Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dorothy George Kilave (2 total)

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji kwa sababu Jimbo letu la Temeke maji yamefika karibu kila kata. Tatizo letu kubwa ni kwamba bomba lile kubwa limepita katika barabara kubwa lakini kuvuta maji kwenda ndani ya nyumba zetu ambapo miundombinu siyo mizuri sana kwenye Kata za Buza na Kilakala na nyumba ziko mbali. Niombe Wizara ya Maji tunapoomba kuvutiwa maji ndani ya nyumba zetu, fedha ile ambayo tunatakiwa kuilipa kidogo ni kubwa, sasa mfikirie tuweze kuvuta kwa nusu ya bei halafu muendelee kutudai ndani ya malipo ya kila mwezi kama vile tunavyofanya luku ili tuweze kuona kila mmoja sasa anapata maji ndani ya nyumba yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU SPIKA: Hilo ni ombi, nadhani utakuwa umeliandika Mheshimiwa Waziri.
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini naomba sasa niseme kwamba sasa ni miaka karibu saba tangu mmelitwaa hili eneo.

Je, haiwezekani kwamba mtachukua tena miaka saba kwa ajili ya kulirekebisha na kuweka mpango huo? Niombe basi kama nilivyosema kwamba wananchi wa Temeke tunatamani kujenga shule za sekondari na msingi kwa sababu tunazaliana sana na maeneo mijini sasa hivi hakuna. Niseme tu kwamba tuombe sasa Wizara yako itupe eneo hili ili sisi katika miaka hii ambayo tumeambiwa tujenge shule za sekondari pamoja na msingi basi tuyapate kwa sababu naona mtakwenda tena miaka saba ijayo katika kutengeneza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali yetu sasa ina mpango gani wa kumalizia fidia kwa wananchi wa maeneo ya jirani karibu na pale ambapo mmetwaa lile eneo lakini yapo maeneo Shimo la Udongo ambapo mlitakiwa kuyatwaa lakini bado hamjalipa fidia. Naomba maswali yangu haya mawili tuweze kujibiwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nomba kujibu maswali mawili ya ziada ya Mheshimiwa Dorothy kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie hatutachukua miaka saba tena. La pili ni kwamba eneo lile ni karibu kabisa na Bandari ya Dar es Salaam na sisi kama Taifa tumekuwa mara nyingi tukijadiliana namna gani kuifanya bandari yetu kuwa effective na efficient na ili iweze kuhudumia waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa. Itakuwa ni makosa ya kimkakati tukiligeuza eneo ambalo halizidi mita 500 au 1,000 kuligeuza kuwa eneo la shule. Nataka tu nimshauri yeye na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Meya wake wa zamani yumo ndani ya Bunge hili ujenzi wa sekondari sio lazima tujenge kwenda…, tuna uwezo wa kujenga maghorofa kwa hiyo nawashauri Manispaa ya Temeke mjenge shule kwa mfumo wa maghorofa na ninyi mna mapato mengi kuliko Manispaa nyingi katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kuhusu fidia katika eneo lile tumebaki nadhani kaya kama mbili au tatu ambazo hazijamaliziwa fidia katika eneo la Kurasini na wale wananchi hawakuwa tayari, lakini wako katika hatua za mwisho kumalizana nao na watalipwa haki yao. Mpango wa Serikali katika lile eneo, eneo la ukubwa wa ekari 20 tunajenga The First Agricultural One Stop Centre ili mazo yetu ya kilimo hasa ya mbogamboga na matunda yaweze kusafiri kupitia Bandari ya Dar es Salaam badala ya sasa yanavyotumika kupitia bandari za nchi zinazotuzunguka.

Kwa hiyo, tunawaombeni sana watu wa Temeke mtuunge mkono kufikia azma hii ili eneo lile liweze kutusaidia kutatua changamoto ya usafirishaji wa mazao na kugeuza kuwa ni export hub eneo lile. Nashukuru.