Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dorothy George Kilave (14 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyeniwezesha kusimama katika Bunge hili la Kumi na Mbili. Pia nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa jinsi ambavyo waliweza kupendekeza jina langu na kunisababisha nikawe Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa kura nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwape shukrani sana ndugu zangu wananchi wa Temeke, wenyewe tumezoea kujiita TMK Wanaume kwa kunipa kura nyingi za kishindo hata leo nimeweza kusimama hapa na kuitwa Mbunge wa Jimbo la Temeke kama mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuishukuru familia yangu pamoja na marafiki zangu. Pia nisiwasahau wanangu; Matrona Kilave pamoja na Samuel Kilave kwa sababu walinitia moyo sana katika kipindi kile kigumu, naamini sasa wanafurahia matunda ya maombi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niunge mkono hotuba ya Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa hapa Bungeni na kitabu cha miaka mitano ambacho nimeweza kukisoma. Namuunga mkono sana kwa jinsi ambavyo hakika mambo mengi ya miaka mitano iliyopita yameweza kufanyika na hata sasa naamini kwa miaka hii mitano mingine yote yaliyoandikwa katika kitabu kile pamoja na Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi yanakwenda kufanyika sawasawa na Ilani yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika elimu. Nishukuru sana Wizara ya Elimu kwa jinsi ambavyo Rais, Dkt. Magufuli, ameweza kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Hata hivyo, lipo moja ambalo napendekeza waweze kulisikia na kuweza kuliweka sawa, nashauri kwamba wajikite kuweka vifaa vya TEHAMA ili hata walimu wetu wanapofanya kazi zao wafanye kazi kwa bidii na tuweze kupata kwa wakati majibu yote ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie suala la afya. Nimpongeze sana Rais, Dkt. Magufuli, kwa jinsi ambavyo ameweza kuweka sekta ya afya kwa namna ya kipekee kabisa. Sasa akina mama tunajidai, tunajifungua bure pamoja na kwamba zipo changamoto chache ambazo naamini Serikali yetu ni sikivu na inakwenda kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika afya hakika mimi nishukuru sana katika kata zangu 13 ni kata chache tu ambazo hazina zahanati. Namshukuru sana Rais, Dkt. Magufuli, pamoja na Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika yote hayo niombe kusema kwamba ipo changamoto ndani ya jimbo langu, sina uhakika kwa wengine, lakini pale ambapo tunakuwa tunauguza na inapofikia yule mgonjwa amefariki, tunapokwenda kuchukua maiti tunadaiwa fedha. Niombe Wizara ya Afya suala hili kidogo linaleta utata ndani ya hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe basi kama Wizara ya Afya itaweza kutoa tamko kwamba tufanye nini pale ambapo tunakuwa tumefiwa tunapohitaji kwenda kuchukua maiti yetu. Labda kama inawezekana tupewe elimu wakati tunapouguza tufanye nini ili tusifikie kudaiwa fedha. Niombe sana Wizara ya Afya iliangalie hili na naamini Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake, wajina wangu Mheshimiwa Dkt. Dorothy ataliangalia hili na kuweza kuona tunapata majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia ni mhanga wa miundombinu katika Jimbo langu la Temeke. Kama nilivyosema tuna hospitali nyingi, tumejengewa na masoko mazuri lakini katika kupita kwenye barabara zile za ndani hakika TARURA sasa waweze kupewa angalau ongezeko la fedha ili tuweze kuona tunapita kwa usalama na kufikia zile sehemu ambapo Serikali yetu imeweza kujenga zahanati pamoja na masoko mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais na nimpongeze sana na Mungu ambariki kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, niwapongeze Mawaziri wa Kilimo wote wawili.

Mheshimiwa Spika, ni kweli inawezekana Mkoa wa Dar es Salaam hatufanyi kilimo lakini naomba kuongelea Halmashauri ya Temeke.

Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo ndio msingi mkubwa wa kukuza kipato na chakula kwa familia na jamii. Jumla ya Kaya 6,118 zenye wakulima 11,270 wanajihusisha na kilimo cha mbogamboga kwenye hekta 6000. Karibu hekta 250 za mihogo na hekta 5,750 za matunda na mbogamboga na uchangiaji wa zaidi ya asilimia 75.

Mheshimiwa Spika, huduma za ugani zinafanyika kwa kutoa ushauri kwa wakulima kuhusu maghala na masoko na maeneo ya uwezeshaji Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Temeke.

Mheshimiwa Spika, tunawakaribisha kuja tuwekeze katika maeneo ili kuleta tija katika sekta ya kilimo. Pia kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji ambazo hazijaanza kwa Temeke, upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo cha mihogo /matunda/mbogamboga yapo na viwanda vya kutengenezea bidhaa za mazao ya kilimo kama zao la muhogo/mbogamboga/na matunda.

Mheshimiwa Spika, nauga mkono hoja na kazi iendelee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyeweza kutukutanisha mahali hapa na hata tukaweza kuanza mfungo siku nzuri hii ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa hotuba iliyojaa matumaini na maendeleo kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa mama Samia Suluhu; najivunia kuwa mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuwapongeza sana Mawaziri wote mlioteuliwa kwa kazi nzuri ambayo najua iko katika nafasi zenu ambayo tunakwenda kuitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba nimeweza kuona mambo mengi ambayo yamesemwa katika hotuba ile ya Waziri Mkuu, kwamba tutakwenda kutekeleza miradi yote ya kimkakati ambayo imepangwa, lakini pia nimeona kwamba yako malengo mazuri ya Serikali iliyoko madarakani bila kusahau kuibua miradi mipya inayokwenda kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende sana pia kuwapongeza sana kwamba tutakwenda kuitendea haki Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwamba mengi tumeyaandika katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, na ninaamini kwa jinsi ambavyo tunakwenda, tutakwenda kuiekeleza kwa ukamilifu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado naomba niendelee kuipongeza Serikali yetu, kwamba imefanya kazi nzuri sana katika miundombinu, hasa miundombinu ya barabara kubwa ambazo zimeonekana kila mahali tunakopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza kwamba tumeweza kuunganisha mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya na hata tunafikia sasa kuona kwamba tunapita kwa ujasiri wote tukitaka kwenda katika mikoa fulani fulani bila kuwa na msongamano wala kuwa na makorongo ya namna tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwamba pamoja na kwamba nawapa hongera kwa kutengeneza miundombinu ya barabara, lakini niseme sasa umefika wakati wa kuona ni namna gani sasa miundombinu ya barabara hizi inakwenda kuunganisha kati ya kata na kata, hata tuweze kuunganisha Kijiji na Kijiji ili tuweze kuona sasa yako mambo mazuri ambayo Serikali yetu imeyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejengewa zahanati nzuri sana katika kata zetu, tumejengewa masoko, tumejengewa stendi za mabasi, hasa kwetu Dar es Salaam. Lakini kutoka kwenye kata yako kufika kwenye kata nyingine kwa ajili ya kwenda kwenye zahanati au kwenye soko au kwenye stendi ya mabasi, hizi barabara kwa kweli ni tatizo. Hazina mwonekano mzuri. Naamini si kwa Dar es Salaam tu lakini naamini kwa hata mikoa mingine, nasemea kama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe sasa basi, kama kuna namna yoyote ya TARURA kuongezewa au kutafutiwa fedha za kuweza kufanya barabara hizi zipitike, niombe sana Bunge lako Tukufu tuweze kupitisha au tuweze kuona namna gani ya kujadiliana ili tuweze kupata fedha za kuwapa hawa TARURA maana naamini tumeongea nao sana lakini fedha walizokuwa nazo ni ndogo sana kiasi kwamba hawawezi kufanya miundombinu katika barabara zetu zile za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama jinsi mwenzangu jana aliongea kuhusiana na Mradi wa DMDP Mkoani Dar es Salaam, Mheshimiwa Bonnah aliongea vizuri sana, lakini bado naomba nisisitize, kama alivyosema sisi Dar es Salaam tunatamani kulima lakini hatuna maeneo ya kulima. Sasa inapendeza sana kama tutapata Mradi huu wa DMDP ili sasa mafuriko yaliyoko katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam yaweze kukatika na hata tuone kwamba barabara zetu zinaweza kupitika vizuri na vilevile kufanya maendeleo katika kata zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, pamoja na mambo mazuri ambayo Serikali imefanya. Lakini naomba pia niweze kuona kwamba Jimbo langu la Temeke nilisemee ya kwamba hakika kabisa kata zile 13 tumekaa vizuri, tumepata maeneo mengi mazuri, lakini bado nalilia barabara hizi za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Temeke wako vijana wengi waliopitia JKT na vilevile walikwenda katika huduma ile ya kujenga ukuta ule wa Mererani lakini pia waliweza kuingia katika kujenga ukuta wa ikulu. Lakini sasa hivi wamerudi na makaratasi tu ya kwamba wamehitimisha kufanya yale mambo lakini tunapokwenda kuomba ajira, vijana wetu hawa wa JKT hawaangaliwi wala hawapewi chochote kwenda kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Serikali yako kwa usikivu kabisa waangalie basi hizi hatma za vijana wetu ili waweze kupata kazi maana ndiyo hasa tunaowategemea katika kipindi kijacho, sisi tunakwenda kuzeeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Temeke tuna tatizo kubwa sana la umeme kukatika kila wakati. Umeme huu sasa sijui umekuaje, mwenzangu wa Mbagala aliliongelea hili. Nami niseme, hata sasa hivi hapa nina meseji ambayo tayari umeme umekatika, kwetu Temeke imekuwa ni salamu sasa hivi kwamba ikifika asubuhi lazima ukatike ama saa mbili au saa tatu au saa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sioni namna gani ambavyo TANESCO watatusaidia ili tuweze kupata umeme kama wenzetu. Na ukizingatia sana kwamba Jimbo letu la Temeke tunayo miradi mingi ya wafanyabiashara na makampuni mengi ya uzalishaji ambayo yanazalisha kupitia huo umeme ili hata sisi wenyewe kama manispaa tuweze kupata fedha za ndani katika makusanyo ya viwanda hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kuunga mkono hoja, lakini niombe haya niliyoyasema tuweze kuangaliwa na kutimiziwa. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Temeke pia niweze kuishukuru sana Serikali yangu kwa jinsi ambavyo inafanya kazi ni miaka mingi ambayo tukiwa tukilia kuhusiana na umeme lakini sasa nikiri kwamba wizara inafanya kazi vizuri sana. Lakini sio nyuma sana kuwapongeza katika hotuba yako Waziri hotuba nzuri ambayo imeleta matumaini kwetu sisi watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizidi kuwapongeza jinsi gani mnafanya miradi ambayo miradi ya kimkakati hasa mradi ule wa bwawa la Julius Nyerere ambalo tuna matumaini nalo litakapoisha hakika hatutakuwa tena na kelele za umeme katika nchi yetu na hata tutakwenda kuuza Jirani. Niwapongeze bado kwa jinsi ambavyo wameweza kujenga sasa ujenzi wa njia ya kuendesha treni ya umeme ambayo tunaamini watanzania wote tuna matumaini ya kwenda kuiona na hata sisi wenyewe kuipanda kabla hata ya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naendelea kuipongeza Wizara ya Nishati kwa jinsi ambavyo mmeweza kuendelea kuipatia kipato TANESCO kwa jinsi ambavyo sasa naona hata mambo mengine yatakuwa yanakwenda kwa sababu mmekuwa mmechangamka na kipato sasa ni kikubwa, na tunaweza kuona kwamba miundombinu inaimarika. Lakini siyo tu niweze kuwapongeza pia kwa kuweza kuangalia madeni sugu na niwatie moyo tuendelee kutafuta madeni yale ili tuweze kuona kwamba sasa nishati inakwenda mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba napenda sana kuwapongeza kwa sababu kazi inaendelea na inaonekana niseme tu kwanza sasa kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina mengi sana ya kusema lakini nimesimama kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Temeke TMK wenyewe tunajiita, ni jimbo lenye viwanda vingi sana naamini mnafahamu hilo. Lakini si viwanda peke yake lakini wananchi tulioko Temeke ni wananchi wengi sana ambao tunatumia nishati hii ya umeme. Lakini imekuwa ni tatizo sasa kwetu pamoja na hongera zote pongezi zote nilizowapa niseme tu kwamba wananchi wangu wa Temeke jimbo letu la Temeke hakika hata hapa niliposimama sasa hivi hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kila siku simu ni hizo imekuwa ni salamu za sisi kusalimiana umeme hakuna hiyo ndio inanishangaza lakini baada ya kufuatilia kwa muda mrefu na ninawashukuru sana mmekuwa mkinisaidia sana hasa naibu wako mara nyingi amekuwa akinisaidia mara kwa mara niseme nakushukuru sana Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kufuatilia hayo yote nimeona ya kwamba sisi tuna vituo viwili ambacho kimoja kinaitwa kingine TOL na kingine kule Tandika hivyo vyote vinatoa megawatt jumla 30 tu. Ambayo Tall wanatoa megawatt 15 na kule Tandika inatoa megawatts 12 ambazo ni 30. Lakini ukiangalia Jimbo la Temeke sisi wenyewe tunahitaji megawatt 117 ili umeme uwake kwa siku zote. Sasa lakini umeme huu hauwaki sijui ndio sababu ambayo hatupati umeme sina uhakika majibu mtaweza kutupa sisi leo wana Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunapata umeme kidogo sana hiyo iliyobaki megawatts 87 tunaambiwa tunapata kutoka Ilala Mkoa wa Ilala wa umeme sina uhakika sana lakini sisi wananchi karibu 125 tunaolipa deni tunaotumia LUKU na hatuna madeni kwa sababu sisi sote mmetufungia LUKU. Sasa niwaombe mtuangalie kwa jicho la kipekee kabisa Temeke, ni jimbo ambao lina watu wengi tunalipa kwa sababu wote mmetufungia LUKU hakuna deni sugu kama nilivyosema kwamba jamani endeleeni kutafuta madeni sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sisi Temeke tunakiri kwamba hatuna madeni sugu hata kule viwandani mkumbuke kwamba ni jimbo ambalo lina viwanda vingi na sisi wenyewe kama jimbo kama halmashauri tunategemea sana kupata fedha kutoka katika yale makampuni au viwanda. Sasa wakikosa umeme siku moja siku mbili kila siku hata sisi makusanyo yetu yanapungua. Kwa hiyo, niombe sana mtuangalie kwa jicho la kipekee kabisa ili tuone kwamba tunaendelea kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia miundombinu ni chakavu sana mimi ninaamini Temeke ni ya siku nyingi sana na miundo mbinu yetu kule ni chakavu kwa sababu kila siku kama nilivyosema umeme unakatika. Yaani imekuwa ni salamu zetu ikifika tu asubuhi saa nne utapigiwa simu hata hapa naweza nikawaonyesha kwamba mama umeme huku hukuna. Ukiangalia jimbo zima tunakata kumi na 13 Kata ya Keko umeme hakuna sasa hivi Mibulani hakuna umeme Kurasini, hakuna umeme Azimio, Mtoni Makangalawe Sandari Buza Yombo Vituka, Kilakala Temeke 14, Chang’ombe na Tandika kote hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana ndugu zangu Temeke ni jimbo ambolo linaangaliwa watu wengi wanakuambia tunaenda TMK ndio kwenye uwanja wa michezo na hata juzi nimeomba kwamba hata ile Arena ije ijengwe Temeke sasa tukikosa umeme namna hii tutafanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana wizara mliangalie hili sio tu lakini vilevile miundombinu yetu ambayo iliwekwa zamani waya zile kupita juu sasa hivi malori mengi yanaingia na kutoka kwenye viwanda vile. Aidha yanachukuwa mizigo au yanapeleka vifaa vingine kwa ajili ya matengenezo sasa yale malori yanakuwa yanagonga zile nguzo au marefu sana yanakata zile waya hilo nalo ni jambo lingine ambalo linaonekana kabisa kwamba linatufanya tuwe tunakosa umeme mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ushauri wangu tuunde mkakati wa makusudi wakuona kwamba sasa ile miundombinu iliyochakaa ifanyiwe kazi ninatamani sana kama fedha ipo na ninaamini fedha ipo kwamba miundombinu hii sasa ifanyiwe kazi na tuweze kuipitisha chini badala ya zile waya zinazopita juu kwa sababu nguzo ni za zamani sana ikiguswa kidogo tu imeanguka umeme hakuna.

Mheshimiwa Spika, na mpaka waje watengeneze inachukuwa muda kwa hiyo niombe sana mkakati huu tuujenge pamoja tuko tayari wana Temeke kusubiri kutoka kwenu na nyinyi muweze kutusaidia ili tuendelee kupata umeme. Kwa hiyo, niombe sana kwa ushauri mwingine wakati tunajipanga kupata miundombinu hii salama niombe sana kitengo cha emergence wasingoje wakaambiwa kuna tatizo la umeme mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwa sababu ni waajiriwa wa TANESCO wana uwezo kabisa wa kufika ofisini bila kuambiwa kwamba kuna tatizo au kuna katizo la umeme wao wenyewe wapite kuhakiki, kutambua na kuainisha sehemu gani ina kasoro kwa kipindi kile kwa sababu wanazijua kila wakati kasoro zinatokea wapi. Kwa hiyo, niombe kabisa kitengo cha emergence sasa tufanye kazi kwa pamoja ili Temeke yetu sasa iwake na sio tena kusema kwamba umeme hakuna maana hizo ndio salamu zetu niwaombe sana ndugu zangu badala ya kusubiri simu za itilafu emergence sana ifanye kazi ya kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo ninaamini hiyo salamu yetu ya umeme hakuna Temeke itaisha. Kwa hiyo, niombe sana ndugu zangu na bado niwape hongera na ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona nami niweze kuchangia machache niliyokuwa nayo. Vilevile namshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, aliyeniwezesha kusimama mahali hapa ili niweze kuongea. Zaidi naomba sana nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri anayoifanya na hata sisi wanawake tunajivunia kuwa wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme nawapongeza sana Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa jinsi ambavyo wameweza kuleta bajeti ambayo naamini na wenzangu wanaamini hivyo kwamba ni bajeti yenye matumaini kwa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kuwapongeza sana na niamini kwamba kile walichokuwa wamekiandika, basi wataenda kukitendea haki ili nchi nzima tuweze kufurahia matunda ya bajeti ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nisiwe nyuma sana, mimi kama mimi nilikuwa nazoea tu kusikia bajeti hii kuisoma au kuangalia katika runinga, lakini napenda pia nijipongeze kwamba ni mmojawapo sasa katika kuhakikisha kwamba bajeti hii inapita vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana niweze kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, mama ambaye amekuwa msikivu, nasi kama Wabunge hapa tulikuwa na vilio vingi ambavyo tumevisema, lakini amekuwa makini na kuvisikiliza hata kuifanya Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba yale tuliyoyasema yanakwenda kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa kilio kikubwa kwanza tulicholia kwa ajili ya barabara zetu za TARURA. Ameweza kutoa fedha shilingi milioni 500 katika kata zetu, nasi kama Wabunge ambao tunakwenda kuziangalia fedha hizi kwa makini, tuweze kupitisha barabara hasa ambazo zina vilio vikubwa vijijini pamoja na mijini kwetu, sisi tunaita barabara za ndani. Mfano kama kwangu, naweza kusema kwamba barabara zile za Tandika hakika ni muhimu sana kwani tunaita Kariakoo ndogo kule kwetu Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwamba tunamshukuru sana kwa fedha hizi. Siyo hilo tu, nampongeza kwa fedha ambazo naamini zinakuja, fedha zile za mashule kwa kujenga Shule za Sekondari katika kata ambazo zina mahitaji makubwa ya shule. Sitasita kuendelea kumpongeza mama yetu Rais kwa jinsi ambavyo hata juzi uwanja wa Mwanza kule ameongea mengi sana. Mama nakupongeza sana kwa sababu kwa hakika umetunyanyua sana wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizidi kuipongeza sana Serikali sikivu kwa kusikia hasa vijana wetu ambao wamekopeshwa bodaboda, wengine wamekuwa wakifanya kazi zile za watu wenye bodaboda, hata hizi faini zimeweza kushushwa sasa na badala ya kuwa shilingi 30,000/=, imekuwa ni shilingi 10,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu ndugu zangu, Wabunge wenzangu, nimetumwa na Jimbo langu la Temeke niwashukuru sana Wabunge wote waliolia kilio hiki na hata sasa vijana wale wanasema watafanya kazi kwa bidii na siyo tu kwamba watafanya bila makosa, lakini watatii sheria bila shuruti. Nawashukuru sana Wabunge wenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mengi ambayo wenzangu wameyaongea hapa, mimi leo nilisimama ili niweze kushukuru na kusema kwamba ahadi hizi zote zilizoweza kuwekwa hapa kwa niaba ya wananchi kupitia Wizara ya Fedha ya kwamba tunatamani kama alivyosema mwezangu hapa yasiwe katika maandishi. Sisi kama Wana- Temeke pia wananchi wote sasa hivi tumekaa macho, tunaangalia kwa macho, inawezekana mimi na wenzangu tunayasoma hapa na kuona kwamba yako kwenye maandishi, lakini wananchi wetu wako macho sasa kuangalia hivi fedha ambazo tunasema tumekwenda kuzitoa kwenye petrol, diesel pamoja na mafuta ya taa kwamba ni shilingi 100 inaongezeka, nasi tunaziomba ziende kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana sasa Wizara ya Fedha mziangalie hizi fedha na mtakapozileta hakika zije katika yale ambayo yanategemea kufanyika pamoja na hizi fedha, zisiwe tu katika maandishi lakini sisi tuko tunatoa macho sasa tuweze kuona barabara zetu kwenye elimu, afya hata dawa zinaweza kupatikana vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu kwamba Wizara ya Fedha nisikilizeni, mtakapokuja kutoa hotuba yenu ya mwisho hapa mtuambie mmeweka mkakati gani wa hizi fedha zinazokusanywa hili zitumike kwa mahitaji yanayotakiwa hasa katika majimbo yetu na hasa katika barabara pamoja na mambo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba naishukuru Serikali yangu sikivu na ninaamini ya kwamba yote waliyoyasema yatakwenda kutimia na Mungu awabarika sana. Ahsanteni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona nami niweze kuchangia baadhi ya masuala ya Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ameweza kunisimamisha mimi hapa pamoja na Wabunge wenzangu tukiwa salama.

Pia napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wangu, Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na hata sasa naamini kabisa huko aliko anatufanyia kazi na anatutendea haki kabisa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Temeke kwa madarasa tuliyopata, ni madarasa mengi sana na ukizingatia kwamba Temeke tunazaliana sana lakini ameweza kutupa madarasa mengi ambayo sasa mabinti pamoja na wavulana hakuna second selection; wote wamekwenda Form One kwa pamoja. Hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata zahanati kila Kata na tumebakiza Kata mbili ambazo ninaamini Kata hizi kwa bajeti inayokuja tutapata. Vifaa ambavyo vimekwenda katika hospitali zetu, kweli ni vya maana sana na sasa tunaringa sana Temeke kwa jinsi ambavyo tunapata tiba za uhakika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amewapa uwezo Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora, mdogo wangu Mheshimiwa Jenista pamoja na mdogo wangu Mheshimiwa Deogratius, kwa kweli kazi mnaifanya na tunashukuru sana, hakika hata sisi tunajivunia ninyi kuwa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenda tu moja kwa moja kwenye Jimbo langu la Temeke, hasa wafanyakazi wa Bandari. Wafanyakazi wetu wa Bandari kipindi kile wengi mliweza kuwasimamisha kwa sababu walikuwa na elimu ya Darasa la Saba, wengine walikuwa wamegushi vitu vingine. Hata hivyo mliwapa namna ya kuweza kujifunza au kujiendeleza ili waweze kuajiriwa tena. Wako baadhi ambao tayari kwa kweli nawashukuru sana waliweza kujiendeleza na wakaweza kuajiriwa upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo moja la wengine ambao hawakuweza kwenda kujiendeleza na sababu kubwa tunapoongea nao wanasema kwamba pesa ambazo walitamani mngekuwa mmewalipa kipindi kile walipoachishwa kazi wangeweza labda kuzitumia kujiendeleza, lakini mpaka sasa fedha zao hazijalipwa, wala hawajui lini watalipwa fedha hizo kwa sababu wametumikia Bandari muda mrefu sana. Pia walitamani wao wenyewe kwamba kama kweli, basi walikosea na hawakuweza kujiendeleza, lakini wanaomba sana wapate hata mafao yao waweze kuondoka ndani ya mji waliokaa hasa kule Temeke. Wakati mwingine wanaomba hata kuajiriwa mahali pengine, lakini umri umewatupa mkono, hawawezi kuajiriwa tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wizara hii iwaangalie hawa watumishi wa Bandari ambao wako kama 196 hivi kama sikosei, muwaangalie upya waweze kupewa fedha zao ili waondoke ndani ya miji hii na kurudi vijijini kwao kuendelea na maisha mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hawa wameshatufata mara nyingi, hata mdogo wangu Mheshimiwa Jenista ameweza kuongea na baadhi na kuliangalia hili jambo, naamini sasa kwa kusema kwangu, nao watasikia, kwa kweli mtawatendea haki ili waweze kurudi makwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko Bandari; wako madereva ambao wanaendesha magari yale makubwa. Siyo madereva tu wa yale magari makubwa, lakini naamini hata madereva hawa ambao wanaotuendesha, labda wanaweza wakawa wanawaendesha hata nyie viongozi wangu mlioko hapo; mishahara yao wanalalamika sana kwamba ni midogo sana, kiasi kwamba hata leo unapompa Dereva gari lile V8 kwa thamani yake na kumwendesha labda Waziri Jenista aweze kufika salama mahali anapokwenda kufanya kazi, hakika anakuwa amebeba mzigo mzito sana. Kwanza gari lilivyo na thamani, lakini pia utu wa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, naomba sana mwangalie upya mishahara yao. Tuone kwamba kazi wanayoifanya inalingana kidogo na mshahara wanaoupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa siyo mkaaji sana kwenye vijiwe lakini nimependa sana wakati wote kuwa ndani ya vijiwe vya wale madereva wa malori kule Bandari. Madereva wetu wa malori, inawezekana ni malori ya Serikali lakini pia ni malori ya wanafanyabiashara binafsi lakini. Mara nyingi nakuwa napita katika vijiwe vile, nakaa, naongea nao na wale Madereva kwa kweli wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wanasema unampa gari ambalo labda ni Scania la thamani kubwa sana, ameweka mzigo wa thamani kubwa sana, anaondoka nao hapa Tanzania kwenda nao labda Rwanda, Burundi, lakini mshahaara wanaopokea ni mshahara mdogo sana ambao utaona mara nyingi malori yetu yanakaa njiani, yanapaki njiani kwa sababu fedha uliyompa aweze kuacha nyumbani, lakini pia hiyo hiyo fedha aweze kujikimu yeye mwenyewe. Kwa hiyo, unaona wengi wanalala ndani ya magari yao katika baadhi ya vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia muwaangalie. Labda mtengeneze namna ya kuweza kuwafikia wale wenye magari makubwa, wafanyabiashara wakubwa wenye magari yao hayo ili mwone mtawasaidiajie hawa, kwa sababu huu ndiyo utawala bora ambao mama anataka. Hawa madereva nao ni wafanyakazi, ndiyo utawala bora unaohitajika uwaone nao wako katika utawala bora unaoelekezwa katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, ninaamini mnasikia na mtakaa na waajiri wao muone wanafanyiwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kuhusiana na Walimu. Walimu wetu pia ni waajiriwa, nao wanatamani kuwa katika utawala bora. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ameweza kujenga madarasa mengi sana nchi nzima, lakini Walimu wetu wanapotoka madarasani kufundisha wanakosa ofisi za kukaa. Ofisi zao wanaweza kutumia labda darasa ndiyo wakafanya ofisi na mahitaji yao ni madawati yale ya shule ndiyo wanafanya meza zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hili linakwenda kwa Waziri wa Elimu, lakini nilikuwa naanzia hapo kwa sababu ya utawala bora, kwamba sasa Walimu hawa wapate namna ya kukaa vizuri ili wanapotoka madarasani, basi wanavyokuja kusahihisha madaftari yale, wakae mahali salama ili wanafunzi wetu ambao tumewawekea madarasa nao wahudumiwe vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Ni kengele ya pili.

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Amiri Mkuu Jeshi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na pili niipongeze Wizara na hasa Mheshimiwa Masauni na Mheshimiwa Sagini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia kuhusu Gereza la Keko; hili gereza limekuwa la zamani na miundombinu yake hairidhishi kwani mahabusu ni wengi kuliko linavyoweza kubeba mahabusu hitajika kwa ukubwa wake. Naomba kuishauri Serikali kwamba ifanye maboresho ya gereza na ikiwezekana liongezwe kulingana na mahabusu wanaoingizwa pale ili kuweka hali ya afya yao vizuri, lakini pia Maafisa Magereza wanaoishi pale nyumba zao haziridhishi kwani ni chakavu pia magari yao ni ya muda mrefu. Niiombe Serikali iliangalie suala hili kwa makini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri na jitihada nzuri inayoendelea kufanyika kwa ajili ya kuiboresha elimu yetu chini ya usimamizi mzuri wa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu, mfano mzuri ni madarasa tuliyoyanayo kwa sasa na hakuna tena second selections.

Mheshimiwa Spika, elimu ni ujuzi na kujua kusoma ni muhimu, hivyo mimi niiombe Serikali ijikite kwenye kufudisha ujuzi kwa mtoto kwa vitendo zaidi kuliko masomo ya darasani mfano mtoto aangaliwe kwenye miaka minne ya mwanzo pale anapoanza shule kwa walimu wetu wenye utaalaam watawajua vijana hawa wanataka kufanya nini hapo baadae basi miaka mitatu ya kufikia darasa la saba waweze kupelekwa kwenye shule ambazo Serikali itakuwa imezitengeneza kwa ajili ya elimu ya ujuzi husika kwa mtoto kwani tutamjenga kijana kuweza kujiajiri au kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, niishauri Serikali kuanzia sasa tuangalie ni jinsi gani tunaweza kuzitenganisha hizi shule za sekondari kulingana na vipaji vya wanafunzi badala ya kusoma masomo yote kwa miaka minne basi wasome ujuzi wanaotegemea kujiajiri au kuajiriwa na hii itapunguza sana upungufu wa ajira kwenye Serikali yetu kwani wengi watajiajiri.

VETA ni muhimu sana lakini vijana wanajiunga baada ya kujiona hawakufanya vizuri miaka minne ya sekondari. Niiombe Serikali yangu sikivu iliangalie hili jambo kwa umakini zaidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mungu kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika kwa ajili ya kuiboresha afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kujitoa kwake kwa Watanzania kufanya kazi nzuri na nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, pongezi nyingi kwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri pamoja na watendaji wa Wizara ya Afya wote.

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi na kazi nzuri inayoendelea kufanyika, naomba nijikite katika Jimbo la Temeke.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Temeke iliyoko ndani ya Jimbo la Temeke imepandishwa hadhi na kuwa ya rufaa ya kimkoa lakini Serikali ilichukua hatua ya kutujengea Kituo cha Afya kilichopo Yombo Vituka kiitwachwo Malawi. Tunashukuru sana na majengo mazuri na ni ya kisasa ni ya ghorofa lakini lifti iliyoko pale ni nzima ila mkandarasi ameifunga isifanye kazi kwani hajalipwa pesa ya kuiweka pale na sasa ni zaidi ya mwaka na wahudumu wanapata taabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa uhai pia nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya katika Taifa letu, hakika Mungu ampe afya njema.

Mheshimiwa Spika, pongezi nyingi ziende kwa Waziri na Naibu wake wa Wizara hii ya Nishati pamoja na watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, niende katika Jimbo la Temeke; niwapongeze sana kwani kazi imewezakufanyika kwa ufanisi, tunashukuru umeme umeweza kuwa stable kuliko miaka ya nyuma, lakini niombe kwa kuwa jimbo letu la Temeke limekuwa ni jimbo la viwanda vingi na umeme umekuwa bado ni mdogo kwani hautoshelezi kwa viwanda na matumizi ya majumbani, lakini pia umeme bado tunapata kutoka Ilala. Tunatamani kupata ongezeko la transfoma kubwa ambayo itatuongezea umeme ukizingatia bado hatupati umeme mfululizo kwani katika wiki tunaweza kukosa, baadhi ya kata ukakatika kwa masaa kadhaa na ukirudi unarudi mdogo na wakati mwingine unarudi kwa baadhi ya mitaa ya kata moja na mitaa mingine ikakosa ndani ya kata hiyo hiyo.

Mheshimiwa Spika, niombe sana muangalie upya umeme unaopita chini ya ardhi, tupate vipuli vyake ili urekebishwe maana kila umeme unapokatika tunaambiwa hitilafu kubwa inatoka kwenye Kituo cha TOL pale Pugu Road, naamini mnapafahamu hivyo niombe sana Wizara ituangalie sana Jimboni Temeke, ni jimbo tunategemea sana mapato yetu ya ndani kutoka kwenye viwanda hivyo visipopata umeme kazi hazitafanyika na pia wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kufanya biashara zao ili mapato yaongezeke na Watanzania wa jimboni wafaidike na kazi nzuri ya matunda ya uongozi mzuri wa Mama Samia, Rais msikivu na myenyekevu.

Mheshimiwa Spika, nawapeni hongera sana kwa maonyesho ya Bungeni yamenifungua na mengi nimejifunza, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na mimi. La kwanza niweze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameweza kunisimamisha mahali hapa ili nami niweze kuongea kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Temeke. Nimshukuru sana Rais wangu Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri anayoifanyia nchi yetu ya Tanzania na hata sasa sisi wanawake tunajiona fahari kwa sababu tunaye kiongozi mwanamke ambaye hakika anaupiga mwingi.

Mheshimiwa Spika, nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Ummy pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa nzuri mnayoifanya, na tunaamini sana kwamba kwa sasa kazi hii itakwenda kufanyika vizuri na Watanzania tunawaamini sana. Lakini si ninyi tu, ni pamoja na timu yenu nzima ya Wizara ya Afya kwa kazi kubwa ambayo mnakwenda kuwafanyia Watanzania. Mimi pamoja na yote najua na ninaamini kabisa kwamba madaktari wapo, wauguzi wapo katika hospitali zetu; lakini nasema ni wachache. Kwa kuwa mmepata nafasi ambayo Rais amewaongezea muweze kuajiri basi tuombe muajiri kwa haraka sana ili hawa watumishi waweze kuwepo katika hospitali zetu nyingi na zahanati ambazo zimeongezwa na Rais wetu mama Samia Suluhu.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nijikite sana katika Jimbo langu la Temeke. Kwanza hospitali yetu ile ya Temeke imechukuliwa na imefanywa ni ya Rufaa ya Kimkoa. Lakini Serikali hamkutuacha hivyo Jimbo la Temeke mkatujengea hospitali nzuri sana ambayo iko Yombo Vituka, na ni hospitali ya kisasa na ni ya ghorofa. Kwa kweli tunawashukuru sana wana Temeke. Lakini pamoja na uzuri wa hospitali ile viko vifaa baadhi vimeshaingia, kwenye wodi zile viko vitanda na kadhalika ambavyo vimeingia.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna tatizo moja kubwa sana. Ni kwamba, ile hospitali ya mwanzo chumba cha operesheni kiko chini, na ni kidogo, kina kitanda kimoja tu. Ikitikea kama wagonjwa wako wamezidiwa operesheni inafanyika kwa mtu mmoja tu. Kwa hiyo niombe sana juu kule tulikojengewa lile jengo la ghorofa kuna chumba kikubwa sana cha operesheni lakini vifaa havijafika na fedha mnazo MSD. Tumetoa karibu mwaka mmoja na nusu sasa lakini hatuwezi kufanyiwa operesheni kule kwenye chumba cha juu. Na kikubwa zaidi kinachoharibu ni kwamba, hospitali ile mmeiwekea lift lakini yule mkandarasi ambaye aliweka ile lift ameifungia; takriban mwaka mmoja na nusu sasa hatuwezi kuitumia kwa sababu anasema anatudai Serikali.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, niwaombe sana, mdogo wangu Ummy mwende, sasa mkaangalie jinsi gani Serikali inaweza kulipa lile deni la mkandarasi ili sasa hata MSD waweze kuweka vile vifaa kwenye chumba kile cha operesheni kule juu ili watu wetu waweze kufanyiwa operesheni wakiwa juu; kama bado mtakuwa mnahitilafiana kwenye kulipana deni la ile lift.

Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania, hasa wana Temeke, naamini tunaipenda Serikali yetu, hivyo hatutaki kusema maneno mabaya kwa ajili ya Serikali. Tunajua ni kati ya ninyi pamoja na mkandarasi. Serikali tayari ninaamini wanatamani kuona sisi tunakwenda kwa lift ile.

Mheshimiwa Spika, na wahudumu ni wachache; pale wanapokuwa kwamba amefanyiwa operesheni chini inabidi wamsukume kwa stretcher kupandisha juu. Hali ni ngumu sana, na wauguzi wale ni wachache sana, kama nilivyosema. Kwa hiyo niombe sana ndugu zangu, lift ile ikafanye kazi. Lakin, pamoja na lift ile, vifaa vile kule juu viwekwe ili kile chumba kisikae bure.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wana Temeke tunajivunia pale kwa sababu tukizidiwa sana inabidi waende Temeke, na Temeke ni ya Rufaa sasa hivi, kupokelewa ni shida. Kwa hiyo naomba sana ndugu zangu, ninakuomba sana hawa wawe wasikivu, na ninaamini Serikali yetu ni Sikivu, kwamba watafanyia kazi hili jambo kwa sababu tayari mlete fedha zingine. Kilakala mnatujengea hospitali nyingine; lakini hii kama haijaisha kule Kilakala kweli itakwisha na kuletewa vifaa?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana, najua Mama Samia ni msikivu sana; tunapokwenda kuomba, kama kuna hitilafu ya fedha kidogo tukiomba naamini tunapewa fedha hizi. Ninamshukuru sana kwa sababu hata ile hospitali juzi tumeweza kuiangalia na mwenge ni hospitali nzuri ambayo tunakwenda kuikamilisha kipindi si kirefu, ile ya Kilakala.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu, lift hii ya pale Yombo Vituka wananchi wanafanyiwa operesheni, yaani ni kama foleni ambayo hata mimi wakati mwingine madaktari wanaponiita naona huruma. kwa kweli najisikia vibaya sana. Niombe sana lift hii ifanyiwe kazi, MSD msikie kilio chetu, kwamba vile vifaa vya chumba kile, hizo taa, sijui za kufanyia operesheni, vitanda hakuna ilhali fedha mnazo. Niombe sana Serikali sikivu iweze kutusikia sisi wana Temeke na kituo kile kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nashukuru kwa kuniona pia niweze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeweza kunisimamisha hapa niweze kuongea na kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri yenye mashiko ambayo mengi yamesemwa mule ndani na mengi yanaonekana yakifanyika kwa yale machache basi ninaamini kama Bunge tutaweza kuyafanyia kazi yaweze kuendelea kufanya kazi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa wangu Mama Samia kwa kazi nzuri ambayo ameifanya na anaendelea kuifanya, amekuwa ni mama bora na amekuwa ni mama ambaye hakika mimi amenikosha sana kuifanya demokrasia sasa inafanya kazi nzuri kwa ajili ya mustakabali mzima wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Samia ameweza kuleta fedha nyingi sana kwenye Jimbo letu la Temeke naweza kusema kwamba ni mabilioni nikianza kutaja moja moja hapa; kwa kweli ninasema inawezekana ni upendeleo mkubwa kwa sababu ni jimbo la mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeweza kujenga mambo mengi, shule za sekondari na kama siku zote tunavyolalamika kwamba tuna watoto wengi kwenye jimbo letu lakini sasa hivi hakuna mtoto anayebaki kuanza shule darasa la kwanza au shule ya awali. Kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri hii ambayo anaendelea kuifanya na ninaamini bado ataendelea kuifanya kwa miaka inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa katika Jimbo langu la Temeke. Jimbo langu la Temeke hasa upande wa eneo la Kurasini. Kurasini imekuwa kama ni eneo ambalo la uwekezaji lakini yapo mambo ambayo kidogo hayafurahishi. Tumekuwa na eneo lile DAWASA ambalo wanakwenda kumwaga maji taka, watu wako pale ambao eneo lile sasa hivi limekuwa kwa kweli ni kero kwa eneo letu la Jimbo la Temeke hasa upande wa Kurasini. Wameweza kulipa fidia kidogo sana na watu bado hawajaondoka kwa sababu hawajamaliziwa fidia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Serikali waliangalie hili tena upya. DAWASA naamini wanalifahamu vizuri na walishapelekana mpaka mahakamani lakini

walivyoambiwa kwamba wamalizie wale watu mpaka sasa hawajaweza kumaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio eneo hilo tu Kurasini kama ninavyosema katika Jimbo letu la Temeke ni eneo la uwekezaji. Wako hawa ndugu zetu wa eneo la EPZ wana eneo kubwa sana ambalo sasa hivi limekaa wazi halifanyiwi kazi. Lakini wako wananchi waliopewa fedha ambazo kuanzia mwaka 2015 wamelipwa mpaka sasa 2023 bado mapunjo yao hayajakuwa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali yangu Serikali sikivu waangalie sasa wananchi hawa kwenye mapunjo haya waweze kufidiwa ili waweze kuondoka katika maeneo hayo hasa lile eneo la DAWASA kwa sababu ni kero, kwa sababu hata DAWASA wenyewe sasa hivi hawalitengenezi hawalifanyii kazi yoyote nzuri ili wananchi wale waweze kukaa mahali salama. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali iweze kuwalipa waweze kuondoka kwa kadri ambavyo afya zao siyo nzuri kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba yapo maeneo mengine ambayo tunatamani sisi kama Jimbo la Temeke tuweze kupatiwa hasa lile eneo la EPZ hawajalifanyia kazi mpaka sasa, sisi wenyewe tunalitamani kama Jimbo la Temeke au Halmashauri yetu ya Temeke tuweze kufanyia kazi. Zaidi ya hayo niombe basi Serikali kama inaweza kuifanyia kazi kwa mapema kuweka uwekezaji pale ninaamini vijana wetu wa Jimbo la Temeke na hasa halmashauri yetu watapata ajira kuliko linavyokaa wazi hivi bila kufanyiwa kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niombe Waziri wa Maji pamoja na Waziri wa Ardhi tuweze kwenda pamoja jimboni tukawasikilize wananchi hawa jinsi gani wanavyolalamika ili tutoe msimamo sasa au Serikali itoe namna gani ya kuweza kuwaondoa wale watu pale kwa fedha ambazo zimebaki ili wananchi wale waende kukaa sehemu zingine nae neo lile Serikali iweze kuendelea kwa mustakabali wanaoweza kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba wananchi wangu wa Jimbo la Temeke wamenituma nimwambie Mheshimiwa Rais tumeweza kuomba na maombi haya tunaomba sana sana Wananchi wa Temeke Mungu azidi kumpa hekima, maono, mafunuo ili aweze kuendelea kuiongoza nchi yetu kwa jinsi anavyoendelea kuiongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niombe pia kwamba Jimbo letu la Temeke na Wananchi wangu wa Temeke wamenituma na kusema sisi kama wana Temeke tunalaani vitendo vya ubakaji, ushoga, usagaji na mambo mengine yote yanayofanana na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mungu kwa uweza wake na napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanyika na hata zile alizoziibua kwa miaka hii miwili yote inaendelea kwa kasi sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pongezi kwa jopo la Mawaziri wote na Naibu Mawaziri kwa kuungana na Rais Samia na Makamu wa Rais Mheshimiwa Mpango na Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa katika kuendeleza mpango mzima wa kuendeleza nchi yetu. Kazi Iendelee.

Mheshimiwa Spika, naomba kuzungumzia jambo la VAT kuongezwa kiwango ndio itapelekea ukwepaji wa kodi na pia ndio inaleta kufanya mazungumzo kati y muuzaji na mnunuzi ya na risiti au bila ya risiti bila kuwa na uelewa wa ukusanyaji VAT bado ugumu wa ukusanyaji wa VAT utakuwa mgumu.

Mheshimiwa Spika, hapa tuangalie zaidi kuongeza wafanyabiashara, ni lazima kuhakikisha wigo unaongezeka ili kuhakikisha idadi ya walipakodi inaongezeka.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 70 wa hotuba ya Waziri wastani wa walipakodi kulingana na ukuaji wa wananchi na ongezeko la mahitaji kwa mwaka 2021/2022 walipakodi waliosajiliwa ni 4,455,028 lakini wenye TIN kati yao ni 1,641,173 ndio maana wafanyabiashara wengi wanakwepa TIN kwa kuona ni usumbufu wa tozo za Serikali.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara iangalie mfumo mzuri wa malipo, kuwe na sheria inayosimamia malipo yaani angalau kuwe na muda maalum wa malipo kwa Serikali mfano malipo ya SDL/PAYE/WCF/Mifuko ya Jamii/VAT na kadhalika. Pia iwepo tarehe maalum kila mwezi na usipolipa kwa muda kuwe na riba adhabu italipwa na muhusika wa kampuni iliyochelewesha malipo ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mwisho niishukuru Serikali yangu kwa miradi yote waliyoleta jimboni Temeke; vituo vya afya, shule za ghorofa, barabara za TARURA na kadhalika, lakini zaidi sana Mradi wa DMDP unaokwenda kuanza mwezi wa Aprili, 2024.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Temeke tunamshukuru sana Rais na wasaidizi wake wote, Mungu Ibariki Tanzania Kazi Iendelee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa ajili ya Mheshimiwa Rais Mama Samia kwa kazi nzuri anayoifanya kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wizara nzima ya Nishati kwa kazi nzuri pamoja na changamoto zilizopo, lakini mmekuwa mnapambana nazo na zinaendelea kutatuliwa, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kuchangia kuhusiana na Jimbo la Temeke ukizingatia ni mji mkongwe na miundombinu ya umeme ni ya muda mrefu. Kwanza nguzo nyingi zimeoza hivyo kupelekea kuanguka kila mara na wananchi kukosa umeme, lakini pia miundombinu inayopita chini ya ardhi inasumbua muda mrefu, niiombe Wizara hii iangalie namna Temeke itakavyoweza kurudi kwenye hali ya kawaida kwani bado umeme wetu tunapata kutokea Ilala. Ni mkakati gani sasa Serikali itafanya kuhusu Temeke kwani ni jimbo lenye viwanda vingi, umeme hautoshi na tunakosa mapato ya ndani kwani kila tukitembelea viwandani umeme haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana mtuangalie upya kwani hali si nzuri, hata TANESCO mnakosa mapato kwani viwanda vingi hawalipi kulingana na utumiaji wa umeme kwani umeme ukipatikana kwa mfululizo nao watafanya kazi kwa muda mrefu na bill zitakuja na kuleta mapato ndani ya Shirika la TANESCO. Niiombe Wizara itushughulikie tupate umeme katikati ya Jiji la Dar es Salaam ambalo ni jiji la biashara, kukosa umeme haieleweki, mtuangalie. Ahsanteni sana.