Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel (3 total)

MHE. NOAH L. S. MOLLE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri , lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali ina nia njema ya kutoa huduma ya maji, kulikuwa na miradi ya mwaka 2009 miradi ya Likamba, Musa, Nengu, Olotushura na Loskito, je, ni lini sasa Serikali itakamilisha miradi hiyo ya muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Maji katika kukarabati Mradi wa Ilmuro inayohudumia Kata za Oljoro na Laroy. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ahadi hiyo ya Mheshimiwa Waziri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Lemburis Saputu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mradi huu ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2009, nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge miradi hii tunakuja kuitekeleza na nimeshafika eneo lake. Nimwahidi namna ambavyo tuliongea pale site tutakuja kufanyia kazi haraka iwezekanavyo na pamoja na hii ahadi ya Mheshimiwa Waziri aliyepita, ukarabati wa Mradi huo wa Ilmuro pia unakuja kufanyiwa kazi hivi karibuni. Fedha tayari zipo na mgao unaofuata na mgao unaofuata na Mheshimiwa Mbunge yupo na atakwenda kutekelezewa mradi huo.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nia ya mfuko huo ni kujaribu kusaidia vijana na akina mama na watu wenye ulemavu katika kukuza ajira, hawaoni sasa ni muda mwafaka wa kuongeza muda kutoka miaka 18 hadi 45 badala ya 18 mpaka 35 ambayo hiyo inawazuia wananchi walio wengi kupata mikopo hiyo na kufanya biashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Noah kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mikopo hii kwa vijana ni kuhakikisha kwamba pia inawawezesha kiuchumi, na hasa vijana wa umri wa miaka 18 hadi 35 kwa maana ya definition ya kijana. Kwa hiyo, wazo lake la kuongeza wigo kutoka miaka 18 hadi 45 linahitaji pia kulifanyia tathmini na kuona kama miaka 45 iko ndani ya umri wa ujana au kama maana yenyewe ya vijana inahitaji kuboreshwa ili kuongeza wigo huo. Kwa hiyo, ni wazo zuri, lengo ni kuboresha na sisi Serikali tunaomba tulichukue hilo tukalitafakari na kuona uwezekano wa kulitekeleza kwa manufaa ya jamii yetu. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, na kutakuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuuliza, kwa kuwa suala la kupanuliwa kwa hospitali hiyo ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kwa muda mrefu; je, hospitali hiyo iko kwenye idadi ya hospitali 21 zitakazokarabatiwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, hospitali hiyo inatoa huduma kwa akina mama na watoto vijijini ambao hawana uwezo wa kupata huduma za afya kwenye hospitali binafsi ambazo ni gharama kubwa, je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa kuiweka hospitali hiyo kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ili na yenyewe iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUNGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Noah Mollel Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie kwamba ahadi zote za viongozi wetu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Nimhakikishie kwamba hospitali hii ya Orturmet ni miongoni mwa hospitali ambazo zimepewa kipaumbele; na nimhakikishie kwamba katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 tumeanza na hospitali 21 awamu ya kwanza; na tutakuwa na awamu ya pili ya hospitali zile nyingine ambazo zinabaki. Nimhakikishie katika awamu hiyo ya pili hospitali hiyo ya Orturmet Arusha ni miongoni mwa hospitali ambazo zitaingizwa ili ziweze kufanyiwa upanuzi na ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hospitali hii inatoa huduma kwa wananchi vijijini na wengi wao ambao hawana uwezo na ndiyo maana Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaingiza kwenye orodha hospitali ambazo zinapewa kipaumbele kwaajili ya ukarabati ili iendelee kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi katika maeneo hayo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Noah kwamba jambo hilo linafanyiwa kazi na mara fedha zikipatikana hospitali hii itakarabatiwa ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.