Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Daniel Awack Tlemai (10 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu ni siku yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge lako tukufu, lakini vilevile niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Karatu kwa kunichagua kwa kura nyingi na hatimaye nikawa jimbo la Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikishukuru chama changu Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini na mimi kupeperusha bendera na hatimaye nikawa Mbunge wa jimbo la Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mchango wangu utajikita katika maeneo ya kilimo kama walivyoongea Wabunge walio wengi katika ukumbi huu, lakini vilevile katika jimbo la Karatu sisi ni wakulima, tunalima mazao ya kitunguu, mahindi na mbaazi, lakini ushauri wangu ni nini kwa Serikali na Wabunge walio wengi hapa wameongea kwamba katika eneo hili la kilimo Wabunge wengi wamechangia kwamba suala hili la kilimo kuwekwa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Karatu imetokea mara nyingi sana katika Wizara ya Kilimo kwamba sasa kipindi chakula kikiwa kidogo ndani ya nchi wanasema mazao yetu tusipeleke nchi za nje, lakini wakati huo mkulima huyo amelima kwa shida, wakati huo mkulima huyo wa Jimbo la Karatu na wa nchi ya Tanzania amelima kwa mikopo ya benki na kila kitu, lakini wakati huo Wizara ya Kilimo inasema tusipeleke mazao yetu nje ya nchi kwa sababu ndani ya nchi hii kuna uhaba wa chakula. Sasa ninataka kujua, hivi ni kazi ya wakulima wa Tanzania kulisha watu waliokuwa mjini ambao wanakaa kwenye baridi na wakati huo sisi tufanye kazi ya kulisha walioko mjini kwamba sasa tusiuze mazao yetu nje kana kwamba ndani ya nchi hii ya Tanzania kuna shida ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa nini mazao yetu tusiuze yakaisha kabisa baadae tukaagiza chakula kutoka nje kikaja ndani ya Tanzania kama tunavyoagiza mafuta yanaisha ndani ya nchi hii na baadae tunaagiza nje ya nchi ili kwamba watu wetu waweze kupata pesa katika eneo hili la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo katika Jimbo langu la Karatu tunalima kilimo cha aina mbili; kuna kilimo cha mvua na kuna cha umwagiliaji na sisi pale tuna tarafa nne katika Jimbo la Karatu lakini Tarafa ya Eyasi inalima kilimo cha umwagiliaji lakini tarafa nyingine zinalima kilimo hiki cha mvua na kule kwenye Jimbo langu la Karatu ukiwa unalima kilimo kile cha mvua unaweza kupata gunia tano kwa hekari mpaka gunia kumi, lakini unapolima kilimo kile cha umwagiliaji unaweza kupata gunia 30 mpaka gunia 40. Sasa ushauri wangu ni nini kwa Wizara hii ya Kilimo? Kwamba Wizara ya Kilimo ijikite katika mito na kutengeneza scheme namna ya umwagiliaji ili wananchi na wakulima walio wengi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waweze kupata mtiririko wa umwagiliaji ili waweze kutoka kwenye gunia tano mpaka kumi waende kwenye gunia 30 mpaka gunia 40 na huu ushahidi ninao katika Jimbo langu la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali katika Wizara hii ya Kilimo; waache kufungua mipaka ya nchi hii kwa muda, waweze kuacha mipaka kwa miezi yote 12 ili wakulima hawa waweze kwenda kutafuta soko kwenye maeneo mengine nje ya nchi hii ili waweze kufaidi kilimo wanacholima kwa shida, kwa jasho, wasiendelee kuambiwa kwamba sasa hawawezi kuuza mazao haya ndani ya nchi hii ya Tanzania wakati huo Serikali haijandaa mpango mzuri wa kununua mazao ya wakulima, na wakati huo kama naweza kupata soko kule Kenya na nikaweza kuuza gunia kwa shilingi 200,000 kwa nini Serikali ndani ya nchi hii ya Tanzania wasiweze kununua gunia kwa hiyo shilingi 200,000 ambayo mimi mkulima naweza kupeleka mazao yangu katika nchi jirani ya Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeshaonekana mara nyingi magari ya watu yakitaifishwa katika mipaka ya Namanga, Kilimanjaro na maeneo mengi sana ya nchi hii kwamba sasa wakati huo mpaka ukifungwa unaweza kukosa gari yako au unaweza ukakosa mazao yako, wakati huo Serikali ikidai ndani ya nchi hii kuna upungufu wa chakula. Mimi naamini siyo kazi ya mkulima wa Tanzania kulisha wananchi wa Tanzania, ni kazi ya Serikali kulisha Watanzania na kujua kwamba chakula kinatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika Wizara ya Maji; katika Jimbo langu la Karatu kuna Mradi wa World Bank ambao una takribani miaka kumi sasa haujaweza kukamilika. Lakini vilevile najua kuna Naibu Waziri wa Maji mwezi wa 12 aliweza kutembelea Jimbo la Karatu wakati huo Jimbo hilo la Karatu kuna mradi wa maji yeye alivyokuja mradi uliweza kutoa maji, lakini baada yayeye kuondoka mradi ule haujaweza kutoa tena maji. Lakini vilevile mradi wa aina hii uko kwenye Kijiji cha Getamo, uko Umbang, uko Endanyewe, uko Buger na Khusumai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika eneo la TRA Wabunge wengi waliongea; katika Jimbo langu la Karatu TRA wameweza kushindwana na wafanyabiashara walio wengi kwa sababu Jimbo la Karatu asilimia kubwa liko kwenye suala la kiutalii. Lakini vilevile hawa watu wa TRA kwa Jimbo la Karatu wamekwenda mbali zaidi, wamekwenda kuwahoji wakulima wa Tarafa ya Eyasi na mimi nikiwepo, kwamba utengeneze mehesabu ya miaka mitatu iliyopita ili uweze kutengeneza hesabu na kuwapelekea watu wa TRA. Sasa kwa Jimbo langu la Karatu inaonekana kwamba hawa watu wa TRA wamekwenda sasa mbali zaidi kwenda kuwahoji wakulima wanaolima kitunguu katika Tarafa ya Eyasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupigania uhai sote tukiwa salama ndani ya ukumbi huu. Awali ya yote nishukuru sana Chama changu lakini vile vile nishukuru sana Serikali ya awamu ya tano, kwa kazi kubwa sana waliyofanya kazi hiyo kubwa waliyofanya imeweza kuleta Wabunge asilimia kubwa ndani ya ukumbi huu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa wale wana CCM waliopitia Chama Cha Mapinduzi wanajua kwamba, chama chetu mwaka wa 2010 ilikuwa na hali gani? Lakini vile vile, unajua changamoto tuliyokuwa nayo mwaka 2015. Lakini baada ya jemedari Hayati Dkt. Magufuli kuingia madarakani mwaka wa 2015 na ndio matunda sasa yameonekana kwa watanzania, kuamini Chama Cha Mapinduzi mwaka wa 2020 kwa kazi kubwa iliyofanyika chini ya jemedari na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nishukuru sana Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally kwa kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni Mbunge wa Jimbo la Karatu ni takribani miaka 25 Jimbo hili halijaweza kuleta Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo, usimamizi mzuri wa Serikali ya awamu ya tano watanzania wengi walikiamini Chama Cha Mapinduzi kwasababu, kuna muda ulifikia kwamba, watanzania walifikiri kwenda kutafuta chama mbadala nje ya Chama Cha Mapinduzi. Lakini mwaka wa 2015 Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani sasa watanzania walio wengi wakaamini kwamba, Chama Cha Mapinduzi kwamba ni chama cha kimbilio ya walio wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme eneo la fidia, katika Jimbo langu la Karatu pale kuna uwanja wa ndege wa Lake Manyara, pale Serikali iliwaambia itawapa fidia takribani sasa miaka sita wananchi wale hawajaweza kupata fidia. Nilikuwa naomba Serikali katika bajeti hii ya ofisi ya Waziri Mkuu, waangalie maeneo haya. Serikali yetu wanaweza kusema tunatoa fidia lakini baadae inaweza kuchukua miaka sita wananchi wale hawaruhusiwi kufanya jambo lolote katika eneo hili la Lake Manyara.

Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri ifikie muda kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na nafikiri ni sikivu, waweze kuangalia maeneo haya ya fidia. Wananchi wetu wanateseka na wakati huo ukifika kwenye haya kama Mbunge, unakutana na maswali magumu kweli na unashindwa kutoa majibu kwa wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikihama kutoka eneo hili la fidia niende kwenye eneo la maji pale Jimboni kwangu Karatu. Pale Jimboni kwangu Karatu Waziri Mkuu ni shahidi alitembelea lile Jimbo la Karatu, pale kuna bodi mbili za maji, kuna bodi ya KARUWASA, na kuna bodi ya KAFIWASA, wana wachaji wananchi wale wa jimbo lile kwa bei tofauti. Hawa KAFIWASA wanachaji bei ya shilingi 3,500/= kwa unit KARUWASA, wanachaji shilingi 1,700/= kwa unit. Na wakati Waziri Mkuu alitembelea jimbo lile wakati akijinadi yeye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa wakati huo, lakini vile vile na Rais wa Jamhuri ya Muungano tarehe 24 mwezi wa 10 alikuja jimboni Karatu na akasema hili halimshindi kurudisha bei moja ya shilingi 1,700/=.

Mheshimiwa Spika, kwasababu hawa watu wa KAFIWASA hata hawakaguliwi na Serikali wanajiendesha wenyewe, wanakusanya hela wenyewe, lakini wakati huo wakichaji/wakiwaonea wananchi kwa shilingi 3,500/=. Na hili tumelilalamikia kwa muda mrefu sana zaidi ya miaka 15 imekuwa ngumu kutekelezwa kwa Serikali, sijajua ni kwa nini? Kwamba, hawa watu wanaweza kunyonya wananchi wa Jimbo la Karatu kwa shilingi 3,500/= kwa unit halafu hakuna jambo lolote na hatua yoyote inayochukuliwa kupitia Wizara husika katika eneo hili la bei kubadilishwa, kuwa na bei moja katika Jimbo lile la Karatu kwasababu, kuna bei ya shilingi 3,500/= kwa unit na kuna bei ya shilingi 1,700/= kwa unit na inashindikana kuja bei ya shilingi 1,700/= kwa unit sijajua shida ni nini katika Wizara hii ya Maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengi wameongelea suala la tembo, kwa Jimbo langu nimezungukwa na hifadhi mbili, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Lake Manyara lakini watu wanasema kwenye Wizara ng’ombe akiingia ni shilingi 100,000/= lakini…

SPIKA: Tayari Mheshimiwa

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Tupange kwenye Bunge hili tembo wakiingia kwenye eneo la wananchi ni shilingi ngapi?

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Awack.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Karatu upatikanaji wa maji ni kwa asilimia 33 ambayo unaunganishwa na bwawa mbili, moja iko kwenye eneo la Patom na nyingine iko kwenye eneo la Bwawani. Na eneo hili la Bwawani limejaa maji na borehole lile haifanyi kazi, na Mheshimiwa Naibu Waziri alituenzi kutembelea Jimbo la Karatu na ukiangalia Mji wa Karatu ni wa kitalii na upatikanaji wa maji ni asilimia 33. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Bwawani waliomba shilingi milioni 440 kwa mwaka jana na mwaka huu lakini kilichopatikana ni milioni 175 katika eneo hili la Bwawani katika Mji wa Karatu. Kuna eneo lakini Ayalabe, Kata ya Ganako, waliweza kuomba 599,131,000 lakini kilichopatikana ni 168,000,000, hizi zingine bado hazijapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii ya mwaka huu kwa Wilaya ya Karatu Wizara imetenga shilingi bilioni mbili na milioni sabini na saba. Sasa hofu yangu ni kwamba kama mwaka jana tuliweza kuomba milioni 599 ikapatikana milioni milioni 168 na wakati huo katika eneo hili la Bwawani waliomba milioni 440 na ikapatikana milioni 175, hofu yangu ni kwamba katika upatikanaji wa pesa, na kama ingeweza kupatikana bilioni mbili ambayo sasa umetenga kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2021/2022, kwamba sasa kama inaweza kupatikana hiyo bilioni mbili angalau changamoto katika Mji wa Karatu na maeneo mengine ya vijijini ingeweza kupungua kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji ule wa Karatu wakazi wako 62,300, uhitaji wa maji ni lita milioni tano lakini upatikanaji kwa sasa ni 1,680,000, sasa wangeangalia kidogo katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la Mji wa Karatu, eneo la Bwawani limejaa maji, na kule wameomba shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa hivi haijaweza kwenda kufanya kazi kutokana na eneo lile kujaa maji, wanaomba ile milioni 175 ambayo sasa ililetwa kwa ajili ya Mji wa Karatu eneo la Bwawani iende katika eneo lile la Ganako ambako sasa kule kazi inaweza kufanyika kwa sababu kule kuna borehole mbili katika eneo hili la Ganako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Waziri ni kwamba hii shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa huwezi kufanya kazi katika Bonde lile la Bwawani iende sasa katika eneo lile la Ganako ili angalau uhitaji wa maji uweze kuongeza. Mradi huu wa Ganako ukikamilika upatikanaji wa maji pale unaweza kwenda kwenye asilimia 61. Ombi langu kwa Wizara ni kwamba ile shilingi milioni 175 ambayo kwa sasa Mji wa Karatu pale Bwawani hauwezi kufanya kazi kutokana na maji yamejaa pale na Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea eneo lile sasa iende katika eneo hili la Ganako ili angalau tutoke kwenye asilimia 33 twende asilimia 61. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la Bwawani maji yanajaa mara kwa mara na watu wanashindwa kupata maji kutokana na eneo lile kujaa maji. Tuliomba Wizarani shilingi milioni 40 kuhamisha pampu pale kwenda kwenye eneo lingine la juu kidogo ili angalau wananchi wasiendelee kuteseka. Niwaombe watu wa Wizara waweze kutupatia shilingi milioni 40, ni hela ndogo sana, ili tuweze kuhamisha ile borehole. Mheshimiwa Naibu Waziri ni shahidi ametembelea maeneo yale na amejionea kwamba kipindi cha mvua watu hawawezi kupata maji katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Karatu maeneo ya vijijini kuna mradi wa World Bank wa vijiji 10, huu mradi una zaidi ya miaka 10 kila siku ni ukarabati maji hayapatikani. Nafikiri katika eneo hili tumetengewa shilingi bilioni 2, kama itapatikana mradi huu wa World Bank kwa vijiji 10 katika eneo la Karatu Vijijini maji yanaweza kupatikana ili na kule kijijini tuweze kufika asilimia kubwa kidogo kuliko tuliyonayo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo lile la Karatu Vijijini upatikanaji wa maji katika Tarafa ya Bulumbulu ni wa njia ya mtitiriko na katika eneo hili wametenga shilingi milioni 520 ikipatikana kwa muda nafikiri tutakuwa tumepiga hatua kidogo kule kwetu Karatu. Mimi sina mashaka maana Waziri ameanza vizuri na namtakia kila la kheri ili angalau eneo hili la maji tuweze kulipatia ufumbuzi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Karatu tunaomba sana hii shilingi milioni 40 tuweze kuipata lakini vilevile tunaomba hii shilingi milioni 175 iweze kwenda eneo lile la Ganako ili angalau wananchi wale wa Karatu waweze kutoka kwenye asilimia 33 kwenda asilimia 61.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi mbalimbali katika eneo letu la Karatu. Kuna mradi huu wa Mang’ola Juu ambao ni wa World Bank ambao kwa sasa wametenga shilingi milioni 100. Vilevile kuna mradi huu ambao unaenda Laja/Umbangw ambao umetengewa shilingi milioni 519. Mradi wa Chemchem umetengewa shilingi milioni 200 na mradi wa Gidbaso ambao umetengewa shilingi milioni 180.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuna mradi huu wa Makhoromba ambao umetengewa shilingi milioni 240. Vilevile kuna mradi wa Kwa tom ambao umetengewa shilingi 65. Pia kuna mradi huu wa Gendaa ambao umetengewa shilingi milioni 45 na mradi wa Endala ambao umetengewa shilingi milioni 136. Pia kuna mradi wa Kilimatembo, Rhotia, Rhotia Kainam, Lositete, Kitete na Marera ambao umetengewa milioni 520 na mradi wa Chemchem, Kambi ya Simba, Huduma, Bashay, Endesh na Endagem umetengwa shilingi milioni 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya fedha kwa jimbo langu ni Sh. 2,412,900,135. Fedha hizi zikipatikana kwa Jimbo la Karatu tutapiga hatua zaidi ya kimaendeleo kwa sababu Mji wa Karatu ni Mji wa kimaendeleo na utalii na sisi si wachovu ni wakulima wazuri tu ambao tunaleta mchango mzuri katika eneo la mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na pia naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi. Nami niungane na wenzangu ambao kwenye wilaya yao hawajapata chochote kwani nami ni mmojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Karatu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri mjue ni jimbo ambalo limekombolewa kutoka kwenye miaka 25 ya kutawaliwa na Vyama vya Upinzani. Wakati tunatafuta kura tukiwa na wenzangu wa Chama cha Mapinduzi wakiwepo viongozi wakuu akiwepo Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Taifa ambapo wakati huo alikuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi kule tuliahidi mengi. Tuliahidi barabara ya kutoka Karatu - Njia Panda - Junction Matala barabara ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu, hiyo ni kilometa 328 ambazo ziko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi lakini hakijatengwa kitu chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutoka hii barabara ambayo Mheshimiwa Flatei anataka kupiga sarakasi imeanzia Karatu, katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi lakini wameenda kuweka kilomita 25 pale Mbulu kwenda Haydom. Barabara hii kwenye Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi imeanzia Karatu – Mbulu – Haydom – Singida. Mimi silalamiki kwamba kwa nini wale wa Mbulu wamepata kilometa 25, niseme tu kwamba sasa Mheshimiwa Waziri sisi Karatu atutengee kiwango kidogo ili na sisi tuwepo katika kula matunda ya nchi hii ambayo tumeyakosa kwa miaka 25 tukiwa chini ya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli pale Karatu Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kilometa 2 katika Mji wa Karatu lakini mpaka leo hakuna hata kilomita moja. Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kilometa 10 kwa mwaka wa 2015 leo ni mwaka 2021 hakuna hata kilometa moja. Mwaka jana tarehe 24 wakati Rais wa Jamhuri wa Tanzania Hayati Dkt. Magufuli akininadi alisema kama anajenga fly overs Dar es Salaam hashindwi kujenga kilometa 10 katika Mji wa Karatu. Sasa nashangaa tena kwenye bajeti hii hamna hata kilometa moja sasa wananchi wale 2025 nitawaaambia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aliongea kwamba mwaka 2025 kwenye Jimbo lake la Tanga hawezi kurudi kama hajafanikisha maendeleo ambayo ameahidi kwa wananchi wa Tanga Mjini. Nami kwa wale wa Karatu tulivyoahidi Chama cha Mapinduzi na tukiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwamba tunaweza kuleta maendeleo kwa speed mkikichagua Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Karatu walijitahidi kuchagua Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, nami kilio hiki nimefikisha kwenu ninyi Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ni ombi langu kwamba maombi haya yatazingatiwa na kilometa hizi kumi ndani ya Jimbo la Karatu tuweze kupata na kilometa hizi kutoka Karatu – Mbulu
– Singida tunaweza kupata, vilevile barabara hii ya kutoka Oldeani – Mangola – Matala – Lalago kule Simiyu; na barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, tuliinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi na wananchi walio wengi waliamini ahadi kubwa sana ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Ni imani yangu kwamba Ilani ile ya Chama cha Mapinduzi ili wananchi waendelee kuiamini, kwamba sasa inaweza kwenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa nafasi kuweza kuchangia wizara hii ya kilimo. Katika Jimbo la Karatu tunalima mazao kama aina takribani nne hivi, tunalima mbaazi, tunalima ngano, tunalima vitunguu na tunalima mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kilimo hiki cha kitunguu kipo Tarafa ya Eyasi na ni tarafa ambayo ina-history kubwa kwa sababu ni tarafa inayolima vitunguu Afrika Mashariki inasambaza kwa mwaka mzima. Na kama alivyoeleza mzungumzaji aliyeongea kwamba vitunguu vyetu vinaenda Kenya kwa asilimia kubwa sana, na soko letu kubwa lipo Kenya kwa asilimia kama 90 hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika eneo hili la kitunguu pale Bonde la Eyasi Serikali ina skimu ambayo imegharimu zaidi ya bilioni moja na andiko tumeandika wizarani mara nyingi kwamba sasa ile miundombinu ya zaidi ya bilioni moja naa katika Kata ya Baray imeweza kufukiwa na mafuriko kwa mbele sasa miundombinu ile kwa takribani sasa miaka mitano haiwezi kufanya kazi na tumetuma andiko wizarani kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, lakini ukienda katika eneo hili la mbaazi kwa mwaka 2014/2015 mbaazi iliweza kufika shilingi 300,000 gunia moja mpaka shilingi 400,000 lakini kwa muda huu mbaazi inauzwa kwa gunia moja shilingi 25,000 mpaka shilingi 30,000, shilingi 35,000. Sasa nilikuwa nafikiri wizara wajiulize wale waliokuwa wanakula mbaazi 2014/2015 wamekwenda wapi au sasa kwenye nchi hizo nini kilichotokea kwamba mbaazi yetu sasa imeshuka kutoka shilingi 300,000 mpaka shilingi 400,000 kuja shilingi 30,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo la ngano, sisi ni wakulima wa ngano na kubwa sana wanalima katika Tarafa ya Bulumburu katika eneo hili la wakulima wa ngano watu wa TBL wanatoa vifaa vyote, lakini wameweka limit ukiivisha kwa heka moja wanasema usiivishe zaidi ya gunia saba, sasa wakulima wangu wao wanaivisha gunia saba mpaka gunia 10 mpaka gunia 12, lakini ukiivisha zaidi ya gunia saba, zile zingine zinazozidi hawataki kabisa na itakuwa ni mgogoro mkubwa katika Tarafa ile ya Bulumburu katika eneo hili la wakulima wa ngano.

Mheshimiwa Spika, sasa wenzangu watu wa wizarani wanatakiwa hilo waliangalie kwamba wanaweka limit kwamba heka yako ikitoa zaidi ya gunia saba ina maana hiyo utajua mahala pa kwenda kuuza, kwa maana watu wa wizarani waangalie sana hilo katika Tarafa ya Bulumburu na imetokea mara nyingi sana na mwaka jana ilitokea na kukatokea mgogoro mkubwa mpaka wananchi wale wakashindwa kulima zao hili la ngano kutokana na kwamba mgogoro unaotokea kwenye kampuni ya TBL. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika eneo lingine la mahindi wizara sasa hivi bei ikiwa 20,000, 25,000 watasema mipaka ipo wazi, lakini ikatokea bei ikaenda kwenye 60,000, 70,000 wanafunga mipaka wakidhani kwamba ndani ya nchi hii kuna njaa ya chakula. Lakini, nashauri wizara kwa muda mrefu kama ilivyokuwa mpaka sasa uko wazi uweze kuwa wazi kwa muda wote wa miaka ijayo, ili wananchi hawa waweze kupata masoko yao maeneo mengine. Kwa wale wanaotokea Kanda ya Kaskazini na imetokea mara nyingi Mkuu wa Mkoa anaweza akatokea akasema kwenye ndani ya mkoa wake kuna njaa, wakati kuna maeneo mengine mahindi yanalimwa mengi yanatakiwa yatolewe kwenye hiyo mikoa mingine ziende kwenye mkoa huo ambao Mkuu wa Mkoa anajidai kwamba Mkoa wake una njaa.

Mheshimiwa Spika, sasa imeshatokea mara nyingi kwamba Wakuu wa Mikoa kusema mikoa yao ina njaa na kwamba watu wa mikoa mingine wanashindwa kuuza mazao yao iwe fursa kwenda kuuza mazao haya kwenye mikoa mingine ambayo ina shida ya chakula. Wenzangu wa Kanda ya kule Ruvuma watu jana waliongelea kwamba kule kwao mahindi yanakosa soko sasa kama kuna mkoa mwingine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawezi kufunga na imetokea mara kwa mara katika Mkoa wa Kilimanjaro, katika Mkoa wa Arusha, Tanga wakisema kwamba kwenye ukanda ule kuna njaa na mimi nadhani hakuna siku itatokea sisi watanzania tukaagize mahindi Kenya sisi tutaendelea kuuza mahindi Kenya na maeneo mengine kwa nchi zilizotuzunguka ndani ya Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana wenzangu wa wizara wasifunge mipaka hii kwa muda muda wafungue mipaka hii kwa muda wote wa miaka yote ambayo sasa wakulima wa Tanzania ili waendelee kupata fursa ya kuweza kuuza mazao yao maeneo mengine ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina mengi sana ya kuongea lakini wenzangu wa wizarani nilikuwa nafikiri kwamba sasa ni muda, lakini leo wametuletea makaratasi haya wakidai kwamba tuweze kuandika maeneo yenye skimu. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba, ina maana hii wizara haina watalaamu mpaka sisi wabunge watuletee ndiyo tuwaletee hapa kwenye Bunge hili tuwaandikie kwamba kuna skimu sehemu fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vitu vingine vya kushangaza katika wizara hii ya Kilimo, leo Mbunge nilete skimu ina maana hakuna mtaalam kwenye Ukanda huu wa Jimbo la Karatu wa kuleta taarifa kwenye wizara hii kusema kwamba kuna skimu iliyolala, kunaskimu inayoendelea kufanya kazi, leo tunaletewa sisi Wabunge tujaze hizo nafasi kwa taaluma ipi tulizonazo sisi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wizara hii inatakiwa ijitafakari sana katika maeneo haya na naamini kwamba inaonekana uwajibikaji kwa watumishi wa eneo hili la kilimo wapo nyuma mno hawaendi na nchi hii ya Tanzania jinsi inavyokwenda. Watu wa wizara waangalie sana hili suala lakini vile vile ni….

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Daniel Awack.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na pili nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais kwa kuendelea kufanya shughuli ya nchi yetu kwa ufasaha zaidi. Katika Jimbo la Karatu tumepata mafanikio makubwa wakati huu kwa mwaka wa fedha tulipokea bilioni 1.2 ambayo ilikuwa inaitwa hela ya Mama Samia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuliweza kupata milioni 700 kwa kukarabati sekondari kongwe ya Karatu, lakini vile vile tulipata milioni 470 kwa ajili ya shule ya kata ya sekondari ambayo inajengwa katika Kata ya Ganako. Pia tuliweza kupata milioni 500 kwa kujenga Kituo cha Afya cha Mbuga Nyekundu. Hata hivyo, niseme kwamba asubuhi Mheshimiwa Getere aliongea kwamba kule TAMISEMI kuna vifungu kwenye hizi milioni 500 tulizopokea ya Kituo cha Afya cha Mbuga Nyekundu, mpaka sasa hivi tulipokea awamu ya kwanza milioni 250, lakini awamu ya pili tumepokea milioni
250. Mpaka sasa tunapoongea, tuna zaidi ya mwezi mmoja shilingi 250 wanaendelea kusema vifungu vya kuhamisha hizo hela mpaka sasa hivi bado, sasa inashangaza kidogo, kama hela inatolewa kutoka Wizarani, halafu inaweza kuchukua siku 30 halafu huduma hiyo isiendelee, kwa kweli hii ni changamoto, mpaka leo hii tuna zaidi ya siku 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliweza kuongea katika Bunge hili kwamba, tulikuwa tuna tatizo la fidia katika eneo la uwanja wa Lake Manyara, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais wananchi wale wamelipwa zaidi ya bilioni 5.9, katika eneo hili la fidia eneo la Lake Manyara. Sisi pia tulifanikiwa kupata hela kwenye hospitali ya wilaya lakini iko hatua zaidi ya 85% na naamini kwamba inaweza kukamilika wakati wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea eneo la TARURA kidogo, hili eneo la TARURA Kwa mwaka jana tulitenga fedha, lakini kwenye hili eneo kuna changamoto kubwa. Mwaka 2010 Karatu tuliahidiwa tupate kilomita mbili za lami, lakini Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano mwaka 2015 alituahidi kilometa nane pamoja na ile ya Mheshimiwa Jakaya 2010 ikawa jumla ni kilomita 10. Mpaka sasa hivi tunapoongea kilomita zilizojengwa katika Jimbo la Karatu ni 0.6 mita, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri shahidi, toka mwaka 2019 mpaka leo hii, kuna kilometa 0.9, mpaka leo haijakamilika, ukiuliza changamoto ni nini? Barabara ilifumuliwa kutoka mwaka 2019, mpaka leo tunapoongelea mwaka 2022. Sasa nina wasiwasi sana kwenye ahadi hizi za viongozi wetu kwamba tutaendelea kupata changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Awamu ya Tano mwaka 2020 wakati akininadi mimi kama mgombea wa jimbo lile, aliweza kusema kwamba tunaweza kwenda kujenga sasa kilometa 10; kama mita 0.9 imeweza kuchukua muda wa miaka mitatu, sasa TAMISEMI ijipange, hizi ahadi za viongozi kwa mwaka wa fedha unaokuja wajipange ni namna gani wanaweza kutimiza ahadi za viongozi wetu wakuu wanaoahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda kuongelea eneo hilo hilo la TARURA kwamba ufanisi wa TARURA ni changamoto kwa sababu wao bajeti inaisha mwezi wa Sita tarehe 30, TARURA wanakwenda kwenye kujenga barabara mwezi Januari au Februari. Sasa nashangaa kidogo kwa nini bajeti ikiisha TARURA isijipange kama wenzetu wa TANROADS wanavyojipanga. Nafikiri kuna changamoto TARURA kwa kujipanga, hofu yangu ni kwamba wataalam walioko TARURA bado ni wababaishaji. Nafikiri waangaliwe upya ma- engineer hawa tunaopewa huku TARURA. Nitatoa mfano, Mkoa wa Arusha tulipewa bilioni 19, lakini ufanisi wa bilioni 19 unakuwa na changamoto katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili kuna muda tulipewa milioni 500. Milioni hiyo 500 tuliambiwa kwamba inaweza kujenga kilometa moja ya lami kwa Jimbo la Karatu ilitangazwa mara nne, mtu wa chini sana aliomba kilometa ile kwa shilingi milioni 750. Sasa nashangaa kidogo kwa nini TAMISEMI wasifanye tathmini ya kutosha kuona kwamba kilometa moja ya lami inajengwa kwa kiwango gani. Nafikiri hii inakuwa ni changamoto mpaka sasa hivi mkandarasi imeshindikana kupatikana kwa kilometa moja hii ya lami ambayo wameweza kutupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujengwa kiwango cha lami kilometa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto katika watumishi; kwa Jimbo la Karatu jumla ya eneo la shule ya msingi tunahitaji watumishi 1,500 lakini walioko ni 964. Ukienda shule ya sekondari tuna upungufu wa zaidi ya 129, ukienda afya tuna upungufu wa watumishi 188. Lakini ukiangalia Wizara watakwambia sasa wameajiri, lakini Serikali iliacha kuajiri muda mrefu, kwa idadi iliyotangazwa ya waajiriwa ambao sasa wataajiriwa, hata wale tu waliostaafu kwa miaka yote Serikali haijaajiri, nafikiri idadi hiyo haitoshi. Kwa maana hiyo ina maana wenzetu wa Utawala Bora wajipange katika eneo la ajira kwamba hao wanaoajiriwa hawatatosha. Tunaomba waangalie eneo hili la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu ni mkubwa katika maeneo yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, awali nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu na wenzake wote Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme katika Jimbo la Karatu tuna changamoto; na bahati nzuri sana Naibu Waziri alifika katika Jimbo la Karatu. Lakini vilevile Waziri alifika takribani miezi mitatu. Mwezi wa pili alifika katika Jimbo la Karatu. Lakini pale Karatu maji yanapatikana kwa asilimia 33 katika taasisi ya Serikali. Lakini kuna taasisi binafsi ambazo upatikanaji wa maji unapatikana kwa asilimia 25.

Mheshimiwa Spika, shida kubwa katika Jimbo ka Karatu ni bei kubwa ya maji. Bei ya maji Karatu kwa unit moja inapatikana kwa Shilingi 3,500. Katika taasisi ya Serikali inapatikana kwa Shilingi 1,750. Lakini Mheshimiwa Waziri alifika katika Jimbo lile na akasema ndani ya siku 30 bei hii inaweza na ikawa uwiano. Hili haihitaji hela ya Serikali, inahitaji kauli ya Waziri kusema bei iuzwe kwa bei fulani katika Jimbo la Karatu. Na mimi siombi niongezewe fedha, mimi ninachohitaji ni kauli ya Waziri kusema bei ya maji ambayo inatokana na maelekezo ya EWURA katika Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alisema jambo hili lingechukua ndani ya siku 30 lakini takribani leo ni miezi mitatu na siku tano. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, hii pia ni sehemu unapofuatilia, unapozunguka nchi hii maamuzi magumu unapofanya maeneo mengine. Sijajua kwa nini Karatu inashindikana bei ile kuwa ya aina moja; kwa sababu kuna wengine wanauza kwa Shilingi 3,500, wengine wanauza kwa Shilingi 1,750. Na ulifika katika Jimbo la Karatu ukasema hata hao wa chini wanaouza Shilingi 1,750 bado wanawaibia wananchi wa Jimbo la Karatu.

Mheshimiwa Spika, napenda sana uweze kutoa kauli katika Jimbo la Karatu, wananchi wale waweze kupata fursa ya kuweza kupata kulingana na bei katika maeneo mengine katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naamini ukiwa katika Jimbo la Karatu ulisema kwamba uliweza kushusha bei ya hapa Dodoma, kama sikosei ilikuwa Shilingi 1,200 au Shilingi 1,300 kwa unit na Arusha na maeneo mengine yaliyoko ndani ya nchi hii mpaka Dar es Salaam. Naamini hilo kwako wewe si kitu kigumu, unaweza kulifanyia kazi kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo lile kuna mradi ambao unaendelea, naamini Serikali ilitoa fedha za kutosha Shilingi zaidi ya Milioni 800. Lakini kuna eneo la Ayalabee limetoa Shilingi Milioni 800 na kuna eneo la Bwawani limetoa zaidi ya Shilingi Milioni 400, lakini mradi ule unahitaji kama zaidi ya Shilingi Milioni 700. Lakini na katika eneo hili la Ayalabee imefika mradi asilimia kama zaidi ya 80 lakini mradi wa Bwawani asilimi ni 34. Asilimia hizi zote 80 zikikamilika asilimia 100 na ile asilimia 34 ikikamilika asilimia 100 tunaweza kupata zaidi ya asilimia 70 katika Mji wa Karatu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri najua alitembelea maeneo mengi katika Jimbo la Karatu wakati umetembelea mwezi wa pili. Tulifika Bonde la Easi ambako upatikanaji wa maji ni wa asilimia zaidi ya 60. Lakini vilevile tulifika katika katika maeneo mengine katika Jimbo la Karatu, upatikanaji wa maji haujazidi asilimia zaidi ya 60 katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwake, na kipindi kile wakati umetembelea Jimbo la Karatu ulituahidi sisi wananchi wa Jimbo la Karatu. Ulisema upatikanaji wa maji Karatu ili shida hii iishee kabisa ilionekana kwamba tunahitaji zaidi ya Shilingi Bilioni 4.5. Na mimi naamini katika Serikali na Wabunge wengi wamesimama katika ukumbi huu kwamba kuna maeneo mengine wapeleke Shilingi Bilioni 10, kuna maeneo mengine wapeleke Shilingi Bilioni 15; na mimi naomba katika eneo hili la Karatu tuweze kupata Shilingi Bilioni 4.5 na Mheshimiwa Waziri uliahidi katika Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na uliahidi wananchi wa Jimbo la Karatu kwamba Shilingi Bilioni 4.5 kwa Serikali si kitu kikubwa sana na ulisema Serikali haifanyi biashara. Kazi kubwa ya Serikali ni kutoa huduma na wananchi wa Karatu walikunukuu vizuri. Na mimi nikuombe umekuja Karatu na wananchi wa Karatu wamekusikiliza vizuri na wamekuelewa vizuri. Nakuomba sana usinitengenezee ajari katika Jimbo lile tuweze kupata huduma ili wananchi wale waendelee kuniamini Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kwamba tumepata katika maeneo kata mbalimbali katika Jimbo la Karatu. Kwa mfano; katika eneo hili la Mang’ola Juu tumepata Shilingi Milioni 191, Kata ya Daa lakini pale Kata ya Kansay tumeweza kupata Shilingi Milioni 225. Vilevile mradi mwingine katika eneo la Mang’ola Balasani tumepata Shilingi Milioni 360. Kuna eneo lingine Kata ya Rotya tumeweza kupata Shilingi milioni zaidi ya 360. Maeneo mengine ya Barai tumeweza kupata Shilingi Milioni 360.

Mheshimiwa Spika, kazi imefanyika na sisi tunashukuru sana Wizara. Nami pia kama Mbunge wa Jimbo wakati naingia kama Mbunge wa Jimbo lile fedha ilikuwa ya Wizara ya Maji kidogo ni changamoto lakini tangu mwaka jana, mwaka huu fedha katika Jimbo lile imepatikana kwa asilimia kubwa. Hata katika hizo hela za UVIKO - 19 tumeweza kupata shilingi milioni 500 na mradi unaendelea na unasambaa katika Mji wa Karatu kwa zaidi ya kilometa 45. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba sasa tumesambaza ule mradi kwa eneo la mabomba tu kwa kilometa 45 ili maji yale yasambae vizuri nahitaji mradi ule ukamilike ambao unahitaji zaidi ya shilingi milioni 800. Na sasa imeshatolewa kama shilingi milioni 600. Kinachohitajika pale ni shilingi milioni 250 na eneo hili la Bwawani hela zimeshaenda zaidi ya shilingi milioni 300. Kinachohitajika pale zaidi ya shilingi milioni 300 ili iweze kufikia shilingi milioni 700. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakuomba hili kwako siyo kubwa na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi naamini siyo kitu kikubwa. Naomba, eneo hili likikamilika katika Jimbo la Karatu tutakuwa tumesogea sana katika eneo hili la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba kazi imefanyika, tunashukuru kwa hili ambalo limefanyika na japo naamini katika mwaka huu wa fedha miradi mingi ile ya mwaka jana wanaimalizia. Naamini hii miradi mkimalizia tutapata maji, kwa sababu katika Jimbo la Karatu kuna changamoto kubwa. Kuna miradi mingine ilikuwa ya miaka zaidi ya nane, saba ilikuwa imemelala lakini baada ya Waziri kuingia na Serikali ya Awamu ya Sita kuingia miradi mingi imefufuliwa na wananchi wetu wanaendelea kupata maji katika eneo la Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi na pia naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha nyingi Jimbo la Karatu kupitia TAMISEMI mwezi huu wa Mei tumepokea zaidi ya shilingi bilioni mbili ya kuendelea kujenga madarasa, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Karatu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kutupatia Jimbo la Karatu fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Watendaji wa Wizara ya Maji na leo nachangia nikiwa na furaha kwamba kuna majukumu makubwa sana kwenye hii Wizara imefanyika katika Jimbo la Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka miwili iliyopita nilikuwa nachangia bei kubwa ya maji katika Jimbo la Karatu, ilikuwa maji kwa Jimbo la Karatu upatikanaji wake kwa unit ni shilingi 3,500, sasa upatikanaji kwa unit katika Jimbo la Karatu inapatikana kwa shilingi 1,300, kwa maana hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kutoka shilingi 3,500 na leo wananchi wa Jimbo la Karatu katika Mji wa Karatu wanapata maji kwa shilingi 1,300 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuunganisha. Karatu kulikuwa na Bodi mbili, kulikuwa na Bodi ya KAFIWASU ambayo ilikuwa inauza maji kwa shilingi 3,500. Kulikuwa na Bodi ya KARUWASA ambayo wanauza maji kwa shilingi 1,750 baada ya kuungana sasa maji yanapatikana kwa shilingi 1,300. Tunakushukuru sana na ninaamini kwamba ni sera ya Wizara kuunganishwa ili wananchi wale wasiendelee kuwa na mwingiliano katika hizi bodi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri pia nakushukuru baada ya kuunganisha wafanyakazi wale wote wa KAFIWASU na wale wa KARUWASA wakaunganishwa hakuna aliyekosa kazi wote sahizi wanaendelea kufanya kazi. Pia ulipendekeza aliyekuwa Manager wa KAFIWASU sasa kuwa Mkurugenzi wa Maji katika Mji wa Karatu na anafanya kazi nzuri sana katika Mji wa Karatu na wananchi wanapata maji. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile jana Mheshimiwa Paresso amechangia akisema kwamba wananachi wa Karatu wanalalamika. Nikuhakikishie nimetoka Jumapili Jimbo la Karatu, wananchi wa Karatu hawalalamiki. Wananchi wa Karatu walipata shida kutoka mwaka 2002 kununua maji kwa shilingi 3,500 lakini niweke kumbukumbu sawa, siyo kwamba Karatu baada ya 2002 ndiyo kwamba mradi wa maji ulianza. Mradi ulikuwepo kabla ya 2002 na ulirithi miradi ya Serikali ambayo ni matenki na ma-lane na wakaendelea kuhudumia kwa bei ghali ya shilingi 3,500. Kwa hiyo, nikuambie Mheshimiwa Waziri hakuna Wananchi wa Karatu wanaolalamika, mimi ndiyo Mbunge wa Jimbo la Karatu, wananchi wamefurahia kuunganishwa kwa ile vyombo, kwa sababu hitaji letu ni maji, sisi hatuna shida na majina ya KAFIWASU na KARUWASA, shida ya wananchi wa Karatu ni wapate maji ili maendeleo yawepo katika Jimbo la Karatu, hatuna shida na KAFIWASU na KARUWASA, lengo letu kubwa ni mwananchi apate huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nikushukuru sana kwa hilo ila nina lalamiko la Wanakaratu, uliwaahidi utawapatia shilingi bilioni 4.5. Hili ndilo lalamiko la Wanankaratu isipopatikana shilingi bilioni 4.5, na nikushukuru kwa sasa mmetoa shilingi milioni 865 kati shilingi bilioni 4.5. Tunachoomba Wanakaratu sasa hizo fedha zingine zilizobaki katika shilingi bilioni 4.5 zipatikane ili wananchi wa Jimbo la Karatu waendelee kupata neema ya maji katika Mji wa Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukipata shilingi bilioni 4.5 upatikanaji wa maji katika Mji wa Karatu utakuwa zaidi ya asilimia 100 katika Mji wa Karatu. Kwa maana hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri tuweze kupatiwa shilingi bilioni 4.5 katika Mji wa Karatu maji yatapatikana kwa zaidi ya asilimia 100. Hii shilingi milioni 865 mliyotoa, inaweza kupeleka maji kutoka asilimia 70 mpaka asilimia 78, tukipata hizo fedha zingine zilizobaki ina maana tunakwenda kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Karatu. Nikuombe sana hii shilingi bilioni 4.5 ambayo umeahidi Wananchi wa Jimbo la Karatu na tulikuwepo Wabunge wote wawili, tulikuwepo Baraza la Madiwani, walikuwepo Wenyeviti wote wa Mitaa katika Mji wa Karatu. Ulituahidi utatupatia shilingi bilioni 4.5. Ombi langu kwako tuweze kupta hiyo shilingi bilioni 4.5 ili wananchi wa Karatu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kuna maeneo mengine hela chache chache zimebaki siyo hela nyingi sana ili mradi ukamilike. Kwa mfano, katika Mji wa Karatu kuna mradi ambao unatekelezwa eneo la Bwawani Mangaki ambao Serikali imeleta shilingi milioni 375 na mradi ule ulikua unahitaji shilingi milioni 640. Tulikuwa tunaomba hiyo hela nyingine kidogo iliyobaki mtupatie kama Wizara, lakini lingine ni shilingi milioni 640 eneo la Kata ya Mang’ola. Tunaomba mtupatie hizo fedha shilingi milioni 640.

Mheshimiwa Spika, lingine ni mradi ambao unatekelezwa katika eneo la Laja ambao unagharimu, umebaki shilingi milioni 136. Tukipata hiyo shilingi milioni 136 inamaana suala la maji katika eneo la Laja linaisha kabisa, vilevile kuna eneo la Chemchem, Mkandarasi pale anahitaji shilingi milioni 192 ili aweze kumaliza majukumu yale ya maji katika eneo la Chemchem. Tukipata hii shilingi milioni 192 kazi pale Chemchem itakuwa imeisha eneo la Kata ya Rotia.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukipata fedha shilingi milioni 64 kumalizia mradi ambao unatekelezwa katika eneo la Mang’ola Juu Kijiji cha Mang’ola Juu Kata ya Daa. Vilevile niseme Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana, wananchi wa Jimbo la Karatu tunakuomba utupatie hizo fedha na mimi naamini ukitupatia hizi fedha nilizotaja hapa ni kwamba katika eneo la Mjini maji yanakwenda asilimia 100, maji katika eneo la vijijini inakwenda asilimia zaidi ya 75. Nikuombe tupatie hizi fedha ili wananachi wa Jimbo la Karatu waendelee kupata neema ya maji ambayo imekosekana kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mimi nikuombe katika Jimbo la Karatu maeneo ya vijijini hitaji letu sisi maji yanapatikana, huwezi kuchimba zaidi mita 100. Kwa hiyo, tunachoomba ni kwamba sasa utaratibu ule wa gari zile za Mkoa ambayo sasa imeletwa kwa Mkoa wetu wa Arusha Mheshimiwa Zaytun amechangia hapa kwamba tayari tuna gari, ombi letu ni kwamba sasa katika eneo la Karatu uweze kutupatia visima vichache katika maeneo ya vijijini ili wananchi wetu waendelee kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na nikutoe hofu wananchi wa Jimbo la Karatu wanakusubiri kwa hamu kubwa sana ili wakushukuru, kwa niaba yao nimkuja kuleta shukrani kwako kwa watu walinyonywa miaka 20 iliyopita kwa shilingi 3,500 na leo tunaendelea kula neema ya shilingi 1,300 kwa unit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye DP maji leo zinapatikana kwa shilingi 1,000 kwa unit. Nikushukuru sana Mungu akutangulie uendelee kutuletea mambo mengine mengi katika Jimbo la Karatu sana, nikushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya kazi kubwa ya Royal Tour na kwa Jimbo langu imeleta mafanikio makubwa sana. Mheshimiwa Waziri ni shahidi mwezi uliopita alikuwepo katika Jimbo langu akiwa na Makamu wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Karatu limezungukwa na hifadhi mbili, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro na Lake Manyara National Park, pia Jimbo langu lina Kata 14, Kata Tisa zimezungukwa na hifadhi lakini vilevile vijiji 29 vimezungukwa na hifadhi katika Jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wameongea changamoto kubwa ya tembo lakini niseme kwamba siku ya Ijumaa tulipoteza mwananchi mmoja katika Kata ya Oldean na leo hii siku ya Jumatatu wanampumzisha. Niseme ni kilio kikubwa kwa Jimbo langu la Karatu pia najiuliza watu hawa wa hifadhi ng’ombe wakiingia kwenye hifadhi wanakuwa makini kweli na sasa hivi ng’ombe mmoja anapigwa faini ya shilingi 100,000 lakini sasa hivi suala la faini ya 100,000 wameacha sasa hivi wamekwenda mbele zaidi wanataifisha mali za wafugaji wetu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo wakiingia kwenye shamba la mkulima hana bei. Ndiyo Mheshimiwa mchangiaji aliyetangulia amesema kwamba kwa hekari moja unafidiwa kwa shilingi 25,000 wakati huo mita 500 hawawezi kuchangia chochote. Mimi pia najiuliza Mamlaka ya Hifadhi za Ngorongoro ilianzishwa mwaka 1959 wakati huo wananchi walikuwepo na ikaweka fire-line katika eneo hilo, ikawekwa mpaka wa Hifadhi ya Ngorongoro na ikawekwa fireline kwenye mpaka upande wa wananchi. Leo wameweka kwenye kanuni zao mita 500 hamna kumchangia hata hiyo 25,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa kama ilivyoelezwa mita 500 mpaka 1000 kama ilivyoelezwa lakini kuanzia kilometa Nne mpaka tano shilingi 75,000. Lakini kilometa Nne mpaka Tano ni shilingi 100,000. Pia, ukiwa na zaidi ya hekari tano hawakupi fidia hata zikiharibiwa hekari 50, wao wanachojua ni hekari tano tu. Huu ni uonevu kwa wananchi wetu na wametuonea kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia najiuliza hao waliopitisha shilingi 25,000 kwa heka Wizarani au TAWA hivi kweli wameangalia na hao ni wakulima kweli? Hivi mwananchi unamsaidia kwa 25,000 kwa hekari? Hata kwa kilimo tu cha trekta haitoshi wakati huo mwananchi amegharamika mpaka anakaribia kuvuna tembo nakwenda kuharibu. Kwa nini tusitunge sheria tembo hawa ni mali ya Serikali na kuna watu wameajiriwa kwa ajili ya kuchunga. Kama tembo hawa wanatoka misituni wanaingia kwenye mali za wananchi siyo kwamba wale wanaowachunga msituni wamezembea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo mpaka wanafika kwenye mali za wananchi kama ng’ombe wetu wanaingia misituni wanakuwa makini kutu–charge shilingi laki moja kila ng’ombe, hao ng’ombe wao wanaotoka misituni wanakuja kwenye mali yetu sisi wananchi halafu wanatupangia na fidia wanatoa wanavyotaka na wanayoona wao inafaa. Pia, inaweza kuchukua hata miaka mitatu mwananchi anaendelea kudai hata hiyo 25,000 anaweza kudai miaka mitatu. Hii siyo sawa. Tukuombe Mheshimiwa Waziri, uangalie kwa upya, kwa sisi tuliozunguka na hizi mbunga tumeumia kweli kwa muda mrefu na wananchi wetu wanaendelea kuteseka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme katika Jimbo langu kuna changamoto kubwa hasa katika kata tatu; Kata ya Oldean, Kata ya Daa na Kata ya Ganako. Wananchi wale wamekuwa maskini kabisa katika muda mrefu kabisa kwa miaka yote ambao wanapakana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro. Mimi sisemi kwanini tumezungukwa na hizi hifadhi, lakini tunachoomba kwa Wizara waweze kuona ni namna ipi ili waweze kuwadhibiti wanyama hawa ambao wanaumiza wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kwa mfano Wilaya kama hii ambayo ina vijiji 29, ina kata tisa imezungukwa na hifadhi, hamna hata gari moja la kufanya doria, Wilaya nzima hamna hata gari moja la kufanya doria. Wale watumishi wamekaa pale hawana hata kazi yoyote, kwa sababu kazi yao kubwa ilikuwa wawasaidie wananchi wetu kuzunguka lakini hawana gari, wamekaa tu ofisini wanapiga mshahara wa bure kabisa hamna kazi na wanaendelea kuwepo katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, katika Jimbo langu nina changamoto na nilikueleza siku ile ulikuwepo na Makamu wa Rais. Katika eneo la Kata ya Buger kulikuwa na changamoto kubwa na bahati nzuri nilipata bahati ya kwenda na Naibu Waziri, wanachobishainia pale wananchi na watu wa uhifadhi ikizidi sana kwa upana ni hatua 30 na maeneo mengine ni hatua 10. Hata hivyo, imekuwa ni mgogoro wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 TANAPA waliweka alama, 2014 wakaboresha, mwaka 2018 wakaingia kwa wananchi zaidi kama ninavyoeleza hatua 30 maeneo mengine hatua 14 lakini ikizidi sana upana huo ni hatua 30. Nilienda na Mheshimiwa Naibu Waziri lilipopata bahati ya kutembelewa, badala ya kupungua kwa ule mgogoro alichokifanya Naibu Waziri, ni kwenda kuongeza ule mgogoro na aliendelea kutoa matamko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa Viongozi au Mawaziri tusiwe Mawaziri wa matamko, tujaribu kusikiliza wananchi wetu. Shida yetu kubwa ni kwamba tunawasikiliza viongozi wale ambao tunawakuta kwenye eneo lile na ambao wako upande wa Serikali. Tunashindwa kutoa fursa kama Kiongozi kuwasikiliza wananchi. Sasa kama Kiongozi wa Serikali upime sasa lile unaloambiwa na mwenzako kule chini linaendana na hali ya wananchi wa eneo husika? Mimi sioni sababu ya wananchi kuendelea kugombana na Serikali yao kwa hatua 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru uliahidi kwamba mwezi huu wa Saba unaweza kwenda kutembelea eneo lile la Buger na mimi nikukaribishe. Sioni sababu ukagawanya Kata, kaya baadhi za wananchi lakini inakata mashamba ya watu na Mheshimiwa Naibu Waziri alisema tutatoa fidia. Wananchi wale wamenituma sisi hatuna shida na fedha bali sisi tuna shida na ardhi yetu ambayo tumekaa nayo toka enzi za mababu. Hatuko tayari kuchukua fidia, kama ni mali yenu kwa nini mnatufidia sisi? Huwezi kutufidia, kama ni mali yako chukua, kama ni mali yetu usitufidie! Sisi hatuhitaji na wananchi wale wamenituma kwamba sisi fidia hatuhitaji, tunachohitaji ni ardhi yetu na siyo eneo kubwa ni eneo dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Serikali mwaka 2011 wanakuja kuweka beacon, wametumia fedha za umma, wanakuja kuweka 2014, wanakuja kuweka 2018 watu hao hao! Unajiuliza, wale waliofanya 2011 ni Serikali kutoka wapi, na hawa 2018 ni kutoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba pia ninakukaribisha katika Jimbo la Karatu, tutakwenda kwenye ile Kata, wananchi wale hawana shida, sisi tunaelewa kwa sababu tumekaa na hawa wanyama muda mrefu, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeanzishwa mwaka 1959 sisi tunakaa nao? Pia, wananchi wale hawana shida na uhifadhi ni katika eneo lile linaloonekana wananchi wetu wananyang’anywa mali yao kwa nguvu kabisa. Kwa sababu 2011 waliweka beacon, 2014 waliweka beacon na 2018 wakasogeza wakaingia kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru kwa nafasi lakini ninamuomba Mheshimiwa Waziri mwezi wa Saba karibu kwenye Jimbo langu tuweze kushusha ile pressure. Siku ile ulipotoa kauli katika eneo la Karatu wale pressure ilishuka. Nami ninaamini kwa jinsi ulivyofanya kule Tarime naamini kwamba kwa Karatu utaweza kuja kufanya vizuri, ninakushukuru na ninakukaribisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Manaibu Waziri wote wawili, pia nawapongeza sana Meneja wa TARURA Mkoa, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, vilevile meneja wangu wa Wilaya ya Karatu wa TARURA.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali katika bajeti ya mwaka jana 2021/2022 katika Jimbo la Karatu kulikuwa na wananchi ambao wamepisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Lake Manyara, lakini naishukuru Serikali katika mwaka huu, wamelipa wale watu kwa zaidi ya 5.9 Bilioni kwa maana wananchi wale wa Jimbo la Karatu wanaishukuru Serikali na mimi kama Mwakilishi wao pia naishukuru Serikali kwa malipo haya ya 5.9 Bilioni naamini kwamba tathmini ilifanyika mwaka wa 2014 na wananchi wale wamelipwa mwaka wa 2022 naamini pia kuna changamoto lakini kwa hili la kulipwa 5.9 naishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme katika Jimbo la Karatu kuna barabara hii ya Karatu - Mbulu - Hydom - Singida, lakini vilevile nilitaka niweke kumbukumbu sahihi Karatu iko Mkoa wa Arusha iko Mkoa wa Manyara, kwa sababu mara nyingi sana Manaibu Mawaziri wanapojibu kwamba wanaitafsiri barabara hii inaunganisha ikiwa ndani ya Mkoa wa Manyara barabara hii ya Karatu Mbulu - Hydom Singida ambayo ni Km 109 ambayo iko kwenye Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, mwaka wa 2010 chini ya Jakaya akiwa mgombea wa Uraisi wakati huo, 2015 Hayati Magufuli akiwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi, mwaka 2020 ikiwa sisi kama wagombea wa Chama cha Mapinduzi wakati ule tuliaminishwa kwamba iko kwenye Ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi na wakati wowote hii barabara inaweza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, changamoto na ngonjera zimekuwa nyingi kupitia Wizara hii ya Ujenzi kwamba mwaka jana tuliambiwa imetengwa Km 25 na mwaka jana walisema wamekosa Mkandarasi aliyeomba kwa Km 25 umeongeze 25 sasa jumla ni Km 50, ambayo itaanzia Mbulu- Hydom, lakini tulifikiri ingeanza tungeshukuru lakini mpaka sasa hivi ipo kimya giza nene. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hii ni ya Km 190 kama alivyoelezea mwezangu ambaye jana alitaka kuruka sarakasi sisi wengine hatuwezi tunaweza kuiseme tu Serikali kwa lugha nzuri na mtuelewe kwamba Wilaya Saba ambayo inaunganisha na ile barabara ya Karatu, Mbulu, Hydom, Singida na maeneo mengine ya Wilaya mbalimbali ndani ya Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara nyingine ambayo ni barabara ya Karatu, Mangola, Matala ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. Ni nia ya Serikali kwamba sasa hizi barabara za kuunganisha Mkoa, kwa mfano kwa sasa Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu bado haujaunganishwa na barabara hiyo ni ya urefu wa Km 328, lakini naamini Wabunge walio wengi ni Wabunge wanaotokana na CCM, tulitembea kwa wananchi wa Tanzania tukiwaaminisha kwamba Ilani hii ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ndani ya miaka mitano tunaweza kwenda kuitekeleza.

Mheshimiwa Spika, naamini sasa tuna takribani miaka miwili utekelezaji katika Jimbo langu kuanzia sasa ni asilimia Sifuri sasa nafikiri imebaki miaka miwili na chenji, je Ilani ile ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo tumewaaminisha Watanzania walio wengi na walioko ndani ya Jimbo la Karatu. Mheshimiwa Waziri tukuombe, kwa sasa changamoto ni kubwa tunajua lakini tuamini kwamba sasa tutathmini kwa miaka hii miwili Je tumeweza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025 kwa kiwango gani ndani ya miaka hii miwili ili mwaka mwingine unaokuja wa fedha tuweze kuona ni namna ipi tunaweza kuweka vizuri Ilani yetu isituletee shida kwa wananchi wetu ambao tunawaongoza na wametupa kipaumbele tuwasemee katika jengo hili Takatifu.

Mheshimiwa Spika, niseme Km 328 kuunganisha barabara ya Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Arusha siyo kilometa nyingi sana, naamini barabara hii itakuwa ni barabara fupi ya kuunganisha Mkoa wa Shinyanga kwenda kuunganisha Mwanza na Mikoa mingine ya huko kama Mkoa wa Mara na Mikoa mingine ya ukanda wa Ziwa. Tunaomba Serikali Km 322 ambayo inaunganisha kibiashara Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Spika, mwaka wa 2015 tulitembelewa kwa wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, leo ni Rais alisema kuna barabara ambayo alituahidi kwa kipindi hicho kwa kiwango wa lami, mwaka 2015 barabara inayotoka Kibaoni inaelekea Endabashi siyo kubwa sana kilometa zake lakini barabara hiyo hata siyo kwa kiwango cha lami tunaomba iwekwe hata kwa kiwango cha moram.

Mheshimiwa Spika, ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)