Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mohamed Lujuo Monni (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya upendeleo kabisa maana nimeomba muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba niseme maneno yafuatayo. Nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye muda wote amenipa uhai na afya ya kuwa hapa. Pili, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Chemba kwa kunipa kura nyingi za kutosha. Tatu, kwa sababu ya muda nakishukuru Chama cha Mapinduzi kwa kunipa uteuzi na hatimaye kuwa Mbunge na leo niko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nichangie kidogo kwenye elimu. Naishukuru Serikali sana kwa sababu ya elimu bure. Hata hivyo, zipo changamoto ambazo zimesababishwa na elimu bure na moja kubwa ni miundombinu. Tumekuwa na idadi kubwa sana ya wanafunzi wanaoingia kila mwaka. Changamoto ambayo tunapata hasa zile Halmashauri ambazo hazina uwezo kuna matamko yanakuja kwamba lazima muwe na madarasa, madawati lakini Halmashauri zenyewe hazina uwezo wa kujenga madarasa lakini pia hazina uwezo wa kununua madawati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mmoja wa athari ambazo zinatokana na haya matamko. Miaka mitatu au minne iliyopita Halmashauri ya Chemba ililazimika kutumia fedha zote za own sources kuhakikisha inanunua madawati lakini mpaka leo tunadaiwa kila mahali. CRDB wanatudai, watu walio-supply vyuma wanatudai toka mwaka 2016 mpaka leo. Sasa mimi nafikiria lazima kuwa na mpango maalum wa kuhakikisha tunakuwa na mfuko ambao au kuwa na mkakati wa kuhakikisha Serikali inachangia kwenye zile Halmashauri ambazo hazina uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo sio rahisi sana lina madhara makubwa sana kwa Halmashauri hizi mpya. Ziko Halmashauri zina uwezo zinakusanya shilingi bilioni 9 mpaka 12 kwa mwaka hata ukiwaambia wajenge hospitali wanaweza! Sasa tumekuwa na changamoto kubwa sana hiyo. Naomba sana Serikali iangalie namna bora kwenye hizi Halmashauri ambazo hazina uwezo wasitamke tu, tutafukuza Wakurugenzi, ma-DC lakini ukweli ni kwamba fedha hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano wa hali iliyotokea na sasa hivi ni hivyo hivyo. Sasa hivi tumeambiwa tujenge madarasa, tununue madawati, Halmashauri yangu zaidi ya asilimia 40 watoto wanakaa chini. Tungependa kila mtoto akae kwenye dawati lakini mimi Mbunge nina uwezo wa kununua madawati ya shule zote za Halmashauri? Haiwezekani! Tumeaambiwa tununue madawati, fedha hakuna na ni kweli fedha hakuna, nini cha kufanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopanga hii mipango lazima i-reflect hali halisi iliyopo huko. Tusipofanya hivyo mipango yetu itakuwa tunaongea tu. Bahati nzuri niseme ukweli kwamba nimesikia michango mizuri sana ya Wabunge, nilikuwa nafikiria tofauti na hali sasa sijui kama Mawaziri wanachukua hiyo mipango inayoelezwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba niongee kuhusu kilimo. Mimi ni mkulima mzuri kabisa. Hata tunayoyaongea kwamba tumetumia shilingi bilioni 180 kwenye kilimo mimi ambaye ni mkulima mkubwa pale Chemba sijawahi kuona kitu hicho. Pia huo mkakati wetu wa kilimo ukoje? Mimi mwenyewe nikilima hata kutafuta soko mpaka niende Nairobi, sijawahi kuona Afisa Kilimo wala mtu yeyote anayenifuta kuniuliza sasa ndugu yangu umelima tufanye ABC, changamoto kubwa ni masoko ya mazao haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni kubwa mno. Tunaongelea kulima, tunaongelea kilimo cha umwagiliaji, Jimbo tu maji ya kunywa hawana, sasa huu umwagiliaji utakuwaje? Hatuna uwezo wa kujenga mabwawa ili tupate maji ya kunywa halafu tunafikiria tujenge kwanza mabwawa kwa ajili ya kilimo. Hii inanipa changamoto kwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali na wakati mwingine najiuliza hivi nani ana wajibu wa kutafuta soko la mazao tunayolima? Tunasema asilimia 75 ni wakulima, mimi nalima lakini watu wengi walioko vijijini, leo utasikia gunia la ufuta Sh.90,000 lakini kesho Sh.40,000.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kuchangia naomba niseme maneno machache. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ambaye amekuwa akitupa uhai na afya njema ya kuendelea kuwatumikia Watanzania. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ameanza vizuri na tuna uhakika wa asilimia zote yale ambayo tumeahidi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi yatatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba mimi nianze kuchangia. Kwanza kabisa nataka nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Hotuba hii imegusa kila eneo, lakini kwangu imekuwa nzuri zaidi kwasababu ameeleza namna gani tunaenda kujenga lile Bwawa la Farkwa. Mradi huu wa Bwawa la Farkwa ndio mradi peke yake ambao unaenda kumaliza matatizo yote ya maji kwenye Jiji letu la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati nzuri mradi huu ukitekelezwa hautamaliza tu changamoto za maji kwenye Jiji la Dodoma, utamaliza pia kwenye wilaya zetu zote za Mkoa wa Dodoma. Bahati nzuri sana Waziri Mkuu mwenyewe ametembelea kwenye huu mradi na yapo maelekezo ambayo aliyatoa, lakini bahati mbaya sana kuna changamoto kwenye maelekezo mengi ambayo ameyatoa hayajatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto hizo ni kwamba, tayari Serikali ilitoa 1.8 billion kwa ajili ya kulipa fidia ya watu wote waliokuwa kwenye maeneo yale na fidia hiyo tayari imelipwa. Wametengewa maeneo ambayo wanatakiwa waende kuishi, lakini bahati mbaya sana tumechukua shule zao, lakini kule hatujaenda kujenga shule. Wamelipwa fidia tunawaondoa, lakini wanaenda sehemu ambapo hakuna shule ya msingi, hakuna zahanati, wametengewa eneo waende, lakini miundombinu ile ya kuwafanya waishi haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Waziri Mkuu alipofika aliwaambia msiwaondoe hawa, jengeni kwanza shule, jengeni zahanati na akaelekeza fedha zitolewe, lakini mpaka leo hii bado ni changamoto kubwa sana. tunaendelea kuwaondoa watu wahame, lakini tunawapeleka sehemu ambako watoto wao watakaa bila kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, tuna mipango mizuri na sisi watu wa Chemba pamoja na Dodoma kwa ujumla tuna uhitaji kweli huo mradi. Na huo mradi ndio peke yake ambao unaenda kuondoa changamoto yote ya maji kwenye maeneo yote yanayozunguka. Lakini bahati nzuri ukisoma andiko la mradi ule limeeleza namna gani kwenye maeneo yale watatengeneza skimu za umwagiliaji kwa hiyo, kwa namna yoyote ile mradi ule una faida kwetu zaidi. Changamoto ni moja tu ni hiyo ambayo nimeieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara ya Maji itoe fedha kama tulivyokubaliana kwa ajili ya ujenzi wa shule na zahanati, ili watu wale wahamie kule. Tukiendelea kwasababu, sasa hivi kuna kama kigugumizi cha watu kuondoka, watu wengine wamehamia, lakini watu wengine bado wapo. Na nikifika kule naulizwa Mheshimiwa Mbunge wanatuambia tuje hapa, watoto wetu watasoma wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kuhusu maji ni huu, lakini pia naishukuru Serikali, tuna mradi pia katika ile miradi ya miji 28 Halmashauri yetu ya Chemba ni moja ambayo inanufaika na bilioni 11 zile. Na bahati nzuri watu wale wanaotekeleza ule mradi tumefika tukafanyanao vikao tukawaomba watu wale waliokuwa wanadai fidia za watu kupisha mabomba ya maji wamekubali wanaondoka na hawahitaji fidia. Niiombe sasa Serikali ifanye haraka kwa ajili ya kutekeleza ule mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niongee kidogo kuhusu kilimo. Sisi sote tuliopo hapa tunafahamu asilimia 77 ya ajira za Watanzania zinapatikana kwenye kilimo, lakini si hivyo tu, tunafahamu asilimia 90 ya ardhi iliyopo Tanzania hii inalimwa na wakulima wadogowadogo. Sasa ni mawazo ya kawaida tungefikiria kwamba, huku ambako watu waliko wengi ndiko tuingize fedha nyingi kwa ajili ya matokeo makubwa, lakini ukweli ni kwamba, bajeti ya Wizara ya kilimo ni ndogo sana na hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe sana kuwa tuangalie namna sehemu ambako tunatakiwa kuwekeza ni sehemu ambako idadi ya wanaochangia uchumi ni kubwa. Idadi ambayo ya waliojiajiri ni kubwa, ili tuweze kutatua changamoto na kwasababu hiyo, tunaweza tukaongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo kuna changamoto kubwa sana kwa wakulima wangu. Moja ya changamoto kubwa ni kile kitu kinachoitwa stakabadhi ghalani. Serikali ina dhamira njema kwelikweli, lakini changamoto iliyopo unawalazimisha watu mpaka kwa bunduki ili wakauze huko kwenye stakabadhi ghalani, sijui ni nini? Unalima mwenyewe, unavuna mwenywe, unapalilia mwenyewe, Serikali hujapeleka hata mbegu, unashika bunduki ili mtu akauze kwenye stakabadhi ghalani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linaleta kero kubwa sana, kule kwangu sasahivi wameanza kuvuna. Nilikuwa na mkutano weekend hii wameanza kuniuliza tumeambiwa tena tuanze kupeleka mazao kule; hivi kweli kama hiyo stakabadhi ghalani ina faida kwa wananchi kwa nini wao wasihamasike kwenda kuuza huko? Unamlazimisha mtu mwenye debe moja aende akasubiri mwezi mzima ndio aje alipwe fedha yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili haliwezi kuwa sawa, nashauri Serikali kwa baadhi ya maeneo au kwa baadhi ya mazao waachane na huu utaratibu kwa sababu kwa namna yoyote ile ungekuwa na faida wakulima wenyewe wasingeukataa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee kidogo kuhusu barabara, kuna barabara yetu ambayo na Mheshimiwa Rais, Hayati, alivyofika kwenye Jimbo langu la Chemba aliahidi. Barabara inatoka Kibarashi inaunganisha mikoa minne, Kibarashi – Kiteto – Chemba hadi Singida. Barabara hii kwenye Ilani imekuwa ikiandikwa mara zote, lakini hakuna hata mwaka mmoja ambao imetengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu ya hayo naomba kuwakilisha. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye mara zote amekuwa akitupa afya njema na uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kidogo sana. Lakini kwanza kabisa nishukuru Wizara na kumshukuru Waziri kwa namna ambavyo mapendekezo yetu sisi Wabunge yamezingatiwa. Kwa hakika kila Mbunge huku nyuma amesema mambo mengi na mengi yameonekana kwenye bajeti hii. Kwa hiyo namshukuru sana lakini pia nampongeza sana yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mkuu, mpango mkuu kwenye bajeti hii unaeleza juu ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. Hili ni jambo kubwa sana na mimi nataka nichangie ni namna gani sasa tunaweza tukafika huko ambako ndiko ambapo mkakati mkuu wa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote wengi wetu tuna Majimbo huko na tunafahamu ili tuweze kufikia mkakati huu lazima tuwe na miundombinu bora na imara. Katika hilo kwanza nimshukuru sana sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha, kwa kuiwezesha TARURA kwa kutoa milioni 500,000,000 kila jimbo. Kwa hakika ametusaidia sana sana kuhakikisha baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayapitiki tunaweza tukapambana nayo ili walau yaweze kupitika kwa urahisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo yapo mambo ambayo nataka nipendekeze. Nafahamu kila Jimbo linahitaji fedha lakini nafahamu kuna maeneo ambayo kiukweli hayapitiki. Moja ya maeneo hay ani majimbo yetu sisi ya vijijini. Sisemi kwamba watu wa Ilala wasipewe, watu wa Kinondoni wasipewe. Hapana. Nafikiria kwamba tumepewa milioni…

MWENYEKITI: Toa mchango wako huna haja ya kutaja Majimbo mengine.

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetaja Ilala kwa sababu wewe ndiyo Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Toa mchango wako ndugu au utakaa sasa hivi hapa. (Kicheko)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni moja, nafikiria kwamba ili tuweze kufikia malengo ya bajeti hii tunafikiria ni lazima tufungue maeneo yote ili yaweze kupitika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Kanda ya Kati, kwa mfano jimbo langu ni wazalishaji wakuu wa alizeti, na sasa hivi tunaenda kufungua viwanda vya alizeti, kama tulivyosema, kwamba mkakati namba moja ni kuhakikisha tunaweka uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu. Katika mazingira hayo yapo maeneo ambayo wamelima alizeti lakini hawana uwezo wa kuzitoa kule kuingiza sokoni. Au, kwa kufanya hivyo, unayatoa kwa gharama kubwa kweli kweli. Maana yake sasa mkulima anazalisha, anatumia fedha nyingi lakini tija yake inakuwa ni ndogo kwa sababu hana uwezo wa kuyatoa au akiyatoa, anayatoa kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo mimi naomba pale TARURA tumeongezewa fedha. Ninakushukuru sana Waziri wa Fedha namna ambavyo umefikiria na umezingatia namna ambavyo tuliongea huku nyuma. Sasa fedha zile zikipatikana naomba basi mgao ule ulenge mahitaji. Tuangalie ni wapi sasa ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie mimi nimeshindwa. Tulielekezwa zile fedha tulizopewa walau tujenga barabara au tujenge kwa kiwango cha changarawe. Lakini ni ukweli kwamba kuna maeneo ambayo hata watoto hawawezi kwenda shule wakati wa mvua. Watakushangaa sana utato amilioni 500,000,000 zile ukajenge kilometa moja ya lami wakati kuna maeneo ambayo hawapo. Mvua zikianza lazima mvua ziishe ndiyo watoto waende shule. Katika kuzingatia hilo, mimi nimuombe sana Waziri wa Fedha, rafiki yangu wa muda mrefu, rafiki yangu wa muda wote. Naomba mnapotoa hizi fedha basi hebu jaribuni kuangalia ni namna gani tunaweza tukaifungua hii nchi kila eneo walau lifaidi au kila eneo walau liweze kupitika kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mimi nakufahamu ndugu yangu Mwigulu Nchemba, ni mtu mchapakazi, mwerevu, anaweza. Sasa tumeongeza fedha kwa ajili ya TARURA naomba basi zitoke, maana tunaweza tukaziongeza lakini kuziongeza na kuzikusanya ni jambo lingine lakini kuzitoa ziende TARURA pia ni jambo lingine. Nafahamu hilo lipo ndani ya uwezo wako Mheshimiwa Waziri. Sisi ambao tuna Majimbo ambayo yapo vijijini tuna changamoto kubwa sana. Naomba sana, fedha hizo zikikusanywa zipekwe huko ili walau zitusaidie kufungua vijiji na vitongoji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu peke yangu kwenye zile kilometa nyingi zinazotajwa nina kilometa zaidi ya 1,000 na zaidi za TARURA, lakini ambazo zinafanyiwa ukarabati au zinaweza kupitika ni asilimia 17 tu. Tafsiri yake ni kwamba maeneo mengi hayapitiki wala hayana uwezo, hata kama una biashara yako huwezi kufanya. Mimi nilitaka kuchangia hilo kuhusu barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba niongee kidodogo kuhusu kilimo. Waziri mwenyewe anakiri kwamba asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo, lakini ni ukweli kwamba hakuna namna ambavyo nchi yetu inaweza kwenda mbele bila kuwekeza kwenye kilimo ambacho ndicho kina watu wengi na hakuna formula zaidi ya hiyo. Ukweli ni kwamba ukitaka ku-solve quadratic equation lazima utumie quadratic formula, hakuna namna nyingine.

Nimejaribu kuangalia na kufanya tafiti kote duniani, ukweli ni kwamba lazima uwekeze kwenye nguvu kubwa, lazima uwekeze kwenye shughuli kubwa ya kijamii inayofanyika. Watanzania wengi ni wakulima lakini sisi tunawekeza kidogo mno. Bajeti yetu walau tungeisogeza ikafika asilimia 10 ya bajeti tungekuwa tunaamini kwamba sasa tunaenda kusaidia watu walio wengi ili waweze kuinuka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hilo mimi Jimbo langu asilimia 95 ni wakulima, na ukitaka kumuuliza mtu anawezaje kupata fedha lazima asubiri wakati wa mavuno ndiyo anaweza kupata fedha na akatunza kwa ajili ya kuhudumia mwaka mzima. Sasa, katika mazingira hayo kuna changamoto kubwa sana kwenye. Moja ya changamoto kubwa sana ni masoko. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri kaeleza vizuri kwenye bajeti hii. Ameeleza namna gani ambavyo anaweza ku-deal na hilo suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine kubwa, na mimi nafahamu ndugu zangu wenye majimbo hapa idadi kubwa sasa hivi ya watu vijijini ni vijana. Vijana ni wengi sana huko vijijini. Mimi nikienda vijijini nikiitisha mkutano nakutana na vijana wengi sana. Wapo vijana wenye degree mbili (Masters) wapo vijana wana degree moja, wapo vijana ambao hawana elimu, wako vijijini wamezubaa kule hawana cha kufanya. Tufanye nini sasa, kwa sababu tukifikiria kwamba waende kujiajiri, wanajiajiri vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kama alivyosema kwenye bajeti yake ninamuomba sana Waziri hili jambo alifuatilie, tuangalie namna gani tunaweza kuwekeza mitaji kwenye hawa vijana. Otherwise tunaweza kutengenza mazingira magumu sana kwao na kwetu sisi ambao mara zote wenyewe ndiyo wanatusaidia kutupigia kura. Nilitamani sana niyaseme hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nilitaka kuongea kidogo kuhusu elimu. Niliwahi kusema huku nyuma, kuna changamoto kubwa sana kwenye Halmashauri hizi ambazo ni changa, Halmashauri ndogo kama ya kwangu mimi ambayo ukikusanya fedha mapato yote kwa mwaka ni bilioni 1.2 na ukiangalia uwezo wa ujenzi wa madarasa ni mdogo sana. Bado narudi kwenye hoja ile ile kwamba ni lazima tuangalie ni wapi. Wakati mwingine unajiuliza maswali makubwa sana kwamba kule Wizara ya Elimu wametoa fedha kwa ajili ya maboma lakini wametoa flat rate. Yaani mtu ambaye anakusanya bilioni 100 unampa flat rate na mtu anayekusanya bilioni 1.2 kwa mwaka. Hii haiwezi kuwa sawa na hatuwezi kuwa tunalenga sasa kuendeleza hizi halmashauri changa au watu walioko. Mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hili ulizingatie vizuri. Mimi naamini wewe unaweza na haya mambo unaweza ukayaweka vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu ambazo zimetolewa na Wizara ya Maji zinaonyesha asilimia 72 ya watu waishio vijijini sasa wanapata maji, lakini kwenye wilaya yangu sidhani kama asilimia 42 inafika. Nilikuwa nategemea sana mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa na kwenye mradi huo tayari Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 7.8 kuwahamisha watu, lakini cha ajabu zaidi, haukutengewa hata shilingi moja kwenye bajeti hii. Wasiwasi wangu mkubwa ni kwamba sasa wale watu wanaenda kurudi pale na hakuna namna tena ya kuja kuwaondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi, kulikuwa na migogoro mingi sana kwa ajili ya kuhakikisha watu wale wanahama pale. Sasa hili jambo limenishtua sana. Nilitamani wakati Waziri anakuja ku-wind-up aniambie kwanini hawakutenga fedha angalau kidogo kwa ajili ya bwawa lile? Ninaamini, ili tuweze kutatua changamoto ya maji kwenye Makao Makuu ya nchi, ilikuwa ni lazima tuanze haraka sana utekelezaji wa mradi ule kwa sababu mradi ule ni katika miradi ya maji ya kimakakati tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara, Wilaya yangu ya Chemba ni katika Wilaya ambazo ni kame kweli kweli na ndiyo maana tumejaribu kufanya miradi mingi ya maji na miradi mingine inashindikana hasa ile ya kuchimba visima. Nasi tunaamini, namna peke yake ya kutatua changamoto za maji kwenye wilaya ile ni kujenga bwawa hili kwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema pia, kuna changamoto nyingine ambazo zinashangaza sana. Tuna visima ambavyo vilichimbwa mwaka 2014. Katika visima vile, wakati huo Halmsahauri siyo RUWASA; walitangaza tenda kwa ajili ya usambazaji. Mkandarasi akapatikana, lakini mpaka leo hii hawajasaini mkataba wa yale maji wasambaze. Mpaka leo, kuanzia mwaka 2014! Vile vile maji yale yamechimbwa kilometa sita kutoka vijiji vilipo. Kwa hiyo, haina faida yoyote kwa sababu lazima watu waweke punda kwenda kuchota maji kilometa sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naiomba Wizara ya Maji ikashughulikie visima vile vitatu ambavyo ni Chandama, Mapango na Machiga. Watu wengi ambao hawajasoma kule kijijini wanashindwa sana kuelewa, inawezekanaje mkachimbe maji, mtangaze tenda, mkandarasi apatikane, halafu msisaini afanye kazi? Wanashindwa kuelewa, nini kinaendelea pale? Naomba Waziri wa Maji atakapokuja ku- wind-up hotuba yake ya mwisho, aseme chochote ili watu wa kule watuelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nimeona mmenipa visima kadhaa vya maji; mmeonyesha kwenye jedwali kwamba tutapata visima 13 kwenye bajeti hii, lakini mmetenga shilingi milioni 180. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa namna ambavyo Wilaya ya Chemba ilivyo dry milioni 180 haziwezi kuchimba visima 13. Sana sana zitachimba visima vinne. Sasa takwimu hizi ni za kwenda kumgombanisha Mbunge na watu wake, kwamba tumetajiwa vijiji ambavyo vinaenda kupata maji, lakini kiuhalisia ni kwamba maji kwa bajeti hii haiwezekani. Namwomba Mheshimiwa Waziri, anapotenga fedha angalie na Wilaya zenyewe na namna gani unaweza kupata maji kwenye mazingira haya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto nyingine hii inaitwa ya manunuzi. Tulipata mradi pale Chemba Mjini na tuliambiwa mradi ule una shilingi milioni 250, lakini mpaka leo umeshindwa kutekelezwa. Ukimwuliza Meneja wa RUWASA, tangu mwezi wa 11 anasema watu wa manunuzi hawajaleta vifaa mpaka leo, miezi sita. Nami nikisimama jukwaani nawaambia ndugu zangu tumepata fedha milioni 250 tunaweka sawa mambo ya maji hapa. Jambo dogo kama hilo, tunatumia miezi sita kununua vifaa vya maji, sijui mabomba, mnatuweka kwenye wakati mgumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana, juzi baada ya Waziri wa TAMISEMI kuja pale, mmetupa shilingi milioni 150. Siku mbili tu kaja, ametoa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuhakikisha maji yanapatikana pale hospitali. Nawashukuru sana, lakini nawaomba msisubiri mpaka Mheshimiwa Waziri aje, tukiwaambia sisi, ndio tumewaambia mahitaji ya watu waliopo kule.


Mheshimiwa Naibu Spika, hilo pia nilitaka niseme, tuachane na utaratibu kwamba manunuzi lazima yafanyike HQ, kila mtu ukimuuliza yanafanyika HQ, sisi tuko Dodoma HQ Dar es Salaam tunahitaji vifaa vya milioni 20 tunasubiri mpaka watu wa Dar es Salaam waje wanunue, hii haiwezi kuwa sawa hata kidogo. Nimwombe Waziri abadili utaratibu au aweke utaratibu ambao ni rafiki ili tunapopitisha bajeti vifaa vile vipatikane kwa haraka zaidi.

Mheshimwa Naibu Spika, nataka pia niongelee juu ya uchakavu wa miundombinu ya maji iliyopo katika wilaya yangu. Tuna miradi mizuri kabisa ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, changamoto kubwa tuliyonayo sasa maji hayapatikani. Shida ni ndogo tu, wakati mwingine unaona


mradi unahitaji milioni 30 tu, lakini kata nzima inashindwa kupata maji kwa sababu tu eti fedha za kukarabati miundombinu milioni thelathini mpaka uende kuomba Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa nimefanya ziara kwenye Kata moja ya Nahoda, tenki limepasuka, tenki lenyewe kulinunua ni milioni moja, watu zaidi ya vijiji sita zaidi ya miezi mitatu hawapi maji. Nimwombe sana Waziri lazima tuwe na utaratibu rafiki ambao unawezesha pale matatizo yanapotokea, pale changamoto za maji zinapotokea waweze kuzitatua kwa urahisi na kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi walau nami nichangie kidogo kwenye mwongozo huu wa Mpango. Kwanza kabisa nichukue fursa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema ambaye amekuwa akitujalia afya njema na uhai na tumekuwa tukikutana hapa mara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Nina hakika kwamba Watanzania wote sasa wana matumaini makubwa, kazi inaendela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwongozo wa Mpango huu nataka nichangie katika sehemu mbili muhimu; sehemu ya kwanza ni kilimo na pia sehemu ya pili ni barabara. Kabla sijachangia nichukue fursa hii pia kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Mwongozo wa Mpango unatupa sisi fursa ya kuwaeleza nini kiwepo kwenye Mpango unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa kwenye kilimo ni utekelezaji wa mipango ambayo ipo.

Nimejaribu kusoma Mpango wa mwaka 2019/2020 mambo mengi yameandikwa, lakini sisi wakulima kiukweli kabisa Serikali haijawekeza vya kutosha. Maneno haya yamesemwa na kila Mbunge, lakini mimi najaribu kuangalia tu kwa takwimu. Kwa mfano, ukiangalia kwenye zana za kilimo, mpaka sasa hivi sisi tuna asilimia 20. Hiyo asilimia 20 yenyewe ni kwenye maandalizi tu, yaani ile hatua ya kwanza kabisa ya kuchambua ardhi ndiyo tunatumia labda matrekta na zana nyingine, lakini kwa mantiki kamili ya kutumia zana za kilimo bado tupo chini ya asilimia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo, hakuna namna ambayo tunaweza tukaisaidia nchi hii ambayo asilimia kubwa ya Watanzania wapo kwenye sekta hii ya kilimo. Ni changamoto kubwa kweli kweli. Sasa hivi tunapoongea, ukifanya ziara kwenye maeneo yote ya Tanzania au hasa Majimboni, mbegu zenyewe hazijafika. Sasa unaanza kujiuliza maswali mengi sana, kwamba kwenye Mpango tumeweka tayari, maana yake hata tukija kusema sasa tuwekeze shilingi trilioni moja, bado changamoto hii itakuwepo pale pale. Kwa maana tumeweka kwenye Mpango, tumepitisha kwenye bajeti, lakini mbegu hiyo bado mpaka sasa hivi haijafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo naliona, ni lazima tuhakikishe tumewekeza vya kutosha kwenye kilimo. Kama hatutafanya hivyo hakuna namna ambavyo tutakwepa watu wengi kuhamia mjini. Ukiangalia population kubwa ya Dar es Salaam ya vijana wengi wanaoitwa Wamachinga ni kwa sababu hakuna kazi kwenye kilimo hicho. Hatujawekeza vya kutosha kwenye kilimo. Tukiwekeza vya kutosha tutapunguza gharama hizo ambazo zimewekezwa kwa ajili ya Wamachinga; majengo yanayojengwa, fedha zile tungewekeza kwenye kilimo, vijana wale wasingekuwa na sababu ya kukimbilia mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi naiona katika mwono huo. Mimi pia nalima, lakini najaribu kuangalia mazingira ya kilimo kile, anaweza akaja kijana akalima mwaka mmoja akaamua bora aende mjini akauze bidhaa mkononi kwa sababu ya mazingira yenyewe yalivyotengenezwa. Nataka niwaombe sana Wizara ya Fedha iangalie namna ambayo itatenga fedha za kutosha waingize kwenye kilimo. Tutaweka Mpango leo, lakini kama fedha hazitaenda huko nina hakika kabisa vijana wengi watakimbilia mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka pia niongelee kuhusu barabara. Tuna barabara yetu; halafu unaweza kujiuliza maswali mengi sana, kwamba tuna barabara ambayo inaunganisha mikoa minne. Mwenzangu Mheshimiwa Mtaturu alikuwa ameiongolea pale kwamba barabara inaunganisha mikoa minne, eti imetengewa kilometa 20 kati ya kilometa 420 na kitu. Sasa sijui wataalamu huwa wanachambua kwa kuangalia vigezo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia barabara hii, ndiyo barabara kubwa iliyobaki, lakini barabara hii ukiangalia faida, niliwahi kumwambia Waziri; hivi nyie mnavyoweka mipango na kujenga hizi barabara mnatumia vigezo gani? Unawezaje kuacha barabara inayounganisha mikoa minne, unaenda kujenga barabara ya kuunganisha wilaya na wilaya halafu umetenga kilometa 70?

Mimi nafikiri kama walivyoshauri Kamati ya Bajeti, wameandika maneno mazuri sana pale, kwamba tukajenge kwanza barabara zile ambazo tayari zipo kwenye mpango zimalizike then ndiyo tuingie kwenye barabara nyingine. Pengine hii itaweza kutibu lile tatizo ambalo wewe unaliona, kwamba wanakuja na Mpango, Wabunge wanasema, lakini mwisho wa siku hakuna ambacho kinafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha sana kwamba una barabara muhimu kuliko zote halafu hiyo ndiyo inatengewa fedha kidogo sana. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kama yupo hapa, Waziri wa Ujenzi wakati ujao, sisi tupo Wabunge wanane ambao tunaguswa na barabara hiyo; nataka nimwambie, ukileta tena kilometa 20 sisi hatutakuwepo tena hapa Bungeni. Kwa sababu ni barabara ambayo ukiangalia faida zake ni kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaenda kupanua Bandari ya Tanga, mizigo yote ambayo inatakiwa kwenda Rwanda na Burundi, lazima ipite kwenye barabara hiyo. Ni kwa namna gani unaenda kujenga barabara nyingine huko kilometa 70, kilometa 80 ya kiwango cha lami…

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa nimekuona.

T A A R I F A

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wasiofahamu, barabara inayozungumziwa hapa ni ya Handeni – Kibilashi – Kiteto – Kondoa – Singida kilometa 460. (Makofi)

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimeipokea taarifa bila wewe kuniuliza, lakini ni ukweli, najaribu kueleza namna ambavyo barabara ile inaweza kusaidia. Najaribu kuangalia, hivi barabara zinajengwa kama unaongeaongea Bungeni au ni Serikali? Ina maana kama haitakuwa Mbunge, barabara hiyo haitajengwa? Kuna vitu vingi vinachanganya sana, kwa namna ambavyo umuhimu wa hii barabara ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana kwamba nimesoma vizuri ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti na ninaomba wauzingatie, wasituweke kwenye mtihani wa kuja kupambana na mipango yao waliyotupangia. Nashauri kama walivyoshauri Kamati ya Bajeti kwamba barabara zile ambazo zipo kwenye Mpango, ambazo zimepangwa muda mrefu sana, zijengwe zimalizwe ndiyo mlete tena mipango mingine ya kujenga barabara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)