Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Lujuo Monni (12 total)

MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. MOHAMED L. MONNI Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga stendi katika Mji wa Chemba ambao unakuwa kwa kasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Wilaya ya Chemba kuwa na kituo cha kisasa cha mabasi. Kwa umuhimu huo Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga eneo la ekari 22 kwa ajili ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi katika Mji wa Chemba ambayo imekadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 643.8 mpaka kukamilika kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Halmashauri ilitenga kiasi cha shilingi milioni 37 kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo ambapo ujenzi wa vyoo na ofisi za muda umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni saba ili kuwezesha wananchi kuanza kupata huduma za stendi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 16 ili kuendeleza ujenzi wa stendi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati unahusisha andiko maalum la mradi linaloandaliwa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kufuata utaratibu huo ili Serikali itafute fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni- Kiberashi-Kiteto – Mrijo – Chemba – Kwa mtoro hadi Singida kwa kiwango cha lami kwa kuwa ipo kwenye Ilani na pia Ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujua Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Handeni – Kiberashi – Kwa mtoro – Singida ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 461. Kati ya urefu huo, kilometa 111 zipo Mkoa wa Manyara, kilometa 171 Mkoa wa Dodoma na kilometa 47.1 Mkoa wa Singida. Barabara hii nikiunganisha muhimu cha Mikoa ya Singida, Manyara, Dodoma na Kanda ya Pwani hasa bandari ya Tanga na Dar es salaam. Kukamilika kwa barabara hii kutapunguza idadi ya magari ya nayopita katika barabara kuu ya kati Central Corridor kuelekea Kanda ya Kati na Kanda ya ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), imekamilisha Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara hii. Kwa sasa Serikali ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Katika Mwaka wa Fedha 2021 jumla ya Shilingi bilioni 6 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2021/22 barabara hii itazingatiwa.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, ni lini Barabara ya Kwamtoro – Sanzawa – Mpendo yenye kilomita 58.2 itajengwa kwa kiwango cha kupitika msimu mzima kwani kwa sasa imekatika kutokana na mvua kubwa na kutojengwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/ 2021, TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga shilingi milioni 84.04 kwa ajili ya matengenezo ya Barabara ya Kwamtoro – Sanzawa – Mpendo yenye urefu wa kilomita 23. Ujenzi wa barabara hii unaendelea ambapo matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 10, makalvati mawili na drift moja umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 42 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 10 na ujenzi wa makalavati matatu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na kazi nyingine Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini, umepanga kufanya tathmini ya miundombinu ya barabara zake zote ikiwemo za Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ili kuandaa mpango wa namna bora ya kutoa vipaumbele vya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ikiwemo ya barabara ya Kwamtoro – Sanzawa –Mpendo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuimarisha usafiri na usafirishaji.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa Watumishi waliohamishiwa katika Halmashauri ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilianzishwa rasmi tarehe Mosi Julai, 2013, baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kugawanywa. Jumla ya watumishi 90 wa idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, walihamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ambao walistahili kulipwa kiasi cha Shilingi milioni 238.7 ikiwa ni stahiki zao za kiutumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilihakiki madeni ya watumishi hao na kuwasilisha Serikali Kuu maombi ya kulipwa madeni hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba katika mwaka wa fedha 2023/2024, itatenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kulipa madeni hayo. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti za kila mwaka ili kuendelea kulipa madeni hayo.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya ujenzi wa Bwawa katika Mji wa Itolwa, Kata ya Jangalo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikamilisha utafiti wa ujenzi wa bwawa la mita za ujazo 106,100 katika Kijiji cha Itolwa Wilayani Chemba. Gharama za ujenzi wa bwawa hilo ni shilingi bilioni 1.7 na katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bwawa hilo. Maji yatakayohifadhiwa katika Bwawa la Itolwa yatatosheleza mahitaji ya wakazi wa Kijiji cha Itolwa.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba uliokwama kwenye ngazi ya lenta kwa miaka mitatu sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba ulianza mwezi Novemba mwaka 2018. Gharama za jumla za ujenzi huu ni Sh.296,000,000. Ujenzi huo umeshirikisha nguvu za wananchi pamoja na Mdau aitwaye Local Investment Climate ambaye alitoa kiasi cha Sh.43,000,000. Ujenzi umefikia kwenye hatua ya lenta na ulisimama kutokana na kukosekana kwa fedha. Kiasi cha Sh.53,000,000 tayari kimeombwa kwenye mfuko wa tuzo na tozo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili kumalizia ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga barabara ya Kwamtoro - Sanzawa hadi Mpendo katika Wilaya ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya marekebisho ya kipande cha Sanzawa – Mpendo chenye urefu wa kilomita 38.2 ambapo shilingi bilioni 2.06 zinahitajika. Serikali imeendelea kuihudumia barabara hiyo ambapo mwaka wa fedha wa 2022/2023 shilingi milioni 48 zimepelekwa kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi yenye urefu wa kilomita Nane kati ya Kwamtoro na Sanzawa katika Vijiji vya Kurio na Moto. Aidha, ukarabati wa box culvert katika Kijiji cha Moto umekamilika. Kwa sasa Mkandarasi anafanya maandalizi ya kuchonga barabara eneo korofi la Kurio lenye urefu wa kilomita Tatu.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, serikali itatenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza kufanya matengenezo kwenye eneo korofi la mawe kati ya Sanzawa na Mpendo lenye urefu wa kilometa 34.2.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za Jimbo la Chemba kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha usafiri na usafirishaji.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Kijiji cha Kalema Maziwani linalounganisha Wilaya za Kiteto, Chemba na Kondoa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujenga upya Daraja la Kalema Maziwani katika barabara ya Kondoa – Bicha – Dalai ambalo lilititia kutokana na mvua kubwa za mwaka 2019. Ili kujenga daraja hilo mnamo tarehe 19 Mei, 2023 Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi na zabuni hizo zimepangwa kufunguliwa Tarehe 05 Juni, 2023, ahsante.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme katika Vijiji vya Chemba?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ambapo, vijiji vyote ambavyo havina umeme Tanzania Bara vitafikiwa na huduma ya umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Chemba, Mkandarasi M/s Sagemcom Limited alipewa jumla ya vijiji 59 ambavyo havikuwa na umeme. Hadi kufikia tarehe 15 Agosti, 2023, vijiji 47 vimeshawashiwa umeme na vijiji 12 viko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na vitakamilika kabla ya mkataba wa mkandarasi kuisha tarehe 31 Oktoba, 2023.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaongeza madaktari na watumishi wa kada nyingine katika Kituo cha Afya Mrijo chenye Daktari na Nesi mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilipata kibali cha ajira na kuajiri Watumishi wa Kada ya Afya 7,340 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ilipatiwa Watumishi 87. Kati ya hao, Watumishi wawili walipelekwa kwenye Kituo cha Afya Mrijo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeajiri Watumishi wa Kada za Afya 8,000, ambapo Halmashauri ya Wilaya Chemba nayo imepatiwa Watumishi wa Afya ambao watapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya ukarabati wa miundombinu ya maji iliyochakaa na kusababisha upungufu wa maji – Chemba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inafahamu changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya maji katika Wilaya ya Chemba na imeanza kuchukuwa hatua kwa Vijiji vya Humekwa na Mlongia ambapo manunuzi ya vifaa kwa ajili ya ukarabati yanaendelea. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itafanya usanifu na kufanya ukarabati wa miradi ya maji kwa Vijiji vya Njoeni Muone, Mtakuja, Bugenika, Msera, Mengu, Pangalua, Wahilo, Wisuzaje, Msaada na Mwailanje. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya zahanati ya Kimu, Rofat, Tumbakose, Songolo na Sori Wilayani Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepeleka shilingi milioni 260 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati 6 za Jangalo, Wairo, Humekwa, Makamaka na Ombiri. Ujenzi wa zahanati hizi umefikia hatua za umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha Zahanati za Nkulari, Nkikima, Mlongia na Handa. Aidha, ujezi wa maboma ya zahanati ya Rofat, Tumbakose na Songolo ambazo zinajengwa kwa nguvu za wananchi bado hazijafika hatua ya lenta ili kupata fedha ya Serikali kwa ajili ya ukamilishaji.