Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel (2 total)

MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa maji kwenye Vijiji vya Engutukoiti, Losineni, Juu, Losineni kati, Oldonyawasi, Lemanda, Lemengrass, Oldonyosambu, Likurat, Olkeejulbendet, Lenigjape, Olkokula, Lemanyati, Lenjani, Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni na Kata za Kimyak, Sambasha Tarakwa, Oloirien, Kiranyi, Likidingla, Sokon II, Olturito, Bangata, Mlanganini, Nduruma, Bwawani, Oljoro na Lahni Musa, Kisango, Mwandet Wilayani Arumeru?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lemburis Saputi Mollel, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli vijiji hivi vilikuwa na changamoto ya huduma ya maji, lakini kuanzia mwezi Disemba, 2020, Vijiji vya Lengijave, Olkokola, Seuri, Ekenywa na Ngaramtoni vimeanza kupata huduma ya maji kutoka kwenye mradi uliofadhiliwa na Shirika la Uingereza la DFID kupitia Shirika la Water Aid Tanzania. Aidha, Vijiji vingine vya Oldonyosambu, Oldonyowasi, Lemanda, Losinani Kati na Juu na Ilkuroti vinatarajiwa kupata huduma ya maji kutoka kwenye mradi huu kupitia upanuzi unaofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Jiji la Arusha kutoka kwenye tanki la maji lililopo kijiji cha Lengijave, lenye ukubwa wa mita za ujazo 450. Kijiji cha Lemanyata kina huduma ya maji kupitia Mradi wa Olkokola – Mwandeti.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/ 2021, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 1.13 kwa Wilaya ya Arumeru kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa Mradi wa Maji wa zamani wa Nduruma – Mlangarini na kukarabati Mtandao wa Bomba unaopeleka maji Vijiji vya Themi ya Simba, Kigongoni na Samaria na ukarabati wa Mradi wa Manyire – Maurani – Majimoto utakaonufaisha Vijiji vya Maurani, Manyire na Maji moto kuwa na maji ya uhakika na Miradi ya Likamba na Oloitushura & Nengungu.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Hospitali ya Wilaya ya Olturumet katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kwa kuipatia jengo la OPD, Wodi ya kulaza Wagonjwa, Jengo la X-Ray na mashine ya X-Ray ili Hospitali hiyo iweze kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemberis Saputu Mollel, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri nchini ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Olturumet Arusha, ambazo zinahitaji ukarabati na upanuzi wa miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Ukarabati wa Hospitali kongwe 43 nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali itaomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kuanza ukarabati wa Hospitali 21 za Halmashauri nchini. Mpango huo utaendelea kutekelezwa kwa awamu hadi ukarabati na upanuzi wa hospitali kongwe zote nchini utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge Noah kuwa Hospitali ya Wilaya ya Olturumet Arusha ni miongoni mwa hospitali ambazo zitafanyiwa ukarabati na upanuzi.