Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Innocent Lugha Bashungwa (26 total)

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji ni tatizo kubwa tuseme nchi nzima, lakini hata Karagwe tuna shida sana ya maji. Wakati wana-Karagwe wanasubiri mradi wa Rwakajunju, Serikali ina miradi ya Benki ya Dunia, lakini kote Jimboni hii miradi haijakamilika. Napenda kuiomba Serikali ieleze wananchi wa Karagwe hii miradi itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi ya Benki ya Dunia, tulikuwa na hiyo awamu ya kwanza ya program ambayo imekwisha Disemba tarehe 30. Sasa tunaingia awamu ya pili ya program ya miaka mitano katika kutekeleza vijiji vile ambavyo havikupata awamu ya kwanza na ile miradi ambayo iko inaendelea. Sasa hivi Serikali imeshapata fedha za kuweza kusukuma miradi ya kwanza ile iliyokuwa imeanza ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, azma ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vilivyokuwa ndani ya program tunakamilisha ili wananchi wetu waweze kupata maji.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, lakini kwa upande wa kahawa, Jimbo la Karagwe tunalima kahawa sana na zao la kahawa bado lina fursa kubwa sana kuwainua kiuchumi wakulima wa kahawa na uchumi wa nchi kwa ujumla lakini mikopo ya TIB imekuwa ni kidogo mno kwenda kwenye kukopesha walimaji wa kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu ni kama ifuatavyo: Kwa vile miche ya kahawa ni ya zamani sana, imepandwa toka enzi za wakoloni na mababu zetu, je, Benki ya Kilimo ina mpango gani wa kuwakopesha wakulima wa kahawa pesa ile waweze kununua miche wakiwemo vijana ambao wana tatizo la ajira na kama miche ikipatikana wanaweza wakajikita kwenye kilimo cha kahawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile kabla ya kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo, TIB ilikuwa ikitoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kupitia Dirisha la Kilimo, kwa nini hii portfolio isitoke TIB ikaenda Benki ya Kilimo ili hii fedha shilingi bilioni 58.8 itumiwe na Benki ya Kilimo kukopesha wakulima wa Tanzania?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Innocent Bashungwa kwa kufuatilia suala la miche ya kahawa na kusema kuwa imechakaa na kwenye hotuba yangu nilisema katika Wilaya na Mikoa inayolima miche ya kahawa wajitahidi kupanda miche 5,000 kwa kila hekari ili kuweza kurejesha heshima ya zao hilo la kahawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ombi lake hili la kuangalia uwezekano wa vijana kukopeshwa fedha kwa ajili ya kupanda miche mipya, niseme tu nitaielekeza Benki ya Kilimo wawasiliane na Mheshimiwa Mbunge na wapangilie safari ya kuweza kufika huko ili wakaangalie mazingira sambamba na vile ambavyo tulishakubaliana watafika pia Kitulo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kukopesha uzalishaji wa mitamba ili wananchi waweze kupata mbegu za mazao haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge na naelekeza uwasiliane na Benki ya Kilimo ili waweze kuwakopesha vijana wapande miche mipya ili kurejesha heshima ya zao hilo la kahawa. Zao la kahawa litaendelea tu kama tutalipokea kutoka kwa wazee wetu na sisi vijana tukaona ni zao la fursa kwa ajira na kwa ajili ya biashara.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wananchi wa Karagwe tunamkumbuka Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa push-up za kihistoria alizozipiga pale Kayanga. Je, Serikali mnaonaje kama mkitusaidia kujenga uwanja wa Wilaya pale Kayanga ili tuweze kumuenzi Rais wetu kwa ule ukakamavu alioonyesha kwa vijana wa Karagwe? Nashukuru sana
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba push-up kwa mara ya kwanza zilipigwa kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge anasema, hii ilithibitisha uwezo wa Rais John Pombe Magufuli wa afya yake, lakini pia ulionyesha kwamba Serikali atakayoiunda ni Serikali ya Hapa Kazi Tu tofauti na wenzetu mgombea wao nadhani hiyo kazi ilikuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara kwa kushirikana na Halmashauri anakotoka Mbunge tunaweze kuzungumza kuona namna ya kushauriana kuweka kumbukumbu hii muhimu ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanywa. Kwa hiyo, Wizara na Halmashauri ambapo anatoka Mbunge tutakaa pamoja tuzungumze tuone namna ya kuweka hii kumbukumbu muhimu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Jimbo la Mkuranga zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Naishukuru Serikali kwa kutuunganisha Jimbo la Karagwe na Jimbo la Kyerwa kwa kuweka mpango wa kujenga kwa lami barabara ya Mugakolongo kwenda Mulongo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri akisaidie Kijiji cha Rwambaizi, barabara imekwepa kijiji na kama mnavyojua barabara huchochea maendeleo. Nipende kumuomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie barabara ya Mgakolongo kwenda Mulongo, ipite kwenye kijiji cha Rwambaizi, ili wananchi wangu wa hicho kijiji waweze kupata maendeleo yatakayokuja na ujenzi wa barabara hiyo la lami, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri barabara anayoitaja ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na kwa mwaka 2016/2017 anafahamu kwamba imetengewa fedha. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Bashungwa, Wizara yetu dhamana yake ni kutekeleza ahadi za ilani ya Chama cha Mapinduzi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha barabara hii katika miaka hii mitano, inakamilika kujengwa kwa lami.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kata za Igulwa, Kanoni, Kituntu, Ihanda na Chonyonyo, zina shida kubwa sana ya maji. Kutokana na shida hii, Serikali iliahidi kuchimba mabwawa katika hizi Kata ili kuwasaidia wananchi kuondokana na adha ya maji. Je, Serikali itachimba lini haya mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashungwa ameuliza kwamba, ni lini Serikali; kuna Kata za Igulwa pamoja na Kata zingine ambazo zina uhaba wa maji, lakini anapenda kujua ni lini basi, Serikali itachimba mabwawa au kufanya utafiti wa kupata ni chanzo kipi cha maji, ambacho kinaweza kikatosheleza Kata hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tumeagiza kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri wafanye utafiti wa mabwawa, ambayo wanafikiri yanaweza yakachimbwa katika maeneo yao ili tafiti hizo ziwasilishwe Wizara ya Maji ili Wizara ya Maji iangalie uwezekano wa kutenga fedha katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 kutegemea na jinsi watakavyokamilisha hizo study. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bashungwa nikuhakikishie na naomba na wewe kama Diwani, basi ushirikiane na Madiwani wenzako katika Halmashauri yako ya Karagwe ili hatua hii, muwafahamishe watalaam waweze kuifanya.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto za Morogoro Kusini zinafanana na Changamoto za Jimbo la Karagwe. Katika Hospitali ya DDH Nyakahanga tuna tatizo kubwa la upungufu wa madawa, vifaa tiba na Wauguzi.
Mheshimiwa Naibu Spka, swali langu ni je, Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo kaka yangu, anaweza kuambatana nami baada ya Bunge hili kwenda kusaidiana nami kutatua changamoto za Hospitali ya DDH ya Nyakahanga
pamoja na kuanza mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya ukizingatia DDH ya Nyakahanga inahudumia Wilaya mbili; Karagwe na Kyerwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba miongoni mwa Wabunge ambao walikuwa wakinisumbua sana katika Sekta ya Afya ni Mbunge huyu wa Karagwe. Ni kweli kabisa, naomba niseme kuwa, pale ana Daktari wake anaitwa Dkt. Sobo ambaye ni kijana mwenzake; naamini kwamba watashirikiana vya kutosha kuhakikisha mchakato wa Jimbo lile unakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, commitment yetu ni kwamba, katika kipindi hiki nitakuwa na ziara katika Mikoa yetu mitano nikianzia Mkoa wa Tanga, Lindi, Pwani Morogoro pamoja na Mtwara, lakini nitapita Ruvuma. Vile vile Mkoa wa Kagera niliupa kipaumbele kwa zoezi maalum katika kutembelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani kwamba kabla ya Bunge lijalo, basi nitajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo tufike eneo lile kubaini changamoto za wananchi wa eneo lile la Jimbo la Karagwe ili mwisho wa siku wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni commitment ya Serikali, tutajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo, hasa nikijua nawe ni mpiganaji mkubwa katika Sekta ya Afya katika eneo lako, tutasukuma kwa kadiri iwezekanavyo wananchi pale wapate huduma bora.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa Serikali wa kuhamisha nyumba zilizokuwa chini ya Halmashauri kwenda Serikali Kuu umeacha watumishi katika Halmashauri ya Karagwe bila makazi, takribani kaya za Watumishi 60 hivi sasa hazina makazi kwa sababu Serikali Kuu imechukua nyumba ambazo zilikuwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Je, Wizara haioni kwamba inabidi iwasaidie watumishi hawa kwa kuiomba NHC ishirikiane na
Halmashauri, Halmashauri tunaweza tukawapa eneo la kujenga nyumba nafuu kwa ajili ya watumishi hawa? Nashukuru
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nyumba zilizokuwa awali za Wizara ya TAMISEMI baadae zikaenda NHC sasa zimerudishwa Serikali Kuu. Hivi sasa wataalam wangu na Wataalam wa Wizara ya Ujenzi wanapima maeneo hayo ili yamilikishwe kwa Serikali Kuu. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba mpya ili ziweze kuboresha mandhari ya Miji, kwa sababu nyumba hizi tangu zimemilikiwa na Serikali za Mitaa na NHC ingawa maeneo yale ni mijini lakini nyumba zimekuwa chakavu na hivyo
zinaleta mandhari mbaya katika miji. Hivyo, lengo la Serikali ni kuzijenga upya.
Pili, kuchukua zile nyumba kuziweka Serikali Kuu hakumaanishi kwamba wale wanaokaa katika nyumba zile sasa wafukuzwe. Mheshimiwa Rais ameagiza kwamba zoezi hili linakoendelea kupima mpaka itakapofikia zamu ya kujenga nyumba mpya katika maeneo hayo, waliomo wanaopanga sasa wabaki katika nyumba hizo wasibughudhiwe na wasifukuzwe. Whether ni watumishi wa leo au watumishi wa zamani wenye mikataba ya kukaa kwenye nyumba hizo wabaki wale wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale wa Karagwe hao hawapaswi kutoka, wakae humo humo whether ni watumishi au wananchi wa kawaida. Nyumba hizi ingawa si lazima wakae watumishi tu lakini kuna sehemu nyingine watumishi wa Serikali wanakaa na wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, waliomo kwenye nyumba hizo wasifukuzwe. Huko Karagwe kama wananisikia wanafikiri kwamba hao wafanyakazi wanatakiwa kufukuzwa hapana. Tunahaulisha tu utaratibu wa umiliki wa Serikali lakini hatuwaondoi wapangaji.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Hata Wilaya ya Karagwe tuna vivutio vingi vya malikale likiwemo eneo ambalo Chief Rumanyika alikaa. Je, Wizara imeweka vivutio vya malikale hizi kwenye orodha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kivutio kinachohusu makazi ya Chifu Rumanyika ni moja tu kati ya vivutio vinavyohusu Machifu wetu wote nchi nzima kila eneo na kila Wilaya. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kama nilivyoeleza hapo awali kwamba ni kuviorodhesha, kuvisajili, kuvikagua na kuona ubora wake na hatimae kuviuza kwa kuangalia sifa zake.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayofanya. Nina swali kuhusu mradi wa Rwakajunju namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri awaambie akinamama wa Karagwe ni lini mradi wa Rwakajunju utatekelezwa ili kuwatua ndoo kichwani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwatulize wananchi wa jimbo la Mheshimiwa Mbunge kwamba Mradi wa Maji wa Rwakajunju unatekelezwa. Mradi wa maji wa Rwakajunju una finacing ya uhakikika kutoka Serikali ya India na tunasubiri sasa hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha asaini mkataba wa fedha. Tayari Wizara tumeshaanza kutafuta Wahandisi Washauri ambao wanahakikisha wanaweka document vizuri. Yule Mhandisi anayefanya usanifu wa mradi huu anakaribia kukamilisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana, nina imani katika mwaka huu fedha tuliouanza juzi 2017/2018 tutaanza utekelezaji wa Mradi wa Rwakajunju ili tuweze kuwatua wananchi ndoo kichwani.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana ambao wanaajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kuzungushwa pale wanapoenda kwenye Mifuko ya Pensheni kudai mafao yao ili waweze kuyatumia kama mitaji ya kujiajiri. Kwa mfano, kule Karagwe Kampuni ya Ujenzi ya Chico iliajiri vijana kwa utaratibu wa mikataba ya vibarua, mpaka hivi sasa wanazungushwa vijana hawa.
Je, Serikali inawasaidiaje vijana hawa kudai mafao
yao ili waweze kutumia hela hii kama mitaji ya kujiajiri?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi ya pekee sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu amekuwa mstari wa mbele sana kufuatilia haki za wananchi katika Jimbo lake na hilo ni jambo jema.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tumekuwa na malalamiko ya namna moja ama nyingine ya wafanyakazi wa namna hiyo ambao wamekuwa wakiajiriwa kwa mikataba, mikataba yao inapoisha walizoea kuwa na fao ambalo si fao sahihi lakini lililokuwa linaitwa fao la kujitoa. Baada ya kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 11, lakini kupitia Sera ya Hifadhi ya Jamii katika nchi yetu na sheria tulizonazo, Serikali pamoja na wafanyakazi wenyewe na vyama vya wafanyakazi, tumekubaliana sasa kuna haja ya kuangalia namna nzuri ya kuwasaidia wafanyakazi wote ambao wamekuwa wakikumbwa na jambo hilo kwa kuanzisha fao lingine ambalo litaitwa ni Bima ya kukosa ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo tumeshaanza kuifanya vizuri kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, niwaombe wafanyakazi wote nchini ambao walikuwa wanaelekea katika fao hilo wavute subira ili matakwa ya kisheria yafanyiwe kazi na ndipo fao hilo litaanza kutolewa kwa mujibu wa sheria ambayo itakuwa imetungwa na Bunge.
Pia ni maagizo ya Mheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi alipokuwa pale Moshi ameendelea kusisitiza kwamba sasa tushughulikie suala hilo na liweze kufungwa kisheria na Wafanyakazi waweze kupata haki zao. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mpango wa kupandisha watumishi madaraja wale wanaostahili lakini kuna changamoto ya wale watumishi ambao wanapandishwa madaraja mishahara huwa inachelewa ku-reflect lile daraja ambalo amepandishwa. Je, ni nini maelezo ya Serikali kuhusu suala hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba ni kweli wako baadhi ya Maafisa Utumishi ambao wamekuwa hawatekelezi wajibu wao kama inavyopaswa na wamekuwa wakichelewesha kurekebisha mishahara katika mfumo wetu wa ulipaji wa malipo ya mshahara wa LAWSON. Nipende kutoa tamko hapa na maelekezo kwa mara nyingine tena, tulishachukua hatua katika Halmashauri ya Bagamoyo, Kilombero, Temeke na nyingine nyingi, hatutamvumilia Afisa Utumishi yeyote au mhusika yeyote katika mamlaka ya ajira ambaye atachelewesha kurekebisha malipo ya mshahara baada ya mtumishi kupandishwa daraja.
Nipende kusema sasa hivi tumeenda mbali itafika wakati tutaanza kuwafungia hata Wakurugenzi wa Halmashauri mishahara yao ili na wenyewe waweze kuona uchungu wa kuchelewesha upandishwaji wa madaraja wa watumishi hao.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Pia katika Wilaya ya Karagwe kuna wahanga ambao wameathirika na wanyama waharibifu hasa tembo na viboko katika kata za Kihanga, Rugu, Nyakasimbi, Nyakabanga, Nyakakika na Bwelanyange, lakini pamoja na kushindwa kuwapa kifuta machozi wananchi hawa, pia vijiji katika hizi kata vinapakana na Pori la Akiba la Kimisi na Burigi na kuna asilimia ambayo inatakiwa kutoka kwenye mapato ya hifadhi kwenda kwenye vijiji ili kuwasaidia katika shughuli za maendeleo. Tumetuma madai katika Wizara kwa muda mrefu, lakini hatujawahi kupata hii fidia ili wananchi hawa nao wafaidike.
Je, ni lini Serikali itatoa kifuta machozi hicho pamoja na yale mapato? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nilisema katika maombi ambayo yameifikia Wizara kwa ajili ya uhakiki, kiwango cha jumla ya fedha takribani shilingi milioni 500 pekee ndicho ambacho kimebaki bila kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuangalia kwenye orodha ile ya wale ambao wanafanya jumla ya madai yawe shilingi milioni 500 nione kama wananchi wanaolizungumzia ni sehemu ya madai hayo. Kwa hiyo, ikiwa hivyo ndivyo, tumesema fedha hizi zinalipwa ndani ya mwaka wa fedha huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa siyo miongoni mwa wale ambao jumla ya fedha shilingi milioni 500 zinadaiwa, basi itakuwa wako katika mchakato; wale ambao bado taratibu hazijakamilika kwenye ngazi za Halmashauri na Mikoa, kwa hiyo, tutakwenda kuhimiza tu ifanyike haraka ili madai hayo yaweze kuifikia Wizara yawekwe kwenye orodha halafu tuweke utaratibu wa ratiba ya kuweza kuyalipa.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kwenye taarifa ya habari ITV kulikuwa kuna kauli kwamba kuna uingizaji wa mbegu fake nchini. Kama kauli hii ina ukweli ni hatari sana kwani inamdhulumu mkulima ananunua mbegu akidhani ni mbegu yenye ubora lakini mbegu hii inakuwa ni feki matokeo yake anapanda havuni anachokitegemea.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kauli hii ambayo ilitoka ITV jana usiku kwenye taarifa ya habari? Nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi nimeiona hiyo kauli au statement iliyotolewa na kituo cha televisheni cha ITV kwamba nilikiri nchini hapa mbegu inayotumika kwa wakulima ni mbegu fake. Naomba nitoe ufafanuzi wa hilo jambo kwamba sikusema hivyo na jambo hilo lililotangazwa halina ukweli wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokisema ni kwamba wakulima wengi nchini bado wanatumia mbegu hafifu na kwa hivyo uzalishaji wao bado uko duni kwa sababu ya matumizi ya mbegu hizo na si kusema kwamba wanatumia mbegu feki. Kwa hivyo, niwaombe tu wenzetu wa kituo hicho cha televisheni wafanye hayo marekebisho ya kauli yangu. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema kwamba Serikali inachokisema ni kwamba bado yako matumizi ya mbegu hafifu kwa wingi hapa nchini na hiyo inatusababishia uzalishaji hafifu na si vinginevyo.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na kwamba wananchi wana haki ya kupata huduma ya watumishi, hasa walimu, wauguzi na watendaji wa vijiji na kata, pia jitihada nzuri ya Serikali inayoifanya ya kupeleka fedha za maendeleo vijijini inahitaji watumishi hawa waweze kusimamia miradi hii. Kwa upande wa Karagwe kuna shortage kubwa ya Walimu wasiopungua 850, kuna shortage kubwa ya wauguzi.
Je, nini tamko la Serikali, maana kila mwaka wa fedha Serikali inasema itapanga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuhakikisha tunakuwa na watumishi wa kutosha. Nini tamko la Serikali kuhusu hii shortage ya watumishi ya sasa hususan Wilaya ya Karagwe? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa walimu na matabibu na wataalam wa idara ya afya na imekuwa ikichukua hatua kuona kwamba tunaziba mapengo haya. Kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, wakati tunaanza sekondari zetu za kata uhaba wa walimu ulikuwa mkubwa sana, lakini Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwepo walimu wa kutosha imefanya jitihada ya kuajiri walimu wengi na hivi sasa katika shule zetu za sekondari, hali ya walimu imekuwa nafuu ukiondoa labda mapungufu makubwa yaliyopo katika upande wa walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi ya kudumu ninamuahidi tu kwamba Serikali itaendelea na kasi ileile ya kuajiri watumishi wa afya na elimu ili wananchi wetu wapate huduma ya afya bora, ili watoto wetu wapate elimu inayojitosheleza. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto za Jimbo la Bukene zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kuweka lami barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Benako - Ngara na barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Murongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango hii mizuri ya Serikali wananchi wanaoishi katika barabara hizi wamesubiri fidia kwa muda mrefu, je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wa Karagwe wanaopakana na barabara ya Karagwe - Benako na Mugakorongo - Murongo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amefuatilia sana barabara za Karagwe na anafahamu kwamba ziko barabara nyingi ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi ya jirani ambazo ziko kwenye mpango wa ujenzi wa lami. Hii ni pamoja na juhudi zake Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana na na sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba wananchi wa Karagwe wanapata huduma hii ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la fidia, tunategemea tutakapopata fedha tutaweza kulipa mara moja. Kwa hiyo, namuomba tu Mheshimiwa Mbunge labda baada ya kikao hiki tuwasiliane ili tuzungumze ofisini tuweze kuona hatua gani tumefikia ili aweze pia kuwapa taarifa wananchi wa Karagwe juhudi ambazo tumefikia upande wa Serikali. Kwa hiyo, tuonane tutalizungumza suala hili.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kuna mgogoro kati ya Pori la Akiba la Kimisi na maeneo ya Rweizinga – Mguruka katika Kata ya Bwelanyange, mwaka jana Bunge liliielekeza Serikali iende katika hayo maeneo na kutatua migogoro hii, lakini mpaka hivi sasa Serikali haijafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua ni lini Mheshimiwa Waziri utaambatana na mimi ili tuende kwenye Kata ya Bwelanyange maeneo ya Rweizinga na Mguruka ili kushirikisha wananchi katika kuweka mipaka mipya kati ya pori la Akiba la Kimisi na Kata ya Bwelanyange? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika maeneo aliyoyataja kulikuwa kuna matatizo na wananchi walikuwa na malalamiko kuhusu mipaka na naomba nimhakikishie kwamba niko tayari wakati wowote mwezi wa Machi, mwaka huu nitatembelea katika Mkoa wa Kagera na tutakapokuwa huko basi tutapata nafasi ya kwenda kupitia na kuongea na wananchi juu ya mipaka hiyo yote aliyoitaja katika maeneo ya Bwelanyange na maeneo mengine yote aliyoyataja.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Karagwe tuna kituo cha ufundi stadi cha KVTC Kayanga. Serikali iliandaa mchoro wa kupanua hiki chuo kwa muda mrefu sasa miaka mingi. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kupanua hiki chuo cha KVTC Kayanga.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali imetenga fedha za kufanya ukarabati wa vyuo viwili. Chuo cha Ufundi Stadi cha Korogwe pamoja na Karagwe kwa hiyo fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, lakini kabla ya kuuliza maswali haya, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali kwa utaratibu uliowekwa sasa wa kuhakikisha hakuna mwalimu anahama mpaka stahiki zake zinalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo; naishukuru Serikali imeongeza annual increment kwa walimu lakini ni lini Serikali itawapandishia mishahara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa nini walimu wanachukua muda mrefu kupandishwa madaraja? Kuna walimu tangu mwaka 2012 mapaka hivi sasa walitakiwa wawe wamepandishwa zaidi ya mara tatu lakini mpaka sasa walimu hawa hawajapandishwa daraja hata mara moja. Je, ni nini majibu ya Serikali? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kazi anazozifanya ikiwemo ushauri wa mara kwa mara anaoutoa kwa Serikali na sisi tunaupokea na pongezi alizotoa kwa Mheshimiwa Rais, tutamfikishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameshukuru kuhusu annual increment, sasa ameuliza ni lini Serikali itapandisha mishahara. Utaratibu huu ambao ulikuwa umesimama kwa kipindi kifupi cha miaka kama miwili hivi kupisha uhakiki wa watumishi, zoezi ambalo limefanywa kwa umahiri na weledi mkubwa, baada ya kuwa tumelikamilisha sasa tutaingia kwenye awamu ambayo tutaboresha maslahi ya watumishi ikiwemo mishahara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu walimu ambao hawajapandishwa daraja kwa muda mrefu. Mimi napenda nikiri kwamba Serikali haijapandisha daraja kuanzia kipindi cha mwaka 2016 hadi 2017, lakini kuanzia mwaka huu wa fedha, matayarisho yanaendelea huko mengi kwa ajili ya kuwapandisha madaraja ikiwemo kuwapandisha wale ambao walistahili kupandishwa tarehe 01 Julai, 2016 na wale ambao walistahili kupandishwa moja mwezi wa saba mwaka 2017 watapandishwa kwa pamoja kwa mserereko. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, na pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana kaka yangu, Mheshimiwa Selemani Jafo na Dada Jenista Mhagama. Baada ya kufika Karagwe na kukuta wilaya ambayo ina watu takribani 360,000 ina Kituo cha Afya kimoja cha Serikali waliweka nguvu na Serikali sasa imetusaidia tumekamilisha hicho Kituo cha Afya cha Kayanga, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa vile Wilaya ya Karagwe ina Kituo cha Afya kimoja cha Serikali, na hivi sasa naishukuru TAMISEMI tunaenda kukamilisha Kituo cha Afya cha Nyakayanja, mnaonaje wakati mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya unaendelea mtupe angalau vituo vya afya viwili ili ku-balance jiografia ya Karagwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa TAMISEMI na Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri, mnaonaje mkae na development partners kwa sababu Kamati ya Huduma za Jamii inaonesha kwamba kuna Wilaya 67 katika nchi yetu ambazo bado hazina Hospitali za Wilaya. Sasa kwa sababu Serikali inafanya kazi nzuri ya kutoa huduma mnaonaje mkae na development partners ili mtengeneze proposal ambayo itatusaidia kukamilisha ujenzi wa Hospitali 67 za Wilaya? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza ndugu yangu, Mheshimiwa Bashungwa kwa jinsi ambavyo anapigana katika jimbo lake kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata huduma ya afya iliyo bora. Katika maelezo yake anaongelea kwamba kuna kituo cha afya kimoja, ni kiu yake kwamba vituo vya afya vingeongezeka walau viwili tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa katika maeneo yote na kwa kufuata uwiano sawia. Kwa hiyo, katika awamu inayokuja naomba nimhakikishie kwamba walau tutahakikisha kwamba kituo kingine cha afya kinapelekwa kule haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anauliza uwezekano wa Serikali kushirikiana na development partners katika kuhakikisha kwamba tunaenda kumaliza tatizo la ujenzi wa Hospitali za Wilaya. Ni nia ya Serikali na milango iko wazi kwa yeyote yule ambaye ana nia njema ya kusaidia Serikali katika ujenzi wa Hospitali za Wilaya, tunamkaribisha, ilimradi katika yale masharti ambayo yatakuwa si ya kudhalilisha nchi yetu, sisi kama Serikali tuko tayari.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuja na utaratibu mpya wa kutoa huduma hii kwa wananchi kupitia NSSF kwa kushirikiana na Azania Bank. Hii ni mara ya pili nauliza hili swali katika Bunge hili la Kumi na Moja kwa sababu ni jambo mahususi. Ili jamii yoyote iweze kutoka kwenye umasikini, lazima kuwe kuna kitu kinaitwa social safety net na huu mpango ulikuwa mzuri kwa sababu katika huduma hii wananchi wangenufaika na pensheni ya uzeeni, pensheni ya ulemavu, pensheni ya urithi, mafao ya uzazi, mafao ya mazishi, mafao ya matibabu na mikopo ya muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuiomba Serikali iwaambie wananchi wa Karagwe, je, tutegemee lini NSSF na Azania Bank watakuja Karagwe ili wale wananchi ambao walitoa ule mchango wa shilingi 20,000 wakasubiri huduma kwa muda mrefu, wategemee wataipata lini? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inaonaje kufanya pilot study kuanzia Karagwe na sehemu nyingine ili tuone namna ambayo tunaweza tukaleta social safety net along side, jitihada nzuri ya Serikali inayoendelea kutupeleka kwenye uchumi wa kati? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anauliza ni lini tutakwenda Karagwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba mikopo hii ilisitishwa kwa sababu mbalimbali ambazo niliziainisha pale juu, mojawapo ikiwa ni kwamba fedha nyingi ambazo zilitolewa hazikurejeshwa kwa wakati na hivyo kupelekea Bodi ya NSSF kukaa upya na kutathmini zoezi zima la utoaji wa mikopo na hivyo, baada ya kujiridhisha na utaratibu huu mpya, sasa shughuli ya utoaji wa mikopo itaanza rasmi kuanzia tarehe 1 Julai, 2017 na ninaamini pia wananchi wa Wilaya ya Karagwe na wenyewe watafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuliweka hili sawa, katika mpango huu wa utoaji wa mikopo kupitia NSSF unawalenga wale wote ambao ni wanachama wa NSSF. Kwa hiyo, namwondoa hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tarehe 1 Julai, 2017 zoezi hili litaanza upya kushirikiana na Benki ya Azania.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu masuala ya pilot study ya social safety net, tumepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge na tutayafanyia kazi ili tuone namna ya kuweza kuwasaidia Watanzania wengi zaidi kupata fursa ya kupata mikopo kupitia katika NSSF.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapokea ushauri wake na tunamshukuru sana kwa ufuatiliaji na nimwahidi tu kwamba haya aliyoyasema, basi nasi tutashirikiana na wenzetu wa NSSF kuona Watanzania wengi zaidi wananufaika kupitia mikopo hii ya NSSF.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyeki, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kirefu cha LUKU ni Lipia Umeme Kadri Utumiavyo. Kwenye ving’amuzi kwa nini Serikali isikae na watoa huduma ili mtumiaji alipie kadri anavyotumia badala ya kulipia kwa mwezi awe ametumia au hajatumia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya makampuni yanayotoa huduma za cable kwa ufupi huwa yanafanya biashara na huwa yanalenga katika kupata faida. Nimhakikishie Mheshimiwa kwamba tumelipokea wazo lake hilo na tutalifanyia kazi kama Serikali tuone namna nzuri ya kulitekeleza.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nataka kujua kutoka Serikalini ni lini Walimu waliohamishwa kutoka shule za sekondari kwenda shule za msingi watalipwa stahiki zao. Kule Karagwe kuna walimu 131 mpaka hivi sasa wanasubiri stahiki zao. Serikali ilitoa shilingi milioni 52 na hela ambayo inayohitajika ni shilingi milioni 430. Sasa nataka kusikia kutoka Serikalini, walimu hawa mnawaambia nini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kusisitiza kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kuanzia mwezi wa pili kwamba uhamishaji wa watumishi usifanyike hadi pale kunapokuwa na fedha za kuwalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna walimu ambao walikuwa tayari wakati huo tamko linatolewa walikuwa wameshahamishwa na ni wengi sio wachache; na kwa sababu walikuwa wameshahamishwa haiwezekani tena kuwarudisha kwenye vituo vyao vya zamani kwa sababu tayari wameshahama na wengine tayari walikuwa wameshapewa baadhi ya fedha na Halmashauri kwa ajili ya kujikimu. Sisi tunawaomba walimu wote wenye stahiki za kulipwa stahili basi waweze kuwa na subira unapoanza mwaka ujao wa fedha kwa bajeti mpya tutahakikisha wamelipwa stahili zao.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwenye miji 17 ikiwemo Wilaya ya Karagwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwa vile Serikali imeshapata fedha ni lini Mradi wa Rwakajunju utaanza? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kuwa kufuatilia kwake kuhusiana na fedha kutoka Serikali ya India mkopo nafuu. Katika huo mkopo pia na yeye ana kiasi cha fedha kwa ajili ya Mradi wa Rwakajunju.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu kwa ufupi kabisa, utekelezaji wa kutandaza mabomba katika eneo lake la Rwakajunju na kujenga matenki unaanza katika mwaka ujao wa fedha.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Karagwe ina idadi ya watu wasiopungua 350,000 lakini tuna A Level moja tu ya Bugene Sekondari na haina maktaba hata moja, lakini pia ina upungufu wa madarasa yasiyopungua 17. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili yuko tayari kuambatana na mimi akajionee hali ilivyokuwa mbaya pale Bugene Sekondari? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bachungwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ni kama amewahisha shughuli kwa sababu swali linalofuata linahusiana vidato vya tano na sita. Hata hivyo, mimi sina shida niko tayari kwenda naye jimboni kwake, kuna maeneo maarufu sana nataka nifike kule kama Chamchuzi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba sina shida na kwenda kwa hiyo tutaongea tuone umuhimu wa kufanya hivyo.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za miundombinu katika hifadhi ya Serengeti zinafanana na changamoto za Hifadhi mpya ya Kimisi na Burigi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka miundombinu katika hifadhi mpya ya Kimisi na Burigi ili hifadhi hii iweze kuchangia mapato katika Halmashauri zetu za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Kagera pamoja na kuchangia pato la Taifa?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na mimi kwenda kwenye Kata za Bweranyange, Rugu, Nyakasimbi, Nyakabanga na Nyakakika ili kutatua migogoro ya mipaka kati ya vijiji kwenye Kata hizi na Hifadhi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wabunge wa Mkoa wa Kagera kwa jinsi ambavyo wameshirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yale yanapandishwa hadhi na sasa Burigi na Kimisi yatakuwa ni mojawapo ya Hifadhi za Taifa. Kwa hiyo, itakuwa ni hadhi ya juu kabisa ya uhifadhi katika nchi yetu. Kwa kweli hongereni sana.
Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kupandisha hadhi maeneo hayo, hatua inayofuata sasa ni kuhakikisha kwamba miundombinu ya maeneo yote yale inaimarishwa, barabara zipitike wakati wote ili kusudi watalii waweze kutembelea katika yale maeneo na Serikali iweze kupata fedha nyingi zinazotokana na mapato ya utalii. Kwa hiyo, hilo litafanyika.
Swali la pili, kuhusu kuambatana naye kwenda katika maeneo hayo, naomba nimhakikishie tu kwamba mara baada ya Mkutano huu wa Bunge tutaambatana pamoja, kwa sababu tunataka kwenda kuangalia sasa baada ya kupandisha hadhi mapori yetu yote yale matano, tuone je, nini kinatakiwa kufanyika? Tufanyeje kuhakikisha kwamba utalii sasa unakua katika ile Kanda ya Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hilo lote, tutalifanya vizuri kabisa na ninaomba tushirikiane ili tuweze kufanyakazi vizuri zaidi.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Naibu Waziri anafanya kazi nzuri, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa butura ulikuwa unamsaidia sana mkulima wa kahawa Mkoa wa Kagera kupunguza ukali wa maisha wakati anasubiri kuvuna kahawa shambani. Je, Serikali imejipangaje kumsaidia huyu mkulima baada ya kuzuia uuzaji wa butura? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, butura ni mfumo ambao wakulima wamekuwa wanauza mazao kabla hawajavuna na ni mfumo ambao umewanyonya kwa miaka mingi. Ndiyo, walikuwa wanapata fedha lakini fedha wanayopata hailingani na thamani ya mazao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ni mfumo ambao sasa hivi Serikali inahakikisha kwamba hautaendelea. Badala yake Vyama vya Ushirika vimeshawishiwa na tunavisaidia kuweka utaratibu ambao utakuwa unaweza kuwawezesha wakulima wenye shida ndogondogo badala ya kuuza mazao kwa bei za chini sana ambazo wananyonywa.