Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Exaud Silaoneka Kigahe (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya ya kufanya kazi ya kujadili na kupitisha Bajeti za Wizara mbalimbali hapa Bungeni. Lakini pia kwa namna ya pekee, naomba niwashukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, wewe Mwenyekiti na Wenyeviti wenzako wenza, Wabunge kwa namna ambavyo mnatuongoza katika Bunge hili kwa weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara na Viwanda na Biashara iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambaye ndiye Waziri wa Viwanda na Biashara. (Makofi)

Naomba pia Wabunge wenzangu wote tuunga mkono bajeti hii ambayo imezingatia miongozo mikuu ya Kitaifa hususan Dira ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea baadhi ya hoja kidogo kulingana na muda. Lakini, hoja nyingine nitamuachia Mheshimiwa Waziri ambaye ndiye mwenye Wizara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niongelee kuhusu ukaguzi wa bidhaa (destination inspection) hususan imeongelewa kuhusu magari hasa yaliyotumika. Utakumbuka kuwa ukaguzi huu sio mara ya kwanza sasa kufanyika katika nchi yetu, umeshakuwa unafanyika huku nyuma, lakini kutokana na baadhi ya changamoto ndiyo tulibadilisha baadaye kuanza kuwa na ile pre-verification of conformity to standards (PVOC) kwa maana ya kukagua nje bidhaa hizo kabla ya kuingia nchini na hasa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona changamoto ambazo tumekuwa tukizipata na Waheshimiwa Wabunge wanajua, kwanza kulikuwa kuna ukosefu mkubwa sana wa ufanisi katika ukaguzi wa magari yao huko nje. Kwanza tozo iliyokuwa inatozwa kodi zile zilikuwa nyingi, muagizaji alikuwa anatakiwa kulipa takribani dola 150 kwa ajili ya ukaguzi ule. Lakini zaidi ya hapo, usumbufu zaidi anapotuma kule, walikuwa wanatuma hela zaidi ya dola 100 kwa hiyo, unatuma dola 150 ya ukaguzi lakini pia unatuma na dola 100 kwa ajili ya handling ya yale makampuni ambayo yanafanya kazi ya ukaguzi kule. Kwa hiyo, unakuta mtu anatuma dola 250 badala ya dola 150. Kwa hiyo, gharama kubwa ya ukaguzi na upimaji ilikuwa ni moja ya changamoto ambazo zilikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mawakala wengi kutokuwa na ofisi na hivyo kuwa na changamoto kidogo kwenye ukaguzi huo. TBS sasa imeanza kukagua magari hapa nchini kuanzia mwezi Machi, 2021 na hakika kazi hii inaenda vizuri na nikutaarifu tu na Bunge lako kwamba kazi ya ukaguzi wa magari yaliyotumika nje unaenda vizuri na baadhi ya changamoto za kawaida ambazo ndizo tunategemea kwa mfano sasa tunapokagua pale baadhi ya magari ambayo hayakidhi viwango yanapewa muda wa kwenda kutengenezwa, halafu yanarudishwa kupata ile certificate ya TRA. Tumeshapata eneo la UDA pale ambapo magari yale ambayo yanahitaji kutengenezwa yanakaa pale yakishatengenezwa taarifa zile zinarudishwa TBS, TBS wanapeleka TRA wanapata ile certificate ya ukaguzi wanaendelea. Nina uhakika asilimia 80 ya magari yaliyokuja sasa yako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na utaratibu uliokuwepo sasa hivi ni kwamba TBS wanashirikiana na wameshatoa maelekezo kwa kampuni yanayouza magari kule nje kuhakikisha kwamba wanaleta magari yenye ubora. Kwa hiyo, na sisi tunatoa rai kwa waagizaji wote wa magari kutoka nje watumie kampuni ambazo zinafahamika. Wasiagize kwenye kampuni ambazo hazifahamiki kwa sababu zile kampuni zimeshapewa maelekezo ya namna ya ubora ambao tunautaka sisi kama nchi kwenye magari ambayo yanaingizwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili suala la ukaguzi wa magari au bidhaa za kutoka nje, lengo kubwa ni kuhakikisha tunakuwa na bidhaa zenye ubora na hivyo tukishamaliza hili tutajiimarisha tayari zaidi ya shilingi bilioni 60 zimeshatengewa kwa ajili ya kuweka mitambo ambayo itafanya ukaguzi wa magari lakini baadaye kukagua bidhaa nyingine ambazo zinaingizwa kutoka nje. Kwa hiyo, lengo ni kuona kwamba bidhaa nyingi zinakaguliwa sasa nchini ili kuepuka baadhi ya kampuni huko nje kutumia udanganyifu lakini pia na wafanyabiashara wengine kuingiza bidhaa ambazo hazina ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusu Electronic Tax System. Huu ni mfumo ambao ulianzishwa kwa ajili ya kukusanya kodi kwa njia za kielektroniki. Lengo kubwa la mfumo huu lilikuwa ni kukusanya kodi ya Serikali. Makampuni au wafanyabiashara wengi hasa wenye viwanda walikuwa na questionable integrity. Ndiyo maana Serikali ikaona sasa ili kuondoka na tatizo hili la kutokuwa waadilifu kwa wafanyabisahara integrity kati ya Serikali na wafanyabiashara ilikuwa chini. Kwa hiyo, tukaanzisha mfumo hu una ufanisi wa mufumo huu umekuwa ni mkubwa ambao kimsingi umdhibiti udanganyifu uliokuwepo unafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao walikuwa hawaripoti taarifa kamili ili waweze kulipa kodi stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo kutokana na mfumo huu yameongezeka, lakini tukubali kwamba katika kufanya kazi yoyote au katika ufanyaji kazi huo kuna changamoto na changamoto kama ambavyo Waheshimiwa wameongelea ni kuhusiana na ile kampuni ambayo inafanya kazi hii kuchukua mapato mengi zaidi kuliko ambavyo Serikali inakusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutaarifu tu kwamba Serikali sasa inafanyia kazi hili na kwa sababu tulikuwa tumekubaliana, tumeingia mkataba na ile kampuni, kwa hiyo, cha muhimu tunaona namna gani tutakavyofanya ili kuhakikisha baada ya mkataba ule kuisha basi tuweze ku-review ile kampuni, lakini pia ikiwezekana tufanye sisi wenyewe hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala unyaufu wa korosho; niliongelee kidogo hili. Ni kweli kuna changamoto hiyo lakini tumeshakubaliana kwamba sasa tunaenda kufanya utafiti ambao utaangalia namna gani tuweze viwango vya unyaufu katika korosho. Utafiti huo utaongozwa na TARI kwa kushirikiana pia na shirika letu la Tanzania Bureau of Standards, lakini pia na Bodi ya Korosho na Chuo Kikuu cha Sokoine, lakini pia na wadau wengine kwa maana ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Vyama Vikuu, TAMISEMI lakini pia na waendesha maghala. Kwa hiyo, hilo pia tuanenda kuliangalia ili tuweze kuona namna gani sasa ya kutatua changamoto hii ya unyaufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo pia kuhusu vifaatiba na dawa za binadamu. Limeongelewa kuhusu viwanda vya vifaatiba na dawa; tuna viwanda zaidi ya 14 sasa; kati ya hivyo, viwanda 12 vinatengeza dawa za binadamu lakini viwanda viwili vinatengeneza vifaatiba na vingine viwili vinatengeneza dawa za kinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kamati ya Kitaifa ambayo inaendelea na upembuzi yakinifu kuhusiana na uanzishwaji wa kiwanda cha vifaatiba katika Mkoa wa Simiyu. Kamati hiyo, iko katika hatua mbalimbali za kuona namna gani ya kuanzisha kiwanda hicho ikiwemo maoni ya hawa Waheshimiwa Wabunge ambayo leo wameyatoa nayo yataingizwa kwenye Kamati hiyo ya Kitaifa ili tuweze kuwa na uhakika sasa wa kuanzisha kiwanda hicho katika Mkoa wa Simiyu. Kusudi ni lile lile kuhakikisha tunatumia malighafi zilizoko nchini kwa maana ya pamba angalau zianze sasa kutumika katika viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba tena kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hoja bajeti hii iliyobeba ajenda kubwa ya Kitaifa na hasa ujenzi wa Tanzania ya viwanda. Hakika, kazi hii ni kubwa na sote tuunge mkono ili iweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru sana na kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi kuwa Naibu Spika wetu katika Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara nipende kwa namna ya pekee kushukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Wajumbe wote kwa vile ambavyo wanatupa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza mipango ya Serikali, na hivyo basi imekuwa desturi ya Kamati hii kutushauri kwa umakini mkubwa kwa nia ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inathamini sana ushauri wa Kamati hii, na tutandelea kufanya nao kazi kwa ukaribu kuhakikisha yale ambayo wanatuelekeza tunayatekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tunaendelea kupitia sera zetu, kuanzia Sera ya Uwekezaji, Sera ya Viwanda Vidogo (SMEs) na biashara ndogo na biashara ili ziendane na mazingira ya sasa ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele na mipango ya maendeleo ya Taifa kwa ajili ya mabadiliko yanayoendelea katika dunia ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara tunatekeleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunatekeleza blue print. Baadhi ya vitu ambavyo vimelalamikiwa sana ni kuwa na sehemu moja ya kuhudumia wawekezaji. Tanzania tunatengeneza sasa kitu inaitwa Tanzania Electronic Investment a single window ambayo hiyo itawezesha sasa wawekezaji kuwa na sehemu moja ambako watapata huduma nyingi ambazo zinatolewa na taasisi zetu. Kwa kuanzia tutaanza na BRELA, TIC na TRA ambazo zitaunganishwa pamoja katika mfumo huo ili kupunguza usumbufu kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaendelea pia kuhamasisha ujenzi wa viwanda vidogo kwa maana ya kuwa na kungani za viwanda ambazo zitasaidia sana, unajua sekta kubwa ya viwanda ni viwanda vidogo, vya kati, lakini pia hatusahau viwanda vikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali tunaendelea kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ili kuwe na ujenzi wa viwanda katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaangalia pia kwa namna ya pekee kuona mifuko ya kuwezesha wajasiriamali inaongezewa fedha, lakini kuhakikisha pia inaboreshwa kwa kuunganishwa ile ambayo inawezekana ili iweze kuwa na tija kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa hili muhimu sana la utekelezaji miradi ya kimkakati ambayo imeongelewa sana. Nia ya Serikali hasa ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, ameelekeza tuone sasa namna ya kukwamua miradi hii mikubwa ambayo itakuwa na impact kubwa sana katika maeneo ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tutaenda kuishughulikia kwa haraka iwezekanavyo, lakini kwa kuangalia kwa weledi ili kuhakikisha tija na manufaa ya nchi nzima kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo ili utajiri huu na maliasili hii tuliyonayo katika hii miradi ya kimkakati ambayo iko chini ya sekta hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inakuwa na tija kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini pia nashukuru Kamati na Wabunge wote ambao wametushauri, ushauri wao tunaenda kuufanyia kazi ili kuhakikisha tunaendelea kuhakikisha tunajenga uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika taarifa hizi za kamati hizi mbili ambazo zimeletwa mbele ya Bunge lako. Kuna mengi yameongelewa ambayo ni ya kujenga kwa hiyo niendelee kushukuru kwa michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge lakini mahususi kwa kamati hizi mbili ambazo zinaendelea kuhisimamia na kuielekeza Serikali katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, yameongelewa mengi lakini kubwa ni kuona namna gani kuboresha au kuziwezesha taasisi ambazo zinatoa huduma katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo taasisi yetu ya ABZA CAMATEC, SIDO, TEMDO, TIC na taasisi zingine ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu. Tunachukua mawazo haya ya Waheshimiwa Wabunge lakini kamati hizi mbili kwa umakini mkubwa kuhakikisha kwamba tunatekeleza majukumu hayo ili tuweze kunufaisha Taifa hili kupitia huduma zinazotolewa katika Taasisi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa suala la utekelezaji wa Blue Print ambalo Mheshimiwa Tarimba amemalizia sasa Serikali inaendelea kuhakikisha kutekeleza hilo lakini tunaangalia na mapungufu mengine ambayo yanaendelea kujitokeza wakati tunatekeleza. Siyo kweli kwamba tunafungia katika kabati lakini tunaendelea kutekeleza hatua kwa hatua na nikuhakikishie Bunge lako liwe na imani nia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ni kuona tunaweka mazingira wezeshi na bora Zaidi ili kuwahakikisha sekta binafsi inakuwa ni kiongozi katika kujenga uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumeongelewa mambo mengi kuhusiana na miradi ya kimkakati ambayo inatekelezwa chini ya Taasisi zetu. Serikali inaendelea kufanya bidi na haraka zaidi lakini kwa uweledi ili miradi hiyo iweze kutekelezwa kwa haraka lakini kwa tija kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Imeongelewa miradi ya Mchuchuma na Linganga, lakini kuhusu viuwadudu na mengine tutahakikisha tunatekeleza miradi hii kwa uweledi lakini kuona maslahi mabana ya nchi yanazingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tunachukua maoni yote na tuhakikishie Waheshimiwa Wabunge lakini kamati zetu mbili ambazo zinatusimamia kwamba tutatekeleza maoni yao na ushauri wao na tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wanatekeleza majukumu ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kamati hizi mbili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, katika mijadala inayoendelea moja ya hoja kubwa ambayo imejadiliwa ni kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali hapa nchini na hasa katika kipindi hiki ambapo tupo katika majanga mbalimbali ikiwemo iliyokuwa UVIKO pia na yale yanayoendelea huko katika nchi za Ukraine na Urusi.

Mheshimiwa Spika, changamoto hii ya mfumuko wa bei siyo ya Tanzania tu ni maeneo yote au dunia nzima na Serikali tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kuona namna gani tunapunguza makali ya maisha ya wananchi katika kuhakikisha bidhaa nyingi zinapatikana kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa sera ya nchi yetu ni kuona tunaachia nguvu za soko huria katika kuendesha biashara. Hiyo haiachi jukumu la Serikali la kuhakikisha tunalinda ushindani wa haki kwenye soko pia kuhakikisha mlaji nae analindwa.

Mheshimiwa Spika, tutakumbuka sote kwamba bei za bidhaa mbalimbali kuanzia mbolea pia bidhaa muhimu kama sukari lakini pia na vifaa vya ujenzi, mafuta ya kula na kadhalika vilipanda bei sana, ilianza mwaka jana mwezi wa Desemba.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali tulianza kuchukua hatua za awali za haraka kuhakikisha tunapunguza makali hayo ambayo yanatokana na bei hizi kuwa juu.

Mheshimiwa Spika, moja ya vitu ambavyo tumefanya kwanza ni kukaa na wazalishaji kuongea nao hasa wale wanaoanzisha bidhaa za ndani. Bidhaa ambazo zilikuwa zimepanda bei sana mwaka jana na hata hivi karibuni zimeendelea nyingine ni pamoja na vifaa vya ujenzi. Mtakumbuka vifaa vya ujenzi vilikuwa vimepanda sana pia vinywaji baridi, tulipokaa na wazalishaji tulikubaliana na kuona maeneo mahsusi ambayo yalikuwa si sahihi na hasa kupitia Tume ya Ushindani ambao wanajukumu la kuhakikisha sheria ya ushindani inatumika kudhibiti vitendo vya kuvuruga mwenendo wa soko au bei ya bidhaa sokoni.

Mheshimiwa Spika, ninyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge wataona kwamba bei za saruji angalau zimepungua kidogo, ingawaje bado tunaendelea kufanyia kazi lakini pia na bei za vinywaji baridi zilipungua lakini pia tunaendelea na kazi hiyo kwa sababu kazi ya kuhakikisha ushindani wa haki na kulinda mlaji ni endelevu siyo kazi ya siku moja.

Mheshimiwa Spika, hivyo tunaendelea kuhakikisha kwamba bei za bidhaa mbalimbali zikiwemo, sasa tumeona bei za vyakula vya kawaida kwa maana ya mchele, maharage na kadhalika navyo pia vimepanda bei. Moja ya changamoto tuliona katika kukaa na wazalishaji na wasafirishaji ilikuwa kwenye eneo la usafirishaji ambalo kimsingi tunaendelea kulifanyia kazi ili tuone ni namna gani ya kuhakikisha tunadhibiti upandaji holela wa bei za bidhaa katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi ni hizo lakini pia hatua za muda wa kati ni pamoja na kuendelea sasa kuhakikisha tunaendelea kuweka vivutio au motisha maalum kwa ajili ya uzalishaji wa ndani, kuhakikisha tunawezesha viwanda vyetu vya ndani vinavyozalisha ili viweze kuendelea kuzalisha kwa tija, hii tumeendelea kuchukua hatua ikiwemo tarehe 25 Machi tuliweza kutia saini mikataba ya utekelezaji kati ya makampuni ambayo yapo kwenye miradi ya kimkakati au mahiri hii ikiwemo Intracom ambao wapo hapa Dodoma watazalisha mbolea, pia Bagamoyo Sugar ambao wataenda kuzalisha sukari pia Taifa gas, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na wale wenzetu NAFO ambao watazalisha Gypsum Board na Gypsum Powder.

Mheshimiwa Spika, hii mahsusi kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa unaoweza kufanyika ndani ufanyike kwa tija ili kuhakikisha tunapunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha tunakuwa na uhakika wa kuwa na bidhaa hizi muhimu tunaendelea sasa kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi na bora ili tuweze kupata wawekezaji wengine kutoka nje kuhakikisha kwamba bidhaa nyingi tunakuwa na uwezo wa kuzalisha nchini badala ya kutegemea kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumeona kwamba mfumuko huu wa bei maeneo makubwa mengi yametokana na tunasema imported inflation ambao umetokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali huko nje, hata kwa malighafi ambazo zinatumika katika viwanda vya ndani lakini ambazo zinatoka nje, zile malighafi ambazo zipo ndani tutaona ni namna gani tutahakikisha tunaweka mazingira ili ziweze kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa hazina bei ghali.

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai kuweza kusimama hapa mbele na kuwasilisha bejeti hii; lakini kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na kuendelea kufanya kazi kama Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nipende kushukuru sana michango ya Waheshimiwa Wabunge kwa kuchangia kwa mtazamo chanya kwenye bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuendeleza kutimiza adhma ya ujenzi wa uchumi wa Viwanda nami nasimama hapa ili niweze kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi kubwa na umakini ambao anaoufanya katika kuendelea Sekta hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mheshimwia Mwenyekiti, bajeti iliyowasilishwa imebeba dhamira kuu ya kuendeleza kasi ya uwekezaji na ujenzi shirikishi na unganishi wa Uchumi wa Viwanda kwa kutambua nafasi ya Sekta Binafsi; kama ambayo Waheshimiwa Wabunge wameeleza kama injini ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda na shughuli za ubia kwa Sekta Binafsi ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa mfumo huu wa maboresho na mengine yanayoendelea nchini likiwemo kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara kwa maana Blue Print unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kushushia ari ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuleta maendeleo endelevu katika nchi na wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya ya awali na mimi niweze kuchangia kidogo kwanza kwenye hoja zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika kuchangia bajeti hii. Kulikuwa na hoja kuhusu Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya TanTrade ambayo imechangiwa pia na Wabunge wengi sana, kuhusu kuona namna gani tunaweza kuisaidia ili kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi ya kutafuta masoko ya bidhaa hasa mazao ya kilimo na bidhaa nyingine. Serikali inafanyakazi kubwa kuhakikisha tunawezesha taasisi zote ikiwemo hii ya TanTrade.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika bajeti hii tunayoendelea nayo sasa tulikuwa tumewapa fedha kidogo lakini mwaka huu tumeongezea kufikia bilioni 1.8 hii maana yake ni kuiwepo kwa dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha masoko ya bidhaa na hasa mazao ya kilimo yanapata masoko ya uhakika kwa kuhakikisha TanTrade inafanyakazi yake vizuri. Lakini Serikali itaendelea kuweka fedha zaidi kuhakikisha TanTrade inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kulikuwa na hoja kuhusu uandaaji wa kanzidata ya viwanda. Ni kweli Kanzidata ya viwanda ni moja ya matokeo ya utafiti na utambuzi wa viwanda ambayo huwa ni fursa kwa uwekezaji na wa rasilimali inayopata hapa nchini.

Kwa hiyo, kanzidata ni kweli itakuwa na taarifa sahihi za viwanda ikiwemo maeneo viwanda vilipo, ukubwa na uwezo wa viwanda hivyo na ajira ambazo zinatokana na viwanda hivyo. Lakini zaidi itaweza kutusaidia kujua malighafi zinazotakiwa kwa ajili ya kuzalisha bidhaa katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa taarifa hizo zitatusaidia pia kuona namna gani tunajua wapi kwa kuwekeza kwenye maeneo yapi, pia ambapo tunaamini yataleta tija. Sasa Wizara kupitia TIRDO tumeshaanza kazi hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine kama vile Ofisi ya Rais, TAMISEMI, NBS, BRELA na SIDO wanaendelea na uhakiki wa kukusanya takwimu za taarifa mbalimbali ambazo zitajumuishwa kwenye kanzidata ya viwanda katika Mikoa mbalimbali hapa nchini na sasa wameanza katika Mikoa ya Kanda ya Mashariki ikiwemo Morogoro na Mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja pia kwenye Kamati kuhusu uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini, ambao pia imechangiwa pia na Waheshimiwa Wabunge wengi. Wizara kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) inakamilisha mfumo wa kielektroniki wa kutoa huduma ya mahali pamoja kwa wawekezaji (Tanzania Investment Electronic Single Window), ambayo itasaidia kuhakikisha tunaondoa baadhi ya changamoto na kupunguza urasimu usio wa lazima ambao umesababisha ucheleweshwaji kwa upatikanaji wa vibali kwa wawekezaji ikiwemo kujaza fomu nyingi na kujirudiarudia kwa sababu ya taasisi nyingi ambazo zinafanya kazi zinazofanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni hoja chache kutoka kwenye Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kidogo kwa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika bajeti hii hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate ambayo aliongelea kuhusu umuhimu wa kuwezesha Bodi ya Maghala ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa uhakika na kwa ufanisi zaidi. Ni kweli nasi Wizara na Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha tunawezesha Bodi hii iweze kufanya kazi yake. Kwa sasa hivi inasimamia baadhi ya shughuli lakini pia tutaleta nadhani maboresho ya Sheria kuona sasa inasimamia maghala yote nchini ili yaweze kufanya kazi zake vizuri, lakini tumeendelea kuwawezesha kwa kuwapa fedha zaidi kila mwaka ili waweze kukamilisha majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alisema hoja ya Bodi hii ihakikishe inaweza kujenga maghala kwenye vijiji na maeneo mengi. Nia ya Serikali ni kuona sasa tutashirikisha sekta binafsi ili nao waweze kufanya kazi zao vizuri lakini pia na sisi kama Serikali tutaendelea kuwezesha ujenzi wa maghala hayo maeneo tofauti tofauti na hasa vijijini ambako ndiko kuna haja kubwa ya kuwa na maghala haya ili wananchi waweze kuhifadhi mazao yao yawe katika ubora unaotakiwa lakini pia kuweza kudhibiti kupata bei bora ya mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Subira Mgalu kuhusu SIDO kuwezeshwa mitaji ya fedha lakini pia kuwezeshwa na vitendea kazi. Ni kweli SIDO ambayo ndio inahudumia viwanda vidogo vidogo na biashara ndogo ndogo kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuona sasa tunaimarisha sekta hii ya viwanda vidogo vidogo ili viweze kusaidia wananchi wengi zaidi kwenye ngazi ya chini ambako ndiko wananchi wengi wanashiriki katika kukuza uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, tutaendelea kuwawezesha SIDO na kuhakikisha teknolojia muhimu katika maeneo tofauti mikoani mpaka kwenye Halmashauri ili angalau zisaidie maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ya kuhakikisha kufanya tathmini ya vile viwanda mia moja vya kila Halmashauri ambavyo tulikuwa tunaendelea navyo. Ni kweli tutaendelea kufanya zoezi hilo la utambuzi wa viwanda vile na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingine ili kuhakikisha kila Mkoa unapata fursa ya kuongeza thamani hasa kwenye eneo hili la mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine pia ya kuona namna gani tunaendeleza kuhakikisha tunahamasisha ujasiriamali. Kama nilivyosema SIDO ndiyo wanasaidia sana katika eneo hili lakini pia na vyuo vingine kama VETA na Taasisi zingine TCCIA na CTI ambao wapo kwenye sekta binafsi kuhakikisha tunawawezesha wajasiriamali katika elimu kwa maana ya ujuzi lakini pia teknolojia lakini na mitaji kuhakikisha nao wanashiriki vizuri katika kuendeleza sekta ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba kusema tena naunga mkono hoja na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote, tuunge mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha Wizara inaweza kutimiza majukumu yake katika Mwaka, 2022/2023. Ninakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu ya kuridhia Azimio la Eneo Huru la Biashara Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja, na kimsingi kama ambavyo wajumbe wengi wamesema labda na mimi niseme tu kidogo. Eneo Huru la Biashara Afrika ni utaratibu wa pamoja wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika unaolenga kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama walivyochangia wachangiaji wengi na kukubaliana na Azimio hili, lengo hasa litakuwa ni kufunguliana masoko ya biashara ya bidhaa na huduma, kuondeleana ushuru wa forodha, pamoja na kulegeza vikwazo na masharti mbalimbali ili kuhakikisha Afrika tunafanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamekubaliana, lakini wametoa baadhi ya maoni kwa upande wa Serikali. Na mimi kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba maoni haya tunayachukua na moja ya mikakati ambayo tunaenda kuitekeleza ni kuhakikisha tunaendeleza kuimarisha mazingira bora au wezeshi ya kufanya biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika hilo kweli kulikuwa kuna changamoto kidogo, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge, na tuliona baadhi ya hata wafanyabiashara wakubwa wakiondoka, wakiondoa mitaji yao na kuwekeza katika nchi zingine, lakini sasa baada ya maboresho yanayoendelea hasa kupitia blue print kama mlivyosema Waheshimiwa Wabunge tunaona tayari wawekezaji wengi wanaanza kurudi kuwekeza hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake hili ni move nzuri ambayo na sisi tuitumie nafasi hii sasa kuvutia mitaji mingi kwa kuweka mazingira wezeshi ili tuanze kuzalisha nchini na kuuza katika eneo hili la biashara la Afrika kwa faida zaidi kulingana na utaratibu tunaoendana nao sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, wameongelea kuhusiana na kuhakikisha sekta binafsi inawezeshwa au inashirikishwa. Hili tunalichukua na kuhakikisha kweli sasa tunaenda ku-engage; na kama ulivyosema wengine tayari sekta binafsi imeshasema faida kubwa ambayo wataenda kuipata au manufaa makubwa ya Tanzania kuridhia mkataba huu wa eneo huru la biashara Afrika, kwamba wao wataenda kufaidika Zaidi, na ni wengi wamesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutaendelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani na hasa kwenye kukidhi viwango, kwa maana ya kuhakikisha unahamasisha uzalishaji wa tija kwenye bidhaa zetu lakini na mazao. Kama walivyosema wengine, kwamba angalau sasa bidhaa zetu na mazao yetu yawe shindani kulingana na soko la sasa, lakini hasa kwenye hili soko la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, wameongelea kuhusiana na sekta ya biashara ndogo, kwamba lazima hawa nao pia tuendelee kuwawezesha. Ni kweli, tuhakikishe sasa sekta ndogo kwa maana wajasiliamali waweze kuzalisha kibiashara kwa kuhakikisha kwamba vifungashio vyao vinakuwa vya viwango, lakini pia hata ubora; na hii tunaenda kuhakikisha tunafanya hivyo kwa sababu sasa hivi tunaenda kuandaa sera ya ubora. Tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba tutaenda kutekeleza au tutaingia tukiwa na nguvu katika soko hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa ujumla wake Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana kuhusiana na umuhimu wa sisi kama Bara la Afrika kuanza sasa kuishi pamoja, kwa maana ya kufanya biashara pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli changamoto mojawapo kubwa sana katika kufanya biashara katika bara letu ni miundombinu. Kwa mfano; utakuta mtu anataka kwenda labda hata Kongo tu hapo, kama kwa njia ya ndege maana yake lazima uende Ethiopia au hata nchi za nje ili kesho yake ulale, uje Kongo, DRC. Sasa unakuta miundombinu hii ndiyo imekuwa na changamoto kubwa sana ya sisi kwenye kufanya biashara katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo moja wapo ya vitu ambavyo vitaenda kutupelekea kuhakikisha sasa tunaimarisha miundombinu yetu hii ni moja ya fursa ambayo naamini, kama alivyosema Mheshimiwa Mwijage na mwingine, kwamba sasa miundombinu hii itajengwa kwa sababu tunajua tunakwenda kufanya biashara kati ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili pia, naona kwa mfano; hata kwenye njia tu za barabara watu wanaouza mazao mbalimbali ikiwemo hata mbao kupeleka Kongo badala ya kukatisha hapa tunaenda mpaka Zambia halafu uanze kurudi hivi. Maana yake kwa miundombinu hii inapelekea bidhaa zetu kuwa uncompetitive, kwamba zitakuwa sasa haziwezi kushindana na bidhaa hata za kutoka ulaya kwa sababu ya miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe, kama ambavyo wote wamekubali, kwamba tuunge mkono Azimio hili kwa sababu lina manufaa mengi kwa nchi yetu, lakini pia kwa Bara zima la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hii hoja muhimu ya Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ambao ni muhimu sana. Kwanza nianze kwa kuunga mkono mapendekezo yaliyowasilishwa katika Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo: Umuhimu wa kutunga sheria hii mpya ya uwekezaji ulizingatia sana maoni ya wadau mbalimbali ambao ni wa ndani na nje ikijumuisha na taasisi za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ambao pia kwa vipindi tofauti wamekuwa wakifanya tathmini ya utekelezaji wa sheria yetu.

Mheshimiwa Spika, pia sheria hii ni sehemu ya utekelezaji wa blueprint. Wachangiaji wamesema wengi, na mimi niseme ile Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment in Tanzania, moja ya changamoto zilizokuwepo ni pamoja na kuwa na sheria na sera mbalimbali ambazo zimepitwa na wakati.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu wa sheria unachangia katika kuhakikisha tunaweka mazingira ambayo yanatabirika kwa wawekezaji wa ndani na wa nje katika nchi yetu. Katika Muswada huu tumeona kwa kuzingatia umuhimu wa Watanzania kupata au kuwekeza kwa kunufaika na vivutio hivi, moja ya maeneo ambayo yameangaliwa ni hayo na kupunguza mtaji au fedha zinazohitajika kupata vivutio kutoka Dola za Kimarekani 100,000 mpaka 50,000. Hii ni moja ya maeneo ambayo yameangaliwa katika Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka sheria hii kama walivyosema wachangiaji wengi, ni ya muda mrefu; ya tangu mwaka 1997 na katika kipindi hiki kuna marekebisho mengi yamefanywa na sasa ikafikia wakati kwamba hatuwezi kuendelea tena kurekebisha, kwa hiyo, lazima tulete itungwe upya kama sheria ya mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli moja ya maeneo ambayo yameangaliwa katika Muswada huu ni kuona namna gani tunaweka sheria hii iwe inatabirika. Moja ya viashiria vilivyokuwa vinavunja moyo wawekezaji hasa kutoka nje, ni kutokutabirika kwa sheria zetu. Ila katika Muswada huu tumeona wameweka sharti la muda wa mradi, miaka mitano. Maana yake mwekezaji akiwekeza anakuwa na uhakika kwamba katika muda ule aliyopewa wa vivutio wa miaka mitano, maana yake hakutakuwa na mabadiliko katika uwekezaji wake. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo wadau wengi walikuwa wanachangia kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Mheshimiwa Spika, sheria hii inaipa nguvu zaidi TIC. Waheshimiwa wachangiaji wa Muswada huu wamesema tuweke kama mamlaka. Ni kweli, moja ya maeneo makubwa ambayo Muswada huu umeangalia pia ni kuipa jukumu la kuratibu na kuandaa jam za uwekezaji nchini (National Investment Branding) Kituo cha Uwekezaji. Kwa hiyo, maana yake imeongezea nguvu tofauti na hapo awali kabla ya Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, sheria inataka tuwe na mfumo wa kielektroniki wa kuwezesha usajili wa miradi utakaounganishwa na mifumo ya taasisi nyingine muhimu zote zinazohudumia wawekezaji hapa nchini. Maana yake Muswada huu unaweza kutusaidia sasa kupunguza malalamiko ya wawekezaji kwenda kutafuta huduma kwenye taasisi tofauti tofauti. Maana yake tukiitekeleza itarahisisha angalau kupunguza ule usumbufu ambao wanapata wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo yameongelewa na wachangiaji ni kuhusiana na suala la One Stop Centre. Ni kweli, katika changamoto mojawapo ambazo wawekezaji walikuwa wanakutananazo ni pamoja na hili la kutokuwa na taasisi ambayo ina mfumo unaohudumia watu wengi kwa mahali pamoja (One Stop Centre).

Mheshimiwa Spika, taasisi nyingine ambazo tunadhani baada ya kukamilika kwa Muswada huu na mfumo huu wa kielektroniki, utapunguza ule usumbufu wa kwenda kwenye taasisi tofauti tofauti ambazo tunaamini katika mfumo huu utawezesha kuwa na sehemu moja ya kupata huduma, au tunasema huduma ya mahali pamoja.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamechangia ni kuona namna gani ya kupunguza usumbufu au tuangalie mindset. Mheshimiwa Tarimba amesema kwa wawekezaji, lakini mtazamo kwa ujumla wa Watanzania kwamba Muswada huu utusaidie sasa pia na sisi wengine kuelewa umuhimu wa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia Muswada huu, sheria hii, pia tunapitia na sera ambazo zitatusaidia kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na sheria hii ya uwekezaji na mazingira haya rafiki ya kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, umeongelewa umuhimu wa kuangalia sekta nyingine ambazo hazisimamiwi na sheria hii. Tunaamini tutaendelea kufanyia kazi kwa maana ya kuhakikisha pia uboreshaji kwenye utendaji wetu wa kila siku katika utekelezaji kupitia Muswada huu na sera ambazo zinatumia uwekezaji, tunaweza kuweka mazingira ambayo yatasaidia na sekta zote ambazo ni muhimu zisiwe changamoto kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kuunga mkono hoja, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote tuunge mkono hoja ya Muswada huu ili uweze kupitishwa.

Mheshimwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)