Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Deogratius John Ndejembi (4 total)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba kuwa wanufaika wa TASAF ni wananchi wenye uwezo badala ya kaya maskini:-

Je, hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nami ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa mema yote ambayo anaendelea kutujalia hadi kufika siku hii ya leo. Pili, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika ofisi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Mpango wa TASAF ni kuzinusuru kaya maskini katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini ulianza rasmi mwaka 2000 hadi 2005; awamu ya pili ilianza mwaka 2005 hadi 2012; na awamu ya tatu, kipindi cha kwanza ilianza kutekelezwa mwaka 2013 hadi Desemba, 2019; na kipindi cha pili cha awamu ya tatu kilianza Februari, 2020 hadi Septemba, 2023 ambapo jumla ya kaya maskini 1,100,000 zimeweza kuandikishwa na wanufaika kunyanyua hali yao ya kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kagera jumla ya kaya maskini 68,915 zimeandikishwa na kuingizwa kwenye Mpango huu wa TASAF. Katika utekelezaji wa kipindi cha kwanza walengwa wamepokea ruzuku kwa takribani miaka mitano. Hali hii imechangia walengwa hawa kuwa na miradi mikubwa ya uzalishaji mali kama mashamba, mifugo na shughuli za ujasiriamali ambazo zimewawezesha wao kuboresha maisha na kujiimarisha kiuchumi. Walengwa kama hao ndio wanalalamikiwa kuwa TASAF inasaidia watu wenye uwezo badala ya kaya maskini. Ukweli ni kwamba kaya hizo ziliingia kwenye mpango zikiwa na hali duni na ziliweza kujikwamua kiuchumi.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni ya kuongeza watumishi 403 wa afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka ya 2015 hadi 2020, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 14,479 wa kada mbalimbali za afya. Katika Mwaka wa Fedha 2020/ 2021 Serikali inatarajia kuanza kuajiri watumishi 75 wa kada mbalimbali za afya kwenye Wilaya ya Hai kwa ajili ya hospitali ya wilaya moja, vituo vya afya sita na zahanati 28 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. DENNIS L. LONDO Aliuliza: -

(a) Je, ni Watumishi wangapi wamerejeshwa kazini baada ya kuondolewa kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti feki na Wafanyakazi hewa?

(b) Je, ni Watumishi wangapi waliorejeshwa kazini wamelipwa stahiki zao kama mishahara ambayo hawakupata kutokana na kuondolewa kazini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia ofisi yangu imewarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara jumla ya watumishi 4,380 walioondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti vya elimu na watumishi hewa. Idadi hii inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa wapatao 3,114.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwarejesha watumishi tajwa, Serikali pia ilitoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia mwezi Disemba, 2020 ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya Kidato cha Nne au kubainika kughushi vyeti. Pia, mnamo tarehe 07 Mei, 2021 Serikali kupitia ofisi yangu ilitoa maelekezo na utaratibu kwa waajiri kuhusu namna ya kushughulikia hatima za ajira za watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya Kidato cha Nne pamoja na malipo ya stahiki zao. Napenda kuwakumbusha waajiri wote kukamilisha utekelezaji wa maelekezo hayo kwa haraka na kwa usahihi ili watumishi husika waweze kupata haki zao mapema.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kusisitiza kwamba msamaha uliotolewa unawahusu watumishi wale tu walioajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004 bila sifa ya elimu ya Kidato cha Nne lakini baadaye wakajipatia sifa za kuajiriwa na haiwahusu watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi au waliotoa taarifa za uwongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi. Utaratibu wa kushughulikia watumishi waliobainika kughushi vyeti ulishatolewa awali na Serikali na watumishi wote waliobainika kughushi vyeti hawastahili kurudishwa kazini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imelipa madai ya mishahara ya jumla ya shilingi 2,613,978,000 kwa watumishi 1,643 waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kimakosa. Uhakiki wa madai yaliyobaki unaendelea na yataendelea kulipwa kwa kadri yanavyohakikiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JANEJELLY J. NTANTE Aliuliza:-

Serikali inawahimiza watumishi kujiendeleza kielimu, lakini baada ya kuhitimu wanapoomba kubadilisha kada huteremshwa vyeo na mishahara:-

Je, Serikali haioni ipo haja ya kuwaacha na mishahara yao ili kujiendeleza isiwe adhabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly James Ntante, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeendelea kutoa Miongozo mbalimbali kuhusu namna ya kuwabadilisha kada/kazi watumishi waliojiendeleza kitaaluma. Aidha, Serikali inatambua umuhimu wa watumishi kubadilishwa na kupangiwa kazi kulingana na taaluma zao. Hivyo, kupitia Waraka wa Barua Kumb. Na. C/AC.44/45/01/ A/83 ya tarehe 01 Desemba, 2009, Serikali iliweka utaratibu wa kufuata wakati wa kuwabadilisha kada watumishi waliojiendeleza kitaaluma ambapo kuna aina mbili za kubadilishwa kada bila kuathiri watumishi waliomo katika kada hizo.

(i) Kumbadilisha kazi mtumishi aliyejiendeleza na kupata sifa zinazompandisha hadhi kitaaluma, mfano Afisa Kilimo Msaidizi kuwa Afisa Kilimo. Watumishi wa aina hii hubadilishwa hadhi na kuingizwa katika kada mpya kwa kuzingatia cheo cha kuanzia cha kada mpya. Iwapo vyeo walivyokuwa navyo vilikuwa na mishahara mikubwa kuliko mishahara ya cheo walichopewa baada ya kubadilishwa, huombewa kibali cha kuendelea kulipwa mishahara waliyokuwa wakilipwa kama mishahara binafsi hadi watakapopandishwa vyeo vyenye mshahara mkubwa kuliko mishahara binafsi. Utaratibu huu pia unawahusu watumishi wa kada saidizi ambao taaluma walizo nazo hazina vyuo vinavyotoa Astashahada/Stashahada au Shahada katika fani wanazofanyia kazi mfano Walinzi na Wasaidizi wa Ofisi.

(ii) Aina ya pili ni kuwabadilisha kazi watumishi waliojiendeleza katika fani nyingine tofauti na zile walizoajiriwa nazo kwa lengo la kukidhi matilaba ya kazi (job satisfaction) bila kuzingatia mahitaji ya mwajiri. Hawa hulazimika kubadilishwa kazi na kuingizwa katika cheo na ngazi ya mshahara wa cheo kipya na hawastahili mishahara binafsi kutokana na kulinda ukuu kazini na kuwajengea uzoefu wa kazi mpya ambazo wamezichagua wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu, Serikali inasititiza watumishi wa umma kujiendeleza katika kada walizoajiriwa nazo ili kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi na kuwa wabobezi katika fani zao. Aidha, watumishi wa umma wanaaswa kupata ushauri kwa waajiri wao wanapotaka kujiendeleza kwenye fani tofauti na wanazofanyia kazi. Waajiri wanao wajibu wa kutenga nafasi za kuwabadilisha kada wale waliojiendeleza katika fani zao ili kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo muhimu inatumika ipasavyo. Aidha, waajiri wahakikishe kuwa wanawashauri vizuri watumishi wao kabla ya kubadilishiwa kada/kazi watumishi waliojiendeleza kwenye fani tofauti. Endapo kwa namna yoyote kuna suala ambalo lina mazingira tofauti na haya, mwajiri au mtumishi mwenyewe anaweza kuomba ufafanuzi kutoka katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wowote.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.