Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Innocent Lugha Bashungwa (25 total)

MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali yasiyokuwa na afya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka jana wananchi wamekuwa wakilalamikia kuhusu suala la dawa zinazoua wadudu. Mwaka huu Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba tunapata dawa ambazo zinaua wadudu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kumekuwa na changamoto kipindi cha kugawa dawa za kuua wadudu kwamba mkulima ambaye amelima na akatupia mahindi kidogo hapewi dawa badala yake anaambiwa alipie dawa hizo wakati mMkulima ambaye hajachanganya na zao lolote anapewa dawa bure. Ni kwa nini Serikali imekuwa ikianza na adhabu kwa wananchi badala ya kutoa elimu ndiyo ianze kuwaadhibu wananchi? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Gimbi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Gimbi anasema viuatilifu ambavyo wamekuwa wakipewa wakulima haviuwi wadudu. Azma ya Serikali ni kuhakikisha viuatilifu vinavyoingizwa nchini vinaua wadudu kama inavyotakiwa. Tayari Serikali kupitia Taasisi ya Kudhibiti Viuatilifu nchini tumewaelekeza kuhakikisha viuatilifu vinavyoingizwa nchini, Sheria ya Udhibiti Ubora wa Viuatilifu unazingatiwa. Mimi katika ziara zangu nimehakikisha viuatilifu vinavyoingizwa kwa msimu huu wa pamba wa mwaka wa 2018/2019 vinazingatia Sheria ya Udhibiti Ubora wa Viuatilifu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko makini na msimu huu wa pamba tutahakikisha viuatilifu vyote vinavyoingizwa nchini vinafaa kwa ajili ya kuua wadudu. Sambamba na hili, Wizara imeelekeza Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na taasisi nyingine ndani ya Wizara kutoa elimu kwa wakulima ili wakulima wetu wajue namna bora ya kutumia hivi viuatilifu kuweza kupata matarajio ya kuua wadudu kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nimshukuru kwanza Naibu Waziri wa Kilimo, Ndugu yangu Bashungwa kwa uadilifu wako, nadhani Mungu atakusaidia utafika unakoenda. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza la kwanza, na hili niliseme wazi kwa Waziri aliyopo na wewe mwenyewe, na kwa Wabunge wote nadhani unalijua hili, tatizo kubwa la pamba ni mambo mawili tu, la kwanza ni bei ya pamba, la pili ni usambazaji wa pembejeo kwa wakati ambao haufai.

Mheshimiwa Spika, suala la bei, naomba kujua kupata ufafanuzi, ni kwa nini sasa Serikali isitafute masoko ya ndani na masoko ya nje kwa wakati muafaka kwa msimu unaofaa, ili Wakulima wa pamba wapate bei nzuri ya kutosha?

Swali la pili kwa kuwa mwaka jana kwa msimu 2018/ 2019 Serikali ilikuja hapa Bungeni ikatuomba wakate shilingi mia kwa kilo ya pamba kwa wakulima, na lengo lilikuwa kupunguza au kufuta kabisa kero ya usambazaji wa mbegu za pamba au madawa kwa wakati muafaka, nini kimetokea mpaka leo Wakulima wa pamba wanateseka na mbegu hazipatikani kwa wakati na madawa hayapatikani kwa wakati, nini tatizo,? Tatizo ni ubovu wa bodi ya pamba? au ni mikakati mibovu ya Wizara ya Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Boniphace Getere kwa namna anavyohangaikia changamoto za Wakulima Jimboni kwake Bunda hususani zao la pamba.

Mheshimiwa Spika, tatizo la bei na usambazaji tayari Serikali chini ya mfumo wa ushirika tunaendelea kuimarisha ushirika ili ushirika uweze kuwajibika kwa Mkulima kwa kuhakikisha Mkulima anapata pembejeo kwa wakati anazingatia ubora na tayari Wizara yetu kwa kushirikiana na Taasisi zilizopo chini ya Wizara tunaendelea kutoa elimu ili wakulima wetu wa pamba wazingatie kupanda kwa kutumia kamba ambayo ina vipimo.

Mheshimiwa Spika, pia, sambasamba na hilo usambazaji wa pembejeo hususani viuatilifu kwa misimu iliyopita vilikuwa vikichelewa lakini tayari Wizara tumeshakaa na kuhakikisha tuna mkakati wa kuhakikisha msimu huu viuatilifu vina wafikia wakulima wetu kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Getere ni kuhusu masoko ya ndani na nje nimuhakikishie Mheshimiwa Getere kwa vile ni mfuatiliaji mzuri tutakaa naye pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mikoa inayolima pamba na kuhakikisha tunakuwa tuna mfumo mzuri ambao utamuhakikishia mkulima kupata bei nzuri lakini na shilingi mia moja ambayo wanakatwa tutaangalia namna ya kuangalia mfumo mzuri ili makato ya mkulima yamsaidie katika kuwa na Kilimo cha tija, ili aweze kupata pato zuri katika msimu wa kuuza pamba, nashukuru.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, vilevile Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo inafanywa kwenye eno hili la ardhi. Najua nia njema ya Waziri aliyejibu swali langu, namfahamu vizuri lakini nimpe taarifa kwamba katika majibu aliyonipa bado umeendelea ule utaratibu wa baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu kupotosha kwenye vitu ambavyo ni vya msingi.

Mheshimiwa Spika, nikianza na baadhi ya majibu yaliyotolewa hapa, mojawapo ya jibu lililotolewa ni jibu ambalo Waziri Mwanjelwa aliwahi kulikataa na kutoa maelekezo tofauti lakini bado jibu hilo hilo limeendelea hapa. Kuhusu exemption tuna barua ya Wizara ya Viwanda ikionesha kwamba mojawapo ya mashamba yaliyopewa exemption, mwaka 2014 Shamba la Gararagua limeuzwa lakini mwaka 2012 tayari mwekezaji aliyenunua mwaka 2014 tuna barua ya Wizara ya Viwanda inayoonyesha kwamba alipewa exemption mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, leo tukiwa hapa hatujui tuna wananchi wetu wa Kata ya Levishi, Kijiji cha Mese mashamba yao ya kahawa yamechukuliwa na TANAPA, Donumoru wananchi sasa hivi wa Kilolepori wanaishi nje, wamebomolewa nyumba zao. Leo hatujui mpaka wa Siha na Wilaya ya Arusha lakini bado huko chini tuna watu ambao wanafanyakazi hiyo. Vilevile kwenye Wizara ya Kilimo tutaona kwamba…

SPIKA: Mheshimiwa Mollel swali sasa.

MHE.DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye swali langu sasa.

SPIKA: Swali moja kwa moja.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Mawaziri wa Wizara husika watakuwa wako tayari kufuatana nami sasa ili twende kwenye maeneo husika kwa sababu tuna Wazungu wanaouza mashamba ya Siha ili wapate mtaji wa kuendeleza maeneo mengine na kuchapa watoto ndani ya Wilaya ya Siha na nitawapa ushahidi hapa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi zitakuwa tayari sasa kukaa chini baada ya Tamko la Rais ili tuone ni namna gani tunaweza tukawapatia wananchi wa Ngarenandume makazi zaidi ya 38,000 wanaoishi kwenye heka 500?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Dkt. Mollel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa namna anavyofuatilia migogoro ya mashamba ya ushirika katika Jimbo lake la Siha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mollel angependa kusikia commitment ya Serikali kama tuko tayari kuambatana naye kwenda Jimbo la Siha ili kutatua migogoro hii. Jibu ni kwamba tuko tayari na mara tu baada ya Bunge tutaelekea katika Jimbo la Siha ili kuangalia migogoro hii katika mashamba ya ushirika. Pia kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakarabati ushirika kwa manufaa ya wananchi wetu.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa wakulima wa zao hilo hapa nchini kwetu wamekuwa wengi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia soko la uhakika wa bidhaa hizo?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa kuna ongezeko la uzalishaji wa spices hapa nchini na sisi kama Serikali, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi, tunayo mikakati ya kusaidia wakulima wetu wa spices kuongeza uzalishaji; sanjari na hilo kuwasaidia kupata masoko ya uhakika. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote ambayo yanatuingia fedha za kigeni tunawasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kuwasaidia masoko ili waweze kusaidia kwenye pato la Taifa na kuingizia Taifa fedha za kigeni.
MHE. NAJMA M. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile spices yaani viungo vya vyakula mbalimbali ni vinaonesha kwamba vina afya zaidi katika miili ya binadamu. Sasa kwa nini Serikali haitumi wataalam wake wakaja Zanzibar kujifunza faida za viungo hizo ili Watanzania wengine walioko Bara ambao hawajui kama vile Wasukuma, Wamasai na makabila mengine waweze kujua na kutumia na kupata afya njema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake tumeupokea, ni kweli hizi spices zina faida nyingi ikiwemo faida kwa upande afya kwa akinababa na akinamama. Ni ushauri mzuri kwa sababu tunatafuta masoko ya nje, lakini pia masoko ya ndani lazima nayo tuyatumie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wanaume wenzangu, ukiangalia spices kuna faida nyingi sana kwa upande wa wanaume na ni namna mzuri ya kukuza soko la ndani. Kwa hiyo, ushauri wa Mheshimiwa Najma tumeuchukua.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Mkinga, Muheza, Korogwe na Lushoto ni maeneo ambayo yanalima kwa wingi mazao ya spices, lakini kwa muda mrefu maeneo haya yamekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za Ugani, masoko duni ya bidhaa hizi na vilevile mazao haya kuuzwa kwa bei ya chini sana. Je, Waziri yuko tayari na wataalam wake kuja kwenye maeneo haya kujionea hali halisi ili kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwa namna anavyofuatilia masuala ya spices kwa niaba ya wakulima hapa nchini ikiwemo Jimboni kwake. Nimeshamhakikishia kwamba Serikali kwa kutambua kwamba spices hizi zina potential kubwa ya kutuingia fedha za kigeni, niko tayari kwenda Mkoa wa Tanga na kufika maeneo ambayo ameyataja kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia kwenye upande wa kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunawasaidia kwenye mambo ya branding na mikakati ya kimasoko ili kilimo chao kiweze kuwasaidia kuwakwamua kutoka kwenye umaskini, lakini uzalishaji wao usaidie kuchangia kwenye fedha za kigeni za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza, naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada kubwa ambazo amechukua kusaidia zao la tumbaku kwa kuja kila wakati katika Mkoa wa Tabora. Pili, naomba nimshukruu pia Naibu Waziri kwa jibu zuri kwamba wataagiza mbolea kwa pamoja yaani bulk procurement ili kusaidia kupunguza bei lakini kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, upatikanaji au uagizaji wa mbolea kwa wakati unategemea sana makisio. Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuhakikisha kwamba makisio yanatolewa mapema ili mbolea iweze kuagizwa mapema na imfikie mkulima kabla ya mwezi Agosti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mkulima anapata moyo wa kulima kutokana na bei anayotegemea kupata. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupata wanunuzi wengi zaidi ili soko lipatikane kwa wakati na kwa ushindani ili angalau mkulima apate bei inayoweza kumsaidia kumudu maisha na kazi kubwa anayoifanya ya kulima tumbaku? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwapongeze wananchi wa Urambo kwa kuchagua Mbunge jembe. Mheshimiwa Mama Sitta anawahangaikia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwagiza Mrajisi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika afike Urambo haraka iwezekanavyo akae na Mkuu wa Wilaya ili waangalie namna bora ya kuratibu utaratibu wa kukusanya madeni kwa wakulima wa tumbaku hasahasa wale wakulima ambao wanadaiwa lakini wanaendelea na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kuhusu kufanya makisio mapema. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mama Sitta pamoja na wananchi wake kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha makisio ya wanunuzi yanafanyika mapema ili wakulima waweze kujua ni kiasi gani cha mbolea wanatakiwa kuagiza na mbolea iwafikie kabla ya mwezi Agosti, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu mkakati wa kuongeza wanunuzi. Naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge na wakulima wetu kwamba kwa upande wa zao la tumbaku tayari Serikali tumekaa na wanunuzi waliopo na kuangalia changamoto zao ambazo tukizitatua zitawawezesha kununua tumbaku zaidi lakini tunaendelea kuongea na nchi ambazo zina mahitaji ya tumbaku ikiwemo China na Misri. Kwa hiyo, kwa mikakati hiyo Serikali itaweza kuwasaidia wakulima wa tumbaku kupata soko la uhakika na zaidi na kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasiaidia kuhakikisha tumbaku yao inatakiwa na inagombaniwa na wahitaji na kufanya hivyo kutasaidia kuchochea bei kupanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Changamoto za zao la tumbaku zinafanana kabisa na changamoto zinazokabili zao la kahawa. Suala hili la pembejeo hasa mbolea imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu wakulima wa kahama wengi wanashindwa kulima kahawa vizuri, wanashindwa kuhudumia mashamba ya kahawa kwa sababu ya bei kubwa ya mbolea. Licha kwamba Serikali inatumia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea wa Pamoja lakini bado haijawa suluhu kwa wakulima wa zao la kahawa. Je, ni lini sasa Serikali itajenga viwanda vya mbolea nchini ili angalau sasa mbolea iweze kushuka bei na wakulima wa kahawa waweze kunufaika na uzalishaji uweze kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumkaribisha Mheshimiwa Haonga pamoja na Wabunge wengine, leo tuna kikao cha wadau wa kahawa kinafanyika hapa Dodoma, kimeanza saa mbili na nusu. Kwa hiyo, baada ya maswali na majibu tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikao hiki na tuweze kupata maoni yenu ili kuboresha mfumo wa ununuzi wa kahawa hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Haonga la lini Serikali itajenga viwanda vya mbolea, majibu ya Serikali ni kwamba inaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha tunajenga viwanda vya mbolea hapa nchini ikiwemo utumiaji wa gesi asilia ambayo tumeigundua ili kutengeneza mbolea na kusaidia wakulima wetu waweze kupata mbolea hapa hapa nchini na kwa bei nafuu.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusu tumbaku kwa sababu tumbaku Tabora ndio siasa yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vingi vya msingi vimekufa au vimesinzia au havifanyi kazi kutokana na mfumo wa zamani uliokuwepo na hasahasa utoroshaji wa tumbaku, kukwepa madeni kupitia vyama vya IF. Sasa mfumo mzuri umewekwa na kwamba madeni yamedhibitiwa. Je, Serikali kupitia Benki ya Kilimo haiwezi kuwadhamini wanachama hawa wa vyama sinzia ili vilime tumbaku kwa mkakati wa kulipa madeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa ufatiliaji wake wa karibu wakulima wake wa tumbaku. Swali la Mheshimiwa Maige ni kwamba TADB inawasaidiaje wakulima kupitia vyama vya msingi. Jibu ni kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada kwanza ya kufufua vyama vya msingi viweze kuzingatia utawala bora (good governance) kwani kwa kipindi cha nyuma vyama vya msingi baadhi ya viongozi walikuwa siyo waadilifu kwa hiyo fedha nyingi zilikuwa zinapotea kwa njia hiyo kwa sababu walishindwa kuzisimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mkakati wa Serikali wa kuboresha ushirika na kuhakikisha vyama vya msingi vinakuwa na viongozi waadilifu basi tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa na TADB na kuangalia ni namna gani tunaweza tukaratibu jambo hili ili wakulima kupitia vyama vya msingi waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Bado narudi kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kuhusu tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye kalenda ya Bodi ya Tumbaku ili pembejeo zifike nchini mwezi Agosti na Septemba, makisio hutolewa tarehe 31 Machi, ndiyo deadline. Sasa makisio yametolewa kwa makampuni matatu ambayo yanafanya biashara hapa nchini; kampuni moja haijatoa makisio, hiyo ina maana wakulima wa Tabora, Chunya, Ruvuma, Mpanda watakosa kulima tumbaku msimu ujao. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuitisha kikao cha dhararu kati ya Bodi ya Tumbaku na Wabunge wanaolima tumbaku ili kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na mimi nakubaliana na yeye kwamba kukaa na wanunuzi kufanya makisio mapema iwezekanavyo ikiwezekana mapema mwezi Machi, ni jambo la msingi kwani litasaidia wakulima wetu kujua ni kiasi gani wanahitaji kuagiza kupitia bulk procurement system.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni kwamba tuko tayari kukaa na huyu mnunuzi mmoja ambaye bado hajatoa makisio? Jibu ni kwamba Mheshimiwa Mwambalaswa niko tayari na baada ya hapa nitatafuta namba zao na kuwapigia simu na kuona kwa nini mpaka sasa hawajatoa makisio kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la MKUKUTA na Ilani ya Chama cha Mapinduzi sekta ya kilimo ilikuwa ikue kwa asilimia 8 ndani ya miaka 10 lakini uhalisia kuanzia mwaka 2011 na 2015 sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.4. Ndani ya miaka ya Awamu ya Tano katika miaka yake mitatu ya bajeti sekta ya kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 1.9. Uhalisia unajionesha kwenye bajeti zake, bajeti ya mwaka 2016/ 2017…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulitenga shilingi bilioni 101 katika sekta ya kilimo lakini fedha iliyotoka ilikuwa ni shilingi bilioni 3 peke yake. Pia mwaka 2017/2018 tulitenga shilingi bilioni 150 ikatoka shilingi bilioni 24. Swali, hii ndiyo tafsiri ya Kilimo ni Uti wa Mgongo katika Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wote tunajua kwamba Watanzania wengi wanaohitimu vyuo vikuu katika Taifa hili ni 800,000 lakini watu ambao wanaajiriwa kwenye sekta rasmi karibu watu 20,000 tu ambapo 780,000 wanakwenda kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Hata hivyo, sekta ya kilimo kumekuwa na tatizo la uwekezaji, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wahitimu hawa wanapewa mikopo ili wajiajiri na wainue maisha yao pamoja na kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Mwakajoka anasema kwamba sekta ya kilimo imekua ikikua kwa asilimia ndogo kinyume na matarajio. Pamoja na mipango mizuri ya Serikali katika kukuza sekta ya kilimo nchini lakini kuna mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri productivity ya kilimo nchini. Hata hivyo, Serikali inayo mipango madhubuti kupitia Mpango wa Kilimo wa ASDP II kama nilivyotaja kwenye majibu yangu ya msingi, kuhakikisha tunatumia ardhi vizuri kwa kilimo, tunazingatia matumizi mazuri ya utumiaji wa maji ili kwenda kwenye kilimo cha umwagiliaji yaani drip irrigation pamoja na mikakati mingine ambayo tumeiweka ndani ya Serikali kupitia Mpango huu wa Maendeleo ya Kilimo wa ASDP II.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mwakajoka ni kwamba tuna vijana wengi ambao wanahitimu kwenye vyuo vikuu lakini kuna changamoto ya ajira; na wanaoenda kwenye kuajiriwa kwenye sekta ya kilimo ni wachache, asilimia ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika hili ni kuhakikisha tunaleta mageuzi ya kilimo na kufungamanisha kilimo na viwanda. Kama unavyojua Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge, Serikali inaendelea kufanya jitihada hizi kuangalia kilimo kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, asilimia 65 ya malighafi za viwandani zinategemea mazao yetu ya kilimo. Sasa mkakati wa Serikali ni kuongeza hizi asilimia ili tuweze kufungamanisha uchumi wa viwanda na kilimo.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa. Niipongeze Serikali kwa hatua inazozichukua kuimarisha soko la tumbaku nchini. Njia mojawapo ya kuimarisha soko la tumbaku kwa upande wa sisi Wanaruvuma ni kufufua Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku kilichoko Songea ambacho kinamilikiwa na SONAMKU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SONAMKU kwa kushirikiana na mnunuzi wanakwamishwa na Serikali kwa kutoilipa VAT return ya jumla ya shilingi bilioni 12 Kampuni hiyo ya Premium Active Tanzania Limited na hivyo kampuni hiyo kushindwa kushirikiana na SONAMKU kuanzisha au kufufua kile kiwanda.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha hizi fedha zinalipwa ili sisi Wananamtumbo tuwe na uhakika na soko la tumbaku kwa kufufua hicho kiwanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wananamtumbo tunajihusisha vilevile na kilimo cha Korosho na Mazao mchanganyiko ya mahindi mbaazi, ufuta, alizeti na soya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha masoko ya mazao haya ili Wananamatumbo tuendelee kupata nafuu lakini na suala la mbolea au pembejeo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin Amandus Ngonyani, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Edwin Ngonyani kwa namna alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kwa kampuni ya Premium Active Tanzania Limited. Nampongeza sana Mheshimiwa Ngonyani na kwa namna anavyohangaikia Wananamtumbo katika kuhakikisha wananufaika na sekta ya kilimo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kufufua viwanda vikiwemo viwanda ambavyo vinachakata mazao yanayotokana na kilimo likiwemo zao la tumbaku. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara ya Kilimo tutakaa na wenzetu upande wa Wizara ya Fedha kuangalia hili suala la VAT ambalo Mheshimiwa Ngonyani ameliuliza kama swali lake la nyongeza namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili ni kuhusu mkakati wa Serikali katika uhakikisha tunapata masoko ya uhakika ya mazao mchanganyiko pamoja na zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha tunapata masoko ya uhakika kwa wakulima wetu kwanza tumeanza na mikakati ya kupata institutional buyers na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, walishuhudia Serikali ikisaini mkataba na World Food Programme kwa upande wa zao la mahindi kwa wakulima wetu na tunaendelea kuongea na institutional buyers wengine ambao watasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara kwa kushirikiana na Balozi zetu nje ya nchi tunaendelea kuwasiliana nao na kuangalia mikakati ya kushirikiana ili tuweze kupata masoko zaidi katika mazao mchanganyiko na mazao ya kimkakati. Kwa mfano, mwezi Mei, kuna timu inaenda China hususan kwa ajili ya kutafuta soko la tumbaku pamoja na parachichi, karanga na mazao mengine.

Kwa hiyo napenda kumhakikishia Mheshimiwa Ngonyani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inaendelea kujipanga na tayari tumefanikiwa katika maeneo ya kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waheshimiwa Wabunge kama Mheshimiwa Ngonyani alivyoshirikiana na Serikali kupata soko la tumbaku kuptia kampuni ya Premium Active Tanzania Limited, basi na wao waendelee kushirikiana na sisi Wizara ya Kilimo kuwasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Moja ya tatizo kubwa la wakulima wa pamba ni bei ndogo kwa sababu inasimamiwa na soko la dunia. Mwaka 2015/2016 na hata 2017, Serikali iliahidi kuanzisha Mfuko wa Kurekebisaha Bei ya Pamba. Nataka kuiuliza Serikali inasema nini juu ya ahadi hiyo ili wakulima wa pamba sehemu zinazolimwa pamba waweze kupata bei nzuri wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kafumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge angependa kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha tunasaidia kuinua bei ya pamba nchini. Kama mnavyojua suala la uinuaji wa bei ya pamba unatokana na factor mbalimbali ikiwemo factor ya tija na chini ya SDP II, Serikali tuna mpango mzuri wa kuhakikisha tunawasaidia wakulima wa pamba na mazao mengine nchini kuongeza tija sambamba na ku-plan mapema masuala ya masoko kwa wakulima wetu.

Kwa hiyo, kwa combination ya factor hizo mbili, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba tutaweza kuleta uchochezi wa kuinua bei ya pamba pamoja na mazao mengine nchini. Nimuombe baada ya hapa tukae tuangalie hata hili suala la Mfuko wa kuinua zao hili inaweza ikawa ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuinua zao hili.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa zao la tumbaku na pamba, ni lini Serikali itaongeza bei kwenye zao la chai katika Wilaya ya Rungwe na cocoa katika Wilaya ya Kyela? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bei linakuwa determined na soko lakini moja ya mkakati wa Serikali kwenye zao la chai ni kuanzisha mnada hapa hapa nchini badala ya kutegemea mnada wa Mombasa. Kuhusu cocoa tunaendelea kuwasiliana na wanunuzi wa cocoa duniani ili kuona kama wanaweza wakanunua cocoa ya Tanzania. Kwa hiyo, mikakati ya Serikali ni mizuri kwa upande wa chai na cocoa na mkakati wa kuwa na mnada wa hapa hapa nchini utasaidia kuwapatia wakulima wa chai bei nzuri. Ahsante.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kampuni ya Alliance One iliyokuwa inanunua tumbaku Serengeti iliondoka wakati ambapo wakulima wako kwenye peak ya kilimo cha tumbaku. Baada ya kuondoka wakulima wakashindwa wapi wauzie tumbaku yao. Kwa kuwa Serikali ina jitihada ya kuwatafutia wananchi wa Serengeti kampuni nyingine ya kununua tumbaku, kwa nini wakulima wanaolima sasa hivi tumbaku wasiruhusiwe kuuza kokote watakako tumbaku yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ryoba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kumtoa wasiwasi Mheshimiwa Ryoba pamoja na wakulima wa pamba, Serikali inayo mikakati mizuri ya kuhakikisha tunawasaidia katika kupata masoko ya uhakika na nitumie nafasi hiui kumpongeza Balozi wetu Mheshimiwa Mbelwa Kairuki, Balozi wa China tunawasiliana nae na kuna ujumbe unaondoka mwezi huu mwishoni kwenda China kwa ajili ya kutafuta masoko ya tumbaku. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Ryoba awe na subira, karibuni tutaweza kuwapa uhakika wakulima hawa wa pamba katika Jimbo lake.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Zao hili la tumbaku ina changamoto zinazofanana na zao la vitunguu swaumu. Je, mna mpango gani sasa wa kusaidia zao la vitunguu swaumu kama zao la biashara kama ilivyo tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbogo Flatei kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitunguu swaumu pia ni zao muhimu ambalo linaweza kuwapatia wakulima wetu kipato na liko kwenye fungu la spices, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwa sababu Serikali tuna mkakati wa pamoja wa kuhakikisha tunasaidia wakulima kupata masoko ya spices, basi na suala la vitunguu swaumu tutaliweka katika hilo fungu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tulipitisha azimio humu Bungeni kwamba msimu wa pamba unatakiwa uanze tarehe Mosi Mwezi Mei kila mwaka. Hivi sasa kuna Walanguzi tayari wameshaanza kupitapita na kununua Pamba kwa shilingi mia tano, mia sita, mia saba. Je, ni nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali la Mheshimiwa Ndassa (Senator) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Senator ni taarifa muhimu sana kwa Wizara ya Kilimo kwa sababu tarehe 29 Aprili, tulifanya Mkutano wa 15 wa wadau wa pamba na baada ya hapo jana tulikuwa tuna kikao cha kupitia mwongozo wa msimu wa ununuzi wa pamba na leo hii tunapitia masuala ya bei elekezi ili kuanza msimu tarehe Mosi Mei, 2019 na taratibu hizi zote ziko kisheria, kwa hiyo yoyote yule ambaye ananunua pamba kabla ya uzinduzi wa msimu wa pamba ambao uko kisheria ni ukiukwaji wa sharia. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa baada ya hapa nitawasiliana na Wakuu wa Mikoa na kuhakikisha Serikali tunajipanga kuhakikisha mkulima hanyonywi…

MWENYEKITI: Ahsante, ameshakuelewa.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): …kwa sababu shilingi mia sita au mia saba ni hela ndogo sana kwa mkulima.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali juu ya majibu ya tumbaku, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, katika jibu la (b) kuhusiana na tozo (Produce cess) kwa kweli Serikali ilipunguza kutoka asilimia tatu mpaka tano. Ukiangalia discount hii ilikuwa ni karibuni asilimia 40 na mkulima hajafaidika. Kuhusiana na tathmini, binafsi kwenye halmashauri zetu tumekwishafanya tathmini mapato yameshuka. Sasa Je, Serikali iko tayari katika mabadiliko ya sheria yanayoletwa sasa hivi Mwezi Juni kwenye Finance Bill kurudisha hii produce cess kuwa asilimia tano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili dogo; Kampuni ya Premium ambayo inanunua tumbaku nchini ikiwemo Katavi, Chunya pamoja na Ruvuma mpaka sasa haijalipa tozo za halmashauri pamoja na kwenye vyama vya msingi kwa sababu kwamba wana madai yao Serikalini ya marejesho ya kodi la ongezeko la thamani (VAT refund) na tangu mwaka jana tunafuatilia na mpaka sasa Serikali haijailipa hii kampuni na wanadai takribani bilioni 12. Sasa Je, Serikali haioni kwamba kutolipwa kwa wakati fedha hizi inachelewesha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbogo kwa namna anavyofuatilia zao la tumbaku kwa manufaa ya wakulima wa tumbaku nchini.

Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbogo anauliza kama tuko tayari kurudisha produce cess kutoka asilimia tatu kurudi kwenye asilimia tano. Kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Mheshimiwa Mbogo ana hoja nzuri lakini kama nilivyojibu ni mapema kwa sababu tuko kwenye fiscal year ya kwanza katika utekelezaji wa hii sheria na Serikali tumesema hatutasita baada ya kufanya tathmini na kuona kuna haja ya kurudisha hiyo produce cess. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira angalau twende kwenye fiscal year kama mbili, tatu halafu baada ya hapo tutafanya tathmini na kuona namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Mbogo, anasema kutolipwa kwa VAT refunds kwa muda kunaathiri malipo kwenda kwenye halmashauri na vyama vya ushirika. Kwa vile suala hili linahusu VAT claims basi nimwahidi Mheshimiwa Mbogo tutakaa na wenzetu Wizara ya Fedha na kuangalia namna ya ku-expedites ili Kamouni hii iweze kulipa madeni ya halmashauri na AMCOS.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nipongeze Serikali kwa juhudi pekee ya kuinua bei ya zao la chai kutoka 241 kwa kilo ya majani mabichi chai mpaka kufikia 315, na nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutembelea Jimbo hili la Busokelo na concern yetu ya zao la chai tuliwaambia na kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, Bonde la Mwakaleli tuna Kiwanda cha Chai ambacho kimekuwa kikizalisha chai lakini kwa msimu, kuanzia mwezi wa Disemba mpaka Juni kila mwaka na hivyo miezi Sita mingine huwa hakifanyi kazi; Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kukifanya kiwanda hiki cha chai cha Bonde la Mwakaleli kiweze kufanya kazi mwaka mzima badala ya sasa tunaki- underutilize. (Makofi)

Swali la pili, hivi sasa katika Jimbo langu la Busokelo tunalima viazi mviringo na ni wakati wa msimu wa mavuno lakini bei yake ipo chini sana, kiasi kwamba hata wanunuzi wa viazi hivi wanawaibia zaidi wakulima wana-collude kwa kushirikiana na yale makampuni yanayotengeneza mifuko kwa kufanya kitu kinachoitwa lumbesa. Kwa mfano, mfuko mmoja ambao una debe tano wao wanafanya debe sita na nusu na wananchi hawa wanakuwa wamekopa wamenunua pembejeo, wamelima kwa shida, lakini bei zao ziko chini na kiasi hiki kinafanya mkulima akate tamaa kabisa kuendelea kulima zao hili la viazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani wewe ukiwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuja site ili uone namna mateso ya wananchi wangu wa Bonde la Mwakaleli, Busokelo pamoja na Wilaya nzima ya Rungwe hadi Uyole - Mbeya kwamba wanahitaji masoko ya uhakika katika zao hili la viazi. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete Mbunge wa Busekelo kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwakibete kwa pongezi kwa Serikali kuongezeka kwa bei ya chai kutoka shilingi 241mpaka shilingi 315 lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Mwakibete kwa kweli anawapambania wananchi wa Busekelo tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Fredy Mwakibete Mbunge wa Busekelo ni kuhusu Kiwanda cha Chai kuzalisha miezi Sita peke yake na yeye angetamani pamoja na wananchi wa Busekelo kuona kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba nitatenga muda niweze kwenda nae Jimboni Busekelo tutembelee Kiwanda hiko tuangalie changamoto zilizopo na kuona ni nini Serikali inahitaji kufanya na upande wa Mwekezaji wanahitaji kufanya nini ili kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mwakibete angependa kuujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wa Busekelo tunawapatia soko la uhakika la viazi mviringo.

Mheshimiwa Spika, katika ziara ambayo nitaifanya tutahakikisha tunatoka na mkakati wa kuwapatia masoko ya uhakika wa viazi mviringo tunaujadili na pale inapowezekana tutawaunganisha wakulima hawa kwenye masoko ya viazi mviringo. Suala la lumbesa, halitasubiri ziara Mheshimiwa Mbunge baada ya maswali tutakaa pamoja tuangalie namna ya kushughulikia jambo hili, haliwezi kusubiri ziara, tutafuta namna ya kuliratibu vizuri ili wananchi wako wasiendelee kupunjwa kupitia mfumo wa lumbesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua lini Serikali itamaliza kufanya tathmini hiyo ya pili na kuweza kulipa fidia kwa wananchi hawa wa Halmashauri ya Makambako ambao walikubali kabisa kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Viwanda na Biashara mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba ndani ya Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla kunakuwa na viwanda vingi vidogo vidogo vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ili wanapoenda kuuza kwenye viwanda vikubwa na kwenye soko la Kimataifa tarajiwa wananchi hawa waweze kupata mapato zaidi na kuinua hali zao za kiuchumi, vilevile ili tuweze kufikia azma ya uchumi wa kati. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge Neema Mgaya kwa namna anavyofuatilia changamoto za wananchi wa Mkoa wa Njombe, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mgaya ni kwamba lini tathimini itakamilika. Kwa kuzingatia azma ya Serikali ya kuhakikisha tunawasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika, jambo hili tunalichukulia kwa uzito na tathmini, tutahakikisha inafanyika haraka iwezekanavyoo na kwa vile kupitia Wabunge, wananchi watatupa ushirikiano katika kukamilisha suala la fidia, basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tathmini itakamilika haraka iwezekanavyo, ili kupitia soko la kimataifa la Makambako, wakulima wanaotoka kwenye Nyanda za Juu Kusini waweze kuzalisha kwa wingi na kupata masoko ya uhakika kupitia soko la kimataifa la Makambako.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mgaya angependa kujua nini mkakati wa Wizara yetu katika kuhakikisha tunaongeza viwanda vidogovidogo ili kuchakata mazao ya wakulima. Nimhakikishi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tayari ina mikakati mizuri, bilaterally kwa kuandaa makongamano mbalimbali nchini, ambapo wafanyabiashara kutoka nchi za SADC, wafanyabishara kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakuja hapa Tanzania kukutana na wafanyabiashara na wenye viwanda hapa nchini, lengo hilo na mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kupitia forum hizi tunavutia uwekezaji lakini tunasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ku-network na wenzao ambao wanatafuta fursa za kuwekeza hapa nchini na kwa vile utekelezaji wa blue print unakwenda vizuri, basi nina imani kabisha mikakati hii itaweza kusaidia kuchochea ujenzi wa viwnada nchini.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya dada yangu; kwa sababu ameji-commit kwamba mnafanya utafiti ili kuona gharama halisi ambazo zitasababisha mfufue.

Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Bunda tulikuwa tuna Ginnery tano ambayo ni Kibara, Ushashi, Mara Rint, Bulamba na Olam na zinazofanya kazi ni mbili. Tatu ukiwepo na Ushashi hazifanyi kazi zinafanya kazi Olam na Bulamba lakini Mara Rinti ni nzima na ina kila kitu tatizo lake ni mwekezaji. Sasa ni lini Serikali mtatafuta mwekezaji ili hii Ginerry ya Mara Rinti ifanye kazi na ipo kwenye eneo very strategic na ikifanya kazi itapunguza changamoto ya ajira kwa akina mama na vijana wa Jimbo la Bunda Mjini na Wilaya nzima ya Bunda kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara tuna kiwanda cha nguo, kipo Musoma. Hata hivyo sasa hivi hiki kiwanda hakifanyi kazi kwa ufanisi na ukiuliza changamoto kubwa kwa nini kiwanda hiki hakifanyi kazi; na kuwepo kwa kiwanda hiki ni kutokana na malighafi ile ya pamba iliyopo kwenye Mkoa wetu wa Mara na maeneo jirani. Sasa nimeuliza changamoto ni mtaji, na kama hakifanyi kazi kwa ufanisi ina maana kunapunguza ajira kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua, ni lini Serikali Mtaongeza mtaji ili akina mama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kutokana na kuwepo kwa kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara?

Sasa ningependa kujua ni lini Serikali mtaongeza mtaji ili wamama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kuwepo na kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri swali la msingi. Serikali imeona umuhimu wa kufanya uchambuzi katika kutekeleza Sera ya zao la pamba ya cotton to cloth kwa hiyo, lipo zoezi la kuhakikisha tunachambua na kuangalia namna bora ya kufufua ginnery zote za pamba kwa sababu value chain ya cotton to cloth inaanzia kwenye ginnery kufanya kazi mpaka kwenye textile industries.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bulaya kwamba hata kiwanda cha MUTEX kiko sehemu ya hili zoezi. Nimeshafika kwenye kiwanda hicho na ninakuhakikishia katika zoezi hili tutafia pia kwenye ginnery hizi ulizozitaja na tunashirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha zoezi hili linafanyika haraka sana iwezekanavyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Naibu Waziri kujibu swali. Baada ya kutoa kodi na tozo 12, mategemeo yetu ilikuwa bei ya mbegu kuwa chini au kuteremka kutoka shilingi 9000/10,000 zimepanda bei mpaka 12,500. Je, kuna uhusiano gani sasa tulipiga kelele huku kuondoa tozo na kodi lakini bado bei ya mbegu imeongezeka. Naomba Mheshimiwa Waziri atuambie pamoja na kwamba tathmini haijaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbegu ni suala muhimu sana katika kilimo, sasa yeye amesema mnatafuta fedha na mnategemea kufanya tathmini, hamuoni tumechelewa kufanya hivyo wakati kilimo kinaendelea kila msimu. Naomba uniambie fedha zitapatikana lini na tathmini itafanywa lini ili bei mbegu ithibitiwe na iteremke? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwa namna anavyofuatilia changamoto za wakulima wake katika Wilaya ya Hanang na napenda kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu amesema kwamba pamoja na jitihada za Serikali kuondoa kodi na tozo, bado bei ya mbegu haijashuka na mkakati wa Serikali katika hili ni kwamba tumetambua kwamba mkulima na mzalisha mbegu wamekuwa wote wakitegemea msimu wa mvua, badala ya mzalisha mbegu kuzalisha mbegu za kutosha wakati wa kiangazi ili aweze kumpatia mkulima mvua zinavyoanza mkulima huyu aweze kupanda.

Mheshimiwa Spika, sasa mkakati wa Serikali ni kwamba kwanza nimpongeze Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amesaidia Serikali kuingia makubaliano na EFAD. Tumeingia makubaliano tumepata bilioni 127.3 na fedha hizi asilimia kubwa itaenda kwenye taasisi za uzalishaji wa mbegu. Na nimuhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu, Wilaya ya Hanang hatutawasahau katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu alikuwa anazungumzia kuchelewa kufanyika kwa tathmini lakini Serikali haijachelewa kama nilivyosema, tayari Serikali imeshapata dawa fedha zimepatikana, sasa tunaenda kwenye utekelezaji. Ahsante sana.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na ni kweli ugonjwa huu umepungua kwa asilimia kubwa, lakini haujaisha. Sasa Serikali kwenye majibu inasema kwamba jitihada zimekoma 2014, lakini ukweli ni kwamba ugonjwa huu bado haujaisha kabisa, bado upo ingawa umepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, napenda kujua ni jitihada gani mahususi ambayo Serikali inayo kutokomeza ugonjwa huu uishe kabisa kwa asilimia 100? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sambamba na ugonjwa huo wa migomba kuna mnyauko pia wa mikahawa, kuna mnyanjano pia wa mihogo unaitwa batobato na yote haya yanalimwa Kagera haya. Napenda kujua ni jitihada gani zinachukuliwa na Serikali kuondoa magonjwa hayo mengine na mazao mengine kama kahawa, migomba, mihogo na mazao mengine?

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Jasson Rweikiza kwa jitihada nzuri za kuhakikisha kwamba tunatokomeza ugonjwa wa mnyauko wa ndizi pamoja mnyauko wa kahawa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jasson Rweikiza ni mkulima mzuri wa ndizi, nilishawahi kutembelea shamba lake. Kwa hiyo, nakupongeza kwa kupambana na jitihada hizi huku nawe ukiwa mkulima kwa kuonesha mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maswali mawili ya Mheshimiwa Jasson Rweikiza, swali la kwanza angependa kujua mikakati ya Serikali ya kutokomeza mnyauko wa migomba, ni kwamba Serikali kama nilivyosema kwenye swali nililojibu wiki iliyopita, Mheshimiwa Rais wetu ametusaidia kupata mabilioni kutoka IFAD; shilingi bilioni 127.3 kwenda kwenye Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI na ASA) kwenye kuzalisha mbegu pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi hasa hasa kwenye magonjwa kama haya ya mnyauko na magonjwa mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Rweikiza kwamba Serikali tayari ina jitihada mahususi za kuhakikisha tunapata fedha za kutosha kupambana na magonjwa haya. Vile vile nikuhakikishie katika bajeti ambayo itaenda TARI na ASA tutahakikisha bajeti kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya mnyauko wa kahawa na ndizi na yenyewe inazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tatizo la huu ugonjwa wa mnyauko katika migomba, linafanana kabisa kwa miaka mingi na mnyauko au ugonjwa wa manjano kwa kilimo cha mpunga ndani ya Wilaya ya Kilombero na mwaka huu athari hii imekuwa kubwa mno. Kila mara nilikuwa nafuatilia hapa kuuliza maswali Bungeni lakini hatujapata jibu kwamba tunafanyaje sisi wakulima wa mpunga kwani tunapata hasara kubwa?

Je, Serikali ina mpango gani wa kutupa majibu wakulima wa mpunga hususan wa Wilaya ya Kilombero, Ulanga, na Malinyi ambapo ndio walimaji wakubwa wa mpunga ili tuepukane na hizi harasa tunazopata kila mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, Serikali inatambua kwamba kuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na moja ya changamoto hizi ni magonjwa ambayo yanashambulia mazao yetu likiwemo zao la mpunga kama Mheshimiwa Susan alivyosema.

Mheshimiwa Spika, Serikali tunatambua mazao haya, ni lazima tuweke jitihada ya kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa wakulima wetu kwa sababu nchi zinazunguka Tanzania zina uhitaji mkubwa wa mchele na mazao mengine. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Susan kwamba Serikali inatambua changamoto zilizopo kwenye mabadiliko ya tabianchi. Kwa kupitia Taasisi zetu za TARI na ASA, tutaenda hata Jimboni kwake kuangalia changamoto alizozitaja ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Serikali yetu kwa ujumla kwa jibu hilo zuri.

Hata hivyo ili tuwe na uelewa wa pamoja kati ya Serikali na wakulima wa tumbuku wa Namtumbo; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuzifafanua changamoto hizo za mnunuzi wa tumbaku zinavyotakiwa kutatuliwa na Serikali kwa ujumla wake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, wakulima wa Namtumbo wanalishukuru sana Bunge lako tukufu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa kwa umahiri mkubwa na Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu kwa kuwawezesha wakulima wa Namtumbo hadi sasa katika minada mitatu tu wamepata shilingi bilioni 5.5 la zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)

Je, Serikali iko tayari kuendelea kutatua changamoto za wakulima wa Namtumbo hususan katika mazao ya korosho, soya, mbaazi na mengineyo na hasa katika korosho wale wakulima wachache ambao mpaka sasa hawajalipwa, wameuza korosho zao mwezi wa kumi hususan wa Tarafa wa Sasawala, lini watalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Ngonyani angependa kupata commitment ya Serikali kama tunaweza tukakaa pamoja na Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wakulima wake ili kuweza kutatua changamoto ambazo anakabiliana nazo huyu mwekezaji PATL. Kwa sababu ya muda na kwa vile Mheshimiwa Ngonyani ni mfuatiliaji mzuri, hili ni swali la pili katika kikao hiki basi nimuahidi kwamba nitakaa naye na tutafute muda kuweza kukaa pamoja na kuainisha hizi changamoto ambazo tayari Wizara tunazifahamu na kuzijadili na kuangalia namna bora ya kuzitatua haraka iwezekanavyo ili mwekezaji huyo aweze kuendelea na uwekezaji, wakulima wetu waweze kupata mahali pa kuchakata tumbaku yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Ngonyani anauliza kama Serikali iko tayari kufanya maboresho na kuongeza jitihada za kuhakikisha mazao ya korosho, soya, mbaazi na mazao mengineyo yanamsadia mkulima Mtanzania na jibu ni ndiyo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mazao yote haya na mengine tunaongeza uzalishaji na tunawasaidia wakulima wetu kuwa na kilimo cha tija na sambamba na hilo tunawasaidia wakulima wetu kuwaunganisha na masoko. Suala la malipo ya korosho nimhakikishie Mbunge kuwa Serikali inaendelea kufanya kila iwezekanavyo kuhakikisha waliobaki ambao hawajalipwa na ambao ni wachache waweze kulipwa malipo yao, ahsante.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa huyu mwekezaji amefanya jitihada kabisa kuhakikisha kwamba anawekeza katika kile kiwanda na amewekeza anadai zaidi ya dola za Marekani milioni tatu na hivi sasa alikuwa amesimama kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikimkabili. Lakini Serikali tumepanga kabisa kwamba ndani ya wiki mbili hizi tutakaa naye ili tuweze kuzungumza pamoja ikiwa ni pamoja na kuangalia suala lile la madai ya VAT ambayo yalikuwa yamekaa muda mrefu ambayo anasema kwamba yamemuathiri katika kuendeleza hiki kiwanda. Kwa hiyo, tutakaa naye pamoja na makampuni mengine yale ambayo nayo yana changamoto hiyo hiyo ili tuweze kuhakikisha kwamba hili suala linafikia mwisho na kusudi waendelee kununua zao letu la tumbaku. Nakushukuru. (Makofi)