Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nicodemas Henry Maganga (30 total)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu la nyongeza; ni lini sasa Serikali itatoa vifaa vya upimaji kwenye wilaya ya Mbogwe? Maana Wilaya ya Mbogwe inakua na ina watu wengi sana, lakini hatuna vipimo vya x-ray pamoja na vipimo vingine. Kwa hiyo wananchi wa Mbogwe wamekuwa wakipata taabu sana wanapopata ajali wale waendesha bodaboda na watu wengine; ni lini Serikali inawahakikishia wananchi wangu wa Mbogwe kwamba itapeleka hivyo vifaa vya upimaji.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu za kununua vifaa tiba katika hospitali mpya 67 za halmashauri kote nchini.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Hospitali ya Halmashauri ya Mbogwe ni moja ya hospitali ambazo zitanufaika na bajeti hii kwa kupata kiasi cha shilingi milioni 500 kadri ya fedha itakavyopatikana ili ziweze kununua vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sijaridhishwa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji kwamba kuna visima 26 Mbogwe. Naomba tu tuongozane naye akanionyeshe pale vilipo hivyo visima virefu vinavyotoa maji, maana mimi ni Mbunge wa Mbogwe na ninaishi Mbogwe na kuna taabu kubwa sana katika Sekta ya Maji. Ndiyo maana nikaiomba Serikali sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mbogwe ni Wilaya ambayo ipo karibu na mradi wa maji pale Kahama, ni vyema sasa Wizara ya Maji itupelekee mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, maana hivyo visima anavyovisema Mheshimiwa, nakuomba twende na wewe, usifuate mambo ya kwenye makaratasi ukajionee na unionyeshe pale vilipo visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ombi lake namba moja limepita, kwani huo ni moto wa namna ya kutekeleza majukumu yangu; nimekuwa nikiambatana na Wabunge wengi, hata weekend hii tu nilikuwa Mbinga. Kwa hiyo, mimi kutembea huko, kwangu ni moja ya majukumu yangu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nicodemus mantahofu, tutakwenda na miradi hii tutahakikisha mambo yanakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia mradi wa Ziwa Victoria, hili Ziwa litatumika vyema kwa maeneo yote ambayo miradi hii mikubwa itapitia. Mheshimiwa Nicodemus, wewe ni Mbunge katika Wabunge mahiri, umekuwa ukifatilia suala hili, tumeliongea mara nyingi na umeonyesha uchungu mkubwa kwa wana Mbogwe. Nikuhakikishie, Mbogwe maji yatafika na katika mwaka ujao wa fedha mambo yatakwenda vizuri pale Mbogwe. Tuonane baada ya hapa, tuweke mambo sawa, tuone namna gani tunaelekea. (Makofi/Kicheko)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimesikia majibu ya Serikali lakini ukweli bado wafanyabiashara wana kilio hapa nchini, hawana raha na Serikali yao kulingana na madeni hayo maana hawakuwa na elimu ya hizi mashine za EFD. Hivyo sasa, naomba Mheshimiwa Waziri utoe kauli ili nchi nzima wajue kwamba walishasamehewa hayo madeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili je, ni lini sasa Serikali itafuta madeni ya mgodi wa Bulyanhulu ili waweze kutimiza makubaliano yao katika mkataba wao wa ujenzi wa barabara itokayo Kahama ya lami kwenda Bulyanhulu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango ya Mheshimiwa Nicodemus Maganga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la kauli ya Serikali kuhusu kusamehe madeni haliwezi kutolewa kwa utaratibu huu. Msamaha wa madeni unatokana na uko kwa mujibu wa sheria, hata yale maamuzi ambayo yalisababisha kusamehe madeni ya kipindi kile yalitokana na utaratibu wa kisheria ambao ulipitishwa na Bunge hili. Kwa hiyo, hatuwezi kusimama hapa tukatoa tu tamko la kusema tunamsamehe nani madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili vilevile kuhusiana na kusamehe madeni na kwenyewe kuna repercussions zake. Kwa mfano, best practice wataalam wanasema kwamba utaratibu ule wa kusamehe madeni hauwezi kufanywa kila wakati kwa sababu unaathiri wigo mpana wa ukusanyaji kodi chini.

Kwa hiyo, lengo kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba kwanza tunawasaidia wale ambao walikuwa na madeni ya muda mrefu, lakini la pili ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakusanya kwa kipindi kile ambacho maamuzi yale yalitoka kwa haraka.

Kwa hiyo, ili msamaha mwingine utoke, lazima tukae chini na kuweza kufanya tathmini na utafiti wa kina kupima athari na faida za kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusiana na hoja ya Bulyanhulu napokea maelekezo yako nadhani ni suala mahsusi kwa hiyo basi tutalifanyia kazi na kumpatia majibu Mheshimiwa Mbunge baada ya kupata hizo takwimu. (Makofi)
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nakushkuru Mheshimiwa Waziri, uzuri umejibu halafu umefanya ziara kwangu, hizo barabara zote ulizozisema ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza ambayo ni hatarishi sana, daraja la Budoda halipitiki toka kwenye kampeni. Je, Serikali haina mfuko wa dharura kwenda kurekebisha madaraja ambayo yanawafanya wananchi kupoteza Maisha? Kuna Kata ya Ngemo, Mtonya pamoja na Ludembela, kuna madaraja mpaka sasa hivi hayapitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wewe Mheshimiwa Naibu Waziri, ulifika kwenye jimbo langu na ukajionea na tulizama mara tatu. Je, kwa sasa hivi na bunge linakwenda kuisha, nikawaambieje wananchi kulingana na ubovu wa barabara hizi ambazo hazipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemus Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ameuliza kwamba daraja la Budoda halipitiki kwa muda mrefu tangu kipindi cha kampeni, kwa hiyo akauliza kama hakuna fedha za dharura. Niseme tu Mheshimiwa mbunge nimelipokea jambo lako na ninalikabidhi kwa TARURA Makao Makuu, ili waende wakafanya tathmini hiyo na watuletee taarifa ili tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la Pili ameuliza atawaambi nini wananchi, kwa kuwa bunge linakwisha na barabara zake bado hazipittiki. Nenda kawaeleze tu kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo ya barabara maeneo mengi nchini. Na katika hatua ya awali ambayo tulioichukuwa ni kupeleka fedha milioni 500 kwenye kila Jimbo, ambazo zitakwenda kujenga barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili waeleze wananchi wako kwamba, mara baada ya bajeti ya Serikali kupita, kikiwemo kile kifungu maalum cha kuongezea fedha za TARURA, tutaongeza fedha katika Jimbo lako ambazo zitasaidi zaidi zile barabara ambazo ni mbovu. Ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala liliopo Longido hata Mbogwe lipo; na ni mpango wa Serikali kila Halmashauri kuunganisha barabara za lami kwenda Makao Makuu ya Mkoa.

Je, Wizara inampango gani kulingana na Jimbo langu la Mbogwe sina barabara inayounganishwa Wilaya kwa Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba tumekuwa tukizungumza mara kwa mara kufatilia ujenzi katika jimbo lake na tumeshawaelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa ili waangalie mipango iliyoko ndani ya mkoa wao, lakini pia tuangalie na hii ya Wizara. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango uliopo wa Serikali ni kuunganisha Mkoa kwa Mkoa, Wilaya na Mkoa na Wilaya kwa Wilaya. Kwa hiyo hoja yako tumeipokea Mheshimiwa Mbunge tutaifanyia kazi kadri ambavyo Serikali itapata fedha. Ahsante.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini namwomba Waziri apate muda twende tukafanye ziara kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Mbogwe ni mji ambao umezingirwa na mapori mengi, hivyo wananchi wa pale wanapata tabu sana jinsi ya kuishi na mapori katikati japokuwa mapori yale hayana sifa ya kuwa na hifadhi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri siku moja twende tuongozane naye ili kusudi twende tukashauriane vizuri ili wananchi wale waweze kuishi katika hifadhi zile. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimepokea ombi hilo na baada ya kikao hiki tutapanga baada ya Bunge tuweke ratiba ya kwenda Mbogwe. Nashukuru sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; Mawaziri wale nane walikuja Mkoani Geita, kule Mbongwe kuna changamoto ya migogoro ya watu wenye uhifadhi, kuna Kijiji kimoja cha Sango, majuzi kimewekewa vigingi katikati ambapo kilishapata GN toka mwaka 1976. Je, Waziri, msimamo huu ukoje, maana wananchi mpaka sasa hivi wana hofu kulingana na kigingi kilichowekwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa amesema kumekuwa na wimbo la ukataji wa mkaa, lakini kuna utaratibu wa kisheria hawa wananchi huwa wanazifuata. Ila kuna hawa Askari Mgambo ambao pengine hawana mafunzo vizuri ya kusimamia hizi sheria; kumekuwa na mgongano pale wanapofanya hizi operation wanawakamata wananchi ambapo wanavibali tayari lakini wanaonekana kuwaumiza na kutowatendea haki. Je, ni nini kauli ya Mheshimiwa Waziri ili kusudi wananchi hao pale wanapofuata sheria zote wafanye shughuli zao vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemas Maganga, Mbunge wa Mbongwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika maeneo ya Mbongwe, baadhi ya vijiji vimeingizwa kwenye Kamati ya Mawaziri Nane na hivi ninayoongea tayari mikoa 13 imekwishatembelewa na maelekezo ya Serikali ni kwamba tunafanya tathmini na wataalam wako katika mikoa hiyo 13 wanafanya hizi tathmini, lakini pia kuona sasa namna ya maeneo ambayo yamehalalishwa kumegwa, yamegwe kwa ajili ya kuachia wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa kuwa maeneo hayo yako ndani ya tathmini ambayo inasimamiwa na Kamati ya Mawaziri Nane wa kisekta, tutaendelea kutoa maelekezo kwamba wananchi wasibughudhiwe wakati tunasubiri majibu ya tathmini hiyo. Kwa hiyo, vigingi visiwafanye wananchi wasifanye shughuli zao za kila siku, na hao wahifadhi tunawaelekeza wasilete vurugu yoyote mpaka pale ambapo tathmini ya Mawaziri nane itakapokamilisha kazi zake.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kwa hawa wananchi ambao wanakutana na changamoto ya kukabiliana na askari pamoja na wananchi. Niendelee kutoa rai kwa wananchi, kwamba tuendelee kufuata sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia uvunaji wa mazao ya misitu.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na changamoto, tunatoa vibali tukiamini kwamba vibali hivi vitatumika ipasavyo, lakini tumekuwa na changamoto ya uanzishwaji wa usafirishaji wa mazao ya misitu kwa kutumia pikipiki. Pikipiki inapita inaenda inavuna mti ambao haujaruhusiwa na wanapita njia zao za uchochoro, wakikamatwa wanasema wameonewa. Tuwaombe wafuate utaratibu na vibali vitolee kwa usahihi, ndivyo hawatakutana na changamoto ya kukamatwana na mazao haya ya misitu.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Waziri Wilaya ya Mbogwe ina migodi midogo midogo inayomilikiwa na wachimbaji wadogo.

Je, Wizara imejipangaje kuwanufaisha wachimbaji hao wadogo ili kusudi na wao waone matunda kwenye Serikali yao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika nchi yetu tuna wachimbaji wadogo katika sehemu mbalimbali, wenye leseni na moja ya kazi kubwa ya Wizara kupitia Taasisi zake za STAMICO na GST ni kuwajengea uwezo kwa kuwapa elimu juu ya Sheria ya Madini, Kanuni za Madini na namna ya uchimbaji bora pamoja na kuwatafutia fursa kwa wawekezaji wakubwa wanaokuja kutafuta madini katika maeneo ambayo yameshafanyiwa utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuishii hapo wachimbaji wadogo hawa pia tunaendelea kuwapelekea elimu ya kujiunga na kujisajili, waweze kufanya uchimbaji wenye tija kupitia taarifa za kijiolojia zinazoonesha madini yanayopatikana katika maeneo yao huko.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali.

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi naomba kuuliza barabara ya kutoka Masumbwe kwenda Geita Makao Makuu ya mkoa ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Masumbwe kwenda Geita imeshafanyiwa usanifu wa kina na sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante; katika hesabu ya Halmashauri 63, je, na Mbogwe imo kwenye hesabu hiyo Mheshimiwa Waziri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama Mbogwe ni Wilaya, sina uhakika sana kwa sababu kuna Wilaya ambazo zina majimbo mawili. Kwa hiyo, hapa kwenye majimbo mawili ina maana tunapokwenda kujenga ni Wilayani, sasa kama Mbogwe ni Wilaya ambayo inajitegemea itakuwa imo, lakini kama Mbogwe ni jimbo miongoni mwa Wilaya ina maana tutakapokwenda kujenga ni Wilayani ambako na Mbogwe ita-share chuo hicho ambacho kitajengwa katika Wilaya hiyo ambayo Mbogwe ipo kwenye Wilaya husika.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili. Kwa kuwa mwaka 2021 tulipitisha bajeti kubwa na tukasema kwamba sasa mbegu zitatolewa na ruzuku, lakini mpaka sasa hivi mbogwe hatujaona kitu chochote. Majibu yake yakoje?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; nina imani hujawahi kufika katika Wilaya ile: Je, uko tayari kuongozana nami baada ya Bunge ili ukaangalie maeneo ya Mbogwe, maana ni maeneo yanayofaa sana kwa kilimo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ruzuku la mazao hasa ya kimkakati yanaendelea kuratibiwa na bodi husika. Natoa maelekezo kwa bodi husika kuhakikisha kwamba wakulima wa pamba katika mikoa ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge waweze pia kufikiwa na ruzuku hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu mimi kwenda Mbogwe, baada ya kikao hiki cha Bunge, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kuangalia suala la kilimo katika eneo lake la Mbogwe.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo Ikungi na Wilaya ya Mbogwe lipo. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea walimu wa Wilaya ya Mbogwe nyumba ili na wao wapate pa kuishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, mkakati wa Serikali sasa hivi ni kutafuta fedha, kadri tunavyopata fedha maana yake tunajenga. Nimeainisha hapa kwamba siku hizi tunajenga Sekondari na kila Sekondari tunaweka nyumba za walimu three in one, yote hiyo ni mkakati wa kuondoa hii adha ya nyumba za walimu. Kwa hiyo. hata hapo Mbogwe nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, Serikali tutaendelea kuleta fedha kwa kadri zitakapopatikana, kwa hiyo aondoe shaka kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Vijiji 34 Mbogwe havijawekewa umeme kabisa, ni lini vitawekewa umeme, vijiji vya Mbogwe ambavyo havijapata umeme toka dunia iumbwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maganga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji vyote ambavyo havina umeme viko katika mradi wa REA III Round Two na tunaendelea kusimamia na wakandarasi kuhakikisha kabla ya Disemba hii kukamilika basi vijiji vyote vimepata umeme kwa mujibu wa mikataba yetu.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Naomba kumuuliza Naibu Waziri; barabara itokayo Masumbwe – Lugunga kuelekea Geita, ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye mpango wa RICE, na sasa hivi kinachoandaliwa ni document tender kwa ajili ya kuitangaza ili barabara hii iweze kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa maeneo ambayo yameainishwa. Ahsante.
MHE.NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri.

Swali la kwanza, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia walemavu ambao hawajiwezi kujiunga na vikundi, kuwasaidia angalau baiskeli ya kutembelea?

Swali la pili; je, Mheshimiwa Waziri uko tayari baada ya Bunge hili tuongazane mimi na wewe kwenda kuwatambua walemavu walioko Mbogwe na kuwasikiliza shida zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali wawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa au utaratibu wa mikopo ya asilimia kumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kundi la watu wenye ulemavu hawalazimiki kujiunga kwenye vikundi, hata mmoja anaweza akakopeshwa mkopo kama yeye na akafanya shughuli zake za ujasiriamali. Tayari wengi wameendelea kupata huduma hiyo kwa kupata mkopo kwa mtu moja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na viti mwendo kwa watu wenye ulemavu utaratibu wa Serikali upo na maafisa maendeleo ya jamii katika maeneo hayo wanaainisha. Tunahusiana na wadau mbalimbali wanaendelea kuwasaidia. Kwa hiyo nitoe wito kwa halmashauri ya Mbogwe kuwatambua watu wenye ulemavu wanaohitaji viti mwendo ili Serikali iweze kuona namna ya kushirikiana na wadau katika kuwawezesha kupata viti mwendo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili la bajeti ili twende Mbogwe tuweze kupitia baadhi ya vikundi ambavyo vimenufaika, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mbogwe ni kubwa iliyo na vyanzo vingi vya mapato, tumeshatenga eneo la kujengewa uwanja wa ndege tayari. Lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Mbogwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge naomba mara baada ya kipindi cha maswali na majibu nionane naye ili niweze kuangalia bajeti kiasi gani tumetenga kwa bajeti ijayo katika eneo lake. Ahsante.
MHE. NICODEMAS HENRY MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, anafahamu usumbufu wanaoupata wafanyabiashara kwenye mipaka yetu, kwa maana ya mipaka ya Kenya na Rwanda, kwa vile kule kila wakati faranga inapanda bei na kushuka lakini shilingi nakumbuka mwaka 1995 enzi za Mkapa ndiyo shilingi ilipanda bei na hii ndiyo inachangia ugumu wa maisha.

Sasa kuna mkakati gani wa kuifanya shilingi yetu iwe na thamani ili wananchi waweze kupata bidhaa kwa bei nafuu kulingana na upandishaji wa thamani?

Swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mfumuko wa dola, kwa sababu kumekuwa na kupanda sana kwa dola bila utaratibu. Leo unakuta dola inabadilishwa kwa shilingi 2,550 lakini jioni ukienda tena unakuta inabadilishwa kwa shilingi 2,800 na hii inafanya Taifa kuwa na maisha magumu, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza. Moja, Serikali imejitahidi kusimamia kuhakikisha la kwanza, thamani ya shilingi haishuki; la pili, ambalo tunalifanya katika mikakati yote hii ambayo unaiona Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu aliyoielekeza ya kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji, malengo ya muda mrefu kwenye hilo ni kwenda kuimarisha, kuongeza thamani ya shilingi yetu. Tutaongeza thamani ya shilingi yetu kwa namna nyingi zikiwemo hizo mbili za kuongeza mauzo nje ili tuwe na dola nyingi. Pili, kwa kuzalisha bidhaa ambazo tunaweza tukajitegemea na tukatumia ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kudhibiti mabadiliko ya haraka haraka ya bei ya dola, Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi cha muda mfupi, tunalishughulikia jambo hili ili kuweza kukabiliana na tatizo ambalo limejitokeza la dunia nzima la upungufu wa dola, ambapo hicho ndicho kinachosababisha mahitaji ya dola yanakuwa makubwa kuliko upatikanaji wa dola na hivyo kufanya bei ya dola kuanza kubadilikabadilika.

Mheshimiwa Spika, hata sasa tuna hatua ambazo tumeendelea kuzichukua ambazo tunaamini zitaweza kusaidia dola ziwepo nyingi sokoni, na zikiwa nyingi sokoni zitasababisha tatizo la bei kubadilikabadilika kuweza kupungua.

Mheshimiwa Spika, tunatoa rai kwa wadau wote wanaoshiriki katika soko la kubadilisha fedha, waendelee kushiriki kikamilifu ili kuweza kuhakikisha kuwa Dola haiadimiki sokoni na hivyo kusababisha bei kubadilikabadilika.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza niseme kabisa Mheshimiwa Waziri sijaridhishwa na majibu haya, hii takwimu uliyoionesha hapa kwamba bado wastaafu 1,780 hawajalipwa lakini niende kwenye maswali mawili labda nitaridhika.

Sasa Mheshimiwa Waziri mnawatambuaje wastaafu ambao walistaafu miaka mingi wakahamia wengine vijijini, hawako kwenye mifumo hii ya kieletroniki na umesema wanafanyiwa uhakiki kuwatambua kupitia akaunti zao tayari wengine walishafungiwa na akaunti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; hauoni ni kumweka mtu kwenye mazingira magumu sana ambaye anaitumikia Serikali wakati wake unapofika wa kustaafu halafu zinaanza chenga za kumlipa mafao yake.

Je, ungekuwa ni wewe ukamaliza Ubunge wako halafu mafao yasipatikane ungefikiriaje Mheshimiwa Waziri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza awali na anasema hajaridhika na majibu, lakini takwimu sahihi za Serikali chini ya mifuko na hizo kwamba wastaafu ambao wanalipwa ni hao 186,605 na kama ana takwimu tofauti basi tunamkaribisha ili tuweze kuangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kuhusiana na suala la wastaafu ambao wako vijijini anasema masuala ya mtandao na kadhalika. Hao wanaendelea kuhudumiwa, katika ofisi zetu zote za mifuko na wanachama wale wamefunguliwa na hawa niliowataja wote wana akaunti hizo za benki na bado kuna desk ambalo linawahudumia wastaafu wetu na tumeajiri watu maalum kabisa wa kutoa huduma hiyo kwa wateja wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama ana jambo mahususi haliwezi kuwa la watu wote ni la hao watu wachache ambao anawasema na kama wapo anifikishie ili niweze kuchukua hatua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni kuhusiana na kwamba ucheleweshaji wa ulipaji wa mafao, imebaki kuwa historia, tumeshafanya mabadiliko sasa hivi tunalipa kieletroniki na kuhusiana na mafao kama ni ulipaji kila mwezi kabla ya tarehe 25 tunalipa fedha hizo. Kwa hiyo, hilo ni suala la kihisroria analolielezea sasa hivi tumefanya mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuwaagiza Wakurugenzi na Mameneja wote wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika Mikoa waendelee kusimamia na kufanya lile suala la compliance kufatilia michango ya wanachama, lakini pili kuendelea kuhakikisha kwamba hakuna mstaafu yoyote ambaye anapata shida katika kipindi hiki, ahsante. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Halmashauri ya Wilaya ya Mbongwe imepakana na wilaya nne, lakini bajeti ya TARURA haitoshi na barabara zinahitaji kufunguliwa.

Je, ni lini Serikali Kuu itatoa pesa kwa TARURA ili kusudi njia zinazounganishwa na Wilaya ya Mbongwe ziweze kufunguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua Wilaya ya Mbongwe inapakana na halmashauri almost nne. Kuna changamoto ya baadhi ya barabara ambazo zinaunganisha Halmashauri ya Mbongwe na halmashauri za jirani. Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaboresha ujenzi wa barabara hizo na tutaendelea kufanya hivyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, Kata ya Ilolanguru, Kata ya Ikobe, Kata ya Iponya na Lubembela zinakabiliwa na changamoto ya mawasiliano. Waziri lini utapeleka mawasiliano Wilaya ya Mbogwe katika Kata hizo nilizozitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Maganga kuna maeneo ambayo yanafanyiwa tathmini lakini kuna maeneo ambayo yapo ndani ya miradi 758. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge miradi hii itakapokamilika lakini na yale ambayo tumeyaingiza kwenye tathmini na fedha zikapatikana tutafikisha mawasiliano ndani ya Jimbo la Mbogwe. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasilano na Teknolojia ya Habari, unakumbuka mwaka 2021 ulifanya ziara kwenye Jimbo langu ukawaahidi wananchi wa Mbogwe minara mitano, lakini mpaka sasa hivi haujatimiza ahadi yako.

Je, ni lini unakwenda kutekeleza ahadi yako ambayo mimi na wewe tulifanya mkutano kule Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nilifanya ziara katika Wilaya na Jimbo la Mbogwe na Serikali iliahidi kufikisha huduma ya mawasiliano, na mwezi wa saba wakandarasi wataingia field kwa ajili ya kuanza utekelezaji mara moja, ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji. Wilaya ya Mbongwe ina maeneo yaliyo na changamoto ya maji. Je, ni lini Mbogwe mtatupa gari hilo la kuweza kuchimbia visima ili wananchi waweze kupata maji safi na salama kupitia hayo, magari mliyoleta?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maganga Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavuyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Maganga anafatilia sana na hili tumeshaongea. Mheshimiwa Maganga naomba uiamini Wizara, mimi mwenyewe na wewe tutakwenda kuhakikisha kazi zinakwenda kuanza kwa wakati na visima vitachimbwa.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mpango wa Serikali ni kuunganisha kwa kiwango cha lami kutoka Wilaya kwenda Mkoa. Waziri ni lini Serikali itaanza kujenga barabara Halmashauri ya Wilaya Mbogwe kwenda Geita Makao Makuu ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maganga Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli huo ndiyo mpango na bahati nzuri barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge zitafadhiliwa na wenzetu wa World Bank kupitia mradi wa RISE ambao sasa hivi wanakamilisha kufanya review ya usanifu wa barabara za kuiunganisha Wilaya ya Mbogwe na Wilaya ya Geita kwa kiwango cha lami. Tunategemea kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa sababu taratibu zinaendelea na ni fedha za World Bank, mara baada ya kukamilisha hizo taaratibu ujenzi utaanza kwa kiwango cha lami. Ahsante.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi, naomba kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni lini barabara ya kutoka Bukombe kuja Katoro yenye urefu wa kilometa 65 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Maana ni siku nyingi iliahidiwa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja inatekelezwa kwa mradi wa Rais, na taratibu zipo zinaendelea kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naomba kuuliza Mkandarasi wa Mbogwe aliripoti toka mwaka jana lakini mpaka sasa hivi hakuna kazi inayofanyika, vijiji 34 havijapatiwa umeme. Ni nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maganga Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya REA III Round II inaendelea katika hatua mbalimbali katika maeneo yetu, kama ambavyo tumewahi kueleza hapa Bungeni kwamba miradi ya REA III round II inazo hatua kadhaa za kufikia ili kuweza mradi kukamilika katika utekelezaji wake. Kwa hiyo, nimwakikishie Mheshimiwa Maganga kwamba naamini katika eneo lake hatua mojawapo katika mradi huo itakuwa inaendelea. Lakini nimwombe kwa sababu lipo banda letu hap ana mkandarasi anayetengeneza mradi huo yuko hapa, Meneja wa Wilaya yuko hapa, Meneja wa Mkoa yuko hapa basi tutembelee pale na tuweze kujua tatizo na kero ambazo zipo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu hayo, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo kwa wawekezaji, wanakuja na leseni sehemu ambapo wanachimba wachimbaji wadogo, wakifika na leseni wanawafukuza bila kuwalipa fidia wamiliki wenye maeneo (ardhi): Sasa nataka kujua, nini kauli ya Serikali kuhusu hawa waliomiliki ardhi yao kwa muda mrefu wanafukuzwa pasipo kupewa malipo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Wachimbajii wadogo wamekuwa na kilio kikubwa cha tozo kwenye mifuko ya mawe: Ni lini Serikali itawapunguzia tozo ya mawe kwenye maduara pale wanapochimba ili kusudi nao waweze kufaidika na kazi zao? (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maganga, Mbunge machachari wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ieleweke kwamba uchimbaji wa madini, ili mtu aweze kuchimba ni lazima awe na leseni ya uchimbaji madini. Kabla hatujatoa leseni kwenye eneo lolote, timu yetu ya wataalam lazima ikague maeneo hayo kujiridhisha nani yupo? Anafanya kazi gani? Kama hawajaomba maeneo hayo, mara nyingi huwa tunawakumbusha kuomba. Inapotokea anatokea mtu amepewa leseni kwa kawaida, na hata Mbogwe tumefanya hivyo; wale waliopewa leseni lazima waingie makubaliano na wenyeji ili kusionekane kuna upunjaji wa namna yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu tozo za mifuko, jambo hili ni jambo ambalo linawezekana kufanyiwa kazi kama tu aina ya uchimbaji unaofanyika utakuwa wa nia ya kuchimba, kuchakata na kuzalisha dhahabu. Ila, kama wachimbaji wenyewe wataamua kugawana mawe, na ni uchimbaji usiokuwa rasmi kwenye rashi, wajue kwamba na Serikali lazima iwe na sehemu ya mgao kwenye migao hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kituo cha Polisi Masumbwe kiko kwenye eneo la CCM na tumeshachukua eneo kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi pale Mbogwe. Je, Serikali inatusaidiaje Mbogwe ili kusudi askari wapate mahala pa kukaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mbunge kwa mahusiano mema na Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi ambao waliweza kutoa jengo linalotumika na Kituo hicho cha Polisi. Hata hivyo kama tulivyokwishasema kwenye majibu yetu ya msingi mbalimbali ni kwamba kipaumbele ni kujenga vituo vya polisi kwenye maeneo ambayo hayana kabisa, Mbogwe ikiwa ni mojawapo tutaipa kipaumbele katika miaka ijayo ili kuweza kujengea kituo chake cha polisi. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbogwe ina barabara nyingi, ukizijumlisha upana wake ni zaidi ya kilometa 3,000, hivyo basi barabara nyingi mpaka sasa hazipitiki Mheshimiwa Naibu Waziri na wewe ni shahidi, tulishawahi kwenda pamoja kwenye hilo jimbo.

Je, ni lini sasa hizi barabara nyingine ambazo haziko kwenye mpango utanipa bajeti ili TARURA ya Mbogwe iweze kuzitengeneza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wilaya ya Mbogwe ina madaraja manne na mpaka sasa hivi madaraja hayo hayapitiki, likiwemo Daraja na mpaka wa Bukombe, Kata ya Masumbwe ambalo linaunganishwa na Kata ya Bugerenga.

Naomba kujua sasa Mheshimiwa Naibu Waziri umejipangaje ili kuweza kunisaidia wananchi wangu waendelee kufaidika na Serikali hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajenga barabara hatua kwa hatua na ndiyo maana hatua ya kwanza Mji wa Mbogwe umeingizwa katika Mpango wa RISE. Hatua nyingine Mheshimiwa Rais alifanikisha kuongeza bajeti ya TARURA ambapo tunafika maeneo mengi. Kwa hiyo, hata hizo barabara ambazo zimebakia tutaendelea kuzijenga kwa kutenga fedha za bajeti katika kila mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa vilevile lengo la Serikali kupitia TARURA ni kufungua barabara hususani katika yale madaraja mabovu yakiwemo hayo aliyoyataja. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya tathmini na tutatenga fedha ili kuhakikisha kwamba yanajengwa kwa wakati, ahsante sana.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mbogwe inazo stand mbili, lakini hali yake ni mbaya sana hasa mvua ikinyesha, mabasi huwa yanapata shida kupita.

Je, ni nini kauli Serikali kuweza kuzikarabati stand hizo ili zikae kwenye standard?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicodemas Maganga, Mbunge wa Jimbo la Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Maganga kwa namna anavyowasemea wananchi wa Mbogwe. Lakini nitoe maelekezo kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe afanye tathmini ya gharama zinazohitajika kufanya matengenezo kwenye stand hizi mbili ambazo ni chakavu sana ili tuone kupitia mapatao ya ndani wanaweza kufanya matengenezo, lakini kama mapato ya ndani hayatoshelezi basi waweze kuwasilisha maandiko ya kimkakati Serikali itafute fedha kwa ajili ya kutengeneza stand hizo. Ahsante.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, barabara ya kutoka Masumbwe – Rugunga - Ushirika kwenda kuunganishwa na Mkoa wa Geita, lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoiainisha itajengwa kadiri fedha zitakavyopatikana kwa kiwango cha lami, ahsante.