Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nishukuru wananchi wangu wa Jimbo la Arumeru Magharibi.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira tuliyonayo ya kuchangia bajeti hii tunaamini kwamba bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu inakwenda kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2021/2022, ndiyo maana hapa tumeanza mchakato huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea ningependa sana kusema maneno machache kabla sijachangia. Nitumie maneno ya Mungu, wakati ule Yesu alipokuja duniani kwa ajili ya kuokoa dunia alikuwa na wanafunzi wake 12. Katika wale wanafunzi, Yesu alitabiri kwamba kuna wawili watakaomsaliti, alikuwa ni Petro na Yuda Iskariote. Alipokuwa pia akiendelea alijaribiwa na shetani sana akampandisha juu ya mlima mkubwa sana akamwambia ukinisujudu nitakupa dunia hii yote itakuwa ya kwako na miliki zote, lakini Yesu akamwambia rudi zako nyuma shetani kwa sababu miliki yote hii ni ya kwangu.

Mheshimiwa Spika, nayasema hayo, lakini pia alipokuwa akiendelea alikutana na watoza ushuru, wakamuuliza sisi tufanye nini Bwana? Akawaambia na ninyi mtosheke na mishahara yenu. Nimeona nianzie na hapo. Nasikitika sana, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambaye aliinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa nguvu zake zote na nia yake yote na moyo wake wote, leo tunapata akina Yuda. Leo kina Yuda wamejitokeza kumsaliti Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano. Inasikitisha, mzee wa watu ametangulia mbele ya haki, hawezi kujitetea, lakini ninyi mlioko ndani na nje mnataka kumdhalilisha. Hakika, asilani kabla hamjamdhalilisha Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano, nina hakika Mwenyezi Mungu atawashughulikia usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifanya kazi ya kuwaaminisha Watanzania kwamba kweli ni Rais anayejali maskini, anayejali Taifa hili kama alivyokuwa mtangulizi wake Rais wa Serikali ya Kwanza Nyerere alifuata hizo nyayo na Serikali zote zingine zilizofuata alionesha njia kubwa. Alipokuwa akitunadi, niliumia sana ninapoona kwenye mitandano watu wanachafua hali ya hewa Magufuli hata panya akitoboa gunia kule nyumbani kwa mtu, Magufuli! Kwa sababu yeye hayupo. Kama kuna watu wamefanya ufasadi kwenye Wizara, Bandari na halmashauri watu wanasema Magufuli, kawatuma? Nasikitika sana, lakini Mwenyezi Mungu atawashughulikia kabla ya siku zao si nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akina Yuda hawakosekani, lakini nawaambia ninyi ambao mnadhani mtaishi milele hakuna nafsi, kila nafsi iliyoko hapa kwenye Bunge hili na nje ya Bunge hili itaonja mauti. Hakuna anayedumu milele wala hatuna mji udumuo katika dunia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, mama Samia Suluhu Hassan alikuwa ni msaidizi wa Dkt. John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Rais wetu wa sasa mama Samia Suluhu Hassan alikuwa mwaminifu na muadilifu na ndiyo maana Mwenyezi Mungu amemuona akawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtaona jinsi gani mama yule, Rais wetu mpendwa amehakikisha kwamba wale waliokuwa wanatazamia kwamba atabadilisha Serikali kwa asilimia sijui ngapi, amesema “Kazi Iendelee”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tusifikiri kwamba kwa mwelekeo huo Mheshimiwa Rais aliyeko ataweza kumsaliti Magufuli. Legacy ya Magufuli itaendelea kubaki sasa na hata milele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niendelee kutoa mchango wangu. Najua kabisa Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani ya Mwaka 2020/2021 imefanya kazi kubwa na hakuna mtu asiyejua, hakuna asiyaona. Kwenye dispensary tumefanya vizuri Chama Cha Mapinduzi, kwenye bandari, kwenye reli, kwenye masuala ya hospitali na kadhalika. Barabara nchi hii ni kubwa lakini imetekelezwa Ilani kwa asilimia 90 kuunganisha mikoa yote ya Tanzania. Hakuna ubishi na anayebisha hapa asimame, hii nchi ni kubwa, hata kule Roma, Mji wa Baba Mtakatifu unajengwa mpaka leo wajenzi wapo wanajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2021/2022, sasa ni kazi yetu kuikumbusha Serikali kwamba kuna upungufu ule mdogo mdogo yaliyoko kwenye vijiji, kata, wilaya na kwa ujumla kwenye mikoa. Ni wajibu wa Serikali yetu kwenda kutekeleza kwa kutumia bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ahadi ya Waheshimiwa Viongozi wetu Awamu ya Tano, Awamu ya Pili, Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne. Awamu ya Tano ambayo kwa sasa ndiyo iliyoongozwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi barabara za lami kwenye majimbo yetu, aliahidi kutengenezwa hospitali, ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu yeye tunamuamini na tunamwona ni mchapakazi, yeye ndiyo anasimamia shughuli za Serikali Bungeni, hebu sasa Serikali ije na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba hizi ahadi ambazo Waheshimiwa Marais wetu wanatoa, Waheshimiwa Mawaziri wahakikishe kwamba wameweka kwenye bundle moja ili iweze kutekelezwa kikamilifu na iweze kuwepo katika reference. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la ahadi linasumbua sana wananchi kwa sababu wanasema Rais ametuahidi kila siku anasema Mbunge wakumbushe, wakumbushe. Sisi ni wajibu wetu kama Wabunge kuikumbusha Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi na imefanya kazi kubwa, imetekeleza ahadi nyingi imepungua hizo ndogo tu, lakini ningeomba ingewekwa kwenye bundle moja ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye jimbo langu Awamu ya Nne iliahidiwa barabara ya Hospitali ya Oturumeti, hospitali ya wilaya kwa lami. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameahidi barabara ya Mianzini – Kimbolo –Ngaramtoni; barabara iliahidiwa na Mheshimiwa Jaffo, barabara ya kwenda Hospitali ya Nduruma, Bwawani na katika majimbo mengine yote Tanzania. Najua hii nchi ni kubwa, lakini ni wajibu wetu kuendelea kuikumbusha Serikali yetu tukufu na sikivu kuhakikisha kwamba imeondoa hizo ahadi za Waheshimiwa Marais wetu.

Mheshimiwa Spika, suala la ajira; kama tunavyojua Serikali inajitahidi, sasa niombe ijitahidi sana kuboresha katika Sekta Binafsi na kwa ajili ya kupata mazingira mazuri ya kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili vijana wetu ambao wanahangaika huku na huku waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kilimo; kuna mashamba makubwa yametelekezwa kama mashamba haya yangeweza kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo wakaunganisha kama wale ma-settler walivyokuwa wanalima kahawa, maharage, mahindi, ingeweza kuleta tija na ajira. Bado naamini kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu itaendelea kuchapa kazi na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanafanya kazi vizuri. Kwa mfano kwenye Jimbo langu, kuna mashamba makubwa kama ya Aga Khan, imechukua mwaka 2006 ikisema itajenga Chuo Kikuu, zaidi ya heka 3,000 hadi leo shamba hilo limesimama, lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500, lakini naamini Wizara ya Ardhi itaekwenda kufuatilia shamba hilo ili kujua hatma yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuchangia katika ardhi na ajira, kuna suala la Mfuko huu wa Akinamama, Vijana na Wenye Ulemavu. Naomba Wizara husika ije na mpango mahsusi wa kuboresha Mfuko ule ukae vizuri kwa sababu, hivi sasa kuna utata mkubwa katika mfuko huo, watu wanaopata mikopo ni 18 – 35, lakini utaona ni jinsi gani bado watu wa age hiyo wako shuleni. Sasa ni vizuri wakaja pia na marekebisho kama itawezekana wakanzia 18 mpaka angalau 40, hapo utapata watu wengi ambao wataongea uchumi na wataanzisha biashara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Afya…

NAIBU SPIKA: Kila Mbunge anayeitwa anachangia kwa dakika tano.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyenipa fursa hii ya kusimama kwenye Bunge lako hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kwenye suala la ukosefu wa dawa kwenye hospitali zetu. Suala hili limekuwa ni tatizo kubwa. tunajua Serikali imejitahidi sana kwenye masuala ya miundombinu, lakini bado tuna changamoto sana kwenye suala la ukosefu wa dawa. Akina mama wanateseka na watoto, wazee wanateseka. Nilikuwa naomba suala ambalo litamfanya Waziri wa Afya na timu yake nzima wasipate usingizi, wasilale usiku, ni suala la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni suala la ukosefu wa dawa kwa sababu ya hujuma, labda wizi kwenye hospitali zetu, naomba hili suala kwa kweli; akina mama na watoto wanateseka, wazee wanakosa dawa na wagonjwa wengine wanakosa dawa hospitalini. Wale wanaoiba dawa hospitalini, basi mwaangalie na kuwaangazia macho sawa sawa kwa sababu katika jambo hili la ukosefu wa dawa kwenye hospitali, ni sawa sawa na kumsindikiza mgonjwa katika mauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anapokwenda hospitali na akakosa dawa, matumaini ya kuishi duniani tena hakuna. Kwa hiyo, nawaomba sana suala hili tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, suala la ukosefu wa madaktari, hili nalo ni changamoto kubwa. Watu wanapokwenda kwenye hospitali wanakosa madaktari, hii bado ni changamoto kubwa mno. Naomba Serikali kwa sababu imetangaza ajira hizo, iendelee kuongeza kasi kubwa kuhakikisha kwamba tunapata madaktari wa kutosha na manesi wa kutosha kwenye hospitali zetu ili kuokoa akina mama wajawazito na watoto na wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wazee kupewa barua ya kwenda kupata dawa kwenye Dirisha la Wazee bado na yenyewe ni changamoto. Wazee hao wanateseka, hakuna dawa. Nilikuwa naomba Serikali iangalie hiyo Sera ya Wazee na yenyewe kwa sababu bado kuna changamoto kubwa, wale wazee wanateseka. Ni vizuri wakaja na mpango mahususi wa kuhakikisha kwamba wazee hawa badala ya kupewa barua kwa Mtendaji wa Kata na Mtendaji wa Kijiji, ni bora wapewe Bima ya Afya, hata kama ni hii iliyoboreshwa, nao wapate iwe ni sehemu ya kuweza kuhakikisha kwamba wazee hawa wanaangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, tuko hapa lakini tunapata matatizo makubwa kwenye majimbo yetu kwamba wananchi wanalia dawa hakuna, wazee wanateseka, watoto wanateseka, akina mama wanateseka, wajawazito na wagonjwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naomba sana, sana sana Serikali yetu Sikivu ya Chama cha Mapinduzi, katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi chonde chonde; na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan alipokuja hapa Bungeni alituambia yeye ni mama, kwa hiyo, machungu ya mama anayajua vizuri. Kwa hiyo, naendelea kuiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ijitahidi sana katika suala la dawa; na Mheshimiwa Waziri usilale usingizi kwa sababu, wamama hawana dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali kama tuna majengo halafu hatuna dawa ni sawa na hakuna hospitali, lakini tukiwa na dawa; hospitali ndiyo dawa. Kama tukiwa na majengo hata maghorofa, kama hakuna dawa, hospitali hakuna; na unafuu wa maisha haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema tena kwamba suala la motisha kwa madaktari na lenyewe ni jambo ambalo Serikali iliangalie kwa makini kwa sababu wale watu wanafanya kazi usiku na mchana, saa 24. Ni sawa na kazi ya jeshi. Wanajeshi wanafanya kazi usiku na mchana kama madaktari. Kwa hiyo, nawaomba pia suala la motisha kwa madaktari na manesi wetu ni suala la msingi na la muhimu sana ili waweze kuwa na moyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado narudia kusema, suala la wizi wa dawa, lazima Waziri asilale usingizi kwa sababu kukosekana kwa dawa ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nichukue nafasi hii pia kukupongeza sana wewe kwa jinsi ambavyo unaongoza Bunge hili, lakini nichukue nafasi hii sana kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amewasilisha hotuba yake na jinsi ambavyo amehakikisha ametekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, hasa kuanzia 2015 hadi 2020.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameonesha umahiri mkubwa sana katika jambo hili. Ukiangalia jinsi ambavyo ameanza katika mwaka 2015 hadi kufikia 2020, watu walikuwa wameanza kusema labda ni nguvu ya soda, lakini kwa kweli, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, amefanya kazi kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na wasaidizi wake kwa kweli, hatuna sababu ya kutokuwapongeza, lakini katika kupongeza huko nakumbuka maneno yako ulikuwa siku moja umesema, Spika wa Bunge la Kenya alisema Mtanzania akisimama, anapongeza halafu anakaa chini, lakini utamaduni wetu Watanzania ni kupongeza. Mtu wa Kenya akienda dukani anasema nataka chumvi hasemi naomba, kama sisi Watanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa pongezi, niende kuchangia kwenye maeneo mawili matatu, kama wenzangu ambavyo wamechangia. Naenda kwenye afya; Wizara ya Afya imefanya kazi kubwa sana. Katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi tunaishukuru Serikali sana kwa kutuletea fedha kwenye vituo vya afya. Kituo cha Afya cha Nduruma kimepata milioni 500, Kituo cha Mbuyuni milioni 400, Kituo cha Musa kimepata milioni 200; hii ni kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais katika kipindi chake ameboresha afya, amefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa katika Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Zahanati nyingi tumewahamasisha wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi kwa ajili ya kujenga kwa dhana ile ya kila kata, kila kijiji kujenga zahanati kufikia lenta, kwa maana ya maboma, ili Serikali iweze kumalizia. Naomba kuishauri Serikali, hasa Wizara ya Afya, ni lini sasa itamalizia hayo maboma ambayo wananchi wamejenga katika kuwahamasisha, ili basi lile lengo la kila kijiji kuwa na zahanati, ili hizi zahanati zikamilike?

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu kuna zahanati nyingi sana kama 11 katika Vijiji vya Ilkerin, Bwawani, Kigongoni kule na kadhalika. Hii itasaidia sana kukamilisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kama Mheshimiwa Rais wetu anavyojali katika masuala ya afya.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Wizara ya afya kwamba, badala ya kuwapa wazee kitambulisho, ni kwa nini sasa Serikali isije kwenye sera yake irekebishe wazee wapewe bima ya afya kama watu wengine. Kwa sababu, katika kupewa vitambulisho hawapati huduma ipasavyo. Hilo nalo naomba Wizara hiyo iliangalie.

Mheshimiwa Spika, suala la upungufu wa Madaktari; hili nalo naomba Serikali ijaribu kuangalia kwa sababu, unakuta Nesi katika baadhi ya maeneo, Serikali imejitahidi sana, lakini bado kuna upungufu katika maeneo machache. Ningeomba Serikali irudie tena kuangalia maeneo hayo kwa ajili ya kupatikana kwa Madaktari katika vituo vyetu vya afya.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara. Serikali imejitahidi sana, nchi hii ni kubwa, lakini Serikali imejitahidi kuhakikisha kwamba, imeunganisha wilaya na wilaya, mikoa na mikoa, lakini naomba kuna ahadi ambazo Mheshimkwa Rais pamoja na viongozi wengine wameweza kutoa katika ziara na hasa wakati wa kampeni, basi katika bajeti ijayo barabara hizo zikumbukwe. Kwenye jimbo langu kuna barabara ambayo imefanyiwa tathmini kwa mfano barabara ya Arusha – Mirongoine – Tera kwenda Kongwa. Naomba hii barabara katika bajeti hii isisahaulike.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ambayo tumeahidiwa pia na Mheshimiwa Rais, Barabara ya Mianzini – Timbolo kutokea Sambasha kwenda Ngaramtoni, hiyo ni barabara ya kilometa 18, Mheshimiwa Rais aliahidi kwa kiwango cha lami. Naomba Wizara husika isisahau kwenye bajeti hii; vile vile barabara ya kwenda Hospitali ya Oturumet, Hospitali ya Wilaya, kilometa tatu; na barabara ya kwenda Hospitali ya Seliani, kilometa tatu. Hayo ni maeneo ya huduma ambayo wananchi hawa wanahitaji kwa ajili ya kupata huduma bora. Pamoja na hayo tunaendelea kuipongeza Serikali kwa sababu, kwa kweli inajitahidi kwa kadiri ilivyoweza kuwafikia wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, niingie kwenye suala la ajira; vijana wetu wengi wanakosa ajira, lakini Serikali imejitahidi kuimarisha sekta binafsi na hata ndani ya Serikali katika kuajiri vijana wetu. Ushauri wangu kuna Mfuko ule wa Akinamama na Vijana na watu Wenye Ulemavu; naishauri Serikali iangalie hiyo Sera ya Mfuko huo kwa sababu, utakuta vijana kuanzia miaka 18 mpaka 35 ndio wanaostahili kupata huo mkopo kwenye halmashauri zetu, lakini ukienda mbali zaidi ukiangalia watu wanaoweza kufanya biashara vizuri ni kuanzia miaka 18 mpaka angalau 40 mpaka 45.

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali iangalie hiyo sera, ili kwa sababu ya ukosefu wa ajira kuanzia 18 mpaka 45 waweze kuingizwa kwenye sera ili waweze kupata hiyo mikopo. Hata hivyo, tunaendelea kuishukuru Serikali kwa sababu, imeondoa riba kwenye Mfuko huo na sasa wengi wananufaika isipokuwa upande wa vijana kuna changamoto kidogo kwa sababu ya hayo mambo magumu. Naomba pia, kuishauri Serikali kuangalia uanzishwaji wa vokundi kuanzia watu watano mpaka na kuendelea. Kwa sasa hivi ni watu 10, wananchi bado wanaona kidogo inawawia vigumu kuanzisha hivyo vikundi kuanzia watu 10 na kuendelea, lakini wakati ule ilikuwa watu watano angalau wananchi wanapata kujiunga vizuri na kuanzisha vikundi kwa ajili ya ujasiriamali. Nina uhakika eneo hili likiboreshwa suala la upungufu wa ajira ambalo kila siku sisi Wabunge na hasa mimi ninavyozungumzia kwenye jimbo langu, kila siku wananchi wananchi wanasema tutafutie ajira. Eneo hili tukiliboresha vizuri nadhani kwamba, wananchi wetu watapata ajira.

Mheshimiwa Spika, suala la NIDA; Mheshimiwa Rais katika hotuba yake alisema ataboresha vitambulisho vya Wamachinga na baadae viwe kama vya NIDA, lakini naomba watu wanaohusika na NIDA hasa Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa kweli, wananchi wanateseka sana katika maeneo mbalimbali kupata huduma kwa sababu ya ukosefu wa vitambulisho hivyo vya Taifa. Hebu iangaliwe kwamba, kuna nini hasa kinachopelekea mpaka wananchi hawawezi kupata vitambulisho kwa wakati, ili waweze kupata huduma. Hasa ukizingatia kwamba, kitambulisho cha Taifa kwa sasa wananchi walio wengi wanahitajika kuwa nacho kwa ajili ya kupata huduma katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, suala la maji; kwanza niishukuru Serikali kwa kutupatia mradi mkubwa wa maji wa bilioni 500 katika Jiji la Arusha ambao unahudumia hasa katika jimbo langu na maji hayo yametoka kwenye jimbo langu. Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua mradi huo mkubwa kwa kweli, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ameonesha ni kiongozi ambaye watu. Ninachoweza tu kusema hapa naomba sasa niikumbushe Wizara iangalie yale maeneo ambayo Mheshimiwa Rais ameahidi, ili maji yaweze kuwafikia waweze kupata. Kwa mfano maeneo yale ya Floraid, Lemong’o, Lemanda, kule Ngutukoit, Losinoni Juu, Losinoni Kati mpaka huku chini kuja Oldonyosambu. Naamini Wizara itajitahidi kwa jinsi ambavyo inamuunga Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, suala la ulinzi na usalama wa wananchi wetu. Kama tunavyojua Serikali yoyote duniani ni Serikali ambayo inahakikisha wananchi wake wanaishi kwa salama na amani. Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imefanya kazi kubwa sana ukizingatia katika kipindi hiki chote cha miaka mitano uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa mno.

Mheshimiwa Spika, nina tatizo kidogo la kushirikiana. Nimwombe Waziri anayehusika wa Ulinzi, kuna mgogoro mkubwa sana na Waziri wa Maliasili, kuna mgogoro ambao haujakaa vizuri kwenye jimbo langu. Ningemwomba Waziri angefika kule kwenye Msitu wa Meru. Wananchi kule…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Elimu imekuwa na falsafa nyingi wakati wa miaka nenda rudi. Kulikuwa na suala la Elimu ni Ufunguo wa Maisha, Elimu ni Bahari, Elimu haina Mwisho. Hayo yote ilikuwa ni kuhakikisha tunahamasisha elimu katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kuhakikisha kwamba elimu katika nchi yetu inasonga mbele. Kama tunavyofahamu elimu ndiyo imefanya Taifa hili likafika mahali hapa. Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema anaitwa J.K. Chesterton alisema: “Education is simply the soul of a society as it passes from one generation to another.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo yote ni mwelekeo wa kuhakikisha kwamba Taifa letu linakwenda kuwa salama kwa sababu wananchi wetu wanapata elimu. Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru TAMISEMI kwa jinsi ambavyo wametuletea fedha za mabweni, madarasa na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nitajikita katika maeneo manne kuhusu vikwazo vya elimu. Vikwazo vya elimu vipo vingi lakini leo nitajikita katika vinne. Kwanza, suala la lugha, lugha ya kufundishia katika shule za msingi kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiswahili, lakini mtoto huyo anapofundishwa Kiswahili masomo kumi na moja, mara moja anatoka kuingia form one, anafundishwa masomo yote Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hawa wanateseka kwa sababu hawajui lugha ya Kiingereza wanapoingia form one. Hii inatuleta utata mkubwa, watoto wanachukia shule, hawapendi shule kwa sababu hawaelewi wanapofundishwa darasani form one mpaka form four na wakati huo huo wanapewa mtihani huo kwa Kiingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Wizara ya Elimu hebu suala hili liangaliwe kwa sababu ukiangalia shule za private kuanzia chekechea mpaka darasa la saba ni Kiingereza, lakini mtoto wa shule ya Serikali anakwenda form one akiwa anajua Kiswahili tu, ushindani huu hauko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Waziri wa Elimu atakapokuja hapa atuambie utafiti huu unasema nini kuhusu mtoto wa darasa la kwanza wa Serikali mpaka darasa la saba, akaja akaingia form one kwenda four inakuwaje? Hapo kuna usawa au tunawatesa watoto kisaikolojia. Naomba tupate maelezo kwamba Serikali inafikiria nini kuhusu hili jambo, kwa sababu hata ukiangalia ufaulu katika za Serikali watoto wanapata zero nyingi. Tunasema tupunguze zero, tutapunguza zero wakati tunawatesa watoto kwa lugha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia shule za private wanafaulu sana kwa kiwango cha juu, kwa sababu wao wametoka Kiingereza shule za msingi, wameingia shule za sekondari lugha ni ile ile ya Kiingereza. Suala hili naomba baadaye Waziri atakapokuja aweze kutueleza vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kingine ni chakula shuleni. Watoto wanateseka, kule shuleni wanasema, Serikali imetoa elimu bure au elimu bila malipo, wazazi wanasema hatuwezi kuchangia maana Serikali imetoa fedha. Sasa ni vizuri Wizara ya Elimu na TAMISEMI itoe tamko kwamba kila mzazi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba mtoto wake anapata chakula au Serikali itoe chakula mashuleni, kwa sababu tunatengeneza Taifa ambalo tunadhani tuna usawa lakini hatuna usawa. Tutatenga watu walionacho na wasionacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wanaosoma private wanakula chakula kizuri mpaka wanamaliza shule, lakini watoto wanaosoma shule zetu za Serikali wanateseka, wanakataa shule, wanaingia makorongoni, wengine wanapata mimba na kadhalika. Ni kwa nini sehemu hiyo Wizara isitoe tamko, imekaa kimya, naomba atakapokuja pia aweze kutujibu kuhusiana na hiyo suala la chakula shuleni watoto wanateseka na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la upungufu wa walimu. Hili ni tatizo, mtoto anakwenda shuleni lakini katika masomo ya physics, chemistry, biology hakuna Mwalimu, lakini mwisho wa siku anapewa mtihani, kuna usawa gani hapo? Naomba Serikali ijitahidi kwa kadri iwezavyo kuwaajiri Walimu hasa wa sayansi ili kuleta usawa katika shule za Serikali na private, vinginevyo tutatengeneza Taifa la wenye nacho na wasio nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala la Walimu liangaliwe, waajiriwe walimu wa kutosha. Nilikuwa nasoma taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema hadi kufikia 2030 inahitajika Walimu milioni 69 kukidhi. Je, Tanzania sisi tumejiandaaje na suala hilo la kuhakikisha kwamba tumekuwa na Walimu wa kutosha. Pia, naomba Waziri atakapokuja atuambie pamoja na kwamba kuna ajira 6,000 za Mheshimiwa Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan amesema waajiriwe, lakini bado kuna haja ya kuongeza jitihada za kuhakikisha kwamba Walimu wanatosheleza ili kuleta usawa katika shule zetu za private na shule za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba suala la elimu ujuzi, wenzangu wamezungumza sana. Tuhakikishe kwamba katika Taifa letu mtu akimaliza, sio anazunguka na vyeti kutafuta kazi, anazunguka na vyeti huku na huku, kazi, kazi, lazima Wizara ya Elimu itengeneze Elimu Ujuzi. Iangalie namna gani itatengeza hiyo sera ili iweze kuhakikisha kwamba watu wetu wanakwenda kusoma lakini wawe na ujuzi wa kutosha kujiajiri na hata kuajiriwa ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi. Naomba nianze kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya; na Wizara hii kwa kweli wamejitahidi kuituliza kwa kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri wanayoifanya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, kuna changamoto mbalimbali ambayo sitaacha kuendelea kuwaambia ili waweze kuendelea kutatua na kuhakikisha kwamba wanazidi kung’aa. Kwanza kabisa urasimishaji wa makazi. Suala la urasimishaji wa makazi ni changamoto. Mmekuja na mpango wa kuwapa makampuni ili waweze kufanya urasimishaji wa makazi, lakini makampuni haya hayana uwezo, kwa sababu hawana wataalam mahususi wa kuhakikisha kwamba wanapima ardhi kwa manufaa ya wananchi. Wamekuwa kama ni matapeli fulani hivi ambao kule kijijini kwanza hawaeleweki, wakienda wanajifichaficha, hawana ushirikiano na viongozi vya wa vijiji, kata na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Wizara nzima wakaangalia eneo hili la urasimishaji wa makazi ikiwezekana waangalie yale makampuni ambayo hayana uwezo, lakini pia waongezee Halmashauri ili iweze kushirikiana kuhakikisha kwamba wananchi wanapimiwa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la wawekezaji kutumia mashamba makubwa kukopa fedha katika Taifa letu na hatimaye kuingia mtini watakapokuwa wamepata hizo fedha. Hili ni suala la kuangalia kwa makini kwa sababu wawekezaji wanakuja wakisema tunawekeza, lakini mwisho wa siku wanakopa fedha kwenye benki zetu na kwenye taasisi zetu za fedha na baadaye wanatoweka na fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano mmoja. Kuna shamba moja kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi Lucy Estate. Mwekezaji huyu alikopa fedha kutoka Benki ya Standard Chartered na baadaye wakakopa NSSF kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni tisa, wametoweka, hakuna uwekezaji wala chochote. Wakati huo huo, baada ya kuona Standard Chartered inataka kuuza hilo shamba na NSSF waliamua kuweka objection mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaona kwamba tunapata hasara kwa sababu ya mali yetu. Shamba ni letu, fedha tumewakopesha, kwa nini tunawaachia hiyo loophole kiasi hicho? Naishauri Serikali kwamba ni vizuri kama mwekezaji anakuja; tuseme umekuja unataka kuwekeza Tanzania kuhusu masuala ya ardhi, basi uwe na asilimia 50 na unachotaka kuwekeza, ndiyo uweze kukopa kwenye Benki zetu na taasisi. Vinginevyo tutaendelea kupoteza ardhi na mwisho wa siku wananchi hawatakuwa na faida na Serikali yetu haitakuwa na faida yoyote. kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja atuambie hili eneo la wawekezaji kutumia loophole hiyo, hatusemi wawekezaji ni watu wabaya, ni wazuri lakini sheria zetu tutaliangalia vipi ili ziwe na manufaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni mashambapori. Kwa mfano, shamba hilo la Lucy sasa ni zaidi ya miaka kama 15, liko, ni shamba zuri, lina rutuba Arusha, hakuna elimu; shamba la Gomba Estate liko pale, ni shamba zuri halilimwi, lakini nazungumzia kilimo. Nitazungumziaje kilimo kama tunaweza kuacha maeneo mazuri kama hayo bila kutumia kwa manufaa ya wananchi wetu ili kuongeza ajira, kukuza uchumi wa nchi yetu? Tunasema kilimo, tunatunza ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri pia maeneo haya ayaangalie kwa sababu inaumiza sana, wananchi hawana ardhi, lakini ardhi inalala miaka 15, 20, 30 hailimwi na ni ardhi ambayo inalimika vizuri, inaingia kila aina ya mazao, inasikitisha na inakera.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Aga Khan ambapo walisema wanajenga Chuo Kikuu tangu mwaka 2006. Wameng’oa kahawa na hilo shamba lilikuwa linaajiri zaidi ya watu 1,500 mpaka 2,000; wameng’oa kahawa, wamefanya nini, wamesema wanajenga Chuo Kikuu tangu 2006, hawajajenga Chuo Kikuu mpaka leo. Je si ukiukwaji wa Sheria za Ardhi Na. 5 na Na. 4 za Ardhi na sheria nyingine za umiliki? Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri sehemu hii usiiangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili shamba wananchi wanalilalamikia ni zaidi ya ekari 4,000 kasoro limekaa; kwa sababu gani? Ni eneo ambalo linaingia aina ya mazao yote, ilikuwa inalimwa maharage, ilikuwa inalimwa ngano na mazao mengine mengi; maua na kadhalika. Wananchi walikuwa wanapata ajira; na Serikali sasa hivi haipati kodi kutokana na mazao ambayo yangelimwa pale hakuna. Tumeacha, tumenyamaza: Je, Aga Khan tunawaogopa, siamini kama Mheshimiwa Waziri Lukuvi anaweza kuwaogopa Aga Khan, kwa sababu hakuna mtu aliyeko juu ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tuko chini ya sheria, kwa hiyo, naomba eneo hili liangaliwe hasa katika shamba la Aga Khan. Naomba Mheshimiwa Waziri atembelee hilo eneo akague shamba lote aone. Asione tu kwamba sisi tunaongea kwa sababu labda tuna chuki, hapana. Tunataka kueleza namna na azima ya wananchi ambao tunataka Taifa letu liende.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba la Gomba Estate pia tumewapa JKT sawa, lakini je, wananchi ambao wako maeneo hayo, wao wanapata nini? Hili nalo tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la Mabaraza ya Ardhi. Mabaraza ya Ardhi inaanzia kwenye ngazi ya vijiji kwa maana ya Kushauri Kata na baadaye Wilaya. Mabaraza haya hasa katika ngazi ya wilaya kuna changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa kesi. Kesi inaweza ikakaa mwaka mzima, miaka miwili, miaka mitatu mpaka minne. Hii siyo sawa, ni kuwakosesha wananchi haki. Hili nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa Mabaraza haya wanatakiwa waangalie namna ya kutoa circular kuwapa posho hasa watu wa kwenye ngazi ya Kata, wanateseka. Tunaepukaje rushwa? Tunasema tunaondoa rushwa kwenye mfumo wa Mahakama, kama watu hao hatujawawekea mfumo mzuri, kwa mfano ufunguzi wa kesi kwenye Baraza la Kata, hayo makatarasi wale watu wanapata wapi kama hakuna chochote ambacho wanapewa kwa ajili ya kuweza kufanya hivyo kazi na kuwaangalia pia namna ya kuwapa posho?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi hasa baina ya wananchi na taasisi zetu za Umma imekidhiri. Kwa mfano, kuna mgogoro wa Kata ya Oldonyosambu, wananchi wale waliondolewa kutoka Oldonyosambu Jeshi letu likachukuwa eneo hilo. Ni vizuri sana kwa sababu ni kwa manufaa ya Taifa letu, lakini sheria inasema, mtu unapotaka kuchukuwa ardhi , mmiliki lazima apewe fidia. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inapotaka kuchukuwa eneo, iwape wananchi fidia na wale wananchi wale wananchi wa Odonyosambu wakumbukwe k wa sababu hii ni haki yao ya msingi. Kuwaondoa bila kuwapa haki yao, siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi na Nengun’g Kata ya Musa walishinda kesi Mahakama Kuu toka mwaka 2016, lakini taasisi yetu ya TMA imeng’ang’ania. Ni kwa nini tusiheshimu sheria? Naomba hii migogoro itatuliwe kwa sababu wananchi wanajiona hawana haki na wakati naamini kwamba chini ya Chama cha Mapinduzi, chama chetu, kimetengeneza ilani ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata haki zao kikamilifu. Kwa hiyo, naamini hili litatendewa haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shamba lingine la Mlangalini Kiserya ,nao halikadhalika ni hivyo hivyo. Wananchi wamenyang’anywa kupitia Jeshi lakini bado hawapati haki zao, kutoka kule Kiserya Kata ya Mlangalini. Nayasema haya ili Mheshimiwa Waziri aweze kuona kwamba kuna haja ya kuangalia hayo maeneo kwa kushirikiana na Wizara nyingine kutatua hii migogoro, maana haileti picha nzuri kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la mabenki kukataa kutoa mikopo kwa kutumia hati miliki ya kimila. Benki nyingi zinakataa hiyo hati kwa sababu wanasema haina value. Sasa ni vizuri Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla tuangalie hati hii, tusije tukawa tunasema tuweke tu hati ya kimila lakini wananchi hawanufaiki. Mtu kuwa na hati ni kwa ajili ya kumsaidia kupata mikopo na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, kama haina value, basi Serikali iseme wazi kwamba hii hati haina value. Kwa hiyo, wananchi wasihangaike kuiweka, lakini naamini kwa sababu Serikali ilikuwa na nia njema, hati hiyo lazima ina value.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba baadaye pia Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind-up, atueleze hiyo hati ni kwa nini mabenki hayapokei na kuna benki nyingine zinasema labda tunaweza tukawapa shilingi milioni tatu tu, mwisho wa hiyo hati. Sababu hakuna. Kwa hiyo, bado kuna changamoto katika hiyo hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangi kwenye bajeti hii ya 2021/2022 katika Bunge lako Tukufu. Na mimi nitakuwa mwizi wa fadhila nisipoishukuru sana Serikali ya mama Samia Suluhu Hassan ya awamu ya sita pamoja na Waziri wa Fedha na Mawaziri wote kwa ujumla kwa jinsi ambavyo wameshirikiana kutengeneza bajeti hii na kuiwasilisha kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo ninaenda kuchangia katika maeneo kadhaa, nikianzia kwenye eneo la ukusanyaji. Ili tuweze kutekeleza bajeti hii na bajeti hii iwe salama lazima Wizara yetu ya Fedha pamoja na taasisi zake zote, zikiongozwa pia na TRA, kuhakikisha kwamba mapato yakutosha yamekusanywa kulingana na bajeti yetu. Kwa sababu bajeti hii inategemea makusanyo ndipo tuweze kuteleza. Kama makusanyo hayatasimamiwa vizuri kama ambavyo wamejitahidi kusimamia ya 2021 malengo yetu haya yote tuliyoyategemea yatashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, kwa jinsi ambavyo Waziri amewasilisha, na alivyojipanga, ninaamini kazi itaendelea vizuri. Katika bajeti hii kama hatutakusanya vizuri hatutapata maji, barabara zile barabara zetu za kwenye majimbo, ukosefu wa maji, vituo vya afya na zahanati haitatelezwa. Lakini naamini Waziri akisimama vizuri, na Mawaziri wote wa idara zote bajeti itatekelezwa na hatimaye makisio haya ya trioni 36 ambayo tumekadiria kukusanya yatakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri ahakikishe kwamba ameweka mifumo rahisi na itakayowavutia walipa ili kodi walipe kodi kwa utaratibu mzuri kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na masharti yasiwe mengi katika kulipa kodi. Kuna watu ambao wanataka kulipa kodi lakini wanapoona huo mlolongo mrefu na vikwazo mbalimbali basi wanashindwa na wanachoka kwenda kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiweka urahisi katika kulipa kodi, tuweke usawa, kwa mfano mtu anapokwenda kupeleka fedha benki mlolongo unakuwa ni rahisi kwa sababu anaweka fedha benki lakini anapotoa inakuwa ngumu. Sisi katika kulipa kodi tunaweka mlolongo mrefu. Ningeomba milolongo hiyo ipunguzwe ili walipa kodi walipe kodi ili miradi yetu iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kukusanya kuna suala la upelekaji wa fedha kwenye majimbo na halmashauri. Hili nalo Mheshimiwa Waziri tunawapongeza kwa kipindi hiki cha 2020/2021 kwa sababu mmejitahidi kwa kweli. Kwa mfano kwenye jimbo langu mmetuletea bilioni mbili na point juu, mmetupa tena milioni 500 ambayo imetolewa na Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa awamu ya sita kwa kweli mmejitahidi. lakini tunaomba basi tutakapokwenda kukusanya tujitahidi tena mara dufu kwa sababu wananchi wetu wanategemea na wanaamini kwamba pale ambapo tutapeleka fedha za kutosha kwenye miradi tuliyopanga, hiyo ndiyo ahueni na furaha; na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi itatimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata tutakapokwenda mbele ya wananchi tutakwenda kifua mbele kwa sababu tumetekeleza ilani ya 2021/2022 bila shida yoyote na watatuelewa vizuri. Kwahiyo naomba hili la upelekaji wa fedha tuhakikishe kwamba tunajitahidi kama tulivyojitahidi 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kupeleka fedha pia nizungumzie suala la uhaminifu na uhadilifu, kwa maana ya nidhamu katika matumizi. Hili suala la nidhamu na uadilifu katika matumizi ni suala muhimu na nyeti kwa sababu kama tutapeleka fedha lakini bila usimamizi tutakwenda kupata panya wanaotoboa magunia, watatoboa miradi yetu mara tutakapopeleka fedha itakuwa hatujatekeleza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tuhakikishe kwamba tumewazuia panya wasiharibu bajeti hii, tumewazua waharibifu, kwa sababu inashangaza sana na inasikitisha pale ambapo watu wanaofanya wizi, ujambazi, ufisadi na ulafi ni wale watu ambao wanalipwa mishahara, wanakaa lakini bado wanatamaa ya kuharibu bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta mtumishi amepewa gari, ofisi, watumishi, wasaidizi, kila kitu lakini bado anaungana na njama za kufanya ufisadi kwenye maeneo ya miradi naomba.

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji kaka yangu anayechangia kiukweli anaongea ukweli kabisa, kwamba hii bajeti imekaa vizuri sana. Kama haitapata panya wakazitafuna hizo pesa tunazozipitisha hapa Serikali yetu itakuwa juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilikuwa nataka nimpe taarifa tu mchangiaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema, watu hawa ambao ni waharibifu tukiwaachia wakienda kukondesha bajeti hii, bajeti hii ikakonda kwa sababu panya, hatutaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Mawaziri wote, kwa sababu watatelekeza bajeti hii, wahakikishe kwamba bajeti hii haitakonda, haitakondeshwa, ili hatimaye malengo, nia na madhumuni ya kutelekeza ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika sekta za maji, barabara, elimu, afya na miundombinu vyote kwa ujumla viweze kufikiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo panya hawa tukiwaruhusu; na inashangaza, kama nilivyosema, mtu analipwa mishahara lakini bado ni mwizi na fisadi, yeye ndiye anaanzisha timu ya kufanya uhalifu. Ifike mahali sisi wote kwa ujumla wetu tupige vita rushwa, tutosheke na mishahara yetu. Kwa sababu hata ukikusanya dunia nzima, hata ukikusanya mali ngapi utakufa utaacha lakini huku umewatesa wa akina mama, hawana dawa, umewatesa akina mama wajawazito pamoja na wagonjwa wengine wakakosa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali hata milango yote ya ofisi za Serikali milangoni tuweke acha kupokea rushwa, acha kutoa rushwa. Tukienda kule msalani iwepo acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kwenye magari ya Serikali tuweke acha kutoa rushwa acha kupokea rushwa. Kila mlango wa Serikali iweke na popote pale panapotolewa huduma; hata mezani pale kama ni kwa Waziri liwekwe bango linalosema acha rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya pili nizungumzie suala la posho ya madiwani. Ninaishukuru sana Serikali kwa sababu imewakumbuka madiwani wetu na kuwaweka kwenye sehemu ya kulipa posho zao kutoka wizarani moja kwa moja. Hilo ni jambo jema sana na ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita. Hata hivyo kwa mshahara huu wa madiwani bado tunaomba Serikali iendelee kuangalia, kwa sababu kimekuwa ni kilio cha muda mrefu. Diwani huyu ndiye anayehangaika na kila kitu katika kata. Vilevile tusiwasahau wenye viti wa vijiji na vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuyaangalie maeneo hayo kwa sababu nao wanateseka sana, wenye viti wa vitongoji na vijiji na hata watendaji wetu wa vijiji ni wachapakazi kule na tunawakabidhi majukumu ya aina mbalimbali. Sehemu hii Serikali yetu imekaa vizuri sana katika masuala ya utawala, lakini naomba basi ikaangalie maeneo hayo kwa kuwa tumetoa fedha hizo za madiwani, na kama zinalipwa na Serikali Kuu naomba Shilingi 250,000 iliyobaki ikawaangalie wenyeviti wetu wa vijiji, watendaji wetu wa vijiji pamoja na wenyeviti wetu wa vitongoji ili nao waweze kuneemeka na Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri atakapokuwa ku-windup wajaribu kutoa waraka maalum wa kuhakikisha kwamba huu utaratibu wa kuwalipa Maafisa Tarafa iko Serikali Kuu lakini hii ya halmashauri itoe waraka unaosema Watendaji wa Kata walipwe kulingana na waraka huu kwenye vituo vya vitongoji kwenye vituo vya vijiji na Watendaji wa Vijiji. Hii itasaidia sana katika kuhakikisha kwamba utaratibu huo uliopangwa kwenye bajeti hii kwa watumishi wetu hawa wa chini inafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la property tax, kwa maana ya kodi ya majengo. Nilikuwa nasema naipongeza Serikali kwa sababu imekuja na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa kodi hii; na muendelee na huo utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba muangalie sana hizi nyumba za tembe, kwa maana ya nyumba za udongo. Unakuta nyumba nyingine ni ya udongo na ina umeme. Je, nayo ni miongoni mwa zinazoolipa proparty tax? Hilo ni suala ambalo Waziri kama ni miongoni au kama si miongoni basi uhakikishe kwamba umeweka utaratibu wa kufanya analysis ya kutosha ili wananchi wetu wasiumie. Ukusanyaji wa kodi ni muhimu ili bajeti hii iweze kufikiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na kazi iendelee. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhili nisipompongeza sana Waziri na timu yake nzima kwa maana ya Naibu wake pamoja na Wizara yake kwa ujumla ikiongozwa na Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kusema kwamba katika usambazaji wa nishati kwa maana ya umeme Tanzania kwa kweli tumepiga hatua kubwa sana. Ukipita kwenye mapori na maeneo mbalimbali ukiona jinsi ambavyo nguzo zinapita utaona jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi kwa kiwango kikubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani ya usambazaji wa umeme bado tunaendelea kusema tunakwenda kusonga mbele na kuikumbusha Serikali kuendelea kumalizia maeneo ambayo bado. Katika usambazaji wa umeme wakandarasi ambao walikuwa wamepewa kazi hii wengine wamekuwa siyo wazuri sana, siyo wote lakini siyo wazuri sana. Hivyo, Wizara ni vizuri ikaangalia kwa makini sana wakandarasi hawa ambao wamekuwa hawafanyi kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi mkandarasi aliyepewa kazi pale amechimba mashimo kwenye maeneo mengine hajaweka nguzo, amesimamisha nguzo hajaweka waya, maeneo mengine hayajakamilisha miradi kwenye vijiji na na kadhalika. Uchimbaji wa mashimo umewafanya wananchi, ng’ombe na mbuzi kuvunjika miguu. Naomba Wizara chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Kalemani (mchapakazi) afike kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi ili kuweka msukumo katika usambazaji wa umeme kwenye Kata za Bwawani, Nduruma, Kisongo, Musa, Mwandeti, Lingijale, Lemanyata, Kimyaq, Sambasha, Ikiding’a, Oljuroto, Tarakwa, Oturumet, Matebesi, Naroi na Oljoro. (Makofi)

Mheshimiwa Sjpika, kama unavyofahamu Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo ambalo limeweka Jiji la Arusha katikati, kwa hiyo sisi tumezunguka Jiji la Arusha kama yai, wananchi wale wanahamu sana ya umeme. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Kalemani aweze kutembelea na kuweka msukumo wa usambazaji wa umeme kwenye jimbo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la bei ya nguzo. Suala hili limekuwa kizungumkuti kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuwa akijitahidi sana kutumia nguvu kubwa kueleza kwenye mihadhara mbalimbali kwamba usambazaji ni shilingi 27,000 lakini jambo hili TANESCO wanapolitelekeza linakuwa kinyume chake. Sasa inawezekana tunailaumu TANESCO lakini kuna nini huko ndani? Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kufafanua zaidi kupitia waraka maalumu, kama ameandika sijui, lakini kama hajaandika atoe waraka TANESCO kwa maana ya TANESCO mikoa yote Tanzania, umeme wa REA ni shilingi 27,000, je, miradi ya TANESCO yenyewe ni shilingi ngapi, ni shilingi 177,000 au kuna tofauti ili mwisho wa siku wananchi waweze kuelewa gharama hii ya shilingi 27,000 na shilingi 177,000. Suala hili ni kizungumkuti katika utekelezaji, Waziri anatamka lakini utekelezaji unakuwa mgumu labda kuna kitu ndani. Hilo nalo Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia na kulitolea ufafanuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, suala la upandaji wa gesi. Ujio wa gesi umepunguza sana uharibifu wa mazingira na huko vijijini gesi hizi ndogondogo kwa mfano hii ya kilo sita imepanda kutoka shilingi 16,000 hadi shilingi 20,000. Sasa hali hiyo inaenda kutusababishia uharibifu wa mazingira, wananchi watarudi tena kwenye kukata miti na kuharibu mazingira. Naomba pia hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa nini gesi ile ya kilo sita ipande kutoka shilingi 16,000 mpaka shilingi 20,000? Hili nalo ni jambo ambalo Wizara inatakiwa iliangalie kwa makini kwa sababu gesi imesaidia sana katika kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kukatikakatika kwa umeme. Kumekuwepo na tatizo la kukatika kwa umeme, hatukatai kwa sababu mitambo ni mitambo tu lakini pale ambapo umeme unakatika ghafla basi tunaomba Wizara isimamie TANESCO iweze kutoa taarifa kwa wananchi kwamba umeme umekatika kwa muda huu na tunategemea uwake kwa muda fulani au siku tatu au nne. Kukaa kimya au kutowaeleza wananchi umeme umekatika kwa sababu gani na ni kwa nini inaleta wasiwasi na hofu na kurudisha pia maendeleo nyuma. Kuna watu umeme ukikatika dakika moja tu wanapata hasara kubwa sana katika kuendesha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, umeme ni nishati ambayo inahitajika sana kwa Watanzania kwa ajili ya kuleta maendeleo tena maendeleo endelevu. Kwa hiyo, niombe kukatika kwa umeme tuwape taarifa wananchi ili waweze kukaa tayari kujua kwamba kuna nini na baadaye watapata kwa wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia muswada huu. Lakini na mimi niungane na wenzangu kutoa pole sana kwa familia ya ndugu yetu ambaye ametangulia mbele ya haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakwenda moja kwa moja kujielekeza kwenye kuunga mkono muswada huu wa kuweka Kiswahili kitumike kwenye sheria zetu na sababu yenyewe ni kwamba ili lugha yoyote iweze kuwa na uhalali, lazima watumiaji wake wawe ni kwa kiwango kikubwa katika sehemu husika.

Kwa minajili hiyo, Kiswahili Tanzania kinazungumzwa na zaidi ya wazungumzaji asilimia karibu 90; asilimia 10 iliyobaki ndiyo inazungumza hiyo lugha nyingine ya kigeni. Kwa hiyo tayari imeshajihalalisha kwamba Kiswahili ni halali kitumike Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni ufanisi wake, kama tutazungumza lugha ya kigeni na ufanisi wake hauwezi kukaa vizuri miongoni mwa jamii tunayoiongoza, tutakuwa hatujatenda haki.

Lakini pia haki za binadamu zinatutaka pia tuhakikishe wananchi wetu wanapata haki za binadamu dhidi ya mazungumzo, kwa sababu unapozungumza lugha usiyoijua inakuwa ni utata na hatimaye unaathirika. Kwa hiyo, hayo ni mambo ambayo tunatakiwa tuyaangalie…

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, muda wetu umetubana sana, hii itakuwa ni taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Salome Makamba, sekunde 30.

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba sheria ilivyo sasa hivi kabla hatujabadilisha kwenye muswada huu inasema lugha ya Mahakama ni Kiswahili na Kiingereza au vyote viwili.

Kwa hiyo hakuna sehemu inayosema lugha ya Mahakama ni Kiingereza, ni attitude za watu wetu wanao- practice sheria ndio wanaotumia Kiingereza peke yake. Kwa hiyo, nadhani tunatakiwa tubadilishe mtazamo wa watu wanaofanya kazi za sheria kuliko kusema kwamba Kiswahili hakitumiki.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana; Mheshimiwa Noah Mollel, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa hiyo na siipokei kwa sababu pia mtoa taarifa ni tabia zao za kutokuwa na heshima, kwa hiyo nadhani sipokei taarifa hiyo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Noah Mollel, hilo neno la kutokuwa na heshima liondoe halafu umalizie mchango wako.

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nafuta, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee, hizi hofu kwanza kabisa za kusema kwamba Tanzania tunakwenda kuji-isolate siyo kweli kwa sababu Tanzania kama Tanzania lazima tuwe na haki ya kumiliki lugha yetu, hiyo ndiyo sifa yetu, ndiyo itatutangaza duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama wenzangu walivyosema, Hong Kong kwa mfano, wananchi walipopiga kelele Serikali ilikuja na muswada wakasema tunahitaji Kichina kiwekwe kwenye sheria zetu. Mwaka 1995 Jaji wa Kwanza wa Kichina alitoa hukumu ya Kichina.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tarehe 11 Machi, 1996 Mahakama zote nchini China zilitoa hukumu kwa lugha ya Kichina kuanzia makosa yote ya jinai na madai, kwa nini sisi Tanzania tunakuwa na hofu? Kazi hii ya kutumia Kiswahili ilianza muda mrefu. Mwaka 2001 kulikuwa na shauri ambalo lilitolewa la Hamisi Rajab Dibagula dhidi ya Jamhuri, 2001 na lilizungumzwa kwa Kiswahili. Kwa nini tunakuwa na hofu? Pia sheria hii ilibainisha wazi kwamba pale ambapo haki inatakiwa kutendeka, parties kwa maana ya pande mbili zitaamua zitumie lugha gani, sasa tunataka nini? Tunataka kuenzi vya wageni, vya wakoloni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)