaka leo, nimetafuta GN ambayo inawapa uhalali NARCO kumiliki ardhi ya Mwisa, sijaipata. Tunapoongea, hawa watu wa NARCO wapo eneo la Mwisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la Mwisa katika Wilaya ya Muleba linahusisha Kata saba; tuna Kata za Kemitembe, Karambi, Kasharunga, Mbunda, Burungura, Ngenge na Rutoro. Ndani ya hizo Kata tunavyo Vijiji 12 na Vitongozi 19. Eneo lote hilo tunavyoongea wananchi hawajui kama leo watalala kwenye nyumba zao, hawajui kama kesho wataamka kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tuna wasiwasi haya maeneo waliyapataje; kwa sababu haya maeneo ni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, ni maeneo ambayo yanakaliwa na vijiji; na vijiji vimepimwa tangu mwaka 1975 na vingine vimepimwa mwaka 2010, lakini hawa watu wanasema ni mali yao.

Mheshimiwa Spika, tunazo sheria za nchi hii; tunayo Sheria ya Vijiji (Land Village Act (No. 5) ya Mwaka 1999, lakini tulikuwa na Sheria ya Land Acquision Act; tunao utaratibu wa kutoa ardhi ya vijiji; tunao utaratibu kwamba Rais akihitaji eneo lolote atalitwaa, lakini kuna utaratibu wa kufanya hivyo. Waziri wa Ardhi ataandaa utaratibu ambao utakuwa gazetted, itatoka GN then hilo eneo litatwaliwa kwa matumizi mapana ambayo yana maslahi mapana kwa ajili ya uchumi na matumizi ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea, nimeangalia kote huko, hakuna kitu kinachofanyika au kilichofanyika. Watu wamekwenda wamepima maeneo ya Halmashauri, maeneo ya vijiji; na leo tunavyoongea, katika Vitongoji vya Kabwensana, Maigabili, NARCO wanahamisha watu kinyume cha sharia. Hawafuati Sheria ya Ardhi ya Vijiji, hawafuati sheria ya kuhamisha makaburi ya wapendwa wetu (Grave Remove Act (No. 9) ya Mwaka 1999, pia hawafuati mila na desturi za Wahaya. Wanakwenda pale, wanafukuza watu, wanawaambia ninyi mnahama, mnatoka hapa mnakwenda kule, hakuna notice iliyotolewa, Waziri wa Ardhi hajatoa notice kwa ajili ya kuhamisha makaburi kama ilivyo kwenye Graves Remove Act. Watu hawana amani, hakuna usalama kwenye eneo la Mwisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili nalisema, nashukuru umekalia Kiti, namwona Naibu wa Waziri ni Mwanasheria, naomba mtusaidie. Hatuwezi kuruhusu vitendo vya namna hii, wananchi wanateseka, wanafukuzwa kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi, naomba niliseme hili: lugha inayotumia kule, wanasema ninyi ni wavamizi. Mimi nashangaa! Mtanzania ambaye amezaliwa Tanzania, amekaa kwenye ardhi tangu mwaka 1975, leo NARCO anamwambia ni mvamizi. Tunalipeleka wapi Taifa? NARCO wanalo tatizo. Naomba, haya mambo yanayoendelea Kagera na Muleba, hayawezi kuishia Muleba tu, yatakwenda hata kwenye mikoa mingine tusipochukua hatua leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo hili lilianza mwaka 2016 kwenye upande wa Mwisa. Wakavamia eneo, wakaanza kupima. Tulipokwenda kwenye uchaguzi wakanyamaza. Tumemaliza uchaguzi, wameendelea na leo wapo wanaendelea. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, ndugu yangu Mheshimiwa Ndaki Mashimba. Mwaka 2021 alikuja Wilaya ya Muleba kwa ajili ya kutafuta suluhu ya Mwisa, tukakaa tukaenda field, tukafanya mikutano na wananchi. Tukawaambia, vijiji ambavyo vimesajiliwa pamoja na vitongoji vyake, kwenye huu mradi wa Mwisa havitaguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetoka kule, hawa NARCO walivyo wa ajabu, wakaanza kuwaambia wananchi msiwasikilize wanasiasa. Mimi nashangaa, kama wanasema msiwasikilize wanasiasa, Diwani ni Mwanasiasa, Mbunge ni Mwanasiasa, wewe Mheshimiwa Spika ni Mwanasiasa; na Bunge hili ni la Wanasiasa; ina maana hawatamsikiliza Diwani, hawamsikilizi Mbunge na hata Bunge lako hawatalisikia. Sasa wengine wa juu yake sitawasemea. Nashindwa kuelewa, hivi NARCO hawa, wanatoka Taifa gani? Wanatumikia Taifa gani? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikubaliana pale, tukaja na kitu tunakiita community ambayo ina maazimio 16. Moja ya Azimio, ambalo ni Na. 16 tukasema Ardhi ya Vijiji pamoja na Vitongoji vyake visiguswe. Tumetoka, leo tunavyoongea, wapo kwenye Vitongoji, wanawahamisha watu kwa nguvu zote. Hapo ukumbuke, hawana GN ya kuwapa hiyo ardhi, kwenye makaburi ya watu wanaleta mifugo kulisha pale. Sasa mila zetu ziko wapi? Sheria ziko wapi? Labda kama Waziri amewapa hiyo ruhusa jana, lakini mpaka leo naongea, hakuna taarifa ya kuhamisha makaburi ya wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipatia fursa ya kuchangia kidogo kwenye hoja ambayo iko mbele yetu. Napenda kuwapongeza Wizara ya Fedha kwa kazi hii nzuri waliyotuletea hapa na ambayo tunaijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Hasunga anasema hapa nilikuwa nasoma kitabu kimoja, kimeandikwa na Professor Keith Penny, Professor of psychology and neuroscience. Kwenye hicho kitabu kuna sentensi moja inasema “it takes money to make money”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunachangia Kamati zetu zile tatu, kulikuwepo tatizo kubwa ambalo tulibainisha. Mashirika yetu mengi yanaendeshwa chini ya mtaji wake, yanahitaji mtaji. Kulingana na hiyo quote ambayo nimeisema, bila kuwekeza kwenye mashirika yetu ya umma tusitegemee miujiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kidogo kwenye kilimo, kwa sababu watu wengi miongoni mwa watu wangu wa Muleba ni wakulima na kama tunavyofahamu zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wamejikita kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tatizo tulilonalo kama nchi, wasemaji wengi wamesema, tunalo tatizo na lazima tutafute tumejikwaa wapi ili tuweze kutoka pale. Nikiangalia mfumo wetu wa Taifa tumejifunga kwenye kanuni na sheria zetu ambazo nyingi zinatukwaza. Kule kwetu Mheshimiwa Bashe anafahamu nimemwona pale, kila ikifika mwezi Julai lazima nimwone Mheshimiwa Bashe. Sisi ni wakulima wa kahawa, lakini ikifika mwezi Julai, Agosti tuna task force nyingi kuliko think tanks za kutuletea suluhu ya matatizo yetu. Tutaunda task forces tunaanza kukimbizana na wakulima wadogo wadogo wenye gunia moja, debe mbili eti magendo, tunawakwaza wakulima na wengi wanakata tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kwetu watu wengi walingoa mibuni na tunayo Sheria ya Kahawa, inasema eti kahawa ni mali ya Serikali. Kati ya sheria mbovu na hiyo ni moja ya sheria mbovu. Mheshimiwa Bashe wakati tunaongea pale alisema anataka free market, sasa inapokuja free market, let make it a free market for every crop for every business, tufungue soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taasisi za udhibiti, tunayo taasisi ya Fair Competition katika nchi hii, tuiachie ifanye kazi yake. Wakati mwingine tunakimbizana na hawa watu wadogo wadogo hawa, ukiangalia wakulima wa kahawa kwa mfano Kagera, zaidi ya asilimia 90 ni wakulima wadogo wadogo ambao baada ya kuvuna mazao yao tunaanza kukimbizana nao. Hayo mazao wanayapeleka wapi? kama kule wanakoyapeleka kuna soko zuri, bei nzuri, kwa nini tusije na utaratibu mzuri tukawawekea utaratibu mzuri wakauze kule tukakusanye kodi sisi kama Watanzania? Kuna tatizo gani kwenye hilo? Tuachane na mfumo wa ku-paralyze soko kwa kuwafungia wakulima kana kwamba ni wezi, kana kwamba ni smugglers, kana kwamba yaani hawana; mazao wamezalisha wenyewe lakini tunapambana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uvuvi, tatizo ni lilelile. Ukiangalia tozo za sekta ya uvuvi na ukizilinganisha na nchi nyingine, ndio maana ukiangalia nchi jirani Uganda, Kenya wanafanya vizuri kwenye uvuvi. Sisi wenye sehemu kubwa ya ziwa tunapata mapato kidogo kwa sababu ya tozo tulizonazo. Huu siyo muujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye tozo tulizonazo kwa mfano fillet, Tanzania ile viwango vya tozo kwa kilo tunatoza shilingi 552, wenzetu Uganda wanatoza shilingi 115, Kenya shilingi 34.51 hizi ni hela za Kitanzania. mabondo sisi tunachaji shilingi 7,500, wenzetu Uganda shilingi 460, Kenya shilingi 34. Vichwa vya samaki sisi tuna- charge shilingi 46, wenzetu Uganda shilingi 115, Kenya shilingi 34, ndio maana tunakula vichwa hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni mtu gani ambaye ataingia kwenye ziwa akuletee wewe mazao ya uvuvi badala ya kuyapeleka kule ambako tozo na tozo nyingine ziko much more user friendly. Sisi kwetu tozo ziko juu sana, tuangalie haya mambo Mheshimiwa Waziri wa Fedha tunapokuja kutengeneza hizi. Tunavutiaje haya mazao kwetu? Ndio maana Uganda tunavyoongea wana viwanda 20, sisi tuna viwanda nane, Kenya wana viwanda vitano, lakini ukiangalia ziwa tunalolimiliki sisi ni zaidi ya asilimia 50, liko kwa upande wetu. Hata ukiangalia mauzo ya nje, tunavyongea leo, Uganda wanafanya vizuri zaidi kuliko sisi na nchi ya pili baada ya Nigeria, lakini sisi tuko wapi kwa sababu ya mifumo tuliyojiwekea ya sheria, kanuni, tumejifungia kiasi kwamba tunajitengenezea umaskini sisi wenyewe kwa kujua au kutokujua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana Mheshimiwa Hasunga alikuwa anasema we are living in the cycle poverty na hii tumeitengeneza sisi wenyewe kwa kanuni zetu, sheria zetu. Tukae chini tuangalie ni wapi kanuni zetu zinatufunga, ni wapi sheria zetu sio nzuri, ni wapi competitive advantage tunaweza tukaitumia tukijilinganisha na mataifa jirani, tusijifungie ndani, tukadhani sisi ni kisiwa, sisi tunafanya biashara peke yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)