Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nicodemas Henry Maganga (24 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Bajeti ya Madini. Naomba nianze kwa kumpongeza Waziri wa Madini kaka yangu Dotto Biteko, kutoka bilioni 168 mpaka bilioni 528 makusanyo hongera sana kaka. Pamoja na kumpongeza naomba niweke changamoto, lazima tufikirie kwamba ni kwa nini mwanzoni tulikuwa tunakusanya pesa kidogo na sasa hivi tunakusanya bilioni 528, ni jambo la kufikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa watu wetu kuna malalamiko makubwa, hasa wachimbaji wadogo. Mimi natokea Jimbo la wachimbaji, Mbogwe. Juzi nimefanya mikutano mitatu kwenye Jimbo langu malalamiko ni makubwa sana. Naomba niishauri Serikali, Mama Samia, Rais wetu, najua maeneo yote yenye uzalishaji wa madini, migogoro ni mahali pake na mimi kwangu nikiri wazi kabisa kuna mgogoro ambao ni mkubwa sana ambao unaninyima sana raha ni wa pale Mbogwe Nyakafuru. Kuna kikundi kinaitwa Isanjabadugu, nashukuru kaka yangu Mheshimiwa Dotto ameniahidi baada ya Mei Mosi tutaenda kutatua huo mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale wananchi wana haki, kama nilivyoeleza kwenye mkutano wa tarehe 27 Februari, kwa Mheshimiwa Rais, Marehemu Magufuli, wale wananchi mashamba yale ni ya kwao, lakini mzungu aliingia kwa kutafiti ikabidi sasa, baadhi ya watendaji wa Serikali wachache waingilie kati, zikafunguliwa kesi mahakamani. Uzuri wananchi wangu wameshinda zile kesi na wana nakala za hukumu, wanatakiwa wakabidhiwe mashamba yao ili waendelee kupokea ile asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Dotto anisaidie sana kwenye Jimbo langu la Mbogwe, maana wananchi wale machozi yao yatatufata siku tukifa, maana wanalia mpaka sasa hivi hawapati chochote wakati mashamba ni ya kwao.

Mheshimiwa Spika, vile vile, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwenye upande wa TRA aliishauri vizuri sana, lakini sekta nyingine ambayo ni ngumu ni hii ya madini. Nilikuwa mfanyabiashara wa madini sasa hivi nimeacha kabisa. Nilichukua mkopo hapa milioni kama 500 na sheria za madini ni mbaya sana, yaani pesa yako ukiichukua tu ukanunua makinikia, wanatoza tozo yaani bila kuangalia mtaji kwamba, umeingiza pesa kiasi gani, wao wanaangalia kulipa tu kodi, ndio maana makusanyo yamepanda namna hii. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tuangalie vizuri huku tukiangalia na wananchi wetu. Kwenye Hotuba yake Mheshimiwa Waziri amesema atawasaidia wachimbaji wadogo na naomba ufafanuzi pale, atawasaidia kwa kuwapa pesa ama kuwapunguzia changamoto zilizoko vijijini? Maana kuna Kamati ya Ulinzi na Usalama pale unapochimba tu duara ukapata mifuko kwa mfano, kumi, ile Kamati ya Ulinzi na Usalama inachukua mifuko miwili halafu watu wanajiita sijui nani nani? Serikali ya Kijiji, mifuko miwili, ukiangalia mtu huyu anayepewa leseni naye anachukua mifuko mitano, kwa hiyo, mchimbaji anakutwa anabaki na mifuko 10, malalamiko ni makubwa sana kwa wachimbaji wadogo. Migodi ya Nyakafuru, Mwakitorio, Geita na Mabomba, ukikaa na wachimbaji wanailalamikia sana Serikali kwa hizi tuzo. Kwa hiyo, Waziri pamoja na Mheshimiwa Rais wafanye juu chini kuhakikisha kwamba, wananchi hawa wanyonge, maana sera ya Chama cha Mapinduzi tulikuwa tukinadi majukwaani kwamba tutawajali sana wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanyonge hawana haki kwenye Taifa hili hawa wachimbaji wadogo. Sana sana labda, naona yanasaidiwa mashirika yale makubwa STAMICO pamoja na mashirika mengine yaliyoyoendelea na wazungu. Hata hivyo, hotuba ya Mheshimiwa Rais ilizungumza kwamba, hata sisi Wabunge tuwe mabilionea, kwa hiyo, hatuwezi kuwa mabilionea hata siku moja, kama umeingiza pesa milioni 100 hujapata hata faida, lakini ukikutana na Afisa Madini unaambiwa ulipe milioni saba hujapata hata faida. Mimi ni mfanyabiashara na nina watumishi wazuri tu tunafanya hesabu wakati ule tunapoenda kulipa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiingia Wizara ya Madini hicho hakipo. Wanaangalia tu umeuza shilingi ngapi wanatoa lolaite (loyalty), wanatoa service levy, pamoja na michakato mingine ambayo haieleweki, haina vichwa wala miguu. Kwa hiyo, tunaweza tukajisifu sana kwamba tumekusanya sana…

SPIKA: Sasa wewe mtani mbona sasa unaongea Kisukuma kwenye mchango wako? (Makofi/Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante mimi si nilikuambia ni Msukuma. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Sasa hiyo lolaite ndio nini hiyo? (Makofi/ Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, nini? lolaite? (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Haya Mheshimiwa, endelea kuchangia. (Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, bado dakika tatu.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba tunaiingizia Serikali pato kubwa na sisi tuangalie wale tunaotoka kwenye maeneo ya hii migodi inayoingiza. Maana hatuna barabara, hatuna afya, yaani wananchi wetu wana shida. Huwezi ukalinganisha na kwamba tumeingiza kwenye pato la Taifa bilioni 528, wakati hatuna chochote tunachopata katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Rais pamoja na wahusika wote watuangalie kwa macho mawili, hii migodi inayotoa dhahabu kwa wingi Geita, hasa Mkoa wa Geita na Shinyanga… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo la kwanza, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu tena kwa siku ya leo kuniona wa maana kwamba niweze kuchangia hii sekta ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Mawasiliano, Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, lakini kuna shida kubwa sijui unakwama wapi kaka. Toka tufahamiane nimekuwa nikikueleza kilio changu cha mawasiliano katika Jimbo la Mbogwe. Jimbo la Mbogwe lina kata 17, vijiji 87, lakini kuna uhaba mkubwa wa mawasiliano. Ninazo kata 17 lakini kata 10 mawasiliano hakuna kabisa, kuna Nyasato, Buligonzi, Ushirika na Mbogwe Makao Makuu pale ambapo halmashauri yangu ya wilaya ndio iinatokea pale lakini hakuna network hivyo, inafanya kazi za Serikali kuwa ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ulimwengu wa sasa mawasiliano ndiyo mtaji wetu mkubwa, tunafanya mambo ya posa ikiwemo transaction za kibenki. Kwa maana hiyo sasa nakuomba Waziri uone aibu ufike Mbogwe ili kusudi uone namna gani vipi, usiangalie maneno tu ya humu Bungeni mnakula kiyoyozi halafu kazi hazifanyiki. Umekuwa mteja mkubwa wa mawasiliano mimi mara nakuona Kigamboni na wilaya zilizoendelea na sehemu nyingine, hebu utuone na sisi vijijini kule kwamba tuna umuhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Jimbo la Mbogwe lina migodi 11 midogo midogo ambapo siku moja Waziri wa Madini amesimama na kulihakikishia Taifa tumeingiza shilingi bilioni 528, lakini wananchi wanaochimba haya madini hawana mawasiliano. Kuna Mgodi mzuri kabisa Nyakafuru na Kanegere, wachimbaji wakienda kwenye migodi ile hakuna mawasiliano. Kaka yangu nihurumie pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano mdogo wangu Mheshimiwa Kundo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata ya Iponya na Lugunga pamoja na Ikungwigazi, Isebya, Ilorwanguru, Mpakali, Mponda na Nhomolwa, haya maeneo ninayoyazungumza Waziri ni maeneo yenye uzalishaji na kuna binadamu wenye akili timamu kushinda hata Wagogo walioko huku Dodoma pamoja na sehemu nyingine na Wazaramo kule. Kwa maana hiyo, nikuombe Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano msikae mjini tu hebu twendeni shamba huko maana mambo mazuri yanatoka shamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nichangie kwenye upande wa mawasiliano kwenye vifurushi. Unapoweka kifurushi inakwambia ni mwezi mmoja, nikiangalia leseni mmetupa leseni za mwaka mzima ni kwa nini napotaka nijiunge na mawasiliano kwenye internet unaambiwa ni mwezi mmoja tu? Hilo nikuombe Waziri uje na majibu kamili, tofauti na hapo mimi jioni nitashikilia shilingi haipo sababu ya kupitisha bajeti yako mpaka utupe ufafanuzi ni kwa nini mtu anapokuwa na Sh.50,000/= kwa mfano, lakini unapoingiza kwenye kifurushi unaambiwa ni siku 30 tu wakati leseni ni ya mwaka mzima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine Mheshimiwa Waziri kwenye sekta yako huku wizi unaongoza sana. Unaona namba tu unaambiwa tuma kwa namba hii, mimi fulani bin fulani tuwasiliane kupitia mawasiliano haya kumbe ni tapeli tu. Najua kuna sheria zetu za mawasiliano zinatuongoza, sijui unaweza kuwa na majibu leo tuna miezi sita sasa unaelekea wa saba, umeshitaki matapeli wa namna hiyo wangapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi zile ukienda Polisi kunakuwa na mizunguko mingi utafikiri hata askari wanajua labda tatizo linalofanyika kwenye wizi wa mawasiliano. Hivyo, kaka yangu kwa kuwa Mama Samia, Rais wetu amekuamini, hebu jaribu kuumiza kichwa hawa matapeli wanaotapeli wananchi na kama unavyojua wananchi wetu hawana uelewa sana, maana hivi vitu ni vipya zamani havikuwepo, kwa hiyo, anapoibiwa mwananchi mmoja hasara yake ni kubwa sana maana umeambiwa tuma kwa namba 07 by hiyo, sasa hivi tuma au unaweza ukapigiwa na mtu akakwambia mimi sijui nani-nani Tigo Pesa huku, tukutane sehemu fulani, lakini ukianza ufuatiliaji unakuta hata kwenye Jeshi la Polisi kituo kizima labda askari ni wawili wanaohusika na hicho kitengo, lakini mwisho wa siku na wenyewe…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hili ambalo analizungumza Mbunge wa Mbogwe ni kweli kumekuwa na wizi mkubwa kupitia mitandao. Hata mimi hapa kwenye simu yangu nimepokea message ambayo inasema tuma fedha kwenye namba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Rais wakati anazungumza na Jeshi la Polisi ameiagiza Wizara watuambie ni kwa nini kama tulifanya usajili wa line kwa kupitia finger prints lakini utapeli huu bado unaendelea. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali jioni hapa wakati inatoa majibu itujibu pia katika hili, naomba kutoa Taarifa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa umeipokea Taarifa?

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa ya Mheshimiwa, naiunga mkono tuko na pamoja kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, naomba niendelee kwa kukushauri Waziri, tunapokushauri kwenye vyombo hapa sio kwamba labda tunakuchukukia, tunakupenda sana, unajua mtu anayekueleza ukweli anakuthamini. Tunatamani sana uendelee kuwa Waziri, lakini umiza kichwa, hiki kitengo chako ni kigumu, watu wanaibiwa, watu wanapoteza haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Jirushe, unaweza ukaweka 10,000/= ukapewa siku 30, dakika 20 pesa inakuwa imeshaisha wakati umeambiwa ni mwezi mmoja. Jaribuni sasa kuumiza vichwa pamoja na CAG na vyombo vingine muangalie tunaibiwa kupitia njia gani, ili kusudi utatuzi uweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho, Mheshimiwa Waziri…

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa matapeli wanaoiba kwa mitandao hawaibi kwa mitandao peke yake mpaka na minara. Hii minara yote imeenda kuwekwa kwenye maeneo ya milima ya vijiji, unaambiwa mwenye leseni yuko Dar-es-Salaam anaitwa Gasper Gap; sasa unashangaa nani aliyempa leseni kwenye mlima wa kijiji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii taarifa pia nampa Mheshimiwa Maganga ajue wanaiba mpaka kwenye minara. Tunaomba Waziri aje atuambie nani mwenye hiyo minara hiyo? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, Taarifa umeipokea?

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa. Unajua mimi naogopa kufunguka sana maana Naibu Waziri pale na Waziri wananiangalia sana na wanafikiria kwamba labda kweli bajeti yao haitapita. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoomba niwashauri Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, hebu tumieni taaluma zenu pamoja na uwezo mliopewa na Mwenyezi Mungu muweze kulisaidia Taifa. Tofauti na hapo sekta hii ndio inaongoza kwa ujambazi na wizi, ina maana hatutasonga mbele. Wananchi wana matumaini makubwa sana na sisi, ili tuweze sasa kuutoa uchumi wetu kwenye kiwango cha kati, tukiacha kuibiwaibiwa huku kwenye minara au kwenye sekta ya mawasiliano lazima tutapiga hatua tu, lakini kama tunawapa shilingi 10,000 inaisha saa 24 hatuwezi kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi watu tumeshalemaa, mimi hapa sasa hivi nikiwa sina simu ninahisi kama niko kaburini. Ina maana simu ni kitu muhimu kuliko vitu vyote. Sasa unapokuwa na simu tena inakulia hela pasipo utaratibu unakuwa kama vile una wake zaidi ya 10 wakati una simu moja kwa ajili ya kupata tu connections. Kwa maana hiyo, mimi Waziri nikuombe sana jitume, pambana, lakini Kanda ya Ziwa lina maeneo makubwa sana yenye milima na lina wananchi wengi sana; hebu ukija Mbogwe sasa mimi nitakutembeza na uone migodi jinsi ilivyo huko. Kuna migodi mingi Mwakitolyo, kwa Mheshimiwa Iddi Kassim kule Nyangalata, kuna Mwabomba, yale maeneo yote hayana mawasiliano. Kwa hiyo, hakuna haja ya kukaa Kigamboni Mheshimiwa ukumbuke uchaguzi mpaka 2025 na hata kama hauna mafuta sisi ni wauza mafuta mimi na mwenzangu Mheshimiwa Tabasam tutakuwa tunachanga kwenye magari yako ili uweze kufika kwa wananchi wenye shida. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo tena kuweza kupata fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya Ardhi. Mimi ni Mbunge wa Mbogwe. Jimbo la Mbogwe ni Wilaya mpya. Nitumie nafasi hii kumshauri mtani wangu, Mheshimiwa Waziri Lukuvi pamoja na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Angeline Mabula.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingi wenzangu wameigusia, mimi naomba kutumia muda vizuri ku-focus kwenye nafasi ambazo ni za muhimu zinazowakabili wananchi wa Tanzania hasa wa Mbogwe. Lipo jambo moja Mheshimiwa Waziri kwenye upande wa hizi taasisi, kwa maana ya Makanisa pamoja na Misikiti, pale ninapotokea Mbogwe, kuna migogoro mingi sana maeneo yale ya taasisi. Nianze kwa kukueleza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Jimbo la Mbogwe ni Wilaya mpya kwanza sina Baraza la Wilaya. Naomba unisaidie sana jambo hilo na uiweke kwenye kumbukumbu zako ili usisahau mtani wangu, itakuwa hakuna nilichokifanya katika mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikusikiliza wakati unatoa hotuba Mheshimiwa Waziri, kiukweli bila unafiki, nimeridhishwa na maelezo yako. Japokuwa sasa nami nimepata hii nafasi ya kukushauri leo mbele ya Bunge hili Tukufu, uniruhusu tu nigusie kidogo ili kusudi pale panapowezekana nawe uweze kujipanga ili kusudi Taifa letu tuweze kusafiri vizuri na tuweze kufika salama safari yetu ya kuelekea 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nasikitika kwa kuanza kumpa Mheshimiwa Waziri shutuma ya sekta yake. Toka niapishwe kuwa Mbunge, kwenye ofisi zangu migogoro mingi ni ya ardhi. Nilipomaliza kuapishwa tu pale, niliporudi nyumbani, nilikutana na watu hawa wa Msikiti wa Masumbwe Mjini, walikuwa na kesi, tayari ilikuwa Mahakamani na baadaye hiyo kesi ikahukumiwa kwamba walipe shilingi milioni 70. Wazee wangu hawa wamekuwa wakilalamika sana, maana Serikali ni moja tunayoiongoza na mpaka sasa hivi hawana uwezo wa kulipa hiyo hela.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuiomba tu Serikali iangalie upya hilo suala, pamoja na kwamba kesi zilishafika Mahakamani, lakini hawa watu hawana uwezo wa kulipa hayo madeni ya nyuma. Kwa hiyo, nakuomba wewe pamoja na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, mwone namna gani mnaweza kuwasaidia watu wenye misikiti na makanisa ili kusudi waendelee kumwabudu Mungu katika roho na kweli pasipo na pressure za madeni. Maana kila Kanisa ukiingia sasa hivi, michango mingi utaambiwa Serikali inatudai na ukiangalia kiuhalisia, hawana uwezo wa kuyalipa hayo madeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, likiisha hili Bunge, afike Mbogwe; maana kwa kuwa Mbogwe kwanza haina Baraza, halafu ni Wilaya mpya ambayo GN yake ilitoka mwaka 2019; kwanza kuna uhaba wa watumishi kwenye sekta yake. Nafahamu Serikali ya Awamu ya Tano tulikuwa tukipigania kuhusu maendeleo na kiukweli huwezi ukapata maendeleo bila kuwa na hati (document) ya kuweza kukufanya ukakopa hata benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mbogwe sasa inakuwa kwa kasi na ni Wilaya inayojitambua ina Mbunge kijana halafu makini, anazijua biashara vizuri, namwomba Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi dada yangu, wafike Mbogwe waangalie Mji wa Mbogwe jinsi ulivyo, ni mzuri. Mbogwe sisi tuna madini lakini pia sisi ni wafugaji, kumekuwa na migogoro kati ya wafugaji na wakulima; wewe Waziri mtani wangu ndio mwenye kutoa maamuzi hayo ukifika. Kwanza ukifika tu wakakuona, wataona kama vile ameshuka Yesu hapa, watakuwa na imani hata wale watumishi wa shetani walioko kwenye Wizara yako ambao wanatumia utapeli kuwatapeli wananchi na kuwapora ardhi yao watakuogopa na wananchi wale watapata haki zao za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mgogoro mwingine ambao nimekuwa nikiuzungumza kwenye mikutano yangu karibia kote. Kuna mashamba haya ya dhahabu, Wilaya yangu ina migodi karibia 22, lakini ukiangalia kila palipo na dhahabu kuna migogoro ya ardhi na kiuhalisia migogoro ya ardhi ya mashamba ya dhahabu haiwezi kutatuliwa na sekta ya madini, maana kila sekta inajitosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa yale maeneo hayajapimwa, kwa busara ya Mheshimiwa Waziri na heshima ambayo umenipa kwanza toka unipokee hapa Bungeni, ukifika utaona jinsi gani unaweza kuitatua hiyo migogoro ili watu waweze kupata zile asilimia na haki zao wenye mashamba yale yaliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kupata dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu, jambo lingine kuna Kata moja inaitwa Bukandwe Kijiji cha Kanegele Kambarage, pale na penyewe kuna mgogoro wa mbuga nzuri ambayo ina rutuba na inatoa mpunga mzuri sana. Ukifika na penyewe utaona jinsi gani uweze kunisaidia, kuna heka karibia 145 ambazo wamekuwa wananchi wakizigombania pamoja na kampuni moja ambayo jina nimelisahau, nitakwambia nikitoka hapa Bungeni ili kusudi uweze kunisaidia Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo changamoto nyingine. Kuna Sekondari ya Kata yangu ya Burugala, Sekondari ilijengwa, lakini wananchi wanavyodai ni kwamba hawajapewa chochote na Serikali. Hivyo sasa, kwa kuwa sekta hii ni yako Mheshimiwa na mtani wangu, tukifika huko mambo hayo nina imani utayamaliza tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Mji wa Mbogwe una kata karibia saba ambazo zimeendelea sana; ukinipa wataalamu wazuri waaminifu, maana mimi katika maisha yangu huwa napigania sana kupata watu waaminifu wa kufanya nao kazi; na ninakumbuka mchango wangu wa kwanza wakati naingia hapa Bungeni, niliishauri Serikali ya Awamu ya Tano kwamba sasa kwa kuwa Serikali imeanza upya; na sisi darasa la saba tupo na tupo wengi tunapiga sana kura, tena kwa uaminifu, huwa tunashinda kwenye misitari, msitubague. Mteue Wakurugenzi hata Darasa la Saba, maana kazi ya Ukurugenzi siyo kazi sana na hakuna kazi rahisi kama kuwa Mkurugenzi. Maana watendaji wapo tu wale Wakuu wa Idara, Wakuu unawaamrisha tu kwamba fanya hiki na hiki. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo sasa, leo hii Awamu ya Sita nitumie nafasi hii tena kurudia maneno yale niliyoyazungumza mwanzoni. Kwa kuwa najua uteuzi naendelea, tupewe nafasi watu wa Darasa la Saba ambao hatuna CV nyingi sana, ila tuna sifa ya uaminifu, ili twende tukazisimamie Halmashauri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu iko kwenye vita ya uchumi, hatuwezi tukaweka michango kwa kukupongeza tu, lazima mzee ukae attention. Kwanza unatakiwa ubadilike, sura yako ni nzuri mno Mheshimiwa Waziri, wakati mwingine na watendaji wako wanakudharau. Wewe una nia nzuri, huwa nakuangalia sana mambo yako, una nia nzuri sana ya kuweza kuliletea mabadiliko hili Taifa, lakini waliomo ndani ya sekta yako hawana mapenzi mema na nchi hii na wala na wewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko Dodoma hapa leo mwezi wa Saba. Jana niliongea na wewe Waziri, wakati naingia hapa Dodoma, mimi niliingia kwa kutafuta maeneo yale hot cake, kuna maeneo mengi tu yenye uwazi ambayo yalikuwa yanaonekana, kama unavyofahamu Mheshimiwa Waziri sisi Wasukuma kwa kuwa tuna roho nzuri sana, ni wepesi wa kuwaamini watu. Baada ya kujaribu kuchukua yale maeneo, tumeingia migogoro ambayo yaani haiwezi ikaisha leo wala kesho. Ufafanuzi ulionipa, nami kwa kuwa ni mwelewa halafu ni senior, nimeshaelewa ni nini cha kufanya ili kusudi hela yangu isipotee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kwa kuwa tuko kwenye vita ya uchumi, badilika uwe mkali kidogo pamoja na Naibu Waziri ili kusudi wakuogope wale watendaji wako, watu waweze kupata haki zao kwa wakati muafaka. Leo Mheshimiwa Waziri utaona watu wengi wanakupongeza, kila mtu anasimama anakupongeza, lakini siku ukikosa haya madaraka, utakuja kuniambia, siku moja Maganga uliongea Bungeni. Hao hao ambao walikuwa wanakupongeza, watakugeuka na kukuona yaani hufai na hukutumia vizuri mamlaka yako wakati ukiwa Waziri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utembelee kwenye Jimbo langu la Mbogwe maana wewe ardhi zote ni za kwako; na kuna mapori mengi ambayo yalishamaliza kwanza kuwa na sifa ya kuwa mapori…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imegonga, nikawa nasubiri umalizie sentensi, naona mambo mazito unaendelea kumwaga hapo. Ahsante sana.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, haya nakushukuru. Basi mchango wangu mwingine nitamwandikia Waziri ili auone, maana nimeshauandaa hapa ninao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na fursa hii niweze kuchangia Sekta hii ya Uvuvi na Mifugo. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi niweze kuweka mawazo yangu kwenye hii Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2020 tulikuwa kwenye uchaguzi. Miongoni mwa vitu tulivyokuwa tukitembea navyo majukwaani, ukisoma ukurasa wa 52 ilani yetu ambayo ilikuwa andiko letu kuu kuweza kuwaomba ridhaa wananchi ili tuweze kuwaongoza katika Chama cha Mapinduzi, tuliahidi kwamba tutawasaidia wafugaji pamoja na wavuvi. Hata hivyo, kila kinachoendelea sasa hivi kwenye hili Taifa, leo ni mwezi wa Saba sasa, unaona kabisa kwamba bado hatujatekeleza huu ukurasa wa 52. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Mashimba pamoja na Mheshimiwa Ulega, kwa kuwa wao ndio wasimamizi wakuu wa Wizara hii, kwanza sheria zilizotungwa za hiyo sekta ni chonganishi, naweza nikasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba hata Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano tulimchukia sana Kanda ya Ziwa wakati akiwa sekta hiyo, lakini ukweli ni kwamba baada ya kukua, nami kuingia kwenye michakato hii ya kisiasa na kuona kabisa sheria ziliwekwa vibaya; kwa maana hiyo mimi nikushauri Mheshimiwa Mashimba, ongea na Mheshimiwa Rais, kuna vipengele muhimu vya kuweza kufanyiwa marekebisho ili uweze kurudi hata Bungeni mwaka 2025, lazima sheria zibadilishwe, maana wafugaji kwenye hili Taifa wamekuwa kama wakimbizi. Wewe ni Msukuma mwenzangu tunaongea lugha moja na tumetoka sehemu moja, lakini kiukweli yaani ukisimamia hizo sheria lazima watu watakuchukia hata kama ni mtoto mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wafugaji wanavyoteseka kwenye mapori hasa kwenye Jimbo langu la Mbogwe, kuna utitiri wa mapori, nilishaongea na Mheshimiwa Waziri tukiwa wawili na alisema atanisaidia, sasa leo nitashika shilingi ili anihakikishie kwamba Mbogwe katika bajeti yake atanisaidia mabwawa mangapi na majosho mangapi ili niweze kuachilia kushika shilingi? Waheshimiwa Wabunge naomba mniunge mkono kwenye hili kama tutashindwana na kaka yangu ili kusudi tupinge, tusiwe tunapitisha tu kila bajeti bila hata kujua kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuzungumzia wafugaji wa Tanzania. Lazima tukubaliane kwamba; unajua katika maisha huwa kuna Kiswahili kinasema tunaishi kwa kutegemeana. Tukirudi kwenye historia ya nyuma, miaka ya nyuma huko, wakati wa utawala wa Mwinyi, ikumbukwe kwamba Wasukuma professional yetu sisi ni wafugaji. Ukiangalia Wamasai miaka ile tulikuwa tunagombana nao maporini, kazi yao ilikuwa kuja kutuibia ng’ombe ili nao waende wakafuge. Sasa hivi ukiangalia Wasukuma wengi wameacha biashara ya kufuga ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Taifa tuna-force kuingia kwenye utajiri; na hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alizungumzia kwamba hata Wabunge tutafute ubilionea. Kwa maana hiyo mimi kama Msukuma sasa, sheria za ufugaji zikirekebishwa vizuri, mimi nitarudi kwenye professional yangu. Hakuna haja ya kuhangaika na network, wala haya mamitandao sijui mara M-Pesa rusha huku, fanya hivi; maana sisi Wasukuma professional yetu ni wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hata maandiko ya Neno la Mungu kulikuwa na Mfalme Daudi, alikuwa ni mchunga ng’ombe; hakuwa hata na Malaria maana alikuwa anakunywa maziwa ya ng’ombe. Hata mimi wakati bado sijaja mjini nilikuwa siugui typhoid, maana maziwa ya ng’ombe yale wale waliosoma sayansi wanaweza wakakuelezea ni nini maana ya kuwa na faida ya ng’ombe. Leo yanapokuja hata maziwa haya ya kiwandani, nakuwa sipati picha maana kila mara magonjwa yanazidi kuwa mengi na mpaka tunataka kuingia kwenye chanjo ambazo hazina sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na kuwadharau wafugaji na sisi Wasukuma tunaonekana washamba kwenye Taifa hili. Ni kweli sisi Wasukuma tuna sifa moja, yaani mkiingia pori moja ni kufyeka kwa kwenda mbele ili kusudi kujaribu kujitandanua kimaisha. Kwa kuwa sasa Chama cha Mapinduzi kiliahidi kwamba kwanza kwenye hizi hifadhi zetu tutapewa maeneo, tupewe sasa maeneo. Huu mwaka ni wa kwanza, bado miaka minne tuingie kwenye uchaguzi mwingine, tusiongee story. Binadamu sisi huwa tunasahau, yawezekana kabisa shida tuliyoipata kwenye kampeni watu wanaweza kuwa wameshasahau, lakini nataka niwahakikishie, tusipotimiza mambo haya, tutapata taabu sana mwaka 2025. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee upande wa uvuvi. Wananchi wangu wengi wako Ziwa Victoria. Nilishawahi kuongea na Mheshimiwa Mashimba na leo niongee naye nikiwa kwenye vyombo. Wavuvi wanapata taabu sana. Kuna mageti; ukitokea pale tulipokuwa na wewe Mheshimiwa Waziri na Rais wa Zanzibar, tulienda kwenye mwalo mmoja wa Mganza, ulisikia shida za wafanyabiashara wale na walikueleza changamoto wanazokabiliana nazo. Yamewekwa mageti mle njiani ya kipigaji. Wanahangaika wafanyabiashara wa dagaa, wafanyabiashara wa samaki wanafanyabiashara kwa shida, wanasumbuliwa na watu hawa wa misitu. Serikali ni moja lakini inakuwa kana kwamba Serikali ziko mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mashimba, kaka yangu, Wizara hiyo kwa kuwa naye ameipenda na Rais wa Awamu ya Sita amemwamini, itendee haki hiyo nafasi. Kumbuka kwamba kuna mwenzio ambaye hata kwenye Ubunge wake amepita kwa wakati mgumu sana, nikimsikia sasa hivi speech zake kidogo saa hivi anatoa hotuba ambazo zina urafiki na wananchi kule anakotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wavuvi wengi wanakufa wakiwa wanakimbizana na operation za mle ziwani. Mwaka 2016 kuna marafiki zangu watatu walikufa wakiwa wanafukuzwa na watu wa maliasili kwenye Kisiwa cha Rubondo walikuwa wanakaa Chakazimbwe. Kuna Visiwa vya Chakazimbwe, Mrumo, Iramba na Mjuno; Mheshimiwa Mashimba ukifanya ziara huko ukaongea na wale watu, utapata ukweli wangu, tarehe ya leo 27 nakushauri pamoja na Naibu wako mfanye ziara kwenye Visiwa vya Yozu, Nyamango humo, mkaongee nao. Wale wa professional yenu wawaambie na ili mje sasa siku moja mlete hata Muswada wa kufanya marekebisho ili kusudi nao waishi vizuri na waweze kuendelea vizuri na uvuvi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye Kamati ya Matumizi nishike shilingi ili kaka yangu anihakikishie bajeti yake atanisaidiaje kwenye Jimbo langu, tusiongee tu maneno maneno hapa halafu mwisho wa siku tusiweze kufanikiwa chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda jambo lingine tena niliweke sawa hapa. Namshukuru Mungu jana mchango wangu mwenyewe nilichangia na niliongea maneno mengi; namshukuru Mheshimiwa Lukuvi ameniahidi vitu vingi atanisaidia. Tukiangalia hii Sekta ya Uvuvi, tukaangalia na hii sekta ambayo tuliichangia jana, ni vitu viwili vinakaribiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, jana kwa kuwa Mheshimiwa Lukuvi alisema atakuja Mbogwe, ni vyema sasa tuje tupitie maeneo na mazingira ya Mbogwe yale ili kusudi tuangalie hata tunapokuja kubadilisha sheria mkaona na usumbufu ule wananchi wa Mbogwe wanaoupata kwenye yale mapori utakuwa umenisaidia sana kaka yangu. Sijui unanisikia Mheshimiwa Mashimba. Nakuona kama unanisikia, lakini naomba andika hiyo halafu uje uitolee maelezo kwenye kuhitimisha hotuba yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nikushukuru wewe, leo ni mara yangu ya tisa sasa kuchangia hapa. Mwanzoni niliongea vitu vingi na nikaiomba Serikali ya Awamu ya Tano iweze kutusaidia na isitubague sisi watu wenye elimu kidogo, lakini karama zetu zinakubali na kuweza kufanya vitu vikubwa kwenye hili Taifa, naomba nawe maneno yangu uyasikilize. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea neno viwanda, ni vyema na sisi tujitegemee na tujitambue. Tusitegemee tu kila kitu; nimemsikiliza mchangiaji wa kwanza anajaribu kutolea mifano Botswana, wapi na wapi; ni vyema tujiamini, kwa sasa tulipo hapa, tuko sawa sawa kabisa. Tukiwa tunachukua mifano Ulaya tu, kila kitu Ulaya, hatutaenda popote pale. Sisi tuliumbwa na Mungu, tuliwekwa kwenye ardhi ya Tanzania, Mungu alituamini, tena akatupa Taifa lenye makabila mengi na Taifa letu halijapata vita hata ya kikabila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema kila mmoja sasa akithaminiwa; msomi amthamini ambaye hajasoma. Huyu ambaye hakusoma, amthamini msomi. Tunaishi kwa kutegemeana, maana hata sisi ambao hatujasoma hatuwezi kuingia kufanya operation kwenye hospitali yoyote, lakini tumekuwa na shida sasa hivi humu Bungeni, kumekuwa na mvutano fulani na kuchukiana sisi kwa sisi; ma-professor na wale wasio ma-professor. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Wabunge, sote humu tuna akili timamu na tumevuka mishale mingi kufika kuingia kwenye jengo hili, tuheshimiane kuanzia leo. Naomba kwa kauli mniunge mkono, hiyo vita isiendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante katika jina la Yesu.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Maganga. Naamini Mheshimiwa Waziri amekusikia vizuri na ninaamini ataweza kukusaidia vizuri.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono akinifafanulia, maana nashika shilingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa mwaka 2022/2023. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunifanya siku ya leo tena nipate nafasi hii adimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu waliotangulia wamesema mengi wamesema mazuri na naungana nao. Sasa nichangie Mpango wa Mwongozo wa Taifa. Nimeusoma wote, nimesoma sura ya pili pale inapoelezea kwamba deni la Serikali limekuwa. Jana wakati Waziri anasoma hapa nimepata meseji nyingi sana kwa Watanzania wanahoji ni kwa nini deni limekuwa kutoka bilioni 564 mpaka bilioni 644 ambayo ni sawa na asilimia 14.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu tuko kwenye kipindi kigumu, wakati huu Watanzania wanatupima, tuko kwenye utekelezaji. Nimpongeze Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia, kiukweli anapambana sana, kweli kabisa yaani bila unafiki mama anapambana, isipokuwa niseme tu wazi maana huwa napenda kusema ukweli, mama anacheza peke yake kwenye uwanja, wasaidizi hawafanyi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu nimeshuhudia hii trilioni 1.3 jinsi ilivyoshuka vijijini kule kwenda kusaidia sekta mbalimbali kama vile afya pamoja na mambo mengine. Mwenzangu Mheshimiwa Tabasamu pale aliweka mfano wake, nami nataka nirudie tu maneno yake yale aliyoyasema, kuna hatari kubwa na hiki ni kipimo chetu cha kwanza sasa Wabunge kwenye maeneo yetu, hizi hela zinaenda kupigwa yaani inavyoonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza imeanza kuonekana mifano mingi mara cement imepanda, nondo zimepanda, yaani kila kitu kumekuwa na migogoro mingi, baada ya pesa kufika kwenye maeneo. Niiombe Serikali sasa iliangalie kwa macho manne, wananchi wanatupima, tukiangalia Ilani yetu yenye kurasa 303, wananchi walituamini kwa moyo mmoja kabisa na tuliahidi mambo mengi katika Ilani hii. Nashauri katika Mpango huu tuchukue vitu vichache tu ambavyo ni muhimu sana kwa wananchi wetu wale wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongelea suala la miundombinu za barabara mkoa hadi wilaya, bado hatujafanya lakini kwenye ilani humu wananchi tuliwaahidi. Ukiangalia kwenye mpango humu milolongo ni mingi, kuna ndege, service, mashirika yasiyo na mbele na nyuma, kwangu mimi naweza nikasema hivyo kwa uelewa wangu. Kwa wananchi wetu wale wapigakura waaminifu kuna vitu muhimu kama vitatu tu; miundombinu ya barabara, maji na afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiboresha hayo maeneo tunaweza tukathaminiwa sana na tukaonwa kweli kupitishwa kwetu, hata kuja humu ndani tutaonekana tunaisaidia Serikali kulikoni kuelekeza matrilioni kwenye masuala ya watu wachache, wanufaika wachache, hawa wengi ambao hawana uwezo wa kupanda hizi ndege wakaendelea kuteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu nazunguka sana kwenye nchi hii. Majimbo mengi nazunguka, ukiangalia pamoja na kwamba tumezungumza kwamba tumetekeleza, lakini kuna sehemu nyingi ambazo bado hazijafanyiwa marekebisho. Hii inasababishwa na mifumo yetu ya manunuzi, maana pesa kweli mwanzoni tu hapa ilitoka milioni 500, lakini ukiangalia mpaka sasa hivi hizo fedha hazijafanya kazi, bado sijui process za manunuzi, mifumo mara imekataa na sasa hivi mvua zinanyesha, ina maana wananchi wanaona kabisa haya ni maneno tunayaongea ambayo hayatekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namshauri Mheshimiwa Waziri, yeye kweli ni mpambanaji na nimemwamini kuanzia kwenye tozo, pale alipokusanya bilioni 48 na akazisema hadharani na akazielekeza kwamba ziende zikajenge vituo vya afya nikamwamini kabisa kweli ana mapenzi mema, lakini kwa kuwa na yeye ni binadamu naomba anisikilize ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu iliyopita nilishauri hapa kwamba, kuna wenzetu Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Vitongoji, hawa watu tumefanya nao kampeni kwenye uchaguzi, walikuwa wakitufungulia mikutano, tungewawekea hata kama ni shilingi 50,000 kwenye huu mpango na wao wajisikie vizuri, kuliko kuona deni linakua halafu wenzetu wanalala njaa, hawana hata shilingi 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa, nimeona kwenye Mpango huu inazungumziwa kwamba maji yanatoka Ziwa Victoria kuja Dodoma. Nikiri tu wazi kwamba Kanda ya Ziwa bado tuna uhaba sana wa maji. Waziri wa Maji naomba hilo waliingize kwenye Mpango maana ni kelele kubwa ambapo mimi na Mheshimiwa Waziri tumewahi kupita Kanda ya Ziwa na kuwaaminisha watu kwamba litakuwepo hili mwaka 2022 na 2023, lakini kwenye mpango humu halimo na wananchi wanahitaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la umeme, nimezunguka na aliyekuwa Waziri wa Nishati, tukawatangazia Watanzania kwamba umeme sasa unakuja tena tuliahidi mwezi huu ungekuwa umekamilika vijiji vyote, lakini mpaka sasa hivi bado sarakasi za kichina mpaka nazima simu kuonekana kwamba sina majibu ya kuwaeleza wananchi. Kwa hiyo Serikali ione umuhimu wa kupeleka umeme katika kila kijiji ambavyo vimebakia. Hii itaturahisishia sisi wanasiasa kuweza kuendelea kuwaongoza wananchi, maana tutakuwa tunatoa ahadi zile za kweli na zinafanikiwa kuliko kuwa tunapanga mipango elfu moja ambayo hatuiwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kwa wachimbaji wadogo, niishukuru Wizara ya Madini mwezi wa Nne ilinipa mkoa wa kimadini na nimekusanya mpaka sasa hivi bilioni 6.49 kwenye Mkoa wangu wa Kimadini Mbogwe. Niwaombe tu wananchi wengine, Wabunge nimeona wamo wengi humu wawekezaji karibu kwenye Jimbo lile, tuje tushirikiane, lakini hii sekta inapaswa iangaliwe vizuri, maana kwenye Mpango huu haimo, haijawekewa kipaumbele kwamba Serikali itasaidiwaje kwenye huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wadogo wanaingiza pesa nyingi na hawajawezeshwa na Serikali. Ukiangalia kuna mashirika Serikali huwa inayapa bajeti na ukiangalia zile hesabu hata ripoti za CAG hayafanyi vizuri, hao wachimbaji ambao wanachimba kwa nguvu yao Serikali ione umuhimu ya kuweza kuwasaidia watu hawa. Kwa mfano mimi hapa kama nimeingiza bilioni sita ni miezi mitatu tu, unaweza ukaona kwamba jinsi gani watu hawa waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa wafanyabiashara; Taifa hili, na-declare interest nauza mafuta, ipo changamoto kubwa kwenye mafuta ya petrol na diesel. Mafuta yanapanda bei kila siku, Serikali ione sasa namna gani inaweza ikatenga bajeti ili kusudi mafuta yakishuka bei kila mwananchi atapata unafuu kupitia hii bidhaa ya mafuta. Jana EWURA imetangaza tena kupandisha bei, wananchi wanalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wakati tunakuja mara ya kwanza Bungeni humu mafuta yalikuwa yanauzwa shilingi 1,900, lakini mpaka sasa hivi mafuta yanaelekea shilingi 2,500, vijijini ambako hakuna vituo mpaka shilingi 4,000, lita moja ya mafuta. Hii inaonekana kabisa kwamba mambo yanaenda vibaya kwenye Taifa letu na sisi Wabunge tunakuwa kama vile hatuyaelewi haya mambo wakati sisi naweza nikasema, ni maprofesa wa mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuiombe Serikali, ina bandari yetu na Waziri wa Nishati ameteuliwa juzi nimshukuru, nilimwona juzi sijui Norway, sijui wapi, alikuwa na mzungu, naomba apambane usiku na mchana, wananchi tunamtegemea ili tuweze kupata unafuu kwenye bidhaa ya mafuta. Mafuta yakipungua bei nauli zitashuka bei. Mafuta haya haya pia ndio yameshikilia uchumi wa nchi. Ukiangalia kwenye bandari yetu pale tunapoingizia mizigo, nahisi kuna michezo ambayo inafanyika pale ndiyo maana mafuta yanakuwa na bei juu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akidhibiti vizuri hapo tunaweza tukaishi vizuri sana na itaonekana kwamba tunamsaidia mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niwaombe Wabunge wote, unajua sisi ni wasaidizi wa mama na anatusaidia kweli kwenye Majimbo yetu, lakini nashangaa Wabunge hatusemi mazuri yale ambayo mama anayafanya. Alijitokeza mchana kweupe akachanjwa, sisi Wabunge wengine tunachanja kimya kimya kwa kujificha. Mama ametupa pesa za barabara, mama anatupa kila pesa anayoipata na anaitangaza hadharani za shule, zahanati na kadhalika. Tunakuwa na ugumu gani kusema mazuri ya mama pale tunapokuwa kwenye mikutano yetu. Kwa kweli niseme kabisa, kuna Wabunge nawaangalia tu, maana hawajui walitendalo, hawasemi kama mama kawatuma amewapa zile fedha wananyamaza tu.

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Sijui wanategemea nini mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna kila sababu hata tutakapomaliza hili Bunge, Wabunge wenzangu, tukiwa tunaifuatilia hii trilioni 1.3 tukamseme mama, maana hata juzi tumemwona akihutubia mataifa na kiukweli mama ni mpambanaji, siwezi nikalinganisha sijui ni mchezaji nani ambaye nilikuwa namjua, labda Messi, ila kila akipiga pasi hivi, wengine wanazubaa tu. Niwaombe Baraza la Mawaziri, kila Waziri ajitathimini kwamba ni kwa nini umepewa kiti hicho na ufikirie hapa Tanzania unafanya nini? Umepewa nafasi utembelee kwenye V8 au umsikilize Mama au ukamshauri na ulete mawazo mbadala ya kuweza kulibadilisha Taifa. Tofauti na hapo hizi nafasi tutaziomba na sisi, tunaziweza kabisa tena tunaziona ni kazi rahisi tu kuliko hata vitu vingine. (Makofi/ Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Maganga, kengele ya pili imegonga.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru sana. (Makofi/Kicheko)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hii taarifa ya Maguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Kwanza, napenda nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuongea kwa niaba ya wana Mbogwe, kuhusiana na taarifa ya madudu yaliyooneshwa na CAG.

Mheshimiwa Spika, hii taarifa ni ndefu, imebainisha vitu vingi. Nimejitahidi kadri ya uwezo wangu kuchambua madudu yaliyooneshwa na CAG. Anasema amepitia jumla ya taasisi za Serikali na mashirika 331, nikajitahidi kujumlisha hasara zinazooneshwa na CAG ambazo zinaonekana za mwaka 2020/2021 mwezi wa Saba japo zipo mpaka za mwaka 2018 na 2019.

Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue vizuri. Kwa vile imetajwa na Halmashauri yangu ya Mbogwe kwamba imo kwenye hati yenye mashaka. Napenda niliambie Bunge lako Tukufu kwamba haya mambo nilisema mapema kwamba nilikuwa siyajui hapo mwanzo, lakini kwa kuwa yamejirudia, naomba nifafanue vizuri ili wananchi wasiwe na hofu kwamba sasa msimamizi wao pamoja na Baraza la Madiwani imekuwaje tena?

Mheshimiwa Spika, ijulikane kwamba hizi taarifa zilizopita ni za siku nyingi. Kwa sasa hivi Mbogwe tuko salama. Nimeikuta Mbogwe ikiwa na mapato ya Shilingi milioni 700 lakini kwa sasa hivi tuko kwenye bajeti ya Shilingi bilioni tatu. Kwa maana hiyo, kwa kifupi sisi tulipoingia tulibainisha na tukaazimia, kipindi hicho Waziri wa TAMISEMI akiwa dada yangu Mheshimiwa Ummy, anajua ripoti ile ambayo tuliazimia Baraza la Mbogwe. Kwa hiyo, nimeona nifafanue tu kwa kifupi hapo.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye asasi. Nimeangalia wanakamati wa Wizara hii pamoja na taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, wameongea kwa hisia kubwa sana. Rafiki yangu wa Magu jana nilimwambia usiwe na wasiwasi tiririka tu, nami huku naandika. Kweli nilikuwa naandika kabisa maana jambo hili ni kubwa. Jambo hili tukilifumbia macho litatuharibu. Naona aibu kufa kwenye meli ambayo naona inaenda kuzama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite kushauri, nimejumlisha hasara zote nikaona Shilingi trilioni 4,590 ni fedha nyingi sana ambapo nikifanya mgao kwa halmashauri zetu 184, tunaweza kujenga barabara kwa ile Ilani yetu yenye page 303. Tuna uwezo wa kujenga lami za kuunganisha Mkoa na Wilaya tukamaliza hiyo ahadi tuliyoitoa kwa kila Mbunge hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zimetajwa taasisi nyingi ukianza na ukurasa wa tatu, imezungumzwa TANESCO kwamba ililipa Dola za Kimarekani 153.43. Uki calculate kwa rate ya leo unapata karibia Shilingi milioni 360. Ukurasa wa pili huu imeonekana Shilingi bilioni 68 ambazo zimelipwa kupitia Shirika la Serikali hii TANROAD, kwa hiyo, naona aibu kwanza kuendelea kuwazungumza hawa watu kwa kuwa wameshazungumziwa na watu wengi, sasa nijikite kushauri tu.

Mheshimiwa Spika, kwa vile jambo hili umelileta kwetu tushauri kwa niaba ya wananchi na mjumbe hauawi, naomba kabisa uchukue hatua kikwelikweli. Najua hakuna Mbunge ambaye hataazimia kwa kitendo hiki kilichofanyika. Sisi sote humu tunapigiwa kura, kuanzia Waheshimiwa Mawaziri, huwa wanapitia kwanza kwenye hii michakato na baadaye wanateuliwa kuwa mawaziri huko. Kwa hiyo, katika maamuzi tutakayoyaazimia kesho, naomba tuungane kwa nia moja ili Taifa letu tuweze kulibadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kumvumilia mtu ambaye anakula kodi za wananchi. Nikiangalia nilikotokea jinsi wanavyolipa kodi wale wafanyabiashara wadogo, ni jambo la kusikitisha, lakini unaona hapa kuna wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi, wanategemea kesi zao ziishie Mahakamani na walishajua hizi sheria zetu ni dhaifu, niungane na mwenzangu Mheshimiwa Tabasam, kuna kila sababu hizi sheria kuziboresha ziseme kabisa vizuri mtu anapoonekana na makosa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nitakuwa labda nje sana, sheria hizi zinatakiwa zitaje, endapo mtu anaonekana ana makosa ya kuhujumu uchumi, pesa za watu wanyonge waliojichanga ili kuisaidia Serikali mtu akazitafuna, zitamke kunyongwa kabisa. Huyo mtu akionekana anyongwe ili watu waogope, kwa sababu sheria tulizonazo sasa hivi watu hawaogopi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeshuhudia Mawaziri wengi wanapiga kelele hata kwenye miradi. Unamwona Waziri anapiga kelele kabisa kwamba hapa hela zimepigwa, zimeliwa; akitoka Waziri, watu wanaendelea kula bia. Hata mimi mwenyewe Mbunge huwa najaribu kufuatilia sana; mimi ni mkali sana kwenye jimbo langu, maana najua likiharibika nimo mimi, itakuwa ni aibu ya hatari sana. Hawa wasomi walishasoma hizi sheria wakaona zina udhaifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali atusaidie Wabunge kwa hilo, tuziboreshe sheria zetu zizungumze vizuri. Hapa hazijazungumza vizuri kwa sasa hivi, tutakuwa tunapiga kelele tu Waheshimiwa Wabunge, mwisho tutaonekana wa ajabu, Bunge tunapigwa vita, Bunge la ajabu, halina maamuzi. Sijui tufikie maamuzi halafu watu wasichukuliwe hatua, tutakuwa wageni wa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya tumesema watu wakamatwe, hawakamatwi, tunakutana nao mitaani, wanatutukana; tuna watoto wana watoto, tufanye nini?

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Nikodemas Maganga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa Mheshimiwa Maganga kwamba Bunge lililopita, nadhani Bunge la Kumi na Moja, tulitoa maazimio humu ndani, Waziri wa TAMISEMI alikuwa Mheshimiwa Jafo, tukasema sheria ile inayolinda fedha za asilimia 10 ipo wazi. Mkurugenzi wa halmashauri yoyote ambaye atakusanya fedha halafu akashindwa kutoa asilimia 10 ya nne nne mbili achukuliwe hatua hapo hapo, kwa sababu fedha zitakuwa zimeshakusanywa naye amekula hizo hela, ajifute yeye mwenyewe kwenye cheo. Alizungumza Mheshimiwa Jafo humu ndani, lakini mpaka leo kuna Wakurugenzi mia moja na kitu wamekula hizo hela na wapo.

SPIKA: Mheshimiwa Nikcodemas Maganga unapokea taarifa hiyo?

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo ya baba yangu kwa mikono yote miwili. Tusifanye vitu vya kuchekesha. Huwa namwangilia Waziri Mkuu anavyofanya ziara kwenye baadhi ya Mikoa na Wilaya, yuko serious kweli baba wa watu, lakini kila akifanya maelekezo sijui kama wale watu huwa wanakamatwa na sijawaona sijui wako Magereza ya nani? Aliwahi kuja kwangu nikiwa bado sijawa Mbunge, nilikuwa mfanyabiashara tu, akatoa maelekezo. Alipotoka tu watu wakaanza kunywa bia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sheria zetu naomba ziseme kabisa. Kwanza zimlinde Waziri Mkuu, akisema kitu, hiyo ni Serikali, aheshimiwe, huyo ni msaidizi mkuu wa Rais. Haiwezekani kila siku tuwe tunazungumza mambo yale yale kama ndugu yangu alivyonipa taarifa. Hivi tunamaliziana heshima. Ndiyo maana watu wengine huwa wanaichukia sana siasa, maana sheria hizi hazijazungumza vizuri. Yaani Mbunge wa Tanzania ni kama mpiga debe wa stendi, ulishaona wapi? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumza haya maneno kwa masikitiko makubwa sana. Haiwezekani Mbunge anahangaika hapa Dodoma miezi mingi anapanga matrilioni, ukiangalia hata kwenye akaunti zao sidhani kama kuna Mbunge ana Shilingi trilioni moja kwenye akaunti yake huko. Leo ndugu zangu wa Kamati wamezungumza kwamba kuna KADCO, haijulikani ni ya nani? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwanza, Wabunge, Bunge hili liseme kabisa, kwanza kuanzia hao mliokuwa mnakaa nao kwenye kamati, waanze nao. Mii nilishawahi kushuhudia pale Kahama, anakumbuka Waziri Mkuu, mwaka 2020 kuna wafanyabiashara walikuwa wanapunguza sukari kidogo tu, tena robo kilo kila mfuko; walishughulikiwa na Mkuu wa Mkoa peke yake. Watu walikuwa na vitambi, mabilioneam wakaishi pale Magereza ya Shinyanga, discipline ikapatikana. Leo watu waliomo ndani ya Serikali hawakamatiki jamani! Haipo sababu sasa ya kutengeneza Serikali! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, namhurumia sana mama yangu. Jana nimeona tumesamehewa kama Shilingi bilioni 31, anajitahidi sana, lakini hizi fedha kama hazina ulinzi, pamoja na misamaha hii ambayo tunapewa na Mataifa, sisi wenyewe kama hatujisimamii, siku moja haya Mataifa yatatudharau, hayatatukopesha tena fedha. Kwa sababu tutakopeshwa na tutafika sehemu tusikopesheke, kila tunachokopwa kinaliwa. Wabunge tunarudi hapa hakuna kinachozingatiwa. Mwisho wa siku watoto wetu wataambulia nini? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiangalia ukurasa wangu wa pili hapa unasema mikataba sijui ilikuweje, TANESCO hapa, hii kampuni ya Symbion, hawa watu wote wakamatwe mara moja. Hili zoezi ni dogo sana, ila ukilikuza linakuwa kubwa, lakini zoezi hili linaweza likamalizwa na mtu mmoja, tena Waziri wa Mambo ya Ndani, hili suala lipo ndani ya uwezo wake. Mara moja tu akitangaza kesho waripoti Dodoma hapa, kwani shida iko wapi? Waripoti wenyewe kesho, tuone trilioni zetu zote hizi, tukajenge barabara, tukafanye na mambo mengine, maisha yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu ukomee hapo, nisije nikayarefusha sana mwishowe nitavuruga, maana nikiwa na hasira huwa nashindwa kuchangia vizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake kuweza kusimama mahali hapa na mimi niwe mmojawapo wa wachangiaji wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 13 Novemba, 2020.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Rais imegusia vitu vingi sana lakini kipo kitu kimoja ambacho wenzangu hawajakisema sana, mimi naomba niweke wazi. Nchi yetu kweli kila mmoja anatamani kwamba tuwe mabilionea lakini binafsi ninavyoangalia hatuwezi kuwa mabilionea kwa sababu ya tatizo la rushwa Rushwa imezidi, imepanda bei.

Mheshimiwa Spika, miaka ya 2000 mimi nilikuwa dereva, tulikuwa tunatoa rushwa kwenye mabasi shilingi 2,000, lakini toka mwaka jana mpandishe faini rushwa imepanda sasa hivi kwenye mabasi wanatoa shilingi 10,000 na kuendelea. Nitoe ushauri tu kwa mhusika, kama yupo ama hayupo lakini ananisikia; sioni kama anafanya kazi kumsaidia Rais kwenye upande wa rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile kwenye sekta ya afya hapa kuna tatizo kubwa sana kwenye upande wa afya. Mimi nazunguka sana kwenye mikoa hii ya Tanzania, kila ukipata tatizo ukaingia hospitali hizi dawa zinazosemwa tunazitoa bure hazionekani kiukweli. Naweza nikawa mlalamishi sana lakini ukweli uhalisia ndio huo.

Mheshimiwa Spika, nizungumze kwa ajili ya wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe ambao wengi wao ni kweli ni watu ambao hawajasoma na Wabunge wengi humu tumepigiwa kura na hao watu ambao hawajasoma. Hivyo sasa naishauri Serikali ione jinsi gani hawa wenzetu ambao wameishia darasa la saba, hawana CV, tunashirikiana nao vipi ili kuepusha migongano. Maana nikiangalia kwa hali ya kawaida kama vile wasomi wengi siyo waaminifu. Tukiangalia kwenye halmashauri zetu Serikali inapata hasara nyingi sana. Ukiangalia upande wa watu hao wa rushwa hawashughulikii ipasavyo, utakuta tu watu wanauawa kwa kuiba kuku, wizi wa ng’ombe, wameuliwa na watu wasiojulikana, sijaona Mkurugenzi hata mmoja amefungwa kwa ajili ya kuhujumu miradi ya Serikali. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea haya maneno nikiwa na experience kubwa sana. Leo ni miezi mitatu sasa mimi nikiwa Mbunge na nimejaribu kufanya operesheni kwenye jimbo langu nikaona matatizo yanatokea jimboni. Hivyo sasa nitoe wito tu kwa wahusika; kuna Waziri wa TAMISEMI, hata jana nilimsema lakini na leo naomba tu nirudie ili nishereheshe ili aone kabisa kwamba ni jinsi gani Wabunge wengine tunapata hasira.

Mheshimiwa Spika, Rais anataka tusonge mbele lakini huku sisi tukijitahidi kusimamia kama wasimamizi wakuu wa halmashauri mapato yanayotumwa juu na mapato yale ya ndani hayaonekani yanaenda wapi. Nikiangalia Jimbo langu mimi la Mbogwe ni jimbo lililo na rasilimali nyingi sana, ukiangalia mauzo ya Geita, dhahabu inayotoka Mbogwe ni nyingi sana. Kuna mapato yanayoitwa ya service levy, halmashauri yangu inabaki kuwa maskini na mimi mpaka sasa hivi najiuliza na mwanasheria wangu wa halmashauri, nimemwambia aangalie kifungu, tufuatilie kabisa mapato yetu ili halmashauri yetu iweze kupiga hatua. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge huyo ni Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, mtani wangu. Yeye anatakiwa akimaliza miaka mitano aandikiwe kitabu kwa sababu ni mtu ambaye ameanzia mbali sana kimaisha; ametuambia hapa aliwahi kuendesha mabasi ya abiria hadi Mbunge. Mnaona jinsi nchi hii ilivyo na rasilimali kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Maganga, endelea na mchango wako.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nilindie muda wangu usinikate, nina vitu vingi vya kuchangia hapa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye miundombinu, barabara mwanzoni zilikuwa zinashughulikiwa na Madiwani, mmekuja mkafanya mabadiliko mkazipeleka TARURA na mimi najitahidi sana kuwasiliana na watu wa TARURA naona jinsi gani hakuna kuwa supported wala kuambiwa kwamba kuna bajeti ya shilingi ngapi zilizopo kwenye akaunti.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ninavyoongea na wewe hapa ndani ya Bunge lako hili Tukufu barabara zangu zimekatika, Waziri Mkuu ni shahidi, waliwahi mpaka kunidharau sana mimi wakati wa kampeni maana barabara yangu moja ya Budoda ilikuwa haipitiki na mpaka sasa hivi haipitiki, kule kuna wananchi wengi sana na wanajifungua kila siku. Sasa ule mto wakitaka kuvuka waje Masumbwe wanasombwa na vifo vingi vimesababishwa na mto huu. Unaweza ukasema kwamba ni kitu cha kuchekesha lakini ni kweli na uhalisia wa vitu vilivyoko kule Mbogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna barabara zangu za kutoka Mponda, tumepakana na Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, barabara zile ni mbaya sana. Kila ukiwafuata TARURA ni watu ambao hawaeleweki kwamba tunazirekebisha au tunafanya nini. Mwishowe nimekuwa kero kwenda kwenye ofisi za TARURA mpaka na mimi naiona hii kazi ya Ubunge ni ngumu sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nilindie muda wangu, bado naendelea. Kwa maana hiyo naliomba Bunge Tukufu hizi barabara bora zirudi tu halmashauri ili hawa Madiwani na wao wawe wanawajibika na kutoa go ahead kwamba turekebishe hapa na hapo, kuliko kumleta mtu mwenye degree, engineer ambaye amesoma physically, hajaona practical na hataki kujifunza na wala hayuko tayari kuwasikiliza wananchi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri Mkuu, alikuja akaniombea kura na nimeshinda kwa asilimia…

SPIKA: Katibu, muongezee dakika tatu. (Makofi/ Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Waziri Mkuu alikuja kuniombea kura na nimeshinda kwa asilimia mia moja. Japokuwa siku ile ukiwa kwenye mkutano wangu unaninadi baada ya kusoma yale maelezo nilipingana na wewe maana mimi huwa ninasali, huwa ninajitahidi sana kutembelea kwenye neno la Mungu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nachotaka niliombe Bunge Tukufu, kwanza sisi Wabunge tuwe na hofu ya Mungu, unajua haya mamlaka tumeyapata kwa nguvu za Mungu. Wapo viongozi kabisa hata hii hotuba wanaipongeza tu na mimi nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa Rais wetu, watu wale wa karibu yake, ukitaka kumjua mtu angalia kwenye mawasiliano, anajua yule Waziri wa Mawasiliano ni nini huwa wanakifanya ili kumjua mtu mnafiki na mkweli. Wapo watu wakisimama majukwaani ni wazuri, wanampongeza kwa asilimia mia moja, huyu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kafanya mambo makubwa, moja, mbili, tatu, hivi na hivi Dkt. John Pombe Magufuli ni mtu mzuri lakini ukimfuatilia yule mtu unamkuta yuko kwenye connection za wizi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, watu wale kama wananifahamu wakitaka labda wanipeleke mahakamani mimi ushahidi ninao. Hata kama nikipoteza mwingine, Waziri wa Mawasiliano ni rafiki yangu, tutachomoa kwenye simu zao tutaangalia huwa wanaongea nini pale wanapoachana na Rais. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, suala lingine naomba kwenye halmashauri zetu hizi tutengeneze sheria za kuwa-limit Madiwani. Kuna Madiwani ni wazee, ni baba zetu na sisi Wabunge tulioingia awamu hii ni wadogo, wao ni wazoefu wengine wana miaka 20 wamo kwenye game. Walishazoea kuiba, hawapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.

Sasa sisi tulioisoma hii hotuba ya Mheshimiwa Rais, tunapokwenda na misimamo hii hii tunaonekana wabaya. Naliomba Bunge hili tukufu tutunge sheria ili tuweze kuwa- monitor wale Madiwani.

Mheshimiwa Spika, halafu kuna kauli moja wanaitumia, nilindie muda wangu, bado kama dakika nne. (Kicheko)

SPIKA: Waheshimiwa, namlinda Mheshimiwa, naomba tumpe nafasi. (Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, kuna msemo mmoja hata hapa Bungeni nimeusikia, ukitaka kufuatilia ile miradi iliyotekelezwa na Chama cha Mapinduzi 2015 mpaka 2020 ukitaka kufuatilia kwamba hili jengo limejengwa kwa bei gani wanakwambia wewe usifukue makaburi, subiria zile fedha zinazokuja ili uanze kufuatilia hapo. Mimi naliomba hili Bunge pamoja na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, najua kuna CAG pamoja na watu wengine na Mawaziri wahusika; tufukue makaburi term hii ili tuonekane tunamsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi namshukuru sana baba yangu mzazi ambaye anaishi kijijini, japokuwa napenda sana aishi na mimi lakini kwa uwezo wa Mungu na mapenzi ya watu wa Mbogwe niko hapa. Nakuomba tu endelea kuniongezea muda hivyo ili niweze kulisaidia taifa langu, hasa watu ambao hawajasoma wakapata vyeti lakini wana akili timamu na wana experience na wana uchungu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, namuomba Mheshimiwa Rais apime hata halmashauri 50 tu akiweka hata Wagogo na Wazaramo, sisi Wasukuma akituweka watasema kwamba kwa kuwa ni wa kwetu, aweke tu ninyi watani zetu ambao ni wa darasa la saba waende wakawe Wakurugenzi kwenye halmashauri muone zitakavyopanda hizo halmashauri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mara ya pili nimesimama mbele ya Bunge hili Tukufu kutumia nafasi hii kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nitumie neno ku-declare interest, mambo yote toka tumeanza kujadili Mpango binafsi nimeuelewa vizuri sana. Niwaombe tu Wabunge wenzangu wote ni vyema tumtangulize Mungu tunapokuwa tunaishauri Serikali tusiishie tu kulalamika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo sana, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja, mimi ni mkulima, mfanyabiashara pia ni mwanasiasa, naomba kwenye upande wa kilimo niishauri Serikali, ni vyema sasa wakulima tupatiwe vifaa vya kilimo kama matrekta, mimi natokea Wilaya ya wakulima pale Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kwenye upande wa biashara, wafanyabiashara tumekuwa na kilio kikubwa kwenye hili taifa la Tanzania. Mimi nilikuwa miongoni mwa wafanyabiashara East Africa Community lakini Watanzania tumefeli kufanya biashara na mataifa mengine. Kwa maana hiyo hii ajenda ni vyema Serikali iichukue kwa mapana na marefu sana, tumeshindwa yaani kila kona tumefeli, masoko yote sisi tunaonekana tuko chini. Chanzo kikubwa kabisa ni haya mabenki yetu ya ndani. Benki za hapa Tanzania riba zake ziko juu sana, ni tofauti na mabenki mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea suala la uchumi lina mapana na marefu sana. Mimi somo langu lilikuwa ni moja tu shuleni, ni uchumi peke yake. Kwa hiyo, tunapokuwa tunaongelea neno uchumi, kwanza uchumi umelenga sana sana kwenye mafuta, mimi nauza mafuta ya petrol na diesel, tukiangalia vizuri Serikali kwenye upande wa mafuta na tukiangalia mataifa mengine yanayotuzunguka bei ya mafuta ni ya chini sana. Kwa maana hiyo Serikali ikitibu kwenye tozo hizo za mafuta zikiwemo faini za EWURA milioni 20 kila kosa moja, tutasonga mbele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Geita ni wachimbaji, kwa kuwa Serikali inatuhakikishia kwamba imekusanya vya kutosha watupe vifaa vya kuchimbia. Sisi tuna elimu kubwa ya uchimbaji ila hatuna capital. Serikali ikituwezesha ikatupa vifaa vya kuchimba wenyewe na sisi tutaishi kwa raha na amani kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine ni elimu, kuna dada yangu pale alizungumza point sana, naomba nimuunge mkono, elimu yetu ya Kitanzania inamuandaa mtu kuwa maskini, tunaandaliwa kuwa waajiriwa. Leo Wabunge wote humu tukiangaliana mfukoni tumetumwa na watu wetu kuja kuwatafutia ajira. Kwa maoni yangu ninavyoona kabisa ajira karibia zote zimejaa, kwa hiyo, ni vema walimu wawe wakweli kuanzia kule shuleni. Nimpongeze Waziri wa Elimu kuna siku moja alitangaza kwamba atapima uelewa maana suala la vyeti walikagua watumishi wote ila kwenye uelewa hapo na mimi bado nafikiria sijui atatumia taaluma ipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa kabisa linalotufanya kurudi nyuma kwenye hili Taifa letu la Tanzania ni kule kutokujituma katika kazi. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na ndugu zangu wote mnaonisikia, tunao ugonjwa Tanzania hapa wa kutokufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu amekuwa ni jemedari mkuu akituhamasisha tufanye kazi. Tatizo kubwa sisi ni wepesi wa kuridhika, tukipata tu hizi posho kidogo na mishahara hii ya Kibunge tunaziacha kazi za msingi za kuweza kutuingizia maarifa na kutuzalishia mali nyingi. Kwa hiyo, niwaombe Wabunge wenzangu sisi ni vyema tukawe kielelezo kwenye jamii tukafanye kazi hata hivi viwanda tunavyovisema na kilimo tukaanze sisi Wabunge kulima ili Taifa letu liweze kupata manufaa. Hata maandiko yanasema sisi viongozi ni barua tunasomwa na watu wote. Kwa maana hiyo tukifanya vizuri kanzia sisi Wabunge na wale tunaowaongoza watatufuata.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imegonga.

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ila muda haujatosha, nitaleta mchango wangu kwa maandishi, ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kuweza tena kupata nafasi hii ya kuweza kuongea yale aliyokuwa akiyafanya marehemu, baba yetu John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru Mungu, ninamshukuru Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi, Mungu amuweke mahali pema peponi. Kweli haikuwa rahisi kwanza mimi binafsi kuweza kufika kwenye Bunge hili tukufu maana ilikuwa kazi ngumu sana, lakini kwa uwezo wa Mungu na uwezo wake kwa juhudi zake Mheshimiwa nikaweza kufika hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge; tarehe 27 mwezi wa pili wakati akitoka Chato Mheshimiwa Rais alipita Jimboni kwangu Mbogwe, aliacha ahadi sitazisahau daima kwenye maisha yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge tarehe 27 mwezi wa Pili wakati akitoka Chato Mheshimiwa Rais alipita Jimboni kwangu Mbogwe, aliacha ahadi sitazisahau daima kwenye maisha yangu. Jimbo la Mbogwe ni Jimbo moja katika majimbo ya Kanda ya Ziwa lilikuwa limesahaulika sana katika awamu zilizopita zote zile nne, hatukuwa na lami, hatukuwa na taa barabarani, lakini Mheshimiwa alipita akatoa ahadi mbele za wananchi na mimi nilipata fursa ya kuongea na wananchi zaidi ya elfu tatu nikimwambia ukweli jinsi ulivyo katika Jimbo na matatizo ya Jimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wiki moja tukamwona mama yetu anatangaza kifo cha Rais wetu, kweli tulipokea kwa masikitiko makubwa. Kwa kawaida sisi asili yetu Wasukuma huwa sio wepesi wa kuamini jambo, hatukuamini yale matangazo ya kwanza na kwa kuwa kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge tuko tofauti tofauti katika Imani, wale wenzetu ambao hawajamwamini Mungu walikataa kabisa, Wasukuma wale wa Kanda ya Ziwa kwamba haiwezekani huyu bwana afe, maana ilikuwa haijawahi kutokea siku moja ameonekana akiwa na malaria au akionekana akitibiwa popote pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mlivyokuwa mnaona Waheshimiwa Wabunge mitandao ilivyokuwa iki-tweet, kuna mtu anaitwa Kigogo, walikuwa wakisoma sana wananchi wangu hasa wa Kanda ya Ziwa wakihakikisha kwamba huyu jamaa wanamsingizia, ila kwa leo naomba niwape tu neno moja Yohana 14:1 ambalo inatutia moyo sote Watanzania bila kujali itikadi zetu na niwaombe tu baba zangu na mababu zangu wale ambao bado hawajamwamini Mungu tukubaliane tu kwamba hii hali imeshatupata na imeshatokea hakuna haja ya kufikiria wala kudhania kwamba labda tutazama. Tanzania naifananisha kama safari ya wana Israel wakati Musa akiwa anawatoa kwenye nchi ile ya shida, aliinuliwa mtu mmoja Yoshua na niseme tu kwa sasa hivi dhahiri kabisa, mimi Mama Samia kiukweli nilikuwa sijamfahamu kivile maana nilikuwa ni mfanyabiashara kazi yangu ilikuwa nikukaa ofisini nilikuwa sifuatilii sana mambo ya siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa Hotuba yake ile ya kwanza tu ya kusema kwamba maumbile yangu ni ya kike imenipa moyo sana na kuzidi kuipenda siasa. Naamini sasa kumbe hata huyu aliyeingia ni mashine ile ile, ni kutwanga na kukoboa. Kwa maana hiyo niwaombe Waheshimiwa Wabunge huu sio wakati wa kampeni, ni wakati wa kufanya kazi kama jinsi Rais alivyokuwa anatunadi kwenye majukwaa kwamba, kuisimamia Ilani yenye page 303, kuna kazi ambazo zimeainishwa mle, tusiwasahau wananchi wetu waliotufanya kufika huku. Nimeona niwakumbushe tu hilo maana tunaweza tukawa tunasema Katiba labda tukiibadilisha tunaweza tena kushindwa kufika mjengoni, matendo yako ndiyo yatakayokufanya kuja huku au usije kabisa huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo niseme, wewe ni mwanamama vilevile na Rais wetu sasa hivi ni mwanamke, nami nina watani wengi sana hapa Wagogo niwatanie tu kidogo kwa kusema, mtutendee haki sisi wanaume hasa Kanda ya Ziwa, tulishazoea kuoa wanawake wengi sana na nimeangalia mfumo wa Katiba huu kumtambulisha mwanamke ni mmoja tu hapa Bungeni na sisi Wasukuma tunaoa zaidi ya wanawake 10, kwa hiyo kuna kila sababu ya kuifanyia marekebisho hiyo Ibara ili kusudi mwenye wake 11, watano au watatu waweze kutambulishwa kwenye Bunge lako hili Tukufu ili wapate haki zao za msingi na wao ni binadamu. Pia kama mnavyoisoma sayansi wanawake ni wengi wanaume tuko wachache, japokuwa unaweza ukawa wewe una mume mmoja ukawa unaumia sana lakini naongea kwa niaba ya Watanzania ili tusijifiche fiche sana; na kwakuwa akinamama sasa hivi wanasema sasa tayari tumeshawapa rungu wasilitumie rungu lao vibaya ili tukashindwa kuwarudisha tena madarakani miaka ijayo, miaka 2025 na miaka mingine. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Makamu kwa Hotuba yake ya mchana aliyoiongea hapa, yeye kwanza amejitambulisha ni mtoto wa maskini na hasa maskini wanakuwaga na akili nyingi sana kuliko watoto wa matajiri. Kwa maana hiyo atumie hekima na busara sasa kuhakikisha kwanza Chama chetu cha Mapinduzi anatupa heshima ili tuweze kurudi tena humu Bungeni kiurahisi. Wabunge wengi wakipata madaraka pamoja na Waheshimiwa Madiwani na viongozi mbalimbali kupitia vyama huwa wanakisahau Chama. Kwa maana hiyo maneno yake yale aliyoyaongea mchana akiyaishi na sisi tukatembelea mlemle, hata kama utokee upinzani wa namna gani tutashinda tena kwa wingi na Watanzania wana imani na sisi sana hasa Chama cha Mapinduzi na mimi kweli imani imezidi kabisa kuongezeka kwamba hiki Chama kweli kiko imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikimwangalia Waziri wa Mambo ya Nje yuko imara, Waziri wa Mambo ya Ndani yuko imara, kwa maana hiyo tusonge mbele kuhakikisha tunalinda rasilimali yetu na heshima ya Taifa letu, asitokee mtu akaja tena kututapeli kwa maneno ama kwa njia moja ama nyingine maana watu wa shetani wamejaliwa kuwa na maneno matamu sana, kama alivyosema Mheshimiwa pale kwamba sasa hivi tuachieni vyama, kweli watu wale wakiachiliwa wana maneno matamu na shetani alikuwa na maneno matamu vilevile hata Edeni pale alipomsogeza Eva akamdanganya Eva kula tena tunda ambalo halina matunda mazuri tukaingia kwenye dhambi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo Watanzania tusiingie kwenye maneno ya kushawishiwa kama vile Eva alivyoshawishiwa Eden tukahukumiwa mwishowe tukaambiwa kufa tulikuwa hatufi lakini mpaka leo tunakufa. Kwa kukiamini Chama hiki cha Mapinduzi, lakini vilevile na sisi Wabunge tuko imara tuna uwezo kabisa wa kufanya chochote kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikutoe wasiwasi tu sisi Wabunge wa awamu hii kiukweli kama ni timu ilikuwa imekuwa sorted, tuko tayari kwa lolote lile na ukitaka kujua Uchaguzi mdogo ule uliotangazwa mchana mimi naomba mnitume Buhigwe huko nikapambane na watu wa upinzani wenye maneno mabaya. Kwa maana mimi walinifundisha nazijua siasa za aina yeyote ile, siasa za matusi, siasa za kistaarabu, siasa za maombi, siasa za aina yeyote ile tutaenda kulipigania Jimbo la Mheshimiwa Philipo Mpango kuhakikisha kwamba linarudi kwenye Chama hiki pamoja na marehemu yule wa Kigoma sijui Jimbo gani, hivi alitokea jimbo gani? Nalo tutahakikisha linarudi kwenye Chama cha Mapinduzi. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu Chama changu cha Mapinduzi uteuzi uliofanywa na Mama yangu Rais, umefanywa kila mtu kweli ameunga mkono hakuna mtu aliyepinga, maana amechagua chombo ambacho kinakubalika mbele ya Mungu na mbele za wanadamu ndiyo maana hakuna kura iliyoharibika. Wakiendelea kufanya hivyo hata kwenye kura za maoni kuchagua mtu anayetakiwa na Mungu maana uchaguzi wa Mungu mwanadamu hawezi akaushinda lakini….

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Nakushukuru sana, naiunga mkono hoja ila naomba Serikali iendelee kutusaidia zile ahadi za page 303, zitekelezeke ili turudi kwa urahisi huku. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kupata nafasi ya kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuletea mpango huu tuujadili hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nipo kwenye Kamati ya Nishati na Madini, tarehe 12 tulifanya ziara kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere Rufiji, ule mradi unaenda vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia, huu maradi umeanza mwaka 1970. Nitumie tu muda huu kuishauri Seikali. Kweli tuna miradi mingi katika Mpango huu wa Taifa, lakini ipo miradi ya kuipa kipaumbele ikaweza kwisha kabla nasi tukiwa hai duniani tukafaidi matunda yake. Simaanishi kwamba labda miradi mingine ninaipinga, hata yenyewe ni mizuri, ila nikiangalia pato letu kwa Taifa la Tanzania, kwa mfano hii SGR ina gharama kubwa sana. Tunaweza tukajikita kule tukafeli kufikisha malengo na mwishoni tukaonekana tu, watu wa ajabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri aliyewasilisha huu mpango, kwa kuwa wewe ni mzoefu sana ndani ya hii Serikali, leo tunajadili huu mpango, tunapitisha mabilioni na matirioni yaende tena kwenye mipango, ila nikiangalia ripoti ya CAG hapa kwenye usafiri wa anga kwamba tuna short ya shilingi bilioni 150, kiukweli kwa mtu mwenye akili timamu, yaani inatia uchungu na inaumiza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia kwenye ili Taifa kuna watu wengine wanafanya kazi bure. Tukishuka chini huku Serikali inapoanzia kwa maana ya Vitongoji pamoja na Wenyeviti wa Serikali wa Kijiji, mimi Pasaka hii sikuila, nilikuwa nafanya ziara kwenye jimbo langu. Ukikaa nao wale watu, madai yao ni ya msingi sana. Hawalipwi mshahara, hawana posho yoyote, wanafanya kazi kubwa za Kiserikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye huu mpango nimeangalia, Mheshimiwa kaka yangu Waziri wa Fedha ni vema ungewaingiza hawa watu ili nao wapate haki yao ya msingi maana wanafanya kazi kubwa sana na wanaumia sana. Japokuwa hawana uwezo wa kuingia ndani ya hili Bunge Tukufu na kuzungumza mawazo yao, wanapoona watu wakubwa wanaleta hasara kwenye hili Taifa, kwa mfano shilingi milioni 150 wakati Watanzania wote tunafurahia sana uwepo wa usafiri wa anga, lakini pale inapoonekana loss yaani hapa ni lazima tukae vizuri tujiulize.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana CAG huyu aliyetoa hii ripoti, maana imetupa dira. Ninamwomba au nawaomba ma-CAG wote, hata tunapopitisha haya mabilioni yaweze kuwa na udhibiti. Nawapongeze Baraza la Mawaziri kwa kuaminiwa tena na Mheshimiwa Rais, maana wengi walikuwa wana-vibrate baada ya hili tukio kubwa tuliyolipata Kitaifa kwamba wengi labda wanaweza wakakosa nafasi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri, sisi Wabunge tuna kazi ngumu sana. Tunapofanya ziara kwenye majimbo yetu tunabaini changamoto na tunawaleteeni, kuna baadhi ya Mawaziri hawatujali vile, tunabaki sasa hatuna majibu na ukiangalia watu wanahitaji kupatiwa majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sehemu nyingi ambazo zinachangamoto kwa mfano Wizara ya TAMISEMI; nampongeza tu dada yangu kwa kuteuliwa, lakini ile sekta ni muhimu sana kwenye jamii, maana vitu vingi vinalenga TAMISEMI. Zipo changamoto Serikali kabla ya mimi kuwa Mbunge ilikaa ikapitisha bajeti kama leo tunavyopitisha mpango huu. Fedha zilienda zikaliwa, watu hawajawahi kuchukuliwa hatua hata siku moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naiomba tu Serikali, hilo iliangalie kwa umakini sana na ichukue hatua haraka iwezekanavyo. Siyo sifa nzuri, wala siyo Uislamu wala Ukristo; kwa mfano, mtu anaonekana kabisa amehujumu fedha za walipa kodi ambao ni wafanyabishara wadogo wadogo, wanachangia kwenye pato hili la Taifa, wanajibana kununua hata nguo, halafu mtu mmoja tu au wawili wanakula pesa za wananchi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko mitaani kiukweli kuna shida kubwa sana. Hata kusema kwamba tuko katika uchumi wa kati, yaani mpaka inafikia wakati mwingine ukiangalia hali iliyoko mitaani jinsi ilivyo mbaya, unaona dhahiri kabisa kwamba sijui walitumia takwimu gani? Unashindwa kujua kwa vile huna elimu ya kuweza kudadavua mambo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa huu siyo wakati wa kampeni, naiomba Serikali, nawe Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni mzoefu na haya mambo ya uongozi, ufanye sasa ile gear uliyokuwa unatumia hata miaka yote ili kusudi hata wenzetu hawa wa maisha ya kawaida waweze kupata maisha rahisi mifukoni. Mshauri Mheshimiwa Rais ili kusudi wananchi wetu wadogo wadogo wawe na pesa kwenye mifuko yao. Sasa hivi huko mitaani hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaongelea viwanda; tuna viwanda 4,460 na kitu, lakini kiukweli hali ni mbaya. Hata wapiga kura wetu waliotupigia kura wana hali mbaya. Tuliahidi barabara; naishauri Serikali tuelekeze nguvu nyingi kwenye miundombinu za barabara na kwenye miundombinu za maji. Kwa mfano mimi natokea Jimbo la Mbogwe. Kutoka ziwa Victoria kufika pale kwenye jimbo langu ni kilomita 80. Nimeangalia huu mpango, hakuna mahali panaonekana kwamba ni lini wananchi wa Mbogwe watapata maji kutoka pale kwenye Ziwa Victoria kwenda pale kwenye jimbo langu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida kubwa sana ya maji, hasa Mbunge unapokuwa msibani, unalazimika unywe maji na baada ya kumaliza kuyanywa, unaenda tena unaugua na unatumia gharama kubwa kutibiwa typhoid pamoja na magonjwa mengine. Kwa hiyo, naiomba Serikali, yaani mpango huu, sawa tunauunga mkono, lakini i-sort vipaumbele muhimu kama vile maji ni kitu cha muhimu na afya. Kuna upungufu mkubwa sana kwenye hospitali, dawa hakuna kabisa kiuhalisia pamoja na vipimo. Kwa mfano pale Mbogwe kwangu, ninamshukuru Waziri wa Afya amefika amejionea hali iliyopo pale Masumbwe. Akina mama kila siku wanajifungua, lakini hakuna X-Ray, hakuna vipimo vya kumpima mtu kubaini kwamba ana shida gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vyema sasa tunapopitisha huu mpango, lazima vitu vingine tuvipe vipaumbele, maana ni muhimu kulika hii SGR pamoja na mambo mengine ya matrilioni na matrilioni ambayo hayana sababu kwa wananchi wetu wale wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi nyingine ni hii ya kilimo. Toka mwaka 1992 nikiwa mdogo, Serikali ya Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, wakulima walikuwa wakipewa mbegu za pamba. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ukifanya huo mpango kwa wakati huu, wakulima wakapata pamba, tutakuwa tumelisaidia hili Taifa. Waheshimiwa Mawaziri mwangalie, unajua sasa hivi tuna nafasi hizi, lakini ipo siku tunaweza tukafungwa pengine kwa kupitisha hii mipango halafu inakuwa haina mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimeshuhudia Serikali ya Rwanda, kuna Mawaziri wamefungwa pale. Walikuwa wakipitisha hizi bajeti zinaenda ndani ya watumishi wa Serikali zinaliwa, hawafuatilii, wanarudi Bungeni tena kujadili, wanatuma tena mabilioni mengine yanaenda, lakini baadaye ufuatiliaji unakuwa haupo, halafu mnarudi Bungeni hapa hapa kupitisha tena bajeti nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mwaka 2015 mlipitisha bajeti, lakini ile miradi haijakamilika na haina kiwango, lakini fedha zilienda na hakuna majibu. Namwomba Mheshimiwa Rais, kasi aliyoanza nayo asilegeze, aendelee hivyo hivyo. Japokuwa anashabikiwa sana na watu, wengine sio wazuri sana kuwaongelea hata hapa. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ukiona unashabikiwa sana hata jimboni, lazima usimame ufikirie, ni kwa nini wananishabikia sana kila mtu? Kuna wengine wanakushabikia ili ukosee kusudi wapate pa kupitia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua tuko kwenye siku za mwisho, lipo hili janga la corona, watu wanapata shida. Ukiangalia Kenya pale, wananchi sasa hivi wanalia, Serikali ilikopa matrilioni na mabilioni, kumbe sijui hata ugonjwa haukuwepo, sasa hivi wananchi hata wale wa kawaida wanachangia lile deni kulilipa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Rais aangalie kwa umakini sana, anapoona anashabikiwa sana na watu, lazima afikirie kwamba hawa watu wanaomshangilia wana heri au wanataka kutuingiza kwenye matatizo kabisa ambayo hatutayamaliza tena? Afuate tu nyayo za Mheshimiwa Rais, siyo lazima afuate zote, ni kuchambua.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua Marehemu akifufuka hata leo akakuta hii ripoti kwanza iliyotolewa juzi hii ya ndege, siyo kweli Marehemu alinunua ndege hizi kusudi zile short, alinunua ili afanye biashara. Hawa watu waliosababisha hiki, wanatakiwa kuchukuliwa hatua. (Makofi/Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge, msicheke. Sisi tunaolipa kodi wenye mitaji ya kuungaunga hatukubahatika hata kuwa na elimu za juu sana, tunajua uchungu na tuna uchungu mkubwa sana na tumekuja humu ndani ili kusudi kuweza kukabana nao hawa wanaojiita wana cv na degree. CV zisitumike kwa ajili ya kuibia watu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waendesha bodaboda wana viparata wanalipa shilingi 20,000. Ina maana vyote vinaingia huku Serikalini, halafu inapoonekana shilingi bilioni 150 amekula mtu mmoja, halafu anabaki tu ana- survive, yaani tuwe serious ili nchi yetu ilete mabadiliko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi kwa siku ya leo tena ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Nimeisoma hotuba ya Waziri Mkuu Mpango wa Bajeti mwaka, 2022/2023 kweli imekaa vizuri sana. Hivyo sasa, nitumie nafasi hii tu kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama alivyokusudia kwenye malengo yake aweze kutufanyia kazi Watanzania.

Nimeangalia katika ukurasa wa 22 amezungumzia Mahakama ambazo zinakwenda kujengwa katika Taifa letu, ikiwemo na Wilaya yangu ya Mbogwe. Kweli nauunga mkono huu Mpango kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kuchaguliwa kuwa Spika wetu wa Bunge Tukufu pamoja na Baraza la Mawaziri wapya pamoja na Manaibu wale waliochaguliwa kwa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sasa kutoa mchango wangu kuiomba Serikali, wajaribu kuzingatia hao Mawaziri waliochaguliwa kufuatilia zile kumbukumbu. Wale Mawaziri waliokuwepo kwamba, kuna ahadi ambazo walizitoa kwenye Majimbo yetu kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wetu. Vile vile, niombe kuwasilisha mawazo ya wengi wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe wananipenda sana na wamenituma kuja kuyasema mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kweli yapo mengi yanazungumzwa na hayana budi kuyakwepa kuyazungumza mahali hapa, maana sisi ndio washauri wa Serikali. Ugumu wa maisha unaongoza sasa hivi mitaani na ugumu huu wa maisha kiukweli kama alivyotangulia kusema Mheshimiwa Iddi hapa, unachangiwa na issue ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, naomba ku-declare interest tu kwamba mimi ni muuza mafuta japokuwa alitaka kuliweka vibaya sana lakini wewe ukalinyoosha vizuri, kwamba, asitunyime kutoa mawazo yetu japokuwa kwamba sisi ni wadau wa sekta hizo, tuishauri vizuri tu Serikali ili kusudi kila mmoja aweze kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, tumekuwa tukishauri hata kwenye Kamati, kwamba, vipo vyombo vya Serikali ambayo vinachangia kumuumiza mwananchi. Ukiangalia EWURA ina masharti mengi sana na tumeshashauri huko kwamba, wabadilishe miongozo ili watu waweze kufungua vituo vya mafuta vijijini. Leo kwenye Jimbo langu kuna baadhi ya sehemu mafuta yanauzwa mpaka Sh.5,000/= kwa lita moja sio Sh.3,000/= peke yake. Sh.3,000/= ni kwa wale walio na vituo vya mafuta, lakini yakiingia kwenye makopo kwa wananchi walio wengi ambako hakuna huduma za petrol station wanauza wanavyotaka wananchi hao. Kwa hiyo, kuna kila sababu tuiombe Serikali iliangalie upya na ilete miongozo hiyo haraka sana, tuifanyie mabadiliko, watu waweze kufungua vituo kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwenye upande wa barabara hapa, wananchi wanatamani sana kuona barabara zinatengenezwa kila mahali. Jimbo langu la Mbogwe ni kubwa lina kata 17 na kila kata ina barabara za msingi, zinaingiza pato la Taifa pamoja na pato la halmashauri. Jimbo langu linahitaji kuongezewa bajeti ya TARURA ili kusudi Meneja wangu wa TARURA, aweze kurekebisha barabara zinazotakiwa kurekebishwa kwenye hiyo Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, wananchi wanahitaji kuona umeme unatengenezwa kwenye maeneo yao. Vipo vijiji ambavyo bado havijawekewa umeme na tumekuwa tukiongea kila wakati humu Bungeni kwamba umeme sasa hii awamu iende kukamilika.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne, wananchi wanahitaji kuona maji kwenye maeneo yao. Wananchi kiukweli hawana mambo mengi sana pamoja na kwamba, mipango ni mingi sana ya Serikali, lakini naishauri Serikali iangalie vitu vya msingi tu vichache, vitatu ama vitano ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu waliotuweka madarakani. Kwa sasa kwa kweli hali ni ngumu sana, uchaguzi ungekuwa ni kesho au keshokutwa, tulikuwa na asilimia chache sana ya kurudi humu Bungeni maana hali ni mbaya. Ukiangalia wananchi kiukweli mtu wa kwanza wanayemlalamikia ni Mbunge na wanatufuatilia sana na wanatuangalia kwamba, Mbunge wetu anaishauri nini Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la Nne wananchi wanahitaji kuona maji kwenye maeneo yao. Wananchi kiukweli hawana mambo mengi sana pamoja na kwamba mipango ni mingi sana ya Serikali, lakini ninaishauri Serikali iangalie vitu vya msingi tu vichache, vitano ama vitatu ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu waliotuweka madarakani.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa kwa kweli hali ni ngumu sana, uchaguzi ungekuwa ni kesho au keshokutwa tulikuwa na asilimia chache sana ya kurudi humu Bungeni maana hali ni mbaya. Ukiangalia wananchi kiukweli wanamlalamikia mtu wa kwanza ni Mbunge na wanatufuatilia sana wanatuangalia kwamba, Mbunge wetu anaishauri nini Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi nitumie nafasi hii kuishauri Serikali ione namna gani mwananchi anaenda kumpunguziwa ugumu wa maisha. Tukiangalia mfano Serikali ya Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne tulikuwa tuna vyanzo vingi, hapakuwa na tozo lakini maisha yalienda. Hapakuwa na tozo kwenye mafuta na kwenye miamala, lakini watu waliishi kwa raha mustarehe, leo hii tuna ndege, tuna meli kwenye maziwa yetu huko pamoja na bahari yanaingiza kwenye Pato la Taifa.

Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ikae ifikirie wananchi hawa kulingana na kilio kwa vile ngoma ikilia sana hupasuka, maana kilio ni kikubwa sana. Kila kijiwe ukikaa unakuta watu wanaliongelea hilo tu kwamba maisha yamepanda sana, maisha yamekuwa magumu sana, nauli imeongezeka kutoka shilingi 1,000 mpaka shilingi 5,000 ukiingia kwenye huko kwenye Wilaya zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali ilione hilo kama jambo la msingi sana ili kuwasaidia wananchi hawa waweze kuishi maisha mazuri.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine hapa ninaiomba Serikali kwenye Wilaya yangu sina chuo cha VETA. Na ukisoma kwenye ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi tuliinadi kwamba, kila Wilaya itakuwa na Chuo cha VETA. Niiombe Serikali sasa ione namna iweze kunisaidia kwenye Jimbo langu kupata chuo cha VETA.

Mheshimiwa Spika, pia jambo linguine ni taa za barabarani. Kwenye kampeni tulikuwa tukinadi kila patakapojengwa lami kutakuwa na taa za barabarani. Kwangu sina taa za barabarani na Mji wangu unakua kwa kasi sana wa Mbogwe na Masumbwe. Kwa hiyo, niiombe Wizara inayohusika na haya mambo waweze kunisaidia wananchi wangu wapate umeme na waondoke gizani ili waweze kunufaika na utawala huu tulionao wa Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine, nikuombe wewe uendelee kutulinda tu sisi ni vijana wako ni wageni humu ndani. Twaweza kuwa tunakukosea kweli, maana hatukusoma chuo kuja kuwakilisha watu humu, kila mtu na lafudhi yake. Kwa mfano, mimi lafudhi yangu inaeleweka ninaweza nikawa ninazungumza kama kwa ukali sana, lakini kumbe ndivyo nilivyo tu. Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa niweze kusikilizwa na niweze kusaidiwa vizuri sana pale ninapochangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu, ukurasa wa 36, amezungumzia issue ya pato la madini. Niiombe Serikali sasa iangalie haya mapato yanayokusanywa kwa wingi kuna sehemu Serikali haiwezeshi. Wachimbaji hawa wadogo hakuna fungu ambalo limetoka Serikali Kuu kama zinavyofanya sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kilimo wanatoa matrekta, wanakopesha matrekta, lakini wachimbaji wadogo ambao hatujawasaidia hawa na wanafanya vizuri ni vyema wakatengenezewa miundombinu angalau ya barabara kwenye migodi yao.

Mheshimiwa Spika, ipo migodi inayozalisha kila siku, lakini haina miundombinu ya barabara, hakuna vituo vya afya kwenye maeneo yale. Dada pale amezungumza UKIMWI unaenea kwa kasi kubwa sana Kanda ya Ziwa, ni kweli watu wanaishi kwa shida, lakini ukiangalia tozo ambazo zinakusanywa ni nyingi na suala hili tumeshalishauri kwenye Kamati. Ninakuomba tu Mheshimiwa Waziri Kaka yangu na umekuwa Waziri wa mfano wa kwanza, maana katika makusanyo nimeangalia kabrasha huko Mawaziri waliopita hakuna Waziri ambaye amewahi kukusanya Bilioni 528 kama mwaka jana, sasa hivi imefika Shilingi Bilioni 400.6 ina maana unaonesha jinsi gani ulivyo mwaminifu Kaka yangu, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe kwa vile wewe unakaa na Rais mwambie kabisa ukweli kuanzia wewe mwenyewe unatokea sehemu za machimbo, una mgodi wa namba moja, namba saba, hakuna miundombinu ya kutosha kwenye maeneo yale, lakini wananchi hawa ni waaminifu wanaingiza pato la hatari kwenye Taifa, aone fungu ili kusudi aweze kutusaidia wachimbaji wetu wapate manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo naomba nikomee hapo ili Serikali sasa iweze kutusaidia tuweze kuishi maisha mazuri na yenye raha. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu ambayo ina page 95, imegusa maeneo mengi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza napenda nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo anayonipa ushirikiano kwenye Jimbo langu la Mbogwe na ikumbukwe tu tarehe 8 Aprili, nimefanya Mkutano pale Kata ya Ilolangulu Kijiji cha Nyashinge, nimepokea malalamiko mengi ya wananchi yanayoishutumu Serikali. Hata hivyo, nimpongeze Rais maana amekuwa ni Rais wa mfano katika Jimbo la Mbogwe. Mbogwe ilikuwa haijawahi kutengenezewa lami, lakini kwa awamu yake tumepokea lami kilomita tano. Mheshimiwa Rais ametu-balance hata kwenye upande wa maji japokuwa kuna maeneo mengine bado hayajaguswa, nizidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Mama yangu aendelee kuwa na moyo wa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametupatia miradi ya umeme pamoja na mambo mengi luluki. Wananchi wangu walikuwa na njaa ya kufa mtu, niishukuru Wizara ya Kilimo nilikuwa nikilia wananisaidia, Mheshimiwa Bashe Mungu amlinde sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukurani hizo, sasa uniruhusu kidogo nijaribu kuingia kwenye ilani yetu ambayo ni mkataba wetu na wananchi waliotuchagua.

Mheshimiwa Spika, neno la Mungu linasema “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. Hapo nipo kwenye maandiko kwanza bado sijaingia kwenye ilani. Ukisoma ukurasa wa 52, unaelezea bayana kwamba wananchi tuliwaahidi nini? Wizara ya Ardhi tulipanga kwamba tutatenga hekari milioni sita kwa ajili wananchi kuchungia ng’ombe pamoja na kilimo. Leo naweza nikasema kwamba haya maswali yanaulizwa sana na wananchi. Ni wapi ambapo tumetenga hasa eneo langu la Mbogwe? Kwa vile Mawaziri wapo sasa wawe makini ili waweze kunijibu huko mwishoni na uzuri Waziri wa Maliasili anakuja kuingia ajipange sasa kuja kunijibu kama anavyonifahamu kaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mbogwe wanapata tabu kwenye mapori. Sheria zinasema mita mia tano, ukisogea mita mia tano ng’ombe wanataifishwa, lakini hapa tuliwaahidi wananchi kwamba tutawatengenezea maeneo na wanifundishe sasa kwa vile hili suala liko kiilani halafu mpaka sasa hivi bado hawajatenga maeneo wananitakia nini mimi Mbogwe?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nigusie kidogo sheria zetu ambazo tumezipitisha hapa Bungeni, zimekuwa zikileta mkanganyiko mwingi kwa wananchi. Lazima Serikali tuishauri vizuri. Ukiangalia Sheria za Madini zinasema mtu anaweza akaomba kwenye mtandao akapatiwa leseni hata kama kuna nyumba. Suala hili kwa vile yananitokea na ninayaishi, yameleta mkanganyiko mkubwa sana kwa wananchi wa Mbogwe. Ukiangalia Kata ya Kanegele migogoro ni mingi Bukandwe pamoja na Masumbwe, wananchi wamekuwa wakilia sana. Mbaya zaidi hawa wawekezaji pale wanapozipokea hizi leseni hawasomi Sheria zinasemaje. Wanaingia na Mapolisi, wanafukuza watu, hawalipi fidia, wanajali masilahi yao, matokeo yake hii nchi inakuwa kama vile imepoteza mwelekeo.

Mheshimiwa Spika, tukikumbuka enzi za Mwalimu Nyerere aliishi vizuri na watu, aliwasikiliza wanyonge. Tunatambua sera yetu ni kukaribisha wawekezaji, lazima tufikirie hawa wawekezaji wanaoingia ni wazuri kwetu au ndio watatutoa madarakani? Tatizo hili hata Chunya, Mbeya lipo, maeneo yote yaliyozungukwa na migodi yanasumbua watu sana. Nikuombe wewe ni bosi wetu hapa Bungeni, utoe maelekezo ikiwezekana kuanzia kwenye Kamati zetu ili tuziangalie upya. Hii sheria inakinzana sana na wananchi wanyonge wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niongezee hapohapo na Mawaziri, tuna Baraza la Mawaziri 24 lazima tuangalie vizuri, hawa Mawaziri wanamsaidia kweli Mama hawa?

Lazima tuwaangalie hawa Mawaziri 24, wanamsaidia Mama au wanaendesha V8 halafu wanakalia kusema Mama anaupiga mwingi? Wananchi wa kawaida waliumia sana juzi wakati Mama anakabidhiwa ripoti ya CAG, kauli aliyoitumia ni lugha ya Kiingereza, alisema stupid! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais ni mtu mkubwa sana kufikia kusema neno pumbavu na mtupishe wakati kuna watu wake wanaomsaidia, ina maana wao hawaoni matatizo haya, hata kama matatizo haya yanafanywa na wataalam. Kwa nini Mawaziri wasichukue hatua mapema? Mwishowe hili suala mbona linatugharimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaombe Mawaziri, sina bifu na ninyi na wala sijaja kutafuta ugomvi hapa, hebu kila mmoja ajitathmini kwenye nafasi yake anamsaidiaje Mama hasa anapoenda Ikulu kukaa naye? Nikiangalia Wizara zipo 24 mpaka na Naibu Mawaziri hawa watu wanatumia kodi za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuingiza suala la maridhiano kwamba vyama sasa tuanze mchakamchaka sasa ndiyo tutajuana sasa mwaka 2025 ni nani Mwanamme na Mwanamke ni nani? Maandamano yameruhusiwa itafika sehemu tuchoke kuwashauri hapa Waheshimiwa Mawaziri hamchukui hatua, kitakachofuatia sisi ni kuandamana na wananchi kuja kwenye familia zenu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi nikakubali kukalisha wananchi fedha zimeliwa na watu wanajulikana!

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, taarifa!

TAARIFA

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba mwaka 2025 au 2030 tutakutana watu wenye sifa na siyo habari ya mwanamke na mwanaume, kusema kwamba nani atakuwa mwanaume na mwanamke ni kudhalilisha wanawake ambao wanafanya kazi nzuri na njema, saa nyingine kuliko hata wanaume. Haya ni masuala ya ushindani wa vigezo siyo masuala ya ‘ME’ na ‘KE’, afute hiyo aliyoisema.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri kwa sababu umemtaka afute hiyo kauli yake. Kwanza hatupiti kwenye Kanuni ya Taarifa kama unataka mtu afute kauli. Pia mimi nilikuwa nafuatilia mchango wake anaelekea wapi kwa sababu niliyekaa hapa mbele ni mwanamke na aliyekuwa anamsifia pia ni Rais ambaye ni mwanamke. Kwa hiyo, nilikuwa naangalia hoja yake. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, nilikuwa naisikiliza hoja yake niielewe halafu ndiyo nijue yale maneno yake yametumika isivyo ama yako sawasawa. Kwa hiyo, kwa kuwa umeomba kuhusu kufuta wacha nimruhusu aendelee na hoja yake kama kutakuwa na hiyo sababu baada ya kueleweka hoja yake, kwa sababu anaendelea kuzungumza tutajua kama anatakiwa kufuta au hapana. Endelea Mheshimiwa Maganga. (Makofi)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi nilindie na muda wangu ili kusudi niweze niweze kuwasilisha mchango wangu vizuri na sikuwa na maana mbaya kwamba nani mwanaume na mwanamke atajulikana maana yake ni nani mchapakazi ambaye anastahili kuaminiwa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tumlinde Rais wetu kwa wivu na nguvu zote, tumekuwa na Naibu Mawaziri tukiwapigia hata simu Wabunge hawapokei, tunawandikia meseji ili washughulikie matatizo ya wananchi hawatujibu. Tunatambua Wizara zipo 24 ambapo mimi Mbunge kwa nafasi yangu ni kuchukua changamoto na kuipeleka mahala husika, ndiyo maana nasema hizi Wizara ziangaliwe upya, mpaka nafika sehemu mbali sana mimi kufikiria hivi! Hivi hawa kwanza waliteuliwaje yaani mpaka nachanganyikiwa nashindwa kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Wizara ya Afya madawa hakuna kwenye vituo vya afya, kilio kila mahala, pale Masumbwe nina kituo kikubwa sana akina Mama wengi wanahangaika. Naishukuru Serikali ilileta vifaatiba lakini mpaka leo havijaanza kufanya kazi, Mawaziri wapo hawahawa wanabadilishwa mara yupo Ustawi wa Jamii mara Maendeleo ya Jamii lakini hawafanyi kazi kiukweli, lazima tushauriane vizuri, najua ni chungu itawauma lakini ukweli lazima tuuseme. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la mikataba. Kwenye suala la mikataba najua kuna Waziri wa Mikataba hapo kuwa makini uje unijibu. Ile Halmashauri ya Mbogwe imeanza kujengwa toka mwaka 2016, Halmashauri ya Mbogwe mpaka leo ni mwaka wa Saba bado haijaisha, Mkandarasi alishakula fedha, Halmashauri tulishaazimia kwamba tupewe hata Mkandarasi mwingine, mpaka sasa hivi Milioni 700 zipo zimekaa tu kwenye account, mikataba haieleweki! Nakuomba utusaidie Mbogwe tuko busy kwanza tulishacheleweshwa zamani mno, ndiyo tumepata kafursa ka huyu Mama anatusaidia na anatusikiliza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, vilevile kingine, ninyi Mawaziri ni marafiki zangu lakini inakuja suala la wananchi mimi sina urafiki. Upande wa Jeshi la Polisi Mbogwe ni Mji mkubwa Askari hawajulikani wanalala wapi? Gari la zimamoto hakuna, nyumba zimejengwa nzuri nyingine zinaungua, kila siku ninauliza maswali humu mnashughulikia mtaleta, hakuna kuona kitu kinatekelezeka. Naomba Waziri kwa vile hii hotuba ya Waziri Mkuu imegusa vitu vyote na wewe ujipange unanisaidiaje Mbogwe ili kusudi niendelee kuwa Mbunge mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla hatujaanza mikutano mwaka kesho niwaombe sana Mawaziri wengi nimewataja, kuna Waziri wa Biashara, kuna Waziri sijui wa Mifugo, kuna Waziri wa Kilimo mbolea na zenyewe ilikuwa shughuli, tulikuwa tunamaliza mikutano kisera vilevile kuna Waziri wa Habari na Mawasiliano mitandao ina-scratch kila wakati lakini inaonekana kwenye maeneo mengine, Waziri wa Nishati na wewe umeme unakatikakatika kila siku majibu hayaeleweki, lazima tushauriane vizuri ili kusudi hata kama tunapongezana suala liko sawasawa, tusikalie kupongezana tu lazima tusuguane ili kusudi tuendelee kushika Serikali.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kunipa muda huo nikushukuru sana na Mungu akubariki sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa heshima siku ya leo tarehe 28 kuweza kufunga dimba la hii Wizara ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru wewe, nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa ardhi na dunia kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hii Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mjumbe wa Kamati ya Madini, kwanza napenda nimshukuru Waziri Doto Biteko Mbunge wa Bukombe, jirani yangu. Nimshukuru pia msaidizi wake Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini pamoja na Katibu aliyeteuliwa hivi juzi wa madini ndugu yangu ambaye jina lake sijalikariri vizuri. Niwape shukrani za dhati ya moyo wangu bila unafiki. Nimshukuru Naibu Katibu wa Sekta hii ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kabisa shukrani ninazozitoa ni za dhati siyo za kisiasa wala za kifitina. Mmekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Mwanzoni tulikuwa hatutembei pamoja. Ilikuwa kata funua kata funua kwa ajili ya kero ambazo zilizokuwa kwenye hii Wizara ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nifahamishe Bunge Tukufu hili kwamba kwanza hii Sekta ya Madini hapo nyuma tulikuwa hatufaidiki nayo sisi kama Wananchi wa Mbogwe. Kulikuwa na makampuni ya nje ambayo yalikuwa yananufaika pekeyake. Mheshimiwa Doto Biteko Awamu ya Tano ulipoteuliwa kuwa Waziri kulikuwa na migodi kwa mfano Nyakafulu likuwa imekaliwa na Kampuni ya RUSROT. Tulikuwa tunaona magari tu yanapishana. Mjie wetu wa Mbogwe Masumbo ulikuwa haujengwi. Mlipowatimua hao mabeberu wananchi wakaingia kuchimba na sasa hivi wilaya ina changamka kwa speed kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshukuru Rais wa Awamu ya Sita Mama yangu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazozionyesha kwa wananchi wote wa hapa Tanzania. Lakini pia napenda niwape pole wachimbaji wenzangu ambao wanahangaika na mihangaiko ya hapa na pale kuchimba kwa nguvu zao wenyewe bila kuwezeshwa hata na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda basi leo nijikite kuishauri hii Sekta ya Madini kwa mambo machache ambayo Mwenyezi Mungu atanijalia kuweza kuyataja. Kwanza ifahamike kwamba ninaposema Mkoa wa kimadini Mbogwe nazungumzia wilaya tatu, ambapo Wilaya ya Bukombe imo, ambapo anapotokea Waziri mwenyewe. Nazungumzia Nyang’hwale ni wilaya ambayo tunaungana kwa pamoja kufanya Mkoa wa kimadini Mbogwe. Naomba niishauri Sekta ya Madini hakuna kosa tunalolifanya kama kuandaa hizi bajeti na kutokuweka vipaumbele vya hii mikoa inayotuzalishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika uzalishaji hapa kwenye Kapu Kuu tumeingiza zaidi ya shilingi bilioni 21 ndani ya mwaka mmoja lakini cha ajabu wale wakusanyaji wanaosimamia hizi shughuli hawana ofisi nzuri. Kwa hiyo, niiombe Sekta ya Madini itenge eneo na iweze kuwajengea watumishi wa madini wanaousimamia huu Mkoa wa kimadini Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze RMO uliyenipa Mheshimiwa Waziri ni RMO ambaye sasa hivi kausingizi sasa kana tulia maana tukero kila kakitokea kakero kwa wachimbaji nampigia simu sehemu fulani kuna mgogoro, anaenda. Ananisikiliza pamoja na wasaidizi wake nampongeza sana wajina langu ambaye anaitwa na yeye Maganga kama mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndugu zanguni huwa siyo mwanasiasa mzuri yaani huwa ninaumia sana pale unapomuona mtu anasimama kuzungumza uongo sehemu yoyote ile. Wamezungumza wenzangu kwamba ukiangalia maandiko yanasema tumewawezesha wachimbaji wadogo tumewawezesha lakini kiuhalisia wachimbaji wadogo hawajawezeshwa chochote kile. Hizi shilingi bilioni 21 ninazozizungumzia ambazo zimeuza mauzo zaidi ya shilingi bilioni 200 ni wachimbaji wenye moko ambao wanaingia kwenye mashimo wenyewe. Serikali inaenda kuchukua pato la taifa na kuingiza kwenye Kapu Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu ukiona mazingira wanayoyaishi. Barabara hazipitiki, watoto wao hawana madawati kwenye mashule, huku Mbunge wao wa Jimbo la Mbogwe nazungumzia shilingi bilioni 200 zimeingia kwenye Kapu Kuu bila kuangalia fedha hizi zilikotoka. Ni kwa nini Serikali isitengeneze utaratibu wa kuwalipa ruzuku na kuwalipa posho wachimbaji hawa wadogo ili na wao waone faida ya kuwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi naweza nikasema haki vizuri haijakaa vizuri na ninaomba unilindie muda wangu nicheze maana bado muda mzuri sana hata nikipiga dakika 15 hamna shida ili kusudi niweke mchango wangu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye mabenki unakuta watu wanasimama huko kwenye Wizara ya Fedha wanasema tumewezesha wachimbaji lakini kiukweli wanamaliza viatu hawa wachimbaji kwenda kwenye mabenki na mikopo hawapewi lakini tukiwa kwenye makongamano na sherehe mbalimbali unaweza ukamwona mtaalam ana-introduce hoja akiwa anasema kabisa tumewezesha wachimbaji wadogo, huwa naumia sana. Kwa kweli hilo suala lishindwe na lilegee kwa Jina la Yesu nianomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba ni- copy na ku-paste mchango wa Mheshimiwa yule wa mzee wangu nanilii, mzee aah! jina nimelisahau yule wa Musoma yule. Mchango wake Getere umekaa vizuri sana. Amezungumza vizuri naomba niunganishe, ni-copy na ku-paste ndiyo maana nimesema hivyo. Mheshimiwa Waziri fuatilia mchango ule na niko pamoja na Getere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani wachimbaji waonekane wanathaminiwa kwenye hii Awamu ya Sita. Hatupendi kuona mazingira yale yaliyokuwa yanatupata miaka ya 1995, wachimbaji waki nanilii wakihila tu wawekezaji wanakuja wazungu kuwafukuza wachimbaji wadogo na kuwafanya kanakwamba wao ni wakimbizi hawako kwenye nchi yao. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri usiingie kwenye laana hiyo wewe. Natamani uweke historia hata kama ukiona mambo yamegoma sana yaani kung’atuka nalo ni neno ukiona mambo hayaendi kwamba sasa wachimbaji wanaenda kuanza kukosa haki zao unaachia ngazi rafiki yangu kabisa tunakuja kulima na kujipanga kufanya shughuli zingine huko Bukombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa sababu tumeona sasa hivi kuna baadhi ya wawekezaji wakija hapa nchini hawawathamini wachimbaji wadogo wazawa. Wakifika wengine wanafikia polisi. Wanapokuta watu wamehila wanawafukuza kwenye maeneo yao. Hawafuati sheria za kuwalipa fidia wenye maeneo ambao wamekaa nayo maeneo miaka nenda rudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana kuanzia wewe kama sheria zetu haziko vizuri tuzirekebishe ili kusudi tuwajali watu wetu. Haiwezekani mtu amemiliki ardhi zaidi ya miaka 100, mtu anaingia kwenye mtandao tu akiwa Australia au Marekani anapewa leseni. Anakuta tayari kuna wananchi wanaishi vizuri pale yeye kwa kuwa ana leseni anakuja na mabunduki anakuja kuhamisha wananchi. Wanabaki wananchi wanalia. Sawa natambua kwamba ardhi ni mali ya Serikali lakini lazima kauzalendo tukaweke sasa. Hii ardhi ya Serikali kuna watu ambao wamemiliki zaidi ya miaka 100, unawaachaje? Kwa nini na wao wasiingizwe kama maeneo yao wamemiliki yenye dhahabu wasiingizwe kwenye leseni humo ili kusudi na wao waweze kufaidika na ardhi yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakujua una uwezo mkubwa kaka yangu. Kabla hata hujawa Mwenyekiti wewe ulikuwa Mwalimu wangu ulikuwa unanifundisha jinsi ya kuishi hapa Bungeni. Kwa hiyo, nikuombe sana kwa power uliyoipata tuweze kuwasaidia wananchi wetu waliotuchagua waweze kunufaika na rasilimali zao ili wawekezaji hawa wanaokuja kwa wingi wawafaidishe wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine hapa Mheshimiwa Waziri napenda nishauri, zipo kero ndogo ndogo ambazo zinaweza zikatuchelewesha zikatufanya hata kutukosesha usingizi tena. Kwa mfano, hizi kodi za matela ya punda, tunasema ni madini ujenzi, nakuomba Waziri hizi kero zingine ndogo ndogo ni kufuta tu ili wenye matoroli ya punda hata Bukombe huko pamoja na Bukombe na Nyang’hwale waweze kufanya shughuli hizi bure. Kwa sababu toka zamani ilikuwa ni bure tu lakini sasa hivi hizi fedha hata kwenye kapu lako huwa haziingii zinabaki halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uwaonee huruma wananchi wako ambao ni wachimbaji wako uwe tayari kama Bashe ambavyo huwa namwona anapambana na mabeberu yanapokuja kununua mazao na kuwadhulumu wakulima na wewe uwe mkali hivyo ili kusudi wananchi wetu waweze kuishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine naomba nishauri hata hii Wizara ya Madini. Niombe maeneo yenye migodi yote barabara nyingi hazipitiki na ni maeneo yana uzalishaji kila siku yanatoa pamoja na kwamba sasa hivi hali siyo nzuri sana. Serikali ione sababu ya kwenda kuweka zahanati ili wachimbaji hawa wanapoumia waweze kutibiwa kwenye maeneo ya karibu. Tumeshuhudia watu wanaumia wakiwa wanachimba wakipondwa hata kuvunjika mguu mpaka akafike kwenye kituo cha afya anafika tayari ameshaathirika na kupata maradhi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kwa vile inakusanya tozo kwenye haya maeneo iyape kipaumbele yawekewe zahanati pamoja na huduma zingine, barabara ziwe safi lakini pamoja na vijiji vile vinavyozungukwa vinavyoathiriwa na madini, Serikali iweze kutoa mchango mkubwa ili kusudi tuweze kuona faida. Haiwezekani kuna wilaya zingine humu nikiangalia zinachukua mabilioni mengi kwenye Kapu Kuu sisi tunaokusanya vingi tunatoka bila bila na kukaa kwenye maeneo chakavu tunabaki tunatukanwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana na kale kaswali kangu ka asubuhi nimeomba uwanja wa ndege. Watu wanahila kule kupanda ndege mpaka aende Mwanza zaidi ya kiometa 360. Mimi hapa nina marafiki wengi tundege tupo tudogo twingi tu hapa twa kuchukua lakini hakuna sehemu ya kutua mpaka ukashuke kwenye migodi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kupitia hii Sekta ya Madini na Mheshimiwa Waziri kwa vile wewe ni wa kwetu kabisa na neno la Mungu linasema asiye wajali wa nyumbani kwao kubali kupambana huko kwenye vikao vya ndani na Mheshimiwa Rais umuombe na sisi tuwekewe kiwanja cha ndege pale Masumbwi mjini eneo lipo tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niseme tunafanya hizi shughuli kwa mujibu wa maelekezo ya Chama kwenye ukurasa wa 105 mpaka ukurasa wa 107 imefafanuliwa hii Sekta ya Madini kwamba tutafanya nini kuanzia mwaka 2020 mpaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana wataalamu wetu pale mnapoandaa hata hizi proposal muendane na mkataba wetu na wananchi kwamba tuliahidi nini kwa wananchi? Tusiende tu yaani kupuyanga tu halafu tuwe kama vile hatujasoma wote humu. Tuwe tunaangalia mkataba wetu na wananchi ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tumeahidi tutawasaidia wachimbaji, tumeahidi tutawasaidia vifaa vya kuchimbia nashukuru nimeona ma-caterpillar wakati nasoma hotuba Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kaka yangu, ninao wachimbaji pale Mbogwe nipe nafasi ya upendeleo wapatikane hata mabilionea hata watano pale kutokana na haya ma- excavator yanayomilikiwa na hili Shirika la STAMICO na Mkurugenzi wa STAMICO nina imani unanisikia. Pale Mbogwe kuna kila sababu ya kuweka CAP. Zikiwa zinachimba hizi caterpillar halafu tukawa na kiwanda CAP watu wanazalisha pale maana sasa hivi miundombinu tunayotumia ni ya plant. Tunachenjua huku tunakunywa sumu lakini tukipata CAP tunakuwa tunazalisha kwa haraka na pato litaongezeka zaidi ya 60%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine GST. Watu wa GST nimeona humu mmeongeza bajeti. Niombe sasa kwenye maeneo yangu hii migodi 88 ambayo wananchi wanachimba wenyewe iende ikafanyiwe research na mtuambie hii migodi dhahabu inapatikana kilometa ngapi kwenda chini ili wananchi hawa wawe na imani wanapokuwa wanapambana wajue kwamba tunazama shimo la urefu wa kilometa ngapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa na cha mwisho kingine niiombe sana Sekta ya Madini. Huwa kuna Kiswahili hawa wanasema kwamba samaki mmoja akioza, wote wameoza. Mheshimiwa Waziri usisite kuchomoa wale wabovu pale wanapoonekana wanakuchanganya, chomoa tupa chini safari iendelee. Hata Yona alitupwa akamezwa na samaki baadaye akaenda kuibukia kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hizi bilioni ulizoziomba 89,357 sina kesi na wewe na wala sitashika shilingi. Nikuombe tu Mwenyezi Mungu akutangulie usiingie kwenye historia tena ya makaguzi makuu haya ya nanilii ya mafisadi nakuombea sana kwa Mwenyezi Mungu usije ukaingia huko wewe. Kila utakayemuona wewe uzuri wewe una mdomo ni mwanasiasa halafu ni mwalimu wangu, sema. Yaani najua ukisema mapema hata dunia inakuelewa siyo kitu kinaharibika wewe umenyamaza tu unalinda ustaarabu. Hakuna cha kulindana yaani wewe ukiona mtu anachanganya pasua ili safari iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na Bwana akubariki sana nashukuru sana (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hii sekta ya nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi kwa kupata nafasi hii adhimu ya kuweza kuzungumza na watanzania wote kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mama yetu, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita kwa kazi anazoendelea kuzifanya hapa nchini ikiwemo kupambana na miradi hii mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake. Kweli shukrani za dhati, wananchi wangu wamenituma nije ni mshukuru. Walifurahia sana walipomwona anazindua Ikulu maana ilikuwa kama vile ndoto, kwamba Ikulu ya Dodoma imekamilika tena kwa kiwango cha juu kushinda hata ile ya zamani. Kwa kweli Mheshimiwa Rais ubarikiwe sana. Pili nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa jinsi unavyotuendesha kwenye Bunge hili Tukufu. Na sisi maombi yetu tu, kwa niaba ya Machifu wa Kisukuma tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu ili kusudi uweze kukamilisha dhima yako uliyokusudia. Na kwa niaba ya Watumishi wa Mwenyezi Mungu, kwa maana ya Makanisa yote Wakristo na Waislamu wamenituma kukwambia usome Zaburi 23:1 nakuendelea. Maneno haya yakutie ngunvu katika safari yako ya mapambano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye hii sekta ya nishati na nianze na hii miradi ya REA. kwanza, nikiri wazi kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati, na nikuombe Mheshimiwa Waziri, ushauri tuliokupa kama Kamati uuzingatie na uufanyie kazi sana maana umesomwa vizuri na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Kitandula pamoja na wajumbe ambao huwa tunakuwa wa wewe kwa pamoja, huwa tunakupa ushauri mzuri sana na ukiufuata utakuwa ni Waziri wa kiwango ambae utaacha historia kubwa hapa Tanzania kwenye hiyo sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, hii sekta yako ina changamoto nyingi na inafahamika katika historia ndio sekta ambayo huwa ni ngumu katika Wizara zote hapa nchini. Hata hivyo, nianze kwa kukushurukuru jinsi unavyonipa support kwenye Jimbo langu maana toka niingie madarakani nilikuwa nina vijiji 34 na kwa sasa bado vijiji 18 ambavyo bado havijapata umeme; naomba nivitaje. Kuna Kijiji cha Nyashinge, Kagongo, Isungabula hiki ni Kijiji kimoja kikubwa sana na huwa kinanipa shida sana ninapoenda pale. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo nikuombe wewe kwa vile mkandarasi yuko chini yako utoe msukumo, pale utakapofanya majumuisho mkandarasi huyu wa Geita afanye faster hapo Isungabula ili wawahi kulala peupe. Pia, kuna kijiji cha Bwendaseko, Kiseke, Nyashinge, Mgerere, Igalura, Burongo, Bushetu, Bukwimba, hiki ni kitongoji kikubwa, kimeamua kupewa Kijiji, na ndipo nilipozaliwa hapo. Pia, kuna Baguta, Kabanga, Buruhe, Ruhala, Mwagimagi, Mponda, Nhungwiza pale niliposoma Shule ya Msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, napenda nikwambie akupendaye lazima atakushauri kwenye Bunge kama hili. Mimi nakupenda sana kwa kweli Mheshimiwa Waziri; lakini kama nilivyotangulia kusema mwanzoni, sekta hii ni kubwa, unaongoza watu wenye akili, maprofesa, lakini hivyo wengine nia zao sio nzuri sana. Ninakuombea sana kwa Mwenyezi Mungu akupe ujasiri wa kutokusita kuchukua maamuzi pale unapoona mambo hayaendi vizuri. Nimeiona bajeti hii ina trilioni 3.48, kwa hali ya kawaida unaweza ukasema ni pesa nyingi lakini ni chache. Kwa kuwa mimi ni mjumbe wa Kamati na changamoto za sekta hii nazijua vizuri, bajeti hii ilitakiwa iende hata trilioni tano kwa jinsi mahitaji yalivyo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tukiangalia kwenye upande tu wa mafuta umetenga bajeti ili kusudi kuwasaidia vijana wanaojishughulisha na uuzaji wa mafuta holela mitaani. Kwanza, nipende kuwapa pole sana wenzangu kwa sababu na mimi ni zao ambalo linalotokana na kuuza mafuta huko mitaani. Niwape pole sana watu wangu wa Masumbwe ambapo tarehe 29 nyumba iliwaka kufuatia kuweka mafuta ya petrol ndani. Mheshimiwa DC wangu alishughulika vizuri sana, pamoja na Jeshi la Poliisi japokuwa hatukuwa hata na kizima moto, mchanga ulitusaidia na Mungu alismama na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwape pole pia wale waliounguliwa na vitanda vyao kwenye Mtaa huu wa Masumbwe Shinyanga B Mungu awasaidie. Kwa sababu hasara hii imetokea, na hata huyu mfanyabiashara yeye hakupanga kwamba nyumba hiyo iungue. Kwa hiyo, Mungu awasaidie muweze kupata mitaji mingine maisha yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nimpe pole mfanyabiashara mmoja tarehe 23 aliunguza nyumba yake kwa shoti ya umeme. Mheshimiwa Waziri hii nayo ni changamoto nikuombe wasiliana na Waziri mwenzako wa Mambo ya ndani ikiwezekana kila mnakopeleka umeme huko mtaani kuwepo na vifaa vya kuweza kuzima shoti za umeme pale zinapotokea. Ni kweli huduma hii ni nzuri lakini pale inapotokea shoti inakuwa ni majuto kwamba ni kwanini niliunganishiwa umeme huu. Mimi nimeyaona kwa macho nyumba za watu zinavyotekekea kwa shoti za umeme. Kwa hiyo, Serikali ilifikirie. Na kwa kuwa hapa nazungumza na Serikali yote mpo, mlifikirie hasa pale mnapowaunganishia umeme wananchi wa vijijini mkumbuke je, ikitokea shoti watazima na nini katika nyumba zao?

Mheshimiwa Spika, kwa mfano mji wa Masumbwe ni mkubwa na hatuna gari la zima moto japokuwa hoja hii nilitakiwa niiwasilishe Mambo ya ndani. Hata hivyo, kwa kuwa wewe Mheshimiwa Waziri uko makini unaweza ukaongea na ndugu yetu ili aweze kutusaidia ili nyimba hizi zinapopigwa shoti ya umeme ziweze kuzimwa kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke jimboni nishauri jambo lingine la kitaifa. Hapa nchini tuna changamoto ya upandaji wa mafuta, na hili mimi nakuomba Mheshimiwa Waziri kwa vile una uwezo mkubwa ukae na wataalamu wako uangalie ni jinsi gani mnamsaidia Mheshimiwa Rais. Kwa sababu sio kawaida Watanzania kununua bei za 3000/3000. Kwa sababu tusiseme maisha tumeyaweza sana, kero zilizoko mtaani nikubwa.

Mheshimiwa Spika, tuna bandari yetu, jinsi gani tunakwenda kuwasaidia wanyonge ili kusudi bei za mafuta na nauli zishuke bei; kwa sababu mafuta yakishuka bei ina maana na vitu vyote vitashuka bei, mabati yatashuka bei na kila kitu kitashuka bei. Kwa uwezo wako uliopewa na Mwenyezi Mungu kaa na wataalamu wako muangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano nchi ya Kenya tumesikia sasa hivi wao wanaagiza mafuta kwa fedha zao za Kenya. Kama Kenya inawezekana kwa nini sisi Tanzania ishindikane kuagiza mafuta kwa fedha zetu? Vile vile, uagizaji wa mafuta zile Sheria zilizopo ni ngumu. Tuachieni Machinga tufuate mafuta wenyewe nje ya nchi ili kusudi muone bei zitakavyoporomoka ili Watanzania waweze kuishi maisha wanayoyataka.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wana imani kubwa na Chama cha Mapinduzi lakini pale maisha yanapoonekana kuwa magumu halafu tukawa kama vile hatuwajali inaonekana kama tumewasahau. Mkumbuke Sera yetu ni kuwasaidia wanyonge. Sasa wanyonge hawa bei za nauli zinapopanda wanashindwa kuelewa kwamba Serikali hii ilitutangazia kutusaidia ama kutukomoa? Kwa hiyo, nikuombe Kaka yangu January kaa na wataalamu wako pamoja na bodi inayohusika kupanga wale waingizaji wa mafuta Sheria hizo zifutwe na watu tuingize mafuta kwa uwezo wetu ili kusudi tuweze kuilinda nchi yetu na kuweza kuileta manufaa mazuri ili watu waishi kwenye maisha mazuri ya kupendeza.

Mheshimiwa Spika, suala lingine, Mheshimiwa Waziri nizidi kukushukuru tu, lakini pale Masumbwe zile transformer zilishazidiwa. Transformer zilizopo Wilaya ya Mbongwe zilikwisha zidiwa, maana kipindi umeme unapita nyumba zilizokuwa zinaunganishawa zilikuwa chache. Hivi sasa kuna viwanda vya mchele kwa hiyo, pale wanapowasha mashine hizi za kukoboa mchele umeme unazima. Utufikirie kutuongezea transformer nyingine kupitia bajeti yako hii ya Trilioni 3.4. kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana na ukipata nafasi utembelee kwenye jimbo langu ili kusudi uje u–solve matatizo yangu. Kwa sababu wewe ni rafiki yangu na urafiki mzuri ni ule wa kujaliana wakati wa shida sio kusubiriana tu huku kwenye raha. Kwa hiyo, nakukariobisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa vile na yeye ni Mbunge mwenzangu kila mara huwa anapita. Naibu Waziri, nikuombe mji wa Masumbwe usipopita kwenye chocho ni lazima wewe uukanyage ili ufike Bukoba. Siku moja utenge nafasi uweze kuzungumza na wafanyakazi wa TANESCO, hawana magari, hawana vitendea kazi vijana hawa wanasumbuka sana kufanya kazi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana kengele ya pili imeshagonga.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana ahsante. Nitaleta mchango wangu wa maandishi kwa yale niliyoacha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili niweze kuzungumza na wananchi wote pamoja na nyinyi Wabunge wenzangu. Napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu huu muda mfupi wa dakika 10 nami niweze kushauri na kutoa mawazo yangu katika Bajeti Kuu hii ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza napenda nimpongeze sana Waziri jinsi proposal alivyoiweka ya bajeti kuu. Nampongeza Mheshimiwa Rais maana nina imani bajeti hii anaijua kikamilifu Waziri hawezi akaleta tu hivi vitu bila kujua Mkuu wa Nchi. Ninachotaka nishauri hapa yapo mambo mengi ambayo yamezungumziwa humu na nashukuru Mungu kabisa toka tarehe 14 nasikiliza michango ya wenzangu. Sasa naomba niweke mchango wangu tofauti kidogo nisifuatishe kule walikopita wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la asilimia 10 wenzangu wengi wamelisema sipendi nilirudie. Pia lipo suala hili la watu wenye umri wa miaka 18 nashauri hapo Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia na ushauri wangu asiliweke kabisa; kwamba kila mtu anapofikisha miaka 18 aingizwe kwenye TIN Number, hilo litatuletea double standard katika maisha yetu hayatakwenda sawa, nashauri Waziri aliache.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine hapa nikumbushie, mwaka jana nilishauri mambo mengi, mengine yalifanikiwa lakini mengine hayajafanikiwa. Naomba niyagusie yale ya muhimu ninayoyaona mimi. Kuna hawa viongozi wa Serikali za Mitaa, napenda awaweke na wao wawe wanapata posho mbalimbali, ili kusudi shughuli wanazozifanya wazifanye kwa moyo mmoja, Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala lingine upande wa TARURA, mwaka jana kila Mbunge tulipewa Shilingi milioni 500, mimi nikaweka mawazo yangu kwamba hizi fedha ziende kwenye vifaa vya ujenzi. Mheshimiwa Waziri alinikubalia kwamba watafanya hivyo, lakini baadaye ulitolewa Mwongozo TARURA ukikataa hayo mawazo. Naomba kwa kuzingatia kama Waziri alivyokusudia kubana matumizi, tukiangalia barabara zote zilizochongwa mwaka jana zimenyeshewa na mvua mpaka sasa hivi maeneo mengine hayapitiki, lakini hapa kama halmashauri zingepewa vyombo vya kutengenezea barabara wangeendelea kuchonga na barabara zingeendelea kupitika. Kwa kuwa, tunakwenda kwa style ya kubanana, nashauri Waziri wasirudi nyuma, sio mbaya hata watumishi wengine wakiwa wanaambulia Noah tu kulingana na hesabu zao za kwenye mishahara katika kuwakopesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana ukiangalia hesabu aliyoitaja Mheshimiwa Waziri juzi hapa na nimekaa siku tatu nikaitathmini vizuri nika-calculate kweli hizi gari kila mwaka zinakufa. Matengenezo huwa yanakwenda kufanyika garage za gharama kubwa lakini sisi wenyewe wengine humu tunamiliki hayo magari. Ukiangalia hesabu wanazotengenezea halmashauri huwa haziendani. Ukiangalia hizi ofisi za manunuzi sana sana ni hasara tupu, ni kuwaingiza hasara wananchi na kushindwa kuwasaidia wananchi kwenye masuala ya msingi. Ukiangalia wananchi wetu kuna kilio kikubwa, tunapitia kwenye kipindi kigumu mwaka huu, nikiangalia hali halisi kwanza kuna dalili ya njaa vyakula vinavyotembea kwenda nje ya Mataifa sidhani kama Serikali itakuwa na stock ya kutosha kuwalisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni mwezi wa Juni lakini mchele unauzwa mpaka Sh.2,500 mjini hapa, mwezi wa Julai tuko kwenye msimu. Mahindi yanauzwa mpaka Sh.120,000 Moshi na magari yanatembea usiku na mchana na nikiangalia watu wetu, ni kama vile hawajiandaa kabisa kwamba kunaweza kukachelewa mvua kunyesha maana hizi skimu zinazosemwa zinaweza zisitusaidie. Kwa hiyo, naishauri Serikali iliangalie hilo suala ikiwezekana tufunge mipaka kwanza ili watu wetu wasife kama hatuna stock za kutosha. Huo ndiyo ushauri wangu kwa Serikali, waliangalie sana hilo suala.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka nilizungumzie ni suala la kupoza maisha kwa mwananchi. Mheshimiwa Rais amefanya jambo jema mwezi uliopita Juni, ametoa Shilingi Bilioni 100 ili wananchi waweze kupata unafuu kimaisha, lakini hiyo fursa wananchi wale wa kawaida hawajaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iangalie na lazima tufahamiane kila mtu rank yake, Rais ni Amiri Jeshi Mkuu, Rais ni mwanzo mwisho akisema kitu ina maana kinatakiwa kizingatiwe, sio Rais amesema tena halafu tangazo lingine linatoka kwamba nauli hazitashuka bei. Niliona watu wa SUMATRA, baada ya kutangaza Rais kwamba natoa bilioni hizi ili maisha yapungue, lakini kuna tangazo lilitoka kwamba nauli hazitashuka. Matokeo yake hizi fedha kama vile zimepotea maana kule Rais alipokuwa amelenga ziende hazijaenda. Kwa hiyo, niishauri Serikali wawe wakali sana katika masuala ya watu wanaojaribu kuleta disturbance katika maisha ya watu hao wanaopata shida kwenye hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuondoa ada kwa kidato cha tano na cha sita, lakini lipo suala moja kwenye shule, michango michango, wanafunzi wamekuwa wakilia sana. Naomba nalo hili Serikali ilitolee ufafanuzi maana kuna hatari unaweza ukaondoa ada lakini michango ikawa mingi, ikawa hakuna ulichokifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niwaombe Mawaziri, sasa hivi kidogo tunaendana nao, maana tumeshazoeana ni miaka miwili sasa. Zipo ahadi nyingi ambazo wamenipa kwenye Jimbo langu, Mawaziri wale waliofika kwenye Jimbo langu na uzuri walifika kampeni nilishaimaliza, nina imani ahadi walizokuwa wakinipa ni za ukweli kabisa. Hivyo, ni wakati sasa wa kuzitekeleza hizi ahadi, maana mimi sio mtani wao wa kusema kwamba labda walikuwa wanatania au walikuwa wanafurahisha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Waziri wa TAMISEMI tumeshaongea na yeye confidential, naomba nilirudie tu hapa, Wilaya yangu inakabiliwa na Makaimu, kila Idara imekaimiwa. Mkuu wa Wilaya mwenyewe sasa hivi kuna Kaimu, ukienda DMO Kaimu, kila sehemu Kaimu, wilaya yangu inakuwa haihudumii vizuri wananchi wangu, unajua Kaimu ni tofauti na bosi mwenyewe, kibarua ni tofauti na tajiri mwenyewe akikuhudumia, naomba waniangalie kwenye Wilaya yangu. Hata hivyo jamani napambana, nime-sacrifice maisha yangu kwa ajili ya hilo Jimbo kutoka Shilingi milioni 700, wilaya ilikuwa haikusanyi lakini mpaka sasa hivi tunakusanya Shilingi Bilioni tatu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha a-sacrifice maisha kama alivyolianzisha hili asirudi nyuma, kodi zetu ziko bandarini pale, huku kwingine ni kama vifaranga tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari pale nina wasiwasi, bado kuna vitu vinapenyezwa, hebu wajaribu hata siku moja kuweka Jeshi wiki moja wasimamie Jeshi watoe hawa waliozoea kusimamia, wasikilize tutapata trilioni ngapi? Hii trilioni 41.48 naiona kwanza ni kidogo sana, hakuna haja ya kuongezea tena chanzo kingine, nashauri hivyo. Hivi vyanzo vilivyopo hebu tuvisimamie tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Mtwara ikisimamiwa vizuri na Bandari ya Tanga, bado migodi, miamala, bado tunahangaikia trilioni 41 tu, hakuna hili suala haliwezekani. Nawaomba waliopewa dhamana wasimameni imara ,wengine huwa tunasali hatujui hata siasa kusema kwamba tuongee sijui tujipendekezeje. Nashauri kabisa katika roho na kweli na wala sihitaji kuleta magumashi sijui longolongo ya mara nini, mara nini, Taifa hili tutarudi nyuma. Rais wa Awamu ya Tano alitangaza vita ya uchumi nina imani haijaisha; na wakumbuke wengine walikuwa Mawaziri, wakati tukitangaziwa sisi wengine tulikuwa tunachunga ng’ombe. Ile vita ya uchumi haijaisha inaendelea mbona wamelala, mbona hatusikii viwanda, kuna vitu vingi vimelalalala, hatusikii Mawaziri wakisema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri wanatembelea V8 na tukimaliza hili Mheshimiwa Mwigulu turudi kwa Mawaziri, hizi gari ziwe zinatumika kwa utaratibu kwa vile tumeamua kubana bajeti. Ikiwezekana kila Waziri akitaka kufanya safari, lazima aangaliwe anakwenda safari gani, anatumia mafuta gani, hapo ndio tutakuwa na usawa ili na wanyonge nao wapate haki yao, ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maganga, hiyo ni kengele ya pili lakini endelea kusimama. Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Maganga tulimtangaza kuwa ni mchezaji bora katika mechi zilizopita. Kwa bahati mbaya tv ilikuwa haiku-zoom kwake na alipata unyonge. Sasa leo nampa nafasi tv zi-zoom kwake ili jimboni kwake wamuone, ndio amekuwa mchezaji bora kwenye mechi... (Makofi/Kicheko)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana au umeniongezea na dakika kidogo niongezee katika mchango wangu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa tena nafasi nzuri ya pekee niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, napenda nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Jumaa Aweso, nilifanya naye ziara kwenye Jimbo langu siku saba zilizopita kutokana na swali ambalo nililiuliza hapa siku hiyo alikuwepo Naibu Waziri wa Maji dada yangu Mheshimiwa Maryprisca Mahundi. Nina furaha kubwa kwa niaba ya wananchi wangu wa Mbogwe, kwanza baada ya kumuona Waziri wa Maji anafika kwa wakati muafaka na akanipa ahadi nyingi ikiwemo gari kwa ajili ya wananchi wa Mbogwe kwa maana ya Meneja wa Maji wa Mbogwe. Cha kusema kikubwa mimi niwaombe tu Wabuge wenzangu leo nisingependa hata nione mtu hata mmoja anashikilia shilingi maana huyu Waziri ni mwaminifu sijawahi kuona Waziri mwaminifu namna hii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Rais wetu, Mama yetu kwa ziara zile anazoendelea nazo huko nje. Sisi kama Wabunge tunampa support asilimia mia moja. Tukio lililotupata mwaka huu lilikuwa kubwa sana na mataifa yalitegemea kuona sisi tunaanguka lakini kwa uwezo na nguvu za Mungu mpaka sasa hivi tunajadili bajeti na mipango yetu kama watu wenye akili timamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, nitumie nafasi hii kushauri, Katiba inasema mimi ni mtunga sheria lakini vilevile nimshauri wa Serikali. Pamoja na pongezi zote kwako Mheshimiwa Waziri nikutie moyo, kuna watu wengi kweli unaenda unawaelimisha pengine walikuwa hawajui majukumu yao, ikiwemo watendaji wako wale wa chini kwenye halmashauri huko wilayani, kuwapa maelekezo mazuri ili kusudi wawe karibu na wananchi na wananchi kiukweli wanaimani kubwa sana na awamu hii. Kwa hiyo, kwa vile umeniahidi mimi vitu vingi na mimi nikuahidi tu, kwanza miradi ile mikubwa ikianza kukamilika pale kwenye Jimbo langu nitaandika jina lako Jumaa Aweso ukumbukwe hata kama siku umekufa kwamba palikuwa na Waziri Awamu ya Sita alikuwa anaitwa Jumaa Aweso. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine sasa hivi mimi naishi hapa Dodoma kwa nguvu za wananchi wa Mbogwe. Nipende tu kumsaidia Mbunge wa hapa Dodoma haipendezi sana tupo Makao Makuu halafu tunakuwa hatuna maji, nyumba zetu tunajenga tunaweka ma-simtank, kwa kuwa wewe ni Waziri wa nchi nzima ukimaliza basi kwenye majimbo yetu yale ya Kanda ya Ziwa ufanye juu chini kama unavyofanya ili na Dodoma hapa tupate maji hayo ya mradi mkubwa wa Ziwa Victoria. Maana maji yetu kule ni mazuri halafu huku tunatumia maji yenye chumvi. Sura yangu mimi nilikuwa mzuri sana sikuwa na sura ya hivi, ninarudi nyumbani tena nikiwa na sura nyingine. Kwa maana hiyo nikuombe ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde tusaidiane tu kuwa tunamkumbusha Waziri wetu ili na hapa tuweze kuupata huo mradi mkubwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi kwa vile natoka Geita, sasa tuna wilaya tano, mwenzangu amezungumza pale, ni vyema wilaya zetu ambazo zipo karibu na Ziwa Viktoria zipewe huo mradi wa maji mkubwa ili kusudi wananchi wa kule waweze kufaidika na maji yao ya Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwaombe tu hata Wabunge wenzangu, nina imani kuna Wabunge wengine baada ya kuchaguliwa hawarudi majimboni kutazama shida za wananchi, tusije tukapata tena kazi ngumu 2025 kukawa na jimbo halina maji tena tukaanza tena kampeni zile za kutumia nguvu sana. Maana wananchi tuliwaahidi kwamba watakuwa na maisha mazuri, tutawapa huduma za maji pamoja na mambo mengine lukuki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Wabunge wenzangu tuwe tunamkumbusha Mheshimiwa Jumaa Oweso ni mtu mzuri sana na atatusaidia tu na nina imani naye maana nimeona kwa vitendo, kuna bilioni karibia 50 mradi mmoja ambao ulikuwa unaenda Katoro, alimpongeza hadharani Engineer mmoja jina nimeshalisahau, kuna dogo mmoja hivi ni Engineer pale Geita alisema ameokoa bilioni karibia arobaini kitu. Kwa maana hiyo, wewe brother ni muaminifu na ungekuwa na tamaa kama watu wengine siwezi kuwataja hapa, wanaomtumikia shetani ina maana hizo ungepiga kimya tu na wala hakuna mtu angekusumbua, kama ni kesi ina maana ingeendelea mbele kwa mbele. Brother wewe ni muaminifu endelea kuwa na imani hiyo na Mungu atakusaidia mambo mengi na siku zako zitakuwa nyingi sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nikupongeze wewe mimi leo nina miezi sita hapa Bungeni, nilikuwa kiukweli sijui kabisa kuongea mbele ya watu wakubwa kama nyie hivi, wakiwemo Mawaziri ambao nilikuwa nawaona tu kwenye screen wakina Prof. Palamagamba Kabudi lakini sasa hivi kwa vile tunaonana vizuri sana. Niwaombe Mawaziri muige mfano kwake huyu Waziri Jumaa Aweso kwenye Wizara zenu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana toka tuanze kuchangia bajeti hapa kila mtu aliyeleta bajeti yake tunaipitisha, ni vyema sasa unapoipokea ile bajeti yako uwe na kumbukumbu kwamba nilipitishiwa bilioni 60 zimefanya kazi hivi hivi. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tupate siku moja kuja kuwahoji hawa Mawaziri kwamba tulipitisha bajeti mwaka 2020 zilienda wapi? Kwa mawazo hayo tutaenda vizuri na wananchi wetu waliopo kijijini kuliko tu kila kitu tutasema ndiyo, ndiyo halafu vitu vyenyewe vinakuwa havifanyiki huko majimboni na vijijini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, wale watumishi wa Mungu mmenielewa lakini wale wenye roho mbaya na dhamira mbaya message sent mjipange. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi wakati huu ya kuweza kuchangia Sekta hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwanza siku ya leo kuniamsha nikiwa salama na Mungu akipenda nategemea kutinga pale Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Uwanja wetu wa Jamhuri pale, ili twende tukaweze kuchuana na hawa TBC. Niwaombe Wabunge wahudhurie, ili waweze kushabikia timu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, naomba kaka yangu Mheshimiwa Damas Ndumbaro pamoja na dada yangu Mheshimiwa Mary Masanja, nijikite leo kwenye ushauri kuliko kuwapondea sana. Sekta hii ni sekta ngumu sana, maana ni sekta ambayo wanafanya kazi na watu. Ni sekta ambayo Wasukuma wanalia, wafugaji. Niliona jana Mheshimiwa Waziri ametengeneza Operation Ondoa Mifugo Kwenye Hifadhi. Unajua kuna vitu vingine unaweza ukakiona kama tu kitu cha rahisirahisi ukakitengeneza mtu mkubwa, lakini baadaye kikaumiza sana wenzako, binadamu wenzio. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe. Ninalo pori ambalo ni la Kigosi, namshukuru Waziri ameniahidi kwamba, endapo atapata advantage kwenye ufalme wake atanisaidia kwani lile pori limesahaulika, barabara hazipitiki, hata wale wataalam wa Mheshimiwa Waziri wale wanaolilinda hawana barabara nzuri za kuweza kupitika. Ni vyema sasa muweke kwenye bajeti hii ili barabara ziweze kuchongwa na ziweze kupitika vizuri ili kuweza kupambana na ujangili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili niombe tu kuishauri hii Wizara, sheria zibadilishwe, binadamu wathaminiwe kuliko kuthamini tembo pamoja na nyoka na wanyama wakali ambao hawana faida kwetu sisi binadamu. Nikisoma maandiko, sisi binadamu tuliumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu, lakini wapo watu ambao wanalinda
kwenye mapori yetu haya hawana huruma, ni watu ambao kweli wanatekeleza hizi sheria. Kwa kuwa, sheria sisi ndio tunazitunga, Waheshimiwa Wabunge pamoja na Waziri, tuzirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwa ni hatari sana mtu labda hata amepotea njia tu akapita kwenye mapori yetu ambayo hayana sifa ya kuwa hata mapori anapigwa risasi. Vilevile ng’ombe, nikiangalia ng’ombe wanachukiwa sana kwenye hii Wizara kana kwamba, yaani sio pato lenyewe. Nikiangalia wengi humu tumeolea ng’ombe, hakuna mtu aliyeoa akatoa mahari ya tembo, kwa hiyo, niombe ng’ombe wathaminiwe sana, tutengeneze utaratibu mzuri kwenye hii sekta. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua katika utalii wasiangalie tu wazungu ndio watalii, hata ng’ombe nao ni watalii, tukipunguza fine, badala ya laki kila kichwa cha ng’ombe tukaweka elfu hamsini hamsini kila ng’ombe atakayekamatwa porini tutakuwa tumepata watalii. Mimi ukiniambia neno watalii kwanza silijui maana Ngorongoro sijawahi kufika. (Kicheko

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri itakuwa ni vyema na Wabunge wengine maana wanaongelea tu hili suala la utalii, hawajafika kwenye pori lolote na wanajaribu kutoa mifano ya Indonesia ya uwongo mtupu. Kwa hiyo, ni vema… (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa, Taarifa. Mheshimiwa Maganga kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kiruswa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumfahamisha mzungumzaji kwamba, kuna bidhaa ya utalii wa mseto ambapo kule ulaya wazungu wanasema go to Serengeti and Ngorongoro to see the lion and the Masai. Kumaanisha kwamba, unaweza kwenda Ngorongoro au Serengeti ukamwona Mmasai ambaye ni binadamu na mifugo na wanyama. Kwa hiyo, biashara ya utalii mseto inawezekana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Yaani unampa taarifa kwamba, Mbogwe pia, wanaweza wakakaa na wanyama porini, ndio unachojaribu kusema?

Nadhani hilo mmefanikiwa ninyi Wamasai, sina uhakika na wao kwa sababu, wao wanyamapori wanakula, ninyi kule kwenu Ngorongoro mmewaacha wanyama waendelee na maisha.

Mheshimiwa Nicodemas Maganga.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilindie muda wangu nina vitu vya msingi hapa na vya maana sana. Naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe, Pori la Mkweni, lilishamaliza sifa ya kuwa pori maana halina tembo, halina wanyama wale wanaoangaliwa na watalii. Pori lile sasa hivi wamejaa Wachina, wanachimba usiku, lakini binadamu wakionekana mle wanavunjwa miguu pamoja na ng’ombe wakiingia mle wanatozwa laki.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wapo vijana wa Mheshimiwa Waziri, ng’ombe wakiwa wanapita hata barabarani, maana pori lile limepakana na barabara ya lami, ile barabara kuu iendayo Kongo, wakionekana ng’ombe wanapita barabarani wanakamatwa wanaingizwa kwenye pori. Lengo na madhumuni kwa kuwa fine ni kubwa, ni laki moja, wanapata mwanya wa kupatia rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta hii , nataka nimweleze ukweli Mheshimiwa Waziri, maana nampenda pamoja yuko na dada yangu, wakae wakijua kabisa watu wanateseka sana walio jirani na mapori. Kwa maana hiyo, ni vyema sasa hata wanapotengeneza huu mpango wa Operation Ondoa Mifugo Porini kwanza wajue kabisa kwamba, wana watu wa aina gani na kidogo Waziri ajaribu kuonesha makucha wasiwe wanawaonea tu watu wenye ng’ombe, maana sisi sote tumetoka huko kwenye ng’ombe, tunajua machungu ya ng’ombe hatujui thamani ya tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, mimi binafsi namchukia sana mtu anayechukia ng’ombe na kuthamini tembo. Maana tembo hawa tunategemea mpaka watu watoke Canada na sehemu nyingine ili tupate pesa za kigeni, lakini sisi wenyewe tukiwekeana utaratibu, tukawa tunachungia kwenye mapori yetu, kwa kuwa mapori yetu haya tuliyopewa na Mwenyezi Mungu ni makubwa, tukaweka fine hata ya shilingi 50,000, lakini vilevile kwenye Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi kwenye ukurasa wa 52 tuliahidi kwamba, tutatenga kwenye mapori yetu maeneo ya kuchungia ng’ombe. Ni vyema na lenyewe hizi Wizara naziona zinafanana, ni kama kurwa na doto, sekta hii pamoja na sekta ya ardhi, wakakaa ili kusudi wakalitengeneza hili suala ili watu waweze kuishi vizuri kwenye mapori yao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nashukuru. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu; kwanza kabisa kwa kuniona wa maana kwa kunipa nafasi ya leo adimu. Zimebaki siku tisa turudi majimboni. Kwa kuwa umenipa msaada mkubwa wa kuweza kuishauri Serikali ninaomba nijikite kuishauri Serikali maana muda hautoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa jinsi tulivyopanga hapa bajeti vizuri, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri kweli bajeti imekaa vizuri sana. Nimeisoma, ina page 98 na nimesikiliza michango mingi ya Wabunge karibia yote inafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na mawazo tofauti. Kwanza nianze na suala la milioni 500 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kila jimbo. Neno la Mungu linasema “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.” Hii milioni 100 ni kilometa moja, milioni 500 ni kilometa moja. Nimeuliza kwenye makampuni yanayouza makatapila; kuna catepillar excavator zinazouzwa na Wachina mpaka milioni
350. Mimi nilikuwa naona kwa mawazo yangu kwenye jimbo langu, kwa kuwa lina matatizo makubwa ya barabara; mngeturuhusu kila Mbunge tukatoa mawazo nikapata excavator la milioni 400 au 350 nikabaki na milioni 150 kwa ajili ya kuweka mafuta ningeweza kutengeneza barabara zaidi ya kilometa 50 na kuendelea na caterpillar likabaki. Halafu hilo caterpillar si kwamba ni la kwangu, ikiwezekana liandikwe Mama Samia Hassan Suluhu, Rais wetu, ni mtu mwema sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine naishauri Serikali, Waheshimiwa Wabunge watu wanataka mabadiliko wako serious. Na mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Mungu amuweke mahali pema peponi; alitunadi kwa nguvu kubwa, na wengine tulishinda hatukuwa na sifa za kushinda; na kuna wengine walishindwa kwenye uchaguzi hawakuongoza katika kura za maoni. Lakini sasa hivi niseme tu nasikitika sana, kuona nchi tena inataka kurudi kwenye upigaji. Kuna watu ndani ya Serikali hawana mapenzi mema na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshauri Mheshimiwa Rais awe na maamuzi magumu kabisa katika hilo, wala asione huruma. Leo nimeshuhudia akiwaapisha Wakuu wa Wilaya na wengine kuwahamisha vituo, kama alivyofanya kwa Mawaziri. Lakini ukweli utabaki kuwa ukweli, watu wale ambao wanatuhumiwa na CAG pamoja na halmashauri zingine ambao wanaonekana kabisa wamekula pesa Serikali ichukue maamuzi magumu, na kwa kufanya hivyo itakuwa na sisi inatusaidia Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa bodaboda Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba bodaboda takriban nchi nzima wanakupongeza sana. Lakini kuna sehemu ya wenyeviti wa vijiji pamoja na vitongoji; Wabunge wengi wameongea na mimi naomba nikazie hapo. Haiingii akilini mtu aliyekuwa ananifungulia mikutano yangu ya Kampeni hana hata shilingi elfu 10 kwenye Taifa ya Tanzania. Mtu huyu ambaye mimi nasimama kumuongoza Kikatiba, kwamba inatakiwa kuwasomea mapato na matumizi wananchi katika michango ya kawaida, hana hata senti 100. Ni suala la kujiuliza haraka haraka bila hata degree, unalijua kabisa suala hili si zuri. Kwa maana hiyo ukija hapa ninakuomba ujaribu kuwaingiza hawa watu ili na wao waweze kupata posho. Tunaposema Tanzania ina mali nyingi angalau na wao at least kwa mwezi wawe na hata 100,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la MSD. Wabunge wengi wanazungumzia suala la afya, na mimi nimekuwa msumbufu sana hapa Bungeni. Nikiangalia takwimu za mwaka 2018 kwenye halmashauri yangu Mbogwe zilitengwa milioni 600 na zilikwenda; lakini cha ajabu nawauliza waliokuwa kwenye system hizi fedha hazikufika ilhali Serikali mpo na wasaidizi wa Rais mpo.

Mheshimiwa Naibu Spika lakini nimshukuru kaka yangu ambaye ni Naibu Waziri alifanya ziara kwenye hospitali zangu na akaona changamoto zilizopo. Nikuombe radhi sana Mheshimiwa Naibu Waziri juzi kwa kumuuliza swali la kushtukiza Mheshimiwa Waziri Mkuu na ukaelekeza mamlaka kwamba watanijibu TAMISEMI lakini ninahitaji hilo zoezi kwa sababu wananchi wa Mbogwe bado wanaendelea kupata shida, akina mama wanakufa katika harakati za kujifungua, bodaboda wamekuwa wakipata ajali wanakosa vipimo kama X-ray pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe watu walio ndani ya Serikali, bajeti hii ni nzuri sana; lakini usiwe mchezo kama wa sarakasi, kama Kanumba na Ray. Tunaweza tukawa tumepitisha bajeti ya kila Idara, na uzuri nimechangia sekta nyingi sana; nimechangia kilimo, bajeti ya madini, na kila ukisoma jinsi Mawaziri mlivyo-introduce, kwamba mtafanya nini, iwe hiyo kweli. Lakini isiwe tu kwamba mmetukaririsha kwamba mtawasaidia kwa mfano wachimbaji wadogo halafu kusiwe na kitu, mtawasaidia wakulima kuwe hakuna kila kitu, tutaonekana watu wa ajabu sana. tukiangalia humu ndani tumo wa Chama kimoja; Mheshimiwa Marehemu aliliona hili baada ya Bunge la Mwaka 2015 kuwa na mivutano ambayo haikuwa na sababu; akaona achague watu wa kumsaidia ambao…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maganga, hebu twende vizuri kidogo. Hili Bunge halina chama kimoja vipo vyama vingine humu ndani.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kurekebisha tupo vyama vingi pamoja na mchanganyiko lakini wengi wetu tupo Chama Tawala. Kwa maana hiyo mimi nawashauri Waheshimiwa Wabunge, tusije tukamsaliti Marehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho naomba nizungumzie kuhusu manung’uniko ya Waheshimiwa Wabunge. Maslahi ya Wabunge yapo kidogo sana; na mimi wakati bado sijaingia humu nilikuwa nafikiria kwamba kuna posho za kutosha. Nimeangalia mabunge mengine kama vile Afrika Kusini pamoja na Kenya na mabunge mengine wanalipa kwa dola. Tusiwaogope wananchi lazima tuwe wakweli tuwaambieni wananchi huku kwenye Ubunge hakuna kitu. Tumekuwa tukitukanwa kwenye mitandao; tumekuwa tukitukwanwa kwenye mitandao, na mimi hii kazi niliiomba kabisa kwa roho yangu moja; na mimi nitasema ukweli daima fitna kwangu mwiko. Fedha inayolipwa posho hapa haitoshi, mishahara haitoshi, mimi ninayeishi na wananchi hakuna kitu kinachoendelea.

Kwa hiyo hilo Serikali iliangalie upya ili nasi tufananane na mabunge mengine, tusiwe wajanja wajanja. Ninaujua utapeli wa kila aina lakini sitaki niwe tapeli kwa wananchi, wananchi wajue kwamba wana Mbunge mwenye fedha kumbe hakuna kila kitu. (Makofi/vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo bado siku tisa, nirudi jimboni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana mheshimiwa…

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA:…wananchi wanajua Mbunge wao anarudi na fedha. (Makofi)

NAIBU SPIKA:…kengele imeshagonga.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie mpango huu kwa siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliusoma mpango na nimeuona lakini mimi kwenye kipengele cha miundombinu tumekuwa na adha kubwa. Barabara zetu zinajengwa kwa


kiwango cha lami kwa pesa nyingi lakini baada ya muda mfupi barabara zinakatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishauri hapa kwenye Bunge lililopita lakini nashauri tena kuwe kuna miundombinu ya mifereji pembeni. Barabara hizi zinakatika kutokana na maji hakuna miundombinu ya mifereji. Nilikuwa ninaomba kuwe kuna miundombinu ya mifereji wakati wa kuweka hizi bajeti ili barabara zetu ziwe salama.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kipengele cha miundombinu kuna kipengele ambacho hakijaguswa, kipengele hiki ni cha majitaka. Kuna adha kubwa ambayo inakuja adha hii ikoje. Kwenye kipengele cha majitaka mtandao wake ni mdogo mno ni mdogo nilizungumzia katika Jiji la Dar es Salaam, lakini sasa tunakwenda kwenye Miji na Majiji yanayokua kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukieleza suala la maendeleo ya watu ni lazima uoanishe na miundombinu thabiti. Nikisema hivyo ninaainisha Majiji yanayokua sasa hivi mfano, mtandao wa majitaka katika Mikoa ya Mwanza ni asilimia 3.1 na Jiji lile linakua kwa kasi. Mtandao wa majitaka katika Mji wa Moshi ni asilimia 5.8 ule Mji ulivyo mkubwa unakua kwa kasi. Iringa asilimia 11, Mbeya asilimia 0.6, Songea asilimia 3.7, Tanga asilimia 9.3, Tabora asilimia 0.1, Arusha asilimia 7.0 lakini inakuja Dodoma asilimia 11 ambako ndiko Wabunge wapo, huu ni mtandao siyo wa kuwafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza kutoa mfano wa Jiji la Dodoma, Jiji hili linakua kwa kasi ya ajabu, linakua kwa maana ya watu, majengo na viwanda vidogo vidogo. Huwezi kutenganisha maisha ya binadamu na masuala haya ya majitaka. Athari hii itakwenda mbali zaidi kama tutaendelea kulifumbia macho wakati Dodoma mtandao wa majitaka ni asilimia 10 tu ya watu wote waliounganishiwa mtandao huu. Je, kesho yetu ikoje, kwa nini tunahangaika kuagiza madawa nje kwa ajili ya malaria, kwa ajili ya magonjwa ya typhoid, kwa ajili ya kichocho na magonjwa mengine


yanayosababishwa na maji, kipindupindu kwa nini ni kwa sababu hatujaweka miundombinu thabiti ya majitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawiwa kusema hili kwa sababu naangalia Dodoma inavyokwenda kulipuka kila mtu anakimbilia hapa. Sasa, watu wa DUWASA kupitia research wanasema hawana bajeti ya kujenga miundombinu mipya na kukarabati ya zamani hawana hiyo bajeti. Kesho yetu iko wapi? Ni kwa nini sasa mtandao huu haupo? Haupo kwa sababu ni gharama kubwa. Mtandao wa majitaka katika hili Jiji na Majiji mengine kwa mita 10 ni shilingi 100,000 ili uunganishiwe kutoka kwenye mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukioanisha unapata kilomita Moja ni Shilingi 1,000,000/= mtu kama mimi mpiga kura wa kawaida, mtu aliyeko kijijini, mtu ambaye analia na msiba wa mazao hayajauzika, wamachinga wanapiga kelele wanapata wapi Shilingi Milioni Moja ya kuunganishiwa huu mtandao? Lakini ukiangalia ni asilimia 30 tu ya watu wote waliounganishiwa kwenye huu mtandao, kwa hiyo asilimia 70 tupo tuna-hang tu. (Makofi)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Njau subiri.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, taarifa.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anayechangia kuhusu Machinga namuunga mkono sana, kweli Serikali inapaswa iwaangalie machinga maana sasa hivi wanateseka sana. Ahsante sana. (Kicheko)

SPIKA: Yaani Maganga bwana. (Kicheko)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninapokea..

SPIKA: Unajua huyo ni Musukuma ameona tu mtoto mweupe hapa! Mheshimiwa Njau endelea. (Kicheko)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninapokea taarifa hii naendelea. Ni lazima tuweze kutibu haya mambo mapema kwa sababu hiki ni kipele cha cancer. Tunapoendelea kufanya maendeleo tujue kwamba, huku chini kuna vitu vingine vitatakiwa vifanyike ili tuweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo naenda kwenye kipengele cha Wakandarasi. Kipengele cha Wakandarasi imekuwa kama wimbo ni mazoea naomba tutoke kwenye mazoea. Kwa sababu, hili ni janga la Kitaifa tena kubwa. Nikisema hivyo tuna ripoti ya CAG ya Machi inasema miradi minne tu kutokana na kucheleweshwa kwa pesa za ile miradi tozo pamoja na faini ni Shilingi Bilioni 101.98 miradi minne. Tunakwenda wapi kama Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wataalam wapo ambao wanakaa….

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Halima taarifa.

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mchangiaji anayechangia vizuri sana, kwamba kwenye ripoti hiyo ya Machi kwenye suala la Wakandarasi CAG amesema taasisi 122 za Serikali zinadaiwa jumla ya shilingi trilioni tatu na zaidi huko. Kwa hiyo, endelea na mchango wako mzuri Mheshimiwa Mbunge. (Makofi/ Kicheko)

SPIKA: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa Felista.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili. Nikisema hivi hili suala huwa tunapita tu as if hakuna kitu kinachofanyika, lakini Taifa limedidimia kwa kupoteza pesa nyingi nashawishika kusema hapa kuna kamchezo kanachezwa kati ya mlipaji na mlipwaji. Kwa nini nashawishika, kwa nini huu ugonjwa umekuwa ni endelevu wakati mikataba ipo, kwa nini wanavunja mikataba, kwa nini Wakandarasi hawalipwi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wakandarasi hawalipwi na adha hii inatokea na kila mwaka linatokea, huu ugonjwa umekuwa ni endelevu ifike mahali huu mguu wa cancer ukatwe ili mtu awe salama. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hii Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa siku ya leo kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia Sekta hii ya Elimu. Kweli sekta hii ina changamoto nyingi, tunao wasomi wengi nchi hii bado maisha yao ni magumu na wanahitaji support kubwa na kupata ajira katika Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa Jimbo langu la Mbogwe. Wananchi wangu wamenituma na hata mwaka 2021 nilisema hapa kwamba Jimbo la Mbogwe sina Chuo cha VETA. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwenye bajeti yenu kwenye mpango huu nitashika shilingi mpaka mnithibitishie kwamba sasa Mbogwe tunaenda kupata chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu wale wanaosema kuhusiana na mitaala yetu hii ya elimu kweli ni changamoto. Ukiangalia sasa hivi nchi hii tupo wasomi wengi sana na hatuna pa kwenda. Nami niweke mawazo yangu sasa kulingana na kwamba nami ni mfanyabiashara mkubwa, nazunguka nchi mbalimbali. Maana elimu neno la Mungu, linasema, “mkamateni elimu, msimwache aende zake.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli naungana na Mbunge wa Manonga, ukiangalia masomo mengine ambayo tunayasoma, hayana faida katika maisha. Unakaa muda mrefu kufundishwa vitu ambavyo havipo, matokeo yake ni kufeli kila kitu; unafeli kimaisha na unafeli katika masomo yako. Ni vyema sasa Profesa, Waziri uliyeteuliwa mwaka huu, ukae uangalie, tunakutegemea sana kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichangie tu kwamba japokuwa wengine mnaweza mkashindwa kunielewa, Tanzania ni kubwa, tuna makabila zaidi ya 120. Mimi nimezunguka Mataifa mengi, unakuta watu wengine wanatumia lugha yao; ni kwanini wanatumia lugha yao? Maana elimu ni biashara. Unajua elimu ni kuchengana kitu kidogo tu! Nawaomba Wabunge hebu tubadilishe sheria ikiwezekana, maana sasa hivi kila Taifa linafundisha Kiingereza, kila mtu anajua. Utamchenga nani na utafanya biashara gani kuingiza faida katika pato la elimu? Mimi wazo langu tuangalie lugha moja katika makabila 120, lugha ambayo itaonekana ni bora, inafaa tuiingize kwenye system watu waje waisomee.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia China wanatumia lugha yao. Tukienda China huwa tunalazamika kuchukua Mkalimani; ukienda Rwanda huwa kuna wakati wanatumia lugha zao; ukienda Burundi, Angola kuna vipindi hata kwenye vyombo vya habari wanatumia lugha zao na wanapata faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri tu wazi kwamba nilishawahi ku-act siku moja kwamba sijui Kiswahili hata Kiingereza. Nilikuwa Taifa fulani sitaki kulisema, nikajifanya sielewi Kiswahili, nikawa naongea Kisukuma tu, lakini kwa vile nilikuwa na bidhaa ambayo wanaihitaji, kwanza yule Mkalimani alipata hela kutokana nami. Maana alichokuwa anawaambia tu tajiri hajui kiswahili wala Kiingereza. Kwa maana hiyo ililazimika mkalimani na mimi halafu anaenda kuwatafsiria kwamba tajiri anasema mkifika hii bei mzigo tutawauzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi kama Taifa, lazima tukae tufikirie tunawachenga vipi kwenye huu ulimwengu wa mapambano ya kutafuta pesa. Nami niwe muwazi tu, ni Msukuma, lugha yangu mkiipa nafasi tukaweka kwenye system humu. Kisukuma kitaingia kwenye computer na Wachina watakuja kujifunza Kisukuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hata Wazungu wakija kwenye migodi yetu wakakuta siku nyingine askari wanazungumza Kisukuma tu, ile hali itawafanya waweze kusoma.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba sisi tuna wasiwasi labda lugha yetu ya Kiswahili au lugha zetu za Kitanzania hazitaweza kutafsiri yale masomo. Nitoe mfano, hadi sasa umri nilio nao sijawahi kusikia kwamba X + Y itatamkwaje kwenye Kiswahili mpaka leo. Ukimwuliza Mwalimu anakwambia ni unknown. Ina maana mpaka sasa unknown XY mtu anafika Form Six anasoma unknown, kitu asichokijua. Kwa hiyo, labda tuna wasiwasi na lugha yetu ya Kiswahili kwamba hatuwezi kutafsiri haya masomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hiyo taarifa lakini nilichokuwa nataka niombe hili suala ni muhimu sana na Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Elimu siyo suala la kuchekesha, ni suala la kukaa kama Taifa, tukaeni tufikirie ni wapi tulipoangukia maana tuliachiwa elimu na mkoloni, tukakaririshwa baadhi ya vitu ambavyo havipo. Hivyo watoto wetu mpaka leo wanasumbuka kuvisomea lakini kiuhalisia wakitoka mashuleni hautaona sehemu umeulizwa maneno X, sijui nini; yaani kinacho-matter katika siasa na elimu ni jinsi gani unajipambanua kupata hela, kupata mafanikio na kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa kuwa sasa hivi nchi yetu inasifika kwa madini pamoja na bidhaa nyingine, na Tanzania ni Tajiri, ni kitu tu cha kuelewana. Tukikubaliana Wabunge hapa, tuweke lugha gani ili Mataifa mengine yaje yajifunze kwetu ili tupate fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lingine tena katika Wizara hii. Naomba kwa vile yeye ndio Waziri wa Elimu, tumepata kweli misaada mingi kutoka kwa mama yetu; majengo haya tuliyopewa ya UVIKO, lakini upungufu bado ni mkubwa. Ukiangalia haya majengo yametolewa, lakini hayana vyoo wala walimu wa sayansi katika mashule hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uone sasa sababu, na ikiwezekana baada ya Bunge hili, naomba Mheshimiwa Waziri twende kwenye Wilaya yangu tukatembelee uweze kuni-support kwa kuwa mabadiliko ni magumu sana. Kama nilivyotoa ushauri hapa kwamba tuingize lugha nyingine, najua itachukua muda, twende na huu mfumo uliopo. Ni vyema sasa, yaani kila sehemu waweze kupata hii elimu iliyopo pamoja na kwamba wengine tumeshastukia tayari. Baadhi ya Wabunge tumeshastuka kwamba tunakoelekea siko, kwamba hautofautishi mtu aliyesoma na yule ambaye hajasoma ukiwaona wanatembea barabarani au wanasimamia miradi yao tofauti na cheti.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba hivi vyeti wanapomaliza chuo kikuu; nimeona katika ukurasa wa 74 hapa, NMB wametoa Shilingi bilioni 200. Unaonaje Waziri sasa hao waliomaliza elimu ya juu wakapata fursa ya kukopa angalau kujiendeleza katika maisha yao tofauti na hii na kusomea tu? Maana kuna watu wazuri, lakini hawana chanzo, pa kuanzia hawana. Kwa kuwa wana address na wana vyeti, wakopeshwe na mabenki ili waweze kufanya biashara pamoja na kufanya vitu vingine. Maana tukiangalia katika soko la ajira na kwenyewe ni changamoto, hatuwezi kuajiri watu wote hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aangalie sasa katika takwimu waliomaliza mwaka 2021 na mwaka 2020, wangapi wakopeshwe waweze kuendeleza maisha yao? Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili na mimi niweze kuzungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbogwe Mkoani Geita ili niweze kuwasilisha mawazo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuwasilisha mawazo ya wana Mbogwe. Kwa vile muda sio rafiki sana naomba niende haraka haraka, lakini ikikupendeza uniongeze kwa sababu ni mara ya pili tu toka Bunge lianze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uwezo wa kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu kuweza kuwasilisha mawazo ya wananchi. Namshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazozifanya kwenye Taifa letu la Tanzania. Najua nguzo kubwa sasa hivi ni mkataba, wananchi wangu wangependa nilielezee suala la mkataba ambalo linagonga kichwa, kila mtu anajiuliza ni nini hatima yake, lakini muda hautoshi. Niwaombe wananchi wangu wa Mbogwe ninakuja mwezi wa saba, tutakuja tufafanuliane na tuelimishane vizuri kuhusiana na hilo suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwatoe wasiwasi, hakuna kitu cha kuharibika mbele ya Mama yetu ambaye ni Amiri Jeshi wetu Mkuu. Kwa hiyo Watanzania muwe na imani kabisa, kwamba nchi iko salama, na bandari haijauzwa. Hayo maneno mnayoambiwa mitaani yapuuzeni, hakuna kitu kama hicho, wala kufikiria suala kama hilo. Na mimi mwakilishi wenu mliniamini na endeleeni kuniamini hivyo hivyo, na mimi ninasimama kwa ajili yenu kuhakikisha kwamba hakuna jambo la kuharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwako, Waziri wa Fedha. Kwanza nikupongeze sana kaka yangu, wewe ni Waziri wa Fedha, ni sekta ambayo ni ngumu kuliko Wizara zote, maana wewe ndiwe umeshikilia fedha. Nikuombee tu kwa Mwenyezi Mungu. Mawe unayopigwa endelea kuvumilia. Hata Yesu alipigwa, wengine walisema alikuwa mwizi wa mbao lakini ki ukweli alikuwa anaponya watu. Kwa hiyo na wewe simama kuhakikisha kwamba Taifa letu tunakwenda vizuri na tuweze kukidhi mahitaji ya watu wetu waliotuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri mambo mawili makubwa. Nimeona kwenye mpango huu Mheshimiwa Waziri amedhamiria kwenda kumwongezea mchimbaji asilimia mbili, naomba hiyo hebu aiache, maana itatuletea kero ambayo haitaisha tena; kwa sababu mpaka sasa hivi wanalipa rate ya asilimia saba lakini vile vile wachimbaji hawa wanakabiliwa na service levy, kwa hiyo ukiweka asilimia mbili tena itakuwa asilimia 9.3. Hii nikumwongezea mzigo mchimbaji na kumuumiza kumtoa barabarani na kusababisha utoroshwaji tena wa madini uendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2017, lengo la kuweka asilimia saba lilikuwa kwamba ninyi Serikali mtajuana huko; nne itaenda madini tatu itaenda TRA. Kwa hiyo hata sasa hivi niwaombe Serikali, kwa kuwa ni wamoja kaeni kwa ajili ya kutupunguzia adha au balaa wale tunaoishi kwenye maeneo ya madini. Muwe mnagawana tu humo kwenye asilimia saba, mtakuwa mnajua wenyewe hii inaenda TRA, hii inaenda madini ili watu waendelee kuzalisha dhahabu na kuchimba na wao waweze kutoka kwenye wimbi la umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili napenda nikushauri Mheshimiwa Waziri, kwenye suala la mafuta kuongezea tena shilingi mia moja, na lenyewe mimi nisingependa iongezeke hiyo shilingi mia moja, itoe. Tunavyo vyanzo vingi vya mapato kwenye Taifa hili ikiwemo Sheria tuliyopitisha ya miamala, najua ni trilioni nyingi tu tutaingiza kama usimamizi ni mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile bandarini pale mpaka sasa hivi kuna wafanyabiashara tuna ushahidi kabisa hawatoi hata risiti. Weka usimamizi mzuri kwenye maduka hayo makubwa ya Kariakoo ili watu waweze kuchangia Pato la Taifa. Nina imani hauta-fail popote pale nakuomba sana kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kwa kuwa hii ni bajeti kuu nizungumzie upande wa maliasili. Ninalo pori pale Mkweni wananchi wangu wanakaa kwa kubanana. Kwenye ahadi zetu kwenye Ilani, tulifanya mikutano mingi tukawaaminisha watu kwamba tutatenga maeneo kwa ajili ya kuchungia ng’ombe. Nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii atenge muda na siku aje anitembelee Wilayani Mbogwe aje alione hilo pori la Kigosi ambalo halina faida kabisa, maana hata wanyama walikwisha, sifa za kuwa pori ilikwishaisha, matokeo yake limekuwa pori la kusulubisha watu, kukamata watu wauza mikaa pamoja na watu wengine. Kwa hiyo niombe tutakapolimaliza Bunge hili Mheshimiwa Mchengerwa aje anitembelee kwenye Wilaya yangu ili kusudi tuangalia hayo maeneo tuweze kuwafungulia wananchi tuweze kuchungia maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niguse Wizara ya ujenzi. Tunazo barabara ambazo walitutengenezea kweli mwaka jana lakini mvua zimenyesha hizo barabara zimeharibika. Nakumbuka mwaka 2021 nilimuomba kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwamba kwenye bajeti zake hizi aniruhusu kwenye halmashauri yangu ninunue caterpillar. Nimeandika andiko maalum naomba ani-support kaka yangu kwenye Wizara yake ya Fedha, twende tukanunue grader ili barabara zinapokatika mvua zinaponyesha tuwe na uwezo wa kutengeneza barabara wenyewe kuliko kusubiria masuala ya bajeti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: … bao kuna matatizo makubwa kusubiria hizi bajeti, mvua zinaponyesha barabara zinakatika wananchi wanashindwa kupita, matokeo yake wanamuona Mbunge hafai, Rais hafai, chama hakifai lakini kumbe dhamira ni nzuri…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nicodemas Maganga, ahsante sana.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: …nitengee hii bajeti na andiko langu unipitishie Wizarani ili kusudi niweze kununua caterpillar. Baada ya kusema hayo machache na mengi nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na fursa hii

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mdogo naomba nijikite kushauri tu kwa maneno machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia katika hotuba hii ya Waziri yote, na ninaomba nishauri mambo machache. Waziri aangalie kumlenga mwananchi mnyonge wa hali ya chini katika bajeti hii ya Shilingi milioni 751. Nakuomba rafiki yangu pamoja na Naibu Waziri Mavunde, msipoangalia hizi fedha zinaenda kuishia kwenye mikono ya watu wachache, hazitamsaidia mwananchi yule wa kawaida anayelima kwa jembe la mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, hisia za Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wote, pamoja na hotuba zote tukiwa kwenye kampeni mwaka 2020 tuliahidi kwamba tutawasaidia wanyonge. Nakuomba Waziri kupitia ubunifu uliouunda kutengeneza kombati pamoja na mavazi special kwa ajili ya mkulima, ufuate mfumo huo huo, tengeneza programu nyingine, acha kutegemea mabenki. Wakulima huwa hawana akaunti benki, lazima ulijue hilo. Wazazi wetu hawana akaunti benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia mkulima, lazima umfikirie mkulima yule wa hali ya chini. Unaenda kumwezeshaje aliye na jembe la sheli ya ng’ombe? Unaenda kumwezasheje yule anayelima kwa jembe la mkono? Mheshimiwa Waziri fikiria mambo kama yale, tutaonekana watu wa maana, washauri wazuri, ukifuata ushauri wangu huu wa mwishoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kule Mbogwe ninazo sehemu nyingi sana, sioni hata sababu ya kufanya utafiti. Kitu kikubwa sana sana huwa ni mvua tu. Mheshimiwa Waziri sijui unanisikia! Sijui umeangalia pembeni! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa, naomba aje na Mpango, Wilaya ya Mbogwe ananisaidiaje? Ninazo Mbuga kubwa ambazo zinahitaji scheme, ukinisaidia skimu hata 20 hutasikia njaa katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nikupongeze tu Mheshimiwa Waziri, mwaka 2021 ukiwa Naibu Waziri nilikuja kwako nikalia kuhusu kiwanda changu cha Kagiri kile ulichokuja kukiangalia na kukifungua. Ulinipatia Shilingi bilioni sita na mwenyewe umeyaona matokeo, tumeingiza faida pamoja na wanakulima wanapewa ruzuku. Mwaka huu tumeandika andiko, tunataka Shilingi bilioni 13, tunataka tuzalishe mafuta wenyewe ya pamba pale Mazumbwe Kagiri na tunataka tuzalishe mafuta ya alizeti. Usisite. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara na wakulima tunajuana, ukisema unahitaji kusaidia wakulima kupitia Jeshi lile uliloligawia pikipiki, sasa hivi wanawajua wakulima. Usiangalie watu wanaokimbia sasa hivi kusajili makampuni, wanakuja kukuangusha hao Waziri, waepuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiria mwaka 1992 katika utawala wa Rais Mwinyi, tulikuwa tukiletewa mbegu za pamba mpaka Kijijini. Sasa hivi mnashindwaje kutuletea moja kwa moja mbegu za pamba, tukalima pamba na tukafaidika? Kwa nini mnapitia Mawakala? Mheshimiwa Waziri hebu jaribu kulifikiria hilo. Wewe uzuri umezaliwa kwetu huko, unajua maisha ya Kijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha naomba zisiishie mjini, zisiende kwa watu wenye makampuni ya mjini. Wakulima walio wengi huwa hawana akaunti. Utaweka akaunti vipi wakati wewe ni Mkulima! Kwa hiyo, kupitia watu wako wale uliowapa pikipiki Mheshimiwa Waziri, wewe kaa nao, waulize huko una wakulima wangapi; ili uweze kuwasaidia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango wako mzuri.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. Mchango mwingine nitaandika kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia Wizara hii ya Fedha.

Mheshsimiwa Spika, jambo la kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii adimu kuweza kuchangia Wizara ya Fedha ambayo inadai shilingi trilioni 14.94. Nimejaribu kuangalia mchanganuo pamoja na Mheshimiwa Waziri kweli mimi sina mashaka kulingana na mchanganuo jinsi nilivyouona hapa kwenye hotuba ya Waziri.

Mheshimiwa Spika, lakini napenda muda wangu huu kuishauri Serikali kama zilivyo kanuni, taratibu na sheria zetu kwamba Mbunge ni mtunga sheria, halafu ni mshauri wa Serikali. Walipakodi nchi hii wanaolipa ni wachache sana, nakuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwanza kwenye Wilaya yangu mnisaidie nipate Ofisi ya Mamlaka ya TRA ili wafanyabishara waweze kupata huduma karibu. (Makofi)

Mhehsimiwa Spika, ukiangalia Mkoa wa Geita sehemu nyingi hazina Ofisi za TRA, pale Mbogwe Ofisi ilishakamilika lakini bado haijafunguliwa. Kwa hiyo nikuombe Waziri ulichukue hili na uweze kunijibu kule mwishoni utakapotoa ufafanuzi wako kwamba sasa Mbogwe inaenda kufunguliwa Ofisi ya TRA ili kusudi wanaeonda zaidi ya kilometa 40 kwenda Bukombe kwenda kulipa kodi waweze kulipia karibu.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, mwaka jana nilisimama hapa, Naibu Waziri wa Fedha alikuwa Mheshimiwa Masauni nilikuwa nawalilia sana wafanyabiashara jinsi walivyokuwa wanapambana na TRA, lakini kwa sasa hivi bila unafiki kwa kweli kumekuwa na mazungumzo na makubaliano mazuri kwenye upande wa TRA.

Kwa hiyo nimpongeze Mkurugenzi wa TRA pamoja na Makatibu Wakuu wa TRA, najua mmeajiri vijana wengi katika sekta hii, niiombe Wizara hii sasa ijitahidi kuwapa mafunzo ili kusudi watakapoenda kwa wateja wetu, wananchi wetu, wafanyabiashara wetu wawe na kauli nzuri ili kuweza kuwafanya watu walipe kwa hiyari kama Rais anavyotaka maana nia ya Rais ni kumuona kila Mtanzania anafurahi, analipa kodi bila kusumbuliwa, watu wasivamiwe kama zamani walivyokuwa wakinyang’anywa na kufungiwa akaunti zao na kwa kweli mimi nikiri wazi tu nimetembea Taifa jirani hapa, kodi wakati ikifika mtu anaenda kabisa kulipa mwenyewe bila hata kufuatwa. Na neno la kodi hili ukiangalia hata kwenye maandiko matakatifu ni itu ambacho kipo halali. Kwa maana hiyo hapo hakuna maswali sana.

Kwa hiyo, tuombe tu hawa mliowaajiri muwape mafunzo ili wasije na munkari na morali za kutoka huko chuoni wakaanza tena kusumbua wananchi wetu na kutochonganisha tena nikawa mchango wangu huu leo nimeomba Ofisi ya TRA halafu wananchi wakaanza kukamatwa na kusumbuliwa, hapo nitakurudia Mheshimiwa Waziri kwa vile wapo chini yako. (Makofi)

Lakini ajenda ya pili nilete malalamiko ya wafanyabiashara hapa nchini, haya mabenki ya ndani yanawakanyaga sana wafanyabiashara wa ndani hapa. Tukiangalia tumetoka kwenye hili suala la corona, mfano kuna watu waliagiza mizigo yao China, kuna watu waliagiza mizigo yao mataifa mbalimbali, lakini wafanyabiashara hao wamekopa katika haya mabenki. Mabenki yameshinda kuwasikiliza, kuwapunguzia riba na kipindi naingia hapa Bungeni hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano alitoa maelekezo kabisa kwamba riba zipungue kwenye mabenki. Lakini pia hata Mama Samia Suluhu Hassan wakati analihutubia Bunge hapa suala la riba aliliongelea hapa Bungeni kwamba riba zipungue. Waziri hizi taasisi zipo chini yako, unafeli wapi? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Waziri ana mamlaka ya kuweza hata kufuta leseni ya hizi benki, maana kweli wanasiasa wengi sasa hivi wanasimama wanasema nchi imefunguliwa, lakini kufunguliwa kwa nchi inaweza ikawa maumivu kwetu sasa. Kama sisi tunapigwa riba za juu wa ndani, halafu mgeni akija anapoozewa riba, inafunguliwaje hapo nchi? Si sisi sasa tumefungwa, wamefunguliwa wa nje! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe Waziri hili lichukulie serious sana, wafanyabiashara wa ndani wanaumia sana, halafu mbaya zaidi hizi taasisi za kifedha hazina kauli kwa wafanyabiashara wa ndani vizuri. Haziwavumilii kwa mfano mtu amerejesha marejesho tisa, bado marejesho matatu tu unaenda kukamata nyumba yake, unaenda kumfilisi, ina maana ulimpa mkopo huo umsaidie au kumfilisi hiyo nyumba aliyonayo?

Mheshimiwa Waziri kwa vile leo nimepata nafasi hii, nakushauri sana Rafiki yangu na nanakupenda sana na mtu anayekupenda ni lazima akueleze ukweli bila kukupongeza pongeza maana yake mtu anaweza akawa anakupa pongezi kumbe anategemea umpe chochote. Mimi ninakushauri kwa vile ni jamaa yangu najua ndoto zako bado Taifa tunakutegea sana. Kwa hiyo, livalie njuga hili na haya ya mabenki ya ndani yaweze kupunguza riba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri wa Kilimo alielekeza mabenki yatoe asilimia tisa tu kwenye kilimo, naona kama kwenyewe kunawezekana. Sasa huku kwingine kunashindikana vipi? Rais wa Kwanza alishasema na wa Awamu ya Sita alishasema riba zipungue, hazipungui. Futa leseni, zitasajiliwa benki nyingine tutakuja kufanya nazo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka nizungumzie hapa hali halisi ya maisha ya Watanzania wale wa kawaida. Kweli tunasema kwamba hali sasa hivi ina unafuu lakini bado hali ni ngumu. Sasa wewe kwa vile ni Waziri wa Fedha, angalia kama kuna sehemu yoyote fungulia fedha ili kusudi zifunguke hata kwa wanyonge zijae mifukoni, maana kwenye kampeni huwa tunasema tunawapigania wanyonge, sasa wanyonge hawajapata fedha bado, ninaangalia tunaenda mwishoni mwishoni bado kuna Bajeti Kuu, na kwenyewe niombe viongozi mnipe nafasi niweze kuruka vizuri na kuweka mchango wangu vizuri maana ninayo mambo mengi, maana sikupata nafasi ya kuchangia Wizara nyingi sana, lakini zipo Wizara ninahitaji nipate nafasi ya kuweza kuwasemea wananchi wangu wa Jimbo la Mbogwe.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo sasa nikuombe Waziri wa Fedha kwa kuwa leo tupo Wizara hii ya Fedha kama kuna uwezekano wowote ule kufungulia mahali popote pale, fedha zifunguke ili kusudi hata na wananchi wangionge nao waende wakanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa jitihada mnazozifanya, tumeona kwa watumishi mmeongeza mishahara, watumishi kwa kweli wanafurahi, walimu sasa hivi kila mwalimu anachekelea, watumishi mbalimbali wanafurahia kwa ongezeko hilo la asilimia 23.3 lakini wapo wengine ambao hawana nafasi ya kuweza kuingia kwenye manufaa haya. Kwa hiyo, ni vyema Waziri kwa vile ni msomi mzuri ujaribu kufikiria jinsi gani unaenda kulisaidia Taifa ili kila mtu apate haki yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. NICODEMUS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, yes naomba kumalizia, mimi nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, maana nafasi ni ngumu sana kuzipata humu ndani, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo ili niweze kuchangia hii Ripoti ya CAG pamoja na Kamati zilizowasilishwa juzi hapa upotevu wa mabilioni uliopatikana katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukupongeza kuchaguliwa kuwa Rais wa Mabunge Duniani, Mungu akubariki sana na akuongoze, akupiganie katika utumishi wako, wanawake wenzako uwaonyeshe mfano kwamba wanawake kweli mnaweza, kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutuchagulia Makonda kuwa Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi. Nampongeza kwa roho ya dhati kabisa, tunamuona Makonda anavyopambana na sisi vijana niseme kwa niaba ya vijana wote Taifa hili tunamuunga mkono Makonda.

Mheshimiwa Spika, Makonda ameanza na Baraza la Mawaziri, ni kwa nini? Ni swali la kujiuliza kama ni mtu mwenye akili timamu. Ni kwa nini ameanza na Baraza la Mawaziri? Kama kweli ni hoja ya Kamati Kuu yote ile ya CCM naipongeza sana.

Mheshimiwa Spika, kiukweli kila nitakapopata nafasi kusema, nitakuwa nasema ukweli tu. Sitaki siasa za kibabaishaji na bora niache kuchaguliwa ila nimesema ukweli na siku nikifa nitaenda mbinguni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikupe taarifa tu kwamba, mpaka jana tumefika Wabunge 168 ambao tumekubaliana kwa pamoja kabisa tutengeneze mpango tupitishe sheria ya kunyonga watu. Tunaangalia mataifa yaliyoendelea, mengine yanatupa misaada na wanazo hizo sheria, ni kwa nini waliweka hizo sheria, watu ni wagumu, watu hawaelewi kabisa, watu huwezi ukawapeleka mahakamani tu na kulipa pesa hizi ambazo wameshaiba. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sio maigizo ni suala ambalo limeorodheshwa humu na CAG. Wezi wote wanajulikana na mimi ninamuomba Mungu nisije nikaponyoka nikaanza kuwataja kwa sababu wanafahamika wezi waliotuibia kwenye hili Taifa.

Mheshimiwa Spika, isipokuwa ninaomba Mungu anisaidie sana nitumie nafasi yangu ya Ubunge kuishauri Serikali. Wananchi wana kilio kikubwa sana. Wanateseka na michango ya kila aina. Ukifuatilia michango wanayochangisha wananchi unakuta kuna shilingi bilioni 11 ambazo zimepotelea kwenye POS. Ninampongeza Mheshimiwa Halima juzi alitusomea hapa kwa wenye weledi mkubwa. Ametaja mpaka na majina ya halmashauri zilizotumika kuiba hizi shilingi bilioni 11. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimsapoti sana Mheshimiwa Simbachawene. Unajua mtu akiongea ukweli wakati mwingine anachukiwa na watu. Jana Mheshimiwa Simbachawene uliongea jambo la ukweli kabisa. Sisi Wabunge kwenye mabaraza ya Madiwani ni wajumbe wa Kamati za Fedha, ninaiomba Serikali hata chama kiwe na muda wa kuwauliza Wabunge kwanza, wewe kwenye halmashauri yako umefanya nini? Kila Mbunge ajieleze hadharani, mpaka upotevu wa fedha unapatikana wewe ulishauri nini kama Mbunge? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ukisoma hii Katiba inajieleza baina kabisa kwamba, Mbunge ni mtu wa aina gani, anatakiwa afanye majukumu gani. Humu tuna hatari, tuna Wabunge wasiojielewa wanasubiria siku ya kuja kulalamika hapa mbele yako. Lakini niwasemee kidogo wale watumishi wanaoisimamia Serikali. Wapo watumishi wengine wana roho ya dhati kuitumikia nchi yao, lakini Serikali Kuu mnawakatisha tamaa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, unakuta mtumishi anafanya kazi halipwi mshahara. Ukiangalia hapa kuna shilingi bilioni zaidi ya 11.998 hii ni malimbikizo watu hawalipwi mshahara mpaka zimefika hizi pesa. Hata kama ni wewe lazima ufikirie, mtu anafanya kazi, mlishakubaliana nae kumlipa mshahara, hammlipi, mnampelekea pesa nyingi za miradi ya maendeleo, hana pesa ya kula nyumbani, matokeo yake afanye nini? Lazima aibe, mimi hapo ndiyo maoni yangu.

Mheshimiwa Spika, shilingi bilioni 11.9 ninaiomba Serikali, kwanza watumishi hawa wana mishahara midogo, ione kila sababu ya kuweza kuwalipa watumishi hawa ili wawe na moyo ule wa kufanya kazi zao kama walivyopangiwa kwenye mikataba yao.

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumzie hili, tuna hawa wazabuni wa ndani, kilio ni kikubwa sana kwa wafanyabiashara. Wamenituma Wafanyabishara kujaribu kuishauri Serikali. Kuna wafanyabiashara wameikopesha Serikali, wengine wamekopesha sementi, wengine mafundi wamefanya kazi kwenye shughuli za Serikali wakiamini kwamba hii Serikali ina pesa, hawalipwi. Niwaombe wasimamizi wote wa Serikali waweze kuwanea huruma hao wazabuni ili waweze kulipwa fedha zao.

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kumpongeza Makonda na nimuombe Makonda andelee kuwa na msimamo wa hivyo hivyo, asirudi nyuma na sisi tupo nyuma yake. Tutampa ushirikiano wa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kweli anakuwa akifanya ziara tunamuona, juzi alikuwa Bukoba tulimuona, juzi amefanya kikao kwenye vyombo vya habari tukamuona, anakemea wezi lakini siwapongezi Mawaziri wale ambao wapo special kumpongeza Mheshimiwa Rais. Ukiangalia kwenye ndimi zao special kumpongeza Mheshimiwa Rais tu. Tukiwauliza wao wamefanya shughuli gani, tukitoa shughuli za Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa lakini sisi wanasiasa huwa tunasema mwisho lakini hoja nyingine zinakuja. Kwenye upande wa mchanga wa ujenzi, Serikali iliweka ushuru wa madini ujenzi. Wananchi wa Mkoa wa Geita wameniomba sana, halmashauri zinazoanzishwa sasa hivi zinashidwa kuendelea kujengwa kwa sababu ya huu ushuru wa madini ujenzi. Serikali iachane na huo ushuru kwa sababu, huo mchanga hauna madini, huo mchanga hauna madini kabisa toka miaka ya nyuma watu walikuwa wakichota bure na matela yao. Kuna wengine walikuwa wana miradi ya matela. Walikuwa wakisomba mchanga wanauza trip moja shilingi elfu tano. Wanajipatia fedha.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wameshapaki matoroli yao kwa ajili ya huo ushuru ni mkubwa, unawasababisha wasiendelee na biashara yao ya mchanga. Serikali iondoe huo ushuru ili kusudi mchanga ambao hauna madini watu waweze kuchota bure, waweze kujenga halmashauri zao.

Mheshimiwa Spika, narudia kukushukuru tena wewe kwa sababu nikiendelea kuzungumza mimi kadri hasira zinavyopanda na wezi waliotoajwa humu na CAG wanajulikana naogopa nisiharibu mchango wangu. Niwaombe tu Wabunge wenzangu wote wale waliobaki kujiorodhesha kwenye hii sheria tunayotaka kuipitisha ya kunyonga, waorodheshe kama na wao sio majambazi, ila kama ni majambazi wanaogopa wasinyongwe basi wasitupe ushirikiano.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mungu akubariki sana. (Makofi)