Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jackson Gedion Kiswaga (44 total)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Kalenga hasa Vijiji vya Wangama, Lupembelwasenga pamoja na Welu kwa kutaja tu vichache tayari walishaunganisha umeme, walishalipia na walishafanya wiring lakini hawajawashiwa umeme mpaka sasa.

Je, Serikali inatoa kauli gani ili wananchi hao waweze kuwashiwa umeme wao? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika maswali ya nyongeza. Vilevile nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuuliza maswali ya msingi sana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wateja wote ambao wameshafanya malipo na wanasubiri kuunganishiwa umeme pamoja na wateja wote ambao wameshafanyiwa survey, lakini wanasubiri kuunganishiwa umeme, tumetoa muda wa miezi mitatu wateja wote wawe wameshaunganishiwa umeme nchi nzima. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Kalenga kwa kuuliza swali hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ili kuharakisha shughuli za kuwaunganishia umeme wateja nchi nzima, tumebadilisha mpango wa wataalam wetu kusubiri magari, badala yake TANESCO itawanunulia magari ma-surveyor wote na ma-technician ili wawahi kuwaunganishia umeme wananchi, ndani ya muda uliokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kuhusiana na suala la maeneo ambayo ni ya mijini; kulingana na swali ninalojibu ambalo Naibu Waziri amejibu vizuri, lakini niongezee kidogo. Iko mitaa mingi ambayo iko karibu na miji na vijijini hasa katika maeneo ambayo ni ya Majiji na Manispaa, likiwemo Jiji la Mbeya, Iringa, Mwanza, Dodoma hapa, mradi wa peri-urban unaendelea na miradi yote katika mitaa 122 itapelekewa umeme ndani ya miezi sita ijayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kule Magunga ukitoka Magunga kwenda Lumuli kuna mradi ambao ulihasisiwa na Marehemu Dkt. William Mgimwa zaidi ya miaka saba iliyopita bahati mbaya haukutekelezwa, lakini sasa tunaishukuru Serikali imepeleka kiasi cha milioni kama 200 hivi kuanza kwa kutengeneza tenki kwa kutumia force account, lakini ninaona kwamba kasi yake ni ndogo.

Je, Wizara ina mpango gani hata kwa kutumia Wakandarasi ili maji yale yafike Kata ya Lumuli ambapo wananchi wake wamesubiria kwa muda mrefu sana.(Makofi)

Swali la pili, kumekuwa na mradi ambao pia ulianzishwa na aliyekuwa Mbunge na Katibu wa Bunge hili George Francis Mlawa wa Nyamlenge. Mradi huu ulikuwa wa maji tiririka ambao ungezifikia Kata kama tano, ukianzia Lyamgugo, Luhota, Mgama, Bagulilwa mpaka Ifunda, lakini sasa mmebadilisha scope mnachimba visima, wasiwasi wangu ni kwamba ikitokea tetemeko la ardhi na kule tupo kwenye bonde la ufa, visima vile mkondo huwa unahama maji yanakosekana.

Je, Serikali sasa ina mpango gani kupeleka pesa za kutosha ili turudi kwenye scope ya zamani na maji yapatikane katika Kata hizo tano ambazo nimezitaja?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru Mheshimiwa Kiswaga kwa kuishukuru Serikali ya Mama Samia, tayari Magunga kazi zinaendela pale tumeanza na hii milioni 200 lakini fedha tutaendelea kuleta kwenye migao inayofuata, lengo ni kuona wananchi wote wa eneo lile wanaendelea kupata maji ya uhakika ya kiwa safi na salama bombani.

Mheshimiwa Spika, kijiji cha Lumuli hapa kipo kwenye mpango wa fedha za mwaka 2021/2022 na mradi huu kadri ambavyo tumeweza kufanya mashirikiano na Mheshimiwa Mbunge tutautekeleza kwa kupitia Mkandarasi lengo iweze kufanyika kwa haraka na wananchi wa Lumuli nao waweze kunufaika na fedha hizi ambazo Mheshimiwa Rais ameendelea kutupatia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, eneo la Nyamulenge pia lipo kwenye mpango wetu wa muda mrefu. Kwa sasa hivi tumechimba visima virefu ambavyo vinatumia pump za umeme kwa sababu ya kuona kwamba kwa muda huu wananchi waweze kuendelea kupata huduma ya maji. Lakini katika mipango ya muda mrefu kama ambavyo tumeendelea kuwasiliana mara kwa mara na tulishaweza kushauriana kwa muda mrefu katika mpango wa muda mrefu chanzo hiki cha Nyamlenge tutakuja kukitumia kwa mradi wa maji ya uhakika maji ya mserereko ambayo eneo lile litapata maji ya kutosha na vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi huu vitaweza kunifaika.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza lakini pia namshukuru dada Grace kwa kuuliza swali ambalo tulikuwa tunajadiliana juu ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, aa ninacho…

SPIKA: Mheshimiwa Jackson kwa hiyo swali hili ulimtuma kumbe ee!

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, tunajadiliana, mimi na yeye tunafanya kazi kwa kushirikiana na kwa tunajadiliana; lakini amewahi kuuliza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kuhusu barabara inayotoka Kijiji cha Wenda kwenda Lupembelwasenga inatokea Mgama. Barabara hii kwa taarifa nilizonazo ilikuwa imetengewa fedha katika ule mpango wa European Union, na tayari nilishauliza RCC lakini sikupata majibu yanayoridhisha.

Je, Serikali inaweza kunipa majibu sasa, kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa sababu ya wakulima wanaotoka maeneo hayo na kuyawaisha kufika kwenye barabara hizi za lami ili awahi huku Dodoma? Ni lini sasa Serikali inaweza kututengenezea? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, barabara hiyo tumeichukua na tutaifanyia upembuzi ili tuone kama inakidhi vigezo vya kuhama ili tuihamishe iende TANROADS naomba kuwasilisha.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika Kata ya Masaka yenye Vijiji vitatu vya Sadani, Wanging’ombe pamoja na Makota havina kabisa maji hata kijiji kimoja. Je, Waziri sasa wakati anaangalia uwezekano wa kupata maji ya kutiririka anaweza hata akatuchimbia visima ili wananchi wa kule waendelee kunufaika na huduma ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nipende kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga. Mheshimiwa Kiswaga ni Mbunge ambaye kwa kweli nimeshazungumza naye mara nyingi na tayari tuna mradi kule tumekubaliana nakwenda kuuzindua.

Nipende kumhakikishia katika masuala ya visima Waheshimiwa Wabunge, hiki ni kipaumbele kimojawapo cha Wizara, tutafika Kalenga, tutachimba visima viwili, yeye ndiye atakayetueleza wapi zaidi kuna tatizo sugu ambalo mitandao ya mabomba ya maji ya kawaida hayafiki, basi visima Mheshimiwa Kiswaga atavipata.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Kitongoji cha Banawanu katika Kata ya Mseke kiko karibu sana na Mji wa Iringa Mjini na kipo katikati ya Tosamaganga pamoja na Uwachani; na hii ilikuwa ni ahadi ya Mbunge ambaye ndiye mimi kwamba tutawapelekea umeme. Je, ni lini sasa TANESCO itapeleka umeme ili hata kunifichia aibu Mbunge mwenzake?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kiswaga kwa kutoa ahadi za ukweli kwa wananchi wake kuwaahidi kuwapelekea umeme. Nawaahidi Waheshimiwa Wabunge wote walioahidi kupeleka umeme kwa wananchi wao kwamba ahadi hizo zilikuwa ni za ukweli na Serikali sikivu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kitongoji alichokisema kama nilivyosema, mradi wetu wa densification ambao sasa tupo IIB utapeleka katika Vitongoji ambavyo vilikuwa havijapata umeme, lakini maeneo mengine ambayo hayajapata umeme kwa sasa kwa maana ya vijiji, vitongoji vilivyomo, tulivyovitaja 1,474 vitapata umeme pia katika awamu hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa wananchi kwamba umeme utapelekwa na ahadi ya Mheshimiwa Jackson Kiswaga itakuwa ni ya ukweli kuanzia mwezi Julai.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa swali la nyongeza kwa kuwa barabara ya kutoka Kalenga kwenda Ruaha National Park ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa hili hasa unaotokana na utalii na kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu ulishafanyika siku nyingi. Na kwa kuwa pia Serikali imeweka kwenye ilani tangu Awamu ya Nne mpaka sasa na imekuwa ikitenga fedha kidogo kidogo. Je, kwa nini sasa Serikali isianze kujenga kidogo kidogo kutokana na hizo pesa wanazotenga maana imekuwa ahadi ya muda mrefu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Kiswaga Mbunge wa Kalenga asubiri bajeti tutakayo pitisha nina hakikika ni kati ya barabara kama endapo bajeti itapita itakuwa ni kati ya barabara ambazo zitatekelezwa kuanzia bajeti tunayoiendea. Kwa hiyo, naomba awe na subira na asubiri tutakapo anza kupitia bajeti ya Ujenzi na Uchukuzi.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kuwa katika bonde lililoko katika Kijiji cha Nyenza kata ya Mabolilwa kumekuwa kuna mgogoro ambao umechukua miaka mitatu pale kwenye Mabaraza la Ardhi. Sasa kwa kuwa na wananchi wangu wameendelea kusumbuliwa kwenda na kurudi nilikuwa naomba kuuliza swali; je, sheria inampa mamlaka gani Waziri ya kuingilia kati endapo mgogoro umechukua muda mrefu kama huu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria Sura Namba 216 ambayo ndiyo inashughulika na utatuzi wa migogoro, Mheshimiwa Waziri hapaswi kuingilia maamuzi yanayotolewa na vyombo vya utoaji haki. Kama kuna changamoto yoyote ambayo inatokea katika maeneo hayo mlalamikaji anayo nafasi ya kumuona Msajili wa Mabaraza ya Ardhi kuweza kupeleka kero yake na atamsaidia hatua ya kwenda mbele zaidi.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri, pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa asilimia 90 mpaka 95 ya wateja wapya kwenye mitandao ya simu wanapatikana kutokana na mfumo huu wa freelancer na Kampuni yetu ya TTCL imekuwa ikisuasua katika kuongeza wigo wake.

Je, lini sasa TTCL au Wizara itaagiza TTCL waweze kutumia mfumo huu ili waweze kuongeza wigo wao?

Swali langu la pili ni kwamba mfumo huu wa freelancer siyo ajira kamili, I mean vijana wamekuwa wakilipwa kwa njia ya commission na haya makampuni kwa mfano yana vijana kama laki moja hivi ambao wako kwenye mfumo huo. Sasa kutokana na kutokuwa na sheria inayotambua mfumo huu, hawa vijana wamekuwa wakitumia wakati mwingine loophole ya kuyashitaki haya makampuni kwamba wameajiriwa na hivyo kuleta hofu ya haya makampuni kuendelea kuajiri hawa vijana.

Je, Serikali italeta lini hapa sheria ili sasa itambue mfumo huu kwamba ni mfumo kamili ambao unasaidia kuajiri vijana wengi ambao hawana kazi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI MAWASILIANO TEKNOLOJIA NA HABARI:
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga Gedion Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -

Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mbunge wa Kalenga Mheshimiwa Kiswaga kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya Jimbo na wananchi wake wa Kalenga. Haya ni matakwa ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia ukurasa wetu wa 96, 97, 98 na ukurasa wa 113 kuongeza wigo wa mawasiliano kufikia asilimia 94. Sasa kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tayari imeshatoa maelekezo kwa TTCL kuanza kutumia mfumo huu na mpaka sasa wana-agrigator watano na freelancer takribani 3000. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia hili ili waendelee kuongeza wigo mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la kamisheni kati ya freelancer na watoa huduma ni suala ambalo Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba inaweka mfumo mzuri ambao utatumika katika kusimamia ili kuwepo na uwajibikaji kwa freelancer pamoja na watoa huduma ili kuhakikisha kwamba tunaondoa hili gap ambalo lilikuwa linasababisha na kutokana na uhalifu uliokuwa unatokea sababu ya freelancer kutumia hizi national ID kwa matakwa yao na si matakwa ambayo yamewekwa kisheria, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa wananchi wa Kijiji cha Magulilwa, Kata ya Magulilwa, Jimbo la Kalenga walishamaliza boma la kituo cha afya siku nyingi sana; je, ni lini Serikali itatukamilishia ujenzi wa boma hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, likiwemo boma hili la Magulilwa la kituo cha afya na maboma mengine yote ya vituo vya afya na zahanati, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumefanya tathmini na kuorodhesha maboma yote na mpaka tarehe 31 Mei, 2021 tulikuwa na jumla ya maboma 8,003 ambayo tunayapa kipaumbele cha kutenga fedha kwa awamu ili yakamilike. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba boma hili la Magulilwa litapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa uvuvi haramu umeathiri sana mapato hasa kwenye mabwawa mengi, pamoja na Bwawa la Mtera ambapo Halmashauri ya Iringa Vijijini imekuwa ikipata mapato yake.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mabwawa yawe mashamba darasa kwenye Halmashauri nyingi pamoja na Jimbo la Kalenga ili tuweze sasa kufundisha vijana wengi pamoja na akinamama na akinababa waanze kutegemea uchumi wa kufuga samaki kupitia haya mabwawa ambayo yatakuwa ni mashamba darasa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mkakati wetu. Katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 kupitia mradi wa AFDP kwa maana ya Agricultural Fisheries Development Program II, tumetenga pesa kwa ajili ya kuweza kutengeneza mashamba darasa ya ufugaji wa Samaki. Hapa walengwa ni makundi ya vijana na akina mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkaribishe Mheshimiwa Kiswaga ili tuweze kushirikiana katika hatua hii. Yawezekana Wilaya ya Iringa Vijijini kwa maana ya Jimbo lake likawa ni sehemu ya wanufaika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mawakala wengi nchini wamekuwa wakisaidia sana wakulima kwa kuwakopesha mbolea na hivyo kuleta nafuu sana kwenye upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima; sasa suala hili limechukua miaka sita. Kwa mfano kwenye Jimbo langu kuna mama mmoja anaitwa Mama Renata Mbilinyi, anadai shilingi milioni 600 na sasa hivi amekaribia kufilisika: -

Je, Serikali haioni haja ya kuharakisha, kwa sababu jambo hili limechukua muda mrefu, ili kuleta nafuu kwa wakulima wetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama maelezo yangu ya awali yalivyosema, ni kwamba hatua za uhakiki zipo mwishoni na pindi zikikamilika, Mawakala wote watalipwa. Kilichochelewesha, kulikuwa na documents zilizokuwa zina- miss, baadhi ya Mawakala wengi walishindwa kuziwasilisha na Serikali iliona kuna umuhimu wa kuwapa muda zaidi kuziwasilisha ili iweze kutenda haki na mtu asidhulumiwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua zipo mwishoni, zikikamilika Mawakala wote watalipwa.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya tabianchi yamesababishwa sana na uharibifu wa mazingira; na mara nyingi ukipita katika milima hii ya Kitonga, Nyang’oro pamoja na kule Makombe unakuta kwamba watu wamekuwa wakichoma mkaa ovyo: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ulinzi sasa kwenye misitu hii ili uharibifu wa mazingira usiendelee. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mikakati mingi tunayoipanga katika kuhakikisha kwamba tunalinda mazingira, hasa katika maeneo hayo. Moja ni kwamba tunaendelea kutoa taaluma kwa wananchi kama sehemu ya wajibu wetu kuhakikisha kwamba wananchi hawaendelei na uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine kikubwa tunachokifanya, tunayo majeshi yetu kule au walinzi wetu ambao tunashirikiana nao na vikosi vingine vya ulinzi pamoja na Jeshi la Maliasili ambao mara nyingi huwa tunajitahidi kushirikiana nao kulinda mazingira katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini mpango wake wa 2024/2025 ni mbali sana. Ione uwezekano wa kurudisha kati 2023/2024. Maswali mawili ya nyongeza ni haya: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Mgama, kipo kituo cha afya na wananchi walishajenga msingi wa wodi, sasa uwezo wao wa kuendelea kujenga ni mdogo: Je, ni lini Serikali itatusaidia kuleta fedha ili tujenge wodi ili wananchi wa vijiji 12 wanaohudumiwa hapo wapate huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Pamoja na kwamba umesema Halmashauri itatenga Shilingi milioni 400, uwezo wa Halmashauri yetu bado siyo mkubwa hivyo. Aliyetangulia, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, aliahidi kuleta Shilingi milioni 300. Ni lini fedha hizo zitakuja Magulilwa ili tukamilishe hiki kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Gideon Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kata ya Mgama kwa kutoa nguvu zao kujenga kituo cha afya na kujenga msingi kwa ajili ya wodi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, afanye tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa wodi hiyo ili Serikali ione namna ya kutafuta fedha kwa kushirikiana Halmashauri kwa maana ya mapato ya ndani kukamilisha ujenzi wa wodi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri wa Nchi, aliahidi kupeleka Shilingi milioni 300 fedha ya Serikali kwa ajili ya kujenga kituo cha afya pale Magulilwa. Katika jibu la msingi tumetenga Shilingi milioni 400 kupitia mapato ambayo ndiyo fedha ya Serikali hiyo hiyo kwa kwa jili ya ujenzi wa kituo cha afya hicho. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park, tayari ilishapewa fedha kwa maana zile fedha za mkopo.

Je, ni lini sasa Serikali itatangaza tender ili hiyo barabara ianze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya kwenda Ruaha National Park Lusembe ina Kilomita 104 na inafadhiliwa na World Bank. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zote za kuandaa zabuni zimeshakamilika na muda wowote itatangazwa kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami barabara yote. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Kalenga lina skimu 19 na nyingi ni chakavu; je, ni lini sasa Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya ukarabati huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wakati najibu swali la Mheshimiwa Kunti, tunayo stock ya miradi yote ambayo ina changamoto na nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaingiza miradi yake pia katika mpango wetu na tutaipitia kuona inahitaji marekebisho gani.

Mheshimiwa Spika, lakini lengo letu kubwa hasa; sisi tulifanya kazi ya kupitia miradi yote, tunataka tufanye kilimo cha umwagiliaji kwa hiyo hatutaliacha eneo lolote, tutayafikia maeneo yote. Lengo letu ni kwenda katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliyetangulia, Mheshimiwa Ummy, alipita Jimbo la Kalenga na akaahidi kunipa shilingi milioni 300 katika Kituo cha Magulirwa pamoja na cha Kibena: Je, ni lini hizo fedha zitakuja ili tuweze kumalizia vituo hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ambacho amekiainisha hapa Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Mheshimiwa Waziri alienda akatoa commitment ya kupeleka fedha. Nasi tuna mpango wetu pale Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba ahadi zote za viongozi zipo katika mipango yetu. Kwa hiyo, litakapokuwa limekamilika hili, basi hizi fedha ambazo zimeahidiwa zitapelekwa katika hayo maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri aliahidi. Ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Bwawa la Mtera lililoko Halmashauri ya Iringa Vijijini kumekuwa na upungufu mkubwa wa Samaki na hivyo kuathiri biashara ya samaki katika Nyanda za Juu Kusini na masoko mengine.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga mashamba darasa ya samaki hasa Jimbo la Kalenga ili sasa tuweze kufundisha vijana wengi kufuga samaki na hivyo kufufua uchumi wa vijana kwa namna hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, juu ya mashamba darasa ya kufugia samaki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo program ambayo itakwenda katika baadhi ya Halmashauri zetu na yawezekana kabisa moja ya Halmashauri itakayofaidika na program hii ya mashamba darasa ya samaki ikawa ni Halmashauri ya Kalenga.

Kwa hiyo, naomba nilichukue jambo hili la Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kulifanyia kazi na wananchi wa Kalenga waweze kufaidika. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Jimbo la Kalenga tulileta maombi matatu ya kujenga majosho katika Kata ya Kiwele, Mgela, Saadani pale Masaka pamoja na Ifunda Udumuka.

Je, ni lini Serikali sasa itatuletea fedha hizo ili tujenge hayo majosho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, anayetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha miradi ya majosho katika vijiji alivyovitaja kwenye Jimbo la Kalenga.

Mheshimiwa Spika, tumeshapeleka jumla ya fedha, shilingi bilioni 5.4 katika Halmashauri 80 na tumebakiza kiasi kidogo cha takribani shilingi milioni 500 ambapo tunataka twende kukamilisha hivi sasa. Mheshimiwa Kiswaga nitaomba baada ya Bunge unipatie hivyo vijiji ili nitazame kuona kwamba kama ni katika vile vilivyosalia na hatimaye viweze kupata fedha na miradi ile iweze kukamilika.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo langu la Kalenga hasa Tarafa ya Kalenga tulipata shida ya mvua na tayari kata zile tumeshaleta maombi. Je, ni lini sasa Wizara itatupelekea chakula kwa haraka ili wananchi wangu wasife?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama maombi yake yamekwishawasilishwa ndani ya Ofisi ya NFRA, nataka nimhakikishie ndani ya siku mbili zijazo, mahindi yatamfikia katika jimbo lake.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini barabara ya kutoka Iringa Mjini kupita Kalenga kwenda Kilolo itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, itategemea na upatikanaji wa fedha na tunategemea barabara hiyo muhimu tuiweke kwenye mapendekezo kwa ajili ya kuijenga katika bajeti ambayo tunaiendea sasa hivi.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante kwa majibu mazuri. Pamoja na hayo nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Lakini pia nitumie fursa hii pia kumshukuru Waziri wa Nishati, kulikuwa na mradi uliosimama wa Solar pale katika kijiji cha Kilambo na sasa amenihakikishia unatekelezwa na naona unaendelea. Namshukuru kwa hiyo hatua maana nchi itapata umeme lakini pia wananchi wangu watapata ajira.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa tamko kwamba ifikapo 2022 Disemba tutakuwa tumemaliza changamoto za umeme kwenye vijiji. Katika Jimbo la Kalenga tuna vijiji vitatu ambavyo havina umeme vya Lwato, Makombe pamoja na Chamgo. Ni nini tamko la Serikali kutimiza hii ahadi yake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Serikali ilitamka kwamba itapeleka umeme kwenye vitongoji kwa maana ya umeme jazilizi, lakini tuna vitongoji vingi ambavyo vimekuwa na malalamiko kwa mfano kanisani pale Kiwele, Banawano pale Tosamaganga pamoja na pale Mangalali.

Je, ni lini Serikali itakamilisha suala hili? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali iliahidi kwamba itakamilisha umeme katika vijiji vyote ambavyo havikuwa na umeme kufikia Disemba, 2022 na ahadi hiyo bado ipo kwa sababu mikataba ilishasainiwa na wakandarasi wako site katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huu wa REA wa 300 mzunguko wa pili na tunaamini kwa kuendelea kusimamia mikataba hii kwa wakati itakamilika ili vijiji vyote ambavyo vilikuwa havina umeme viweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili ni kweli kwamba tunavyo vitongoji vingi ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme, lakini Serikali kama ilivyoeleza kwenye swali la msingi ni kwamba tayari umeme jazilizi utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao na kwa kadri ya pesa inavyopatikana huduma hii itazidi kuendelezwa kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapata umeme na watumiaji wote wanaweza kupata umeme kwa wakati.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga vyumba vya kuhifadhia maiti katika Vituo vya Afya vya Nzihi pamoja na Kiponzero? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilishatoa maelekezo ya Halmashauri zote kuanza kwa kutumia mapato ya ndani kwa ujenzi wa miundombinu ambayo iko ndani ya uwezo wao ikiwemo majengo ya kuhifadhia miili ya marehemu kwa maana ya mochwari. Kwa hiyo, naomba Halmashauri ya Wilaya ya Iringa iangalie uwezekano wa kuanza ujenzi wa mochwari kwenye vituo vya afya vya Nzihi na Kiponzero. Pia Serikali tukipata fedha, tutaunga mkono juhudi hizo za Halmashauri. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Shule za Jimbo la Kalenga pamoja na Shule ya Kalenga Primary School karibu kabisa na fuvu la Mkwawa haina maji. Je, ni mpango gani wa Serikali wa kuchimba visima sasa badala ya kupeleka maji ya mserereko maana kuchimba visima ni kazi rahisi katika shule zote za Jimbo la Kalenga? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uchimbaji wa visima katika maeneo ambayo ni rafiki tutaendelea kwa sababu tayari tunafanya zoezi hilo. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge wa Kalenga kama eneo lake linafaa kwa visima mantahofu visima vitakuja kuchimbwa na watoto watapata maji shuleni.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kijiji cha Ndihuli kilichopo Kata ya Magulilwa kilijenga boma zaidi ya miaka saba. Je, ni lini sasa Serikali itatuonea huruma ipeleke fedha hapo tuweze kumalizia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awasilishe maombi hayo kupitia kwa Mkurugenzi ili tuweze kuona namna ambavyo tutatenga fedha kwenye bajeti za miaka ijayo kwa ajili ya kukamilisha boma hili kwa ajili ya zahanati.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwezi Desemba Meneja Mkoa wa Iringa ndugu yangu Jumbe aliniahidi kupeleka umeme katika Kijiji cha Usengerenidete, mpaka sasa nimeshapelekwa kwenye vyombo vya habari mara nne, je, ni lini sasa TANESCO watatoa angalau fedha za dharura kutoka Makao Makuu watupelekee hili hao wananchi wapate umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ameomba yeye mwenyewe fedha za dharura na jambo hili nilikuwa sijalipata naomba baada ya session hii ya maswali, niende kwake tukajadiliane, nijue tatizo ni nini na tuweze kulitatua tatizo hilo ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo ya umeme. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza: -

Je, ni lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Kata ya Kiwele, Kijiji cha Kiwele na Kata ya Nzihi, Kijiji cha Kipera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokuwa nimeshasema hapo awali, tayari maelekezo yalikuwa yametolewa kwa mameneja wote wa TARURA wa mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatenga fedha kwenye barabara hizi na madaraja haya ambayo ni viunganishi vya kata na kata na Wilaya na Wilaya. Na ninaamini katika barabara ambayo Mheshimiwa Kiswaga ameitaja nayo Meneja wa TARURA Mkoa na Wilaya watakuwa nayo wameifanyia kazi.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo langu la Kalenga limekuwa halina chanzo cha uhakika cha maji ambacho kinaweza kikapeleka maji kwenye kata zaidi ya moja. Mfano Kata ya Masaka haina maji kabisa. Je, ni lini sasa Serikali itatafuta chanzo kimoja kikubwa ili tuweze kupeleka maji zaidi ya kata moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo haya anayotaja Mheshimiwa Mbunge ambaye ni Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira. Ni kweli vyanzo vyake vinapata changamoto kama chanzo kile cha Nyamlenge kwa sasa tunashuhudia wote kwamba kinaendelea kujaa mchanga lakini watu wetu wa bonde wanaendelea kufanya kazi nzuri kuhakikisha vyanzo vinabaki salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maeneo yote ya Kalenga tunaendelea kufanya utafiti, tunatarajia kutumia labda Mto Lyandemberwa ambao unaweza ukasaidia eneo la Kalenga kupata maji safi na salama yakiwa bombani.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitakuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa imethibitika pasipo shaka kwamba maendeleo sio miujiza. China wana Vyuo karibu 7,294 vya shule za ufundi. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Sera ya kuwa na vyuo kama ilivyokuwa kwenye Sera ya Afya kwamba kila Kata, sasa Sera hii iende kwenye kila jimbo na hasa majimbo ya vijijini ili tuwafundishe sasa watu wetu kulima katika maeneo madogo, tija kubwa pia ili waweze sasa kubadilisha udongo badala ya kuchoma majani wawe wanafukia? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua sana umuhimu wa elimu ya mafunzo ya amali ambayo mara nyingi tunaita mafunzo ya ufundi stadi na ndio maana sasa hivi tume-register vyuo takribani 809, vya Serikali 77 na vingine vilivobaki ni vya watu binafsi na bado vile vile Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi stadi 65, kimoja cha Mkoa wa Songwe na Vingine 64 kwa ajili ya kila wilaya. Pamoja na hivyo kama ambavyo tutakuja kulieleza Bunge lako katika Semina ambayo tutakuja kukuomba, Mabadiliko ya Sera na Mitaala ambayo yanafanyika yataongeza ufundishaji wa elimu ya amali (ufundi stadi katika Shule za Serikali) ili kuhakikisha kwamba kweli tunaongeza ujuzi kwa wanafunzi wetu wanaohitimu, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika barabara muhimu kiuchumi kutoka Kalenga kwenda Uwasa imeharibika sana eneo moja la Kiponzelo.

Je TARURA inampango gani wa dharura kuweza kutupa fedha kwa ajili ya kurekebisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa barabara hizi ambazo zimeathirika sana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini TARURA ilikuwa na bajeti ya bilioni 11 kwa ajili ya dharura lakini sasa wameomba fedha iweze kuongezwa kutoka bilioni 11 na kwenda bilioni 46 ili kuweza kutengeneza barabara mbalimbali nchini ikiwemo za Kalenga kule kwa Mheshimiwa Kiswaga.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya kwenda Ruaha

kutoka Iringa Mjini iliahidiwa kwamba tutatangaza mwezi wa sita, mpaka sasa haijatangazwa; je, tutatangaza lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kulikuwa na taratibu zilikuwa bado hazijakamilika lakini zinakamilika, na baada ya hapo hiyo barabara itatangazwa ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kituo cha Afya cha Nzihi na Kituo cha Afya cha Mgama kwa kweli havina kabisa wodi za akina baba na wamekuwa wakilalamika muda mrefu na nimeshaomba mara kadhaa. Je, ni lini sasa Serikali itatujengea hizo wodi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa wodi katika Kituo cha Afya Nzihi na Kituo cha Afya Mgama kama nilivyokwishakusema kwenye majibu ya msingi, Serikali baada ya ujenzi wa vituo vya 807 sasa tunaenda kuona ni namna gani tunapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi kwenye vituo vya afya vilivyofanyiwa ukarabati na kupewa majengo yale ya awali yaliyoenda kujengwa katika vituo vya afya na tutaangalia pia kuhusu Kituo hichi cha Nzihi na Mgama.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Kalenga Kata za Masaka pamoja na Kianga zina changamoto ya mawasiliano kwa muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipokee changamoto ya mawasiliano hayo ili tuweze kukaa na kuweza kuyapitia vizuri lakini naamini kwamba katika kata zake, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna minara tumempelekea katika jimbo lake na tunaamini kwamba kwa kiasi hicho kikubwa ni zaidi ya asilimia 70 ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hizi kata ambazo amezitaja tunazipokea kwa ajili ya utekelezaji, ahsante sana.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Iringa Vijiji ina majimbo mawili ambayo ni Kalenga pamoja na Isimani na tayari upande wa Isimani mwenzangu alishaomba tupate Halmashauri. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ombi hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kupandisha hadhi majimbo kuwa Halmashauri yanafuata vigezo, na Halmashauri ambazo hapo nyumba zilikidhi vigezo zilipewa hayo mamlaka. Kwa hiyo, hili lililoombwa na Halmashauri ya Isimani maana yake lipo katika utekelezaji, kwa hiyo, sisi kazi yetu ni kuendelea kupitia vigezo na jambo hili litakapokuwa limekamilika maana yake tutatangaza kupitia sheria ambazo ziko nchini. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali kwa majibu mazuri, ingawa shule hii ya Kalenga tayari imeshatimizi vigezo. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Kata nyingine ya Sekondari ya Isimila ambayo ina Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, hii ina wasichana na wavulana. Mwaka 1999 aliyekuwa Rais wakati huo Mheshimiwa Hayati Mkapa alipita pale na akaahidi kujenga ukuta ili kuwalinda wanafunzi pale lakini mpaka leo haujakamilika.

Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunafahamu kule Marekani wameanzisha kitu kina Ben Carson Reading Clubs, huyu mwana sayansi Ben Carson alipata maarifa yake kwa kusoma kwenye maktaba.

Je, Serikali ni lini sasa itajenga Maktaba kwenye shule za Kata zote katika Jimbo la Kalenga.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ambayo ilitolewa ya ujenzi wa ukuta katika shule ya sekondari Isimila bado ipo na sisi niseme tu kwamba katika mipango yetu tumeiweka, kikubwa ambacho tunatafuta sasa hivi kwa sababu tuna mipango mingi sana ya kutafuta fedha, tutakapopata fedha kwa ajili ya kujenga maana yake tutaanza haraka iwezekanavyo. Lengo la Serikali kwa sasa ni kuhakikisha shule zote nchini zinapata maktaba zikiwemo hizo za Kalenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kikubwa tu ambacho tunabanwa sasa hivi ni bajeti lakini tunaendelea kutafuta fedha na ninaamini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan tunaweza tukalifikia hili kama tulivyofanikiwa kwenye madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali sasa nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa kuwa katika Mahakama ya Tarafa iliyopo pale Kiponzelo ilishatokea miaka ya nyuma hapo kwamba wakati mtuhumiwa anasafirishwa kwenda Ifunda alitoroka na kuonesha kwamba kulikuwa hakuna usalama.

Je ni lini sasa Serikali itaanza angalau kujenga vituo hivi vya polisi kwenye maeneo ya Tarafa hasa pale Kiponzelo?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili Ifunda tuna Kituo cha Polisi kikubwa bahati mbaya hatuna gari wala nyumba za polisi; je, ni nili Serikali sasa itaturekebishia angalau kupata gari hapo Ifunda? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu mfungwa aliyetoroka kwasababu ya umbali kama nilivyosema katika nyakati tofauti ninapojibu maswali haya kadri tutakapopata fedha tutajenga vituo vya polisi viwe karibu kabisa na maeneo ambayo yanahitajika ikiwemo karibu na Mahakama zilizopo ngazi ya Tarafa na ninajua pia mpango wa Serikali upande wa Wizara ya Katiba na Sheria ni kuweka Mahakama hizi katika kila Kata. Kwa hiyo niendelee kusisitiza wadau mbalimbali wakiwemo Serikali za Mitaa wadau kama yeye Mheshimiwa Kiswaga mwenyewe ana mpango wa kusaidia kujenga kituo cha polisi, vituo hivi vitakapojengwa tutapeleka askari.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali la pili kwamba kuna kituo lakini hakina gari wala nyumba nimeeleza mara kadhaa hapa kulingana na bajeti yetu ya mwaka huu na mkataba tulionao na kampuni ya Ashok Leyand tunayo magari ambayo tutapokea 78 mwezi huu, lakini vilevile hayo magari 78 yameshapokelewa ni taratibu za kuyatoa bandarini lakini mpaka mwezi Septemba tutakuwa tumekamilisha magari 396. Maeneo yenye changamoto kama haya ya Kalenga yatazingatiwa, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ameshasaini mkopo wa trilioni 1.2 ambao unahusisha ujenzi wa barabara kadhaa, viwanja kadhaa pamoja na barabara ya kwenda Ruaha National Park inayopita Jimboni Kalenga.

Je, ni lini sasa Serikali tutegemee kuona kazi zinaanza kutekelezeka? Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; napenda kujibu swali la nyongeza la Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, World Bank wameshakubali kuijenga barabara ya kutoka Iringa kwenye Ruaha National Park na ni kati ya hizo fedha ambazo ni 1.7 trillion. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo sasa kinachosubiriwa tu nikuanza taratibu za manunuzi. Ahsante.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa barabara kutoka Iringa kwenda Pawaga kupita Kihwele - Kalenga ipo kwenye kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Je, ni lini sasa Serikali itaweza kuijenga kwa kiwango cha lami? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara iliyotajwa ipo kwenye Ilani lakini tu nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuwezi tukaanza barabara zote kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kadri tutakavyokuwa tunakwenda basi hii barabara itakuwa ni moja ya barabara ambazo zitajengwa kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kiponzero ni moja ya vituo kongwe katika Jimbo la Kalenga, bahati mbaya mpaka leo hakina cha chumba cha mortuary; je, ni lini Serikali itatupa jokofu pamoja na chumba cha mortuary?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza na narejea kusema kwamba maelekezo yameshatolewa kuhakikisha kwamba Wakurugenzi wanajenga majengo ya kuhifadhia maiti. Pia wananunua majokofu katika vituo vyote vilivyopo ambavyo vinatoa huduma kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, namuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa Vijijini kuhakikisha wanaanza kujenga jengo la mortuary, lakini pia wananunua jokofu kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kiponzero, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Kalenga limekuwa kinara wa kuendeleza mila na tamaduni; je, Serikali haioni haja sasa ya kutujengea hata kituo cha utamaduni katika Jimbo hilo la Kalenga ili tuweze kuendeleza utamaduni wetu wa Kihehe? (Makofi)

Swali namba mbili, kwa kuwa Makumbusho ya Mkwawa ambayo ndiyo sehemu ya kuenzi mila na tamaduni zetu yako katika eneo la makaburi ya familia ya Mkwawa na Uchifu wa Mkwawa upo hai. Je, Serikali haioni haja sasa katika vile viingilio wakawa wanatupa hata asilimia moja au mbili ili kuendelea kuimarisha ule utamaduni wetu na uchifu wetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusuana na kujenga kituo cha utamaduni pele Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, inaendelea kufanya tathmini ya kutambua maeneo ya kiutamaduni ili kutoa maelekezo mahsusi kwa mamlaka husika za mikoa na wilaya, namna ya kuyaenzi na kuyahifadhi maeneo haya. Kwa hiyo, hili la kujenga kituo cha utamaduni pale Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge ninalichukua na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo italifanyia kazi na muda utakaporuhusu tutaweza kufanya hivyo. (Makofi)

Swali lake la pili kuhusuana na sehemu ya malipo ya maonesho ya kaburi la Chifu Mkwawa kwenda kwa familia, namuahidi Mheshimiwa Mbunge pia nalichukua na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Makumbusho ya Taifa kuona namna ambavyo hili linaweza kufanyika na familia ya Chifu Mkwawa ikaweza kufaidika na sehemu ya kiingilio cha makumbusho yale, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kiponzero ni moja ya vituo kongwe katika Jimbo la Kalenga, bahati mbaya mpaka leo hakina cha chumba cha mortuary; je, ni lini Serikali itatupa jokofu pamoja na chumba cha mortuary?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jackson Kiswaga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza na narejea kusema kwamba maelekezo yameshatolewa kuhakikisha kwamba Wakurugenzi wanajenga majengo ya kuhifadhia maiti. Pia wananunua majokofu katika vituo vyote vilivyopo ambavyo vinatoa huduma kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, namuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa Vijijini kuhakikisha wanaanza kujenga jengo la mortuary, lakini pia wananunua jokofu kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kiponzero, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na ahadi ya Mheshimiwa Waziri kutembelea Jimbo la Kalenga ambalo najua Waziri ataifanya, lakini napenda kujua ni lini sasa atatupa fedha za haraka angalau turekebishe Bwawa la Wellu katika Kata ya Ruanda ili lisaidie wananchi pale katika kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaelekeza timu ya wataalam kufika katika eneo husika, mimi mwenyewe pia nitafika, ili tuone hali halisi na tuone namna ya kuweza kuwakwamua wananchi katika eneo hilo kwa sababu tumejipanga kuhakikisha kwamba sekta hii ya umwagiliaji inachukua hasa kipaumbele katika bajeti yetu inayokuja. Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mimi mwenyewe nitafika na wataalam watafika kuoa namna ya kuweza kuwa-rescue wananchi katika eneo hilo.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kuwahakikishia wananchi wa Masaka kwamba sasa unapeleka mawasiliano. Pamoja na majibu mazuri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Kalenga lilipewa minara kumi: Je, hizo Kata nyingine za Kihanga pamoja na Ulanda nazo zitajengwa kwa pamoja? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimetoa ufafanuzi, miradi yote ambayo imeshaainishwa katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali upo katika hatua ambazo nimemaliza kuzielezea na tuwe na subira Waheshimiwa Wabunge. Naamini kabisa kwamba, hatua zote ambazo ni za ndani zikishakamilika, sasa tukishahamia site na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kusimamisha ile passive structure haimalizi hata wiki tatu na ukija kuhakikisha kwamba unafunga zile active equipment haimalizi hata wiki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukishamaliza process za ndani hizi, tukahamia site nina uhakika ndani ya mwezi mmoja au miwili minara hiyo itakuwa inakamilika katika kila eneo ambalo tutakuwa tunapeleka huduma ya mawasiliano, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Ruaha National Park utasainiwa?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Barabara ya Iringa – Msembe – Ruaha National Park, sasa hivi tuko kwenye evaluation na inafadhiliwa na World Bank. Baada ya kukamilisha taratibu hizo, barabara hiyo itaanza kujengwa. Ahsante.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali hii ya Awamu ya Sita inatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Katibu Mkuu Daniel Chongolo ambaye ni mstaafu, alivyopita Jimbo la Kalenga aliahidi kuleta shilingi milioni 500 kujenga Kituo cha Afya Kata ya Lyamgungwe ndani ya miezi mitatu: Je, Serikali itatekeleza lini agizo hili ambalo ni halali kabisa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inatekeleza kwa ufanisi mkubwa sana Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na maeneo yote ambayo Serikali imeahidi kujenga vituo vya afya baada ya kujiridhisha na vigezo, tutakwenda kupeleka fedha kwa awamu kwa ajili ya kujenga vituo hivyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Kiswaga kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, itakwenda kufanya tathmini eneo hilo kuona kama linakidhi vigezo na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, ahsante.