Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jackson Gedion Kiswaga (14 total)

MHE. JACKSON G. KISWAGA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kiasi cha shilingi milioni 200 zilizoahidiwa na Waziri wa Maji Mwaka 2017 alipotembelea mradi wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Magubike Kata ya Nzihi uliokarabatiwa na WARID kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.3?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa maji Kijiji cha Magubike upo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Mradi huo unahudumia vijiji sita vya Kata ya Nzihi ambavyo ni Nzihi, Kipera, Kidamali, Nyamihuu, Magubike na Ilalasimba. Kwa lengo la kuboresha huduma ya maji katika vijiji hivyo na kufikisha huduma ya maji katika vitongoji vingine ambavyo havina huduma ya maji, mwaka 2017 Waziri wa Maji aliahidi kutuma shilingi milioni 200 kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa Magubike.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza ahadi hiyo, Serikali mwezi Juni na Agosti, 2021 imetuma jumla ya shilingi milioni 180 ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita tisini elfu katika kijiji cha Nzihi, ulazaji wa bomba umbali wa kilomita 11.25 kwa ajili ya jamii kuingiza maji majumbani. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2021 na kukamilika ifikapo mwezi Januari 2022. Kukamilika kwa kazi hizo kutaboresha huduma ya maji katika vijiji husika pamoja na vitongoji vya Mji mwema B, Mbega na Kayungwa ambavyo havina huduma ya uhakika ya maji.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawafanya Wabunge kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Ardhi kutokana na ukweli kwamba migogoro mingi ya ardhi na mashamba hupelekewa kesi wao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu namba 27 cha Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi, Sura Namba 216, baadhi ya watu wenye madaraka kama vile Wabunge, Wajumbe wa Halmashauri za Wilaya, Kata na Vijiji hawana sifa ya kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya. Lengo la kifungu hiki ni kuwezesha mgawanyo wa madaraka na utendaji kazi katika Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wabunge ni wawakilishi wa wananchi wote katika maeneo yao endapo Mheshimiwa Mbunge atakuwa Mjumbe wa Baraza la Ardhi, wakati wa kutoa maoni ama maamuzi yanayompa ushindi mwananchi wa upande mmoja na kumnyima ushindi mwananchi wa upande wa pili suala hili linaweza kusababisha malalamiko yanayohusu mgongano wa maslahi kutokana na nafasi zao.

Aidha, Wizara yangu inaendelea kutoa elimu kwa Wajumbe wa Mabaraza ya Kata, Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Umma kwa ujumla kuhusiana na taratibu za utatuzi wa migogoro ya ardhi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni uamuzi wa kutaka ifikapo tarehe 1 Mei, 2021 wasajili wa namba za simu za mkononi mitaani (freelancers) wawe katika maduka unaweza kufuta ajira zaidi ya 40,000 na kudhoofisha lengo lake la ajira milioni nane ifikapo mwaka 2025?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalanga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tarehe 16 Februari, 2021 Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwaelekeza watoa huduma kutekeleza takwa la kikanuni la usajili wa laini za simu kibayometria kwa kuwatumia mawakala wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni ya 10 ya Kanuni za Usajili wa Laini za Simu ya 2020 (The Electronic and Postal Communications (SIM Card Registration) Regulations, 2020 GN No. 112 ya 2020.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa freelancers kwenye sekta, kiuchumi na katika kulinda ajira zao, tarehe 14 Aprili, 2021 Serikali ilisitisha zuio kwa watoa huduma kutowatumia freelancers katika usajili wa laini za simu kibayometria, kwa kutoa taarifa kwa umma na kwa kuwaandikia watoa huduma barua ya kuondoa zuio hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma imetengeneza rasimu ya mwongozo wa kuwatambua na kuratibu kazi za freelancers ili kuondoa mapungufu yaliyojitokeza na kuweka bayana uhusiano kati ya watoa huduma na freelancers, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isiwalipe angalau robo ya madai Mawakala wa mbolea za ruzuku katika Jimbo la Kalenga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa madai ya mawakala walioshiriki katika utoaji wa rukuzu ya pembejeo za kilimo kwa msimu wa 2014/2015 na 2015/2016 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jimbo la Kalenga. Wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku, uhakiki wa awali uliofanyika na kubaini kuwepo kwa udanganyifu. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuchukua hatua za kufanya uchunguzi na uhakiki wa kina ili kubaini kiasi halisi cha fedha kinachopaswa kulipwa.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, uhakiki wa madai ya mawakala upo katika hatua za mwisho. Mara uhakiki ukiisha, malipo yatafanyika. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga Vituo vya Afya katika Kata ya Lyamugungwe na Kihanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipeleka Shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vitatu katika Wilaya ya Iringa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kupitia mapato ya ndani imetenga Shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Magulilwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya Kata ya Lyamungungwe na Kihanga, Serikali itajenga Kituo cha Afya cha kimkakati katika Kata ya Kihanga ambayo itatengewa fedha kwenye bajeti ya mwaka 2024/2025. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Maabara kwenye Zahanati zote za Jimbo la Kalenga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya afya kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi ya afya ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka fedha shilingi bilioni 27.8 kukamilisha maboma ya zahanati 555. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma ya zahanati 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kalenga lina jumla ya zahanati 36 na kati ya hizo, zahanati 11 zinatoa huduma za maabara na zahanati 25 zinatoa huduma za maabara za msingi. Ili kuboresha huduma, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za maabara katika zahanati zote nchini zikiwepo zahanati za Jimbo la Kalenga, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka transfoma yenye uwezo mkubwa wa njia tatu katika Kijiji cha Nyamihuu Kata ya Nzihi Jimboni Kalenga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Nyamihuu ni miongoni mwa vijiji vilivyopata huduma ya umeme kupitia miradi ya usambazaji wa umeme vijijini awamu ya kwanza (REA I) na kufungiwa transfoma ya KVA 100. Huduma ya umeme katika kijiji hiki imesambazwa katika vitongoji nane kati ya vitongoji 12. Vitongoji vinne vilivyobaki vimewekwa kwenye mpango wa kusambaza umeme jazilizi unaotarajiwa kutekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mwaka wa fedha 2022/ 2023.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali imepanga kuongeza transfoma ya pili yenye uwezo wa KVA 100 katika kitongoji cha Wilolesi katika kijiji cha Nyamihuu ili kupunguzia mzigo wa transfoma iliyopo kuhudumia kijiji chote.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italifanya somo la kilimo kuwa la lazima kwenye Vyuo vya Ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi kutoa mafunzo yanayozingatia shughuli za kiuchumi za maeneo husika na Taifa kwa ujumla ili kuwawezesha wananchi kutumia kikamilifu fursa na rasilimali zilizopo nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imekuwa ikifanya upembuzi yakinifu kabla ya uanzishaji wa fani za ufundi ili kubaini mafunzo yanayofaa kutolewa katika vyuo hivyo kulingana na fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo husika. Kozi ya kilimo ni miongoni mwa Kozi zinazotolewa katika Vyuo vya Ufundi Stadi vya Kihonda, Dakawa, Katavi, Arusha na Manyara. Aidha, katika Vyuo vipya 64 vya Wilaya vinavyojengwa, kutakuwa na karakana moja kwa kila

chuo kwa ajili ya kutoa mafunzo yatakayozingatia shughuli za kiuchumi katika eneo husika ikiwemo kilimo, nashukuru.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Vituo vya Afya vya zamani ikiwa ni pamoja na kujenga Chumba cha kuhifadhi Maiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya. Tayari Ofisi ya Rais TAMISEMI, imekwishakusanya orodha ya vituo vya afya vinavyohitaji ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais TAMISEMI, ilipoanza kusimamia mpango maalum wa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya msingi mwezi Oktoba 2023, jumla ya vituo vya afya 379 kati ya vituo vya afya 697 vimekarabatiwa na kuongezewa miundombinu iliyopungua ikiwemo wodi za uzazi, vyumba vya upasuaji na majengo ya kuhifadhia maiti. Jumla ya majengo 117 ya kuhifadhia maiti yamejengwa na kuwekewa majokofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kukarabati vituo vya afya 50 kupitia fedha za Mfuko wa Afya wa Dunia, ili kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa mama mjamzito. Serikali, itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati vituo vya afya ili kuviwezesha kutoa huduma zinazokosekana likiwemo jimbo la Kalenga.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini Barabara kutoka Kijiji cha Kalenga kupitia Kata za Ulanda, Maboga, Wasa - Madibila zitapandishwa kuwa za Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya Mwaka 2007, kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya Mwaka 2009, Kifungu cha 43(1) na (2) na kifungu cha 44(1) kupitia Tangazo la Serikali Namba 21 la tarehe 23 Januari, 2009, limeainisha vigezo vya utaratibu wa kupandisha au kuteremsha hadhi barabara toka daraja moja kwenda daraja lingine.

Mheshimiwa Spika, mapitio ya upandishaji hadhi wa barabara hii ulifanyika mwaka 2019 na Wizara Ujenzi na Uchukuzi, yalibaini barabara hiyo kukosa sifa kama barabara ya mkoa (regional road) na hivyo kupewa hadhi ya barabara za Wilaya katika kundi la mkusanyo (collector roads).
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule ya Sekondari Kalenga iliyopo Kata ya Ulanda kuwa ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maelekezo ya Serikali ni kuwa na Shule ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita katika kila Tarafa zikiwemo Tarafa zilizoko katika Jimbo la Kalenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatafuta fedha katika mwaka 2022/2023 za ujenzi wa bweni la kulalia wanafunzi ili kukamilisha vigezo vya kupandishwa hadhi ya kuwa na Kidato cha Tano na Kidato cha Sita.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi katika Mahakama za Kata nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuwa na vituo vya polisi kila kata na ndio maana imeanzisha utaratibu wa Polisi Kata inayoongozwa na Mkaguzi wa Polisi. Ujenzi wa vituo hivyo utaendelea kufanyika kwa awamu kutegemea upatikanaji wa fedha. Vituo hivyo hutumiwa na mahakama zilizoko kwenye kata husika pindi vinapohitajika, nashukuru.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaenzi Tamaduni za Makabila ili kulinda maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunaenzi tamaduni za makabila kwa lengo la kulinda maadili ya Mtanzania Serikali inafanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamza ni kuendesha Tamasha la Kitaifa la Utamaduni ambalo hufanyika kila mwaka. Tamsha hilo linashirikisha vikundi vya utamaduni kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara na Visiwani, ambalo linahusisha shughuli mbalimbali za kiutamaduni, kama vile maonesho ya vyakula vya asili, urembo na utanashati, michezo ya jadi, teknolojia na sayansi jadia. Pia, Tamasha hilo linahusisha mashindano ya ngoma za asili, upishi na uandaaji wa vyakula vya asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hayo, Tamasha hilo huambatana na mdahalo wa namna ya kupambana na mmomonyoko wa maadili. Hivyo kupitia tamasha hilo, wananchi wanasherehekea, wanaenzi, wanatunza na kuendeleza tamaduni zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili Serikali inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kama vile makongamano, semina, mikutano na warsha kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuthamini utamaduni na maadili ya Mtanzania

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, inaendelea kufanya Tafiti mbalimbali ili kubaini mila na desturi zinazo kubalika katika jamii ili ziendelezwe na zisizofaa waachane nazo, ambapo hadi sasa jumla ya tafiti 286 kuhusu mila na desturi za maeneo ya Kihistoria zimefanyika;

Mheshimiwa Mwenyekiti na mwisho inaendelea kushirikiana na wadau na kuwahimiza kufanya matamasha mbalimbali ya utamaduni nchini kote, ili kuhakikisha mila, desturi na tamaduni zetu zinalindwa na kuendelezwa.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu Kata ya Masaka – Kalenga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliingiza Kata ya Masaka katika zabuni ya kufika huduma ya mawasiliano Vijijini kupitia Mradi wa Tanzania ya Kiditali, ambapo Kampuni ya Simu ya Vodacom ilishinda zabuni hiyo ya kufikisha huduma hiyo katika Kata ya Masaka yenye Vijiji vya Kaning’ombe, Saadani pamoja na Makota. Mpaka sasa Vodacom inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji katika ujenzi wa mnara huo.