Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daniel Awack Tlemai (25 total)

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 na mgogoro uliopo umekuja mwaka 2003 ambao umeweza kuchukua maeneo ya wananchi wa eneo hili la Kata ya Mbulumbulu, Kijiji cha Lositete. Sasa ni nini majibu ya Serikali kwa sababu mwaka 1959 kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, hakukuwa na mgogoro, lakini mgogoro umekuja baada ya marekebisho ya mwaka 2003.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni lini Waziri yuko tayari kuongozana nami ili ajionee katika maeneo ya Kata ya Mbulumbulu, eneo la Lositete ili kuona kwamba wananchi jinsi wanavyopata shida katika eneo hili la Lositete? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati hifadhi hizi zinaanzishwa mwaka 1959, wilaya zilikuwa ziko ndani ya wilaya za zamani. Kwa mfano; Karatu ilikua ndani ya Mbulu na sasa hivi Karatu iligawanywa, lakini pia na Ngorongoro ni Wilaya, kuna Monduli na kadhalika. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, ni kwamba haya maeneo yalienda kutafsiriwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa pamoja na Wilaya na walishirikishwa wananchi kutambua ile mipaka.

Mheshimiwa Spika, huu mpaka ambao unagombaniwa ni mpaka ambao ni wa muhimu sana kiuhifadhi; kwanza unatunza maji, unatunza mazingira, lakini pia, hawa wananchi walioko kwenye maeneo yale wanang’ang’ania kuingia mle kuchunga mifugo yao. Hatari itakayojitokeza ni kwamba maeneo mengi tunaenda kuyamaliza na tutasababisha kuwepo na tatizo la kukosa maji na wananchi katika maeneo yale wataweza kuathirika.

Mheshimiwa Spika, niwaombe wananchi watambue kwamba Serikali ina nia njema ya kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya jamii zinazozunguka maeneo hayo. Pia eneo lile tumelihifadhi kwa ajili ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo kuna eneo ambalo ni msitu ambao unahifadhiwa kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya wenyeji waliomo ndani yake. Niwaombe sana wananchi watambue kwamba Serikali ina nia njema na inawapenda ndiyo maana inahifadhi maeneo haya kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Spika, ombi lake la pili la kuongozana na mimi, nimtoe wasiwasi tutaongozana wote kama ambavyo nimefanya kwenye ziara zangu nyingi baada ya Bunge la mwezi wa Sita kuisha, kwa hiyo tutakwenda pamoja. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali iliahidi kwa muda mrefu sana Barabara ya Karatu – Mbulu – Singida na mpaka sasa hamna dalili yoyote ya kujenga kwa kiwango cha lami. Je, ni lini Serikali itatenga hela kwa ajili ya Barabara ya Karatu – Mbulu – Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Karatu – Mbulu – Singida ni kati ya barabara ambazo zimeainishwa kwenye ilani na ambazo zinategemea kujengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Karatu na wananchi wa Karatu na wote watakaonufaika na barabara hizi kwamba, kadiri Serikali itakavyopata hela na katika kipindi hiki cha miaka mitano barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali iliahidi babarara ya Njiapanda Mang’ola, Matala Mwausi Lalago, kwa kiwango cha lami kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi sasa ni lini bararara hiyo itajengwa kwa kiwango cha Lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea kupitisha ama kuleta bajeti yetu ili iweze kujadiliwa naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira ili kipindi cha bajeti tutaitolea maelezo sahihi kuhusu hiyo barabara ambayo ameisema na nimhakikishie tu kama nilivyosema kwenye majibu mengine ya msingi na wananchi wa Jimbo lake kwamba barabara ambazo zote zimeahidiwa na kuwa kwenye Ilani zipo kwenye mpango wa Kipindi cha Miaka Mitano na tutazijenga kadri ya fedha zitakapoendelea kupatikana. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na kwamba sijaridhika na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mauaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika Hifadhi ya Lake Manyara; imetokea mwaka 2005, ikatokea mwaka 2015 na ikatokea tarehe 28/10/2020 ng’ombe wapatao zaidi ya 10 walipigwa risasi wakikutwa kijijini wakidai kwamba wamefuata nyayo. Askari wa Game Reserve wakaenda mpaka nyumba ya mtu huko kijijini na ng’ombe kumi kupigwa risasi.

Vilevile tarehe 28 mwezi wa Novemba, walipigwa risasi watu wanne kule msituni na kuchomwa moto. Nami ni shahidi, nikaenda msituni kule kuwatafuta wananchi hawa na kupata mabaki na mabaki yale yakapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali:-

Je, ni lini wananchi wale watapata majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, Hifadhi ile ya Lake Manyara ikihamishwa mipaka mara kwa mara kila mwaka kutoka Hifadhi ya Lake Manyara:-

Je, Waziri yuko tayari kufuatana nami kwenda kujionea mpaka jinsi unavyohamishwa katika Lake Manyara National Park?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niendelee kutoa pole kwa wananchi wa Karatu kwa kadhia hii ambayo waliipata. Niwakumbushe tu kwamba, wananchi kwa asilimia kubwa wanatumia nguvu ikiwemo kutotii sheria za uhifadhi na hivyo kusababisha hawa Askari sasa kujichukulia sheria ambazo kimsingi wananchi wangetii kusingetokea vurugu yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuendelee kushirikiana kuelimisha hawa wananchi. Hili suala la tarehe 28/11/2020 naomba tu waendelee kuwa subira kwa sababu ni taarifa za kiuchunguzi na Askari tayari walishachukua sample na wakapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Hivyo, majibu yatatolewa na Jeshi la Polisi baada ya kufanyika uchunguzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili. Niko tayari kuongozana naye kwenda kuangalia maeneo haya na kuonesha mipaka halisi kama ambavyo ameomba. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwenye majibu ya Waziri, Barabara hii ya Karatu – Mbulu – Haidom – Sibiti, lakini kwenye Ilani kuna barabara hii ya Lalago – Mwanhuzi – Kolandoto – Matala – Karatu. Sasa kwenye majibu ya Waziri amesema kilometa 25 kupitia Barabara ya Karatu – Mbulu, sasa ni lini Barabara ya Lalago
– Kolandoto – Mwanhuzi – Matala – Karatu itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara zote mbili ambazo amezitaja ziko kwenye bajeti lakini pia zinajengwa kwa awamu kwa Kulandoto na maeneo mengine ambayo yametajwa tutaenda hatua kwa hatua kadri ambavyo tutapata fedha. Lakini bahati nzuri kwamba ipo kwenye bajeti, pia vipande baadhi vimeanza kujengwa kwa mwaka wa fedha huu ambao unaendelea, ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ilituma Wizarani mara nyingi kwamba kuna mashamba hayo aliyoyataja Mheshimiwa Naibu Waziri, kati ya mashamba 33 yanayoendelezwa kwa robo moja tu katika mashamba yale yote 33; lakini kwa kuwa shamba hili la Bendhu mmiliki wake alifariki na akamwachia mwanae ambayo yupo nchini Zimbabwe na baadaye wafanyakazi wale hawajaweza kulipwa muda wote tokea mmiliki yule aliyefariki namba moja na yule aliyeachiwa shamba hilo hajaweza kuonekana mpaka muda huu. Sasa ni lini majibu ya Serikali kwamba hili shamba la Bendhu wafanyakazi wale wote wanaweza kupata haki yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Waziri atakubaliana nami kwenda katika Jimbo la Karatu kuona mashamba haya 33 yote, ajionee kwamba haya mashamba hayaendelezwi. Kwa mfano katika Kata ya Oldeani hata mahali pa kuzika mtu hakuna kwa sababu mashamba yale yote yapo chini ya uwekezaji na wakati huo kutoka Fireland Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa msitu mwingine baada ya Fireland ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro. Je, ni lini Waziri atafuatana na mimi kwenda katika Jimbo la Karatu kujionea mashamba haya hayaendelezwi katika majibu aliyotoa kwamba anaona mashamba haya yanaendelezwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daniel, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda karatu mimi na yeye tumeshakuwa na maongezi tutakwenda na tutapanga tarehe pamoja ambayo tutakwenda kutembelea, kwenda kuangalia hayo mashamba na matatizo ya wakulima wa vitunguu ambao wanakabiliana nayo. Pia kuhusu Shamba la Bendhu nimeshajibu kwenye swali la msingi Serikali sasa hivi hatuwezi kusema jambo lolote kwasababu jambo hili lipo mahakamani tunasubiri shauri hili liishe mahakamani then tunaweza kufanya intervention.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa viongozi wakuu waliahidi kiwango cha kilimeta 10 katika Mji wa Karatu mwaka 2010 – 2015 na 2015 - 2020 mpaka leo hii hatuna hata kilometa moja: sasa ni lini ahadi ya viongozi wakuu itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Awack kuhusu ahadi za Viongozi wa Kitaifa ya kujenga barabara kilometa kumi katika Mji wa Babati, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kazi ya Serikali ni kujenga barabara hizo kama zilivyoahidiwa na Viongozi wa Kitaifa. Ujenzi huo kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zitajengwa katika awamu hii ya miaka mitano. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira na kadri bajeti itakavyoruhusu, hiyo barabara ya kilomita 10 itajengwa katika Mji wa Babati. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika Wilaya ya Karatu kuna Mji Mdogo wa Karatu, sasa huu Mradi wa REA umelenga sana kwenye vijiji na pale Mji wa Karatu wanasema ni mjini lakini ni bado vijijini sasa ni lini Serikali ina mpango gani katika ile miji midogo ambayo umeme huu wa REA haujapelekwa ili kuwasaidia wananchi wakiwemo wa Jimbo la Karatu wa Mji wa Karatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Awack, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli upelekaji wa umeme unaofanywa na Serikali uko katika picha na maeneo tofautitofauti; ziko hizo tunazoziita REA ambapo tumekuwa na awamu kadhaa, lakini iko miradi ya densification, inapeleka umeme kwenye vitongoji, lakini hiko miradi tunaita peri-urban.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya peri urban inapeleka umeme kwenye maeneo ya miji lakini ambayo bado yana asili ya vijiji, Jimbo la Bukoba Mjini likiwemo na kwa Karatu ikiwemo, maeneo ya Mwanza yakiwemo, Geita ikiwemo, tutahakikisha kwamba kufikia mwezi Februari tumeanzisha huo mradi wa peri-urban unaoweza kupeleka umeme kwenye maeneo ambayo ni ya mijini lakini bado yana asili ya vijiji ili na sisi pia tuweze kunufaika na umeme huo.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika Mji wa Karatu tuna bodi mbili za maji, Bodi ya KARUWASA inauza maji kwa shilingi 1,700 kwa unit, Bodi ya KAFIWASU inauza maji kwa kwa unit 3500. Sasa ni lini Serikali itaweza kuweka bei ya uwiano katika Jimbo la Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Karatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi gharama za kulipia maji zimekuwa zikifanyiwa marekebisho kila inapobidi kwa kuzingatia uendeshaji wa mradi wa maji wa eneo husika. Hivyo, kwa Jimbo la Karatu nao mchakato unaendelea na tunaamini kabla ya mwaka huu wa fedha kukamilika basi bei hizi zitakuwa rafiki na itakuwa kwa manufaa zaidi ya wananchi.
MHE. DANIEL T. AWACK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru Serikali kwa bei elekezi katika eneo la Mji wa Karatu. Pamoja na shukrani hizi nina swali moja la nyongeza. Je, ni lini Serikali itatoa bei elekezi katika maeneo mbalimbali vijijini kutokana na kwamba kwa sasa bei ni tofauti kati ya kijiji na kijiji na hizi bei huwa inaamuliwa na Jumuiya za Maji Vijijini? Je, ni lini Wizara itatoa bei elekezi katika maeneo mbalimbali katika Jimbo la Karatu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, kubwa ambalo nataka nilieleze Wizara yetu ya Maji eneo la vijijini, tunatoa huduma kupitia Taasisi yetu ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA). Tulifanya tathmini kuona baadhi ya maeneo ya mjini na vijijini unakuta eneo la vijijini walikuwa wakilipa gharama kubwa katika suala zima la ulipaji wa maji. Wizara imeshatoa bei elekezi, ipo miradi ambayo inatumia nishati ya umeme, ipo miradi ambayo inatumia nishati ya jua. Kwa hiyo tumetoa maelekezo kila mradi kutokana na pump zinazotumika imewekwa hela yake rasmi kwa ajili ya kulipa hususan kwa maeneo ya vijijini.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi; je, Serikali itajenga lini skimu ya umwagiliaji katika Bonde la Eyasi ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji unaoendelea kwenye bonde hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ya mwaka huu wa fedha Skimu za Eyasi zimebainishwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji katika bajeti hii na katika utekelezaji wa mradi huo hivi sasa tupo katika hatua ya manunuzi ya kumpata mkandarasi ili utekelezaji uanze mara moja.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Je, ni lini Serikali itamalizia Mradi wa Bwawani katika Mji wa Karatu ili kukidhi uhitaji wa maji katika Mji wa Karatu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Awack, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ameulizia kuhusu kumalizia mradi ambao tayari upo kwenye utekelezaji. Miradi hii tunapoianza inakuwa na ukomo wake, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutasimamia vizuri mradi ule ambao Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ndio alifika pale na kutatua hii changamoto, hivyo tutasimamia kuhakikisha ndani ya muda wa mkataba mradi unakamilika.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante: -

Mheshimiwa Spika, kuna korongo la Mto Barai katika Kijiji cha Durgeda ambalo linaleta uharibufu katika chemchemi ya Mto Durgeda. Waziri alitoka mwezi huu wa Tatu katika neo lile alisema kwamba, utekelezaji ungeanza ndani ya mwezi mmoja.

Je, lini utekelezaji wa Mto huu Barai utaanza ili kuokoa chemchemi ya Mto Durgeda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel AwaCk, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, korongo hili ni moja ya maeneo ambayo Bonde la Mto Pangani wanashughulika nalo. Hivyo, niseme tu kwamba, shughuli zitaendelea na sasa hivi wapo kwenye maandalizi wanakuja kutekeleza majukumu yao.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwakuwa Benki hii ya Kilimo imeanzishwa kwa namna ya kuwasaidia wakulima wa Tanzania na hii benki inapatikana katika center ya Makao Makuu.

Je, Wizara ina mkakati gani wa hii benki hata kama itashindikana kwa kila Mkoa angalau iende kwenye kila ukanda wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja kwanza ieleweke Tanzania Agricultural Development Bank, siyo Commercial Bank is a Development Bank. Kisera tusitajarajie nami nataka niwe mkweli mbele ya Bunge lako Tukufu. Tusitarajie TADB kuwa na matawi kama alivyo CRDB na NMB, huo ndiyo ukweli. Jukumu la kisera la TADB ni Benki ya Maendeleo ambayo moja ya function yake ni ku- de risk sekta ya kilimo kwa kutoa dhamana kwenye commercial banks, ili commercial banks ziweze kuwakopesha wananchi, hili ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tumeitaka TADB iwe na ofisi katika Mikoa na Kanda, sasa hivi Kanda ya Kati wapo, Kanda ya Magharibi wapo, Kanda ya Ziwa wapo, Kanda ya Kaskazini wameshafungua ofisi. Kwa hiyo, wana ofisi zao. Wanachokifanya sasa hivi TADB ni kuwa na makubaliano na commercial banks ambazo zitafanya kazi na wao na wao wanatoa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako kuwaambia sekta ya kilimo sasa hivi imekuwa ikipata mikopo mingi sana kutokana na guarantee zinazotolewa na Tanzania Agricultural Development Bank. Tunaendelea majadiliano na TADB kuboresha na kufanya awareness kwamba namna gani huduma zao zinaweza kuwepo katika taasisi za benki, katika Mikoa na Wilaya ili angalau wawe na madawati waweze kufanya kazi vizuri na Commercial Banks.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tusidhani kwamba TADB ni kama ilivyo CRDB, NMB ama ilivyo Akiba Commercial Bank hii ni Development Bank ina majukumu yake ambayo yamewekwa wazi. Nasi tunawaomba Waheshimiwa Wabunge tuache kuitaka TADB kwenda Wilaya, bali tui- demand TADB itoe dhamana kwenye Commercial Banks ili wakulima wadogo wadogo wasiokuwa na dhamana waweze kukopesheka kirahisi na Commercial Banks. (Makofi)
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Barabara aliyoitaja ya Mbulu- Singida ni tofauti na barabara ambayo ameuliza muuliza swali ambayo inatoka njia panda ambayo inaelekea Mangola ambayo inaelekea Matala ambayo inaelekea Lalago ambayo pia imeunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. Sasa ni lini Serikali itatoa majibu sahihi ya barabara hiyo kuanza kama alivyotoa majibu ya barabara ya Mbulu-Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Awack, Mbunge wa Babati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ziko barabara mbili ambazo nazifahamu kutokea Babati. Aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge na niliyoitaja ni barabara ambazo zinakwenda parallel na zinakwenda kukutana mbele. Nimesema Serikali imeamua kujenga kwanza Barabara ya Serengeti bypass ambayo inaanzia Babati – Mbulu - Haydom kwenda Sibiti. Ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Lake Manyara Airport utajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Spika, uwanja alioutamka Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa viwanja ambavyo vipo chini ya Benki ya Dunia na tayari tupo katika mchakato wa kutangaza tenda ili viwanja hivi viweze kujengwa kikiwemo na Kiwanja cha Tanga, ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara hii imeahidiwa toka Serikali ya Awamu ya Nne na iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Je, ni lini Serikali sasa itatenga angalau kwa kilomita chache ili kuwezesha wananchi wale wa Bonde la Eyasi kuweza kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko ya nchi ya jirani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tunatambua kwamba barabara hii ni muhimu sana. Kama nilivyosema katika jibu la msingi, barabara hii ilitakiwa ijengwe lakini imejengwa barabara ambayo ni Serengeti Southern Bypass.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inachofikiria kufanya ni kujenga walau kilometa 50 ambazo zitaanzia pale Njia Panda hadi eneo la Mang’ola ambalo lina uzalishaji mkubwa sana na hasa zao la vitunguu. Kwa hiyo, Serikali sasa inafikiria kulifanya halafu baadae ndiyo ije kukamilisha kipande kilichobaki ambacho kinapita sehemu kubwa ya mbuga, ahsante.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Kama katika Mji wa Karatu waliweza kushusha bei kutoka shilingi 3,500 mpaka shilingi 1,300 kwa unit. Je, inashindikana nini katika jimbo hilo hilo katika eneo la RUWASA vijijini majini kuuzwa kwa shilingi 2,500, kwa nini kwenye jimbo moja isishushwe bei ikawa ya uwiano Karatu Mjini na Karatu Vijijini ikawa na bei moja kuliko kuwa na bei mbili katika Mji wa Karatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za maji hazifanani kwa sababu ya teknolojia zinazotumika kusambaza maji. Teknolojia ambayo inatumika eneo la RUWASA ni tofauti na pale mjini. Kwa hiyo sisi kama Wizara tunachokifanya ni kuhakikisha bei zinakuwa rafiki kwa wananchi wa eneo husika. Kwa hiyo, kwenye maeneo haya ambayo yanahudumiwa na RUWASA bei ziko tofauti kwa namna ambavyo maji yanasukumwa na gharama za uendeshaji.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga skimu katika Bonde la Eyasi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Machi, 2023 tulisaini mikataba ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mabonde 22 ya kimkakati hapa nchini Tanzania likiwemo Bonde la Eyasi. Kwa hiyo maana yake skimu zote za Eyasi zitajengwa katika mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya kilometa 10 katika Mji wa Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakaa naye Mheshimiwa Mbunge kwa sababu bado sijaelewa ahadi hii ilikuwa iko vipi. Nitakaa naye Mheshimiwa Mbunge ili aweze kunielewesha vizuri ahadi hii ya kilometa 10 ilikuwa ni ahadi ipi na tuweze kujua kama ni ya TANROADS au ni ya kwetu halafu tuone ni namna gani tunaweza tukapata fedha ya kuanza kutekeleza walau kwa kilometa moja moja ili iweze kukamilika kule Karatu.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, ni lini barabara ya Oldiani – Mang’ola – Matala – Lalago itajengwa kwa kiwango cha lami na kuwa ni barabara inayounganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu? Ni Sera ya Wizara ya Ujenzi kuunganisha Mkoa kwa Mkoa. Ni lini ujenzi wake utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyotaja ni kweli, ni barabara kuu, lakini mpango wa Serikali kwa sasa ni kutafuta fedha kwanza kuijenga kutoka Oldiani mpaka Mang’ola kwenye eneo ambalo wanazalisha sana zao la vitunguu. Kadri tutakavyopata fedha, basi tutaendelea kutoka Mang’ola hadi Sibiti kwa kiwango cha lami, lakini kwa sasa Serikali tunafikiria kuijenga kwa kiwango cha lami Oldiani Junction mpaka Mang’ola, ahsante.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Barabara ya Kibaoni – Endabash itapandisha kuwa hadhi ya Mkoa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoka kusema hapo awali, kwa mujibu wa Sheria ile ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya Mwaka 2009, zinaelezea ule utaratibu, inatakiwa mchakato uanze kwao wenyewe kwa kupendekeza barabara hiyo kupandishwa hadhi kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa, kisha aandikiwe Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mwenye dhamana ya barabara na atume timu kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa barabara hiyo, ndipo barabara hiyo iweze kupendekezwa na kufikiriwa kupandishwa hadhi.

MHE. DANIEL T. AWACK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ahadi hii ya kilometa kumi ni toka Rais wa Awamu ya Nne, na leo tuko na Rais wa Awamu ya Sita; je, ni lini ahadi hii ya kilometa kumi itatekelezeka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Karatu uko center ya mji wa kiutalii, kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Lake Manyara, National Park na hifadhi ya Serengeti. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kujenga kilometa kumi ili kuimarisha mji uwe wa kiutalii katika Mji wa Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Awack, Mbunge wa Jimbo la Karatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali tutaendelea kutenga fedha kila mwaka kuhakikisha ahadi za viongozi wetu wakuu ambazo walizotoa zinatekelezeka katika Jimbo la Karatu. Serikali inaona haja muhimu kabisa ya kuhakikisha kwamba barabara hizo zinakamilika kwa sababu ya umuhimu wa eneo la Karatu hususan katika sekta ya utalii.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsnate. Wananchi wa Kijiji cha Kambi ya Simba Kata ya Bulumbulu wamejenga ghala kubwa ya kuhifadhia mazao yao lakini halijakamilika.

Je, lini Serikali itaweza kwenda kukamilisha lile ghala iliyopo katika Kijiji cha Kambi ya Simba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la awali. Ni kwamba NFRA wamefanya tathmini ya maghala yote nchini na wameshatupatia hiyo taarifa, tunachokifanya sasa hivi sisi tunatafuta fedha na maghala yote nchini tutamaliza kwa fedha za ndani, likiwemo ghala hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema.
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Kata ya Endamaghang na Kijiji cha Endamaghang kuna mgogoro uliodumu muda mrefu na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro toka mwaka wa 2003. Sasa ni lini Serikali itaweza kutatua mgogoro huo ambao umedumu tangu mwaka 2003 mpaka leo hii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tuna migogoro mipya na migogoro ambayo Kamati ya Mawaziri Nane inaendelea kuitatua. Kwa hii migogoro mipya nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeendelea kuhamasisha maeneo yote ambayo yana migogoro hii tuanze pia kuyapitia upya na kuyatolea ufafanuzi ikiwemo kutatua au kutafsiri mipaka kati ya ramani za vijiji na ramani za hifadhi.

Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tutafika katika eneo lake ili tuweze kutoa ufafanuzi na pale ambapo itaonekana ramani zimeingiliana, basi Wizara ya Ardhi watatatua changamoto hii na tutaendelea kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa.